Wanafunzi wakoma
kutumia vibatari
TATIZO lililokuwa likiwakabili wanafunzi wa
Shule ya Sekondari ya Kata ya Tulya, wilayani Iramba, mkoani Singida la kutumia
mishumaa na vibatari wakati wa kujisomea usiku, hatimaye limepatiwa ufumbuzi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Asasi ya
The Bourke Family Foundation(BFF) ya nchini Marekani, kuipatia shule hiyo
msaada wa taa za umeme wa jua katika maktaba ya shule hiyo.
BFF pia imewapatia taa za umeme wa jua
wanafunzi wote wa shule ya sekondari Tulya, zitakazowawezesha kujisomea nyakati
za usiku ili wafanye vizuri katika masomo yao.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mwanafunzi wa
kidato cha tatu shuleni hapo,John Eliudi John alisema kabla ya kupatiwa msaada
huo wa umeme wa jua, walikuwa wakitumia
mishumaa na vibatari, ambavyo viliwasababishia kuumwa na vifua kutokana na
moshi waliokuwa wakiuvuta..
“Lakini kwa sasa tumepata sola, najua
tutaongeza juhudi katika kusoma na tutasoma kwa muda mrefu zaidi ya pale
mwanzoni tulivyokuwa tunafanya, kwa hiyo nawashukuru waliotusaidia kwa hilo,”alisisitiza.
Mwanafunzi
mwingine, Mwanaidi Athumani, alisema
kabla ya kupatiwa umeme wa jua ,walikuwa wakipata madhara mbalimbali wakati
walipokuwa wakijisomea.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo madhara hayo ni
pamoja na makaratasi ya mitihani waliyokuwa wakijisomea kuungua na wengine nyumba walizokuwa wakiishi
kuteketea kwa moto.
Mwenyekiti wa Taasisi PEN TRUST,Mungwe
Athuman, alibainisha kwamba taasisi ya kujitolea ya BFF kutoka nchini Marekani,
imeamua kutoa msaada wa umeme wa jua kwenye maktaba zote 160, zilizopo mkoani
Singida.
Akizindua mradi huo wa umeme wa jua, Mkuu wa
Mkoa wa Singida,Dk. Parseko Kone, alifafanua kwamba asasi hiyo ya BFF iliamua
kusaidia taa hizo kwa kila mwanafunzi wa shule zilizopo pembezoni, ili
wajisomee kwa urahisi.
Mkuu wa Shule hiyo,Daud Mavyombo,
aliwashukuru wafadhili kwa msaada huo na kueleza changamoto zingine zinazoikabili
shule hiyo kuwa ni upungufu wa walimu wa sayansi,kukosekana mabweni ya
wasichana, ukosefu wa maabara na vifaa vyake.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru