Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Saturday, 11 January 2014

Mauzo ya dhahabu Nje yashuka

NA MWANDISHI WETU, MWANZA

MAUZO ya Dhahabu nje ya nchi yemeshuka kwa kiasi cha asilimia 14.8 wakati mauzo ya almasi yakipaa maradufu kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013.
Kushuka kwa mauzo hayo ya wachimbaji wakubwa na wadogo, kulisababishwa zaidi na kufungwa kwa migodi ya Tulawaka, Resolute, kushuka kwa kasi ya uzarishaji na uuzaji wa nje na kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia.
Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Tawi la Mwanza, Mussa Mziya, alisema katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu kanda ya Ziwa kwa nje ya nchi yalipungua kwa kiasi hicho kufikia dola za Marekani milioni 1,901.2 (karibu sh. 2.5)  milioni kutoka dola 2,232.3 (zaidi ya sh. bilioni tatu) kwa mwaka 2011/2012.
Kiasi cha dhahabu kwa wachimbaji wakubwa, kilipungua kutoka kilo 39,544.8 mwaka 2011/2012 hadi kufikia kilo 37,796.3 kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013 huku madini hayo yakianguka kwa asilimia 10.9 kutokana na kuimarika kwa dola.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioisha Juni 2013, thamani ya madini toka kwa wachimbaji wadogo pia iliporomoka kwa asilimia 55.8 kufikia dola milioni 5.5 (zaidi y ash. Bilioni saba) milioni kutoka dola milioni 9.4 (zaidi ya sh. bilioni 1.7) zilizopatikana mwaka 2011/2012.
“Thamani ya dhahabu pekee kutoka wa wachimbaji wadogo kwa kipindi tajwa ilishuka hadi dola milioni 3.9 kutoka dola milioni 8.3 milioni mwaka 2011/2012 kutokana na kuanguka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia wakati thamni ya almasi kutoka kwa wachimbaji hao wadogo ikipaa,” alifafanua.
Alisema almasi ya wachimbaji hao ilipanda hadi dola milioni 1.8 kutoka dola milioni 1.2 kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wake.
Mauzo ya almasi nje ya nchi yaliongezeka mara dufu kufikia dola milioni 44.8 milioni katika mwaka 2012/2013 kutoka dola milioni 11.5  mwaka 2011/2012.
Kuongezeka kwa mauzo ya almasi kulichangiwa na uhuishaji mkubwa  katika mgodi wa almasi wa Williamson Diamond, ulioko Mwadui mkoani Shinyanga.

Mwanza kwafukuta

NA PETER KATULANDA, MWANZA

MTUNZA Fedha na Karani wa malipo wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wamesimamishwa kazi huku wahasibu wawili na mtunza stoo ya vitabu vya mapato, wakitakiwa kupelekwa polisi.
Wakati watuhimishi hao wakikumbwa na ‘dhoruba’ hiyo, Mweka Hazina wa Jiji, Rengise Eringia, amenusurika kutimuliwa baada ya kupewa onyo kali na kutakiwa kujirekebisha ndani ya miezi mitatu kuanzia juzi.
Watumishi hao wanadaiwa ‘kutafuna’ mamilioni ya fedha za jiji hilo, zikiwemo sh. milioni 28 za ushuru wa samaki zilizokusanywa katika kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Tanzania Fish Processors (TFP).
Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, alisema mamilioni hayo yalipokusanywa, badala ya kuwekwa kwenye akaunti ya halamshauri, yaliwekwa katika akaunti binafsi ya mfanyakazi mmoja ambaye amekiri kutenda kosa hilo.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji, siku moja baada ya kugomea bajeti ya mwaka 2014/2015 ya zaidi ya sh. bilioni 87.2, kwa madai kuwa vyanzo vingine vya mapato ya ndani havikuainishwa.
Wakiongozwa na Meya Mabula na Naibu wake John Minja (CCM), katika Kikao cha baraza cha Januari 9 mwaka huu, madiwani hao walidai bajeti hiyo imetengenezwa kwa ajili ya maslahi ya watu binafsi (watumishi wa jiji) na siyo wananchi wa Mwanza na hivyo kuapa kutoipitisha hadi itakapokidhi maslahi ya wananchi.
Baada ya uamuzi huo ambao umekuwa wa kwanza katika historia ya jiji hilo, Mabula alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Hassan Hida, aitishe kikao cha Kamati ya Fedha kupitia upya na kurekebisha bajeti hiyo kabla ya kikao cha Baraza kukaa na kupitia vyanzo vya mapato vilivyo chakachuliwa.
Kamati hiyo juzi ilipochambua mapato ya jiji, baadaye iliketi kama kamati ya nidhamu na na kujadili watumishi hao ambao wanadaiwa kujikusanyia mamilioni hayo ya fedha kwa kutumia kitabu kimojawapo cha kukusanyia mapato katika kiwanda hicho.
Baada ya kikao hicho, ndipo baraza lilipokaa nalo kulazimika kujigeuza kama Kamati na kuwajadili watumishi hao kabla ya kutoa maamzi hayo magumu huku makachero wakiwa wamezingira ukumbi wa jiji hilo ili wawatie mbaroni wahasibu hao na kuambulia patupu.
Akitangaza uamuzi huo, Mabula aliwataja wahasibu waliosimamishwa na watatakiwa kufikishwa kwenye mkono wa sheria kuwa ni Rabisante Meena (Mhasibu Mkuu wa Mapato), Edwin Magere  ambaye ni Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Mpato na Mariam Mjema (Mtunza Stoo Msaidi wa Vitabu vya Mapato.)
Wengine waliosimamishwa kwa ajili ya uchunguzi wa ndani ni Geoffrey Liana (Mtunza Fedha wa Dirishani) na Mary Mushi Mhasibu Mkuu wa mapato ya jiji hilo.
Mabula ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, alidai kwamba huo ni mwanzo tu bado wanaendelea kufatilia baadhi ya ubadhilifu unaodaiwa kufanywa na watendaji wa jiji hilo katika miradi mbalimbali kabla ya kuwachukulia hatua.
Wakati kikao hicho kikiendelea, makachero wa polisi walionekana kutanda katika maeneo ya jengo la Halmashauri ya jiji hilo wakisubiri kuwatia mbaroni watumishi ambao waliamriwa kufikishwa kwenye mkono wa sheria lakini waliambulia patupu baa ya watumishi hao kuondoka mapema baada ya kuhojiwa na Kikao hicho.

UVCCM ‘yawavaa’ watangaza nia

NA CECILIA JEREMIAH

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umelaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama kwa kuanza kuwanadi wagombea kinyume cha kanuni zilizopo.
Viongozi walionywa na UVCCM ni Wenyeviti, Makatibu, Madiwani na wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakitumika kuwanadi wagombea hao kinyume cha taratibu na kanuni za Chama.        
Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa, Paul Makonda, alisema viongozi hao wamekuwa wakifanya kampeni kabla ya muda haujafika, hivyo wanatakiwa kuacha vitendo hivyo na badala yake wanapaswa kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo.
“Kamati ya maadili ya CCM ina wajibu wa kutafsiri hasira ya wana-CCM na viongozi wao kwa vitendo ikiwemo kufuatilia suala hilo na kuwachukulia hatua endapo wakibainika kuhusika na vitendo hivyo,’’alisema.
Aliseam UVCCM inawataka wale wote walioanza kampeni za urais, ubunge na udiwani, waachane na vitendo kwa kuwa muda haujafika.
Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, alioa taarifa ya kulaani vitendo vya baadhi ya viongozi ndani ya Chama kuanza kampeni za urais kabla ya wakati.

Sunday, 5 January 2014

Kikwete awashukia vigogo wapotoshaji

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amewashukia baadhi ya viongozi na kuwataka kuacha kupotosha mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya kwa maslahi binafsi.
Pia amewahakikishia wananchi kuwa maoni zaidi yataendelea kupokewa kwa ajili ya kupata katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya wengi kupitia wabunge wa Bunge la Katiba.
Rais Kikwete alisema hayo jana, alipopokea matembezi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuyaenzi Mapinduzi katika Uwanja wa Maisara, mjini hapa. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni pia  alihudhuria.
Alisema katika Bunge Maalumu la Katiba, wananchi watakaotaka serikali tatu au mbili wanayo nafasi ya kutoa maoni, hivyo kuwaonya wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuhusu mchakato mzima wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwake na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwakumbusha vijana kuwa, Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyowakomboa wazalendo wa Zanzibar na si uhuru wa Desemba 10 uliotolewa na Uingereza, kwani ulikuwa wa bandia.
Kutokana na hilo, aliwataka vijana kuyaenzi kwa nguvu zote Mapinduzi na kwamba, vijana wa CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na watu wanaojaribu kupotosha ukweli.
“Vijana mtambue vizuri kuwa Mapinduzi yaliyofanywa na wazee wetu ndiyo halisi yaliyotuweka huru na kukomesha unyama na udhalilishaji, yale ya Mwingereza yalikuwa feki. Tunapaswa kuyalinda na kukabiliana na wote wanaotaka kupotosha kwa maslahi yao,’’ alisema.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuyaendeleza Mapinduzi, ambayo misingi yake inaendelea kutekelezwa, ikiwemo wananchi kupewa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Rais Kikwete alisema malengo ya Mapinduzi ni kuwapatia wananchi elimu kuanzia ya msingi hadi  sekondari, ambayo katika utawala wa kikoloni yalikuwa hayatekelezwi.
Aliwataka vijana na wananchi kwa jumla kujitayarisha kujitokeza kwa wingi kusherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao ni wa kupigiwa mfano barani Afrika.
UVCCM WAMVAA WARIOBA
Kwa upande wake, UVCCM imemvaa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuhusu mapendekezo ya muundo wa serikali tatu.
Umoja huo umesema mapendekezo yake ni kinyume cha misingi ya waasi wa taifa, ambayo ni ya serikali mbili kwa lengo la kuhakikisha Muungano unadumu na kupunguza gharama.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM (Zanzibar), Shaka Hamdu Shaka, alisema wameshitushwa na Rasimu ya Katiba, kwani ina dalili za kuleta mpasuko wa taifa iwapo serikali tatu zitapitishwa.
Alisema rasimu imekosa mashiko ya makubaliano ya waasisi wa taifa la Tanganyika na Zanzibar, wakati wakiunganisha mataifa hayo na kuzaliwa Tanzania.
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alisema wameshangazwa na rasimu kupendekeza muundo wa serikali tatu.
“Vijana tunawaheshimu viongozi wakiongozwa na Jaji Warioba, lakini tunasema warudi tena, kwani serikali tatu zinatishia umoja na mshikamano wa taifa,’’ alisema.
Awali, Mapunda alisema matembezi hayo yaliyoanza Desemba 22, mwaka jana, yaliwahusisha vijana 1,200 yakilenga kuamsha shamrashamra za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwaweka tayari vijana kushiriki maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Mapunda alisema CCM imejizatiti kushinda uchaguzi huo kuanzia nafasi ya rais, wabunge, wawakilishi na madiwani.


Zitto aipasua CHADEMA

NA FURAHA OMARY

JAJI John Utamwa wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, leo atatoa uamuzi wa ama kutoa au la zuio la muda kwa Kamati Kuu ya CHADEMA, kutojadili au kutoa uamuzi kuhusu uanachama wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Uamuzi huo unaosubiriwa kwa hamu na CHADEMA na Zitto, utatolewa saa nne, asubuhi, mahakamani hapo, baada ya Ijumaa, Jaji Utamwa kusikiliza maombi ya Zitto, aliyoyawasilisha chini ya hati ya kiapo.
Kwa upande wake, Dk. Kitilla Mkumbo, amesema hajutii kufukuzwa CHADEMA, kwa kuwa huo si mwisho wa harakati zake kisiasa.
Zitto kupitia wakili Albert Msando, diwani wa CHADEMA, kata ya Mabogini, Moshi, Januari 2, mwaka huu, alifungua kesi namba moja ya mwaka 2014 na kuwasilisha maombi chini ya hati ya kiapo.
Kesi hiyo iliyofunguliwa dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho na Katibu Mkuu wa CHADEMA, ipo mbele ya Jaji Utamwa na imepangwa kutajwa Februari 13, mwaka huu.
Anaiomba mahakama iiamuru Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote cha chama hicho, kutojadili na kuchukua uamuzi kuhusu uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na baraza kuu la chama hicho.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba mahakama imuamuru Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, ampatie mwenendo wa kikao cha Novemba 22, mwaka jana, cha baraza kuu ambacho kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake zote za kichama.
Maombi ya Zitto yalisikilizwa Ijumaa, iliyopita, mahakamani hapo, ambako kulitokea vurugu kati ya wafuasi wa CHADEMA na wanaodaiwa kumuunga mkono Zitto, kabla na baada ya Jaji Utamwa, kusikiliza hoja za wakili Msando na mawakili wa CHADEMA, Tundu Lissu na Peter Kibatala.
Akiwasilisha maombi hayo katika ukumbi namba moja uliokuwa umefurika wafuasi wa chama hicho, Msando aliiomba mahakama kutoa zuio la muda kwa kamati kuu ya CHADEMA, isimjadili Zitto kwenye vikao vyake kuhusu uanachama.
Msando mbele ya Jaji Utamwa alidai wanaomba amri ya zuio kwa sababu Zitto ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na kwa mujibu wa Katiba, mtu atakuwa mbunge kutokana na chama cha siasa.
Alidai endapo kamati kuu ya chama hicho itakaa na kufikia uamuzi ambao utasababisha apoteze uanachama, matokeo ya uamuzi huo, hayataweza kufidiwa kwa sababu muombaji atapoteza nafasi ya ubunge na hataweza kuwawakilisha wananchi waliomchagua kwa kura ambao si wa chama hicho pekee.
Msando alidai Zitto pia atapoteza nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na iwapo mahakama haitatoa zuio hilo, ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi kutokana na mazingira ya kesi na nafasi ya uongozi.
Aliiomba mahakama katika kutoa amri ya zuio la muda iangalie maslahi ya wengi na si faida ya wachache na madai ya CHADEMA kwamba taarifa za kikao kilichomvua nyadhifa za kichama Zitto zimechelewa kwa sababu zitakamilika baada ya kikao cha kamati kuu cha Ijumaa iliyopita, ni kinyume cha katiba ya chama hicho.
Lissu kwa upande wake alidai Zitto hakuwa na haja ya kwenda mahakamani kwa kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kikao cha kamati kuu kilikuwa kinataka kumvua uanachama.
Alidai katika nyaraka za Zitto alizowasilisha mahakamani alisema: “Wana CHADEMA na wapenda demokrasia watambue mimi ni mwaminifu, nitakuwa wa mwisho kutoka katika chama, nitafuata utaratibu ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.”
Lissu alidai utaratibu wa chama hicho ambao Zitto anasema ataufuata ni kukata rufani na ameshaandika taarifa ya kusudio la kukata rufani na ameandika maombi ya kupatiwa mwenendo wa uamuzi.
“Kama amekubali atafuata utaratibu hadi kuhitimisha mgogoro huu, ugomvi wa kuja mahakamani ni upi?” alihoji.
Alidai akifukuzwa uanachama hakuna madhara yoyote yatakayopatikana kwa sababu Katiba inasema jimbo likibaki wazi, uchaguzi utaitishwa ndani ya siku 90. Alidai Zitto anapaswa kuheshimu chama kilichompa ubunge, akiwa na mgogoro akae ajadiliwe.
Kwa upande wake, Dk. Kitilla alisema umaarufu iliyopata CHADEMA kutoka kwa wananchi unailevya na kuwapofua jambo ambalo litawagharimu.
Alisema anashindwa kuelewa kazi ya chama hicho, kwani chama cha siasa kina wajibu wa kuongeza wanachama jambo ambalo wanakwenda kinyume chake kwa kuita vyombo vya habari na kutangaza kufukuza wanachama kila mara.
“Siasa si kazi ambayo inanipatia ajira, hivyo kufukuzwa CHADEMA si jambo ambalo litanishughulisha, kwani kuondoka huko si mwisho wa kufanya harakati zangu za kisiasa.
Nawashangaa CHADEMA wakati wenzao CCM wanazunguka mikoani kukiiimarisha Chama, wao wapo katika vikao vya kufukuzana,” alisema.
Aliongeza: “Kwa sasa tayari katika baadhi ya maeneo wanashusha bendera na kuchana kadi kutokana na kutoridhishwa na fukuza-fukuza isiyokuwa na tija.”
Alisema hawezi kuomba msamaha, kwani hajaona kosa alilofanya, pia kitendo cha kumfukuza hakitamuathiri, kwani ana ajira na alikuwa hakitegemei katika kumuendeshea maisha.
Dk. Kitilla alisema kwa sasa hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa.
Alisema dhambi ya kufukuza watu ndani ya chama hicho bado itaendelea kukitafuna, kwani tangu Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA) aingie madarakani, Zitto ni kiongozi wa tano kuondolewa madarakani.

Mgeja awakomalia vigogo wa ujangili

Na mwandishi wetu, arusha

WIMBI la ujangili na usafirishaji wa nyara za serikali zikiwemo pembe za ndovu, hauwezi kukomeshwa iwapo vigogo wanaohusika na mtandao huo wataendelea kufichwa bila kuchukuliwa hatua.
Hatua hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuna baadhi ya watendaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi, hushiriki kwenye biashara ya pembe za ndovu, jambo linalosababisha tembo kuuawa kila kukicha.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema hata wawekezaji wanaoingia nchini, wanapaswa kuchunguzwa kwani, wengine hujihusisha na biashara haramu ikiwemo ya pembe za ndovu.
Mgeja, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alikuwa akitoa salamu za Mwaka Mpya wa 2014.
Alisema kwa muda mrefu sasa, baadhi ya watendaji serikalini na kwenye taasisi zake, wanatajwa kujihusisha na biashara hiyo.
Alisema hata katika taarifa ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyowasilishwa bungeni, baadhi ya watendaji wa serikali wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama, wabunge na wanasiasa, wametajwa kuhusika kwenye ujangili ikiwa ni pamoja na kuhujumu operesheni hiyo.
“Watendaji wa serikali wanatajwa katika ujangili na biashara haramu, tunatakiwa kuanza kuwashughulikia kwanza, ndipo baadaye twende kwa wadogo.
“Wananchi wanajitoa muhanga kuwataja, lakini serikali imekuwa na kigugumizi kuwachukulia hatua.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza, imewataja baadhi ya watendaji na wabunge kuwa walihusika kuihujumu kwa kuwa wako kwenye mtandao, tuchukue hatua kumaliza tatizo hili,’’ alisema Mgeja.
Alisema biashara ya pembe za ndovu mbali na kuteketeza wanyama kama tembo, lakini imeichafua Tanzania kimataifa, lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kukomesha.
Kufuatia hali hiyo, Mgeja alitoa wito kwa viongozi wa dini nchini, kuliombea taifa ili kuondokana na matukio mabaya yanayotokana na watendaji waliopewa dhamana kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Pia, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuanzisha madarasa maalumu kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo hasa kwa vijana, yanayoendelea kwa sasa nchini ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo.

Mama alilia haki ya kuishi na mwanaye

Na Rabia Bakari

MKAZI wa Kinondoni Dar es Salaam, Nuru Dominick, ameziomba taasisi za kisheria, kumsaidi ili kupata haki ya kuishi na mwanaye Abdurahim Abdul (2).
Abdul, kwa sasa anaishi na baba yake Abdallah Masoud, baada ya kutengana kutokana na sababu za kifamilia na kwamba, shauri hilo lilifikishwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Nuru alisema aliolewa na Masoud mwenye asilia ya Kiasia, lakini baadaye kulitokea ugomvi na hatimaye kutengana.
“Baada ya kutengena, akagoma kunipa mtoto na ameniwekea masharti magumu ambayo anajua kwa sasa sitayaweza...mtoto wangu ana miaka miwili, siko radhi awe mbali na uangilizi wangu,” alisema Nuru.
Alisema kesi hiyo ya mtoto imepita katika hatua mbalimbali kuanzia ya familia na hatimaye kupelekwa Baraza Kuu la Waislam Tanzania, ambako huko nako, waliamua mtoto aishi na baba yake bila kujali athari na umri alionao.
Alisema baada ya kuolewa mwaka 2009, Masoud alimbadili dini pamoja na kumuachisha kazi, lakini akiwa kwenye maisha ya ndoa, ndugu wa mumewe walimnyanyapaa hali iliyozua ugomvi, na hatimaye kuachana.
Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Masoud alikiri kuishi na mtoto huyo na alisema hayuko tayari mwanaye alelewe katika mazingira mabovu na yasiyoridhisha.
“Hapa nyumbani nina mke na wafanyakazi, mtoto atalelewa, kinachomsumbua Nuru ni wivu, kuona mtoto analelewa na mama wa kambo, naelewa mtoto ni wetu sote na haki ya kukaa naye, lakini atafute mazingira mazuri kwanza, niridhike, ndipo nitampa mtoto,” alisema.
Hata hivyo, Nuru alisema Masoud alimwachisha kazi hivyo masharti anayompa ili kumrejesha mtoto huyo anatambua hataweza kuyatimiza na kuwa ni sehemu ya kuendelea kumnyanyasa.

Muuguzi aishi ‘Leba’, huduma zasimama

Na Jumbe Ismailly, Ikungi

HUDUMA za kujifungua katika Zahanati ya Kata ya Iglansoni wilayani hapa, zimesimama kwa muda, baada ya chumba kilichokuwa kikitumika kufanywa nyumba ya muuguzi mkuu wa zahanati hiyo, Meriani Misai.
Uongozi wa zahanati hiyo iliyopo tarafa ya Ihanja, mkoani Singida, ulifikia uamuzi huo baada ya Meriani kutokuwa na nyumba ya kuishi kwa kipindi kirefu sasa.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iglansoni, Rehema Majii, dari la nyumba ya kuishi muuguzi huyo, lilianguka kutokana na popo kugeuza makazi yao.
Alisema Meriani alikuwa akishindwa kulala hususan kipindi cha mvua, kutokana na nyumba yake kuvuja kila mahali.
 “Kila mvua ilipokuwa ikinyesha ilikuwa ni adha kwa muuguzi wetu, alikuwa akilazimika kukaa kwenye kiti mpaka asubuhi bila kulala kutokana na nyumba yake kuvuja.
Tumelazimika kufanya utaratibu wa kumuhamishia katika moja ya vyumba vya Zahanati hii kutokana na kukosa sehemu ya kuishi,” alisema Rehema.
Alisema baada ya mtumishi huyo kuhamia kwenye chumba hicho, huduma za kujifungua zimesimama katika Zahanati hiyo.
Kwa upande wake Meriani, alisema ameishi katika nyumba hiyo kwa miaka mitatu huku popo wakiwa wamejaa na kusababisha nyumba kutoa harufu mbaya.
Alisema kwa sasa wajawazito wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 50 kufuata huduma hizo katika zahanati ya Kata ya Muhintiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Magayane Protace, alisema alimuagiza Rehema kumtafutia nyumba ya kupanga ambayo halmashauri italipia gharama za pango kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa, wakati nyumba hiyo inafanyiwa ukarabati.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dk. Henry Mbando, alisema kutokana na dharura hiyo iliyojitokeza, wameshafanya tathimini, ambapo zaidi ya sh. milioni sita zinahitajika kuifanyia ukarabati nyumba hiyo.

Friday, 3 January 2014

CCM yakunjua makucha

Na Hamis Shimye

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekunjua makucha yake dhidi ya wanachama wanaotangaza nia ya kugombea uongozi kabla ya wakati na kwamba wataitwa kwenye kamati Kuu na kuhojiwa.
Mbali na kuwaita na kuwahoji, kimesema wale watakaobainika kuwa wamekiuka taratibu watachukuliwa hatua za kinidhamu bila kujali umaarufu au nafasi zao.
Kauli hiyo nzito na ya aina yake ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa wa CCm (Bara), Philip Mangula, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wanachama hao ambao mbali na kuonyesha kila dalili za kutangaza nia hasa nafasi ya urais, wamekuwa wakifanya mambo ambayo ni kinyume cha utaratibu na kwamba hali hiyo inaleta nyufa ambazo zinaweza kukisambaratisha Chama.
Alionya kuwa wanachama hao wanaopita sehemu mbalimbali kujaribu kushawishi watu ili kukubalika juu ya azma yao, wanaopasa kuacha mara moja vitendo hivyo.
“Wanachama hao wasipoacha tabia hiyo wasitarajie kuteuliwa kuwa wagombea wa CCM, labda wawakilishe vyama vyao vya kijiweni na si Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Mangula alisema kila mwanasiasa anapasa kutii kanuni na maadili ya Chama, ambapo viongozi nao wanapasa kusimamia hilo.
“Ikiwa hauzingatii kanuni na taratibu za Chama basi wewe hufai kuwa kiongozi wa CCM labda ukateuliwa na chama chako cha kijiweni ndiyo ukiongoze na si chama hiki,” alisisitiza.
Alisema viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa, wanapasa kutumia vikao vya Kamati za Siasa kuwaita, kuwahoji, kuwaonya na hata kuwachukulia hatua viongozi na wanachama  wanaojipitisha na kutangaza nia za kugombea.
Mangula alisema huu si wakati wa uchaguzi bali ni kipindi cha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa viongozi walioko madarakani, ambao walichaguliwa 2010.
“Chama hakina ajenda ya uchaguzi mkuu. Anayejitokeza na kusema yeye anafaa, huyo ana ajenda binafsi na hajatumwa na Chama. Na wale wanaojifanya wasafi wajiulize mikono yao hainuki damu ya rushwa?,”alisema.
Alisema kila kiongozi anapasa kuheshimu kanuni za uongozi na maadili kwa kuwa ndizo nguzo za uwajibikaji kwa viongozi wote wa CCM.
Mangula alisema kanuni hiyo, imeelekeza kila kuhusiana na mambo yasiyoruhusu na anapojitokeza mtu anapokwenda kinyume cha mambo hayo anaonyesha udhaifu mkubwa.
Kutokana na msimamo huo, aliziagiza Kamati za Siasa za Matawi hadi Mikoa kulitazama jambo hilo na kuwapa taarifa wote wanaojipitisha pamoja na kuwasilisha taarifa zao Makao Makuu ya Chama.
Katika hatua nyingine, Mangula aliipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutoa rasimu ya pili ya Katiba Mpya na kusisitiza kuwa huu ni wakati wa Chama kujipanga kwa kuelimisha wanachama wake, hasa baada ya Tume kukusanya na kuchambua maoni.
“Nayaagiza matawi yetu kuanzia chini kutoa elimu ya kutosha kuhusiana na rasimu hiyo, ili kuwaelemisha wananchi wakubali au kukataa,”’alisema.
Pia, alisema ajenda muhimu kwa CCM kwa mwaka 2014 ni Katiba Mpya na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo ni wakati wa kuwaelimisha  wanachama na wananchi juu ya mambo hayo na si vinginevyo.
Vinara wa makundi kuitwa
Kuhusu uchaguzi mkuu wa Chama mwaka 2012, alisema kilipokea malalamiko 94 ambapo na kamati ya Maadili ya Chama.
Mangula alisema baadhi ya malalamiko yameshafanyiwa kazi kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na jumuia za Chama, ambapo malalamiko mengine hayakufanyiwa kazi baaada ya kuchambuliwa na kuonekana hayana msingi.
“Malalamiko yaliyofuatiliwa na kufanyiwa kazi ni 33, ambapo idadi hiyo imepungua kutokana na baadhi ya nafasi moja kulalamikiwa na zaidi ya mtu mmoja. Kamati Kuu imeshafanya uamuzi juu ya malalamiko matatu,’’alisema.
Mangula alisema malalamiko hayo ni kwa wilaya za Momba, Longido kurudia uchaguzi wa nafasi za Mwenyekiti wa Wilaya na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) huku Wilaya ya Lindi nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya.
Alisema baada ya mchakato huo kumalizika Kamati Kuu imeongeza miezi sita kushughulikia malalamiko yaliyobakia huku Tume ya Udhibiti na Nidhamu ikibaini chanzo kikubwa cha matatizo ni makundi, ambapo imepanga kuwaita baadhi ya watu ambao wanaonekana wanaweza kukivuruga Chama.

Wafuasi wa Zitto, CHADEMA wazichapa

NA FURAHA OMARY

WAFUASI wa CHADEMA na wale wanaodaiwa wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, jana walitwangana makonde nje ya viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hali hiyo ilijitokeza kabla na baada ya Jaji John Utamwa kusikiliza maombi ya Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kuiomba mahakama itoe zuio la muda kwa Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote kumjadili na kuamua kuhusu uanachama wake.
Vurugu hizo zilianza mapema saa 3.30 asubuhi, baada ya mahakama kutamka kwamba maombi ya Zitto ambayo amefungua dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho, yatasikilizwa saa 4.30 asubuhi. Wafuasi wa chama hicho, ambao walikuwa wamefurika  walianza kumzomea Zitto, kwa madai ni fisadi na kwamba kesi aliyofungua inawapotezea muda.
Kutokana na hali hiyo, Zitto, aliyekuwa akilindwa na mabaunsa wawili na vijana wengine wawili, aliondoka eneo hilo na kwenda kukaa katika chumba maalumu kwa usalama wake.
Hali hiyo ilisababisha Wakili wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuwaita wanachama hao na kuwasihi watulie wasikilize walichoitiwa mahakamani hapo ili wasizuiwe kuingia mahakamani.
Hata hivyo, ilipotimia saa 5:50 asubuhi, wafuasi hao walianzisha fujo tena na kutaka kumpiga mtu mmoja kwa madai anawarekodi, jambo lililomlazimu mmoja wa askari kanzu kuingilia kati na kumuokoa mtu huyo.

Zitto amefungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kujadili suala la uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Aidha anaomba Mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uangozi ili akate rufaa.
Maombi ya Zitto, anayewakilishwa na Wakili Albert Msando, diwani wa CHADEMA, kata ya Mabogini, yalianza kusikilizwa saa 6.53 mchana, mbele ya Jaji John Utamwa.
Msando aliiomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Juzi Mahakama iliamuru Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wa Zitto katika Mkutano uliofanyika jana baada ya kutupilia mbali pingamizi la Chadema na kukubali ombi la Zitto.
Akiwasilisha hoja zake Wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika Chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 22, mwaka jana.

Kangoye asisitiza uwezeshaji vijana

Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye, amesema vijana wakiwezeshwa kikamilifu kushiriki shughuli za uzalishaji, umasikini nchini utakuwa historia.
Pia, amewaasa vijana kutumia elimu walizonazo kujiajiri ili kuharakisha maendeleo, badala ya kukaa vijiweni na kubaki kuwa walalamishi huku wakati mwingine wakitumiwa na wanasiasa kama ngazi ya kutimiza malengo yao.

Kangoye ambaye amekuwa mhamasishaji mkubwa wa vijana nchini, amesema Tanzania inaweza kuwa taifa linalotoa misaada kwa nchi zingine na kuachana na utegemezi iwapo vijana wataitambua na kutumika kikamilifu kwa shughuli za maendeleo.
Aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na vijana katika sherehe za kusimikwa Kamanda wa UVCCM wilaya na makamanda wa kata wilayani Kongwa, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisimikwa kuwa Kamanda wa Vijana wawilaya hiyo.
Kangoye ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela ni alama ya harakati za vijana katika maendeleo na ukombozi wa Bara la Afrika na kwamba, walianzisha mageuzi hayo wakiwa vijana.
“Vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kukataa umasikini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mageuzi ya kiuchumi katika taifa letu. Tanzania inaweza kuwa taifa linalotoa misaada badala ya kuwa tegemezi iwapo vijana watajitambua na kuitoa kuleta maendeleo.
“Muda wa kukaa vijiweni na kuilalamikia serikali haupo, tuna fursa na rasilimali nyingi zinazoweza kuleta mageuzi ya kiuchumi na kutufanya kuwa taifa tajiri,” alisema Kangoye.
Alisema harakati zozote ziwe na kisiasa, kiuchumi na kijamii huanzia kwwa vijana na kwamba, ni wakati sasa wa kuamka na kuleta mageuzi kwa maslahi na ustawi wa Tanzania ya sasa na inayokuja.
Naye Ndugai akizungumza baada ya kusimikwa, aliungana na Kangoye kwa kuwataka vijana kujituma katika shughuli za uzalishaji ili kuacha kuwa tegemezi.
Alisema kuna vijana wengi wenye elimu na ujuzi wa kutosha, lakini hawataki kufanya kazi na badala yake wanasubiri serikali iwafanyie kila kitu suala ambalo haliwezekani.
“Tufanye kazi ndugu zangu ili tuachane na umasikini na kuwa tegemezi, fursa zipo za kutosha kinachotakiwa ni kuamua kama alivyosema DC Kangoye ili tulete mageuzi kwenye taifa letu,” alisema.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kongwa, Asia Alamga, alisema kabla ya kuwasimika makamanda hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kutembelea wafungwa, wagonjwa kwenye hospitali za wilaya na kata na kutoa misaada ya kijamii.

TPA: Tumekamata meno ya tembo

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekiri kukamata kontena la meno ya tembo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, imegoma kulizungumzia suala hilo kwa madai kwamba atafutwe Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na Wizara ya Maliasilia na Utalii kwa kuwa ndio wenye mamlaka ya kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Profesa Joseph Msambichaka, alisema hayo  jana wakati waandishi wa habari walipotaka kupata taarifa kamili kuhusu kukamatwa kwa kontena hilo bandarini.
Profesa Msambichaka alisema hawezi kusema kitu chochote kuhusiana na suala hilo na kushauri atafutwe Dk. Mwakyembe na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa ndio wahusika wakuu.
Alisema suala hilo liko katika hatua ya juu ya utendaji wa kiusalama na kwamba watakapowaletea ripoti wataweza kulizungumzia.
“Sijaletewa taarifa kamili kama mwenyekiti lakini taarifa kama Mtanzania ninazo, muda muafaka ukifika mtapewa taarifa,”alisema.
Mwenyekiti huyo aliwataka waandishi wa habari wawe na subiri katika suala hilo kwani linashughulikiwa na vyombo mbalimbali vya dola.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuridhika na majibu ya mwenyekiti huyo ambapo walimuomba waitiwe  Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande,  ili aweze kutoa taarifa kamili na ikiwezekana wapate picha ya kontena hilo.
Mwenyekiti huyo aliendelea na msimamo wake wa kuwataka wasiwe na subira wakati suala hilo linashughulikiwa.
Kontena hilo linadaiwa kukamatwa juzi bandari hapo na maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Matukio ya kuuawa kwa tembo yamekithiri nchini na hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alisema sense ya ndovu katika Pori la Hifadhi ya Selous imekamilika, lakini taarifa yake inatisha kwani kuna ndovu 13,084 mwaka 1976 walikuwa na tembo 109,419.
Alisema watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1579 na shehena kubwa ya meno ya tembo na nyara nyingine na watuhumiwa walishafikishwa mahakamani.

Kipande apigiwa chapuo TPA

NA NJUMAI NGOTA

BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeshauri Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Madeni Kipande, aendelee na ikiwezekana aongezewe muda.
Kutokana na hali hiyo, bodi imeomba Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kusitisha mchakato wa kumpata mtendaji mkuu mpya ili apate fursa ya kuleta maendeleo makubwa ya uongozi chini yake na asimamie malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa kasi.
Mwenyekiti wa bodi ya TPA, Profesa Joseph Msambichaka, alisema hayo jana wakati akitangaza uteuzi wa viongozi waandamizi wa mamlaka hiyo katika ofisi za TPA  makao makuu, Dar es Salaam.
Profesa Msambichaka alisema wamemshauri Dk. Mwakyembe asitishe mchakato huo kwa kuwashindanisha waombaji kutoka ndani na nje ya nchi, angalau kwa mwaka mmoja.
Alisema Kipande kwa ufanisi na nguvu ile aliyoanza nayo mwaka jana imeiletea tija TPA na kwamba ushauri huo Waziri alipokea na kuwaarifu kuwa ataufanyia kazi.
“Hii ni kwa kuzingatia ongezeko kubwa la ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo TPA imeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa wizi na upotevu wa shehena zikiwemo kontena ndani ya bandari,”alisema.
Profesa Msambichaka alisema wameongeza ufanisi wa kuhudumia makontena na meli zinazotia nanga bandarini, kurejesha imani kwa  wateja wa nje kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi.
Alisema TPA walipata hati safi kwa mwaka 2012/2013 na kuvuka malengo ya BRN kwa kuhudumia shehena zaidi ya tani milioni 13 mwaka jana ikilinganishwa na tani milioni 12.05 mwaka 2012 na tani takriban milioni 10.4 mwaka 2011.
Mwenyekiti huyo alisema bodi imefanya uteuzi katika nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi baada ya hatua zilizochukuliwa na bodi za kuwaachisha kazi viongozi waliopatikana na makosa mbalimbali katika uendeshaji wa bandari.
Mbali na uteuzi, alisema wameanzisha utaratibu mpya katika ngazi ya wakurugenzi ambapo ajira zao zitakuwa za mikataba ya miaka mitano  na si wa kudumu kama ilivyokuwa awali na kwamba ikiwa utendaji wao utakuwa wa ufanisi wataongezewa muda.
Aliwataja walioteuliwa na nafasi zao kwenye mabano ni Mhandisi Alios Matei (Naibu Mkurugenzi Mkuu-Miundombinu), Awadh Massawe (Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam), Peter Gawile (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu) na Mhandisi William Shilla (Mkurugenzi wa Uhandisi).
Wengine ni Mkurugenzi wa Tehama, Phares Magesa; Mkurugenzi wa Utekelezaji, Hebel Mhanga;  Mkuu wa Ulinzi, Lazaro Twange; Meneja wa Gati la Mafuta, Kapteni Andullah Mwingamno, Mameneja Ununuzi na Ugavi, Mashaka Kisanta na Michael Simba.
Profesa Msambichaka alisema wamemuongezea muda wa miezi sita Naibu Mkurugenzi Mkuu, Clemence Kiloyavaha ili kupata muda zaidi na kumtafuta mrithi wa nafasi hiyo mwenye sifa zinazostahili.
Nafasi zingine ambazo mchakato wa kuwatafuta wenye sifa ni za  Mkurugenzi wa Sheria na Meneja Mawasiliano.

Thursday, 2 January 2014

Familia ya Dk. Mgimwa yacharuka

NA WAANDISHI WETU

MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia juzi, mjini Pretoria, Afrika Kusini, unatarajiwa kuwasili nchini kesho.
Kwa mujibu wa taarifa, mwili wa Dk. Mgimwa utarejeshwa nchini saa saba mchana, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. Alifariki dunia katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Serikali kwa upande wake imeunda kamati ya kitaifa ya kuratibu mazishi ya Dk. Mgimwa, inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Wakati hayo yakiendelea, familia ya Dk. Mgimwa imesema haifahamu lolote kuhusu uvumi kuwa kifo chake kimetokana na kulishwa sumu.
Familia hiyo imesema itatoa tamko baada ya kupata taarifa ya serikali na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Lukuvi alisema kamati hiyo na nyingine ndogo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, zimeundwa ili kuratibu mazishi ya Dk. Mgimwa.
Lukuvi alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili kesho, saa saba mchana na ndege ya Shirika la Afrika Kusini na utapelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, kabla ya kupelekwa Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Alisema Jumapili mwili wa Dk. Mgimwa utapelekwa kwenye viwanja vya Karimjee kwa ajili ya ibada na utoaji heshima za mwisho kabla ya kusafirishwa kwa ndege kwenda Iringa kwa maziko.
Lukuvi alisema utoaji heshima za mwisho, utatanguliwa na rambirambi na ndipo umma utafahamishwa ugonjwa uliosababisha kifo cha Dk. Mgimwa.
Kuhusu kamati inayoongozwa na Dk. Christine, alisema inaratibu mazishi mkoani Iringa ambako yatafanyika maziko.
Alisema Jumapili mwili wa Dk. Mgimwa utapokewa katika Uwanja wa Ndege wa Nduli saa 10 jioni na utapelekwa ukumbi wa Siasa na Kilimo, mjini Iringa, ambapo wananchi na viongozi watoa heshima za mwisho.
Lukuvi alisema baadaye utasafirishwa kwenda nyumbani kwao kijiji cha Magunga na maziko yatafanyika Jumatatu, saa sita mchana.
Katika hatua nyingine, familia ya Dk. Mgimwa imewaonya wanaosambaza uvumi kuwa ndugu yao amefariki dunia kutokana na kulishwa sumu.
Familia hiyo imesema itatoa taarifa kuhusu kifo chake baada ya kupokea taarifa ya serikali na madaktari.
Msemaji wa familia hiyo, Charles Nyato, alisema hawajui chochote kuhusu sumu, bali wanatambua alikuwa anaumwa na alikuwa akitibiwa Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amemtumia rambirambi Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kifo cha Dk. Mgimwa.
Dk. Sheni alisema atakumbukwa kutokana na utumishi uliotukuka kwa serikali na wananchi wa Tanzania.
“Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, mpendakazi, mzalendo, mwenye busara na upendo kwa wenzake,” alisema.
Rais Sheni pia amewapa pole wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dk. Mgimwa.
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alisema Dk. Mgimwa alikuwa mtu wa pekee, asiyekuwa na majivuno licha ya kuwa  waziri na kwamba, alizoea kumtania kwa kumuita mbunge wa mtaa wao wa Ruvu, ulioko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alisema Dk. Mgimwa, aliyekuwa akishiriki kazi nyingi mtaani kwao kabla hajawa mbunge wa Kalenga na baadaye waziri, hakubadilika kwani aliendelea kuishi maisha yale yale, ikiwemo kushiriki kazi za kusafisha mitaro mtaani hapo.
“Nyumbani kwake ndiko nilikuwa nikihifadhi vitu vyangu vya ujenzi. Alikuwa mtu wa kawaida, nilipokuwa mbunge na yeye bado, alikuwa ananieleza mambo mengi na hata kunidadisi vitu kuhusu siasa. Sikujua naye alipenda siasa,’’ alisema.
Dk. Mgimwa aliyezaliwa Januari 20, 1950, ameacha mjane Jane na watoto sita. Aliwahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za fedha na baadaye kufundisha katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza.
Mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye ulingo wa siasa na kuibuka na ubunge katika jimbo la Kalenga. Mwaka juzi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kuchukua nafasi ya Mustafa Mkulo, aliyeachwa katika uteuzi wa Rais.

Wafumwa wakizini, mume aua kwa mkuki

NA SHAABAN MDOE, LONGIDO

MKAZI wa Longido mkoani Arusha, James Lohutu, ameuawa kwa kuchomwa kwa mkuki ubavuni baada ya kufumaniwa na mke mtu wakifanya mapenzi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na Uhuru jana, walisema Lohutu (51) alichomwa na mkuki huo nyumbani kwa mwanamke huyo na kwenda kufia eneo la mbali kidogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alitihibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema lililotokea Desemba 31, mwaka jana, saa moja asubuhi, baada ya Lohutu kukutwa na mume wa mwanamke huyo Elisante Ndetaiwa (38).
Kamanda Sabas, alisema baada ya mume huyo kumkuta Lohutu na mkewe, alimchoma kwa mkuki sehemu ya ubavu upande wa kushoto ambapo, alijitahidi kujiokoa kwa kukimbia, lakini aliishiwa nguvu na kuanguka eneo jirani na uwanja wa mpira wa Shule ya Sekondari Longido na kufa.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa eneo hilo na wapita njia na kisha kutoa taarifa kwa Polisi ambao walifanya uchunguzi wa haraka na kubaini tukio hilo na kisha kumkamata mtuhumiwa.
“Kinachoonekana marehemu huyu baada ya kuchomwa na mkuki huo, alijitahidi kujitetea kwa kukimbia, lakini alipofika katika uwanja huo alianguka na kufa, nafikiri ni kutokana na kuvuja damu nyingi,” alisema Kamanda Sabas.
Aidha Kamanda huyo, alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa huyo, alisema alikua na taarifa za muda mrefu kuhusu Lohutu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe, ambapo alianza kufanya uchunguzi wake na ndipo siku hiyo aliwafuma.
“Kwa hiyo ukiangalia kwa umakini mkubwa ni kwamba kabla ya mtuhumiwa huyu kufanya tukio hili, alikua na taarifa za uhusiano wa kimapenzi baina ya mkewe na merehemu, hivyo haya ni mauaji yaliyosababishwa na wivu wa kimapenzi,” alisema Kamanda Sabas.
Kufuatia tukio hilo, Polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi na kisha atafikishwa Mahakamani.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Longido, ukisubiri utaratibu wa maziko unaofanywa na ndugu zake.

Hofu ya bomu yazua taharuki


NA RABIA BAKARI
HALI ya taharuki jana iliwakumba wakazi wa eneo la Shekilango, jijini Dar es Salaam, baada ya kuona kitu aina ya chuma kilichokuwa kimejifukia ardhini na kuonekana sehemu ya juu, wakidhani kuwa ni bomu.
Taharuki hiyo ilizuka majira ya saa 3:00 asubuhi.
Hata hivyo, Polisi baada ya kupata taarifa, walifika katika eneo hilo na kukifukua kitu hicho na kuondoka nacho kwa ajili ya kukifanyia uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uchunguzi wa awali kufanyika, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, alisema wamegundua kwamba, kitu hicho si bomu na wala hakina kemikali yoyote inayoweza kuleta mlipuko.
“Kitu hiki (huku akikionyesha kwa waandishi wa habari), kinafanana na bomu, umbile na muonekano wake, lakini si bomu...ila tutaendelea kuchunguza ili kujua ni mabaki ya kitu gani, hivyo tunawatoa hofu wananchi kwamba wasiwe na wasiwasi,” alisema Kamanda Wambura.
Hata hivyo, alisema wamefarijika kuona mwamko wa wananchi wa kutoa taarifa pindi wanapohisi kitu cha hatari na kuwataka kuendelea kuwa makini.
“Tatizo ambalo bado lipo, ni kutochukua tahadhari, kwani baada ya kuhisi kwamba kuna bomu, wengi walisogelea eneo hilo, hali ambayo kama kweli kungekuwa na kitu cha mlipuko, kungetokea madhara makubwa.
Aliwatahadharisha watu kukaa mbalina eneo la tukio ili kuzuia kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Wambura, alisema, Polisi wamejipanga kuzuia uhalifu kwa kuongeza nguvu mara mbili ya kipindi cha sikukuu, na kuwataka wahalifu wakatafute eneo la kuishi.
“Kama hali ilivyoonekana wakati wa sikukuu, ndio itakuwa hivyo sikukuu zote na siku zote,” alisema.

Mume amuua mkewe baada ya kumfumania


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MKAZI wa Inyala, Huruma Layton, ameuawa kwa kipigo na mumewe, akimtuhumu kumfumania akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.
Huruma (20), alifumaniwa na mumewe Ezekiel Mwakabenga (21), akiwa anafanya mapenzi na mwanaume mwingine kwenye nyumba wanayoishi na mumewe huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10:00 alfajiri.
Alisema hali hiyo ilimfanya Mwakabenga kukosa uvumilivu na kuanza kumshambulia mkewe kwa kumpiga sehemu mbalimbali za  mwili.
“Mwanaume aliyekuwa anafanya mapenzi na Huruma alifanikiwa kukimbia, ndipo Mwakabenga alipoanza kumshambulia mkewe huyo sehemu mbalimbali za mwili wake kwa ngumi, mateke na fimbo, na hivyo kumjeruhi vibaya, hali iliyofanya awahishwe hospitalini,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema Huruma alifikishwa Hospitali ya Rufani Mbeya na alifariki dunia saa 5:00 asubuhi, alipokuwa akiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Msangi, Mwakabenga ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Inyala, tayari ametiwa mbaroni na uchunguzi zaidi kuhusiana na mauaji hayo unaendelea kufanywa na polisi.
Utakapokamiliki, mtuhumiwa atafikishwa Mahakani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabiri.
Katika tukio lingine; fundi ujenzi na mkazi wa Nsalaga jijini Mbeya, ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni.
Kamanda Msangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:00 usiku, maeneo ya Itezi mashariki, Tarafa ya Iyunga, mjini Mbeya.
Msangi alimtaja marehemu kuwa ni Christopher Mnyamba (20), ambaye alichomwa kisu na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Ndele.
“Marehemu Mnyamba alikuwa na mwenzake aliyekuwa amempakia kwenye baiskeli na walipofika eneo la tukio, walikutana na vijana wawili waliokuwa wamekaa barabarani, waliwaomba njia ili wapiti, lakini kukatokea kutoelewana baina yao, hali iliyosababisha kuibuka kwa ugomvi baina yao,” alisema Msangi.
Alisema katika ugomvi huo, Ndele alitoa kisu na kumchoma Mnyamba shingoni kisha kukimbia.
Marehemu alikufa alipokuwa akipatiwa  matibabu katika Hospitali ya Rufani Mbeya.
Kamanda Msangi, alisema upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea pamoja na kumsaka mtuhumiwa ambaye mpaka sasa haijajulikana amekimbilia wapi.

Polisi mgodi wa Resolute kuchunguzwa


Na Chibura Makorongo, Nzega
POLISI mkoani Tabora, wamesema watafanya uchunguzi kuwabaini askari wake wanaolinda eneo la mgodi wa Resolute, ambao wanadaiwa kuchukua rushwa kisha kuwaruhusu wavamizi kuingia katika eneo linalochimbwa dhahabu.
Wachimbaji wadogo waliotimuliwa eneo la Kijiji cha Mwanshina ambalo linadaiwa kumilikiwa na mgodi huo, walimweleza Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala na viongozi wengine kuwa polisi walikuwa wakiwaomba rushwa.
Malalamiko hayo yalitolewa kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Dk. Kigwangala, ambapo walisema pamoja na kufukuzwa, lakini polisi huchukua rushwa ya mpaka sh. milioni tatu, kisha huwaruhusu watu kuingia ndani ya eneo la mgodi na kuchimba dhahabu usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Peter Ouma, alisema wanajipanga kuanza kuchunguza tuhuma hizo na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
“Nimesikia malalamiko ya wachimbaji kuwa Polisi wetu wanaolinda eneo la mgodi hupokea fedha kutoka kwa baadhi ya matajiri na kuwaruhusu kuchimba dhahabu usiku,’’ alisema.