Saturday, 18 April 2015

Viongozi wa mitaa kuingizwa darasani


NA MARIA AROPE, DODOMA
KUFUATIA viongozi wa ngazi ya chini kutopewa semina elekezi na miongozo kabla ya kuanza, kazi shirika lisilo la serikali mkoani Dodoma la NGONEDO linatarajia kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali za vijiji 1,580.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mratibu wa shirika hilo, Edward Mbogo, alisema viongozi hao watatoka katika vijiji 42 ambapo wananchi 350,000 watanufaika.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo itaanza kutekelezwa katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa.
“Ili kuweza kufuatilia utekelezaji wa mradi na kama iwapo halmashauri za vijiji husika zinafanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu na mafunzo ya utawala bora waliyoyapata kutoka NGONEDO vijiji vilivyo ndani ya mradi vitapatiwa nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi,” alisema
Alifafanua kuwa vijiji  hivyo vitanufaika na kupatiwa vifaa na samani za ofisi vyenye thamani ya sh. milioni 13.6 kwa mkoa mzima.
“Miongoni mwa vifaa ambavyo watanufaika navyo ni pamoja na mafaili, vifaa vya ofisi vya aina mbalimbali vya kufanyia kazi  na kabati za kuhifadhia nyaraka, masanduku la maoni pamoja na mbao za matangazo,” alisema.
Alisema vifaa hivyo ni kwa ajili ya kukuza ufanisi na kuimarisha utawala bora katika shughuli za utendaji kazi.
Mbogo alivitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kuwa Sejeli, Mbande, Vilundilo, Lupeta, Bumila, Makutupa, Kingiti na Lukole.
Alisema mradi huo pia utatoa mafunzo ya utawala bora kwa viongozi na wanachama wa NGONEDO ili kuratibu michakato ya utawala bora katika maeneo yao kama asasi za kiraia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru