Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Wednesday, 22 April 2015

Watumishi mafisadi kitanzini  •  Serikali yaibuka na mwongozo mpya
  •  Tume ya Maadili yapewa meno makali

NA WILLIAM SHECHAMBO
SERIKALI imeendelea na mikakati ya kuwadhibiti viongozi wa umma wanaokiuka maadili na kushiriki kwenye vitendo vya wizi na ufisadi, ambapo sasa imeunda mwongozo mpya utakaotumika kuwabana.
Mwongozo huo ambao unatajwa kuwa suluhisho na mwarobaini wa watumishi wezi na wanaokwenda kinyume, pia utaipa meno zaidi ya kiutendaji, Sekretari ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa sasa sheria na kanuni zinazoongoza maadili ya viongozi wa umma, lakini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makusudi ama kusahau, baadhi ya viongozi wamekuwa wakizipuuza,  hivyo kusababisha matatizo ya kimaadili, hususan kuibuka kwa vitendo vya kifisadi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, mwongozo huo uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utaanza kutumika kwenye mwaka wa fedha 2015/2016.
Mwongozo huo utaanza kutumia rasmi kabla ya kufanyika kwa matukio makubwa nchini, ikiwemo kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, ambao vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili vimekuwa vikishamiri.
Akizungumza kwenye warsha ya wadau ya kujadili rasimu ya mwongozo huo, Dar es Salaam, jana, Kapteni Mkuchika, alisema serikali ina nia madhubuti ya kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili.
Alisema kupitia mwongozo huo, jitihada za serikali kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025, zinazosisitiza uongozi bora na utawala wa sheria, zinapewa nguvu kutokana na uwepo wa programu maalumu zinazohamasisha maadili  katika kila idara ndani ya sekta za umma na binafsi.
Mkuchika alisema mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaoota mizizi kote nchini, yanahitaji ushirikiano wa sekta zote, wananchi na asasi za kiraia,  ambapo adui mkubwa kati ya wengi ni rushwa na ufisadi, ambao kwa kiasi kikubwa unatekelezwa na viongozi wa umma.
Alisema maadili ya viongozi wa umma ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kukuza heshima ya taifa, hivyo serikali inafanya kila linalowezekana kutoa uwezo kwa Sekretarieti ya Maadili na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili matatizo hayo kutoweka nchini.,
Waziri huyo alisema nchi ilitikiswa na vitendo vinavyotokana na mmomonyoko wa maadili ya viongozi wa umma katika kipindi kifupi kilichopita, hali iliyoliletea aibu taifa na kuilazimu sekretarieti ya maadili kuwahoji watuhumiwa.
Waziri Mkuchika alisema ni lazima somo la maadili likaingizwa kwenye mitaala ya elimu kuanzia  shule za msingi mpaka elimu ya juu, ili kukomesha tatizo la ukosefu wa maadili kwa jamii, kwasababu utaratibu uliokuwa unatumika awali wa kupeleka vijana wote JKT kuwafundisha maadili kwa nyakati hizi hauwezekani.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema taasisi yake haitaendekeza vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kiongozi yeyote wa umma awapo kazini au atakapostaafu.
Alisema tangu kupatikana Uhuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kujenga na kukuza uadilifu kwa viongozi wa umma na sekta ya umma kwa kutumia sera, sheria, kanuni na miongozo, ukiwemo unaotarajiwa kutumika hivi karibuni.
Jaji Salome alisema kutumika kwa mwongozo huo ni mwendelezo wa juhudi hizo za serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo wakati huu wa kuelekea uchaguzi, viongozi husahau maadili na kufanya mambo kwa akili zao.
Alisema watapambana na kila kiongozi anayepotoka kimaadili kwa kutumia miongozo, kanuni na sheria, ili Tanzania iwe mahali salama kuishi kwa kuzingatia haki na usawa.
Aidha, alisema ili kuipa ‘meno’ sekretarieti ya maadili, serikali itaona namna ya kufanya  kuiruhusu imshitaki mtuhumiwa moja kwa moja mahakamani, wakiwemo wa ufisadi, badala ya kusubiri ruhusa kutoka kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP).
Sambamba na hilo, Mkuchika alisema Sekretari hiyo ambayo awali ilikuwa ni kitengo kidogo cha maadili ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), itapewa hadhi ya kuwa Tume, ili  ijitegemee  kama ilivyo kwa TAKUKURU.
“Taasisi hii ni muhimu sana, awali ilikuwa kitengo tu ndani ya jeshi; tukaona umuhimu wake tukakimegua ,ikawa na hadhi hii, sasa tumeona umuhimu wake zaidi kwa maendeleo ya maadili ya viongozi nchini, hivyo inabidi iwe tume, kama ilivyo TAKUKURU,” alisema Mkuchika. 

Hali ya mazingira inatisha- Dk. Bilal


NA MWANDISHI WETU 
UHARIBIFU wa mazingira nchini umezidi kuongezeka hivyo kutishia kutoweka kwa rasilimali na viumbe hai muhimu na kuchochea ongezeko la umasikini.  
Miongoni mwa athari za uharibifu huo wa mazingira ni kuwepo kwa athari kubwa kwa sekta tegemeo kwa uchumi wa nchi na maisha ya binadamu kama kilimo, uvuvi, utalii na madini.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania ikiwa moja ya nchi zinazoendelea, imekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kwamba hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la umasikini. 
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya uharibifu wa mazingira na umasikini. Kadri hali ya umasikini inavyoongezeka, ndivyo pia uharibifu wa mazingira unavyoongezeka,” alisema.
Dk. Bilal alisema ripoti hiyo inaonyesha kwamba ongezeko la uharibifu wa mazingira nchini linatokana na kuendelea kufyekwa kwa misitu, kuharibiwa kwa vyanzo vya maji, uchomaji moto na kuzagaa kwa taka ngumu. 
Sababu zingine, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni uchafuzi wa maji unaotokana na utiririshaji wa maji machafu ya viwandani na nyumbani na upotevu wa baioanuai.
Mbali na sababu hizo, Dk. Bilal alisema ongezeko la hali hiyo linaashiria kuwepo kwa upungufu katika kubuni, kutekeleza na kusimamia sheria, kanuni, mikakati na programu zilizowekwa kwa ajili ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira. 
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais aliziagiza taasisi za serikali na wadau kuhakikisha mazingira yanalindwa na wakati huo huo hatua kali zinachukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na uharibifu wa mazingira. 
“Mazingira ni mhimili wa sekta za uzalishaji kama vile kilimo, utalii, uvuvi na madini. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha mazingira na maliasili zetu zinatumika katika njia endelevu kwa kuzingatia uwiano mzuri kati ya matumizi ya rasilimali,” alisema.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhandisi Dk. Binilith Mahenge, alisema kila mwaka nchini takriban hekta 400,000 za misitu zimekuwa zikipotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya kuni na mkaa. 
Sambamba na hilo, Dk. Mahenge alisema kati ya mwaka 2000 na 2011 kumekuwa na ongezeko la matukio ya uchomaji moto ambapo yaliyoripotiwa ni 1,123,000. Matukio hayo yameripotiwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Tabora, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro. 
Pia, alisema uharibifu wa mazingira unachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya majitaka katika miji mikubwa. 
Alisema asilimia 50 ya miji mkubwa nchini ina mifumo ya majitaka, ambayo hata hivyo haitoshelezi kwa kuwa inahudumia asilimia nane tu ya wakazi wa maeneo hayo.
Akitoa neno la shukrani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema ripoti hiyo imewazindua wadau wengi, hivyo ni wajibu wa kila sekta kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele. 
Alisema ni wazi kwamba uharibifu wa mazingira na umasikini ni chanda na pete hivyo jitihada za maskusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda mazingira kwa lengo la kuoresha maisha wa binadamu na viumbe hai.
“Suala la usimamizi wa sheria, sera, kanuni, taratibu na programu za hifadhi ya mazingira ni suala ambalo halina mjadala. Hatuna budi kuzisimamia ili kulinda mazingira na wakati huo huo kuchukua hatua hali dhidi ya wanaoharibu mazingira,” alisema. 
Nyalandu alisema ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa mazingira, sheria na sera zilizopo hazina budi kufanyiwa mabadiliko na kutoa adhabu kubwa kwa wale wanaokiuka.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na mawaziri Samuel Sitta (Uchukuzi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi Maalumu), Samia Suluhu Hassan (Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano) na Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele.
Pia walikuwepo makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa wizara na washirika wa maendeleo wakiwemo kutoka mashirika ya maendeleo ya Canada (CIDA) na Denmark (DANIDA).

Majambazi yavamia kanisani na kuiba


Na Clarence Chilumba, Ruangwa
WATU watano wamevamia na kuvunja madirisha ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Malolo na kuiba chombo kinachotumika kuhifadhia ekaristi takatifu (TABERNACULO).
Imeelezwa kuwa majambazi hayo yalidhani chombo hicho kimetengenezwa kwa dhahabu.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 usiku, baada ya majambazi hayo kuvunja madirisha ya kanisa hilo.
Kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa makongwe na yenye historia kubwa hapa nchini, ambalo lilijengwa mwaka 1939.
Paroko wa kanisa hilo, Theophan Membe, alisema siku ya tukio alikuwa Lindi kuhudhuria misa takatifu ya mapadre wa jimbo la Lindi, iliyoongozwa na Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Bruno Ngonyani.
Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kigango cha Malolo, Cleophas Nnonjela, na badaye walitoa taarifa polisi.
Membe alisema parokia ya Malolo ni miongoni mwa parokia zilizotoa wasomi wengi mkoani Lindi kutokana na historia yake.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Roma za kanisa hilo, sehemu inayoibiwa Tarbenaculo, ukristo hufa mpaka wahusika walioiba kifaa hicho watakapokiri kuwa wameiba.
Membe alisema baada ya wahusika kukiri kama wameiba, askofu wa jimbo anaondoa dhambi ya mauti kutoka kwa waumini kwenda kwa wezi hao.
Alisema kutokana na kuibiwa kifaa hicho, waumini wa kigango hicho watakosa baadhi ya huduma ikiwemo ibada ya Jumapili, misa ya kila siku asubuhi, misa ya katekista na upigwaji wa kengele zinazoashiria saa kwa waumini.
Alisema katika kipindi hicho huduma za ubatizo, kipaimara, komunio takatifu, kitubio, misa za mazishi, mpako kwa wagonjwa, sherehe za ndoa na masuala yote ya msingi yanayohusu Kanisa Katoliki hayatakuwepo.

Wasomi wawaonya wanasiasa


NA KHADIJA MUSSA
WANASIASA wametakiwa kutotumia changamoto za Muungano kama mtaji katika majukwaa yao.
Hata hivyo, watu wanaopinga Muungano wametakiwa kusoma historia yake na kufahamu sababu za kuanzishwa kwa kuwa wengi wao wanakosa hoja za msingi.
Pia, serikali imepongezwa kwa kupiga hatua katika ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Uhuru baadhi ya wasomi waliipongeza serikali kwa kupiga hatua za kimaendeleo katika kipindi cha miaka 51 ya Muungano.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, aliwaasa wanasiasa kudumisha Muungano kwa kuwa unafaida kubwa kwa taifa.
Alisema changamoto za Muungano zilizopo zisitumike vibaya kutaka kuuvunja bali uimarishwe kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Bakari alisema mwarobaini wa kutatua changamoto za muungano ni kupitishwa kwa katiba inayopendekezwa kwa sababu inatoa muongozo mzuri.
Hata hivyo, alitoa rai kwa viongozi walioko madarakani kuhakikisha wanawaongoza vizuri wananchi ili dhamira ya waasisi wa Muungano iweze kufikiwa.
“Wanaopinga Muungano wanatakiwa kusoma historia na watoe maelezo kwa nini waasisi wa taifa waliamua kuleta Muungano na wasiwasemee watu kuwa hawautaki wakati hayo ni maoni yao,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Hoseah Kayumbo, aliipongeza serikali kwa kupiga hatua katika kuboresha sekta ya elimu hususan ujenzi wa maabara.
Alisema wakati wakisherehekea maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wananchi hasa wanasayansi wanapaswa kujivunia hatua iliyofikiwa.
“Wanasayansi tunajivunia muamko wa serikali  kujenga maabara ambazo zitawezesha kizazi kijacho kuendesha uchumi wa kisayansi,” alisema.
Alisema nchi inawajibu wa kuendelea muungano hata kama uongozi utabadilika na wenye kulalamika wataendelea kuwepo licha ya kuyaona mafanikio yaliyofikiwa.
Naye Mwenyekiti wa UPDP, Fahm Dovutwa, alisema Muungano ni mzuri na unatakiwa kuenziwa kwa sababu matatizo yaliyoko yanazungumzika.

Kilifu ataka makada wanaokubalika CCM


NA SOLOMON MWANSELE, MBARALI
MBUNGE wa Mbarali, Modestus Kilufi, amekiomba Chama kufanya tathimini ya watu watakaogombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Aidha, alisema viongozi ambao hawakubaliki wasigombee tena na badala yake wateuliwe wanaokubalika.
Kilufi alisema hayo jana kwenye kikao cha kamati ya siasa ya Chama ya wilaya ya Mbarali, kilichohudhuriwa na Katibu wa Chama mkoa wa Mbeya, Mwangi Kundya.
Kundya yupo katika ziara ya kuzitembelea wilaya zote za Mkoa wa Mbeya na katika ziara hiyo ameambatana na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Bashiru Madodi.
Ziara hiyo ina lengo la kukagua uhai wa Chama na maandalizi ya uchaguzi mkuu.
Kifuli alisema ni lazima Chama kijipange vya kutosha kwa ajili ya kuwapata wagombea kwenye ngazi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo. 
“Katibu hata mimi nikionekani sifai basi nielezwe mapema, wananchi wa jimbo hilo wana imani kubwa na CCM, hivyo awekwe mtu anayefaa,” alisema.

Kadi za kliniki zazusha balaa


Na Ahmed Makongo, Bunda
WANAWAKE katika Jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara, wameilalamikia hatua ya hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali na binafsi kuwauzia kadi za kliniki kwa gharama ya sh. 2,000.
Walitoa malalamiko hayo jana mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, ambaye yuko ziarani kuhamasisha shughuli za maendeleo na kukagua ujenzi wa maabara katika sekondari za kata.
Walidai baadhi ya wauguzi wa hospiali, vituo vya afya na zahanati katika jimbo hilo, wanawauzia wajawazito kadi za kliniki na kwamba, vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika kwa muda mrefu sasa.
“Hapa wake zetu wakienda kliniki wanauziwa kadi ambazo zinatakiwa zitolewe bure hivyo tunakuomba utuondoshe kero hiyo,” alisema Stephano Sasta.
Kwa upande wake, Mirumbe alisema ataunda tume ya kufuatilia kero hiyo, ambapo alisema kadi za kliniki ni mali ya serikali na zinatolewa bure.

NHC sasa waingia mkataba na DSE


NA MOHAMMED ISSA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limeingia mkataba na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wa mauzo ya sehemu ya eneo la ofisi katika mradi wake wa Morocco Square ulioko Kinondoni, Dar es Salaam.
Mkataba huo ulitiwa saini jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu na Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Moremi Marwa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mchechu alisema mkataba huo utagharimu sh. bilioni 3.3 na kwamba malipo yatafanyika kwa awamu nne katika kipindi cha miaka mitatu.
Mchechu alisema mradi wa Morocco Square una ukubwa wa mita za mraba 105,000, na utakamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Alisema mradi huo umebuniwa kulingana na mahitaji ya majengo ya sasa na ya baadaye ambapo utakuwa na huduma zote muhimu na utaboresha mazingira ya biashara katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema makubaliano waliyofikia yatatoa fursa kwa DSE na mawakala wake wa soko la mitaji kutumia jengo hilo.
Mchechu aliwataka wanaohitaji maeneo ya ofisi, biashara na nyumba za kuishi katika mradi huo wafike ofisi za NHC kwa ajili ya kukamilisha taratibu za manunuzi.
Kwa upande wake, Marwa alisema lengo la DSE ni kuziwezesha kampuni kupata mitaji.
Alisema soko hilo litanunua sehemu ya mradi wa Morocco ambapo wataweka ofisi zao.
Marwa aliongeza kuwa DSE inaendelea kuboresha shughuli zake na mwaka huu, kampuni tano zitasajiliwa.

RC Shy afunga mgodi


Na Chibura Makorongo, Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, amesitisha shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika machimbo madogo ya Kaole yaliyopo Kata ya Lunguyu wilayani Msalala.
Alisema ameamua kusitisha kwa muda shughuli za uchimbaji kwa ajili ya kupisha timu ya watalamu kutoka   mgodi wa dhahabu Bulyanhulu kuendelea na kazi ya kutafuta watu wengine waliofukiwa na kifusi.
Rufunga alitoa amri hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika machimbo ya Kalole, ambapo aliwapa pole kwa kupoteza ndugu waliofariki kwa kuangukiwa na kifusi cha udongo.
Alisema serikali imefikia uamuzi wa kufunga kwa muda shughuli za uchimbaji kutokana na watu 19 kupoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalole, Khamis Misungwi, alisema zaidi ya wachimbaji wadogo 400, wanaendesha shughuli zao katika mgodi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema maiti 18 zilitambuliwa na ndugu zao na mmoja bado hajatambuliwa.
Hata hivyo, Rufunga aliwataka viongozi wa serikali ya kijiji kutoruhusu watu kuendelea na uchimbaji katika eneo hilo.

REA: Upatikanaji wa umeme kuongezeka


Na Mwandishi Wetu
KIWANGO cha upatikanaji wa nishati ya umeme kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2030, umesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Meneja Utaalamu Elekezi wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, alisema hayo alipomwakilisha Mkurugenzi wa REA katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu na wajasiriamali wa usambazaji vifaa vya umeme (nishati) itokanayo na mionzi ya jua.
Katika mafunzo hayo yanayomalizika leo katika Hoteli ya Kebis jijini Dar es Salaam, Mhandisi Nyamo-Hanga, alisema kiwango cha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi mijini na vijijini kimeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2007 hadi asilimia 36 mwaka 2015.
“Kiwango hiki kinatarajiwa kufikia asilimia 75 mwaka 2025 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 ambao ni mwaka wa dira ya kimataifa ya ‘Nishati Endelevu kwa Wote.’
Meneja Mkuu wa Energy Plus, Bernadetha Daud, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wadau kujua namna bora zaidi ya kukisia uwezo wa mifumo na matumizi ya sola kwa watumiaji binafsi na taasisi.
“Unajua bado kuna uelewa mdogo kwa watu maana wengi hawajajua faida za matumizi ya sola… wengi wanadhani gharama za sola ni kubwa, lakini hawakumbuki kuwa umeme wa sola hauna malipo ya mwezi,” alisema.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Energy Plus ya Tanzania kwa kushirikiana na Africa Energy ya Marekani,  Mhandisi Nyamo-Hanga, alisema  teknolojia ya sola ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa imewezesha watumishi wa umma kukubali kwa moyo kufanya kazi hata maeneo ya vijijini.
“Teknolojia ya sola ni jibu kubwa kwa matatizo ya umeme. Zamani kabla ya sola watumishi wengi walikuwa wakikataa kwenda kuhudumia vijijini maana wanajua hakuna hata umeme, lakini sasa wanakwenda bila shida,” amesema.
Mtendaji Mkuu wa Ageco Energy, Vincent Mughwai, alisema umeme wa sola una manufaa kwa kuwa unafika hata maeneo ya vijijini ambako bado ni ndoto kupata umeme toka gridi ya taifa.
Mshiriki mwingine ambaye ni Meneja Masoko na Mauzo wa Ensol Tanzania Limited, Samanchogu Kihore, alizitaja faida za matumizi ya sola kuwa ni pamoja na kutumika maeneo yote yakiwemo ya vijijini hata katika nyumba za nyasi, kutokuwa na gharama endelevu za kuzalisha na kutumia umeme kwa kuwa baada ya kuunda mfumo, hakuna gharama za malipo ya mwezi, mafuta wala matengenezo kwa kuwa haiharibiki kirahisi.
“Umeme wa sola hauhitaji nishati nyingine kama mafuta wala maji wakati wa kuuzalisha kwani unatumia jua ambalo halilipiwi na hauna kelele wakati wa kuzalisha wala kutumia, hivyo ni rafiki mkubwa wa mazingira,” alisisitiza.

Vijana washauriwa kuchangamkia fursa


Na Genofeva Matemu, Maelezo 
VIJANA katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, wametakiwa kuimarisha miradi ya mfano inayokopesheka.
Rai hiyo ilitolewa na mhamasishaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Ester Riwa, katika semina ya ujasiriamali iliyofanyika katika Kata ya Monduli Juu.
Alisema Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa ukiwawezesha vijana,  hivyo wanatakiwa kubuni miradi ili waweze kukopesheka.
Ester aliwataka vijana kuwa na mwamko utakaowawezesha kujiletea maendeleo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Monduli, Rose Mhina, aliwataka vijana kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mikopo.
Alisema serikali inatoa mikopo kwa vijana yenye riba nafuu, hivyo wakati umefika kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo.
Hata hivyo, Ofisa Ushirika wa halmashauri hiyo, Ester Tarimo, aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo katika kujiletea maendeleo.

TASAF yafafanua


NA Lisa Said, Tanga
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga, amesema kuwa mfuko huo kutoa fedha kwa ajili ya kuziwezesha kaya masikini sio kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali ni mipango ya serikali kuleta unafuu wa kipato kwa wananchi wake.
Aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao cha kazi kilichowashirikisha wadau wa mfuko huo kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar wakiwemo waratibu wa TASAF wilaya na mkoa, waandishi, maofisa wafuatiliaji  na wahasibu kwenye halmashauri.
Pia, Mwamanga alisema kuwa muungano waliouweka kati ya watumishi wa halmashauri na waandishi hao sio ‘ndoa ya mkeka’ bali ni endelevu lengo likiwa kuona wanashirikiana na kuufanya mfuko huo ulete tija kwa wananchi.
“Mpango huu unaofanywa na TASAF kugawa fedha kwa kaya masikini si wa CCM kama watu wanavyoghani, mpango huu ni wa serikali katika kuzikwamua kaya masikini kiuchumi na kuleta maisha bora kwa Watanzania wote,” alisema.
“Ili kuonyesha kinachofanywa ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, mpango huu umewashirikisha waandishi wa habari. Muungano huu haujawahi kutokea, na waandishi msije mkadhani muungano huu kati yenu na sisi ni ndoa ya mkeka, bali ni jambo endelevu,” alisema Mwamanga.
Mwamanga alisema kwa kuwashirikisha waandishi kwa kina kwenye Mpango wa TASAF III ni kuwasaidia kuweza kuandika habari zilizo sahihi na wasikubali kupotoshwa na baadhi ya watu, ambao hawajui nia yao ni nini.
Alisema TASAF imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na ndiyo mradi mkubwa barani Afrika ambao umewezesha kuwafikia wananchi wengi, huku ukionekana jinsi unavyofanya kazi kuanzia matumizi ya fedha na uratibu wake, hivyo waandishi na wananchi ni vyema wauunge mkono.
Mratibu  wa TASAF wilaya  ya Lushoto, Beatrice Shemdoe, alisema kuwa  wilaya yao imejipanga kunufaisha kaya za watu masikani 10,779 ikiwa  ni  kutoka  katika vijiji 146 kwa kuziwezesha kupata uhakika wa chakula, gharama za matibabu  na elimu.

Tuesday, 21 April 2015

Mageuzi makubwa yaja  •  Shule 250 kufungiwa huduma ya intaneti
  • Vijiji 480 kuunganishwa huduma ya simu
  • Serikali kuzibana kampuni za simu nchini

NA KHADIJA MUSSA
MIKAKATI ya serikali ya kutoa wataalamu wengi wa sayansi imeendelea kutetekelezwa kwa kasi, ambapo imetia saini mikataba kusambaza huduma za mtandao kwenye shule mbalimbali nchini.
Mikataba hiyo iliyotiwa saini jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, iko miwili ya kupeleka huduma za mawasiliano vijijini na kuunganisha mtandao wa intaneti katika shule utakaogharimu sh. bilioni 26.28.
Katika mikataba hiyo, serikali imeonya kuwa itazifuta kampuni ambazo zitashindwa kutekeleza makubaliano ya kufikisha mawasiliano kwa wakati katika vijiji 480 vilivyoainishwa.
Onyo hilo la serikali linatokana na kampuni hizo kushindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wa kupeleka huduma za mawasiliano vijijini, ambapo nyingi zimetekeleza kwa asilimia 50 tu.
Akizungumza wakati wa kutia saini mikataba hiyo, Profesa Mbarawa alisema awamu ya tatu ya kupeleka mawasiliano vijijini utahusisha kata 102 ambapo vijiji 480 vitanufaika nayo.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ulihusisha kata 52, ambao ulitekelezwa mwaka 2013 na umekamilika kwa asilimia 99.05 na awamu ya pili ilihusisha kata 86 na ulitakiwa kukamilika mwaka jana na hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 50.
“Awamu ya kwanza kuna kata nne kati ya 52 ambazo bado hazijamazilizika, jambo ambalo halikubaliki na kama mtu ameshindwa kutekeleza mkataba wake afungiwe na katika hili sitakubali,” alisema.
Mkataba wa mradi huo ambao utahusisha kata 102 na kugharimu sh. bilioni 14.02 umesainiwa kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) na kampuni za utoaji huduma za mawasiliano.
Kampuni zilizotia saini mkataba wa utoaji huduma ya mawasiliano kwa awamu ya tatu na idadi ya kata katika mabano ni Tigo (42), Vodacom (36), TTCL (19) na Airtel (5).
Alisema bado kuna changamoto kubwa ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini, hivyo kuzitaka kampuni hizo kuhakikisha zinatekeleza mikataba ili kila mwananchi apate huduma popote alipo.
Waziri huyo alisema katika kuhakikisha huduma ya mawasiliano inawafikia wananchi wote, serikali ilianzisha utoaji wa ruzuku kwa kampuni zinazotoa husika ili kupeleka mawasiliano kwenye maeneo yenye uchumi hafifu.
Alisema serikali kupitia UCAF itatoa ruzuku ya asilimia 100 ambayo inatolewa kulingana na eneo yakiwemo maeneo ya mipakani ambayo ni lazima yawe na mawasiliano wakati wote ili kuimarisha ulinzi na usalama.
Alisema UCAF ilianzishwa mwaka 2006 ambapo hadi mwaka 2010 anaingia katika wizara hiyo hakukuwa na kazi yoyote iliyotekelezwa ambapo alilazimika kubadilisha uongozi jambo ambalo limeleta mafanikio na sasa mawasiliano yanaendelea kufika kwa wananchi.
“Ni mafanikio makubwa yaliyopatikana itakuwa kichekesho kwa waziri atakayekuja ashindwe kufanya vizuri zaidi, na akishindwa kuna tatizo kwa sababu sasa teknolojia imebadilika,” alisema.
Awali, Mtendaji Mkuu wa UCAF, Mhandisi Peter Ulanga, alisema mbali na kutia saini mkataba na kamapuni za mawasiliano, pia waliingia mkataba na kamapuni ya Avanti inayotoa huduma za mtandao wa intaneti kwa ajili ya kuziunganishia shule 250 za serikali. 
Pia alisema wataanzisha vituo 25 vya kufundishia walimu wa masomo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, mradi unaotarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya UCAF, Profesa John Nkoma, aliwaomba wananchi wabadilike na kutumia huduma ya intaneti kwa faida na si vinginevyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. John Mngodo, alisema huduma ya kuunganisha intaneti katika shule za serikali itasaidia kuboresha elimu.

Msaidizi wa Gwajima kortini


NA FURAHA OMARY
MSAIDIZI wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, George Mzava, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mzava (43), mfanyabiashara na mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, alifikishwa  mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka ya kukutwa na bastola ya kiongozi huyo na risasi kinyume cha sheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alimsomea Mzava mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera, baada ya mshitakiwa huyo kujisalimisha.
Mzava akisindikizwa na wakili wake, Peter Kibatala, alifika mahakamani hapo ili kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi iliyofunguliwa Ijumaa iliyopita, ambayo washitakiwa wenzake watatu, akiwemo Gwajima, walisomewa mashitaka yao.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao walisomewa mashitaka yanayowakabili Ijumaa na kuachiwa kwa dhamana ni Askofu Msaidizi Yekonia Bihagaze na Mchungaji Geoffrey Milulu.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wote wanne wanakabiliwa na mashitaka matatu.  Gwajima anakabiliwa na shitaka la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi anazomiliki kihalali katika usalama huku wengine wakidaiwa kukutwa nazo kinyume cha sheria.
Akimsomea mashitaka yanayomkabili Mzava, Kweka alidai Machi 29, mwaka huu, katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni A, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo na wenzake, Bihagaze na Milulu, walikutwa na bastola aina ya Bereta bila  kuwa na kibali au ruhusa kutoka katika mamlaka zinazohusika.
Katika shitaka la pili, Mzava na wenzake hao wanadaiwa siku hiyo wakiwa hospitalini hapo, walikutwa na risasi tatu za bastola na 17 za bunduki aina ya shotgun bila kuwa na kibali au ruhusa kutoka mamlaka zinazohusika.
Mshitakiwa huyo alikana mashitaka hayo, ambapo Wakili Kweka alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Dyansobera alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka mshitakiwa kutia saini dhamana ya sh. milioni moja na kuwa na mdhamini mmoja mwaminifu atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.
Mshitakiwa alitimiza masharti hayo, hivyo aliachiwa kwa dhamana hadi Mei 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa.

Mamia wauaga mwili wa DC Kyerwa


 NA REHEMA MAIGALA
RAIS  Jakaya Kikwete, ameongoza mamia ya waombelezaji kuuaga mwili wa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Luteni Kanali (mstaafu) Benedict Kitenga.
Mwili wa Kanali Kitenga uliagwa jana katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo wa CCM na serikali walihudhuria.
Kabla ya kufariki dunia, Kanali Kitenga alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na shinikizo la damu.
Anatarajiwa kuzikwa leo katika Makaburi ya Kola, manispaa ya Morogoro.
Kanali Kitenga alizaliwa Juni 15, 1953 katika kijiji cha Shungu wilayani Kilombero, Morogoro. Alitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 36 kabla ya kustaafu rasmi Juni 30, 2008.
Mara baada ya kustaafu utumishi ndani ya JWTZ, Rais Kikwete alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara na baadaye Kyerwa, ambapo hadi anakutwa na umauti alikuwa akiingoza.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, alisema Tanzania imempoteza mtu muhimu na aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linasonga mbele.
“Hili ni pigo kubwa tulilopata kwa mzee wetu. Tutamkumbuka daima kwa umakini wake katika shughuli zake za kila siku,” alisema Mongella.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alieleza kushitushwa kwake na kifo cha  Kanali Kitenga na kusema alikuwa kiongozi mhamasishaji wa maendeleo.

Tani 10,000 za chakula kutolewa kwa wahitaji


NA RACHEL KYALA
SERIKALI itagawa tani 10,000 za chakula kuwasaidia watu ambao wanakabiliwa na njaa kutokana na uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo nchini.
Hatua hiyo imetokana na zaidi ya watu 400,000 kukabiliwa na njaa wakiwemo 42, 414 ambao hawana uwezo kabisa wa kununua chakula na wametengewa kupatiwa tani 1,000 bure.
Hata hivyo, tani zingine 9,000 zinatarajiwa kuuza kwa sh. 50 kwa kilo kwa watu 381,722, ambao kwa kiasi wana uwezo wa kumudu kununua chakula kwa bei hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama wa Chakula, Onasimbo Mpika, alisema jana kuwa wilaya zitakazohusika na mpango huo ni Korogwe, Monduli na Longido, Nzega, Same, Mwanga, Pangani, Magu, Kishapu, Bunda, Kwimba, Rorya na Shinyanga.
“Pamoja na wilaya hizo, yapo maeneo mmbalimbali nchini yenye uhaba wa chakula ambayo tayari yameshafanyiwa tathmini na hali kuonyesha kuwa yanastahili kupata chakula cha bei nafuu,” alisema. 
Alitoa mfano wa wilaya hizo kuwa ni Chamwino, mkoani Dodoma, ambayo watu 13,031 wanahitaji tani 312.

Ukaguzi wa vyama vya hiari waanza rasmi


NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema inaendelea na ukaguzi wa vyama vya kijamii na kwamba vikibainika kukiuka matakwa ya kisheria,  vitafutwa.
Taarifa iliyotumwa na Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, kwa  vyombo vya habari jana ilisema kutokana na orodha waliyo nayo, vyama 10,000 vya kijamii na taasisi za dini, vimesajiliwa katika wizara na kwama vitakavyofutwa ni vile ambavyo haviwasilishi taarifa za kila mwaka za ukaguzi wa hesabu zao.
Taarifa ilisema kama vyama hivyo havilipi  ada ya kila mwaka, kama sheria inavyotaka ni lazima vitafutwa lakini kwa vile ambavyo vinatekeleza matakwa hayo ya kisheria, havitafutwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, orodha ya vyama vitakavyofutwa itatolewa kwa awamu, kuanzia wiki hii na kwa kuanzia itahusu vyama vilivyosajiliwa mkoni  Dar es Salaam.
Aidha, ilisema kuwa ni vyema ikaeleweka kuwa zoezi linaloendelea kwa sasa halihusiani na taasisi zinazoelezewa kujiingiza katika masuala ya kisiasa na pia wizara  haihusiki na usajili wa NGO.

Saturday, 18 April 2015

Meli Zanzibar kufuatiliwa kwa setilaiti


Na Antar Sangali, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezindua mradi wa kufunga vyombo vya mawasiliano ya meli na boti za uvuvi ili kuweza kuziona zikiwa baharini na kufuatiliwa kwa setalaiti kulinda usalama wa abiria pamoja na kupambana na vitendo vya uhalifu, usafirishaji dawa za kulevya, uharamia na ugaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alitoa msimamo huo wakati akihudhuria  mafunzo ya mradi wa kuviona vyombo baharini vikitoa huduma au kufanya kazi za uvuvi na kuvifuatilia kupitia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Balozi Seif alisema serikali imeanzisha mradi huo kwa vile Zanzibar ni kisiwa kinachojitegemea njia za usafiri wa baharini na anga na kwamba, kuna haja ya vyombo vya baharini kufungwa vyombo ili kukabiliana na uhalifu.
Alisema ili kukabiliana na  uharamia na meli za uvuvi zinazovua kinyume cha sheria, usafirishaji dawa za kulevya na kulinda usalama wa watu, mradi huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kuondoa vitendo ambavyo ni kinyume na utaratibu wa kisheria.
Makamu huyo alisema ili kufanikisha masuala hayo, umakini na utaalamu unahitajika katika kusajili vyombo hivyo ili wavuvi wadogo wasishindwe kulipia gharama za huduma baada ya kila boti kutakiwa kufungwa vifaa hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Maalim, alisema teknolojia itakayotumika chini ya mradi huo ni mpya ambayo itasaidia kubaini vyombo vilivyopata usajili moja kwa moja vinapokuwa baharini huku watendaji wakibaki ofisini.
Maalim alisema kila mkoa utakuwa na kituo cha kupokea mawasiliano na ZMA itaandaa kanuni maalumu kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri na uvuvi vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Mtendaji Mkuu wa SRT Technology kutoka Uingereza, Simon Tucker, alisema teknolojia hiyo ya mawasiliano imeleta mafanikio kwa nchi zilizokuwa zikikabiliwa na tatizo la biashara haramu za magendo, uharamia na ugaidi.
Tucker alisema teknolojia hiyo imetumiwa na nchi mbalimbali za visiwa ikiwemo Madagascar, Saud Arabia, Vietnam ambapo imesaidia kuondoa matatizo ya uvuvi haramu na kukabiliana na matukio ya utekaji meli kwa muda muafaka.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 60 na vifaa vitafungwa huku kila chombo kikitakiwa kugharamia ufungaji wa vyombo hivyo.

Atangaza kuwania ubunge Arumeru


NA SHAABAN MDOE, ARUMERU
JOTO la ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki limezidi kupanda baada ya kada wa CCM wilayani humo, Elirehema Kaaya, kutangaza kuwania kiti cha ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kaaya ambaye aliwahi kugombea nafasi hiyo mwaka 2005 na 2010, alisema juzi, kuwa hajakata tamaa kwa kuwa anaamini amejipanga kikamilifu.
Mtangaza nia huyo ambaye kwa sasa ni Ofisa Uhusiano wa Jiji la Mwanza, alisema kilichomsukuma kuwania ubunge ni pamoja na kusukumwa na dhamira ya kutatua kero mbalimbali za wakazi wa jimbo hilo, hususan migogoro ya ardhi.
Kaaya alisema jimbo hilo ni miongoni mwa majimbo yenye utajiri mkubwa ikiwa ni pamoja na vivutio vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA), lakini wananchi hawanufaiki na rasilimali hizo.
Alisema endapo Chama kitampa ridhaa kupeperusha bendera, ana uhakika wa kunyakua ushindi kwa kuwa amejipanga kutangaza sera zitakazowavutia wananchi.
ìSitawapa pombe za viroba vijana, hususani wale wanaoendesha bodaboda. Nimejipanga kuwatangazia sera zitakazowavutia katika mikutano yangu,îalisema Kaaya.

Zimamoto Mwanza walilia vitendea kazi


NA PRISCA MSHUMBUSI, MWANZA
JESHI la Zimamoto na Uokoaji jijini hapa linakabiliwa na uhaba wa vifaa vya uokoaji wakati wa mafuriko, suala linalosababisha kupata wakati mgumu kipindi mafuriko.
Akizungumza na gazeti hili, ofisini kwake, jana, Kamanda wa kikosi hicho mkoa humo, Andrew Mbate, alisema wanapata tabu wakati wa uokoaji pindi mafuriko yanapotokea.
Mbate alisema jeshi hilo halina vifaa vya kutumia katika uokozi wakati wa mafuriko suala linalosababisha walazimike kutumia vifaa bandia kuweza kuwasaidia wahanga wa mafuriko.
ìTuna vifaa bandia ambavyo tunatumia kuweza kuwanusuru wahanga wa mafuriko navyo haviaminiki katika shughuli hiyo, ila tunafanya hivyo ili kuweza kuwasaidi kwa wakati huo,î alisema Mbate.
Alisema wakati wa mvua na mafuriko hasa maeneo ya mabondeni, yanaweza kutokea maafa na kuwataka wakazi wa sehemu hizo kuhama kwa kuwa vitendea kazi vilivyopo ni vya bandia ambavyo haviaminiki katika shughuli hiyo.
ìKwa tahadhari nzuri ni bora wakazi wa mabondeni watoke, hasa kwa hapa Mwanza maeneo ambayo yana shida ni Mabatini. Ni bora wakatoka mapema kwani mvua bado zinaendelea kunyesha,î alisema.
Pia aliiomba serikali kujenga mifereji imara inayoweza kupitisha maji kwa urahisi kuepusha mafuriko yanayotokana na maji ya milimani.

Atakiwa kukanusha kauli ya upotoshaji


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
CHAMA cha Maalbino Tanzania (TAS) mkoa wa Mbeya, kimemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya mjini, John Mwambigija, kuwathitibitishia Watanzania kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahusika na vifo vya watu wa jamii hiyo.
Katibu wa chama hicho mkoani hapa, William Simwali, alisema hayo jana wakati akizungumza na MZALENDO kuhusu kauli iliyotolewa na Mwambigija akiwa kwenye mkutano wa hadhara juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Simwali alisema ni jambo la ajabu kwa baadhi ya wanasiasa kugeuza na kutaka kuwadanganya watu kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakitokea kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu jambo ambalo si sahihi.
Alisema hivi karibuni Mwambigija akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwira wilayani Rungwe, alisema mkakati wa kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ni mkakati unaotengenezwa na CCM, jambo ambalo si kweli
ìKwa sababu mauaji haya yameanza kuanzia mwaka 2006 na yaliendelea hadi mwaka 2009, na hakukuwa na uchaguzi wowote. Yakaanza tena mwaka 2011/2015, hivyo ina maana Tanzania kila mwaka ni mwaka wa uchaguzi? î alihoji Simwali.
Aliongeza wanasiasa aina ya Mwambigija wanatakiwa wawe wanatafuta maneno ya maana ya kuzungumza mbele za watu, hasa kwenye majukwaa ya kisiasa na siyo kutaka umaarufu kwa kuwaaminisha watanzania, mambo ambayo hayapo na kumtaka kukanusha kauli aliyotoa au kuelezea ukweli wake.
Kwa mujibu wa Simwali, hatu hiyo ya Mwambigija kusema jukwaani kuwa CCM ndiyo inayoua maalbino kwanza ni kukitendea dhambi Chama hicho.

Karatasi za chooni zafichia wahamiaji


NA WILIUM PAUL, MOSHI
POLISI mkoani Kilimanjaro inawashikilia wahamiaji haramu 52 ambao ni raia wa Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria wakitokea Kenya kwenda Malawi na baadaye Afrika Kusini.
Wahamiaji hao waliokamatwa jana saa 8.23 za asubuhi wakati askari wakiwa doria katika eneo la Changbay, barabara kuu ya Moshi ñ Arusha wilayani Moshi, walikuwa raia 44 wa Ethiopia.
Kamanda Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alisema raia hao walikuwa wakisafirishwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T209 BVL, ambapo lilikuwa limepakia karatasi cha matumizi ya chooni maarufu kama toilet paper ambalo lilikuwa likiendeshwa na Elisha Manyani (45).
Mtu huyo alikamatwa na wenzake watatu ambao Hamza Ali (24), Isaya Patrick (25) na Steven Swame(39) wote wakazi wa Arusha.
ìWahamiaji hao walikuwa wamepakizwa kwenye gari aina ya Fuso, ambapo katika gari hiyo, bodi ilikuwa imegawanywa sehemu mbili nyuma kulikuwa kumewekwa toilet paper na katikati palikuwa pamewekwa raia hao likiwa limefungwa turubai, jambo ambalo lilikuwa gumu kubaini kama ndani kuna raia hao,îalisema Kamwela.
Alisema majira ya 8.45 asubuhi raia wengine wanane walitiwa mbaroni katika eneo la eneo la KDC kwenye Kata ya Kiboroloni, ambapo walikutwa wakizagaa katika pori dogo karibu na mto Rau.
Kamanda alisema wanaendelea na uchunguzi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
ìHatutawafumbia macho raia hao wa Kitanzania wanaoshirikiana katika kusafirisha wahamiaji haramu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa na hata kutaifisha mali zao pindi watakapokutwa na hatia,” alisema.

Watalaamu vyuo vya Kiislamu kukutana Z,bar


Na Antar Sangali, Zanzibar
Wataalamu 40 kutoka vyuo vikuu tisa vya Kiislamu vya Nchi za Afrika Mashariki na Malasyia watakutana Zanzibar kujadili maendeleo ya mitaala pamoja na kuangalia njia bora za kuwaepusha wanafunzi kutojihusiaha na matumizi mabaya ya mitandao ya jamii inayochangia kuwaingiza katika ugaidi na uhalifu.
Akizungumza mjini hapa, jana, Profesa Abdulrahaman Hikmany wa Chuo Kikuu cha Al Sumait cha Zanzibar, alisema mkutano huo wa kimataifa utaanza April 18 hadi 19, mwaka huu.
Profesa Hikmany alisema lengo la mkutano huo ni kuchambua maendeleo ya mitaala ya elimu kwa vyuo vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini wa Afrika.
Alisema utandawazi kwa njia moja au nyingine una faida na hasara, na kutoa mfano kuwa binadamu hawezi kukatazwa asitumie kisu ila jambo la msingi kumpa njia kukitumia kwa tahadhari.
“Kusudio la mkutano huo ni kuibua mbinu mpya endelevu katika mitaala na kuelemisha vijana kuhusu madhara na taathira za za utandawazi na mawasiliano, simu na mitandao katika matumizi ya komyuta, tunachotaka wafahamu tija na na kama zake hakuna chema kisicho na athari. Ndiyo maana kuna wanaotumia dawa za kulevya licha ya hatari ya jambo hilo,îalisema.
Aidha alitaja teknolojia za mawasiliano kuwa zimerahisisha kazi za utafiti kufanyika muda mfupi na kwamba, eneo hilo limeathiri baadhi ya vijana kuitumia vibaya mitandao kinyume na mahitaji na kutumbukia katika matatizo ya uhalifu.
Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Fikra ya Kiislamu yenye makao yake nchini Malaysia. Vyuo vikuu vingine vitakavyoshiriki ni Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro, Chuo Kikuu cha Umma (Kenya), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Abdulrahaman Al  Smait (Zanzibar), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Uganda, Chuo Kikuu cha Mussa Bin Bique (Msumbiji), Chuo Kikuu cha Kiislamu (Sudan Kusini), Chuo Kikuu cha Kiislamu (Malaysia) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ambacho kitashiriki mkutano huo kama mtazamaji na mwalikwa.

UWT mkoani Arusha yawakataa walimu


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Arusha umetangaza kuwakataa walimu kusimamia uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais.
Aidha umewanyooshea kidole baadhi ya askari kwa kuwa na mapenzi yaliyopitiliza dhidi ya wanasiasa, hali inayosababisha washindwe kutenda haki katika maamuzi mbalimbali.
Msimamo huo ulitangazwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa UWT mkoani humo, Flora Zelote, alipokuwa akizungumza katika kata mbalimbali za Wilaya ya Arusha kwenye ziara ya kukagua uhai wa jumuia hiyo na Chama kwa ujumla.
Alisema kutokana na hali hiyo, UWT Arusha ina mpango wa kufikisha mapendekezo kwa Tume ya Uchaguzi na makao makuu ya Chama kuona namna ya kuwapata wasimamizi wengine wa uchaguzi mbadala wa walimu.
Mwenyekiti huyo alisema Chama Cha Mapinduzi kimeonekana kama mpangaji katika nyumba yake kutokana na mabaya yanayofanywa dhidi yake na watumishi wa umma, huku kikiendelea kukaa kimya.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha viongozi wa CCM taifa kurejesha majina ya wagombea yatakayopendekezwa toka mikoani.
Alisema hali ilivyo sasa Chama kinapaswa kuheshimu zaidi matakwa ya wananchi ya nani wanamtaka badala ya kuendelea ya kuwapendekeza watu kwa utashi wa wachache.
ì Nitoe msimamo wa jumuia yangu Mkoa wa Arusha, tutapendekeza wagombea kwa matakwa ya wananchi watakaowachagua na tutawafikisha kwao ili wafanye maamuzi sahihi, wakifanya vinginevyo wakawaleta wa kwao tutawapa taarifa waje kuwafanyia kampeni,î alisema Zelote.

Thursday, 16 April 2015

Nyalandu atekeleza maagizo ya Kinana


NA MWANDISHI WETU, MBARALI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amemaliza mgogoro wa ardhi uliokuwa ukifukuta kwa zaidi ya miaka saba kati ya wananchi wa vijijii 21 na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Nyalandu, ambaye yuko ziarani mjini hapa, jana aliwaeleza wananchi kuwa serikali haiwezi kuwaacha wananchi wake wakanyanyasika hivyo ni lazima ichukue hatua.
Uamuzi huo wa serikali wa kumaliza mgogoro huo, ni utekelezaji wa maagizo ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuitaka serikali kuhakikisha inamaliza tatizo hilo.
Zaidi ya wananchi  1500 wa vijiji 21 wilayani Mbarali, walitakiwa kuhamishwa kutokana na madai ya kuingia kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, jambo ambalo limekuwa likipingwa kwa muda mrefu sasa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini hapa jana, Nyalandu alisema serikali ya CCM ni sikivu na siku zote iko kwa maslahi ya wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi waliofika kusikiliza hatimaya maeneo yao, Nyalandu alisema msimamo wa serikali ni kuwalinda watu wake.
Alisema mgogoro huo umekuwa kero kubwa na kuwafanya wananchi kushindwa kuwa na uhakika wa maisha yao, hivyo serikali haiwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua.
Alisema Kinana alitoa maelekezo kwa serikali na wananchi kukaa mezani na kutafuta njia za kumaliza tatizo hilo, ambapo kwa sasa limefikia mwisho.
“Serikali ya CCM ni sikivu na iko kwa ajiliya Watanzania. Hivi karibuni Mzee Kinana alipita hapa mkamweleza kero yenu na alifikisha malalamiko yenu serikali na niko hapa kwa ajili ya utekelezaji.
“Naomba niseme kuwa vijiji vinavyotakwa kuhama vitaendelea kuwepo na ninaagiza kufanyika kwa ukaguzi wa mpaka katika GN 28 ili kuhakikisha haki inatendeka katika suala hili.Huu mgogoro ni lazima ufike mwisho na uamuzi huu una baraka zote za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,” alisema.

Alisema maeneo ambayo yana mgogoro mengi ndiyo kilimbilio na uchumi wa wananchi wa Mbarali kutokana na kuendesha shughuli za kilimo na makazi, hivyo serikali haiwezi kuchukua uamuzi ambao utakuwa na madhara kwa wananchi wake.

Kauli hiyo ya Nyalandu ilipokewa kwa furaha na wananchi waliofurika uwanjani hapo, ambao walisikika wakiimba nyimbo za kukipongeza CCM kwa kujali maslahi ya wananchi wake.
Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Nyalandu alikutana na uongozi wa CCM wilaya ya Mbarali pamoja na Kamati ya Siasa kuzungumzia mgogoro huo pamoja na kupata maoni.
Pia alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, ambapo alipewa taarifa kuhusiana na mgogoro huo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha mwafaka unapatikana.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo, alisema mgogoro huo umeleta mpasuko mkubwa na kusababisha wananchi kukosa imani na baadhi ya viongozi.
Alisema msimamo wa CCM ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi na kufanya shughuli za uzalishaji mali kwenye vijiji na maeneo wanayoishi, hivyo kutaka kuondolewa si sahihi.
Naye Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, alisema mgogoro huo umedumu kwa miaka mingi na kuwa ni lazima mwafaka ufikiwe ili kuleta amani na utulivu ambao umeanza kutoweka miongoni mwa wananchi.

Mazito yaibuka‘magaidi’ Kidatu  •  Imamu awakana Makwendo na wenzake

NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
DEREVA  wa bajaji, Alphonce Maurus, aliyebeba watu wanaodhaniwa kuwa watuhumiwa wa ugaidi, Kidatu wilayani Kilombero, ameweka hadharani namna alivyomfahamu mmoja wao.
Amesema mtuhumiwa ambaye aliuawa na wananchi baada ya kumjeruhi polisi, Hamad Makwendo, alijihusisha na mchezo wa kareti na masuala ya dini ya Kiislamu.
 Dereva huyo huyo aliwaeleza waandishi wa habari waliofuatilia taarifa za kina za tukio hilo jana kwamba Makwendo alikuwa hana kazi maalumu ya kumwingizia kipato.
Maurus alitoa taarifa hizo katika kata ya  Chikago, Kidatu wilayani Kilombero ambapo watu 11 walikamatwa na polisi  msikitini wakiwa na silaha, milipuko na sare za jeshi.
Alisema siku ya tukio, saa tatu usiku, akiwa katika  eneo lake la kufanyia kazi, walitokea watu 11 ambapo watano pamoja na mwenyeji ambaye ni marehemu, walipanda katika bajaji yake na wengine sita walipanda katika bajaji mwenzie.
Alisema watu hao walitaka kufikishwa katika msikiti wa Suni na kwamba wakati wote wa safari, mwenyeji wao ndiye alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili huku wenzake wakisikiliza bila kujibu kitu.
  ‘’Tuliwafikisha hadi eneo walilotaka na kisha tuligeuza na yule mwenyeji wao, ambapo tulipofika manyasini tulisimamishwa na polisi wakitaka kujua tumetoka wapi na tunkwenda wapi.
“Yule mwenyeji alishuka na kuanza kukimbia jambo lililofanya askari kuanza kumkimbiza huku na sisi tukifuatilia nyuma,’’ alisema.
Alisema Makwendo alipofika mbele alimkata polisi mmoja na jambia  na ndipo polisi walifanikiwa kumpiga risasi na wakamchukua na  walimchukua na kumpandisha katika gari lao.
Maurus alisema wananchi walifika katika eneo hilo na kuzingira gari hilo na kumshusha mtu huyo huku wakitishia kuchoma moto gari la polisi.
Akizungumzia  mwonekano wa watu hao, dereva huyo alisema walivalia mavazi ya jamii ya Kihindi, maarufu kama Punjabi, huku umri wao ukionekana kati ya miaka 20 na 25 tofauti na mwenyeji wao alieyonekana na umri wa takribani zaidi ya miaka 30.
 Kwa upande wake, askari aliyejeruhiwa, Koplo Nasoro Dabi, ambaye amelazwa katika zahanati ya Polisi Mkoa wa Morogoro, alisema siku ya tukio, akiwa na askari wenzake walisimamisha bajaji aliyopanda Makwendo.
Alisema baada ya bajaji hiyo kusimama, mtuhumiwa huyo alikimbia, hali iliyoashiria kuwa ni mhalifu hivyo kuwalazimu askari watatu, akiwemo yeye kumfukuza.
‘’ Wakati tukimkimbiza, nilikuwa mbele na kwamba tulipofika katika giza alichomoa jambia na kunishambulia. Askari wenzangu waliokuwa nyuma yangu walifyatua risasi na zingine kupiga juu hali iliyosababisha wananchi wengi kujitokeza kumpiga na kumchoma moto,’’ alisema.
Alisema wakati tukio hilo likiendelea askari wengine walifanya mawasiliano na Mkuu wa  Kituo cha Ruhembe kwa ajili ya kuwaongezea nguvu.
Naye Mganga Mkuu  Zahanati ya Polisi Morogoro, Mrakibu Thomas Kawala, alisema walimpokea askari huyo anaendelea na matibabu.
Kawala alisema  askari huyo alifika zahanati hapo akiwa na maumivu makali  lakini kwa sasa anaendelea vyema na matibabu.
Mmoja wa Kiongozi wa Msikiti  wa Masjid Salah Al – Fajih , Mohamed Manze, alisema wakiwa viongozi na waumini, hawakuwa na taarifa zozote za ujio wa watuhumiwa hao na kwamba katika msikiti huo wako vijana wanne ambao huwa wanalala na kujisomea hapo.
Alisema siku ya  tukio watuhumiwa hao walifika msikitini hapo saa nne ambapo ibada ya mwisho ilikwishafanyika na waumini kutawanyika, ambapo walikuwa wamebakia vijana hao peke yao.
Manze alisema  walitumia mwanya huo kuingia na kujihifadhi bila taarifa zozote kwa uongozi wa msikiti, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu za msikiti huo.
Hata hivyo, alisema wakiwa waumini wa msikiti huo, hawakupendezwa na suala hilo kwa kuwa limewachafua na kuwaharibia sifa na kwamba Makwendo hakuwa muumini wao.
Alisema hawana nasaba na kikundi chochote kinachojihusisha na uhalifu  na kwamba wanalaani vibaya watu wanaotumia dini katika masuala hayo ya uhalifu.

Mtanzania aula AU


Na  Mwandishi Maalumu, New  York
BRIGEDIA Jenerali Sara Rwambali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ameteuliwa kuwa Mwakilishi Maalumu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika (AU), Sudan Kusini.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU,  Dk. Nkosanzana Zuma,  katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari alisema makazi ya Brigedia Jenerali Sara yatakuwa Juba.
Dk. Nkosanzana amemteua Josephine  Charlotte Kala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuwa Mwakilishi Maalumu na Mkuu wa Ofisi ya AU nchini Ivory Coast na makazi yake kuwa Abidjan.
Wengine walioteuliwa ni Madame Nyiramatama kutoka  Rwanda, anayekuwa Mkuu wa Ofisi ya AU nchini Chad  na  Dk. Arvin Boolel kutoka Mauritius anayekuwa Mwakilishi Maalumu wa AU  nchini Burundi.
Alisema uteuzi huo ni sehemu ya kuhakikisha uwepo  wake katika kila eneo na kuunga mkono juhudi zinazolenga kukuza amani na usalama barani Afrika.
Alisema mwaka huu AU imejikita katika uwezeshaji wa wanawake, hivyo anatumaini kwamba itanufaika na utaalamu na uzoefu mkubwa na uwezo wa kiuongozi kutoka kwa wateuliwa hao.
Mwenyekiti huyo pia alitoa wito kwa wadau wote kuwapa ushirikiano viongozi hao walioteuliwa ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa maslahi ya Afrika, huku akitoa shukrani kwa wawakilishi ambao wanamaliza muda wao.

KESI YA MUME WA MBASHA


Daktari aanika taarifa ya vipimo  

NA ATHNATH MKIRAMWENI
SHAHIDI wa nne katika kesi ya tuhuma za ubakaji inayomkabili Emmanuel Mbasha, mume wa mwanamuziki wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, jana alidai mahakamani kuwa hakuona dalili zozote za kuingiliwa kimwili mlalamikaji.
Hayo yalidaiwa na daktari wa Hospitali ya Amana, Migole Mtuka, ambaye alimfanyia vipimo msichana huyo.

Daktari huyo alidai katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwamba vipimo alivyomfanyia msichana huyo anayedaiwa kubakwa na Mbasha, havikuonyesha kitu chochote.
Dk. Migole alidai kuwa binti huyo alifika hospitalini hapo Mei 26, mwaka jana, kwa alili ya kufanyiwa vipimo. 
Alidai kwamba binti huyo alipofika hospitalini hapo, alimfanyia kwanza vipimo vya macho kisha kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, ambavyo hutolewa bure. 
Dk. Migole  alidai kwamba baada ya kumtaka kwenda kufanya vipimo vya maabara, akiwa na baadhi ya ndugu wa familia yake, hakwenda bali aliingia mitini na kurejea Juni 3, mwaka jana, baada siku nane kupita.
Alidai baada ya kufanyiwa hivyo, vipimo hivyo  vilionyesha kuwa hakuna kitu chochote alichofanyiwa, kwa maana ya kubakwa au kuingiliwa na mwanamume katika mwili wake na kuwajazia fomu aina ya PF3 kwa kile alichokiona.
“Binti huyo hakuonekana kuwa na ujauzito, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na wala mbegu za kiume katika sehemu za siri,” alidai daktari huyo.
Hata hivyo, baada ya kutolewa ushahidi huo, Hakimu Flora  Mujaya, hawakuweza kusikiliza ushahidi mwingine kutokana na taarifa za msiba wa hakimu mwenzao, zilizofika mahakamani hapo.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa upande wa Jamhuri Aprili 20, mwaka huu.
Mbasha anadaiwa kuwa Mei 23 na 25, mwaka jana, alimbaka binti  mwenye umri wa miaka 17, ambaye  anadaiwa ni shemeji yake  huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Wadaiwa sugu wa ardhiwafikishwa mahakamani


NA RACHEL KYALA
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imezifikisha mahakamani kampuni 11 ambazo ni wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Miongoni  mwa kampuni hizo zinadaiwa ni S.H Amon, Highland Estate na Costix Limited  ambazo zinadaiwa sh. milioni 80.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba, Wilaya ya Ilala, Yose Mlyambina, alisema malalamiko dhidi ya kampuni na watu binafsi 120, yaliwasilishwa katika baraza hilo na Kamishna wa Ardhi, Dk. Moses Kusiluka.
Alifafanua kuwa S.H Amon, inadaiwa sh. milioni 38.2, Highland Estate sh. milioni 19.9 na Costix Limited sh. milioni 12.8.
Alisema Kamishna  wa Ardhi aliwasilisha madai hayo chini ya mfumo wa wadaiwa kutoruhusiwa kutoa utetezi isipokuwa kwa maombi maalumu ambapo mahakama hiyo itatoa siku 14 kwa watakaokuwa na hoja.
Mwenyekiti huyo alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia ili kuliongezea pato taifa ambapo Watanzania wengi wanapuuza suala hilo.
Mlyambina, alitaja madhara mengine ya baadhi ya watu na kampuni kutolipa kodi huku wengine wakilipa kuwa ni kuleta taswira ya mfumo wa kibaguzi na kuchochea wanaolipa kuacha kufanya hivyo.
Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo, Walter Lungu, alisema wizara ilichukua hatua ya kuwashitaki wadaiwa sugu baada ya kukagua hesabu zake na kugundua inapoteza kiasi kukubwa cha pato.
Alisema mbali na matakwa ya kisheria, hatua hiyo ni  utekelezaji wa amri ya Waziri William Lukuvi, aliyoitoa  kuanzia Januari  hadi Machi 30 kwa wadaiwa sugu kulipa, vinginevyo wangefikishwa mahakamani.
Kampuni zingine zilizofikishwa mahakamani ni Jessa Industries, St, Mary’s International Academy, St. Mary’s International Limited na Murzah Oil Mills,  Zake Construction Limited na Noor Investment Limited.

Watanzania waishio Yemen kurejeshwa


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imedhamiria kuwarudisha nchini Watanzania waishio Yemeni, kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Ali Ahmed Saleh.

Alisema ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi ni wanafunzi, wanarudi nchini wakiwa salama. 
Membe alisema awamu ya kwanza ya kuwarudisha ilifanyika hivi karibuni chini ya uratibu wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania ulioko mjini Mascut, Oman.
Alisema katika awamu hiyo Watanzania 25, walirudishwa na kwamba juhudi za kuwarudisha wengine zinaendelea. 
“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko yanayoendelea Yemen wanarejeshwa salama,” alisema. 
Alisema Watanzania hao wengi wao wamefika katika miji ya Sarfat na Al-Mazyouna iliyoko katika mpaka wa Oman na Yemen.
Membe alisema raia hao walituma maombi ya dharura kwenye ofisi za ubalozi, kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili operesheni ya kuhakiki, kuadnikisha na kuwarudisha lilianza mara moja.
Alisema awamu ya pili ya kuwahakiki itaanza hivi karibuni, ambapo Watanzania 64 wataruhusiwa kuingia Oman na kurejeshwa Tanzania. 
Membe yuko Oman kwa ziara ya siku moja ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

IGP Mangu awapa neno Waislamu


NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, ameungana na viongozi wa dini ya Kiislamu kukemea vitendo vya uhalifu.
Ili kudhibiti vitendo hivyo, amezitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto  ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza makundi yanayofanya mambo hayo.

IGP Mangu alisema hayo jana katika  mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa Kiislamu katika kuimarisha usalama nchini yenye kauli mbiu isemayo ‘Amani na usalama ndio maisha yetu’.
Mafunzo hayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu nchini.
IGP Mangu alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama. 
Naye Mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania, ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Ulamaa la BAKWATA, Sheikh Abubakar Zuber, alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani ambazo zimeanza kujitokeza.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki salama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mataka, alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yoyote hata ndani ya msikiti, hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyi Baraka, Sheikh Issa Othman, alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao.

Mengi afanya mazungumzo na Balozi wa Malawi


NA FURAHA OMARY
MWENYEKITI wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, amekutana na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo ya kibiashara.
Dk. Mengi na Balozi Hawa walikutana jana, mjini Dar es Salaam, katika makao makuu ya kampuni za IPP.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Hawa alisema Malawi iko tayari kuingia ubia na Tanzania kwa ajili ya masuala ya kibiashara.
Pia, alimweleza Dk. Mengi, kwamba wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na sekta binafsi na kwamba nchi yake ipo tayari kuingia ubia na Tanzania.
Mbali na hayo, Balozi huyo alisema Malawi na Tanzania zinapaswa kujenga ushirikiano na kutumia fursa ya jukwaa la uwekezaji litakalofanyika Juni mwaka huu nchini Malawi.
Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Dk. Mengi alisema katika kukomesha mauaji hayo, hakuna budi kupambana na wauaji na wale wanaonunua viungo vya albino.
Kwa upande wake, Balozi Hawa alisema Malawi inaangalia kwa makini na imelipa uzito wa juu tatizo la mauaji ya albino.
Alisema Malawi inafanya kila jitihada kuona tatizo la mauaji ya albino linakwisha.
Balozi Hawa alisema hayo, baada ya Dk. Mengi kutaka kujua kutoka kwake, ushiriki wao katika mapambano na vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa albino.

Hakuna tishio la ugaidi Mwanza-Mulongo


PETER KATULANDA, MWANZA
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo, amesema mkoa huo uko salama na hakuna tishio lolote la ugaidi.
Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga kukabiliana na tishio lolote linaloweza kujitokeza.
Mulongo aliwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea na shughuli zao kama kawaida na wasiwe na hofu yoyote.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama ya mkoa huo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi, kwenye kongamano la vijana wanawake wa vyuo na sekondari.
“Kuna baadhi ya watu wachache wanasambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mwanza iko kwenye mipango ya kuvamiwa na magaidi, taarifa hizo si sahihi na hazina ukweli wowote,” alisema.
Hata hivyo, Mulongo aliwataka viongozi wa chama tawala na serikali, wasioweza kasi ya utendajikazi wa CCM, kuachia ngazi.
 Katibu wa Chama mkoani hapa, Miraji Mtaturu, aliipongeza jumuiya hiyo kutokana na kazi nzuri inayofanya.
Aidha, Amina alisema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea uwezo na uelewa wa masuala mbalimbali vijana.

Manispaa ya Ilala yatoa tuzo katika shule zake


NA EMMANUEL MOHAMED
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, imetoa tuzo kwa shule za msingi na sekondari zilizofanya vizuri kitaaluma na uboreshaji wa mazingira kwa mwaka 2014, zilizoko kwenye wilaya hiyo.
Katika hafla hiyo, Shule ya Sekonsdari ya Zanaki, iliongoza na kupewa tuzo.
Aidha, Shule ya Sekondari Minazi Mirefu, iliipata tuzo ya uboreshaji wa mazingira.
Tuzo hizo zilitolewa kwa shule za serikali na zisizo za serikali zilizofanya vizuri katika mitihani ya darasa la nne,  darasa la saba na kidato cha nne.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymound Mushi, alikabidhi tuzo hizo jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Saalam, wakati maadhimisho ya siku ya elimu na kilele cha mazingira.
Mushi alisema mpango huo ulioanzishwa ni sehemu ya mikakati ya serikali katika Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alisema utoaji wa elimu bora una uhusiano na usafi wa mazingira na kwamba inasaidia kuongezeka kwa ufaulu wa shule za wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu wilaya hiyo, Angela Marembeka, alisema utoaji wa tuzo hizo ni moja ya motisha na itasaidia kuchochea ufanyaji kazi stahiki.

Askofu awashauri viongozi Dar


NA REHEMA MAIGALA
MWENYEKITI  wa Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste Tanzania (PPFT), Askofu Pius Ikongo, amewashauri viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, kubadilisha ratiba ya ufanyaji wa usafi barabarani.
Alisema wafanya usafi wanatakiwa  kufanya kazi zao  jioni, kuanzia saa 12, ili kuepukana na msongamano mbalimbali  ambayo inakwamisha utendaji wao wa kazi .
Akizungumza na Uhuru jana, Dar es Salaam, Pius alisema bado suala la usafi haliridhishi katika Jiji la Dar es Salaam, kwa sababu ya msongamano na foleni za magari .
Alisema usafi ukifanywa jioni, jiji litaonekana kuwa safi kila siku, hata magari ya kubebea taka  yataweza kufanya kazi mara tatu kwa siku.
 “Ratiba ya usafi lazima ibadilishwe, jiji linatakiwa kufanyiwa usafi jioni, ili kujiepusha na msongamano ya magari na watu inayosababisha usafi usafi usifanyike vile inavyotakiwa”alisema Pius.
Pius aliongeza ratiba hiyo ikibadilishwa, Jiji la Dar es Salaam litaonekana safi wakati wote kama ilivyo miji ya nchi za jirani.
 Alisema wafanyakazi hao wanatakiwa wawe barabarani  wakiwa wamevalia sare zao rasmi kwa ajili ya kulinda mazingira, hasa kwa watu wanaochafua kwa makusudi.
Pius alitolea mfano kwa nchi za jirani kama Afrika Kusini na Kenya kuwa ni nchi ambazo zinazofanya usafi jioni, hali  inayofanya miji katika nchi hizo kuwa safi.

Wednesday, 15 April 2015

JUA LA KUDUMUWATU wa Korea kila siku ya Aprili 15, husherehekea kuzaliwa kwa Rais Kim II Sung aliyezaliwa mwaka 1912 na kufariki mwaka 1994, ambapo huiita siku hiyo kama Siku ya Jua.
Rais huyo ndiye mwanzilishi wataifa la kijamaa la Korea, siku hiyo huitwa siku ya jua kutokana na kiongozi huyo kuwa na hadhi ya juu na mvuto mithiri ya jua.
Siku hiyo huwa ni siku ya kihistoria ambayo huonyesha zama mpya za historia ya mwanadamu, zama za uhuru iliyotokana na falsafa ya Juche, yenye kutambua kuwa nguvu ya watu ndiyo yenyekusukuma mafanikio.
Tangu kuanzishwa kwa falsafa ya Juche, watu waliokuwa wakikandamizwa na kufanywa watumwa wa ukoloni, waliweza kuwa viongozi walioshika hatamu ya taifa lao baada ya mawimbi mazito ya uhuru kusambaa duniani.
Juche, iliweza kuwafikia mpaka moyoni mwa watu duniani, kukusanyika kusoma na kutapakaa kwa falsafa hiyo katika mataifa mengi kukiwa na taasisi zipatazo 1100 katika mataifa zaidi ya 100 ambapo katika kila bara kumekuwa na taasisi za kutoa elimu kuhusiana na falsafa ya Juche.
Rais Kim II Sung, alikuwa akiwapenda watu kwa mtazamo kuwa “Wananchi ndiyo Mungu wangu” ikiwa kama ndiyo kauli mbiu kwenye maisha yake kwa kuwa kila siku alikuwa akijichangaya na watu kwa ukaribu.
Alihakikisha watu wanapata huduma bure za afya na elimu katika taifa lote pamoja na kuondoa mfumo wa kodi kandamizi.
Akiwa kama Baba kwenye jamii ya Wakorea, aliweza kuhudumia familia yake kwa ukaribu , katika maisha yake wananchi walipenda kumuita “ Baba kiongozi” kuliko jina la cheo chake alichokuwa nacho.
Pia, alikuwa mwenye upendo kwa wageni bila kujali mataifa yao, falsafa, mitizamo ya kisiasa na imani za kidini.
IFUTAYO NI MIFANO THABITI.
Septemba 1964, Rais wa Kituo cha Redio cha Guinea alipata ugonjwa wa kuambikizwa alipokuwa ameitembelea Korea akiwa kama kiongozi wa msafara wa waandishi wa habari aliokuja nao.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, Kim II Sung alitoa amri ya kutibiwa kwa kiongozi huyo kwa gharama zozote huku jopo la madaktari waliobobea wakipelekwa kumtibu.
Aliweza kufanyiwa upasuaji kwa kipindi cha masaa saba pamoja na kuwekewa damu alipokuwa  amelezwa hospitalini.
Rais Kim II Sung alihakikisha kiongozi huyo anapatiwa tiba bora, ambapo wakati aliporejeshwa nchini Gunea alisafirishwa kwa ndege ya Korea akiongoza na jopo la madaktari.
Kreisky, Kansela na Mwenyekiti wa zamani wa chama cha kijamaa cha Austria alikuwa hawezi kutembea kutokana na kukabiliwa na maradhi.
Rais Kim II Sung, aliwatuma jopo la madaktari kutoka Korea kwenda Austria wakiwa na madawa ghali aina ya Koryo na hatimae waliweza kumtibu Kiongozi huyo.
Kim II Sung, wakati wa uhai wake kutokana na ukarimu wake aliweza kuwatembelea watu kutoka mataifa ya kigeni zaidi ya 70,000 wakiwemo, Stalin, Julius Nyerere kutoka Tanzania, Mao ze Dong, Zhou Enlai, Fidel Castro, Norodom Shehanouk, Ho Chi Minh,  Tito na Lasana Konte.
Baadhi yawageni walipenda ukarimu wake na walitamani kurudi tena kumtembelea ambao katia yao alikuwa Luise Rinser, mwandishi wa vitabu kutoka Ujerumani.
Wakati alipokutana na Kim II Sung, waliamini kuwa ni kama Mungu ambapo Muhubiri kutoka Marekani Billy Graham alisema taifa la Korea linaongozwa na kiongozi ambaye Mungu amelifanikisha.
Wakati rais Kim II Sung, alipofariki Julai 1994, watu wengi duniani walihisi mbingu zimeanguka huku jua likizama ingawa jua lilikuwa likiangaza.
Mwili wake umehifadhiwa katika Jengo la Kumsusan, lijulikanalo kama Nyumba ya Jua. Watu wa Korea wanaikumbuka April 15 kama siku ya kuzaliwa kwake.
Kauli mbiu ya katifa la Korea ni “Kiongozi wetu mkuu, Komredi Kim II Sung, yupo nasi kila siku” na “Tuinue mikono yetu kuunga mkono fikra za kimapinduzi za Kiongozi wetu Komredi Kim II Sung!” huku picha yake ikipamba kwa tabasamu lake zuri.
Tamasha la Kirafiki la Mwezi Aprili la sanaa za kimataifa, hufanyika kuazimisha siku ya kuzaliwa kwake. Pamoja na maonyesho katika mlima Myohyang, zikionyeshwa zawadi zilizowasilishwa kwake baada ya kifo chake kutoka kwa viongozi wa mataifa ya kigeni, wanasiasa na wanajamii.
April 1995, mwaka mmoja baada ya kifo chake, tamasha la shujaa wa kabila la Jua lilifanyika Nigeria. Katika tamasha hilo mfalme wa jamii ya Ummuozzi alisema “Rais Kim II Sung, ni jua linaloangaza usawa wa ubinaadamu. Licha ya kufariki kwake, daima atakuwa nasi kama jua linavyoa angaza”
Kama Jua linavyoa angaza hivyo Rais Kim II Sun, ni moyo wa usawa kwa wanaadamu.
MANGYONGDAE
MANGYONGDAE ni mji aliozaliwa kiongozi mwanzilishi wa Taifa la kijamaa la Korea Kim II Sung Aprili 15, 1912.
Mji huo unajulikana zaidi kutokana na uzuri wake tangu enzi za Karne kutokana na kuzungukwa kwa mabonde na mlima mrefu wa Mangyong.
Katika mabonde hayo watu wanafurahia mandhari nzuri ya ndege wazungukao mabonde hayo, katika mji huo aliozaliwa Rais wa taifa la Korea unaendelewa kutunzwa kama hazina ya taifa.
Wageni wanashangaa na kuvutiwa namna nyumba ya kiongozi huyo ilivyokuwa  ya kawaida ukilianganisha na makazi ya viongozi wengine ulimwenguni.
Kiuhalisia ilikuwa nyumba ya mtumishi kwenye mabonde na makaburi ya Bwanyenye katika mji wa Pyongyang.
Familia yao ilikuwa masikini sana kukidhi kugharamia nyumba ya namna hiyo iliyotokana na Babu yake mkubwa kuwa mtunza makaburi ya Bwanyenye na kumfanya aweze kuishi hapo.
Katika nyumba hiyo ndipo waliishi wazalendo waliojitolea maisha yao kulitumika taifa lao kwa kizazi hadi kizazi.
Kim Ung U, ambaye ni Babu yake mzaa babu wa Kim II Sun, aliongoza kuizamisha meli ya General Sherman uliyofanyiwa ukarabati na kuitwa Shenandoah, meli hiyo ya Marekani iliivamia Korea katika kipindi cha katikati ya Karne 19.
Mababu wa rais wa taifa la Korea walishirikiana kwa juhudi za dhati kupitia shughuli za kimapinduzi kwa watoto na wajukuu zao wakiwa kama wakulima wa kawaida.
Nyumba hiyo pia ilikuwa makazi ya Baba yake Kim Hyong Jik, kiongozi imara aliyepinga uvamizi wa Japan katika taifa la Korea, Mjomba wake Kim Hyong Gwon na mdogo wake Kim Chol Ju, walijitolea maisha yao kwa ajili ya kufanikisha harakati za  mapinduzi kisha kujipatia uhuru.
Mama yake Kim Kang Pan Sok, kiongozi shujaa aliyewaongoza wanawake wa Korea pia aliishi katika nyumba hiyo kwa kipindi kifupi.
Ndani ya nyumba hiyo kuna dawati pamoja na jiwe la wino lililokuwa likitumiwa na Kim II Sung wakati akiwa shuleni, pamoja na meza, ubao wa kuchorea, chombo cha kubebea moto, jembe, mkeka na kibao cha kushonea.
Aidha kuna chungu cha kuwekea maji hivyo maisha ya wazazi wa Rais huyo yalikuwa ni masikini hadi kufikia hatua ya kushindwa kununua jagi au ndoo za kisasa wakati huo za kutunzia maji.
Kutokana na mfumo huo wa maisha, babu na wazazi wa kiongozi huyo walimfundisha namna ya kuishi maisha ya kizalendo kulingana na mwenendo wa familia ya Mangyongdae waliokuwa tayari kufariki pasipo kusita kwa manufaa ya taifa.
Uwanja wa mieleka, eneo la kusomea pamoja na mwamba mithiri ya manoali waliokuwa wakitumia kucheza wakati wakiwa askari ambapo Kim II Sun hamasa za kishujaa dhidi ya ufedhuri wa Japan bado vinaendelea kutunzwa.
Kim II Sung, aliondoka nyumbani baada ya baba yake alipoanzisha harakati za kupigania uhuru wa taifa hilo mwaka 1923.
Akiwa na umri wa miaka 11 alisafiri kwa miguu umbali wa kilometa 250, akitokea Kaskazini Mashariki ya China kwenda Mangyongdae kujifunza zaidi uhalisia wa taifa lake akiwa peke yake.
Januari 25, 1925, akiwa anasoma nchini kwake, alipewa taarifa yakuwa baba yake amekamatwa na askari wa Japan hivyo aliondoka Mongyongdae na kuapa kuwa hatorudi katika ardhi hiyo mpaka atakapo likomboa taifa lake.
Baada ya miaka 20, alirejea tena na kuanzisha harakati za mapambano dhidi ya unyonyaji uliokuwa ukifanywa na Japan na kufanikisha kulikomboa taifa hilo Agosti 15, 1945.
Akiwa amerejea kwa mafanikio alitembelea kiwanda cha chuma cha Kangson (Kwa sasa Chollima Steel Complex) kwa dhamira ya kuijenga Korea mpya licha ya njia ya kiwanda hicho ndiyo yakuelekea nyumbani kwao.
Baada ya kuanzisha chama cha Wafanyakazi wa Korea, Oktoba 10, 1945 akisaidiwa na wananchi awaliojawa na furaha katika mapokezi ya kihistoria yaliyofanyika Pyongyang, Oktoba 14, 1945, aliweza kuingia nyumbani kwao akitumia mlango uliojengwa kwa fito.
Bibi yake alimkimbilia alipofika barazani kwa kumbusu na kumlaki kwa kumwambia “kwanini umerejea nyumbani kwa kuwaacha nyuma baba na mama yako”.
Hali hiyo ilitokana na kuwa wanafamilia wengi waliiacha nyumba hiyo na kwenda kushiriki vita vya ukombozi lakini Kim II Sung ndiye pekee aliyerejea.
Tangu hapo, Rais Kim II Sung, popote pale anapouona mlango uliojengwa kwa fito hukumbuka ni wanafamilia wenzake wangapi waliotoka katika mlango wa aina hiyo na wangapi walirejea.
Kwa sasa Mangyongdae ni ardhi ya mapinduzia ya watu wa Korea iliyobarikiwa na maendeleo ya Dunia yaliyoamini katika falsafa ya Juche na kuhamasisha baada ya uhuru.
Wananchi wa Korea kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wageni wamekuwa wakitembelea eneo hilo kukusanya ujuzi wa Kiongozi huyo pamoja na kupanda miti na maua.
Zaidi ya watu milioni 120 wameshatembelea mji wa Mangyongdae katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Tuesday, 14 April 2015

Taasisi za dini kufutwa  •  Ni zilizoshindwa kuwasilisha mapato na matumizi 
  •  Zingine zajiingiza kwenye siasa kinyume cha sheria 

NA MWANDISHI WETU 
TAASISI za dini ziko hatarini kufutwa katika orodha ya usajili kutokana na kuvunja sheria kwa kushindwa kutoa taarifa za mapato na matumizi ya hesabu za fedha kwa mwaka, imeelezwa.  
Kazi ya kuzifuta taasisi hizo,  inatarajia kufanyika Jumatatu ijayo, baada ya kukamilisha uchambuzi wa taasisi hizo na kwamba itaanzia jijini Dar es Salaam na baaadaye mikoani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu mustakabali wa nchi.

Alisema taasisi hizo ni zile ambazo hazifuati matakwa ya kisheria ikiwemo kuwasilisha taarifa za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada.
Chikawe alisema baadhi ya taasisi hizo ambazo zinakiuka sheria pia katika siku za hivi karibuni viongozi wa taasisi hizo, wamekuwa wakitoa matamko yanayoashiria kuingilia masuala ya kisiasa, kinyume cha sheria na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Waziri Chikawe alisema matukio hayo yamekuwa yakisababishwa na hamasa za kisiasa au baadhi ya watu waliokuwa wakitumia muda huo kutekeleza ajenda zao kwa kisingizio cha vuguvugu za kisiasa.
Alisema viongozi wa taasisi hizo wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi lakini ni kinyume cha sheria Sura ya 337, kutumia uongozi wao kushawishi waumini kutekeleza matakwa yao ya kisiasa.
Waziri alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitoa matamshi ya kulenga na kushawishi wafuasi wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba Inayopendekezwa au kuhusu uchaguzi mkuu  wa Oktoba, mwaka huu.
“Matamshi haya yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo na hivyo serikali inatoa onyo kali kwa vikundi, zikiwemo taasisi hizo kuepuka kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini,” alisema.
Pia katika mkutano huo, Chikawe alizungumzia suala la viongozi wa dini wanapochangisha pesa na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachodaiwa kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbaliz za uongozi.
“Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni huku katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizi zinaeleza wazi kuwa kitendo hicho si kazi ya taasisi hizo,” alisema.
Alisema kuendelea kwa matukio hayo ya taasisi hizo kushiriki katika mambo ya kisiasa kunahashiria kuvurugika kwa amani na utulivu wa nchi.
Alisema matukio hayo yanahashiria uvunjifu wa amani na utulivu na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha taasisi hizo pamoja na viongozi wake wanadhibitiwa. 
Wiki iliyopita,Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,  Josephat Gwajima, alihojiwa kwa takribani saa sita katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalumu  ya Dar es salaam.
Gwajima alihojiwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa na matusi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, Februari, mwaka huu.
Kabla ya kufikishwa Kituo cha kati, alihojiwa katika  Kituo cha Polisi cha Oysterbay wiki mbili baada ya kuzirai akiwa kwenye kituo kikuu cha polisi na kupelekwa katika hospitali ya TMJ, Mikocheni kwa ajili ya matibabu. 
Mbali na kumhoji, polisi walimtaka kuwasilisha orodha ya mali zake, fedha alizo nazo katika benki tofauti, hati ya kumiliki helkopta, makanisa yake yote na ndugu zake walio hai na walio kufa.
Gwajima alitakiwa  kurudi tena kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kesho.