Saturday 23 November 2013

Yametimia CHADEMA


NA SULEIMAN JONGO, NYASA
HASIRA za wanachama wa CHADEMA kutokana na kuvuliwa uongozi kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, zimeanza kuibuka  baada ya vijana wa chama hichoi wilayani Nyasa, kujiengua.
Wakati hali ikiwa hivyo,  Zitto na viongozi wengine waliovuliwa uongozi, leo wanatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuweka mambo hadharani kuhusiana na CHADEMA.
Vijana hao kwa makundi makubwa, wamejiengua katika chama hicho na kukabidhi kadi zao kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ikiwa hatua ya kupinga iliyochukuliwa na Kamati Kuu ya CHADEMA dhidi ya Zitto.
Mbali na yaliyojitokeza wilayani Nyasa, wanachama wa chama hicho mkoani Kigoma wamepanga kufanya maandamano makubwa kupinga hatua ya chama hicho ya kumvua uongozi Zitto na wenzake.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya CHADEMA, kutangaza kumuondoa mbunge huyo katika nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama hicho ikiwemo za naibu katibu mkuu na naibu kiongozi wa upinzani bungeni.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake katika mkutano uliofanyika jana wilayani hapa, Timoth Ndunguru, alisema hatua ya CHADEMA kumtimua Zitto kwenye uongozi, imedhihirisha wazi vijana hawana nafasi ndani ya chama hicho.
Alisema kutokana na hatua hiyo, kundi la vijana 50 wameamua kundoka CHADEMA, kutokana na kuonyesha wazi kuwa viongozi wake  hawataki hoja vijana na changamoto zake.
“Nilijiunga CHADEMA kutokana na kuvutiwa na siasa za Zitto ambaye kwetu hapa Lituhi tumekuwa tukivutiwa sana na mwanasiasa huyo kijana, lakini kitendo cha chama kutangaza kumvua nyadhifa zake za ndani ni wazi kinachofuata ni kufukuzwa kabisa uanachama.
“Kwa hali hii tunatamka rasmi kujiondoa ndani ya chama hiki na sasa tunajiunga na CCM na tunaomba tupokewe. Tuliamini  katika demokrasia, lakini imekuwa kinyume chake,” alisema Ndunguru.
Alisema kwa sasa CHADEMA imekosa demokrasia ya kweli , hivyo kitendo cha kumfukuza Zitto ni wazi vijana sasa hawana nafasi ndani ya chama hicho.
Alisema wamefuatilia mwenendo wa CHADEMA, lakini sasa wanaona umefika wakati wa kuondoka katika chama hicho na kutangaza kujiunga CCM huku wakimuomba Kinana kuwapokea.
Kwa upande wake,  Kinana alisema vijana wanatakiwa kuwa makini kwa kupima sera za kila chama kabla ya kujiunga nacho.
“Ni wakati muafaka kwa vijana kutambua wana wajibu wa kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi lakini pia kilichotokea CHADEMA ni somo kwenu kujua umefika wakati kujiunga CCM.
“Sisi tukiahidi tunatekeleza na tukishindwa tunawaeleza ila kubwa kwenu vijana mnatakiwa kutambua taifa hili linategemea mchango wenu kuliendeleza na chama ambacho kitafanikisha hilo ni CCM ambacho kinatambua wajibu wake kwa jamii,” alisema Kinana.
Katibu Mkuu wa CCM alitumia nafasi hiyo kuhamasisha vijana wa mkoa huo kujikita zaidi kwenye shughuli za maendeleo huku akiahidi kuwa chama chake kitahakikisha kinawasimamia katika kutimiza malengo yao kwa kulitumikia taifa.
KIGOMA KUZIZIMA
Kutoka Kigoma, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa wanachama wa CHADEMA mkoani humo wamepanga kufanya maandamano makubwa na kurejesha kadi zao kupinga uamuzi wa chama hicho kumvua Zitto uongozi.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana kutoka kwa viongozi wa chama hicho, wanaomuunga Zitto, maandamano hayo tayafanyika leo mchana kuanzia Kibindo hadi Mwandiga. Katika maandamano hayo, pia watachoma vipeperushi na bendera za chama.
Walisema mbali na leo, pia wanatarajia kufanya maandamano kama hayo siku astakapowasili Zitto mjini Kigoma na kwamba watafanya hivyo kumpongeza kama shujaa anayependa haki.
Katika hatua nyingine, Zitto anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari leo kuelezea mambo yaliyojitokeza hadi kuvuliwa kwake uongozi na pia mustakabali wake kisiasa.
CHADEMA MORO LAWAMANI
Naye Mwandishi Wetu kutoka Morogoro, anaripoti kuwa viongozi wa CHADEMA katika serikali ya kitongoji cha Mgudeni kijiji cha Mkangawalo, kata ya Mngeta wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamelalamikiwa kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji wananchi wa eneo hilokuwapakia katika pikipiki na  kuwafunga pingu mikono katika machuma ya pikipiki .
Wananchi hao walisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara  wakati wa ziara ya Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Rojas Romuli, uliofanyika katika kitongoji hicho.
Wananchi hao walisema viongozi hao ambao wengi ni viongozi wa serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na afisa mtendaji aitwaye Rajabu Kipolelo   wamekuwa wakiwafanyia wananchi  vitendo hivyo pale wanaposhindwa kulipa faini mbalimbali.
Mmoja wa wananchi ambaye aliwahi kufanyiwa unyanyasaji huo, Maduka Mwela,, alisema alitakiwa kulipia sh. 300,000 kama malipo ya kodi ya ardhi na kwamba alitoa sh. 180,000 za awali lakini cha kushangaza siku iliyofuata alikuta amewekewa alama ya msalaba mwekundu katika shamba lake kisha kufuatwa na askari mgambo na kumkamata.
Alisema mgambo hao walimfunga mkono mmoja nyuma ya pikipiki  baada ya kumpakia na kisha kuondoka naye hadi kwa mtendaji wa kijiji.
‘’ Nilipofika mtendaji huyo alinipokea kwa maneno ‘’nyinyi ndio mnakaa vikao  na chama chenu cha CCM halafu mnapinga kulipa ada ya ardhi, tulibishana kwa saa kadhaa,” alisema.
Alisema wananchi wa kijiji, baada ya kuona tukio hilo,, waliandamana hadi katika ofisi ya mtendaji kushinikiza mwenzao ambaye ni balozi wa CCM aachiwe na ndipo alipomwachia.
Kwa upande wake, Richard Mwamwanga, mjumbe katika serikali ya kijiji, alisema viongozi hao wamekuwa wakijipangia bei za ada kinyume cha utaratibu, kwa lengo la kuwakomoa wananchi.
Alisema awali wakati serikali ya kijiji hicho ilipokuwa ikiongozwa na CCM, walikuwa wakilipia ardhi sh. 20,000 ambapo walipoingia walipandisha hadi kufikia sh. 40,000 kwa ekari.
Hata hivyo mjumbe huyo alisema mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, ambaye anatokana na CHADEMA, Stelatoni Njaani, amekuwa akiongoza kwa njia ya udikteta kutokana na uamuzi anaotoa hataki mtu mwingine ahoji.
Naye Deus Makaranga, katibu wa baraza la wazee kijijini hapo alisema kuwa viongozi hao kwa kushirikiana na mtendaji huyo wamekuwa wakitoa risiti feki katika kulipia mashamba pamoja na michango mbalimbali ya maendeleo.
Alisema wamekuwa wakitumia risiti moja kuandika mchango zaidi ya mmoja sambamba na kutoa risiti  kwa watu tofauti zenye namba zinazofanana.
Kwa upande wake, Gidius Alois Mwagombeka, alisema yeye alikuwa mweyekiti wa kitongoji cha Mkangawalo na kwamba viongozi wa CHADEMA walimfanyia hila kwa kumtuhumu kufanya ubadhilifu wa fedha za maendeleo katika kitongoji hicho hali iliofanya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti,  kumwondoa madarakani.
Alisema kuwa hiyo ilikuwa mwaka jana na kwamba tume iliundwa katika kitongoji hicho dhidi ya tuhuma hizo na kubaini kuwa si za kweli.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru