Sunday 5 January 2014

Muuguzi aishi ‘Leba’, huduma zasimama

Na Jumbe Ismailly, Ikungi

HUDUMA za kujifungua katika Zahanati ya Kata ya Iglansoni wilayani hapa, zimesimama kwa muda, baada ya chumba kilichokuwa kikitumika kufanywa nyumba ya muuguzi mkuu wa zahanati hiyo, Meriani Misai.
Uongozi wa zahanati hiyo iliyopo tarafa ya Ihanja, mkoani Singida, ulifikia uamuzi huo baada ya Meriani kutokuwa na nyumba ya kuishi kwa kipindi kirefu sasa.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iglansoni, Rehema Majii, dari la nyumba ya kuishi muuguzi huyo, lilianguka kutokana na popo kugeuza makazi yao.
Alisema Meriani alikuwa akishindwa kulala hususan kipindi cha mvua, kutokana na nyumba yake kuvuja kila mahali.

 “Kila mvua ilipokuwa ikinyesha ilikuwa ni adha kwa muuguzi wetu, alikuwa akilazimika kukaa kwenye kiti mpaka asubuhi bila kulala kutokana na nyumba yake kuvuja.
Tumelazimika kufanya utaratibu wa kumuhamishia katika moja ya vyumba vya Zahanati hii kutokana na kukosa sehemu ya kuishi,” alisema Rehema.
Alisema baada ya mtumishi huyo kuhamia kwenye chumba hicho, huduma za kujifungua zimesimama katika Zahanati hiyo.
Kwa upande wake Meriani, alisema ameishi katika nyumba hiyo kwa miaka mitatu huku popo wakiwa wamejaa na kusababisha nyumba kutoa harufu mbaya.
Alisema kwa sasa wajawazito wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 50 kufuata huduma hizo katika zahanati ya Kata ya Muhintiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Magayane Protace, alisema alimuagiza Rehema kumtafutia nyumba ya kupanga ambayo halmashauri italipia gharama za pango kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa, wakati nyumba hiyo inafanyiwa ukarabati.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dk. Henry Mbando, alisema kutokana na dharura hiyo iliyojitokeza, wameshafanya tathimini, ambapo zaidi ya sh. milioni sita zinahitajika kuifanyia ukarabati nyumba hiyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru