Awataka wanaoamini wasambaze ujumbe
NA MWANDISHI WETU
ASKOFU
Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp
Kardinali Pengo, amesema msimamo wake kuhusu katiba inayopendekezwa, uko pale
pale na ametaka wanaoamini alichosema, wasambaze ujumbe wake kwa wengine.
 |
| Muadhama Polycarp
Kardinali Pengo |
Akizungumza
na Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), hivi karibuni, Askofu Pengo
alitoa wito kwa waumini kuachwa huru wafanyeuamuzi kuipigia kura ya ndiyo au
hapana katiba hiyo, badala ya
kushinikizwa na viongozi wa dini.
Aidha,
alisema kamwe hawezi kubadili kile alichosema, kwani ni ukweli anaouamini na
alishaweka hilo wazi.
Askofu Pengo alisema hayo jana, wakati wa ibada Maalumu ya Shirikisho la Kwaya
Katoliki (SHIKWAKA), iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Kipawa, jijini Dar es
Salaam, ambako kwaya zaidi ya 100 zilishiriki.
“Jana (juzi), baada ya ibada kule Kurasini, walikuja waandishi wa habari na
tukaanza kujadiliana na baadaye nilipomaliza wengine kisirisiri walijadili kwa
nini sikusema chochote kuhusu katiba inayopendekezwa, sasa ndugu zangu niseme
mara ngapi?” alihoji.
“ Hivi ni nani anaweza kufikiria naweza kubadili maneno niliyosema, leo niseme
kweli na kesho hapana. Nitakuwa mtu wa aina gani wa kubadili maneno na
misimamo,”alisema.
Alifafanua kuwa alishasema ukweli anaoujua, hivyo hana sababu ya kuurudia na
kwamba kufanya hivyo ni kutafuta ugomvi.
"Yale
niliyosema kuhusu suala hilo nimesema mara moja na ni mara moja tu basi,’’
alisisitiza.
Askofu Pengo aliwataka waumini na wasio waumini waliomsikia na kukubaliana na
aliyosema, kuwa ni wakati wao kuendeleza taarifa hiyo kwa kusambaza sehemu mbalimbali.
Akirejea
habari za kufufuka kwa Yesu, alisema kusambaza msimamo wake kutaenea kwa watu
wengi zaidi, kwani ndivyo injili ya ufufuko wa Bwana Yesu ilivyoenea kwa Petro,
ambaye awali wakati wa mateso ya Yesu, alimkana, lakinibaada ya kufufuka
alisambaza taarifa hizo.
Askofu Pengo alisema mashemasi kama Filipo,Stephano na wengine, hawakumwachia
Petro kusambaza ufufuko wa Bwana Yesu, ila kila walipokwenda walitamka kuhusu
ufufuko na hakukuwa na haja ya kumwita Petro kuelezea ufufuko huo.
Alisema wasingefanya hivyo injili isingefika duniani kote.
“Hivyo
hivyo, wale walioamini niliyosema kuhusu msimamo wangu wa katiba inayopendekezwa,
waendelee kusambaza kila wanapokwenda kwa manufaa ya nchi,” alisisitiza.
Alisema ndivyo inayofundishwa na fumbo la ufufuko wake Yesu kuwa jambo jema
halitegemei mtu mmoja kurudia rudia, kwani atakera watu.
Askofu
Pengo alisema anapoongelea tamko lake kuhusu katiba si kwamba, anataka kugeuza
nafasi ya ibada kuwa mahali pa kutangaza siasa au shughuli za kijamii, bali
neno lolote analofanya ni ukweli wake na hatobadili.
Alitaka waumini kusimama na kusema potelea mbali katika kusimamia ukweli wa
kile wanachoamini kwa kuwa jasiri bila kuogopa.
Vitendo
vya ugaidi
Aidha,
Pengo alizungumzia tukio la ugaidi nchini Kenya, lililosababisha vifo vya watu
zaidi ya 147 na kusema hakuna aliyefikiria kuwa nchi hiyo inaweza siku moja kuzingirwa na watu na
kufanyika mauaji yenye msimamo wa imani za dini.
Alisema ingawa nchi hiyo ilikuwa na malumbano kadhaa, lakini si dini. Alisema
tukio hilo halipendezi si kwa Waislamu wala Wakristo.
“Tumwombe Kristo atuponye na kutuepusha na balaa hilo na yasiendelee kutokea
kwa jirani zetu, huku kila mmoja akihakikisha kuwa na ujasiri wa kubaki na
msimamo wetu,’’ alisema.
Waraka wa maaskofu
Mwezi uliopita, Askofu Pengo wakati akifungua
mafungo ya WAWATA, yaliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam,
alikosoa waraka wa maaskofu kupitia Jukwaa la Kikristo, uliotaka waumini kupiga
kura ya hapana kwa katiba inayopendekezwa.
Alisema
kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawana uwezo wa kufanya uamuzi sahihi.
Awali,
Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi
katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma katiba inayopendekezwa na
kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya hapana.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste
Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Waliompinga Pengo
Baada ya Askofu Pengo kutoa msimamo wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima, alimkashifu na kumtuhumu kusaliti viongozi wenzake wa
Kikristo, kitendo kilichosababisha kukamatwa na kuhojiwa.
No comments:
Post a Comment