Thursday 2 January 2014

Wafumwa wakizini, mume aua kwa mkuki

NA SHAABAN MDOE, LONGIDO

MKAZI wa Longido mkoani Arusha, James Lohutu, ameuawa kwa kuchomwa kwa mkuki ubavuni baada ya kufumaniwa na mke mtu wakifanya mapenzi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na Uhuru jana, walisema Lohutu (51) alichomwa na mkuki huo nyumbani kwa mwanamke huyo na kwenda kufia eneo la mbali kidogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alitihibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema lililotokea Desemba 31, mwaka jana, saa moja asubuhi, baada ya Lohutu kukutwa na mume wa mwanamke huyo Elisante Ndetaiwa (38).
Kamanda Sabas, alisema baada ya mume huyo kumkuta Lohutu na mkewe, alimchoma kwa mkuki sehemu ya ubavu upande wa kushoto ambapo, alijitahidi kujiokoa kwa kukimbia, lakini aliishiwa nguvu na kuanguka eneo jirani na uwanja wa mpira wa Shule ya Sekondari Longido na kufa.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa eneo hilo na wapita njia na kisha kutoa taarifa kwa Polisi ambao walifanya uchunguzi wa haraka na kubaini tukio hilo na kisha kumkamata mtuhumiwa.

“Kinachoonekana marehemu huyu baada ya kuchomwa na mkuki huo, alijitahidi kujitetea kwa kukimbia, lakini alipofika katika uwanja huo alianguka na kufa, nafikiri ni kutokana na kuvuja damu nyingi,” alisema Kamanda Sabas.
Aidha Kamanda huyo, alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa huyo, alisema alikua na taarifa za muda mrefu kuhusu Lohutu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe, ambapo alianza kufanya uchunguzi wake na ndipo siku hiyo aliwafuma.
“Kwa hiyo ukiangalia kwa umakini mkubwa ni kwamba kabla ya mtuhumiwa huyu kufanya tukio hili, alikua na taarifa za uhusiano wa kimapenzi baina ya mkewe na merehemu, hivyo haya ni mauaji yaliyosababishwa na wivu wa kimapenzi,” alisema Kamanda Sabas.
Kufuatia tukio hilo, Polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi na kisha atafikishwa Mahakamani.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Longido, ukisubiri utaratibu wa maziko unaofanywa na ndugu zake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru