Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Sunday, 17 May 2015

Uwanja wa ndege wa shambuliwa



KABUL, Afghanistan
WATU watatu wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko katika uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo mjini Kabul.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema mtu mmoja alijitoa mhanga kwa kujilipua ambapo aliwalenga wanajeshi wa kimataifa nje ya lango kuu la uwanja huo.
Lango hilo hutumiwa na vikosi vya kijeshi vya kigeni, ambapo bado haijabainika endapo walinusurika na shambulio hilo.
Msemaji wa polisi alisema, shambulio hilo lilifanyika karibu na ofisi za safari za ndege nchini humo zilizoko nje ya uwanja.
Shambulizi hilo linafanyika ikiwa ni siku tatu baada ya mwanamgambo mmoja kuwaua watu 14 wakiwemo raia tisa wa kigeni mjini humo.

Nkuruzinza aonya





RAIS Pierre Nkuruzinza, ametoa onyo kali kuhusiana na jaribio lingine lolote la kutaka kuchukua madaraka ya nchi hiyo kwa kutumia nguvu.
Alisema jaribio la namna hiyo halipaswi kufanyika tena na serikali itahakikisha inakabiliana na makundi yenye nia ya kuvuruga amani kwa kuwa vitendo hivyo vitasababisha umasikini na vita.
Nkuruzinza alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Marekani kumuonya kutoendelea na nia ya kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Marekani imesema kitendo cha Nkuruzinza kugombea tena urais, kitazorotesha usalama nchini humo na kutishia misaada ya kimataifa.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jeff Rathke, alisema nchi hiyo inawasiwasi kufuatia uwezekano wa kutokea ghasia zaidi baada ya Nkurunziza kurejea Burundi.
Alisema Marekani inamtambua Nkurunzinza kama rais halali wa Burundi licha ya kusisitiza kiongozi huyo kutowania muhula wa tatu.
Baadhi ya maofisa wa kijeshi walioshiriki kuongoza mapinduzi wamekamatwa huku wengine wakitokomea na kusakwa na majeshi watiifu wa serikali.
Kiongozi wa mapinduzi hayo Generali Godefroid Niyombare, anaendelea kusakwa

Wakimbizi wa Burundi wahifadhiwa Lake Tanganyika



KUFUATIWA kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kutoka Burundi, uwanja wa michezo wa Lake Tanganyika, umetumika kwa muda kuhifadhia wakimbizi wakati wakipatiwa msaada wa chanjo na matibabu.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UNHCR, idadi ya watu 100,000 wamekimbia nchini Burundi kufuatia mzozo wa kisiasa unaoendelea.
Idadi kubwa ya wakimbizi hao wamepokelewa nchini Tanzania huku wengine wakikimbilia nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Uganda. Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Karin de Gruijl alisema idadi imeongezeka zaidi siku chache zilizopita huku wengine wakiishi kwenye fukwe za Ziwa Tanganyika.
Alisema kufuati hali hiyo, wengine wamehifadhiwa kwa muda kwenye uwanja wa Lake Tanganyika kwa ajili ya chanjo, ukaguzi na baadae watapelekwa kwenye kambi za wakimbizi.
Alisema malori 17, yaliyobeba vifaa muhimu kama vile vyandarua dawa na mahema yanapelekwa Kigoma.

Wanaume “vicheko” Kenya



WANAUME nchini hapa wamepokea kwa furaha kusainiwa kwa sheria itakayokabiliana na vitendo vya unyanyasaji hususan majumbani.
Sheria hiyo iliyosainiwa na wiki iliyopita na rais Uhuru Kenyata, inatarajiwa kuwapa ahuweni wanaume waliokuwa wakipigwa na wake zao na kushindwa kuripoti matukio hayo polisi.
Matukio ya wanaume nchini Kenya kupigwa na wake zao yamezidi kuongezeka na kuhatarisha amani katika familia.
Baadhi ya wanaume walisema wamekuwa wakipigwa na wake zao mara kwa mara na kuwafanya kutokua na amani kwenye ndoa zao.
Walisema kinga hiyo ya kisheria itakuwa ni fundisho kwa wanawake wenye kuendekeza tabia za kuwapiga kwa kudai kuwa wameshindwa kutimiza mahitaji ya ndoa na familia madai ambayo wameyakataa.
Kukithiri kwa matukio hayo kunasababisha kuanzishwa chama cha kutetea haki za wanaume na kutaka kuitishwa kwa mgomo wa wanaume kwenye ndoa mpaka sheria hiyo itakapopitishwa.
Mmoja wa waathirika wa vipigo hivyo ni Simon Kiguta, ambaye alipigwa na kujeruhiwa vibaya na mkewe ambapo tukio hilo liliamsha hasira za wanaume wengi nchini hapa.

HABARI ZA MICHEZO KIMATAIFA


Van Gaal aiponda Chelsea

 LICHA ya Chelsea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu, Kocha Mkuu wa Manchester United Louis van Gaal, amesema Arsenal ina kiwango bora zaidi kuliko Chelsea. 


Van Gaal alisema kikosi cha Arsenal kiliweza kuonyesha kandanda safi huku wachezaji wake wakiwa katika kiwango cha juu tofauti na Chelsea.


Kocha huyo alisema Chelsea imetwaa ubingwa huo kwa bahati na iliweza kuzichanga karata zake katika safu ya ushambuliaji na kumalizia vyema mipira na ndio maana iliweza kuvuna pointi nyingi.


Alisema kwa upande wa Arsenal wao ndio walioongoza kwa kuonyesha kandanda safi na la kuvutia lakini iliteleza kwa kufanya makosa madogo madogo ambayo ndiyo yaliyoigharimu timu hiyo.


"Naweza kusema kuwa Arsenal ndio timu bora msimu na hakuna ubishi katika hilo licha ya Chelsea kutwaa ubingwa, " alisema Van Gaal.


Kocha huyo alisema kuna haja sasa ya kujipanga vyema kwa ajili ya msimu ujao ili kikosi chake na timu nyingine ziweze kufanya vyema katika ligi.


Mourinho amwagia sifa Terry

KOCHA wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya England  Jose Mourinho, amesema bila ushawishi wake John Terry asingekuwa katika kikosi hicho.
Mourinho alisema katika kipindi kirefu ameweza kumshawishi Terry kuendelea kuichezea timu hiyo licha ya kutaka kuondoka mara kwa mara.Kocha huyo alisema kila Terry alivyotaka kuondoka alimzuia kwani alikuwa muhimu sana katika kikosi chake na ndio maana alikuwa akimzuia."Nimekuwa nikimzuia Terry kuondoka kwa kuwa mimi kama kocha najua umuhimu wake kwani ameweza kuisaidia sana timu," alisema Mourinho.Alisema mchezaji huyo pamoja na wenzake wameweza kushirikiana vyema na kuiwezesha timu yake kunyakua ubingwa msimu huu.Terry mwenye umri wa miaka 34, ameweza kuichezea Chelsea  mechi za msimu mzima kwa kipindi cha dakika 90.


Kocha Newcastle alia na kiwango




KOCHA Mkuu wa Newcastle John Carver, amesema amesikitishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake katika mchezo wa Ligi Kuu England.Katika mchezo huo, Newcastle ilipokea kipigo cha mabao 2-1, dhidi ya QPR.Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Carver alisema timu ilipoteza mchezo huo baada ya kucheza chini ya kiwango.

Carver alisema timu yake ingeweza kushinda lakini safu ya ulinzi ilimuangusha baada ya kukosa umakini na kuruhusu wapinzani wao kupenya na kupata mabao.

"Timu yangu ilicheza chini ya kiwango hali ambayo imesababisha kupoteza mchezo wetu dhidi ya QPL lakini matokeo hayo hayatatukatisha tamaa," alisema Carver.

Kutokana na matokeo hayo, Newcastle inashika nafasi ya nne kutoka mkiani baada ya kujikusanyia pointi 34 wakati QPR ipo nafasi ya pili mkiani ikiwa na pointi 30.

Rodgers:Hakuna kama Gerrard





KOCHA wa Mkuu wa Liverpool, Brendan Rodgers, amesema hakuna mchezaji anayeweza kuchukua nafasi ya nahodha Steven Gerrard.

Rodgers alisema kuondoka kwa Gerrard katika kikosi hicho ni pengo kubwa kwa kuwa nahodha huyo alikuwa hodari na mtu aliyejituma.

Kocha huyo alisema mchezaji huyo alikuwa ni moja ya wachezaji ambao wameisaidia Liverpool kupata mafanikio makubwa.

"Kuna wachezaji wengi na wazuri England, lakini  Liverpool haiwezi kupata mchezaji mzuri kama Gerrard ambaye hawezi kufananishwa na mchezaji yeyote kutokana na mchango wake," alisema Rodgers.

Nyota huyo aliagwa juzi katika mchezo wake wa mwisho ambapo Liverpool ilikubali kipigo cha mabao 3-1, katika mchezo uliopigwa katika dimba la Anfield.

Mchezaji huyo alijiunga na klabu hiyo miaka 17 iliyopita na msimu ujao atavaa jezi ya LA Galax





Wednesday, 22 April 2015

Watumishi mafisadi kitanzini



  •  Serikali yaibuka na mwongozo mpya
  •  Tume ya Maadili yapewa meno makali

NA WILLIAM SHECHAMBO
SERIKALI imeendelea na mikakati ya kuwadhibiti viongozi wa umma wanaokiuka maadili na kushiriki kwenye vitendo vya wizi na ufisadi, ambapo sasa imeunda mwongozo mpya utakaotumika kuwabana.
Mwongozo huo ambao unatajwa kuwa suluhisho na mwarobaini wa watumishi wezi na wanaokwenda kinyume, pia utaipa meno zaidi ya kiutendaji, Sekretari ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa sasa sheria na kanuni zinazoongoza maadili ya viongozi wa umma, lakini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makusudi ama kusahau, baadhi ya viongozi wamekuwa wakizipuuza,  hivyo kusababisha matatizo ya kimaadili, hususan kuibuka kwa vitendo vya kifisadi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, mwongozo huo uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utaanza kutumika kwenye mwaka wa fedha 2015/2016.
Mwongozo huo utaanza kutumia rasmi kabla ya kufanyika kwa matukio makubwa nchini, ikiwemo kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, ambao vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili vimekuwa vikishamiri.
Akizungumza kwenye warsha ya wadau ya kujadili rasimu ya mwongozo huo, Dar es Salaam, jana, Kapteni Mkuchika, alisema serikali ina nia madhubuti ya kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili.
Alisema kupitia mwongozo huo, jitihada za serikali kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025, zinazosisitiza uongozi bora na utawala wa sheria, zinapewa nguvu kutokana na uwepo wa programu maalumu zinazohamasisha maadili  katika kila idara ndani ya sekta za umma na binafsi.
Mkuchika alisema mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaoota mizizi kote nchini, yanahitaji ushirikiano wa sekta zote, wananchi na asasi za kiraia,  ambapo adui mkubwa kati ya wengi ni rushwa na ufisadi, ambao kwa kiasi kikubwa unatekelezwa na viongozi wa umma.
Alisema maadili ya viongozi wa umma ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kukuza heshima ya taifa, hivyo serikali inafanya kila linalowezekana kutoa uwezo kwa Sekretarieti ya Maadili na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili matatizo hayo kutoweka nchini.,
Waziri huyo alisema nchi ilitikiswa na vitendo vinavyotokana na mmomonyoko wa maadili ya viongozi wa umma katika kipindi kifupi kilichopita, hali iliyoliletea aibu taifa na kuilazimu sekretarieti ya maadili kuwahoji watuhumiwa.
Waziri Mkuchika alisema ni lazima somo la maadili likaingizwa kwenye mitaala ya elimu kuanzia  shule za msingi mpaka elimu ya juu, ili kukomesha tatizo la ukosefu wa maadili kwa jamii, kwasababu utaratibu uliokuwa unatumika awali wa kupeleka vijana wote JKT kuwafundisha maadili kwa nyakati hizi hauwezekani.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema taasisi yake haitaendekeza vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kiongozi yeyote wa umma awapo kazini au atakapostaafu.
Alisema tangu kupatikana Uhuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kujenga na kukuza uadilifu kwa viongozi wa umma na sekta ya umma kwa kutumia sera, sheria, kanuni na miongozo, ukiwemo unaotarajiwa kutumika hivi karibuni.
Jaji Salome alisema kutumika kwa mwongozo huo ni mwendelezo wa juhudi hizo za serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo wakati huu wa kuelekea uchaguzi, viongozi husahau maadili na kufanya mambo kwa akili zao.
Alisema watapambana na kila kiongozi anayepotoka kimaadili kwa kutumia miongozo, kanuni na sheria, ili Tanzania iwe mahali salama kuishi kwa kuzingatia haki na usawa.
Aidha, alisema ili kuipa ‘meno’ sekretarieti ya maadili, serikali itaona namna ya kufanya  kuiruhusu imshitaki mtuhumiwa moja kwa moja mahakamani, wakiwemo wa ufisadi, badala ya kusubiri ruhusa kutoka kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP).
Sambamba na hilo, Mkuchika alisema Sekretari hiyo ambayo awali ilikuwa ni kitengo kidogo cha maadili ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), itapewa hadhi ya kuwa Tume, ili  ijitegemee  kama ilivyo kwa TAKUKURU.
“Taasisi hii ni muhimu sana, awali ilikuwa kitengo tu ndani ya jeshi; tukaona umuhimu wake tukakimegua ,ikawa na hadhi hii, sasa tumeona umuhimu wake zaidi kwa maendeleo ya maadili ya viongozi nchini, hivyo inabidi iwe tume, kama ilivyo TAKUKURU,” alisema Mkuchika. 

Hali ya mazingira inatisha- Dk. Bilal


NA MWANDISHI WETU 
UHARIBIFU wa mazingira nchini umezidi kuongezeka hivyo kutishia kutoweka kwa rasilimali na viumbe hai muhimu na kuchochea ongezeko la umasikini.  
Miongoni mwa athari za uharibifu huo wa mazingira ni kuwepo kwa athari kubwa kwa sekta tegemeo kwa uchumi wa nchi na maisha ya binadamu kama kilimo, uvuvi, utalii na madini.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania ikiwa moja ya nchi zinazoendelea, imekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kwamba hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la umasikini. 
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya uharibifu wa mazingira na umasikini. Kadri hali ya umasikini inavyoongezeka, ndivyo pia uharibifu wa mazingira unavyoongezeka,” alisema.
Dk. Bilal alisema ripoti hiyo inaonyesha kwamba ongezeko la uharibifu wa mazingira nchini linatokana na kuendelea kufyekwa kwa misitu, kuharibiwa kwa vyanzo vya maji, uchomaji moto na kuzagaa kwa taka ngumu. 
Sababu zingine, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni uchafuzi wa maji unaotokana na utiririshaji wa maji machafu ya viwandani na nyumbani na upotevu wa baioanuai.
Mbali na sababu hizo, Dk. Bilal alisema ongezeko la hali hiyo linaashiria kuwepo kwa upungufu katika kubuni, kutekeleza na kusimamia sheria, kanuni, mikakati na programu zilizowekwa kwa ajili ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira. 
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais aliziagiza taasisi za serikali na wadau kuhakikisha mazingira yanalindwa na wakati huo huo hatua kali zinachukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na uharibifu wa mazingira. 
“Mazingira ni mhimili wa sekta za uzalishaji kama vile kilimo, utalii, uvuvi na madini. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha mazingira na maliasili zetu zinatumika katika njia endelevu kwa kuzingatia uwiano mzuri kati ya matumizi ya rasilimali,” alisema.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhandisi Dk. Binilith Mahenge, alisema kila mwaka nchini takriban hekta 400,000 za misitu zimekuwa zikipotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya kuni na mkaa. 
Sambamba na hilo, Dk. Mahenge alisema kati ya mwaka 2000 na 2011 kumekuwa na ongezeko la matukio ya uchomaji moto ambapo yaliyoripotiwa ni 1,123,000. Matukio hayo yameripotiwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Tabora, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro. 
Pia, alisema uharibifu wa mazingira unachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya majitaka katika miji mikubwa. 
Alisema asilimia 50 ya miji mkubwa nchini ina mifumo ya majitaka, ambayo hata hivyo haitoshelezi kwa kuwa inahudumia asilimia nane tu ya wakazi wa maeneo hayo.
Akitoa neno la shukrani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema ripoti hiyo imewazindua wadau wengi, hivyo ni wajibu wa kila sekta kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele. 
Alisema ni wazi kwamba uharibifu wa mazingira na umasikini ni chanda na pete hivyo jitihada za maskusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda mazingira kwa lengo la kuoresha maisha wa binadamu na viumbe hai.
“Suala la usimamizi wa sheria, sera, kanuni, taratibu na programu za hifadhi ya mazingira ni suala ambalo halina mjadala. Hatuna budi kuzisimamia ili kulinda mazingira na wakati huo huo kuchukua hatua hali dhidi ya wanaoharibu mazingira,” alisema. 
Nyalandu alisema ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa mazingira, sheria na sera zilizopo hazina budi kufanyiwa mabadiliko na kutoa adhabu kubwa kwa wale wanaokiuka.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na mawaziri Samuel Sitta (Uchukuzi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi Maalumu), Samia Suluhu Hassan (Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano) na Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele.
Pia walikuwepo makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa wizara na washirika wa maendeleo wakiwemo kutoka mashirika ya maendeleo ya Canada (CIDA) na Denmark (DANIDA).