Thursday, 6 September 2012

Nape awashukia CHADEMA


NA PETER KATULANDA, MWANZA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka viongozi wa CHADEMA kuheshimu vyombo vya sheria na kuwajibika kisiasa, hasa kutokana na mfululizo wa matukio ya mauaji na kujeruhi watu katika mikutano ya operesheni za chama hicho.
Pia, imevitaka vyama vya siasa na wanasiasa, kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria, kulinda amani na utulivu uliopo nchini ili tamaa na uchu wa madaraka usiendelee kupoteza maisha ya wananchi.
Wito huo ulitolewa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Nape Nnauye, alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali jijini hapa.
Nape alisema katika operesheni za chama hicho Septemba 2, mwaka huu, mkoani Iringa, zilijitokeza vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwanahabari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa askari watatu wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU).
Alisema Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho cha mwandishi huyo wa habari na kujeruhiwa kwa askari hao.
Nape alisema CCM inachukua nafasi hiyo kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huo na kutoa wito kwa tume zilizoundwa kuchunguza suala hilo, akitaka zichunguze tukio hilo kwa umakini na weledi ili kubaini chanzo cha vurugu hizo na mazingira ya kifo cha Mwangosi.
Hata hivyo, aliomba uchunguzi huo ufanyike kwa muda mfupi ili ukweli uweze kubainika mapema na hatua zinazostahili zichukuliwe bila upendeleo kwa wahusika.

“Unaponyooshea wenzako kidole wawajibike, anza na wewe, matukio haya si mazuri kutokea mara kwa mara kwenye shughuli za chama cha siasa, ni aibu inayohitaji uwajibikaji hata kama ni ya kisiasa,” alisema Nape na kuongeza viongozi wa CHADEMA wana roho ngumu na ujasiri usio wa uwajibikaji.
“Hatutetei upande wowote, tunataka tamaa ya madaraka isipoteze maisha ya watu... CCM imesikitishwa mno na mfululizo wa watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini, hasa zilizofanyika kwa kukaidi amri halali ya vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.
Katibu huyo aliyataja matukio mengine ambayo CHADEMA imesababisha vurugu na mauaji kuwa pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM mkoani Singida na hivi karibuni mkoani Morogoro, ambapo Ally Hassan aliuawa.
“Matukio haya sio mazuri kwa chama cha siasa, kwa nini wanaopoteza maisha ni wengine na siyo wale wanaozianzisha?” alihoji Nape na kuongeza mstaarabu wa siasa angeachana na siasa za kupoteza maisha ya watu, kwani watu hao hawarudi.
Akifafanua, alisema vifo hivyo vimekuwa vikisababishwa na chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi ambayo ni ile ile iliyovipa uhalali vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa Katiba na si uroho na matakwa ya wanasiasa wake.
Alisema CHADEMA ingesubiri siku chache zilizobaki kabla ya mchakato wa sensa kumalizika ndipo kiendelee na mikutano yake, hivyo mauaji hayo yasingetokea, lakini kimekuwa kikikebehi na kukaidi amri za polisi kwa kauli za ‘tupo tayari kwa lolote’, jambo ambalo ni ishara ya kujiandaa kwa fujo hizo.
Katibu huyo alisema kwamba kwa kuwa CCM inatii amri halali za vyombo vya serikali, ndiyo maana iliahirisha mikutano yake ya hadhara iliyokuwa ifanyike katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mkoani Kigoma.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru