Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Wednesday 26 March 2014

Pata Nakala yako LEO kwa bei ya Sh. 700/= tu


Bunge lachafuka


Mohammed Issa na Theodos Mgomba, Dodoma

HALI ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ilichafuka jana, huku baadhi ya wajumbe wakitaka kupigana baada ya Tundu Lissu, kuwasilisha waraka usiohusu masuala ya bunge kwa siku hiyo.
Lissu aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, na kutoa waraka aliodai ulitaka kuwasilishwa mbele ya wajumbe na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho.
Baada ya kusimama, Lissu alionyesha waraka aliodai ni takataka na haufai kujadiliwa, maneno ambayo yaliwaudhi baadhi ya wajumbe.
Waraka huo uliibua maneno kwa baadhi ya wajumbe, ambao walitaka aeleze ameupata wapi.
Wajumbe: Sema umepata wapi waraka huo, sema tueleze mbona sisi hatuna.
Lissu: Mwambieni Mwenyekiti (Sitta), awape, anao.
Malumbano hayo yalisababisha baadhi ya wajumbe kuongea kwa sauti, ndipo Sitta aliposimama na kusema: “Ndugu wajumbe, tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa Bunge ni nzito sana na zinaelekezwa kwake wala yeye hahusiki.”

Alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ndiye anayeweza kupeleka marekebisho yanayohusu kanuni.

Baada ya Sitta kueleza hayo, Abdallah Bulembo, alisimama na kuomba mwongozo.
Bulembo:  Sisi ni watu wazima, kanuni ndiyo zilizotuleta humu, vikao vya kuzomea haviwezi kuwasaidia Watanzania. Kama vikao vya UKAWA ndiyo hivyo, ni vyema wasiotaka kuendelea na mchakato huu waondoke watupishe sisi tuendelee.

Wajumbe: Haondoki mtu hapa, heee heee heee.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisema bunge linaendeshwa kwa kanuni, haiwezekani mtu mmoja akapitisha mambo peke yake.

Alisema kama ana hoja ya kubadilisha kanuni afuate kifungu cha 87, vinginevyo haitawezekana.
Othman alimtaka Sitta kukataa kuburuzwa na kwamba, bunge linaongozwa kwa kanuni.
Kauli hiyo iliwafanya wajumbe kulipuka kwa furaha, huku wengine wakipiga kofi kwenye meza.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Fredrick Werema, alisema:
“Mambo yote yatafanywa kwa maridhiano ambayo yanataka tufuate kanuni.”

Wajumbe walizomea na kumfanya Jaji Werema kusema, nimeshazoea kuzomewa, nilikuwa mwalimu nilifundisha elimu ya msingi mpaka chuo kikuu.

Jaji Werema alisema waungwana ni vyema wakafuata kanuni ya 87 (i), ambayo inasema Bunge Maalumu linaweza kuzifanyia marekebisho au mabadiliko kanuni zitakazowasilishwa kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu.

Baada ya kauli hiyo, wajumbe walipiga kofi, ambapo Jaji Werema alisema: “Sijazoea kupigiwa kofi nikizungumza.”

Jussa Ismail Ladhu, alisema majukumu ya kamati ya uongozi ni kujadili na kupanga ratiba za Bunge Maalumu la Katiba, ambapo hadi sasa hazijapangwa.

Alisema kamati ya uongozi haina sababu ya kushughulikia Kanuni za Bunge Maalumu.
Sitta alisema migogoro yote ya kanuni huamuliwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Alisema tuhuma zilizotolewa na wajumbe ziwasilishwe kwenye kamati hiyo.
Mwenyekiti Sitta alisema shughuli iliyokuwa ifanyike haitaendelea.
Baada ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe walinyoosheana vidole kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kuzorotesha shughuli za bunge.

SITTA ALONGA

Baadaye Sitta akizungumza na waandishi wa habari alisema imebainika kuna kikundi cha watu wachache kilichojipanga kuharibu mchakato wa katiba mpya.


Alivitahadharisha vikundi hivyo kuwa ghiliba na hujuma wanazotaka kufanya kukwamisha mchakato huo zimeshabainika.
“Nipo imara, ingawa kazi hii ni ngumu, lakini nawaomba wananchi waelewe kuwa hawa wenzetu hawana nia ya kutufikisha kule tunakotarajia,” alisema.

Sitta alisema vurugu zinazoendelea kufanywa bungeni ni matunda ya  maazimio ya baadhi ya mikutano iliyofanywa mfululizo na kikundi cha  Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA).

Alisema baadhi ya maazimio ya umoja huo, ambao chimbuko lake ni vyama vya upinzani ni mkakati wa kutoka ndani ya bunge na kuhakikisha wanakwamisha kila kitu kinachowasilishwa.
“Si hilo tu, bali wenzetu hawa katika maazimio yao walishapanga kuwa kama maslahi ya UKAWA hayatatimizwa na mwenyekiti wa Bunge hili, hakuna kitakachofanyika mpaka kieleweke, sasa hii ni nini,’’ alihoji.

Alisema UKAWA wanadai Kamati ya Uongozi lazima ifumuliwe, jambo ambalo ni dalili ya kutaka kutofikia mwisho mwema wa mchakato wa katiba.

“Nashangaa, wenzetu hawakujitokeza kugombea nafasi za kuongoza kamati, aliyejitokeza ni Profesa Lipumba pekee na alishindwa na mama Anna Abdallah, sasa CCM imeshinda, wanaanza kuleta siasa za vurugu, hatutafika.


“Kwa utaratibu wa mabunge mengine kuwepo kwa vikundi kama hivyo si jambo baya, kama nia ni kushauriana katika kupata mambo mazuri lakini, kwetu imekuwa kinyume,” alisema.

Alisema tuhuma alizotupiwa na Tundu Lissu, hazikumtendea haki kwa kuwa ni kauli za wongo na uzushi, ambazo zinawapotosha wananchi.

Hata hivyo, alisema kauli za Lissu kamwe haziwezi kumkatisha tamaa ya kufanya kazi hiyo adhimu ya Watanzania.
Alisema ameshapeleka malalamiko kwenye Kamati ya Kanuni ili kuangalia ukweli wa tuhuma hizo dhidi yake.
Kuhusu waraka uliodaiwa kutaka kubadili kanuni ndani ya Bunge uliotolewa na Lissu, alisema haukupangwa kwenye kazi za bunge za jana jioni.
Alisema inashangaza kuona mjumbe huyo alichukua wapi nyaraka ambayo Kamati ya Uongozi ilitoa kwenda Kamati ya Kanuni, lakini kabla haujafanyiwa kazi, aliuchukua na kuuleta bungeni akidai kuwa ni kazi ambazo zipo katika orodha ya jana.
Hata hivyo, Sitta alikiri kuwa kuna kanuni ambazo kamati imebaini zina kasoro na zinapaswa kufanyiwa marekebisho na si zile zilizosomwa na Lissu bungeni.

Polisi wadaiwa kuua dereva wa bodaboda


Na Mwandishi wetu.

ASKARI Polisi wa Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Dar es Salaam, wanadaiwa kumpiga hadi kufa dereva bodaboda, Salehe Said.
Said (18), mkazi wa Magomeni Kagera, alifariki dunia Machi 23, mwaka huu, saa saba usiku katika Hospitali ya Mwananyamala, ambapo awali akiwa na wenzake watano walifikishwa kituoni hapo na dereva teksi.
Inadaiwa dereva huyo wa teksi, alimfikisha Said na wenzake katika kituo hicho kutokana na kutokea mgogoro wa kugombea abiria katika kituo hicho cha mabasi.
Kwa mujibu wa baba mlezi wa marehemu, Leonard Mkomo, baada ya mwanawe kufikishwa kituoni hapo, alihoji sababu ya kufikishwa na ndipo askari polisi wakaanza kumshambulia kwa kipigo.
Alisema mara baada ya kipigo hicho, hali ya mwanawe ilianza kuwa mbaya na ndipo akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na kufariki dunia siku hiyo hiyo saa saba usiku.

“Baada ya kifo hicho mwenzake na marehemu waliokuwa wakishikiliwa kituoni hapo waliachiwa, jambo ambalo linatia shaka na kusisitiza kuwa polisi walitumia nguvu kubwa katika kukabiliana na tukio hilo,’’alisema.
Mkomo alisema familia inafuatilia tukio hilo, na wapo katika mpango wa kuonana na Mkuu wa Polisi Mkoa maalum Kinondoni, Camillius Wambura kumweleza hali halisi kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa bado hatujapata ushirikiano wowote kutoka polisi, tunatarajia kuonana na Mkuu wa polisi Kinondoni aweze kutusaidia juu ya tukio hili” alisema.
Pia, alisema familia bado haijafikia uamuzi wa kumzika marehemu kwa kuwa wanafanya uchunguzi wa mwili wa marehemu ili kupata uthibitisho zaidi na baadae wataandaa taratibu za mazishi.

Sefue aridhishwa ujenzi bomba la gesi


NA FURAHA OMARY

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameelezwa kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoa Mtwara hadi Dar es Salaam.
Amesema miradi huo ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambao ulipokuwa ukianza watu walikuwa wakikebehi.


Balozi Sefue aliyasema hayo juzi mjini Dar es Salaam, alipotembelea kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi 1, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bomba la gesi.
“Baada ya siku mbili kutembelea mradi wa gesi, napenda kuipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kusimamia mradi huo ambao ni sehemu ya BRN. Kuna watu wakati tunaanza walikebehi, lakini tumeona utekelezaji unavyokwenda vizuri na tuna matumaini utakamilika kadri ulivyopangwa.” alisema.
 Katibu Mkuu Kiongozi aliihimiza wizara hiyo kusimamia vizuri mradi huo na makandarasi nao wanapaswa kujua kwamba serikali haitaki mchezo kazi ikitolewa lazima ikamilike kwa wakati uliopangwa.
“Hatuna mchezo lazima kazi ikitolewa ikamilike kwa wakati. Wananchi wameshateseka sana kuhusu umeme kama alivyoagiza Rais ifike mahali tuseme tatizo la umeme sasa basi,” alisema
 Balozi Sefue aliwahimiza makandarasi na wizara hiyo kuhakikiasha kila kitu kinakamilika kwa wakati.
Aidha, aliihimiza wizara hiyo kukusanya uzoefu wa nchi nyingine duniani ambazo ziliwahi kutumia gesi kwa kuwa kuna zilizofanikiwa na zisizofanikiwa ili kujifunza.
Pia alisema gesi ni kichocheo cha uchumi kukua, hivyo lazima kujenga uchumi vizuri kwa sababu ipo siku gesi itaisha na wasimamie vizuri mapato ya gesi ili kuwa na manufaa yatakayodumu.
Balozi Sefue aliwatoa hofu wale wanaodhani wananchi wanaopitiwa na mradi huo hawajanufaika na kuwataka kwenda Mtwara na Lindi kujionea.
Alisema wananchi hao wamenufaika kwa watoto kupewa udhamini na kupata maji safi na ajira mbalimbali. 

Mgombea CUF adaiwa kumjeruhi katibu UWT

KAMPENI ZA UBUNGE CHALINZE

NA MWANDISHI WETU

WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikitoa tamko la kuvitaka vyama kufanya kampeni za kiungwana na kuzingatia sheria, Chama cha CUF kimeanza kutia dosari kampeni za uchaguzi jimbo la CHalinze, baada ya mgombea wake, Fabian Skauki, kumjeruhi Katibu wa UWT Kata ya Ubena, Jesca Mlimilwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji (mstaafu) Damian Lubuva, alisema wamefikia hatua ya kutoa tamko hilo, baada ya kuona baadhi ya vyama vimeanza kukiuka sheria.

“Katika kufuatilia kampeni hizo, NEC imebaini baadhi ya vyama vimekuwa vikitumia lugha za chuki na zisizo na staha na hata kuhamasisha wananchi kuchukua sheria mkononi au kutoa vitisho kwa wapiga kura kwa lengo la kuzuia wasishiriki uchaguzi huo,” alisema.
Habari kutoka Chalinze zilidai kuwa Skauki akiwa na wafuasi wa chama hicho walivamia ofisi ya CCM, tawi la Tukamisasa, Kata ya Ubena kwa madai ya kuwakuta na daftari la wapigakura.
Mgombea huyo ambaye alijitambulisha kuwa ofisa usalama wa taifa, alimvamia na kumtengua mkono wa kushoto katibu huyo huku wenzake wakifanya uharibifu wa vifaa vya ofisi na kuvunja vitu Mbalimbali.
Akizungumza na Jesca nyumbani kwake kijiji cha Mwidu mbele ya waandishi wa habari Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alilitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

“Sitarajii kuendelea kumuona mgombea wa CUF uraiani kutokana na uvamizi walioufanya. CCM haitavumilia matukio ya kutumia nguvu kupiga watu na kuwateka na itahakikisha hatua zinachukuliwa.
“Tukio hili limetukera CCM...tutaongeza nguvu ya vijana wetu ili walinde viongozi wetu wa ngazi mbalimbali,” alisema Nape.
Nape alisema polisi hawatakiwi kuwa na kigugumizi ni lazima mgombea huyo akamatwe kwa kuwa hana mamlaka ya kupiga na kukamata mtu.
Jesca aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alikuwa ofisini na wenzake akamuona Skauki akiingia ofisi kwake na kumuuliza kwa nini ana orodha ya wapiga kura kwani itasababisha akose kura.
 Alisema wengine hawatambui lakini yeye alimpiga na kumnyonga mkono ambao sasa umefungwa plasta gumu.
Alisema baada kumpiga alimkamata na kumpakia kwenye gari lake na kumpeleka Kituo cha Polisi Mdaula.
Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Sauda Mpambalyoto, alisema kabla kuanza kampeni vyama vyote vilikutana na kamati ya ulinzi na usalama na kusaini makubaliano ya kufanya kampeni za kistaarabu lakini CUF imeanza kukiuka.
 Mratibu wa Uchaguzi wa Kata ya Ubena na Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, amelaani kitendo hicho na wamefungua kesi wakitaka pamoja na mambo mengine CUF ifidie uharibifu iliyoufanya.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Samuel Sarianga, alisema si kosa kuwa na orodha ya wapiga kura kwa kuwa vyama vyote vilipewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema anafuatilia tukio hilo na kwamba hatua zitachukuliwa.
Akifafanua Jaji Lubuva alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni  za uchaguzi jimboni humo Machi 13, mwaka huu, NEC imekuwa ikifuatilia kampeni katika maeneo mbalimbali ya jimbo na vyama vilivyosimamisha wagombea kwa kuzingatia ratiba iliyowekwa na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya kushauriana na vyama husika.
Jaji Lubuva alisema NEC inakemea kwa nguvu na kulaani vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa na kutaka ikumbukwe matumizi ya lugha za kejeli, vitisho na kuzuia wapiga kura kushiriki uchaguzi ni ukiukwaji wa sheria.
Alionya kwamba kwa yeyote atakayebainika kukiuka na kuvunja sheria atachukuliwa hatua kali na atakayeshukiwa kufanya vitendo hivyo akabidhiwe kwenye vyombo vya sheria na si kuchukua sheria mkononi.

“Tume inatarajia kuona kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura jimboni humo anatumia haki yake ya kikatiba na sheria ya kupiga kura kwa amani na utulivu, pasipo vitisho wala kubugudhiwa,”aliongeza.
Wananchi  wa Chalinze watapiga kura kumchagua mwakilishi wao Aprili sita mwaka huu, na uchaguzi huo unafanyika kuziba nafasi iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo, aliyefariki dunia hivi karibuni.

Ridhiwani ahadharisha wawekezaji

KAMPENI ZA UBUNGE CHALINZE

NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA wa Ubunge wa CCM, Ridhiwani Kikwete, ametangaza vita dhidi ya wawekezaji katika machimbo ya kokoto waliongia mikataba ya kinyonyaji na kusababisha migogoro na wananchi.
 Amesema akiwa mbunge hatavumilia kuona wananchi wakinyonywa na wawekezaji kutokana na mikataba mibovu inayowaneemesha binafsi na kuwaacha wananchi katika hali ngumu.
Ridhiwani alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea katika jimbo hilo.


“Hatuhitaji wawekezaji wa kututia umasikini...wananchi wana haki ya kunufaika na matunda ya uwekezaji na si kama ilivyo sasa ambapo hata ajira kwa vijana imekuwa taabu,” alisema  Ridhiwani ambaye ni mwanasheria.
Alisema akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha mikataba yote inapitiwa upya na kuweka utaratibu mzuri ambao wananchi watanufaika.
Mgombea huyo, alisema wapo wawekezaji wamekumbatia maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyandeleza wakati wapo wenye uwezo wa kuyaendeleza kwa faida ya jamii.
Akizungimzia kero hiyo, Diwani wa Kara ya Lugoba, Rehema Mwene, alisema wawekezaji wengi wanakiuka utaratibu wa kusaidia huduma za jamii kwenye maeneo waliyowekeza. 
Alisema wanashindwa kushirikiana na vijiji kuboresha miundombinu wakati magari yao makubwa yanayobeba hadi tani 30 yanapita kwenye barabara hizo na wengine waliochukua vijana wachache wanashindwa kuwalipa mishahara kwa wakati.

Tatizo la maji kuwa historia Chalinze




KAMPENI ZA UBUNGE CHALINZE

NA MWANDISHI WETU

TATIZO la maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Chalinze litakuwa historia baada ya kuanzisha mradi wa kuchimba visima.
Mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alitoa ahadi hiyo jana katika kijiji cha Diozile wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo.
Alisema kuchimba visima ndilo suluhisho la haraka la kutatua kero ya maji ili wananchi ili waondokane na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo
Ridhiwani alisema awamu ya tatu ya mradi wa maji wa Wami inaelekeza kufikisha maji hadi kwenye vitongoji lakini mradi huo unawezekana ukachelewa bali huduma hiyo ni muhimu.

“Nitachimba visima viwili Diozile ili mama zangu waondokane na adha ya kufuata maji maeneo ya mbali kwenye lambo linalofahamika kama lambo la Kikwete,” alisema.
Aliahidi kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho kujenga zahanati ili kina mama wapate huduma kina mama wapate huduma bora za afya  ya uzazi.
Mapema, Diwani wa Kata ya Msoga, Mohammed Mzimba, alisema maji na zahanati ni changamoto kubwa kwenye kijiji hicho.
Alisema wanawake wanakonda kwa kuchota maji hivyo kumuomba Ridhiwani akiingia bungeni, ajenda yake ya kwanza iwe maji.

Tuesday 25 March 2014

Hali tete bungeni



  •  Sitta ashukiwa ukiukwaji kanuni
  •  Kamati ya Uongozi kaa la moto
  •  Profesa Lipumba asusa uteuzi

NA LILIAN TIMBUKA, DODOMA
BAADHI ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamemshukia Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, wakimtuhumu kwa kukiuka kanuni.Samuel Sitta
Wengine wanapinga uamuzi wake wa kutaka kujadiliwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, ya ufunguzi wa bunge na iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Wakizungumza baada ya kuahirishwa kikao cha bunge jana, walidai Sitta amekiuka kanuni kwa kutenga muda na kuruhusu hotuba hizo zijadiliwe bungeni.
Evord Mmanda, aliyekuwa mjumbe wa kamati iliyoandaa Kanuni za Bunge, alisema hazijaonyesha kipengele kinachoruhusu kujadiliwa kwa hotuba hizo, badala yake zinapaswa kutumika kwa mwongozo katika kupatikana katiba bora.
“Rais alipohutubia bunge kanuni iliruhusu, Jaji Warioba naye alihutubia kwa kufuata kanuni. Ni kanuni gani inaonyesha bunge linaweza kuzijadili hotuba hizo, lazima tufuate kanuni, tusitake kupoteza muda kwa mambo ambayo hayajapitishwa kisheria,” alisema.
Abdallah Bulembo, alisema kwa wajumbe kutaka kushinikiza kujadiliwa kwa hotuba hizo ni sawa na kumkejeli kiongozi mkuu wa nchi, ambaye ndiye aliyewateua.
Bulembo alisema wanaotaka kushinikiza hotuba hizo zijadiliwe wana lao jambo, na hawana nia ya kuwatendea haki Watanzania wanaowawakilisha.
“Rais ndiye aliyetuteua na alikuja kutupa mwongozo wa kufanya kazi ya kutunga katiba. Alitupatia busara kwa kutuongoza wapi tunapaswa kupita, leo tunakuja na hoja ya kutaka kujadili kwa kukosoa kile alichokielekeza, huu ni sawa na utovu wa nidhamu,” alisema.
Hamis Dambaya, alisema haoni dhana ya kutaka hotuba hizo zijadiliwe na kwamba, kufanya hivyo ni kupoteza muda.
“Rai yangu kwa wajumbe ni kuwa, huu muda wa kutaka tuanze kujadili hotuba ni vyema ukatumika kufanya mambo mengine yaliyotuleta hapa,” alisema.
Dk. Ave -Maria Semakafu, alisema hotuba hizo zinapaswa kutumika kama nyenzo ya kufanyia kazi katika majadiliano.
“Rais Kikwete alishatuambia wazi kuwa, yale yalikuwa mawazo yake na akaasa akili zetu tuchanganye na za wengine ili tupate majibu sahihi ya nini kifanyike na uamuzi gani tuufikie,” alisema.
UTEUZI KAMATI YA
UONGOZI MOTO
Wakati huo huo, uteuzi wa majina ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi uliofanywa na Sitta ulizua tafrani na kusababisha Profesa Ibrahim Lipumba, kugomea uteuzi wake.
Baadhi ya wajumbe walioomba mwongozo baada ya Sitta kutaja majina ya wajumbe watano aliowateua, walilalamika kuwapo upendeleo katika uteuzi.
Walioteuliwa kuungana na wenyeviti wa kamati zingine kuunda Kamati ya Uongozi iliyoanza kazi jana ni Fakharia Hamis Shomari, Mary Chatanda, Amon Mpanju, Profesa Lipumba na Hamad Abuu Jumaa.
Mohamed Habib Mnyaa, alisema uteuzi huo haukuzingatia uwiano, ikizingatiwa hoja inayotarajiwa kuteka mjadala wa bunge ni ya Muungano, ambao unalalamikiwa na Wazanzibari.
“Kama katika Kamati ya Uongozi, ambayo ndiyo inatengeneza ajenda za kuja kujadiliwa ndani ya bunge ina Wazanzibari watano kati ya wajumbe 19, unatarajia kuna haki itatendeka hapo, mwenyekiti hujatutendea haki,” alisema.
PROFESA LIPUMBA
ASUSA UTEUZI
Profesa Lipumba alisema suala la uwakilishi wa Zanzibar ndani ya bunge katika kila nyanja ni la muhimu.
“Naona CCM mmejipanga vyema kutumaliza, Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa uteuzi wako lakini natangaza siko tayari kukubali uteuzi huu, naomba jina langu liondolewe,” alisema.
Alisema hakubali uteuzi huo, ambao alidai unalenga kumfanya aonekana kutumiwa na CCM kwenye uamuzi wa kila jambo, hivyo anawaachia walioteuliwa waendelee na kazi na yeye atabaki kuwa mjumbe.
“Nasubiri tuje tupambane huku ndani kwa hoja,” alisema.
John Mnyika, alisema uteuzi umekosa sura ya uwiano wa pande zote za Muungano na wa makundi mbalimbali.
Alisema kamati hizo zitaendelea kulalamikiwa kwa kuwa CHADEMA imekosa wawakilishi.
SITTA AJIBU MAPIGO
Mwenyekiti Sitta alisema uamuzi wake hauwezi kumfurahisha kila mtu ndani ya bunge.
“Kwa mfano Fakharia, ametoka Zanzibar, Lipumba ametoka CUF, sasa mlitaka nifanyeje zaidi ya hapo, wakati kanuni inanitaka nizingatie uwiano, jinsia na makundi mbalimbali ya uwakilishi, na ndicho nilichofanya,” alisema.
Valerie Msoka, akizungumza nje ya ukumbi wa bunge alisema kila mjumbe alipewa uhuru wa kugombea lakini baadhi hawakufanya hivyo na sasa wanalalamika.
“Kama mjumbe hakujitokeza kugombea asilalamike, kwa kuwa demokrasia imefuatwa na watu hawakutaka kujitokeza. Ifike mahali  tutambue tuko hapa kwa ajili ya nini, badala ya kuendelea kusikiliza malalamiko kila siku, hatutafika,” alisema.
Alisema bunge limetawaliwa na siasa za vyama na ubinafsi, ambao hauwezi kumkomboa Mtanzania.

Watendaji wabovu waadhibiwe -Kinana


NA SULEIMAN JONGO
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ametaka wana-CCM kuwa wakali dhidi ya watendaji wabovu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama.
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akishuka kutoka kwenye tanki la mradi wa maji katika eneo la Tabata Kimanga, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wakati wa ziara yake, wilayani Ilala, Dar es Salaam, jana. Tanki hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 200,000 za maji litakapokamilika litahudumia wakazi wa maeneo wa Tabata Kisiwani na Tabata Kimanga. Picha zaidi.uk.18. (Na Bashir Nkoromo).

Ameagiza kusimamiwa miradi ya Chama na kutokubali wachache wanufaike zaidi kuliko CCM.
Kinana alisema hayo jana wilayani Ilala, Dar es Salaam, alipozungumza na wana-CCM kwa nyakati tofauti akiwa ziarani.
Alisema baadhi ya watendaji wa CCM na serikali kwa makusudi wamekuwa wakikwamisha maendeleo, ambayo ni kiunganishi kati ya Chama na wananchi wanaoendelea kukiweka madarakani.
Kinana alisema huu si wakati wa kuendelea kuwatazama watendaji wa aina hiyo, ambao wanadumaza maendeleo bali wachukuliwe hatua stahili na kwa wakati muafaka.
Katibu mkuu alisema ni vyema kila kiongozi akahakikisha anatekeleza wajibu wake kikamilifu ili kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM, iliyoahidi kutatua changamoto mbalimbali, zikiwemo za miundombinu, nishati, maji na afya.
Alitaka kila kiongozi, wakiwemo wa serikali na waliowekwa madarakani na wananchi, akajipima kabla ya kupimwa na wapiga kura au mamlaka yake ya uteuzi.
“Hatuko tayari kumuacha yeyote tunayeona anatupeleka kusikotakiwa au kwenda kwa kasi isiyoendana na malengo yetu. Wana-CCM kokote mliko hakikisheni mnawabana watendaji wabovu ili wafanye kile tulichoahidi kwa wananchi,” alisema.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya siku nne mkoani Dar es Salaam, alisema huu si wakati wa kuendekeza umangimeza na kutowajibika kwa kuwa Watanzania wanataka kuona maendeleo na utekelezaji ahadi.
“Watanzania wamechoshwa na maneno na ahadi zisizotekelezeka, wanataka vitendo. Tutawabana viongozi wanaoendekeza umangimeza badala ya kusimamia maendeleo na kuwatumikia wananchi,” alisema.
Alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakijisahau kwa kukaa ofisini, kwa kuwa wana uhakika wa kupokea mshahara, huku wananchi waliowapa uongozi wakitaabika na kuvuja jasho kutafuta maendeleo.
“Ikiwa tutatekeleza mkataba  tulioingia na wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, ni wazi Watanzania watatuamini tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani. Tukifanya tofauti na tuliyoahidi katika Ilani, tutambue watatushangaa na kutubeza,” alisema.
Kinana alisema CCM haiko tayari kuona kikundi cha watu kikiandaa mikataba mibovu, ambayo haikinufaishi Chama.
“Viongozi wa CCM wa ngazi zote simamieni miradi ya maendeleo kikamilifu. Sehemu iliyo na matatizo ya mikataba undeni tume na kufanya uchunguzi. Haiwezekani watu wachache kuingia mikataba mibovu isiyokinufaisha Chama,” alisema.
Alisema hayo baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Asaa Simba, kueleza Chama wilayani humo kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ya mikataba mibovu ya miradi.
Simba alimuomba Kinana kusaidia harakati za kuwapata wanasheria wa CCM kutoka makao makuu ili kusimamia urekebishaji wa mikataba hiyo.
“Moja ya changamoto tulizozikuta wakati tukiingia madarakani ni mikataba isiyoridhisha. Mfano hapa tulipo (makao makuu ya CCM Wilaya ya Ilala) fremu zinakodishwa kwa sh. 250,000 kwa mwezi kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na maeneo mengine. Mkataba huo ni wa miaka 35,” alisema.
Kinana alitembelea miradi ya maji na shule katika kata za Buguruni, Tabata Kisiwani na Gerezani. Leo atakuwa wilayani Temeke.
Wakati huo huo, CCM Wilaya ya Ilala imemuomba Kinana, kuingilia kati sakata la madereva wa bodaboda kuzuiwa kuingia katikati ya jiji.
“Ndugu Katibu Mkuu tunakuomba uingilie kati suala la madereva wa pikipiki kuingia katikati ya jiji kwa kuwa ni tatizo lililowagusa wengi, wakiwemo madereva na abiria,” alisema Simba.

Wabunge wajipanga kumng’oa Spika EAC



  • Wakerwa kumruhusu mumewe kuhudhuria Bunge
  • Rais Kenyatta atua kutuliza hali ya hewa, awasihi 

NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WABUNGE wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) leo wamepanga kumng’oa Spika wa bunge hilo, Dk. Margerth Ziwa, wakimtuhumu kwa mambo mbalimbali, ikiwemo dharau.
Wakizungumza na Uhuru baada ya Mwenyekiti wa Jumuia hiyo ambaye ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kuhutubia Bunge hilo, baadhi ya wabunge walisema wamekuwa wakililalamikia kwa muda mrefu mume wa Spika huyo waliyemtaja kwa jina moja la Babu kuhudhuria vikao vya bunge kama mbunge, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za bunge hilo.
Pia walilalamikia kitendo cha Spika kuwaajiri baadhi ya ndugu zake kwa kuwapa mikataba ya muda mfupi ya kufanya kazi kwenye bunge huku kukiwa na watu wengine wenye uwezo ambao hawapewi nafasi hizo.
Wabunge hao kutoka karibu nchi zote wanachama, walisema kipindi cha mashindano ya mpira wa  mabunge ya nchi wanachama yaliyofanyika  Uganda hivi karibuni, Spika huyo aliwapeleka wananchi wa kawaida kuchezea timu ya bunge la Uganda kama wabunge.
“Ni kweli leo lazima tumgo’oe spika kwa kuwa ameshindwa kufikia viwango vya kiutendaji na anatudharau wakati sisi tumepewa dhamana na nchi zetu kwa ajili ya maslahi ya Jumuia nzima na si mtu binafsi,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Hata hivyo, mmoja wa wabunge hao ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, aliliambia Uhuru kuwa Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, alimsihi mwenyeviti wa wabunge kutoka nchi wanachama kuzungumza nao ili wasimng’oe.
Akizungumza kwa lugha ya Kiingereza alisema: “Waandishi huko ndani Mwenyekiti wa Jumuia anamuombea spika aendelee kubaki kwenye nafasi yake lakini  sisi hatuko tayari kuendelea kufanya kazi naye. Kazi  ya kwanza tukayoifanya kesho (leo) kabla ya bunge kuanza ni kuhakikisha tunamng’oa.
“Kuong’olewa kwa spika ni mkakati wa wabunge wote hapa hakuna cha Mganda wala Mtanzania. Hili  ni jambo ambalo tumeazimia kwa pamoja kuwa lazima aachie nafasi hiyo ndipo kikao cha bunge kiweze kuendelea.”
Alisema kuna watu wenye uwezo wa kuongoza bunge hilo ambao ni wasikivu na kwamba hawaoni shida kumg’oa katika nafasi hiyo kwa ajili ya kumuweka mtu mahiri anayechukua ushauri anaopewa na wabunge.
Mkutano huo wa tano na kikao cha pili cha bunge hilo, kinafanyika katika ukumbi wa Bunge uliopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya EAC kwa wiki mbili.

Mzindakaya atema cheche katiba mpya


NA MWANDISHI WETU 
MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Chrisant Mzindakaya, amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutambua kwamba wanatunga katiba ya Watanzania na si watawala.  

Sambamba na hiyo, amepongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Ijumaa iliyopita kuwa ilikuwa dira ya majadiliano kwa lengo la kupata katiba bora itakayolinda Muungano.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mzindakaya alisema baadhi ya wanasiasa wametanguliza maslahi binafsi kwa ajili ya kujipatia madaraka badala ya uzalendo na maslahi ya taifa.
“Ni lazima watu watambue kuwa duniani kote watawala ni wa kupita, watakaa madarakani kwa kipindi kifupi na kuondoka, lakini wananchi wataendelea kubaki. Kwa hiyo tuunde katiba kwa maslahi ya taifa na si watawala,” alisema.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete, Mzindakaya ambaye aliwahi kuwa mbunge kwa miaka 44, alisema ilijaa uzalendo na kuitakia Tanzania amani, umoja, utulivu na usalama. 
Alisema hotuba hiyo ilionyesha dhamira ya dhati aliyo nayo Rais katika kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya itakayokuwa mwongozo kwa taifa kwa miaka 50 ijayo au zaidi.  
“Matakwa ya katiba mpya ni wazo la Rais Kikwete mwenyewe kwani alishasema kuwa wakati umefika wa kuwa na katiba mpya. Ndiyo maana hata hotuba yake ilikuwa na uchambuzi wa kisayansi wa namna katiba mpya inavyopaswa kuwa kiuchumi, kisiasa na kijamii,” alisema.
Hata hivyo, Mzindakaya alisema: “Nimeshangazwa na baadhi ya watu wanaoiponda hotuba ya Rais, watu hao akili zao zimeganda na wanaonekana kutaka mambo yao na si hoja. Duniani kote hotuba ya Rais huwa dira ya kuongoza nchi na katika suala hili la katiba, ndiyo dira ya kuongoza majadiliano kwenye bunge la katiba.” 
Alisema Rais Kikwete ameshamaliza kazi hivyo wanachopaswa kufanya wajumbe wa bunge hilo maalumu ni kuhakikisha wanalinda maslahi ya taifa ikiwa pamoja na kudumisha Muungano. 
Juu ya Muungano, Dk. Mzindakaya alisema serikali tatu ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu hakuna katiba ya Tanganyika, nchi ambayo baadhi ya wanasiasa wanaitaka. 
“Hivi kwa akili za kawaida, unaanza kuengeneza katiba ya Muungano wa serikali tatu wakati serikali mojawapo haipo? Ni jambo ambalo haliwezekani. Kama wana nia ya kufanya hivyo wanapaswa kwanza kuwa na Tanganyika ndipo waendele kwenye Muungano wanaoutaka.
Kama wanataka Tanganyika basi wanapaswa kuahirisha bunge mpaka Tanganyika izaliwe kwanza. Kuendelea na fikra hizo ni sawa kuota ndoto za mchana,” alisisitiza.

Wanachama wapeleka kilio CHADEMA


WAKATI kampeni zikishika kasi jimbo la Chalinze, baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wamekitosa chama hicho.
Viongozi walioihama CHADEMA na kujiunga CCM ni Katibu wa kata ya Msata, Mrisho Issa, Katibu wa Uhamasishaji, Nasibu Msakamali na  mjumbe Subira Mrisho.
Kwa nyakati tofauti walikabidhi kadi zao za CHADEMA kwa viongozi wa CCM kwenye mikutano ya kampeni jimboni Chalinze.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akiwapokea baadhi ya wanachama hao wapya alisema wamefanya uamuzi sahihi.
Mgombea wa CCM, Ridhiwani Kikwete, alikabidhi kadi kwa vijana 40 katika mashina ya wakereketwa waliojiunga na Chama na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Akizungumza na vijana wa Pongwe Kiona, aliahidi akiwa mbunge atahakikisha wanawezeshwa ili kupiga hatua katika maendeleo.
“Natambua shida zenu, naomba mjiunge pamoja kwenye vikundi ili mnufaike na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya kinamama na vijana,” alisema.
Alisema CCM imetoa heshima kubwa kwa vijana kwa kumteua kugombea ubunge, hivyo hawezi kuwaangusha, ikizingatiwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa.

Kiama cha wala rushwa chaja


VIONGOZI wa vijiji wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, hivyo kuwa chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji wametangaziwa kiama.
Wanadaiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kugawa ardhi holela bila kuwashirikisha wananchi, hivyo kuibua migogoro.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kihangaiko, Madesa na Pongwe Msungura, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitaka wananchi wasiwachague watu wa aina hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.
Nape alisema CCM haiko tayari kuona wakulima wakinyanyaswa na watu waliowachagua.
Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa mikubwa katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Mbeya na mingine ya Kanda ya Ziwa, hivyo ni lazima serikali ichukue hatua.
“Haiwezekani wakulima wateseke kwa kupoteza nguvu kwenye kilimo halafu wafugaji walishe mifugo yao na kutumia fedha kumaliza kesi.” alisema.
Alisema suluhisho ni kuweka mipaka ya ardhi kwa kuzingatia idadi ya watu na si mifugo.
Nape aliahidi kushirikiana na mbunge kuhakikisha serikali inamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mkulima Matogolwa Chamburi, alisema mwishoni mwa mwaka jana, shamba lake la mahindi liliharibiwa na ng’ombe na alipojaribu kupambana na mfugaji alishambuliwa.
Alisema alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mbwewe, lakini mkuu wa kituo alimtaka wakakubaliane na mfugaji ili wamalize kesi kwa kuwa itakuwa usumbufu.
Matogolwa alisema baada ya mvutano alilipwa sh. 40,000 na kulazimishwa kufuta kesi licha ya kutumia sh. 30,000 za nauli ya pikipiki kwenda na kurudi Pongwe.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alisema suluhisho la migogoro hiyo ni kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Sitta apangua mitego mikali


NA LILIAN TIMBUKA, DODOMA
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, jana alipangua hoja za mtego kuhusu uteuzi wa wenyeviti wa kamati za maridhiano za bunge hilo.

Wajumbe hao, asilimia kubwa kutoka Zanzibar na wale wa vyama vya upinzani, walionyesha hofu, ambayo ilitulizwa na Sitta baada ya kufafanua kuwa, uchaguzi lazima uzingatie Kanuni ya 55 (1).
Kwa mujibu wa wajumbe hao, kutokana na idadi iliyopo ambayo inautofauti kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa na wajumbe wengi ndani ya bunge, huenda wenyeviti wengi wakatoka katika Chama au Tanzania Bara.
“Sioni sababu ya ninyi kuwa na hofu, kinachoongoza hapa ni kanuni ambayo inapaswa izingatiwe; na imeeleza wazi, kama mwenyekiti atatoka Bara, makamu atatoka Zanzibar na inaeleza pia tuzingatie jinsia,” alisema Sitta.
Licha ya majibu hayo, baadhi ya wajumbe waliendelea kuomba mwongozo wakihoji suala hilo.
Sitta alisema uchaguzi hauwezi kubeba dhana za wajumbe wanazozifikiri bali utafuata sheria na kanuni, hivyo kila mjumbe ana haki ya kugombea katika kamati bila kujali anatoka kundi gani au jinsia.
“Nadhani mkifuata mwongozo wa kanuni mtafika kule mnakotaka kufika, na hofu hizi mlizoanza kuzionyesha zitaisha,” alisema.
Sitta alisema kamati zilizoundwa jana zinatarajiwa kuanza kazi ya kuchambua Rasimu ya Pili ya Katiba, Ijumaa wiki hii.
Alisema baada ya uchaguzi kukamilika, leo atatangaza majina ya viongozi wa kamati hizo na za Uandishi, Kanuni na Maadili.
Mwenyekiti alisema leo itaundwa Kamati ya Uongozi inayotokana na wenyeviti wa kamati zote. Kamati 12 za Maridhiano zenye wajumbe kati ya 52 na 53 kila moja zimeundwa, huku Kamati za Kanuni na Haki za Bunge na ya Uandishi, zikundwa na wajumbe 24 kila moja.
Sitta alisema uteuzi wa wajumbe katika kila kamati umezingatia uwiano wa wajumbe na jinsia na kwamba, wajumbe wa Kamati ya Uandishi na ya Kanuni na Haki za Bunge, ni wajumbe kwenye kamati zingine.


Hotuba za JK, Jaji Warioba kutikisa
Hotuba zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, zinatarajiwa kujadiliwa kesho bungeni.
Akijibu ombi lililotolewa na Julius Mtatiro, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Sitta alisema muda umetengwa wa kuzijadili hotuba hizo.

Mtatiro aliomba mwongozo kuomba hotuba hizo zijadiliwa kabla ya kazi za kamati hazijaanza ili kuondoa minong’ono inayoendelea miongoni mwa wajumbe.
“Mwenyekiti naomba mwongozo wako katika hili, binafsi naona ni vyema hotuba hizi mbili za Rais na ya Jaji Warioba, zijadiliwe na wajumbe kabla hawajaanza kazi,” alisema.
Alisema kuna dhana imejengeka miongoni mwa watu kuwa Rais Kikwete alijibu hotuba ya Jaji Warioba.
“Ili kuondoa haya yote, unaonaje na Jaji Warioba naye akaitwa tena aje ajibu kile kilichoelezwa na Rais,” alisema.
Sitta alisema haiwezekani akaitwa tena bungeni, bali kitakachofanyika ni kwa wajumbe kupewa muda wa kuijadili.

Wazazi yampongeza JK


Jumuia ya Wazazi ya CCM, imempongeza Rais Kikwete, kwa kutoa hotuba iliyozungumzia mambo muhimu kuhusu mustakabali wa taifa.
Katibu wa Wazazi, Seif Shaban Mohamed, alisema jana kuwa hotuba hiyo ilikuwa na mambo mazito, ambayo Watanzania wengine walikuwa hawafahamu.
“Tunaunga mkono hotuba ya Rais Kikwete kwa kuwa imefunua macho Watanzania wengi, kazi iliyobaki ni kwa wajumbe wa bunge kukaa na kuweka utaifa mbele ili tupate katiba,” alisema.
Alisema Rais Kikwete alihimiza mshikamano, amani na utulivu katika kupata katiba mpya, ambayo rasimu yake itajadiliwa na wajumbe.
Katibu alisema hotuba hiyo ilikuwa na mambo yenye uwazi na ukweli kwa kuzungumzia athari zilizojificha katika muundo wa serikali tatu
Kamati namba moja: 
Ummy Mwalimu (Mwenyekiti)
Profesa Makame Mbarawa (Makamu)
Kamati namba mbili :
Shamsi Vuai Nahodha (Mwenyekiti)Shamsa Mwangunga (Makamu)
Kamati namba tatu:
Francis Michael (Mwenyekiti)
Fatuma Mussa Juma (Makamu)
Kamati namba nne :
Christopher Ole Sendeka (Mwenyekiti)
Dk. Sira Ubwa Mwamboya (Makamu)
Kamati namba tano:
 Hamad Rashid Mohammed (Mwenyekiti)
Assumpter Mshama (Makamu)
Kamati namba sita:
Stephen Wasira (Mwenyekiti) 
Dk. Maua Abeid Daftari (Makamu)

Kamati namba saba:
Hassan  Ngwilizi (Mwenyekiti)
Waride Bakari Jabu (Makamu)
Kamati namba nane:
Job Ndugai (Mwenyekiti)
Biubwa Yahya Othaman (Makamu)
Kamati namba tisa: 
Kidawa Hamid Salehe (Mwenyekiti)
William Ngeleja (Makamu)
Kamati namba 10: 
Anna Abdalla (Mwenyekiti) 
Salmin Awadhi Salmin (Makamu)
Kamati namba 11:
 Anne Kilango Malecela (Mwenyekiti)
Hamad Massaun (Makamu)
Kamati namba 12: 
Paul Kimiti (Mwenyekiti) 
Sheiba Kisasi (Makamu)

Usafiri Moshi ovyo ovyo



  • Wananchi washindwa kusafiri
  •  Stendi yageuka uwanja wa soka

Na Rodrick Makundi, Moshi
USAFIRI katika mji wa Moshi na maeneo ya pembezoni, jana zilisimama kutwa nzima baada ya wasafirishaji kugoma kutoahuduma kwa madai ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani.
Mgomo huo ulianza jana alfajiri, baada ya wamiliki wa mabasi hayo kuyafungia, hali iliyosababisha kituo cha mabasi cha mjini Moshi kubaki wazi kwa muda wote wa mgomo.
Baadaye, madereva na makondakta wa mabasi, waligeuza kituo hicho kuwa uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu, kitendo kilicholazimu jeshi la polisi kuingilia kati.
Hatua hiyo ya jeshi la polisi ilidaiwa kuibua vurugu zilizosababisha gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, lenye namba za usajili T743 ADC, kurushiwa mawe na kusababisha kioo cha nyuma kuvunjika.
Chanzo cha mgomo huo kilidaiwa ni baada ya madereva kupinga kitendo cha askari wa usalama barabarani kuwakamata na kuwatoza faini kuokana na makosa mbalimbali, bila kuwapatia stakabadhi.
Mgomo huo uliwafanya abiria waliokuwa wanafanya safari zao kwenda  katika wilaya zote za Kilimanjaro na mkoani Arusha kukwama kwa takribani kutwa nzima huku wakishuhudia mpira wa miguu uliokuwa unachezwa kituoni hapo na madereva na makondakta hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madereva hao walisema kitendo hicho kinaashiria rushwa na kwamba fedha zinazotozwa hazifiki kunakohusika, badala yake kuishia mikononi mwa wajanja wachache.
Madereva hao waliwatuhumu baadhi ya maofisa wa polisi mkoani Kilimanjaro kwa kufanya mambo kinyume cha taratibu, hivyo kuchochea mgomo huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wasafirishaji katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA), Hussein Mrindoko, alidai kuwa kitendo cha  baadhi ya askari kugoma kutoa stakabadhi wanapotoza faini, limekuwa jambo la kawaida.
Mrindoko alisema wamiliki wa magari ya abiria wamekuwa wakiumizwa na faini zinazotozwa kwa zaidi ya mara tatu kwa kutwa kitendo ambacho kimegeuka kuwa mtaji kwa baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Kilimanjaro.
Kutokana na mgomo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alilazimika kuitisha kikao cha dharura na wadau wa usafirishaji pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama.
Kwenye kikao hicho, baadhi ya maofisa wa polisi waliokuwa wakituhumiwa, walijitetea kwa baadhi ya makosa waliyotuhumiwa nayo, akiwemo mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro, kudai kwamba alichukua hatua ya kumpiga mmoja wa wamiliki wa mabasi baada ya kutokea hali ya kutoelewana.
Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi katika Kituo Kikuu cha Mabasi Moshi, Henry Nguvumali, alipinga madai ya madereva na wamiliki wa mabasi ya abiria yaliyotolewa kwa mkuu wa mkoa dhidi yake.
Mkuu huyo wa kituo, alituhumiwa kuwa mlevi aliyepitiliza na kwamba amekuwa akifanya mambo yasiyoendana na maadili ya jeshi la polisi ikiwemo kujisaidia ovyo nyuma ya mabasi bila kujali umati mkubwa wa watumiaji wengine wa kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema wadau wote wanapaswa kuzingatia sheria kwenye majukumu yao ya kazi na  kuahidi kuchukua hatua dhidi ya askari waliobainika kukiuka maadili ya kazi na kutenda mambo kinyume cha taratibu.
Gama kwa upande wake, aliwasihi wamiliki wa mabasi ya abiria kurejesha huduma kwa kuzingatia kwamba kitendo cha kugoma kimeathiri uchumi wa watu na mkoa kwa jumla.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffari Michael, alisema kushindwa kutoa huduma za usafiri katika kituo hicho kumeisababishia hasara halmashauri hiyo. Alisema  Manispaa imekuwa ikikusanya sh. milioni 25 kwa mwezi hivyo, mapato hayo yatapungua.
Tayari Gama ameagiza SUMATRA kuandaa utaratibu wa vikao vya mara kwa mara vya wadau wa usafirishaji kwa ajili ya kuzikabili changamoto zinazojitokeza yakiwemo malalamiko ya wadau


Mkurugenzi Bodi ya Utalii ang’olewa


NA KHADIJA MUSSA
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk. Aloyce Nzuki, ameng’olewa katika wadhifa huo, kutokana na utendaji usioridhisha.
Add caption

Uamuzi wa kung’olewa Dk. Nzuki ulifikiwa jana baada ya awali Bodi ya Wakurugenzi ya TTB kuwasilisha mapendekezo wizarani kutaka aondolewe.Hata hivyo, kabla ya kufikiwa uamuzi huo jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alikutana na Bodi ya TTB kuzungumzia kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa kwake.
Kikao cha pamoja kilihudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya TTB, akiwemo Mwenyekiti, Charles Sanga, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamoud Mgimwa, Katibu Mkuu Maimuna Tarishi na Naibu Katibu Mkuu, Selestine Gesimba.
Kutokana na hoja zilizowasilishwa na bodi, Nyalandu aliridhia kung’olewa kwa Dk. Nzuki, ambaye atapangiwa kazi nyingine na nafasi yake kukaimiwa na Devota Mdachi.
Devota ni Mkurugenzi wa Masoko wa TTB. Nyalandu ameagiza mchakato wa kumpata mtendaji mwingine wa taasisi hiyo uanze mara moja na uwe umekamilika ndani ya siku 21.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao kilichofanyika wizarani, Sanga alisema mapendekezo ya kutaka Dk. Nzuki kuondolewa ni ya muda mrefu.
Alisema Dk. Nzuki ameshindwa kufanya kazi inayotakiwa, hivyo bodi ilipendekeza kwa waziri mwenye dhamana kuingilia kati kuiwezesha TTB kusonga mbele kwa ufanisi.
Sanga alisema katika utendaji kazi suala la uzalendo na utaifa ni muhimu likazingatiwa na kwamba, bodi itahakikisha inafanya kazi kwa ufanisi.
Nyalandu alisema ameridhia mapendekezo hayo baada ya kupokea barua iliyotiwa saini na wajumbe wa bodi ya TTB, ikimshauri amuondoe Dk. Nzuki.
Alisema azma ya serikali ni kuhakikisha sekta ya utalii inakua kwa kasi na kwamba, kupumzishwa kwa Dk. Nzuki hakuna maana kuwa amekosea, bali ni utaratibu wa kawaida serikalini.
Nyalandu aliagiza bodi kuitangaza nafasi hiyo ili Watanzania wa ndani na nje wenye sifa za kuomba wafanye hivyo ndani ya siku 21 kuanzia leo.
Aliitaka bodi kuhakikisha kasi ya kuutangaza utalii na vivutio vyake inaongezeka maradufu na asingependa kusikia majibu ya kushindwa na nchi jirani, ikiwemo Kenya

Wafanyakazi Shoprite wagoma


NA JUMANNE GUDE
WAFANYAKAZI wa maduka ya Shoprite ya jijini Dar es Salaam, wamegoma kuendelea na kazi wakishinikiza mwajiri awalipe stahili zao kabla ya kukabidhi kwa mmiliki mpya.
Taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo, zinasema maduka hayo ambayo ni maarufu kwa kuuza bidhaa mbalimbali, yameuzwa kwa mwekezaji mwingine na kwamba wafanyakazi wake bado hawajalipwa malipo mbalimbali hivyo kuamua kuingia kwenye mgomo.
Mgomo huo ulianza jana saa mbili asubuhi katika duka la Kamata, ambapo wafanyakazi wakiwa na mabango walilipuka na kuanza kushinikiza kulipwa fedha za likizo na matibabu.
Msemaji wa wafanyakazi hao, Bahati Kalolo, alisema mwajiri huyo amekuwa mkaidi kuwalipa haki zao na kwamba hata alipoitwa katika Baraza la Usuluhishi hakutokea.
Kalolo alisema wanamdai mwajiri wao huyo zaidi ya miaka minane, lakini haelekei kuwalipa na kwamba maduka hayo yameshauzwa kwa mmiliki mwingine.
Alisema wamefuatilia suala hilo hadi Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), lakini hakuna msaada waliopewa, hivyo kulazimika kuingia kwenye mgomo ili kushinikiza kupata ufumbuzi wa suala hilo.
“Hatufahamu huyu jamaa anataka kutuacha vipi, maduka haya yameshauzwa kwa raia wa Kenya na wiki ijayo atakabidhiwa lakini mpaka sasa hatujalipwa haki zetu,” alisema.
Mfanyakazi mwingine, Mohamed Athumani, alisema wanamtaka mwajiri huyo kutengeneza jedwali la kila mfanyakazi litakaloonyesha kiasi atakacholipwa.
Athumani alitoa ushauri kwa serikali kuwa wawe makini na wawekezaji wanaokuja nchini kutokana na tabia ya kuwanyanyasa wafanyakazi wazawa na kuhakikisha haki zao zinapaitkana.
Hata hivyo, waandishi walipomfuata mmiliki wa Shoprite, ili aweze kuzungumzia madai hayo, walifungiwa ndani ya chumba na badala yake askari ndio walioruhusiwa kuingia ndani kwa mwajiri huyo

Kinana: Ridhiwani hatafuti umaarufu


Na Mwandishi Wetu, Chalinze
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mgombea wa ubunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, hagombei kwa kutaka umaarufu bungeni au kwenye jamii bali ni kushirikiana na wakazi katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Kinana

Pia kimeahidi kushirikiana naye bega kwa bega atakapochaguliwa kushika nyadhifa hiyo katika kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa Chalinze.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo jana wakati akimnadi Ridhiwani katika kata za Mdaula, Ubena na Msolwa. Alisisitiza kuwa CCM iko tayari kushirikiana naye kwa sababu inaamini suluhisho la matatizo ya wakazi wa jimbo hilo ni kumchagua Ridhiwani.
“Ridhiwani si mgeni wa siasa, alianzia tangu utotoni hivyo hagombei kwa ajili ya kutafuta umaarufu wala kutaka utukufu. Mna kila sababu ya kuwa kifua mbele kwani ni mtu anayejua kero zote za jimbo na atakayetetea maslahi ya wananchi ikiwemo kusaidia matatizo yote yanayowakabili,” alisema.
Kinana alisema kwa sasa siasa za kukebehiana zimepitwa na wakati hivyo Ridhiwani ana uhakika kutokana na kujiuza kwa sera za Chama chake ambazo si za kubabaisha.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Ridhiwani alisema changamoto nyingi zinajirudia katika maeneo mengi ikiwemo migogoro ya ardhi, afya, elimu,  maji na vijana kuhitaji mitaji ili kujikwamua kiuchumi.
Alibainisha kuwa katika vipaumbele vyake endapo atachaguliwa atahakikisha anashughulikia makandarasi wa miradi ya maji na barabara ambayo mingi inakwamishwa au kutomalizika kwa wakati kwa ajili yao. Alisema makandarasi wasiotekeleza majukumu yao lazima wawajibishwe.
Pia aliahidi kuongeza zahanati katika kila kijiji ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Kwa  upande wa elimu, alisema atahakikisha anashirikiana na halmashauri kuongeza vyumba vya madarasa, maabara, kujenga matundu ya vyoo na katika shule za sekondari kuziwekea umeme ili  kuwawezesha wanafunzi kujisomea nyakati za usiku.
Kuhusu  kuwezesha vijana kujikwamua kuchumi, aliahidi kuzungumza na idara husika itakayoweza kuongeza mfuko wa fedha za mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kujiinua kimaisha.
Katika kilimo, alisema atajitahidi kuwasaidia wakazi hao kuondokana na kilimo cha jembe la mkono na kuwawezesha kutumia matrekta ambacho kitawaongezea tija.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawamba, ambaye ni mbunge Bagamoyo, aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kumchagua Ridhiwani kwa sababu ana uwezo wa kupigania matatizo yanayowakabili.
Awali, msafara huo ulifungua mashina mawili ya UVCCM Ubena Zomozi likiwemo la madereva boda boda na la wajasiriamali wauza koroshon

RC Mara afariki dunia


MKUU wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, amefariki dunia leo asubuhi. Habari zaidi zinasema Tuppa alifariki baada ya kudondoka akiwa kwenye ofisi za mkuu wa wilaya. Endelea kufuatilia uhuruonline na kwa undani zaidi kwenye gazeti la UHURU toleo la Kesho.

Thursday 20 March 2014

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, jimbola Chalinze, uliofanyika juzi katika uwanja wa Miembesaba. Katika uchaguzi huo unaofanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Said Bwanamdogo, CCM inawakilishwa na Ridhiwani Kikwete.

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, akimsaidia Ridhiwani kupanda jukwaa la wasanii wakati wa mkutano huo.

RIDHIWANI akiwasalimia wananchi waliohudhuria mkutano huo.

WANANCHI wakimshangilia Ridhiwani.

UZINDUZI WA KAMPENI ZA CCM CHALINZE

MWANACHAMA wa CCM aliyehamasika akionyesha picha ya Ridhiwani

Wednesday 19 March 2014

Kinana awasha moto Chalinze


NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakishindani na wapinzani bali na matatizo ya wananchi.
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimnadi mgombea wa Ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika jan, kwenye Uwanja wa  Miembesaba, Chalinze mkoani Pwani.(Picha na Bashir Nkoromo)

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo jana, alipozindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Chalinze, kwenye viwanja vya Polisi.
Uzinduzi wa kampeni za CCM ulipambwa na burudani zikiongozwa na kundi la TOT, ngoma za asili na Mwinjuma Muumini. Kinana na ujumbe aliofuatana nao aliingia uwanjani akiongozwa na msafara wa vijana waliokuwa wamepanda pikipiki.
“Tunatambua hapa hatushindani na upinzani, bali tunashindana na matatizo ya wananchi, kwa Chalinze atakayesimamia hilo ni Ridhiwani Kikwete,” alisema.
Alisema CCM ni Chama chenye kuleta majawabu kwa Watanzania, hivyo wananchi wasikubali kurubuniwa na wapinzani.
Kinana alisema kuna wapinzani ambao ni watu wa ovyo, wanaotembea na mitambo ya kutengeneza chuki, ugomvi na uongo miongoni mwa Watanzania.
Alisema baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikitembeza bakuli kuwataka wananchi kuvichangia, badala ya kuwaletea maendeleo.
Katibu Mkuu aliyemnadi Ridhiwani kwa wananchi, alisema ni mgombea kijana atakayeweza kukaa na vijana kutatua kero zao kwa karibu kuliko mtu mwingine.
Kutokana na hilo, aliwaomba wananchi wamchague kwa kura nyingi za kishindo.
Aliwaomba vijana kuwa karibu na Ridhiwani kwa kuwa CCM inajipanga kuhakikisha kazi zote za ukandarasi wanapatiwa, hivyo kwa utaratibu utakaopangwa, yeye ndiye atakuwa kiunganishi.
“Chagueni mbunge atakayetatua matatizo ya wananchi, atakayekwenda kuungana na asilimia 74 ya wabunge wa CCM kufanya kazi za wananchi,” alisema.
Kinana alisema CCM inatambua matatizo ya Chalinze, yakiwemo ya maji, ambayo Ridhiwani atakuwa na nafasi ya kuendeleza yaliyoachwa na aliyekuwa mbunge Said Bwanamdogo, aliyefariki dunia  hivi karibuni.
Alisema CCM imefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, ambapo kuna ongezeko la wahitimu wa vyuo vikuu.
Katibu Mkuu alisema wakati Rais Jakaya Kikwete, anaondoka madarakani idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu itafikia 200,000.
Alisema serikali imejipanga kukabiliana na tatizo la uhaba wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na kwamba, dawa za serikali zitagongwa nembo maalumu ili kudhibiti wizi.
KAMPENI ZA KISTAARABU
Awali, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM itaendelea na kampeni za kistaarabu.
Hata hivyo, alisema waliozoea fujo wakithubutu kufanya hivyo hawatavumiliwa.
“Tunajua ni wasindikizaji lakini katika kusindikiza wakitufanyia fujo watakiona cha mtema kuni lakini tumejipanga kufanya kampeni za kistaarabu,” alisema.
Alisema CHADEMA imeanguka na kilichobaki ni kufanya hitima na kwa kuwa haijajua anguko lake linatokana na nini, itaendelea kushindwa.
Nape alimuahidi Kinana kwamba, Aprili 7, mwaka huu, atampelekea zawadi ya ushindi wa CCM jimboni humo kwa asilimia zaidi ya 90. Uchaguzi utafanyika Aprili 6.
Alisema Ridhiwani anakubalika, hivyo hakuna shaka ya kutwaa jimbo hilo kwa kuwa ni la CCM.
KAULI YA MAMA SALMA
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wilaya ya Lindi Mjini, na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, alisema Ridhiwani ni kijana mwenye maadili, hivyo anatosha kuwa mbunge wa Chalinze.
“Nimekuja kwa kofia mbili, kwanza mzazi, maana chereko na mwenye mwana, Ridhiwani mwanangu amelelewa ni kijana mzuri mwenye maadili.
“Pili ni MNEC wa Lindi Mjini, ndugu zangu, CCM ndiyo Chama. Msijaribu kuonja sumu kwa kuwa haionjwi, mchagueni Ridhiwani awe mbunge wa Chalinze, mpeni ushindi wa kishindo,” alisema.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alimnadi Ridhiwani akisema ni kijana aliyelelewa kwenye maadili, hivyo hana shaka.
Aliwasihi wafugaji wa asili ya kimasai wamchague Ridhiwani kwa kuwa anayetafutwa ni mbunge na si kiongozi wa  kimila.
“Hapa tunafanya kampeni ya kumchagua mbunge si kiongozi wa kimila, hivyo msihadaike na mgombea wa CHADEMA kwa kuwa hatoshi ubunge, labda kiongozi wa kimila,” alisema.
Sendeka akiimba taarabu, alisema Ridhiwani ni kada aliyeiva na anatosha kuwa mbunge wa Chalinze.
Meneja wa Kampeni, Steven Kazidi, ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, alisema Ridhiwani ni biashara inayouzika, hivyo ushindi ni jambo la uhakika.
Alisema Ridhiwani ni kiongozi aliyeanzia Chipukizi, akawa kiongozi wa UVCCM katika ngazi mbalimbali za mkoa na taifa na sasa ni MNEC, hivyo ana historia katika Chama.
Imani Madega, ambaye alishindwa na Ridhiwani katika kura ya maoni ndani ya Chama, alisema kura hazikutosha na sasa wafuasi wake na wana-CCM wakipiganie Chama.
“Kura hazikutosha, uongozi unapangwa na Mungu, nimegombea mara tatu jimbo la Chalinze lakini sikushinda kwa kuwa Mungu hajapenda, hivyo tumuunge mkono Ridhiwani, tuondoe vinyongo tukunjue nyoyo, tukipiganie Chama,” alisema.
RIDHIWANI ALONGA
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, uliohudhuriwa na umati, Ridhiwani aliahidi neema kwa wananchi wa Chalinze.
Aliahidi endapo atashinda ubunge, jambo la kwanza atakalofanya ni kuhakikisha Shule ya Msingi Machala, iliyoko kata ya Mkange, inajengwa upya kutokana na kutokuwa na hadhi, kwa kuwa ina darasa lililojengwa kwa udongo na kuezekwa nyasi.
Kwa kushirikiana na wananchi alisema kutawekwa utaratibu wa mpango bora wa matumizi ya ardhi ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Tutatenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kila upande uweze kuendesha shughuli zake katika mazingira salama bila migogoro,” alisema.
Ridhiwani alisema wafugaji katika mikutano yake ya kampeni wamempa cheo cha Oleogwanan, ambacho anaamini atakitumia kukaa pamoja nao kutatua changamoto hiyo.
Aliahidi atahakikisha anavalia njuga suala la afya ya uzazi kwa kinamama na watoto, kwa kuboresha huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya.
000

Kificho amkana Warioba


NA EPSON LUHWAGO
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, amemkana Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na baraza.
Kificho, ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema hayo jana, siku moja baada ya Jaji Warioba kuwasilisha bungeni Rasimu ya Katiba.

Jaji Warioba alisema mapendekezo yenye mwelekeo wa kuwepo serikali tatu yalitolewa pia na Baraza la Wawakilishi, lililopendekeza kuwe na mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 jana, Kificho alisema waraka uliotolewa na Baraza la Wawakilishi haukupendekeza hivyo, bali hiyo ni tafsiri ya Jaji Warioba na tume.
“Tulichosema katika waraka ule juu ya muundo wa Muungano ni kwamba, kutokana na Baraza kuwa la mchanganyiko, wajumbe kutokana na vyama vyao (CCM na CUF) hatutoi pendekezo lolote kwa kuwa kila upande una maoni yake,” alisema.
Alisema ndani ya Baraza la Wawakilishi, CCM inataka muundo wa sasa wa serikali mbili, wakati CUF haina msimamo kamili kwa kuwa kuna wakati inataka serikali tatu na mwingine serikali mbili.
Kificho alisema katika waraka wa baraza uliowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hakuna sehemu inayoeleza kuwe na serikali tatu bali hiyo ni tafsiri ya tume.
Alisema alikuwa mjumbe wa Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 iliyokuwa na wajumbe 22 na katika suala la serikali tatu, wajumbe tisa, akiwemo yeye na Profesa Haroub Othman (sasa marehemu) walipinga.
Kwa mtazamo wake, Kificho aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, serikali tatu hazikubaliki kwa kuwa uwepo wake ni kuvunja Muungano.
“Serikali tatu ni kuvunja Muungano, ikiwa hivyo, tutakuwa na serikali mbili zenye nguvu na ile ya Muungano itakuwa dhaifu inayoelea elea tu,” alisema.
Alisema katika miaka 50 ya Muungano kuna mambo mengi yamefanyika, ikiwemo Watanzania kuwa wamoja na wanaoishi kwa amani na mshikamano.
Hata hivyo, alisema kuna kero kadhaa ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili kudumisha Muungano na kwamba,
yaliyotajwa kwenye rasimu kuwa changamoto au upungufu, yanazungumzika na kupatiwa ufumbuzi, lengo likiwa kuufanya Muungano kuwa imara.
KINGUNGE AMSHANGAA
Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale -Mwiru, ameijia juu tume kwamba imefanya kazi ambayo haikutumwa ya kupendekeza serikali tatu.
Kingunge ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema jana kuwa, tume imekiuka hadidu za rejea, ambazo mojawapo inataka kulinda na kudumisha Muungano, kwa kuwa mapendekezo yake ni ya kuuvunja.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na TBC1 jana, alisema ameshangazwa na tume chini ya Jaji Warioba, kwa kukiuka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Warioba na wenzake walipewa kazi ya kuwauliza wananchi watoe maoni  juu ya katiba mpya kwa lengo la kulinda na kudumisha Muungano. Wameacha waliyotumwa na kutuletea wanayoyataka. Hata katika uwasilishaji rasimu amejikita zaidi katika yale wanayoyataka na ya wananchi wameyaweka pembeni.
“Tume iliambiwa izingatie uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haikuheshimu hayo na matokeo yake imependekeza shirikisho lenye washirika wawili, ambao ni Zanzibar na Tanganyika,” alisema na kuongeza:
“Hawazungumzii Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, badala yake Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo zilifutika kwa kuungana ili kuwa na moja kubwa zaidi. Wanafufua jamhuri mbili, wanapata wapi mamlaka hayo?”
Alisema haiwezekani kuwa na nchi tatu ndani ya taifa moja. “Kwa vyovyote vile, huwezi kuwa na mtu mwenye uraia wa nchi mbili katika nchi tatu.
“Ilichokifanya tume, badala ya kujenga imebomoa. Kama ni kero hata kaya ina kero zake, huwezi kusema kwa kuwa mimi na mke wangu tuna ugomvi basi tuachane, hiyo si sahihi.
“Matatizo yanaletwa na wanadamu na watu wa kuyatatua ni wanadamu wenyewe. Vivyo hivyo, hata kwa suala la Muungano kero zilizopo zimesababishwa na watu, hivyo ni watu wenyewe ndio wa kuzitatua,” alisema.
Alisema kwa kupendekeza muundo wa serikali tatu, tume ya Warioba imeshindwa kutafakari matokeo na athari zinazoweza kujitokeza.
Kingunge alisema ilichopaswa kufanya tume ni kuziainisha kero zilizopo na kutoa njia ya kuzitatua ndani ya Muungano uliopo na si kuleta pendekezo la kuwafarakanisha wahusika.
Alisema wamesikia yaliyomo ndani ya  Rasimu ya Katiba, hivyo kazi ni kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutafakari kwa kina na kuandika katiba.
Kingunge aliasa wajumbe kulinda na kudumisha Muungano na kutambua wao ni nani, wametoka wapi, wako wapi na wanataka kwenda wapi.
“Tukishajitambua na tukaelewa kwa kina historia ya Muungano, tusiingie mahali tukafanya uamuzi ambao utatufanya tujute siku zijazo.
“Kitendo cha Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964 kilikuwa cha kihistoria na cha kimapinduzi. Lengo lilikuwa tuwe na taifa moja kubwa na lenye nguvu. Miaka 50 imepita tunataka kuuvunja, tunakwenda wapi?” alihoji.
Alisema baada ya miaka 50 ya Muungano, uamuzi wa kuwa na katiba mpya ni muafaka lakini inayotakiwa ni yenye kulinda Muungano na si kuuvunja.