Thursday 29 January 2015

Hatuna mpango wa kulifungulia gazeti la Mwanahalisi-Nkamia


SERIKALI imesema haina mpango wa kulifungulia gazeti za Mwanahalisi, ambalo ililifungia kwa muda usiojulikana kutokana na ukiukwaji wa taaluma ya uandishi wa habari.
Aidha, imesema haina mpango wa kupunguza kodi ya uzalishaji wa magazeti kutokana na gharama ndogo ya kodi inayotoza kwenye magazeti hayo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, wakati akijibu swali la nyongeza la Joseph Mbilinyi, (Mbeya Mjini-Chadema), .
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali italifungulia gazeti la Mwanahalisi, ambalo alidai lilifungiwa bila sababu za msingi na lile la The East African ambalo ililifungia hivi karibuni.
Naye mbunge Ibrahimu Sanya (Mji Mkongwe-CUF), alihoji mpango wa serikali wa kupunguza gharama za kodi ya uzalishaji wa magazeti kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuyanunua kwa bei nafuu na kupata taarifa mbalimbali.
Mbunge huyo pia alihoji hatua ya serikali kupunguza gharama ya kodi kwenye betri za redio na kuongeza kiwango kwenye betri hizo, kutokana na umuhimu wake kwa wananchi, ambao wanategemea redio kupata taarifa.
Nkamia, alisema serikali haina mpango wa kukifungia chombo chochote cha habari bila sababu za msingi na haitasita kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa chombo kitakachokiuka misingi hiyo.
Aidha, alioa rai kwa waandishi wa habari kutumia vyema kalamu zao kwa kuandika habari ambazo haziwezi kuhatarisha amani ya nchi na kuzingatia misingi ya taaluma yao.
Hata hivyo, waziri huyo alikiri kwamba bei ya magazeti nchini ni kubwa na hali hiyo inatokana na gharama za uzalishaji, uendeshaji, usambazaji na utumishi.
Alisema serikali inawahimiza wananchi na halmashauri za wilaya na miji, kuanzisha vyombo vya habari vya kijamii, yakiwemo magazeti, redio na televisheni ili kuziba ombwe la kukosa habari na taarifa katika maeneo hayo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru