Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Thursday, 29 January 2015

Mnyukano bungeni  • Serikali yaipa rungu polisi kudhibiti uhalifu
  • usinde apongeza vinara wa vurugu kupigwa
  • Sadifa achafua hali ya hewa, Shekifu ang’aka

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
MVUTANO kuhusiana na sakata la Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa  Ibrahim Lipumba, kukamatwa na kufunguliwa mashitaka, umeendelea kutikisa bungeni.
Jana, wabunge walipata fursa ya kujadili suala hilo, ambapo wengi waliwashutumu wenzao wa upinzani kutokana na kuchochea vurugu na kulipaka matope jeshi la polisi pindi linapochukua hatua.
Wamesema iwapo wanasiasa wataheshimu amri halali za mamlaka, likiwemo jeshi la polisi, matukio ya kutiwa mbaroni na wakati mwingine kupigwa yatakuwa ni ndoto kutokea.
Hata hivyo, serikali imesema Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa wote wanaokiuka sheria bila kujali cheo, dini wala elimu yake.
Akitoa kauli ya serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema ni muhimu kwa Watanzania kufuata sheria na kujaribu kuvuraga amani ni kosa, hivyo hakuna atayefumbiwa macho.
Alisema matukio ya watu kuvunja sheria kwa makusudi yamezidi kuongezeka huku wengi wakiwemo wanasiasa wakifanya hivyo kwa lengo la kutafuta umaarufu wa kisiasa.
Kutokana na hilo, Chikawe alisema serikali itaendelea kuchukua hatua kali ili kuhakikisha raia na mali za wananchi zinaendelea kulindwa.
Akizungumzia tukio la kukamatwa kwa Profesa Lipumba, Chikawe alisema Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilipokea barua kutoka CUF ikiomba kufanya maandamano na mkutano wa hadhara.
Alisema barua hiyo yenye kumbukumbu namba CUF/OK/DSM/PF/0027/2A/F2015/1, iliyoandikwa Januari 21, mwaka huu, ilioomba kufanya maandamano kuanzia Temeke kupitia Sudan, Kichangani na kuishia Mbagala Zakhem, ambako mkutano ungefanyika.
“Profesa Lipumba pamoja na viongozi wenzake akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya, walikutana na Kamishna wa Polisi, Simon Sirro na kujadiliana kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi lilibaini mambo matatu, ambayo ni maandamano hayo yaliyokuwa yafanyike siku hiyo, si halali na yangesababisha chuki miongoni mwa wananchi, kuwepo kwa dalili za vurugu na tishio la ugaidi kwenye baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, alisema siku ya tukio, polisi walipata taarifa za kuwepo kwa mkusanyiko wa wafuasi wa CUF maeneo ya Temeke waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali yakisomeka  ‘Polisi acheni kutumika na CCM’.
Chikawe alisema baada ya polisi kufika eneo la tukio huku Profesa Lipumba akiwepo hapo, walitakiwa kuacha kufanya maandamano, lakini walikaidi amri hiyo.
Alizitaja baadhi ya namba za magari hayo kuwa ni T823 CJM na T237 ARR, ambayo yalionekana yakifanya msafara kuelekea eneo ambalo chama hicho kilipanga kufanya mkutano wa hadhara.
Alisema kuwa baada ya Kaimu Kamanda wa Temeke kupata taarifa hizo, alitoa agizo la kuwataka waache, lakini waliendelea.
Baada ya kutotii amri hiyo, amri ya kumkamata Profesa Lipumba na wafuasi wake ilitolewa na hatimaye kufikishwa mahakamani.
Serikali ilitoa taarifa hiyo baada ya James Mbatia (mbunge wa kuteuliwa), kutoa hoja bungeni ya kutaka tukio hilo lijadiliwe.

Kibajaji afyatuka
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na kuwapongeza kwa kazi hiyo.
Alisema katika kudhibiti maandamano hayo askari wamefanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ikiwa ni pamoja na kumwadabisha na kumtia mbaroni mhamasishaji.
Alisema miaka ya nyuma polisi walikuwa wakiwashikisha adabu na kuwatia mbaroni wafuasi, lakini sasa hivi wamemlenga mhusika mkuu na huo ndio utaratibu.
Aidha, aliwataka wabunge wenzake kuhakikisha wanaishi kwa kuheshimiana kwa kuwa kila mmoja anaweza kufanya vurugu ama kuzomea bungeni pindi wengine wanapozungumza.
Hata hivyo, alisema sababu kubwa ya kushamiri kwa zomea zomea na vurugu zisizo na msingi bungeni chanzo ni kiti cha Spika kwani, hakitoi adhabu kali kwa wanaokiuka kanuni.
“Mheshimiwa Spika kiti chako kinayumba kwa sababu akizungumza mbunge wa CCM, upinzani wanazomea na wewe umekaa kimya tu, kwani sisi hatuna midomo ya kuzomea?
“Mbunge mwenzako akiwa anazungumza wewe unakaa kimya sio kuzomea, mbona humu kuna watu nawajua hawajawahi kuzomea Mbowe , Zitto Cheyo, sasa nyinyi wengine ndo mnajua sana kuzomea au nini? Kwani nyinyi maneno yenu yanatufurahisha?” Aling’aka Lusinde 
kuhusu sakata la kupigwa kwa Profesa Lipumba, Lusinde alisema kuanzia sasa ni vyema polisi wakawapiga wahusika wenyewe na si wafuasia wao.
Alisema kila nchi ina utaratibu, hivyo anayepinga utaratibu huo kwa makusudi anapaswa kuchukuliwa hatua.
“Hata huko kwenye vyama vyao kuna katiba na taratibu zao, ukienda kinyume unafukuzwa kama kina Zitto na Kafulila, huo ni utaratibu na ukipenda kachumbali ujue ina pilipili nayo uipende,” alisema.
Alisema wapo wanachama waliotaka kugombea uenyekiti katika vyama hivyo, lakini matokeo yake walifukuzwa uanachama kama adhabu, hivyo hakuna sababu kwa wanaokiuka sheria kulaumu polisi.

Nkumba: Maslahi ya taifa kwanza
Akichangia taarifa na hoja hiyo, Said Nkumba (Sikonge-CCM), alisema ni vyema wabunge wakawa wamoja katika masuala yenye maslahi kwa taifa.
Alisema ni kweli kuwa CCM ndicho chenye kushika dola, lakini si mambo yote yanayofanyika hapa nchini ni ya CCM.
“Mbunge akiinuka cha kwanza ni kuilaumu CCM, huko ni kukosa ajenda, ni vyema wote tukawa kitu kimoja na kuangalia namna bora ya kutatua tatizo hili,” alisema.
Alisema haiwezekani kila mwanasiasa afanye analotaka, hiyo ni sawa na kambare ndani ya mto kila mmoja anasharubu.
Alisema nchi yeyote inaendeshwa kwa sheria hivyo ni lazima kuwepo kwa utii wa sheria.

Sadifa achafua hali ya hewa
Naye Sadifa Sadifa akichangia hoja hiyo, nusura achafue hali ya hewa na wapinzani wasuse tena kikao baada ya kusema kuwa CUF haina tofauti na Saccos.
Kauli hiyo iliamsha hasira miongoni mwa wabunge wa CUF na kumtaka kuifuta huku wengine wakiwa wamehamaki na kusimama.
Hata hivyo, mbunge huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, alisema hafuti kauli hiyo hadi hapo wabunge wa upinzani watakapofuta kauli kuwa CCM ni mafashisti.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuingilia kati na kumtaka Sadifa kufuta kauli hiyo, ambapo naye aliridhia na kuifuta.
Hata hivyo, alisema hakuna haki isiyokuwa na mipaka, hivyo wanasiasa wasitumie vibaya haki hiyo.
Aliwataka wanasiasa kuacha kutumia hoja hiyo ya kupigwa kwa Mwenyekiti wa CUF kisiasa na kwamba, kiongozi huyo hakupigwa kisawasawa bali aligusgwa guswa tu.
Naye Yahya Kasim Issa (Chwaka-CCM), alisema inashangaza kuona vyama viwili tu nchini ndiyo vinalalamika kila mara juu ya utendaji kazi wa jeshi la polisi pamoja na mambo mengine .
Alisema Tanzania kuna vyama 24 vya siasa , lakini ni Chadema na CUF, ndivyo vinavyolalamika kila kukicha hivyo kuashiria kuna mambo maovu wanafanya.

Dola iheshimiwe-Shekifu
Henry Shekifu (Lushoto- CCM), akichangia hoja hiyo, aliwashukuru wabunge wa CCM kwa utulivu na ukomavu wa kutoonyesha hamaki.
Alisema  nchi  inataka amani, Watanzania wanahangaikia amani na CCM ndiyo imeifikisha nchi ilipo sasa.
“Mimi sitaki kutetea maovu, lakini nitatea yale yaliyo na haki na ambayo yanasimamia ukweli, hakuna nchi isiyo na polisi duniani, hakuna nchi isiyo na jeshi duniani,” alisema.
Alisema mara nyingi vurugu zinatokana na kuvunja kanuni na sheria za nchi,duniani kote matatizo yanatokea kwa sababu ya watu kukiuka sheria na kutotii utawala wa sheria.
Alisema  binafsi alishawahi kuwa mkuu wa mkoa na alisimamia amani.
“Mama Kamili ananifahamu vizuri sana, kwa nia njema tulifanya kazi vizuri na alikuwa mtiifu kwa sababu  ukimuambia usifanye anaacha.
“Hakuna uongozi wowote duniani ambao ukiambiwa usifanye jambo kwa mujibu wa sheria na wewe unaendelea kufanya,  hakuna serikali itakayokuvumilia,” alisema .
Alisema bunge linataka kutumika kama chombo cha kubadilisha serikali kila siku na kusisitiza kuwa hilo  haliwezekani.
Alisema  dhamana ya nchi imepewa CCM, hivyo haiwezekani kuona amani inavunjika au wananchi wanapata matatizo iangalie tu.
“Waziri nakuomba usiogope, tafuta ukweli kama ulivyosema  kuwa tume ya haki za binadamu inafanya kazi na wewe umeagiza kitengo cha malalamiko kipokee,  kifanyie kazi,” alisema.
“Ulivyoahidi kama yapo malalamiko, utaratibu utumike ukweli, ufahamike, wanaohusika wachukuliwe hatua, ndio hekima za utawala. Waziri katika hili, tunamwambia awajibike kwa lipi? Alikuwa Dar es Salaam wakati fujo  zinatokea, awajibike kwa lipi?” Alihoji.
Alisema kwa mtindo huo, bunge litawajibisha wangapi kwani, hakuna serikali ya namna hiyo duniani.
Alisema wabunge wamepewa kazi ya kuwaletea maendeeo wananchi, na sio kuwa chanzo cha vurugu na matukio ya kuvunja amani .
“Hatuwezi kukubaliana kupambana na vurugu bila kusimamia vyombo vinavyostahili,mimi napendekeza juhudi zinazofanywa kujua haki na tume ya haki ya binadamu iliyoamua kuchunguza iendelee na kazi na sisi tupewe taarifa na wananchi wajue,” alisema
Mbunge huyo alisema endapo wabunge wa CCM wasingependa kusimamia haki, wabunge wa upinzani wasingeshinda jambo kwa kuwa ni wachache ndani ya bunge
Alisema CCM ndiyo iliyoshika dola na kama ingetaka kufanya mabaya, ingeweza, lakini ni lazima kuwepo na utawala wa sheria.
Akihitimisha hoja yake, Mbatia alisema kunahitajika mabadiliko ya haraka katika jeshi hilo.
Alisema kitendo kilichofanywa cha kupiga hadi watoto, kinaonyesha kuwa hakuna weledi ndani ya jeshi hilo.

Maadhimisho miaka 38 ya CCM yapamba moto


NA  DUSTAN   NDUNGURU,   SONGEA
MAANDALIZI ya sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameanza kushika kasi mkoani Ruvuma, baada ya kuanza kuwasili kwa viongozi wa Chama kwa ajili ya sherehe hizo, zitakazofanyika Februari Mosi, mwaka huu, katika viwanja vya Majimaji.
Miongoni mwa viongozi walioanza kuwasili ni pamoja na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa,  Abdallah Bulembo na Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoani humo.
Wageni hao wamewasili huku kukiwa na shamrashamra za kila aina, ambapo katika makao makuu ya ofisi za CCM mkoa, vipo vikundi mbalimbali vya ngoma, ambavyo hutumika kuburudisha viongozi wanaowasili ofisini hapo.
Akizungumzia sherehe hizo, Nape alisema CCM ndicho chama pekee chenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania, na kwamba ushahidi upo wazi kwenye utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi baada ya kuitekeleza kwa vitendo.
Alisema kutokana na utekelezaji huo, Watanzania wameendelea kukipenda Chama, hali iliyokiwezesha kuibuka kidedea katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa.
Nape alisema licha ya wapinzani kubeza  mafanikio yaliyofikiwa, bado Watanzania wamekuwa wakikipa ushirikiano Chama  kwa kukichagua, ambapo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, CCM kitaibuka kidedea dhidi ya vyama vya upinzani.
Aidha, aliwataka Watanzania kuwa makini na viongozi wa vyama pinzani pindi wanapotoa kauli za kashfa kwa chama kilichopo madarakani, kwa sababu hawana dhamira ya kweli ya kuwatumikia.
Nape alisema wapinzani wanashindwa kuwasaidia wananchi kutokana na kutokuwa na  sera zinazolenga kuwakomboa, ikilinganishwa na CCM.
Kwa upande wake, Bulembo alisema  wazazi kote nchini wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanawaelekeza vijana wao juu ya umuhimu wa kudumisha amani na utulivu uliodumu tangu nchi ilipopata uhuru.
Alisema jumuia hiyo ni moja kati ya kiungo muhimu katika kufanikisha ushindi wa CCM, hivyo kwa kuwa wazazi ndio wenye jukumu la kuwaelimisha vijana wao, wanapaswa kufanya hivyo ili wasirubuniwe na viongozi wa upinzani.
«Wazazi wenzangu kamwe tusikubali vijana wetu kurubuniwa na viongozi kutoka kambi ya upinzani. Tuwaelekeze juu ya umuhimu wa kuunga mkono jitihada za CCM, ambazo zimewaletea maendeleo, lakini pia wahamasisheni wajiunge na Chama chenye nia ya kweli ya kuwainua vijana,» alisema.

Mtanzania afanyiwa unyama wa kutisha ‘Sauzi’  •  Akatwa sehemu za siri, ajeruhiwa vibaya mgongoni, tumboni na kwenye jicho

NA MWANDISHI WETU
MFANYABIASHARA aliyefahamika kwa jina la Jumanne Tevez, mkazi wa Dar es Salaam, amefanyiwa unyama baada ya kudaiwa kukatwa uume wake na wenzake.
Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zilisema kuwa Tevez, amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini akipatiwa matibabu.

Chanzo chetu hicho ambacho kipo karibu na familia ya mfanyabiashara huyo, kilieleza kuwa taratibu zinafanywa ili mke wake pamoja na kaka yake waweze kusafiri kwa ajili ya kwenda kumchukua.
“Hizo taarifa ni za kweli kabisa na hivi ninavyokuambia mke wake na kaka yake wanatarajia kuondoka kesho ili wakamchukue. Amelazwa katika hospitali moja huko Afrika Kusini na hali yake si mbaya sana.
“Yule jamaa kama unavyojua alikuwa mtu wa dili wa muda mrefu, hivyo inawezekana alitofautina na wenzake ndio maana wakamfanyia kitu mbaya, si unajua hawa jama wa poda (dawa za kulevya), humalizana wenyewe tu,” kilisema chanzo hicho kilipozungumza na Uhuru, jana.
Habari zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimuonyesha mfanyabiashara huyo akiwa amevuliwa nguo zote huku akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni.
Tevez, anadaiwa kufanyiwa unyama huo baada ya kuwadhulumu wafanyabiashara wenzake wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Habari zinadai kuwa, mfanyabiashara huyo alifanyiwa unyama huo, Afrika Kusini baada ya kubainika kuficha dawa hizo.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kuficha mzigo aliopewa kutoka Afrika Kusini kuuleta Tanzania na kwamba baada ya kufika nchini, aliwaeleza wenzake kuwa mzigo huo umepotea.
Maelezo hayo yalionekana kuwaudhi waliompa mzigo huo, ndipo walipomuita Afrika Kusini, ambako baada ya kufika, waliamua kumfanyia unyama huo.
Picha mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinamuonyesha Tevez, akiwa na jeraha mgongoni, tumboni na jicho lake la mkono wa kushoto.
Mfanyabiashara huyo alijipatia umaarufu mkubwa jijini Dar es Salaam,baada ya kufunga ndoa na msanii maarufu wa muziki wa taarab, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ ama jike la Simba.
Katika nyimbo mbalimbali alizokuwa akiimba, Isha anasikika akimtaja mwenza wake huyo wa zamani waliyetengana.
Akizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mmoja wa marafiki wa Tevez, alisema amepata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema baada ya kusoma habari hizo na kuona picha, alimpigia simu rafiki mwingine wa karibu wa mfanyabiashara huyo, ambaye naye alikuwa hajapata taarifa kamili.
“Ninachoweza kukueleza ni kwamba habari hizi nimeziona pamoja na picha kwenye mitandao ya kijamii, nimejaribu kufuatilia kwa rafiki yake mwingine, ambaye yupo karibu naye sana, lakini hakunieleza ipasavyo mkasa huo.
“Hadi sasa kwa kweli tupo njia panda, inawezekana ni kweli, lakini bado hizi taarifa rasmi kutoka kwa familia wanazificha sasa subiri tuone. Cha kusikitisha zaidi baadhi ya watu wanasema amevuta (kufariki dunia), lakini yote hayo hatujathibitishiwa,” alisema.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilisema haijapata taarifa za kuteswa kwa mfanyabiashara huyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema wizara haina taarifa hiyo na kwamba wataendelea kuzifuatilia kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Godfrey Nzoa, hakuweza kupatika kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipo hewani muda wote.

Wanaowanyanyasa wafanyabiashara wadogo kukiona


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA.
SERIKALI imesema itawashughulikia wale wote wanaowanyanyasa wafanyabiashara wadowadogo, akiwemo afisa tarafa wa Kariakoo kwa kisingizio cha kusafisha miji.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Pinda alisema kumekuwa na unyanyasaji huo, ikiwemo unyang’anyaji wa mali katika maeneo mbalimbali kwa kisingizio hicho cha kuweka miji safi.

“Hata mimi nimerushiwa picha moja ikionyesha waswahili hawa wakigawana vitu, hii siyo sahihi.
“Picha hiyo nami nitawatumia watu wa TAMISEMI ili wawachukulie hatua hao waliopo kwenye picha na huyu afisa tarafa tutashughulika naye,” alisema Pinda.
Alisema ni vyema mamlaka za miji kukaa pamoja na wadau hao ili kuangalia njia sahihi ya kuweka miji safi badala ya kuwanyanyasa.
Pinda alisema kwa Ilala, jambo hilo lina sura tofauti na linahitaji utaratibu maalumu.
Alisema hata Ulaya wafanyabiashara hao wapo, lakini wamepewa maeneo maalumu kufanya biashara zao na kwa siku maalumu.
“Wabunge wa Dar-es-salaam tukae pamoja na mamlaka husika tuone tunafanyaje ili kuboresha  suala hilo,» alisema.
Awali katika swali lake, Zungu alisema hakuna mbunge asiyetaka mji kuwa msafi na mpangilio mzuri. Alisema kinachofanyika Kariakoo ni kuwanyang’anya mali zao wafanyabiashara wadogo wadogo na kina mama lishe.
«Mheshimiwa Waziri Mkuu, kinachofanyika Jijini Dar es Salaam ni dhuluma na unyanyasaji mkubwa na hasa huyu afisa tarafa mtoe kabisa,» alisema.
Mbunge huyo alisema katika nchi zingine, sekta isiyo rasmi imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Alitolea mfano nchi ya Kenya kuwa, sekta hiyo inachangia katika pato la taifa zaidi ya sh. Trilioni moja.

Wafuasi 30 wa CUF wapandishwa kizimbani


NA FURAHA OMARY
WAFUASI 30 wa Chama cha CUF, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la kufanya mgomo baada ya kukatazwa kukusanyika na kuandamana.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Emmilius Mchauru na kupelekwa rumande katika gereza la Segerea, kutokana na barua za wadhamini kutakiwa kuhakikiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ni Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano au Kasakwa (29), Shabani Polomo (40), Juma Mattar (54), Mohammed Kirungi (40), Athumani Ngumwai (40), Shaweji Mohamed (39) na Abdul Juma (40).
Wengine ni Hassan Saidi (37), Hemed Joho (46), Mohamed Mbarucu (31), Issa Hassani (53), Allan Ally (53), Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (53), Mohamed Mtutuma (33) na  Salehe Ally (43).
Pia wamo Abdi Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salimu Mwafisi, Saleh Rashid (29), Abdallah Said (45), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athumani Said (39), Dickson Leason (37) na Nurdin Msati (37).
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo aliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya kula njama za kufanya uhalifu, kufanya mkusanyiko usio halali na kufanya mgomo baada ya makatazo halali ya Polisi.
Maugo alidai  Januari 27, mwaka huu, maeneo ya wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote walikuja njama ya kufanya uhalifu.
Shitaka la pili na tatu yanawakabili mshitakiwa wa kwanza hadi wa 28, ambapo wanadaiwa siku hiyo katika ofisi za CUF, karibu na Hospitali ya Temeke, bila halali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano yasiyo halali kwenda viwanja vya Mbagala Zakhem.
Katika shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo maeneo ya mzunguko wa Mtoni Mtongani, Temeke, waligoma bila kujali tangazo halali lililotolewa na Polisi kuhusu kukusanyika na kuandamana isivyo halali.
Washitaka walikana mashitaka, ambapo Wakili Maugo alidai upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana kwa washitakiwa.
Maugo aliomba kabla ya washitakiwa kupatiwa dhamana, waweze kufanyia uhakiki barua za wadhamini kwa lengo la kuhakikisha wanafika mahakamani.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala uliomba washitakiwa kupatiwa masharti nafuu ya dhamana.
Hakimu Mchauru alitoa masharti ya dhamana kwa kuwataka kila mshitakiwa kujidhamini kwa dhamana ya sh. 100,000 na kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.
Hata hivyo, Hakimu Mchauru aliahirisha shauri hilo hadi leo na kuamuru washitakiwa kurudishwa rumande kutokana na muda kuwa umeisha wa kuweza kuzifanyia uhakiki barua hizo.
Washitakiwa hao waliondolewa mahakamani hapo kupelekwa mahabusu katika gereza la Keko na basi kubwa la Magereza huku wakisindikizwa na gari la Polisi.

Utalii utaubeba uchumi-Mkapa  •  Nyalandu asema malengo lazima yatimie

NA WILLIAM SHECHAMBO
RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amesema ana imani na sekta ya utalii nchini kuwa ni suluhisho la kudumu kwenye maendeleo endelevu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuliko sekta nyingine.
Amesema imani hiyo inatokana na idadi kubwa ya sekta binafsi nchini, zinazoweza kushirikiana na serikali katika jitihada za kuijengea uwezo sekta hiyo kwa gharama yoyote huku wakitanguliza kwanza maslahi ya taifa.
Mkapa aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, kwenye mkutano wa sita wa kujadili hali ya uchumi, ulioandaliwa na Benki ya Dunia na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema licha ya kuwa na uelewa hafifu wa masuala ya utalii, ni mtaalamu wa uchumi, ambaye muda wote aliokuwa madarakani kwenye nyadhifa tofauti serikalini, aliamini kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu.
“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa sekta ya utalii kuwa hawaoni matumaini kama inavyoelezwa kinadharia. Ninaiamini serikali, inafanya kazi na sekta binafsi kwa kiasi kikubwa na mimi siku zote ninajua pande hizi zikishirikiana hakuna kinachoharibika,” alisema Mkapa.
Aliongeza kusema kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo mengine ya nchi, hasa nyanda za juu kusini, kwa sababu kwa muda mrefu vivutio vya kaskazini na visiwa vya Zanzibar ndiyo vimepewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia hapa nchini, miaka kumi kuanzia sasa sekta ya utalii itawezeshwa katika maeneo yote, ikiwemo kuboresha miundombinu na itasaidia ongezeko la pato la taifa kwa takribani sh. bilioni 16.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwenye mkutano huo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Phillip Dongier, alisema sekta ya utalii ndiyo pekee inayoweza kuitoa Tanzania mahali ilipo sasa kiuchumi kutokana na uwepo wa vivutio vingi vya kipekee.
Alisema baadhi ya mambo ambayo yanakwamisha sekta ya utalii nchini kuzalisha kama inavyotarajiwa na wengi ni pamoja na ushirikishi mdogo wa jamii kuhusu uhifadhi, mifumo mibovu ya kuendesha shughuli za utalii, ikiwemo kulipia gharama za utalii kwa njia ya mtandao na tozo kubwa la kodi.
Dongier alisema mapungufu hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka na wizara husika na wadau wengine wa utalii, zikiwemo sekta binafsi ambapo serikali kwa kiasi kikubwa inatakiwa kuhakikisha inasimamia suala la kupungua kwa kodi kwenye masuala yanayohusu utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema serikali imeshaanza kufanya jitihada za kuifanya sekta ya utalii kuwa tegemeo kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kufungua utalii nyanda za juu kusini mwa Tanzania, kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Alisema pia kuwa wameendelea na mapambano dhidi ya ujangili kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na kutafuta usuluhishi kati ya Tanzania na Kenya kwenye masuala ya utalii, ambayo siku chache zilizopita kulikuwa na kutokuelewana baina ya pande hizo.
Alisisitiza kuwa kamwe hakutakuwa na vita ya kibiashiara kwenye sekta ya utalii kati ya Kenya na Tanzania, kwani wanafanya mazungumzo ya amani ya kutafuta suluhisho na kamwe Tanzania haipendezwi wala kunufaika na matatizo ya kiusalama yanayoikumba Kenya kwa sasa.
Nyalandu alisema sekta ya utalii nchini licha ya kuandamwa na changamoto kadhaa, imeendelea kufanya vizuri katika kuongeza fedha za kigeni, ambapo mwishoni mwa mwaka uliopita kulipokuwa na hofu ya ugaidi kutoka nchi jirani ya Kenya na maambukizi ya virusi vya ebola, bado idadi ya watalii haikushuka chini ya kiwango.
“Tulikuwa na hofu juu ya hali ya utalii itakavyokuwa nchini kwenye miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliopita kutokana na hali ya usalama ilivyokuwa kwa wenzetu jirani (Kenya) na maambukizi ya ebola barani Afrika, lakini hali ilikuwa nzuri sana kwa sababu wageni bado waliendelea kuingia nchini kwa wingi,” alisema Waziri Nyalandu. 

Mwijage: Siridhishwi na mradi wa usambazaji umeme vijijini


Na Happiness Mtweve,Dodoma
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Charles  Mwijage, amesema haridhishwi na utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini.
Mwijage, ambaye alikaa ofisini kwa siku tatu baada ya kuteuliwa, alisema hayo jana wakati akijibu maswali ya nyongeza ya mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed  Shabiby.
Alisema mpaka sasa utekelezaji wa usambazaji umeme katika mkoa wa Manyara ni asilimia sita, Pwani asilimia 22 na Kagera asilimia 52, kasi ambayo bado ni ndogo.
Mwijage alisema atawasilisha taarifa hizo kwa aliyemteua iwapo REA hawatatambua majukumu yao na kuyatekeleza kwa wakati.
Katika maswali yake, Shabiby alitaka kujua kama waziri yuko tayari kuambatana naye jimboni kwake akiwa na watendaji wa REA na TANESCO ili kuona kazi inavyoendelea.
Mbunge huyo pia alitaka kujua hatua zitakazochukuliwa kwa wataalamu wa wizara, ambao wamekuwa na tabia ya kuwapa mawaziri taarifa za uongo na hivyo kutoa majibu ya uongo endapo watadhibitika.

TWB kufungua vituo vidogo vijijini


BENKI ya Wanawake Tanzania (TWB), itaendelea kufungua vituo vidogo  vya kutunzia fedha katika maeneo ya vijijini ili kuwawezesha wanawake kuondokana na kuacha kutunza fedha kizamani.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana wakati akijibu swali la nyongeza la Roman Selasini (Rombo-Chadema).
Selasini aliitaka serikali kuzungumza na benki ili zifungue vituo vidogo vya kutunzia fedha katika maeneo ya vijijini na hatimaye wanawake waondokane na utaratibu wa kizamani wa kutunza fedha.
Katika swali la msingi, Mariamu Kasembe (Masasi- CCM), alitaka kujua ni watu wangapi wamenufaika na TWB na ni kutoka mkoa gani.
Pia, alihoji ni vikao vingapi vya wanahisa vimefanyika tangu mwaka 2007 ilipoanzishwa benki hiyo.
Naibu Waziri alisema benki hiyo ilianzishwa mwaka 2009, na hadi kufikia  mwaka 2014, ilishatoa mikopo kwa wateja takribani 12,992, (wanawake 11,350 na wanaume 1,642), yenye thamani ya sh. 24,868,782,000.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Iringa na Ruvuma.
Pindi alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2009 na kusajiliwa rasmi Julai, 2013, benki hiyo imeshafanya vikao vitano vya wanahisa kuanzia 2011  hadi 2014.
Alisema kikao cha kwanza cha wanahisa kilifanyika Aprili Mosi, 2011 na kikao cha pili kilifanyika Aprili 14, 2012.
Alivitaja vikao vingine kuwa ni kikao cha tatu kilichofanyika Mei 2013, kikao cha nne kilichofanyika Desemba 13, 2013 na kikao cha tano kilichofanyika Desemba 13, 2014.

Hatuna mpango wa kulifungulia gazeti la Mwanahalisi-Nkamia


SERIKALI imesema haina mpango wa kulifungulia gazeti za Mwanahalisi, ambalo ililifungia kwa muda usiojulikana kutokana na ukiukwaji wa taaluma ya uandishi wa habari.
Aidha, imesema haina mpango wa kupunguza kodi ya uzalishaji wa magazeti kutokana na gharama ndogo ya kodi inayotoza kwenye magazeti hayo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, wakati akijibu swali la nyongeza la Joseph Mbilinyi, (Mbeya Mjini-Chadema), .
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali italifungulia gazeti la Mwanahalisi, ambalo alidai lilifungiwa bila sababu za msingi na lile la The East African ambalo ililifungia hivi karibuni.
Naye mbunge Ibrahimu Sanya (Mji Mkongwe-CUF), alihoji mpango wa serikali wa kupunguza gharama za kodi ya uzalishaji wa magazeti kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuyanunua kwa bei nafuu na kupata taarifa mbalimbali.
Mbunge huyo pia alihoji hatua ya serikali kupunguza gharama ya kodi kwenye betri za redio na kuongeza kiwango kwenye betri hizo, kutokana na umuhimu wake kwa wananchi, ambao wanategemea redio kupata taarifa.
Nkamia, alisema serikali haina mpango wa kukifungia chombo chochote cha habari bila sababu za msingi na haitasita kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa chombo kitakachokiuka misingi hiyo.
Aidha, alioa rai kwa waandishi wa habari kutumia vyema kalamu zao kwa kuandika habari ambazo haziwezi kuhatarisha amani ya nchi na kuzingatia misingi ya taaluma yao.
Hata hivyo, waziri huyo alikiri kwamba bei ya magazeti nchini ni kubwa na hali hiyo inatokana na gharama za uzalishaji, uendeshaji, usambazaji na utumishi.
Alisema serikali inawahimiza wananchi na halmashauri za wilaya na miji, kuanzisha vyombo vya habari vya kijamii, yakiwemo magazeti, redio na televisheni ili kuziba ombwe la kukosa habari na taarifa katika maeneo hayo.

Elimu ya msingi kuendelea kutolewa bure


SERIKALI imesema elimu ya msingi inaendelea kutolewa bure kwenye shule za serikali licha ya kwamba wazazi wanachangia kwa kiasi kidogo.
Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa jana, na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Adam Malima, wakati akijibu swali la Dk, Hamisi Kigwangwala (Nzega-CCM), aliyetaka kujua kwa nini serikali inakusanya kodi kwa wananchi na kisha kuchangiwa huduma za afya, elimu na maji badala ya kutoa huduma hizi bure.
Malima, alisema chanzo kikuu cha mapato ya serikali yoyote ni kodi, ambayo hukusanywa na serikali ili kugharamia matumizi yake, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara na mafao ya watumishi wa sekta ya umma, wakiwemo walimu, watabibu, mapolisi na watumishi kwenye taasisi  za ulinzi na usalama, kujenga miundombinu ya barabara, umeme, maji kuweka mingira bora ya kutoa elimu , afya na kadhalika.
«Ni kweli kuwa wananchi wanachangia malipo kwenye baadhi ya huduma hizi zinazotolewa na serikali kwa bei, ambayo sehemu kubwa ina ruzuku, yaani imefidiwa na mapato ya kodi na vyanzo vingine,» alisema.
Alisema hiyo hufanya huduma kupatikana kwa gharama ndogo, ikilinganishwa na gharama halisi za huduma hizo zinazotolewa na watu binafsi.
Malima alisema ukweli huu ulijitokeza miaka ya nyuma, kipindi hicho huduma hizo zikiwemo afya, elimu na maji zilikuwa zinatolewa bure, ambapo walishuhudia upungufu mkubwa, ikilinganishwa na mahitaji, kama vile upatikanaji wa dawa.
Alisema kwa kutambua hali hiyo na kwa kuzingatia uwezo wao mdogo kimapato, serikali imeanzisha utaratibu wa wananchi kuchangia upatikanaji wa huduma hizo, wakati serikali pia nayo ikiwa ni mmoja wa wanaochangia.
« Hivyo, bei zinazotozwa katika utoaji wa huduma hizo ni mchango wa serikali na wananchi, « alisema.
Aidha, alisema elimu ya sekondari inalipiwa ada kwa gharama ya chini, ikilinganishwa na gharama halisi za kutoa huduma husika.

Wednesday, 14 January 2015

Mfanyabiashara wa samaki auawa kwa risasiNa Ahmed Makongo, Bunda

MFANYABIASHARA wa samaki ameuawa kwa kupigwa risasi na mwingine kujeruhiwa kwa risasi katika matukio mawili tofauti, yaliyotokea wilayani Bunda mkoani Mara.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philpo Kalangi, alithibitisha jana kutokea kwa matukio hayo alipozungumza na Uhuru kwa njia ya simu.

Alisema tukio la kwanza lilitokea juzi saa 3:00 usiku, katika eneo la Nyasura mjini hapa.

Alisema mfanyabiashara huyo, Mkome Marwa (39), akiwa na mke wake, wakati wakirejea nyumbani kwao, alipigwa risasi na mtu au watu wasiofahamika.

Kilangi alisema katika tukio hilo, muuaji hakupora kitu chochote na kwamba ofisi yake imetuma askari katika wilaya ya Bunda  kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kumsaka muuaji.

Kamanda Kalangi alisema Marwa, ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyasura mjini Bunda, alipoteza maisha usiku huo huo wakati akipewa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza.

Akisimulia tukio hilo, Kalangi alisema baada ya kupigwa risasi, mfanyabiashara huyo na mkewee walikimbilia katika nyumba ya jirani kuomba msaada, lakini wenye nyumba walifunga geti.

Katika tukio la pili, Kamanda Kalangi, alisema lilitokea eneo la Bunda Day, ambapo  Ndaro Malemi (25), alijeruhiwa kwa risasi  na mtu asiyefahamika wakati akielekea nyumbani kwake.

Akisimulia mkasa huo akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda, Malemi alisema alimuona mwanaume huyo, aliyekuwa amevaa koti jeusi, ambaye alimvizia njiani na kumwamuru ampatie kila kitu alichokuwa nacho.

Alisema alipoona hivyo, aliamua kukimbia na ndipo alipopigwa  risasi mbili na mtu huyo, ambaye alitokomea kusikojulikana bila kuchukua kitu chochote.


“Aliniweka chini ya ulinzi na kuniambia nitowe kila kitu, mimi niliposikia hivyo na kuona bastola, niliiacha baiskeli yangu, nikatimua mbio, ndipo akanipiga risasi mbili,”alisema.


Akizungumza na Uhuru, daktari wa zamu, Dk. Amosi Manya, alisema  walipokea majeruhi wawili hospitalini hapo, ambapo mmoja alikuwa na hali mbaya na kupelekwa Bugando, lakini alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Dk. Amosi alisema hali ya Maleni inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu hospitalini hapo. Maleni alipigwa risasi kifuani.

Kwa mujibu wa Kamanda Kilengi, hakuna aliyekamatwa na polisi kuhusu matukio hayo na bado wanaendelea na uchunguzi.