Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Thursday, 13 November 2014

Uadilifu katika kodi kuipaisha nchi kiuchumi



NA WILLIAM SHECHAMBO
ENDAPO kila Mtanzania atalipa kodi kwa uadilifu na serikali ikitumia mapato hayo kama inavyostahili, Tanzania inaweza  kuingia kwenye kundi la nchi zenye uchumi wa kati kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja, imeelezwa.
Sababu nyingine, ambayo imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania, ni uzalendo wa kununua bidhaa za nyumbani na kudai risiti.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati wa mahojiano maalum na kituo kimoja cha televisheni nchini.
Alisema Watanzania ndio watakaoitoa Tanzania ilipo sasa kiuchumi na kiupeleka hatua nyingine mbele, ambayo itaiwezesha nchi kujitegemea kwa asilimia zaidi ya 90 kwenye uandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha.
Mwigulu alisema kutokana na ukosefu wa uadilifu miongoni mwa Watanzania, hasa wenye kipato cha juu, nchi imeendelea kutegemea wahisani wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, hali inayosababisha kasi ya uchumi kuwa ndogo.
Alisema tatizo kubwa lililoko kwenye ukuzaji uchumi, ambalo serikali inaendelea na jitihada za kulitatua ni kuongezeka kwa tofauti kati ya wenye nacho na wasio nacho, ambapo wenye nacho ndio kundi linaloongoza kwa kukwepa kodi.

“Changamoto tuliyonayo ni tofauti kubwa iliyopo kati ya tajiri na masikini. Tunaendelea na mapambano ya kulipunguza hili pengo ili kila mwananchi awajibike kwa usawa wa stahili yake na kwa uadilifu wa hali ya juu,” alisema Mwigulu.

Aidha, alisema moja ya mikakati iliyopo ni kusimamia utoaji wa kodi kwa matajiri kwa kuziba mianya yote wanayoitumia kukwepa wajibu wa kulipa kodi na kisha kuyatumia mapato hayo kwa ajili ya kuwahudumia masikini.
Naibu waziri pia alisema kupitia matumizi sahihi ya mashine za EFD, serikali ina uhakika wa kupata zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanayotokana na kodi, ambayo awali yalikuwa yanapotea kwa sababu tofauti.
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia umuhimu wa kudai stakabadhi kwa kila manunuzi wanayoyafanya, na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo, wameshiriki ukusanyaji wa kodi za mapato, ambazo ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kuhusu upotoshaji ulioko juu ya mabadiliko ya noti ya sh. 500 kuwa sarafu, Mwigulu alisema si kweli kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imefanya hivyo kutokana na mfumuko wa bei.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mzunguko mkubwa wa noti ya sh. 500, hali inayosababisha gharama kwa BoT za kuzalisha noti mpya kila mara, kwa idadi sawa ya noti nyingi za sh. 500 zilizoharibika.

DUCE kupunguza uhaba wa walimu


NA EMMANUEL MOHAMED


CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu,(DUCE), kimeanza mkakati wa kupunguza uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi nchini kwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa masomo hayo.
Mkakati huo umeongeza wadahiliwa 1700 wa masomo hayo kwa mwaka huu, katika chuo hicho, huku kukiwa na jumla ya walimu 20,000 wa masomo hayo nchi nzima.
Hayo yalielezwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, jana , wakati akiwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza DUCE.
Profesa Mukandala alisema mkakati huo umeanza vizuri, kwani serikali imeanza kuboresha miundombinu ya Mfumo wa Habari na Mawasiliano, (TEHAMA) kwa lengo la kuongeza maarifa ya ziada kwa masomo hayo kwa wanafunzi.
Alisema juhudi za serikali na  DUCE imefanikiwa kujenga maabara kubwa tatu za sayansi, ili kuongeza uwezo wa mkakati huo wa kupokea  wanafunzi  wengi zaidi wa masomo hayo ya sayansi.

“Tuliomba kuongezewa idadi ya wadahiliwa  wa masomo ya sayansi kwa Taasisi ya Usajili wa Vyuo Vikuu, (TCU), kwa mwaka huu na walituunga mkono katika juhudi za mkakati huo,” alisema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Godliving Mtui, alisema  awali chuo  kilikuwa na uwezo wa kupokea  wanafunzi  wachache wa masomo ya sayansi, hivyo mkakati huo utapunguza uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.
 

Ndugai alalamikia mauaji ya wakulima Kiteto


THEODOS MGOMBA 
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
 NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema amesikitishwa na mauaji ya wakulima yanayoendelea kutokea katika wilaya ya Kiteto,   ambayo inapakana na jimbo lake la Kongwa na kuitaka serikali kuingilia kati.Ndugai alifikia hatua hiyo jana baada ya Mozza Abeid  (Viti Maalumu-CUF) kuomba mwongozo wa Spika. 
Akitumia kanuni ya 68(7), Moza alisema kumekuwa kukitokea mauaji ya kutisha ya wakulima katika wilaya ya Kiteto. 
Moza alisema katika kipindi cha mwaka huu, zaidi ya wakulima 30 wameuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa. 
“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako, huko Kiteto yamekuwa yakitokea mauaji, ambayo yanaendelea siku hadi siku. Watu wenye silaha za jadi wamekuwa wakivamia familia za wakulima na kuwaua bila uwoga huku serikali ikiwa kimya. Nini maana yake?’’ Alihoji mbunge huyo. 
Akiwa amekerwa na jambo hilo, Naibu Spika alisema anasikitishwa na mauaji yanayoendelea katika eneo hilo. 
“ Sisi watu wa Kongwa tumeshamuachia Mungu mambo haya. Watu wanauawa hovyo kama vile siyo Tanzania,” alisema. 
Naibu Spika alisema mauaji hayo yamekuwa yakifanyika kwa kutumia silaha mbalimbali zinazomilikiwa na wauaji, zikiwemo bunduki aina ya SMG. 
“Silaha zimezagaa hovyo huko, ni kama vile hakuna serikali katika eneo hilo huku watu wanaohusika na usalama wa raia wakiwa kimya,’’ alisema. 
Akihitimisha mwongozo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Wizara Maalumu) Mark Mwandosya, alisema haiwezekani mauaji hayo yaachwe yakiendelea. 
Alisema kazi ya serikali ni kulinda maisha ya wananchi wake na mali zao na si kuacha wananchi wake wanauana. 
Alisema hivi karibuni, Bunge litapokea taarifa ya tume teule, ambayo inachunguza matatizo ya migogoro ya ardhi, wafugaji na wakulima. 
Mwandosya alisema katika kujadili taarifa hiyo, suala hilo la Kiteto pia litajadiliwa.

Kesi ya vigogo TPA kusikilizwa Desemba


NA FURAHA OMARY
KESI ya matumizi mabaya ya madaraka, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na Naibu wake, Hamad Koshuma, imepangwa kuanza kusikilizwa Desemba 2, mwaka huu. 
Mgawe na mwenzake, wanadaiwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Contruction, bila ya kutangaza zabuni. 
Washitakiwa hao walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando. 
Mwendesha Mashitaka, Jackson Chidunda alidai shauri linakuja kwa  ajili ya kuanza kusikilizwa. 
Hata hivyo, Hakimu Augustina aliahirisha shauri hilo kwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Arufani Isaya, anayesikiliza shauri hilo hakuwepo. 
Hakimu Augustina aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 2, mwaka huu, kwa kuanza kusikilizwa. 
Washitakiwa hao wanadaiwa  Desemba 5, 2011, katika Mamlaka ya Bandari Tanzania, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa na mamlaka hiyo, kama mkurugenzi mkuu na naibu mkurugenzi mkuu, katika utekelezaji wa majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutia saini mkataba wa biashara kati ya TPA na kampuni hiyo ya China. 
Inadaiwa  mkataba huo ulikuwa ni wa upanuzi wa gati namba 13 na 14 katika bandari hiyo, ambapo walifanya hivyo bila kutangaza zabuni, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma. 
Inadaiwa  kitendo hicho kililenga kuipatia faida kampuni hiyo ya China.