Tuesday 23 December 2014

Hizi ni salamu kwa watendaji wazembe



NA KHADIJA MUSSA
RAIS Jakaya Kikwete, amesema watendaji watakaozembea katika kutelekeza majukumu yao watashughulikiwa kikamilifu.
Amesema watendaji wanapaswa kufahamu kuwa serikali ipo na hukasirishwa pindi mambo yanapokwenda kinyume na matarajio.
Pia amesema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Tawala na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia, wa kutengua nafasi za wakurugenzi sita, kusimamia wengine na kutoa onyo kali.
Akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, jana, Rais Kikwete alisema, uamuzi wa kuwatimua kazi wakurugenzi hao ulistahili na umefanyika kwa wakati mwafaka.
Alisema hatua hiyo itakuwa fundisho kwa watandaji wengine waliopewa dhamana ya kusimamia masuala mbalimbali ikiwemo uchaguzi.

“Uamuzi huu ni sahihi kabisa na nimeubariki…haiwezekani watu wanaharibu kazi na serikali ikae kimya. Hawa tumewapa jukumu la kusimamia uchaguzi na mwakani ndio watasimamia uchaguzi mkuu, sasa tukiacha mambo yaende hivi tutaharibikiwa,” alisema.

Alisema watendaji hao wanapaswa kutambua kuwa serikali ipo na wenyewe wapo na kwamba, wanajua kukasirika na kuwajibisha wazembe.
Wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa na watapangiwa kazi zingine kulingana na taaluma zao wakati uchunguzi zaidi ukiendelea ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mkuranga, Benjamin Majoya.
Wengine ni Abdalla Ngodu (Kaliua), Masalu Mayaya (Kasulu), Goody Pamba (Serengeti), Julius Madiga (Sengerema) na Simon Mayeye (Bunda).
Waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni wakurugenzi watendaji watano ambao ni Felix Mabula (Hanang’), Fortunatus Fwema (Mbulu), Isabella Chilumba (Ulanga), Pendo Malabeja (Kwimba) na Wiliam Shimwela (Sumbawanga Manispaa).
Alisema Wakurugenzi wengine watatu wanapewa onyo kali na watakuwa chini ya uangalizi ili kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi ni Mohamed Maje (Rombo), Hamis Yuna (Busega) na Jovin Jungu (Muheza.
Hawa alisema wakurugenzi wengine watatu walipewa onyo na kutakiwa kuongeza umakini wanapotekeleza majuku yao ni pamoja na Isaya Mngulumu (Ilala), Melchizedeck Humbe (Hai) na Wallace Karia (Mvomero).
Hata hivyo, alisema licha ya kuwepo kwa dosari ndogo ndogo uchaguzi wa serikali za mitaa umekwenda vizuri.
Halmashauri 21 kati ya 165 ndio uchaguzi wake ulikumbwa na dosari kwenye baadhi ya maeneo yake ikiwemo kuzuka kwa vurugu.
Tayari Rais Kikwete alisema ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha inakamata na kuwachukulia hatua wote waliohusika na vurugu hizo.
Alisema bila polisi kuchukua hatua kali, tabia na vitendo hivyo vinaweza kugeuka na kuwa mambo ya kawaida kwenye uchaguzi.

Dar yampa Krismas JK
Mkuu wa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadik, amesema kukamilika kwa ujenzi wa maabara kwenye sekondari zake, ni zawadi ya mwaka mpya kwa Rais Jakaya Kikwete.

“Ujenzi wa maabara umekamilika kwa shule zote 281 za serikali hapa Dar es Salaam, ambazo zilitakiwa kujengwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo lako (JK),” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa kutoa agizo hilo kwani, walikuwa wamelala lakini waliamka na kufanya kazi usiku na mchana.
Alisema zawadi nyingine kwa Rais Kikwete ni ushindi wa CCM kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kwa mkoa wa Dar es Salaam, CCM kimepata ushindi wa asilimia 75 na wapinzani kugawana zilizosalia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru