Saturday 11 January 2014

Mwanza kwafukuta

NA PETER KATULANDA, MWANZA

MTUNZA Fedha na Karani wa malipo wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wamesimamishwa kazi huku wahasibu wawili na mtunza stoo ya vitabu vya mapato, wakitakiwa kupelekwa polisi.
Wakati watuhimishi hao wakikumbwa na ‘dhoruba’ hiyo, Mweka Hazina wa Jiji, Rengise Eringia, amenusurika kutimuliwa baada ya kupewa onyo kali na kutakiwa kujirekebisha ndani ya miezi mitatu kuanzia juzi.
Watumishi hao wanadaiwa ‘kutafuna’ mamilioni ya fedha za jiji hilo, zikiwemo sh. milioni 28 za ushuru wa samaki zilizokusanywa katika kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Tanzania Fish Processors (TFP).
Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, alisema mamilioni hayo yalipokusanywa, badala ya kuwekwa kwenye akaunti ya halamshauri, yaliwekwa katika akaunti binafsi ya mfanyakazi mmoja ambaye amekiri kutenda kosa hilo.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji, siku moja baada ya kugomea bajeti ya mwaka 2014/2015 ya zaidi ya sh. bilioni 87.2, kwa madai kuwa vyanzo vingine vya mapato ya ndani havikuainishwa.
Wakiongozwa na Meya Mabula na Naibu wake John Minja (CCM), katika Kikao cha baraza cha Januari 9 mwaka huu, madiwani hao walidai bajeti hiyo imetengenezwa kwa ajili ya maslahi ya watu binafsi (watumishi wa jiji) na siyo wananchi wa Mwanza na hivyo kuapa kutoipitisha hadi itakapokidhi maslahi ya wananchi.
Baada ya uamuzi huo ambao umekuwa wa kwanza katika historia ya jiji hilo, Mabula alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Hassan Hida, aitishe kikao cha Kamati ya Fedha kupitia upya na kurekebisha bajeti hiyo kabla ya kikao cha Baraza kukaa na kupitia vyanzo vya mapato vilivyo chakachuliwa.
Kamati hiyo juzi ilipochambua mapato ya jiji, baadaye iliketi kama kamati ya nidhamu na na kujadili watumishi hao ambao wanadaiwa kujikusanyia mamilioni hayo ya fedha kwa kutumia kitabu kimojawapo cha kukusanyia mapato katika kiwanda hicho.
Baada ya kikao hicho, ndipo baraza lilipokaa nalo kulazimika kujigeuza kama Kamati na kuwajadili watumishi hao kabla ya kutoa maamzi hayo magumu huku makachero wakiwa wamezingira ukumbi wa jiji hilo ili wawatie mbaroni wahasibu hao na kuambulia patupu.
Akitangaza uamuzi huo, Mabula aliwataja wahasibu waliosimamishwa na watatakiwa kufikishwa kwenye mkono wa sheria kuwa ni Rabisante Meena (Mhasibu Mkuu wa Mapato), Edwin Magere  ambaye ni Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Mpato na Mariam Mjema (Mtunza Stoo Msaidi wa Vitabu vya Mapato.)
Wengine waliosimamishwa kwa ajili ya uchunguzi wa ndani ni Geoffrey Liana (Mtunza Fedha wa Dirishani) na Mary Mushi Mhasibu Mkuu wa mapato ya jiji hilo.
Mabula ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, alidai kwamba huo ni mwanzo tu bado wanaendelea kufatilia baadhi ya ubadhilifu unaodaiwa kufanywa na watendaji wa jiji hilo katika miradi mbalimbali kabla ya kuwachukulia hatua.
Wakati kikao hicho kikiendelea, makachero wa polisi walionekana kutanda katika maeneo ya jengo la Halmashauri ya jiji hilo wakisubiri kuwatia mbaroni watumishi ambao waliamriwa kufikishwa kwenye mkono wa sheria lakini waliambulia patupu baa ya watumishi hao kuondoka mapema baada ya kuhojiwa na Kikao hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru