Thursday 18 December 2014

Matokeo yamtikisa Mbowe



  • Mrema, Mbatia wapotezana
  • Escrow sasa yamliza Kafulila
  • Nape: Hizo ni salamu kwa wapinzani  

HALI si shwari kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuzoea viti vingi kwenye maeneo ambayo ni ngome za vigogo wa umoja huo.
Mkoa wa Kilimanjaro, ambako wanatoka Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, James Mbatia, wameangukia pua na kuondoka kimya kimya kurejea Dar es Salaam, baada ya matokeo kutangazwa.
Mbatia, ambaye anawania jimbo la Vunjo akijipanga kupambana na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, aliweka kambi kuhakikisha chama chake kinapata viti kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kujiwekea mazingira mazuri ya kutoa ushindani.
Hata hivyo, vigogo hao waliambulia patupu baada ya wagombea wa CCM kuzoa viti lukuki. Mkoa wa Kilimanjaro una vijiji 515, Vitongoji 2,247 na Mitaa 60.
Kwa upande wa vijiji, CCM imeshinda 336, Chadema 124, NCCR-Mageuzi 27 huku TLP kikiambulia viti nne na CUF sifuri.
Kwa vitongoji, CCM imeibuka na viti 1,365, CHADEMA 460, NCCR-Mageuzi 132, TLP 17 huku CUF wakiambulia kiti kimoja.
Nafasi ya uenyekiti wa mitaa CCM imeshinda mitaa 28 na CHADEMA mitaa 27.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai, alifika kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kufahamu matokeo, ambapo baadaye aliondoka kwenye mazingira yaliyowashangaza wengi.
Katika Jimbo hilo, CCM kilishinda vijiji 34 huku CHADEMA kikipata viti 25, ambapo kwa Vitongoji CCM kilipata viti 104, CHADEMA 44 na CUF wakiambulia kimoja.
Katika Jimbo la Vunjo, ambapo Mrema na Mbatia wameanza kuparurana, CCM ilipata vijiji 76, CHADEMA 45, NCCR-Mageuzi 27 na TLP kikiambulia vijiji vinane.
Jimbo la Moshi Mjini, linaloongozwa na Philemon Ndesamburo, CCM ilizoa mitaa 28 na CHADEMA 27.
Upande wa Vitongoji CCM ilizoa viti 343, CHADEMA 201, NCCR-Mageuzi 132 na TLP 17.
Jimbo la Mwanga, ambalo linaongozwana Profesa Jumanne Maghembe, CCM iliwabwaga wapinzani kwa kupata vijiji 66, CHADEMA 27 huku katika vitongoji CCM ilipata viti 263 na CHADEMA 19.
Jimbo la Same, CCM iliibuka kinara kwa kupata vijiji 78, ikifuatiwa na Chadema 17 na katika uchaguzi wa vitongoji, CCM iliongoza kwa kupata 405 na Chadema 87.
Katika Jimbo la Siha, CCM iliibuka mshindi kwa kujikusanyia vijiji 52, CHADEMA vinane na kwa upande wa vitongoji CCM ilipata 149 na CHADEMA 21.
Jimbo la Rombo, linaloongozwa na Jopseph Selasini wa CHADEMA, CCM iliibuka kidedea kwa kushinda vijiji 30, CHADEMA 22 huku kwa Vitongoji CCM ikizoa 101 na CHADEMA 80.
Katibu CCM alonga
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Deogratius Ruta, alisema matokeo hayo ni salamu kwa wapinzani mwaka 2015 na kwamba ndoa ya mkeka waliyofunga itazidi kuwamaliza.
Alisisitiza kuwa CCM inaendelea kujipanga katika kuwahudumia Watanzania na kuhakikisha majimbo yote yaliyokwenda upinzani yanarudi.
Escrow yashindwa kumbeba Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini-NCCR Mageuzi, David Kafulila, ameangukia pua baada ya chama chake kuangushwa vibaya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kafulila, ambaye alijigamba chama chake kufanya vizuri wilayani Uvinza, alishindwa kufurukuta licha ya kupata umaarufu kidogo baada ya kushirikiana na wabunge wengine kuibuka kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika uchaguzi huo, Tarafa ya Nguruka ambayo ndiyo ngome ya Kafulila  yenye vijiji 19, NCCR-MAGEUZI imeambulia kiti kimoja huku CCM ikibeba 16 na vingine vitarudia uchaguzi. 
Mbali na kuanguka katika tarafa ya Nguruka, Kafulila pia aliangukia pua kwenye Kata ya Uvinza, mahali ambako amezaliwa kwa kushinda viti vitano huku CCM ikizoa 12.
Nape asema ni salamu 2015 
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ni salamu kwa wapinzani kwa uchaguzi mkuu ujao wa mwakani kwamba wataendelea kusota.
Kimesema ushindi wa CCM wa asilimia 84 katika uchaguzi huo uliofanyika  Jumapili, wapinzani licha ya kupambana kwa miaka 22, wameambulia asilimia 15.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.
 Alisema CCM imeshinda kwa kiwango hicho bila kufanya kampeni licha ya vyama upinzani kufanya kampeni za nguvu zilizoambatana na hila, njama, faulo na fujo. 
“Kwa miaka 22 wamepambana kujaribu kuaminiwa na wananchi lakini bado ni dhaifu na hawana uwezo wa kushika dola. Wataendelea kuwepo kwa ajili ya kuleta changamoto kwa serikali ya CCM.
“Ukuaji wa mtoto huyu upinzani ni sawa na mtoto mdogo asiye na virutubisho. Bado kasi ya wananchi kuwaamini ni ndogo na sisi  CCM tunapenda wakue zaidi ili kuleta chachu ya mabadiliko,” alisema.
Alisema kwa matokeo hayo ni wazi wapinzani wanapumulia mashine kutokana kwa kuwa ngome zao zikiwemo za wabunge machachari, zimechukuliwa na CCM.
Nape aliwataka wapinzani waliopewa dhamana watumikie wananchi kwa kuwa waliowachagua wametumia demokrasia wakiwa na nia thabiti ya kujenga mfumo wa ushindani.
Alisema katika nafasi za mitaa ambayo uchaguzi haujafanyika hakuna sehemu ambayo upinzani utachukua, hivyo wana imani hatua hiyo itaendeleo kujenga uwezo wa CCM katika kuwajibika kwa wananchi.
Nape alisema kazi kubwa ya Chama ni kuhakikisha kinatekeleza Ilani na kuleta maendeleo kwa sababu hakuna upinzani wa kutetemesha wala kutisha kwa matukio hayo ya serikali za mitaa.
“Tumebaini udhaifu wa wapinzani hususan CHADEMA hawana safu za kutosha wala ushindani wa kushika dola kwani hata wajumbe waliowasimamisha kugombea, wengi wao hawajui hata ilani za vyama vyao,” alisema.

Kasoro za uchaguzi
Kuhusu kasoro za uchaguzi huo, Nape alisema kumekuwepo na usimamizi wenye upungufu wa makusudi na Chama hakikubaliani nayo na kitachukua hatua.
Aliitaka serikali kuacha kumung’unya maneno kwa kuwa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo hazihitaji tume bali ni kuchukua hatua ikiwemo kuwatimua wakurugenzi na watendaji waliokwamisha uchaguzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru