Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Monday, 15 June 2015

Hispania yaridhishwa
na kazi ya  TASAF

SERIKALI ya Hispania imeridhishwa na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya mbalimbali nchini ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania  (TASAF).
Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya vijiji vya Wilaya ya  Bagamoyo kwa wanufaika wa mpango huo, Balozi wa Hispania nchini, Luis Cuesta Civis,  alisema mpango huo unaonyesha unatekelezwa kikamilifu na kwa mafanikio makubwa.
Alisema lengo la serikali ya Hispania na nchi nyingine wafadhili ni kuona umasikini unapungua kwa kasi nchini Tanzania na ikiwezekana kuutokomeza, ifikapo mwaka 2025.
“Tumeridhishwa na utekelezaji wa mpango, kwani tumepata  fursa ya kuzungumza na walengwa kutoka kaya masikini na kutudhihirishia manufaa yake,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa TASAF,Ladislaus Mwamanga, alisema mpango wa kunusuru kaya masikini na uhawilishaji fedha ni moja ya mipango ya serikali  katika kuhakikisha inapunguza wimbi la umasikini
Mwamanga alisema utekelezaji wa mpango huo umekuwa ukitekelezwa katika njia kuu mbili, ikiwemo mpango wa kunusuru kaya masikin na mpango wa utoaji wa ajira za muda.
Naye Mratibu Mkazi wa Shirika  Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo(UNDP),Alvaro  Rodriguez, aliipongeza jamii katika
maeneo waliyoyatembelea na kueleza kwamba kila penye mafanikio panahitaji mipango ya uhakika .

Alisema jambo kubwa ni kuweka dhamira  ya kweli  katika ushiriki na utekelezaji wa mpango huo, hivyo wanapaswa kuupiga vita umasikini kwa vitendo.

 ‘Fanyeni uamuzi sahihi
 uchaguzi mkuu Oktoba’

WAKATI Taifa likielekea katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Watanzania wametakiwa kufanya uamuzi sahihi, ili kuwapata viongozi watakaowaletea maendeleo.
Pia  wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika katika daftari la kudumu la wapigakura, ili watumie haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.
Wito huo ulitolewa juzi na Askofu wa Jimbo la Shinyanga,  Liberatus Sangu, katika sherehe ya Jubilee ya miaka 55 ya Padri Paul Fagani, wa  Parokia ya Kanisa Katoliki la  Mt. Petro Songambele Nkololo, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, iliyofanyikia kanisani hapo.
Askofu Sangu alisema katika kipindi hiki, Watanzania hawana budi kuchunguza kwa makini na kufanya uamuzi sahihi, ili kuwapata viongozi watakaotumikia taifa kwa uadilifu na weledi.
Mbali na hilo, askofu huyo  aliwataka waumini wa dini hiyo kupiga vita mauji ya vikongwe pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi, huku akibainisha kuwa dini hiyo haikubalini na jambo la binadamu kumtoa roho mwenzake.

Katika Jubilee hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Wilaya ya Bariadi, Padri Paul Fagani, alihitimiza  miaka 55 ya upadri, tangu alipopata daraja hilo nchini Marekani, ambapo mwaka 1960 alikuja Tanzania na kuanzishwa  Parokia ya Buhangija Shinganya kama Paroko Msaidizi na mwaka 2007 alianzisha Parokia hiyo ya Mtakatifu. Petro Songambele Nkololo.

Wanafunzi wakoma
kutumia vibatari
 
 TATIZO lililokuwa likiwakabili wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Tulya, wilayani Iramba, mkoani Singida la kutumia mishumaa na vibatari wakati wa kujisomea usiku, hatimaye limepatiwa ufumbuzi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Asasi ya The Bourke Family Foundation(BFF) ya nchini Marekani, kuipatia shule hiyo msaada wa taa za umeme wa jua katika maktaba ya shule hiyo.
 BFF pia imewapatia taa za umeme wa jua wanafunzi wote wa shule ya sekondari Tulya, zitakazowawezesha kujisomea nyakati za usiku ili wafanye vizuri katika masomo yao.
 Akizungumza  baada ya kupokea msaada huo, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo,John Eliudi John alisema kabla ya kupatiwa msaada huo wa umeme wa jua,  walikuwa wakitumia mishumaa na vibatari, ambavyo viliwasababishia kuumwa na vifua kutokana na moshi waliokuwa wakiuvuta..
“Lakini kwa sasa tumepata sola, najua tutaongeza juhudi katika kusoma na tutasoma kwa muda mrefu zaidi ya pale mwanzoni tulivyokuwa tunafanya, kwa hiyo nawashukuru waliotusaidia kwa hilo,”alisisitiza.
 Mwanafunzi mwingine,  Mwanaidi Athumani, alisema kabla ya kupatiwa umeme wa jua ,walikuwa wakipata madhara mbalimbali wakati walipokuwa wakijisomea.
 Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo madhara hayo ni pamoja na makaratasi ya mitihani waliyokuwa wakijisomea  kuungua na wengine nyumba walizokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Mwenyekiti wa Taasisi PEN TRUST,Mungwe Athuman, alibainisha kwamba taasisi ya kujitolea ya BFF kutoka nchini Marekani, imeamua kutoa msaada wa umeme wa jua kwenye maktaba zote 160, zilizopo mkoani Singida.
 Akizindua mradi huo wa umeme wa jua, Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk. Parseko Kone, alifafanua kwamba asasi hiyo ya BFF iliamua kusaidia taa hizo kwa kila mwanafunzi wa shule zilizopo pembezoni, ili wajisomee kwa urahisi.

Mkuu wa Shule hiyo,Daud Mavyombo, aliwashukuru wafadhili kwa msaada huo na kueleza changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni upungufu wa walimu wa sayansi,kukosekana mabweni ya wasichana, ukosefu wa maabara na vifaa vyake.