Monday, 15 June 2015

Uandikishaji wapigakura
Mwanza waingia dosari

KAZI ya uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu, mkoani hapa, imeingia na dosari, baada ya wananchi kuleta fujo, hali iliyosababisha polisi kuingilia kati kutuliza ghasia hizo.
 Tukio hilo lilitokea juzi alfajiri, katika kituo cha Shule ya Sekondari Nganza, Kata ya Mkolani, mjini hapa, ambapo mahudhurio ya wananchi yalikuwa makubwa, hivyo kusababisha kusukumana katika foleni.
 “Huu sio uungwana hata kidogo, haiwezekani nimeamka alfajiri nije kujiandikisha, napanga foleni, halafu mtu anakuja na kutaka kukaa mbele yangu, lazima tutazipiga, alisikika akisema mwananchi mmoja.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamalango, Ndaki Lugiko, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kudai kuwa zilisababishwa na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino, ambao walilazimisha waandikishwe kwa madai ya kuwahi mitihani.
Alisema lilitokea kundi  la zaidi ya watu 300, wakitaka kuandikishwa, hali iliyosababisha  wananchi  kukataa na kuwataka wapange foleni.
Katika kata hiyo, wananchi waliitaka tume kuongeza mashine za BVR kwa kuwa mwitiko wa wananchi ni mkubwa, huku mashine hizo zikishindwa kustahimili idadi hiyo ya watu.

Mmoja wa wananchi, Lernad Lambati, alisema ili kupata kitambulisho wanachukuwa muda mwingi kutokana na upungufu wa mashine, hivyo kuathiri  shughuli za mtu mmoja mmoja na serikali kwa jumla katika uzalishaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru