Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Friday, 27 March 2015

Pengo amfikisha Gwajima polisi  • Ni kwa tuhuma za kumkashifu, kumtukana
  • Kova amtaka kujisalimisha haraka kituoni

NA MWANDISHI WETU
KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameingia matatani na sasa ametakiwa kujisalimisha polisi kwa ajili ya kuhojiwa. 
Habari za kuaminika zinasema hatua ya Gwajima kutakiwa kujisalimisha polisi inatokana na tuhuma za kutoa matamshi ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Taarifa ya Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa vyombo vya habari jana, ilisema Gwajima anatakiwa kujisalimisha kutokana na tuhuma za kashfa na matusi.
Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wamepokea malalamiko ya kukashfiwa na kutukanwa hadharani kutoka kwa Kardinali Pengo.
Alisema kupitia mitandao ya kijamii, kuna sauti na video zikimwonyesha Gwajima akimkashfu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo, jambo ambalo limeonekana kuwaudhi wengi.
Kamishina Kova alisema baada ya tukio hilo, jitihada mbalimbali zimefanyika katika hali ya kawaida ili kumpata Gwajima bila mafanikio.
“Jitihada zimefanyika lakini hakuna mafanikio. Sasa tunamtaka ajisalimisha haraka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu bila kukosa na wala asisubiri kukamatwa,” alisema.
Alisema ni muhimu kwa Gwajima kuripoti mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.
Kamishna Kova alisema tayari jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi kuhusiana na shauri hilo unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake.

Wanafunzi wamkana Lowassa


NA  WAANDISHI WETU
VIONGOZI wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu mjini  Dodoma, wamekanusha kumchangia fedha na kumwomba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kugombea urais. 
Pia wamewataka wanafunzi wenzao kujitambua na kutumia muda wao kwa mambo ya msingi kwa ustawi wao na taifa, badala ya kujingiiza katika mambo ya siasa za aina hiyo.
Taarifa iliyotumwa na Uongozi wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, ilisema kundi lilijikusanya Machi 22, mwaka huu, nyumbani kwa Lowasa, likijitambulisha kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma na kutoa matamko mbalimbali pamoja na  kuutangazia umma kuwa wanamtaka agombee urais .
Taarifa hiyo ilisema jambo hilo si la kweli na wanalaani vikali kitendo cha watu wachache kwenda kwa Lowassa na  kujifanya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mkoani Dodoma.
“Sisi kama wasomi ambao jamii inatutegemea hatuwezi kuandamana na kujikusanya katika nyumba ya kiongozi yeyote kumwomba agombee urais wakati tunajua fika hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya taasisi yao,” ilisema taarifa hiyo.
Kilichofanyika ni kuudanganya umma na taasisi zake kupitia kivuli cha  vijana wachache kutoka vyuo vya dodoma waliolipwa fedha ili waweze kufanya jambo hilo.
Ilisema taarifa hiyo kuwa Mkoa wa Dodoma una vyuo takribani vinane  na jumla ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo ni zaidi ya 35,000 ambapo Chuo Kikuu cha Dodoma peke yake, kina wanafunzi wasiopungua 22,000, kulinganisha na watu 230 waliojikusanya nyumbani kwa mbunge huyo, wakiwemo wamachinga na wenyeviti wa jumuia ya wazazi. 
Taarifa hiyo iliongeza kwua licha ya wenyeviti hao waliotoka katika mikoa mbalimbali na wamachinga, idadi ya wanafunzi waliokuwepo katika tukio hilo hawazidi 150 ambayo ni sawa na asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.
“Kwa akili ya kawaida, asilimia iliyokuwepo pale ni ndogo hivyo wanashangazwa na dhambi wasiyoifanya ambapo wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma hivi sasa wako katika muhula mpya wa masomo.
“Sisi kama vijana wasomi na tunaotegemewa na jamii zetu tutakusanyika na kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali zinazotukabili na kwa mwanasiasa ambaye uadilifu wake unatiliwa shaka,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza hawakubaliani na wanafunzi wachache kuchafua na kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu hivyo ambao hawajahusika na tukio hilo, si haki na haikubaliki.
Pia ilisema wanatoa wito kwa wanafunzi wote nchini na jamii yote kwa ujumla kuacha kuzungumzia maamuzi ya mtu binafsi na wasikubali kutumika kwa wanasiasa wanaotumia fedha kwa ajili ya kuwalaghai.

NAPE AMPONGEZA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwa kusitisha utaratibu wa kuyapokea makundi yanayokwenda kumshawishi agombee urais, anaripoti THEODOS MGOMBA kutoka Dodoma.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Same.
Kauli hiyo ya Nape inakuja siku moja tu baada ya Lowassa kutangaza kusitisha makundi mbalimbali kwenda na kumshauri kugombea nafasi hiyo.
Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya CCM ambayo yeye ni mmoja wa wanachama wake.
Alisema alichokuwa akikifanya Lowassa ni kuanza kampeni mapema  kabla ya wakati jambo ambalo ni ni uvunjifu wa kanuni, katiba na taratibu za Chama.
Kwa upande wa wapambe, Nape alisema makada wa wanachama wanaotaka  kugombea urais kupitia CCM, ni lazima wafuate taratibu za kichama.
Alisema ni vyema wataka urais hao wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao kwa kuwa wanaweza kuwasababishia kukosa sifa.
Aaliwashauri wanaotaka kugombea nafasi hiyo ya urais  kupitia CCM kutowasiliza wapambe wao kwa kila wanachoambiwa maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha sifa za kugombea urais.
Nape alisisitiza kusisitiza kuwa ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya Chama hicho ili wawe salama kinyume na hapo watajipoteza sifa.
Aidha Nape alisema CCM itatenda haki kwa wanachma wote watakaofuata taratibu katika uchaguzi huo bila kujali ni nani.

Thursday, 26 March 2015

Wasioichagua CCM wanajikomoa


NA THEODOS MGOMBA, VUNJO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wananchi wanaochagua upinzani kuongoza katika maeneo yao  hawaiadhibu CCM, bali wanajiadhibu wenyewe.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo juzi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Vunjo.
Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidhani kuwachagua wapinzani katika maeneo yao ni moja ya njia ya kuiadhibu CCM.
Alisema mawazo hayo ni potofu, kwani vyama wanavyovichagua havina serikali inayoiongoza, wala mawaziri.
“CCM ndiyo yenye serikali, yenye mawaziri na hata wakuu mbalimbali wa idara, ambao ndiyo wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo na si viginevyo.
“Inashangaza kuona mtu anachagua upinzani kwa kudhani eti anaiadhibu CCM, hii si kweli, kwani hata hao wapinzani ndani ya Bunge ni wachache kuliko wa CCM,” alisema Kinana.
Alisema hivi sasa wapinzani wameunda umoja unajulikana kwa jina la UKAWA ili kukusanya nguvu.
Kinana alisema pamoja na kuunda umoja huo, bado wapinzani kila mmoja anataka kuongoza au kutoa mgombea wa nafasi mbalimbali, ikiwemo ya urais.
“Sasa kila mmoja anataka kugombea urais wakati walishakubaliana kuwa watakuwa na mgombea mmoja, hii inaonyesha kuwa watu hawa wana uroho wa madaraka na si kuwatumikia wananchi,” alisema.
“Nataka kuwaambia ndugu zangu kuwa katika uchaguzi mkuu ujao,  CCM itashinda kwa kishindo na huo UKAWA utageuka na kuwa UKIWA, hivyo mnaopigia upinzani mjiandae kuwa wakiwa,” alisema.
Katibu Mkuu aliwaasa wakazi wa jimbo hilo kuacha kuchagua viongozi wao kwa majaribio, kwani kwa kufanya hivyo wanajikosesha maendeleo.

Kinana aipongeza NHC


KATIBU Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana juu ya ufyatulishaji wa matofali.
Kinana alitoa pongezi hizo  baada ya kuanza kutembelea Jimbo la Vunjo, juzi na kukagua kikundi cha vijana wanaojishughulisha na ufyatuaji wa matofali.
Alisema NHC mbali ya kazi nzuri ya kujenga nyumba kila sehemu, pia imekuwa ikitoa mashine za kufyatulia matofali kwa vikundi mbalimbali vya vijana.
Kinana alisema mpango huo wa NHC umekuwa ukiwasaidia  vijana kwani umewapunguzia  tatizo la ajira kwa kujiajiri na kuuza matofali yao.
Alisema kutokana na vijana kujitokeza na kuanzishavikundi vingi vya ufyatuaji wa matofali hayo ni vyema sasa halmashauri nazo zikawasaidia kwa kuwapa mashine za ziada.
Kwa mujibu wa Kinana  pamoja na kuwapa mashine hizo pia ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuwapa zabuni ya kufyatua matofali pale inapotokea halmashauri inahitaji kujenga majengo mbalimbali, ikiwemo shule.
“Sasa vijana hawa wamejitokeza na kunda kikundi chao cha kufyatua matofali, basi na ninyi halmashauri mwangalie uwezekano wa kununua matofali yao pale mnapokuwa mnajenga majengo mbalimbali, kama madarasa na menginyeo, ili kutia  moyo.
“Nampongeza sana  Mkurugenzi wa NHC, Nehemia Mchechu na watumishi wenzake kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba,   kwa kutoa mafunzo kwa vijana hawa pamoja na kuwapa nyenzo mbalimbali,’’ alisema.
Alisema si kosa kwa watu wengine nao kuiga mfano wa shirika hilo katika kuwasaidia vijana na makundi mbalimbali kujiondoa katika tatizo la ajira.
Kinana alisema hata hivyo ni vyema vikundi zaidi vya vijana vikaundwa na kuomba msaada wa kupatiwa mafunzo, ikiwa ni pamoja na vifaa kwa ajili ya kufyatua matofali, ili  wajiajiri.

CCM yaitaka serikali kuacha urasimu


SERIKALI imeshauriwa kupunguza urasimu wa ufanyaji biashara katika maeneo ya mipakani, ili wananchi wengi  watumie fursa hiyo katika kujiongezea kipato.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Himo.
Alisema Tanzania ni nchi pekee ambayo mikoa yake zaidi ya 14 imekuwa ikipakana na nchi za jirani.
Kinana alisema  iwapo wananchi wa mikoa hiyo wakitumia fursa hiyo ya kupakana na nchi jirani kufanya biashara, kutawasaidia katika kuwaoongezea kipato.
“Ni lazima serikali ikaona namna njema ya kupunguza urasimu kwa wananchi kufanya biashara ya mipakani, ili waweze kuingia  katika nchi hizo jirani na kuuza bidhaa zao na kurudi,” alisema.
Alisema inashangaza kuona kuwa kunakuwa na urasimu wa wananchi kupeleka bidhaa zao nje ya nchi hizo.
“Mtu akitaka kuuza nje kitu anaambiwa hapana ni lazima kuuza humu humu ndani, sasa Kenya bei ni nzuri, mnamkataza asiende kuuza kwa kuwa hana kibali cha kusafiria kwanini?
«Huu ni urasimu na hata ningekuwa ni mimi, ningeuza bidhaa yangu hata mbinguni kama bei inakuwa nzuri huko kuliko hapa,» alisema Kinana .
Kinana alisema kumekuwa na ushuru ambao pia unachangia wananchi walio mipakani kushindwa kuuza bidhaa zao nje za nchi wanazopakana nazo.
Alisema ni vyema sasa kukawa na urahisi wa Watanzania kuuza bidhaa zao nje ya nchi kwa kuwaandalia utaratibu wezeshi wa kufanya hivyo.
Kinana alisema hivi sasa serikali haifanya biashara, hivyo ni kazi yake kuweka utaratibu  kwa wananchi kufanya biashara.

Wanaojipitisha kusaka uongozi watakiwa kusubiri


NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM,  Dk. Edmund Mndolwa, amesema viongozi wanaojipitisha kwa ajili ya kutaka uongozi ndani ya chama, wanawachanganya wananchi, hivyo wasubiri muda ufike.
Aidha, amewataka baadhi ya viongozi wa CCM, wanaowatumia viongozi wa dini kuwatetea wakati wanapokosolewa, kuacha mara moja tabia hiyo.
Dk. Mndolwa alisema hayo mjini Dar es Salaam, jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema muda wa kupata wagombea ndani ya chama haujafika, hivyo si vyema kwa baadhi ya makada kuanza kujipitisha kwa ajili ya kusaka uongozi na wanaofanya hivyo wanawachanganya wananchi.
Dk. Mndolwa alisema katika siku za hivi karibuni, baadhi ya viongozi wanawatumia viongozi wa dini kuwatetea wanapokosolewa na kwamba tabia hiyo haikubaliki.
Hata hivyo, alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, pamoja na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa kukiimarisha chama.
Alisema ziara zinazofanywa na viongozi hao zimekirudisha chama kwenye hadhi yake na kwamba viongozi wengine wanapaswa waige mfano wa viongozi hao.
“Katibu Mkuu wetu (Kinana), pamoja na Nape wanafanya kazi kubwa ya kukijenga chama, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuiga mfano huo. Ziara zao zimekiimarisha chama na kuleta matumaini mapya,” alisema.
Wakati huo huo Mndola alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa  CCCM,  Rais Jakaya Kikwete, kwa uamuzi wake wa busara wa kufuta ada za shule.

Wednesday, 25 March 2015

Askari wanaswa na sare za JWTZ  • Wakutwa na mamilioni ya noti bandia


Na Chibura Makorongo, Simiyu
ASKARI wa Jeshi la Polisi na Magereza, wametiwa mbaroni kwa kukutwa na noti bandia pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda Charles Mkumbo
Askari hao ni Konstebo Seleman Juma (25) wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu na Edmund Masaga (28), ambaye ni askari Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema askari hao walitiwa mbaroni juzi saa 9:00 alasiri katika mtaa wa Old Maswa wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika katika kibanda cha kutolea fedha kinachomilikiwa na Mwalimu wa Sekondari ya Old Maswa, Kassian Luhende (29), kwa lengo la kuweka fedha.
Alisema baada ya Luhende kupokea fedha sh. sh. 100,000, alizitilia shaka na kubaini si halali na kuomba msaada kwa wafanyabiashara wenzake na kuwakamata watuhumiwa hao.
Hata hivyo, katika mahojiano baada ya kukamatwa, mmoja alitoa kitambulisho cha kazi na kubainika kuwa ni askari na mwingine alidai ni dereva wa bodaboda.
Kamanda Mkumbo alisema katika kuwapekua watuhumiwa hao, PC Juma alinaswa na noti bandia zingine zenye thamani ya sh. milioni 1.9. Pia, alikutwa na sare za JWTZ.

JK achochea upimaji virusiNA SULEIMAN JONGO, DODOMA
SERIKALI imempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuongeza hamasa ya upimaji virusi vya ukimwi na kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, aliyasema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2014.
Alisema uamuzi wa Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma Kikwete, kujitokeza hadhari kupima afya zao mwaka 2007, kuliongeza hamasa na kuchochea upimaji kwa hiyari.
Jenista alisema hatua hiyo iliongeza idadi ya watu wanaojitokeza kupima kwa hiyari kwenye vituo na maeneo mbalimbali yanayotolewa huduma hiyo nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Jenista, kabla ya Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete, kujitokeza hadharani na kupima afya zao, idadi ya waliopima kwa hiyari ilikuwa ni watu milioni 2.2 pekee.
Alisema baada ya Rais Kikwete kutoa hamasa hiyo, idadi ya waliojitokeza kupima kwa hiari hadi Desemba, mwaka 2014, ilikuwa ni watu 25,468,564.

"Tunampongeza Rais kwani hivi sasa suala la kupima kwa hiyari kwa Watanzania ni la kawaida. Si ajabu wala hakuna woga kwa Watanzania kwenda kupima," alisema.

Akizungumzia madhumuni ya muswada huo, alisema unalenga kuongeza mapambano zaidi.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, alisema kumekuwepo changamoto katika utekelezaji wa shughuli za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), unaochangiwa na upungufu uliopo kwenye sheria iliyoanzisha tume hiyo.
Alisema wakati sheria hiyo ilipotungwa, iliandaliwa katika mazingira kama ni jambo la dharura, lakini hadi sasa ni miaka 30 imepita na tatizo liko palepale.
"Kutokana na upungufu mbalimbali, serikali imeona ni vyema kuleta marekebisho haya ili kuiongezea nguvu katika mapambano hayo," alisema.
Katika muswada huo, serikali imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Ukimwi, utakaokuwa na  uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na tatizo hilo.
Akichangia muswada huo, Diana Chilolo (Viti Maalum- CCM), alisema licha ya TACAIDS kufanya kazi kubwa, serikali imekuwa ikichangia asilimia tatu tu ya fedha za mapambano dhidi ya ukimwi.
Alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia kufungua mlango zaidi kuweza kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Naye Maria Hewa (Viti Maalum- CCM), alisema aliunga mkono pendekezo la kuzitaka halmashauri ziwe na mifuko inayoweza kushughulikia masuala ya ukimwi kuanzia kwenye halmashauri.
Aidha, alipendekeza sheria hiyo iwe na kipengele kitakachodhibiti matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya mapambano dhidi ya ukimwi.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya,  Kamishna Msaidizi Godfrey Nzowa, amesema mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya nchini, yanahitaji uadilifu na weledi miongoni mwa viongozi, wanausalama na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na Uhuru kuhusiana na sheria mpya iliyopitishwa na  Bunge, Nzowa alisema kitendo kilichofanywa na wabunge ni cha kupongezwa na ni wajibu wao kutunga sheria mpya, kuzifanyia marekebisho na kuziondoa sheria zinazoonekana hazina tija kwa wakati husika ili kuleta maendeleo endelevu ya taifa kiuchumi.
Alisema adhabu zilizowekwa za sh. bilioni moja au kifungo cha miaka 30 jela kwa watakaokamatwa huku wasafirishaji wakiandamwa na kifungo cha maisha, zinaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa biashara haramu ya dawa za kulevya endapo uadilifu utakuwepo.
Alisema uadilifu kwenye mapambano ya dawa za kulevya ndio msingi wa mafanikio, hata ziwepo sheria kali kiasi cha kutisha, kutokana na uwepo wa fedha nyingi kwenye mtandao wa biashara hiyo, jambo linalosababisha tamaa kwa baadhi ya watendaji wa vyombo vya usalama, viongozi na wananchi kwa ujumla.

“Kwa uzoefu wangu, uadilifu ndio kila kitu kwenye mapambano haya. Sheria kali sawa ziwepo, ila kila mtu kwa nafasi yake azingatie weledi kwenye kila hatua anayoichukua kuwafikisha wahalifu mikononi mwa sheria kwa sababu fedha zinawapa tamaa watu wengi,” alisema Kamishna Nzowa.

Gari la kitalii lanaswa na shehena ya bangiNA LILIAN JOEL, ARUSHA
GARI la Kampuni ya Kitalii ya Wengert Windrose, linashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa likiwa limepakiza shehena ya magunia 11 ya bangi.
Gari hilo namba T 695 ARR aina ya Toyota Land Cruiser, likiendeshwa na Frank Faustine, lilikamatwa eneo la Ranch wilayani Longido.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema gari hilo lilikamatwa saa 5:00 usiku na kwamba, bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda Kenya.
Juzi, wabunge waliibana serikali wakitaka kuwekwa kwa sheria kali ili kudhibiti wimbi la uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.
Wakichangia  Muswada wa Sheria ya Dawa za Kulevya, wabunge walipendekeza kuwepo kwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa hadharani kwa watakaotiwa hatiani.
Hata hivyo, akiwasilisha muswada huo bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema ili kuiongezea ukali sheria hiyo, adhabu kwa watakaokutwa wakitumia au kufadhili dawa za kulevya zimeongezwa na kuwa kali zaidi.
Alisema kifungu cha 12 cha Sheria iliyopo, adhabu ya kujihusisha na kilimo cha mimea ya dawa za kulevya (mfano bangi), inapendekezwa kuwa adhabu yake iwe faini isiyopungua sh. milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka 30 au vyote kwa pamoja.
Jenista alisema kosa la kufadhili biashara ya dawa za kulevya, kwa sasa adhabu yake ni faini ya sh. milioni 10 wakati kwenye sheria inayopendekezwa, adhabu ni faini ya sh. bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30.

“Kwa makosa ya kusafirisha na kufanya biashara ya dawa za kulevya, sheria ya sasa imetoa adhabu ya faini au kifungo cha maisha wakati katika sheria inayopendekezwa, adhabu inayowekwa ni kifungo cha maisha peke yake hivyo, kuondoa uwezekano wa wahalifu kupewa adhabu ya faini ambayo hulipa bila shida yoyote,” alisema.

Alisema sheria inayopendekezwa imeweka adhabu kali zaidi kwa watakaowashawishi au kuwahusisha watoto kujiingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya na inapendekeza adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 kwa kosa hilo, tofauti na sheria ya sasa ambayo ipo katika eneo hilo.
Tayari wabunge wamepitisha muswada huo na kinachosubiriwa ni kutiwa saini na Rais ili kuwa sheria kamili.

CCM imeleta maendeleo Moshi Vijijini- ChamiMBUNGE wa Moshi Vijijini, Cyril Chami, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeleta maendeleo makubwa katika jimbo hilo tangu kiliposhika madaraka.
Chami alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mikocheni,   katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Alisema awali jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na viongozi kutoka vyama vya upinzani kwa muda wa miaka 10.
Chami alisema katika kipindi hicho chote, hakuna maendeleo yaliyopatikana, jambo ambalo linaoonyesha kuwa wapinzani hawana uwezo wa kuleta maendeleo kwa wananchi.
Alisema katika kipindi chake cha uongozi, jimbo hilo limepiga hatua kubwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari na maabara.
Ilielezwa kuwa  shule mbili za sekondari zilijengwakatika  kila kata na kufanya idadi ya shule kuwa 39.
Mbunge huyo alisema hali hiyo inatokana na kutumika vizuri kwa Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo, ambao kwao kipaumbele ni elimu.

"Katibu mkuu, hapa sisi tumeweka kipuambele chetu kuwa ni elimu, hivyo mfuko wa jimbo pamoja na fedha zangu na wafadhili wetu, tumezielekeza huko,” alisema.

Chami alimlalamikia diwani wa CHADEMA kwakuzusha uongo kuwa mbunge huyo hajafana jambo lolote la maendeleo.
Akizungumza katika mkutano huo Kinana aliwataka wakazi wa kata hiyo kuachana na maneno ya wapinzani kwani kazi yao ni maneno.