Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Tuesday, 9 September 2014

Pinda awataka wanasheria wawe wazalendo


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka wanasheria kutoka nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, waweke mbele maslahi ya wananchi wa kawaida wakati wanapoingia mikataba na wawekezaji kwenye sekta ya madini.
Alitoa wito huo jana wakati akifungua semina ya siku tano juu ya mafunzo ya kuingia makubaliano na mikataba kwenye sekta ya madini kwa wanasheria wa sekta ya umma kutoka nchi wanachama wa Jumuia hiyo ulioanza leo kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na washiriki wa mkutano huo kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania, Pinda alisema wanapaswa wawajali sana wananchi walio maskini kwa sababu wao hawana fursa ya kuingia kwenye vikao kama vyao na kutoa sauti juu ya kile wanachokitaka.
“Muwapo ofisini kwenu au kwenye miji yenu mikuu, mnapojadiliana na wawekezaji na kufikia makubaliano kuhusu rasilimali za nchi, siku zote muwafikirie hawa watu wa chini, walio maskini ambao ni wengi na wako nje ya majengo yenu.
“Wao ndiyo wadau wakuu, lakini hawana uwezo wa kuingia kwenye vikao kama hivi. Sote tunatambua kwamba wameishi na hizo rasilmali kwa vizazi vingi tu. Licha ya umaskini wao, wanaishi juu ya ardhi ambayo chini yake kuna utajiri tele wa madini na rasilimali nyingine.  Ninawasihi sana muwafikirie watu hawa kabla ya kufanya maamuzi yoyote,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema ili jambo hilo liweze kufanikiwa, ni lazima wanasheria kama wadau wa mwanzo kabisa, wawe tayari kukataa kupokea fedha chafu na vishawishi kutoka kwa wawekezaji na siku zote waweke uzalendo mbele kwa maslahi ya nchi zao.
“Rasilimali za bara la Afrika hazijaleta maendeleo kwa wakazi wa bara hili kwa sababu wanaofaidika ni makampuni makubwa kutoka nje na watu wachache sana wenye nafasi huku walio wengi wakiambulia patupu. Ni theluthi moja tu ya mikataba ya uchimbaji madini inayolifaidisha bara zima la Afrika, ikilinganishwa na faida ambayo bara la Amerika Kusini inanufaika nayo,” alisema.
Ili kuepukana na hali hiyo, Waziri Mkuu alisema umefika wakati wa kukataa kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za kimataifa na kuhakikisha kuwa kampuni hizo zinalipa kodi katika kila nchi husika ya Afrika Mashariki.
“Natumaini hii semina itasaidia kutufungua macho katika maeneo ambayo mikataba yetu na sheria zetu zilikuwa zinalegalega, ili kuanzia sasa tuweze kunufaika na rasilimali zetu,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda alisema umefika wakati wa kuhakikisha serikali za nchi husika zinaweka sera madhubuti na miongozo ya kisheria itakayohakikisha mikataba inayoandaliwa kwa ajili ya utafutaji na uendelezaji wa madini na rasilimali zake inazinufaisha nchi kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema semina hiyo ni muhimu kwa sababu wanaolengwa ni wanasheria kutoka Afrika Mashariki na Afrika ndilo eneo pekee lenye rasilmali ambazo bado hazijaendelezwa.
“Wanapaswa kutambua kwamba mfanyabiashara yeyote akija ni lazima anatafuta faida. Na ukilala tu, yeye anapata faida kubwa sana. Wakienda kusaini mikataba, hawa wanasheria wanapaswa kuangalia sheria za nchi husika, lakini pia wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuacha tamaa. Wanatakiwa wafanye maamuzi kwa niaba ya wananchi,” alisema.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema sekta ya madini ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa haraka hapa nchini, lakini inachangia chini ya asilimia moja ya ajira zote.

Wakulima sasa kupewa pembejeo kwa ruzuku

  • Mawakala waliokuwa wakitumia vocha kunywa pombe kitanzini
Na Hamis Shimye
SERIKALI imesema inaanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima na kuachana na utaratibu wa vocha, ambao ulikuwa unafanyika kinyume na utaratibu.
Imesema hali hiyo inasababishwa na ubadhirifu uliokuwa unafanywa na mawakala wasiokuwa waaminifu, ambao walikuwa wanatumia pesa kunywea pombe na malipo kufanya kwa kutumia vocha za pembejeo.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza, alitoa msimamo huo wa serikali jana, wakati alipokutana na wawakilishi wa benki mbalimbali nchini.
Katika kikao hicho, Waziri Chiza alisema serikali imeamua kuja na mfumo mpya wa kuwawezesha wakulima kupitia vikundi vyao ili waweze kukopa katika benki.
“Lengo tufanye utaratibu huu na kila benki nchini, ambapo wapo walioonyesha nia ya kuanza na sisi katika huu utaratibu mpya, wengine wamesema wataanza mwakani,’’alisema.
Chiza alisema utaratibu wa vocha za pembejeo ulikuwa na matatizo lukuki, ikiwemo mawakala kujinufaisha wao na si wakulima waliokusudiwa na serikali.
Alisema wameshachukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuwafungulia mashitaka mawakala wote waliokwenda kinyume, ikiwemo wale waliokuwa wanazitumia vocha kunywa bia.
“Kulikuwa hakuna usimamizi mzuri katika vocha za pembejeo. Utaratibu huu mpya wa mikopo kupitia mabenki utakuwa mzuri na utamnufaisha mkulima,’’ alisema.
Chiza alisema utataribu huo utaanza kutumika muda si mrefu kuanzia sasa baada ya taratibu kukamilika, ikiwemo benki kukubali taratibu zinazotakiwa na serikali.

Kivuko kipya cha Mv Dar kuwasili nchini mwezi ujao

NA MUSSA YUSUPH
SERIKALI imetangaza kukamilika kwa ujenzi wa Kivuko kipya cha Mv Dar es Salaam,
kitakachokuwa na uwezo wa kuvusha watu zaidi ya 300 kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.
Kukamilika kwa kivuko hicho, kinachotarajiwa kuwasili nchini katika kipindi cha wiki tatu zijazo,kunatokana na jitihada za serikali katika kupunguza msongamano wa magari na shida ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Mbali na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya abiria, kivuko hicho pia kitakuwa na kasi itakayowezesha kufanya safari zake haraka zaidi, kuliko vivuko vingine vilivyopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema Kivuko hicho kilichoigharimu serikali sh. bilioni 7.9, kinatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Bagamoyo na Dar es Salaam kwa kufanikisha shughuli za kibiashara kati ya pande hizo kwa haraka zaidi.
Aliongeza kuwa tayari mkandarasi kutoka nchini Denmark ameshaanza utaratibu wa kukisafirisha kuja Dar es Salaam, hivyo wananchi wategemee kuanza kufanya kazi mara tu baada ya kuwasili kwake.
Wakati huo huo, Waziri Magufuli amezindua kivuko cha Mv Kigamboni kilichokuwa kikifanyiwa ukarabati na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kamandi ya Wanamaji.
Katika uzinduzi huo, Magufuli alilipongeza jeshi hilo kwa kukamilisha ukarabati wake kwa haraka zaidi na kuokoa zaidi ya nusu ya fedha iliyokuwa ikitarajiwa kutumika katika ukarabati huo kama ungefanyika nje ya nchi.
Alisema awali, serikali ilitaka kukipeleka kivuko hicho Mombasa, Kenya kwa ukarabati, lakini kutokana na uwezo wa juu walionao wahandisi kutoka JWTZ, ndicho kilichoisukuma kulipatia jeshi hilo kazi ya ukarabati.
Aidha, ili kuepukana na tatizo la kupungua kwa kina cha maji, Waziri Magufuli aliliomba jeshi hilo kuhakikisha ifikapo kesho jioni, kivuko hicho kinaingizwa baharini na kuanza kuhudumia wananchi, ombi ambalo lilikubaliwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kamandi ya Wanamaji, Brigedia Jenerali, Rogastian Laswai, alisema jeshi limefanya kazi kwa uzalendo na idadi kubwa ya vifaa walivyotumia katika ukarabati huo ni vya kutoka nchini.
Alisema wamefanikiwa kuokoa fedha za kigeni, ambazo zingetumika kununua baadhi ya vifaa na kuwalipa wahandisi kutoka nje ya nchi na wamehakikisha usalama wa kivuko unabakia katika mikono ya Watanzania licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali.

Wanafunzi 808,111 wa darasa la saba kufanya mitihani leo

NA RACHEL KYALA
SERIKALI imewataka wakaguzi wa elimu katika ngazi zote nchini, kuhakikisha idadi ya wanafunzi 808,111 wanaopaswa kufanya mtihani wa darasa la saba inatimia.
Aidha, imewataka wakaguzi hao kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi na walezi watakaowaelekeza wanafunzi hao kufanya vibaya katika mitihani hiyo kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa sababu zisizo za msingi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema jana kuwa, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwaagiza watoto wao kuandika madudu ili wasifaulu mtihani, badala yake kuwafanya vitega uchumi vya familia kwa kuwatafutia kazi ama kuwaozesha.
“Hivi karibuni nilifanya ziara wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma kwa lengo la kuionya jamii hiyo, ambayo imekuwa na tabia ya kuwafanyia ngoma za kuwapongeza wanafunzi wanaofeli au kutofanya mtihani wa darasa la saba na kuwataka waache tabia hiyo mara moja,” alisema.
Alisema alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha anawachukulia hatua kali za kisheria wote watakaofanya jambo hilo mwaka huu, na kuwataka wakuu wengine wa mikoa na wilaya kufanya hivyo.
Naibu Waziri huyo pia amezionya kamati za mitihani za mikoa na wilaya nchini, kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo na kuwataka wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Nawaasa wasimamizi wa mitihani kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani serikali itachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za mitihani,” alisema.
Alisema jumla ya shule 15,884 zinatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, zikiwa na jumla ya watahiniwa 808,111, wavulana wakiwa 378,470, sawa na asilimia 46.84, na wasichana 429,641, sawa na asilimia 53.16.
Alibainisha kuwa watahiniwa 783,223 watafanya mtihani huo kwa lugha ya kiswahili na 24,888 kwa kiingereza. Watahiniwa wasioona walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 86 huku wenye uoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa wakiwa 714.

Ajali yaua padri na wengine wanne

NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
WATU watano, akiwemo Padri wa Kanisa Katoliki, Paulo Mwanyalila, wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani Mbeya.
Katika ajali hiyo iliyomwua Padri Mwanyanyila, gari lenye namba za usajili T241 BKZ aina ya Toyota Coaster, liligongana na gari liingine ambalo haijafahamika aina wala namba zake za usajili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi,(pichani) alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa moja jioni katika barabara ya Mbeya- Tukuyu, eneo la Garijembe, kata ya Utengule wilayani Mbeya.
Msangi alisema mbali
na Padri Mwanyanyila, wengine waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Edina Jason (22), mtu moja aliyejulikana kwa jina la Mortina (30) na mwanamke mmoja ambaye hajajulikana jina.
“Katika ajali hii iliyoua watu wanne, pia ilisababisha watu watatu kujeruhiwa ambao ni Samwel Sanga (34), Mawazo Gasper na mtoto mwenye umri kati ya miaka miwili na mitatu, ambaye hakuweza kufahamika jina lake,” alisema.
Alisema chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa na kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani Mbeya na pia majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa hospitalini hapo.
Msangi alisema madereva wa magari yote mawili walikimbia baada ya  ajali hiyo na msako mkali wa kuwatia mbaroni unaendelea ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika ajali ya pili, mtoto Grolia Revocatus (2), amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Mbeya- Iringa, eneo la Itewe wilayani Mbeya.
Msangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.30 usiku na kuwa dereva wa gari lililosababisha ajali hyo alikimbia baada ya kutokea kwa ajali hiyo na jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Aliwataka madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Mkurugenzi apinga kurejesha fedha


Na Chibura Makorongo, Itilima
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Abdallah Malela, amepinga agizo la kurejesha fedha za halmshauri mpya ya Itilima zilizotolewa na Hazina.
Pia anadaiwa kuwatimua ofisini kwake madiwani wa Itilima waliokwenda kudai fedha hizo.
Kauli hiyo ilitolewa katika baraza la madiwani wa halmashauri ya Itilima na Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri, Khamis Mughata, ambaye alisema kamati yake ilishindwa kudai fedha hizo kutokana na mkurugenzi huyo kuwafukuza ofisi kwake.
Alibainisha kuwa kamati yake ilikuwa ikifuatilia mradi wa maji wa Lugulu-Zanzui ulioko ndani ya wilaya hiyo, ambapo walibaini ubovu wa miundombinu na matumizi mabaya ya fedha katika ununuzi wa vifaa.
Mughata alisema mradi huo ambao pesa zake ziko katika halmshauri ya Bariadi, ulikataliwa na mkurugenzi huyo kuukabidhi katika halmshauri yao, ikiwa pamoja na kukataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa ubadhilifu huo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Itilima, Leornad Masele, alisema alishindwa kupata fedha wanazodai kutoka Bariadi kutokana na mkurugenzi huyo kugoma kukutana naye.
Awali, uongozi wa mkoa wa Simiyu, uliagiza wataalamu wa fedha wa kila halmshauri kukutana kwa ajili ya kuchunguza kiasi gani kinadaiwa, ambapo ilielezwa kamati hizo za wataalamu zilikuta na kupata takwimu sahihi za madeni hayo.
Alisema kwa maelekezo ya katibu tawala mkoa, wakurugenzi wote walitakiwa kukutana ili kumaliza hoja hiyo ya madeni, ambapo alieleza mkurugenzi mwenzake wa Bariadi amekataa kukutana naye bila kutoa sababu maalumu.
Katika kikao hicho, madiwani waliazimia kwenda kumshitaki mkurugenzi huyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa kukaidi agizo la serikali kuu.

Jela miaka 15 kwa shambulio la aibu


NA SOPHIA ASHERY, A3
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Hassan Seleman (23), kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la shambulio la aibu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Juma Hassan baada ya mahakama  kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Karani wa mahakama hiyo, Felister Mosha, alidai kuwa Seleman alitenda kosa hilo Oktoba 23, mwaka jana, maeneo ya Kitunda Migombani, jijini  Dar es Salaam.
Felister alidai kuwa Seleman alimchukua mtoto wa miaka mitatu (jina linahifadhiwa), aliyekuwa akitoka shule na kwenda naye nyumbani kwao na kisha kumuingizia vidole sehemu za siri.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Hassan alisema ametoa adhabu hiyo kwa kuwa kitendo kilichofanywa na mshitakiwa ni cha kulaaniwa.
Alisema adhabu hiyo ni fundisho kwa mshitakiwa pamoja na wengine ambao wamekuwa wakifanya vitendo kama hivyo vya aibu.

Vijisenti vyamfikisha kortini


SOMOE NKHOMEE, TUDARCO
MKAZI wa Dar es Salaam, Ally Mohammed, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, akikabiliwa na shitaka la wizi wa sh. 55,000.
Mohammed (22), alifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa shitaka na karani Lucy Rutabanzibwa, mbele ya Hakimu Mkazi Christina Luguru.
Lucy alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 4, mwaka huu, saa nane alasiri maeneo ya soko la samaki la Ferry, wilayani Ilala.
Alidai mshitakiwa aliiba sh 55,000 mali ya Khadija Hussein, aliyefika sokoni hapo kwa ajili ya kununua samaki.
Mshtakiwa alikiri shitaka hilo na kurudishwa rumande hadi Septemba 11, mwaka huu, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka serikali ya mtaa na kila mmoja kutia saini ya bondi ya sh 200,000.

Rungwe yapania kumaliza tatizo la mabara, madawati


NA MWANDISHI WETU, TUKUYU
HALMASHAURI ya Wilaya Rungwe, imetenga sh. milioni 150 kwenye bajeti yake ya mwaka 2014/2015, kununua vifaa vya maabara na kufunga mifumo imara ya gesi, katika shule zake 28 za sekondari zilizoko wilayani humo.
Kiasi hicho cha fedha kitatengwa kupitia ruzuku ya kukuza mtaji katika Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alisema hayo alipokuwa akielezea mkakati wa kujenga na kutumia maabara kwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani hapa.
Veronica alisema walimu wa masomo ya sayansi waliopo ni 154, kati ya walimu 336 wanaohitajika hivyo kuna upungufu wa walimu 182 lakini kwa masomo ya sanaa hawana upungufu kwa sasa.
Alisema kimsingi, karibu shule zote 28 za sekondari zinafanya mafunzo kwa vitendo na kufanya mitihani isipokuwa mbili alizozitaja kuwa ni Kimampe na Ziwa Ngozi.
“Mkakati uliopo ni kuimarisha vyumba vinavyotumika kama maabara kwa kuhakikisha tunaziwezesha shule kutengeneza mfumo wa kusambaza gesi katika vyumba vilivyotengwa nna tayari tumefanya mazungumzo na atakayefanya kazi hiyo,” alisema Veronica.
Aliongeza kuwa sh. 500,000 zimetengwa kwa kila shule, hivyo jumla ya sh.14,000,000 zitatolewa kutoka kwenye ruzuku ya kukuza mtaji katika serikali za mitaa.
Mkurugenzi huyo alisema mikakati mingine iliyopo ni kuziwezesha shule kununua vifaa vyote vya maabara vinavyohitajika ambapo kila shule itapewa sh.milioni 1.5. alisema katika ununuzi huo sh. milioni 42 zimetengwa kupitia ruzuku ya serikali za mitaa.
Veronica aliongeza wanatengeneza stuli 994 na meza 633 zinazopungua ili kuwezesha kila mwanafunzi kuwa na meza na kiti chake anapokuwa kwenye chumba cha maabara.
“Meza na viti hivyo zitatengenezwa kutokana na miti inayoendelea kukatwa ili kutengeneza samani za shule za msingi na sekondari na sh. milioni 65 zimetengwa kwa kazi hiyo,” alisema Veronica.
Kwa mujibu wa Veronica, pia wanatarajia kumalizia ujenzi wa maabara katika shule za Isongole, Mpuguso, Lupoto na Kisiba ambapo wametenga sh. milioni 94 kwa ajili ya kazi hiyo sambamba na kuziwezesha shule za Kimampe na Lake Ngozi kununua maabara za kuhamishika ambapo kila moja itapewa sh. milioni mbili.
Mkurugenzi aliongeza wanatarajia kuanza ujenzi wa vyumba 52 ili kukamilisha idadi ya vyumba vitatu kwa kila shule ambapo kila mwaka watakuwa wanatenga kwenye bajeti kiasi cha sh. milioni 150 kwa ajili hiyo.
Kwa upande wa shule za msingi, alisema yanahitajika madawati 26,670 wakati  yaliyopo ni 14,196 sawa na asilimia 53 ya mahitaji hivyo kuna upungufu wa madawati 12,474.
Kwa shule za sekondari, alisema zinahitajika meza 15,426 na viti 15,426 na kuwa zilizopo ni 14,707 na viti 14,707 hivyo kuna upungufu wa meza 719 na viti idadi hiyo hiyo.
Veronica alisema kwa sasa halmashauri inavuna msitu wake ulioko  Simike ambapo mbao 6,500 zinatarajiwa kuvunwa kwa ajili ya kutengeneza madawati, viti na meza kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Alisema hadi mwishoni mwa wiki iliyopita ya mbao 2,131 zilikuwa zimepasuliwa na kuhifadhiwa ili zikauke.

Waliokufa, majeruhi ajali ya basi waanza kutambuliwa


NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
MAITI mbili kati ya nne za ajali ya basi la kampuni ya Air Bus iliyotokea juzi wilayani Gairo, zimetambuliwa.
Basi hilo lilipata ajali likiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora.
Aidha, majeruhi 30 wa ajali hiyo bado wamelazwa katika hospitali za Berega na ya rufani ya mkoa wa Morogoro, wakipatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul,  alisema jana ofisini kwake mjini hapa kuwa waliotambuliwa ni Amina Rashid (50), mkulima na mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam na Makoye Hamis (34) mkulima na mkazi wa Tabora.
Kamanda huyo alisema na tayari ndugu wamezichukua maiti hizo kwa ajili ya kusafirisha na kufanya utaratibu wa mazishi.
Kamanda Paul pia alitaja majina ya majeruhi hao 30 na kwamba majeruhi 16 wamelazwa Hospitali ya Berega na majeruhi 14 wamelazwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro.
Aliwataja majeruhi waliolazwa Morogoro kuwa ni Amood Said, Augustino Mbago, Novatus Patrick, Paulo Lucas, Single Salum, Jieleza Salum, Lazaro Clemence, Omary Amiri, Laurencia Deo na Neema Hamis wote watoto, Nasra Hassan, Hadija Yusuph, Asha Kobongo na Halima Adam.
Wengine waliolazwa katika hospitali ya Berega ni Rajabu Juma, Uweso Chamalupe, Emanuel Joel, Bakari Edmond, Fidelis Laurent, Mashala Shagembe, Magembe Salum, Isaya Clemence, Julieth Magomba, Joha Athumani, Esta Chagoma, Asha Musa, Lidya Claud, Helieth Kayaya, Daniel Lanford na Anjela Michael.
Kamanda huyo alisema kuwa hali za majeruhi zinaendelea vizuri na kuwataka wananchi kujitokeza kutambua maiti mbili zilizobaki ambazo ni za wanaume.
Pia alisema jeshi hilo mpaka sasa linamtafuta dereva wa basi ambaye alitoweka kusikojulikana baada ya kutokea kwa ajali.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 5.45 katika eneo la Berega, Gairo ambapo  basi la Airbus lilipinduka na kuacha njia na kutumbukia katika daraja la Mto Mkange na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 34.

3,000 wahitimu mafunzo ya polisi


Na Rodrick Makundi, Moshi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Haji Omar Kheir, atakuwa  mgeni rasmi katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali ya askari polisi.
Mafunzo hayo yanayoendelea katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA) mjini hapa, yatafikia tamati keshokutwa ambapo wageni mbalimbali akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu, watahudhuria.
Akizungumza na waandishi jana, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, Matanga Mbushi, alisema wanafunzi wa uaskari 3,213 wanahitimu mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa Mbushi, wanafunzi wa uaskari waliojiunga chuoni hapo walikuwa 3,509, ambapo 296 kati yao walishindwa kuhitimu mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu na kughushi vyeti.
Alisema wanafunzi 212 walifukuzwa kutokana na kubainika kuwa waligushi vyeti na wengine 84 wakifukuzwa kwa utovu wa nidhamu.
Idadi ya askari wanaohitimu mafunzo hayo inahusisha askari wa  uhamiaji waliojiunga na mafunzo chuoni hapo wapatao 43, ambapo wanaotarajiwa kuhitimu ni 41 wakiwemo wanaume 24 na wanawake 17.
Tofauti na miaka mingine, Mei 9, mwaka huu, jeshi la polisi lilitangaza kuwafukuza chuo askari 212, baada ya kuthibitika kughushi vyeti na wengine 25 waliachishwa mafunzo baada ya kubainika kuwa na matatizo ya kiafya na wengine utovu wa nidhamu.
Hatua hizo zilitokana na ushirikiano kati ya jeshi la polisi nchini na baraza la taifa la mitihani (NECTA), kufanya uamuzi wa kuhakiki vyeti vya wanafunzi wote 3,415 waliojiunga na mafunzo hayo Desemba mwaka 2013.

Umekwapua simu? Sasa utakiona


NA EMMANUEL MOHAMED
MATHIAS Abdallah (64), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Kinondoni kwa kosa la wizi wa simu ya mkononi.
Karani Alfred Lengalenga alidai mbele ya Hakimu Hakimu Anna Kihiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Jumapili iliyopita maeneo ya Mwananyamala. Alidai kuwa aliiba simu aina ya Samsung Note 3 na Nokia Obama, zenye thamani ya sh. milioni moja, mali ya Mzurimwema.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo, na kumlazimu Hakimu Kihiyo kumsomea masharti ya dhamana kutokana na kutokamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo.
Hakimu Anna alimtaka mshtakiwa awasilishe mahakamani hapo wadhamini wawili, wenye ajira za kudumu watakao tia saini ya bondi ya sh. 500,000.
Mshitakiwa alirudishwa rumande,kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi itatajwa tena Septemba 19, mwaka huu.

Kizimbani kwa ubakaji


NA EMMANUEL MOHAMED
MKAZI wa Dar es Saalam Juma Omary, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu shitaka la ubakaji.
Omary (65), alisemewa shitaka hilo jana, mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka Faustine Sylvester mbele ya Hakimu Boniphace Lihamwike.
Sylvester alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 19, mwaka huu, muda usiofahamika, katika mtaa wa Mkunguni, Kinondoni.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo na alirudishwa rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Lihamwike alimtaka awe na wadhamini wawili,
ambao watumishi wa Serikali. Kesi itatajwa Septemba 22, mwaka huu.

Watakiwa kuacha kubweteka, wafanye kazi


NA PRISCA MSHUMBUSI, MWANZA
WAKAZI wa kata ya Mbugani jijini Mwanza, wametakiwa kujitolea ili kujiletea maendeleo badala ya kusubiri kufanyiwa kila kitu na serikali.
Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa
Mtaa wa Mabatini Kaskazini, Ntobi Boniface, alipozungumza na  waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alisema kujituma huleta maendeleo katika jamii.
Alisema kuwepo changamoto hususan katika utengezaji wa barabara za mitaa, ujenzi wa maabara na miradi mingine ya maendeleo, ni kikwazo kwa maendeleo.
“Tuna tatizo la barabara kwa muda mrefu, hali inayosababisha wananchi wakati wa mvua kushindwa kutoka nyumbani, lakini jitihada zinaendelea ili kuboresha mazingira na wananchi wanapaswa kutuunga mkono katika hili,” alisema.
Alisema wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara kuhamasisha jamii kushiriki shughuli za maendeleo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Kuhusu hali ya usalama, Boniface alisema ni nzuri na kuwa wananchi wamekuwa wakishirikiana vyema kupitia Polisi Jamii kwa kuwa kila raia ana jukumu la kulinda amani.

Friday, 5 September 2014

JK: Nitaiacha nchi pazuri


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete, amesema ataondoka madarakani akiwa ameiacha nchi mahali pazuri na kwamba, atakuwa na mengi ya kukumbukwa.
Amesema serikali yake imefanya mambo mengi kwa ajili ya Watanzania na kwamba, sekta karibu zote zimepiga hatua kubwa kimaendeleo.

Pia amewataka Watanzania kuombea mema mazungumzo baina yake na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), yenye lengo la kutafuta maridhiano kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Ameeleza kuwa siku zote amekuwa akifungua milango kwa watu wanaotaka kumuona kwa ajili ya masuala mbalimbali ya kitaifa na angependa kuona mchakato wa Katiba Mpya ukikamilika kwa mafanikio.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dodoma katika Chuo cha Mipango, ambapo alieleza masuala mbalimbali ya maendeleo na mikakati inayoendelea kufanywa na serikali.
“Nitaondoka madarakani nikiwa nimeiacha nchi mahali pazuri, ikiwa na mengi ya kukumbukwa na kuigwa.
“Tumejenga barabara nyingi za lami, miradi ya maji, umeme na elimu imeboreshwa kwa mafanikio makubwa. Tumepiga hatua kubwa na inastahili kuungwa mkono,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa pamoja na kupata mafanikio hayo, bado serikali imeendelea na jitihada zake katika kuboresha sekta mbalimbali na huduma za kijamii.
Alisema kuwa hivi karibuni atazindua miradi mingine mikubwa katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na Sera ya Elimu, ambayo tayari imekamilika.
Miradi ya maji
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayetembea kilomita nne bila ya kupata maji.
Rais Kikwete alisema hadi sasa asilimia 65 ya miradi ya maji imetekelezwa vijijini na asilimia 90 mijini.
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji.
MIUNDOMBINU
Rais Kikwete alisema lengo la serikali ni kuunganisha barabara za lami mkoa kwa mkoa.
Alisema kwa mkoa wa Dodoma, sh. bilioni 44 zimetengwa kupeleka umeme vijijini.
Rais Kikwete alisema huduma za simu zimesambaa kwenye maeneo mengi hapa nchini na kwamba kazi iliyobaki ni ndogo.
ARDHI
Kiongozi mkuu huyo wa wananchi aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi.
Alisema mipango ya matumizi ya ardhi itaepusha migogoro mingi inayotokea hapa nchini.
Rais Kikwete alisema kuhusu migogoro ya ardhi iliyotokea Kiteto, Morogoro na Tanga, wanaangalia namna ya kuimaliza.
AFYA
Alisema mafanikio makubwa yamepatikana na kwamba amefurahishwa kuona wananchi wameshirikishwa kikamilifu katika sekta hiyo.
Rais Kikwete alisema wilaya za Kongwa, Bahi, Chamwino, Dodoma Mjini na Chemba hazina hospitali za wilaya, hivyo  aliwaagiza watenge maeneo na serikali itasaidia kujenga hospitali hizo.
Alisema mkoa wa Dodoma umevuka lengo kwa kina mama kujifungilia hospitali.
Rais Kikwete alisema maambukizi ya ukimwi yanapungua na kwamba ni vyema yafikie asilimia ziro.
EBOLA
Alisema taarifa zinaonyesha watu 3,500 wameambukizwa ugonjwa wa Ebola Afrika ya Kati.
Rais Kikwete alisema ugonjwa huo ni hatari na ambao ni mpya na kwamba hauna tiba wala kinga.
Alisema ugonjwa huo unabebwa na ndege kama sokwe, swala na popo na kwamba mtu anaweza kuambukizwa kwa kugusa damu, majimaji au maiti.
Rais Kikwete alisema dalili zake ni homa kali, kichwa kuuma pamoja na kutokwa damu sehemu zote zilizokuwa wazi.
Alisema tayari wameshaunda kikosi kazi kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mkutano na TCD
Kuhusu mkutano wake na wajumbe wa TCD, alisema Mwenyekiti wa kituo hicho, John Cheyo, alimuomba kukutana kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbalimbali.
Alisema alikubali ombi hilo na Agosti 30, mwaka huu, walikutana na wajumbe wa kituo ambapo, masuala mbalimbali, ukiwemo mchakato wa Katiba Mpya na hatua ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) lilijitokeza.
Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya mambo waliyokubaliana na kupeana majukumu juu ya namna ya kuyashughulikia na kuwa wanatarajia kukutana tena wiki ijayo.
“Tumekutana na kuzungumza, lakini tumepeana kazi za kufanya na tutakapokutana tena wiki ijayo, tutaona tumefikia wapi,” alisema Rais Kikwete.

Serikali ya Tanganyika yakataliwa


Na Peter Orwa, Dodoma
SERIKALI ya Tanganyika imeendelea kupingwa, ambapo wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge Maalumu la Katiba, wamesema haiwezi kuwa na tija kwa Watanzania.
Kamati nyingi zilizoundwa kwa ajili ya kuchambua Rasimu ya Katiba na ambazo zinawasilisha maoni yake bungeni, zimepinga kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika.
Mapendekezo ya kuwepo kwa serikali ya Tanganyika, yamo kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
UHURU imebaini kuwa tangu kamati hizo zilipoanza kuwasilisha taarifa zake bungeni, imedhihirika karibu zote zilizowasilisha maoni yake kwa upande wa hoja ya walio wengi, hawakubaliani na kuwepo Serikali ya Tanganyika na wamedhihirisha kupitia maoni yao.
Kwa mujibu wa baadhi ya mawasilisho ya juzi jioni na jana asubuhi, sehemu kubwa ya kamati zilipinga uwepo wa serikali hiyo ya Tanganyika.
Akiwasilisha maoni yake juzi jioni, William Ngeleja kutoka Kamati Namba Tisa, alipinga kuwepo fursa ya kuwa na serikali ya Tanganyika, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jana, Suleiman Jaffu, msemaji wa Kamati Namba 12, naye alihimiza kuwa katika kamati hiyo, wameafikiana kuondoa Tanganyika na kuwa na Tanzania Bara kama ilivyo sasa.
“Ibara ndogo ya (3) na ya (4) irekebishwe kwa kufuta maneno ‘la Tanganyika’ na kuweka neno ‘Tanzania Bara. ” ilisomeka sehemu ya mawasilisho ya Jaffu kuhusiana na Ibara ya 117 ya rasimu hiyo.
Ibara ya 118 ikisomeka :“Ibara ndogo ya (2) neno ‘Tanganyika’linapendekezwa kufutwa na badala yake lisomeke Tanzania Bara.”
Maoni kama hayo ndio yalijitokeza jana kutoka kwa Juma Lawi, kutoka Kamati Namba Nane, ambayo yalisimama katika hatua zote ikitambua ’Tanzania Bara’ na si Tanganyika.
Kwa upande wake, Dk. Dalali Kafumu, kutoka Kamati  Namba 10, alisema kamati yake imepinga uwepo wa Serikali ya Tanganyika na badala yake itakuwwepo serikali ya Tanzania Bara.
“Rasimu ifanyiwe marekebisho na muundo unaopendekezwa na Kamati yangu ni wa serikali mbili, hautakuwa na Bunge la Tanganyika,” alisema Dk. Kafumu.

Thursday, 4 September 2014

Uenyekiti waipasua CHADEMA

  • Mikakati kumtosa mpinzani wa Mbowe yaiva
  • Wagombea wengine wageuzwa kiini macho 
  • Mtandao wa Zitto hatari, kuendelea kufyekwa 
NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza majina ya makada wake wanaowania nafasi za uongozi ngazi ya taifa huku majina ya vigogo na wabunge yakisheheni.
Tayari uchaguzi huo umezidi kukiweka njiapanda chama hicho kutokana na makada wengi kuenguliwa kwenye ngazi za majimbo na mikoa, ikiwa ni mkakati wa kuwatosa wanachama wapenda mabadiliko.
Hata hivyo, katika orodha hiyo iliyotangazwa mjini Dar es Salaam jana, majina ya wagombea wanaowania nafasi ya Mwenyekiti Taifa haikuwekwa hadharani.
Freeman Mbowe
Nafasi hiyo inawaniwa na Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe, Daniel Luvanga, Gambaranyera Mongateo na Kansa Mbarouk, ambaye anatajwa kuwatia vigogo wa chama hicho matumbo joto.
Pia, anadaiwa alikuwa swahiba wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, ambaye mtandao wake ndani ya chama hicho umeendelea kusambaratishwa kutokana na kuwa na misimamo na kutokubali kuyumbishwa. 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uratibu wa Kanda wa CHADEMA, Singo Kigaila, alisema majina ya wagombea nafasi ya mwenyekiti yanaendelea kuchambuliwa.
Alisema Kamati ya Uchaguzi inaendelea kuyapitia kwa umakini majina na taarifa za wagombea kabla ya kutoa maamuzi sahihi kulingana na vigezo.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA zimesema, kinachofanyika kwa sasa ni kuangalia mikakati ya kuwachinja baadhi ya wagombea ili kutoa fursa kwa Mbowe kupata ushindi wa kishindo.
Chanzo hicho kimesema kuwa, kazi ya kuchambua taarifa za wagombea wa nafasi hiyo haiwezi kuwa ngumu kwa kuwa idadi iliyojitokeza ni ndogo na wote ni makada wanaofahamika.
Kimesema nafasi ya Kamati Kuu ya CHADEMA ambayo, ndio nyeti katika chama cha siasa, ina wagombea 56 huku idadi inayotakiwa ni wajumbe wanane, ambao wote taarifa zao zimepitiwa na majina kutangazwa.
Miongoni mwa wanaowania ujumbe wa Kamati Kuu ni Profesa Mwesige Baregu, Bernad Saanane, Ansbert Ngurumo, Suzan Kiwanga, John Mwambigija, Methayo Torongey, Rose Kamili, Vicent Munghwai, Mwita Mwikabe Waitara, Alphonce Mawazo na Chiku Abwao.
Habari zaidi zimesema kuwa, hatua ya Mbarouk kuchukua fomu kupimana ubavu na Mbowe, imewashitua baadhi ya viongozi kwa kuwa hawakutarajia kada huyo kijana kuibuka.
Hatua hiyo inatokana na ushawishi mkubwa aliokuwa nao Mbarouk ndani ya CHADEMA huku kansa ya mpasuko iliyoikumba ikiendelea kukitafuna ndani kwa ndani.
“Hawawezi kutangaza majina ya wagombea wa uenyekiti hadi mikakati yao ya kumfyeka Mbarouk itakapokuwa imekaa vizuri. Wanafahamu uwezo na nguvu ya ushawishi aliyokuwa nayo huyu kijana, hivyo ni lazima wajipange. 
“Kinachofanyika ni kuhakikisha wanakata jina lake mapema ili wajihakikishie kutawala tena, hivyo wakifanya mambo kwa haraka, kuna wengine wanaweza kukimbilia mahakamani kusimamisha uchaguzi,” alisema na kuongeza: 
“Bado kuna makada hawafurahishwi na mwenendo wa CHADEMA na kwamba, wanaweza kupiga kura za maruhani na kusababisha fedheha iwapo Mbarouk atasimama mbele ya wajumbe kuomba kura.”
Dalili za kumdhibiti Mbarouk zilianza kuonekana siku aliyotangaza kuchukua fomu, ambapo aliwekewa mizengwe mbalimbali huku wafuasi na walinzi wake waliomsindikiza wakizuiwa kuingia ofisini.
Mbarouk alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Tabora, ambapo kabla ya kukuchukua fomu kuwania nafasi hiyo, alijiuzulu nyadhifa zake zote na kuonya kuwa, amejitokeza kwa lengo la kumdondosha Mbowe.
Vigogo BAWACHA
Nafasi nyingine ambayo inatarajiwa kukipasua chama hicho ni ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), ambapo vigogo kadhaa wakiwemo wabunge wamejitosa kuipigania.
Waliojitosa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Iringa, Chiku Abwao na Lilian Wassira. Wengine ni Janeth Rithe, Rebecca Magwisha na Sophia Mwakagenda.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema Lilian ndiye alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuongoza baraza hilo, lakini kutokana na misimamo yake, amewekewa wapinzani.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mwanasiasa huyo kijana na mwenye kukubalika, anapata wakati mgumu kwenye kusaka ushindi. Kwa sasa washindani wakubwa kwenye kundi hilo ni Chiku na Halima.
Chanzo chetu ndani ya CHADEMA kimesema kuwa, baadhi ya makada hao walichukua fomu za kuwania nafasi hiyo siku za lala salama na kwamba, walipata msukumo wa kufanya hivyo.

MAUAJI YA MAHABUSU


Mazito yaibuka tena 

  • MOI yazuia jalada la marehemu, yataka malipo 
  • Familia, Polisi waendelea wavutana 
NA MWANDISHI WETU
MAITI ya mtuhumiwa aliyedaiwa kupigwa na kusababisha kifo chake akiwa mahabusu, imeshindwa kufanyiwa uchunguzi ili kutoa fursa kwa ndugu kuendelea na taratibu za maziko.
Liberatus Damian, alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kufikishwa kwa matibaabu akiwa hoi kwa kile kinachodaiwa kupigwa akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Stakishari, Dar es Salaam.
Hata hivyo, jana ndugu na jamaa wa marehemu walifika hospitalini hapo kwa ajili ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi, lakini ilishindikana baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa yaFahamu ya Muhimbili (MOI), kuzuia jalada.
Jalada hilo lilizuiwa kutokana na taarifa kuwa marehemu anadaiwa zaidi ya sh. 260,000 za matibabu wakati alipofikishwa hospitalini hapo.
Kadhia hiyo imetokea ikiwa ni siku moja tangu Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kuunda jopo la kuchunguza tukio hilo.
Habari zimedai, Damian alikuwa amehifadhiwa kituoni hapo na alifariki Agosti 31, mwaka huu, katika Hospitali ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mwanasheria wa familia hiyo, Bagiliye Bahati, alisema jana walipanga kufanya uchunguzi wa mwili wa Daniel, lakini uongozi wa MOI ulizuia jalada.
Alisema walifika hospitalini hapo saa 3:00 na kukutana na jopo la wachunguzi hao wa polisi pamoja na wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa ajili ya kuchunguza mwili.
Hata hivyo, uongozi wa MOI ulitaka kwanza kulipwa kwa deni hilo ndipo ukabidhi jalada hilo kwa hatua zinazofuata, ambapo polisi na familia walianza kurushiana mpira nani anapaswa kulipa.
Polisi walisema hawana fedha za kulipa deni hilo huku familia ikisema jeshi la polisi ndilo linapaswa kulipa kwa kuwa ndugu yao alipelekwa hospitali na polisi, ambao ndio waliosababisha matatizo yote.
Mwanasheria huyo alisema baada ya kutofikiwa kwa muafaka wa nani alipe, ilipofika saa 8:00 mchana, waliondoka na kukubaliana kukutana tena leo ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Jitihada za kuutafuta uongozi wa MOI kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi suala hilo zilishindikana baada ya wahusika kutokuwepo ofisini.

Wednesday, 3 September 2014

Asomewa mashitaka wodini


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, jana ilihamia katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, kwa ajili ya kusomewa mashitaka mtuhumiwa Abdulkarim Thabit Hasia anayedaiwa kufanya uwakala wa kusajili vijana kujiunga na kundi la Al Shabaab.
Hasia ambaye amelazwa katika hospitali hiyo kwa takriban miezi minne, ilikuwa asomewe mashitaka na kuunganishwa na wenzake, Mei mwaka huu lakini ilishindikana kutokana na kutokuwa na fahamu.
Mshitakiwa huyo alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali Augustino Kombe, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mustapher Siyani, akiwa katika wodi Grade One.
Kabla ya kusomewa mashitaka, Hakimu Siyani alimweleza mshitakiwa kwamba anaunganishwa katika kesi inayowakabili watu 11 ambao walishafikishwa mahakamani.
“Nimekuja ili usomewe mashitaka yako, kwani mara ya kwanza nilikuja Mei, mwaka huu, lakini hakuwa na fahamu. Tumeamua kuja leo (jana) kwa kuwa unaelewa kinachozungumzwa na baada ya kusomewa utakuwa chini ya uangalizi wa askari magereza,” alisema Hakimu Siyani.
Pia alimwarifu mshitakiwa kwamba hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Kombe alimsomea  mshitakiwa mashitaka 16 ya ugaidi na kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, kwa kutajwa.
Hata hivyo, waandishi wa habari walikutana na vizingiti vya kuzuiwa kupiga picha na askari aliyekuwepo wodini na kutakiwa wawasiliane na polisi, ambao nao waliwataka kuwasiliana na uongozi wa hospitali.
Waandishi walipowasiliana na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Josian Mlay, naye alirusha mpira kwa wauguzi wa wodini na kudai wao ndio wenye idhini ya kutoa kibali cha mgonjwa kupigwa picha.
Kwa upande wao, wauguzi nao walidai hawana mamlaka bali mwenye ridhaa ni mgonjwa mwenyewe.
Kesi hiyo imeahairishwa hadi Septemba 17, mwaka huu, itakapotajwa tena na washitakiwa wako mahabusu.
Kabla ya mahakama kuhamia hospitalini hapo, washitakiwa wengine katika kesi hiyo, walilalamika mbele ya Hakimu Siyani juu ya ndugu zao kuzuiwa kuingia kufuatilia kesi mahakamani.
Pia walidai mshitakiwa mwezao ambaye yuko hospitalini alikuwa mzima hadi siku anakamatwa na sasa amekatwa mguu kutokana na mateso ya polisi.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Siyani alisema mahakama haijazuia ndugu zao kufika kusikiliza kesi hiyo na kusema tarehe zijazo wafike mahakamani na hakuna haja ya kuzuiwa.
Kuhusu madai ya mwenzao kukatwa mguu, Hakimu Siyani alisema kila mshitakiwa anatakiwa awasilishe malalamiko yake na si kumsemea mwenzake.

Korti yapokea simu 102 kama ushahidi


NA SYLVIA SEBASTIAN
MAHAKAMA ya Wilaya Ilala, imekubali kupokea simu 102, kama kielelezo cha shahidi Koplo Furahin ambaye alitoa ushahidi wa kesi ya wizi wa simu inayowakabili washitakiwa sita.
Pia imeamuru kwamba mwenye mali akabidhiwe simu zake kwa kuwa hazina pingamizi.
Washitakiwa hao katika kesi hiyo ni Idd Pawa, Hamada Mohammed, Haji Waziri, Yusuph Muhangwa, Hashimu Idd, Ally Omary na Mathias Ndunguru.
Washitakiwa hao walipanda kizimbani jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Hassan kwa ajili ya kuendelea na shahidi wa nne upande wa Jamhuri.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Juma Hassan alisema mahakama imeamua kupokea kielezo hicho kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Koplo Furahini alidai alikuchukua maelezo ya washitakiwa wanne na wote walikiri na kurudi mahabusu na Februari 4, mwaka huu, ambapo aliwapeleka kwa mlinzi wa amani katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga.
Shahidi huyo alidai walikamata simu 102 na kila mmoja alikuwa na fungu lake la simu ambapo mshitakiwa Mohammed alikutwa na simu 15, Waziri (simu mbili), Mohangwa simu (10), Matihas (25) na mwingine alikutwa na simu 45, ambaye hayuko kwenye hati ya mashitaka.
Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 9, mwaka huu, kuendelea na shahidi mwingine wa upande wa Jamhuri. Washitakiwa wako nje kwa dhamana.
Washitakiwa hao wanadaiwa Januari 27, mwaka huu,  katika Uwanja wa Ndege wa Kimatiafa wa Julius Nyerere,  Dar es Salaam, waliiba kasha  moja lenye simu 460 aina ya TECNO na Itel kutoka katika ndege ya Qatar iliyokuwa ikitoka China.
Inadaiwa simu hizo zina thamani ya sh. milioni 19.4 mali ya Sued Chemchem.

DAWASCO yawapoza wakazi Kidunda


NA  LATIFA GANZEL, MOROGORO
MAMLAKA ya Maji Safi na Taka Dar es Salaam (DAWASA), imewahakikishia wakazi wa Kidunda, wilayani Morogoro  kwamba inapitia upya  baadhi ya malalamiko juu ya fidia zao  katika mradi wa bwawa la Kidunda na kuyapatia ufumbuzi.
Hayo yalibainishwa jana na Mthamini wa Mali za DAWASA, Mhandisi  John Kwecha, alipzungumza na waandishi wa habari mjini hapa juu ya malalamiko hayo.
Alisema  baada ya kulipa fidia katika eneo la mradi wa bwawa la Kidunda, wamepokea malalamiko  ya wananchi 168 kati ya 1,239  ambao walilipwa fidia  ili kupisha ujenzi wa bwawa litakalosaidia upatikanaji wa maji katika mikoa ya Morogoro, Pwani na  Dar es Salaam.
‘’Tulianzisha dawati maalum kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wakati wa ulipaji fidia hizo ili tuweze kushughulikia. Baadaye   tulipata malalamiko na tutayafanyia kazi kwa kufanya uhakiki upya ili kutenda haki,’’ alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi, alisema uhakiki mali za wakazi hao, ulifanyika kwa kuwashirikisha wataalamu wa ardhi na viongozi wa vijiji kabla ya kuwapatia fomu zinaoonyesha mali zao.
‘’Katika jambo kama hili lazima kunatokea  upungufu, na kwamba suala la kulipa fidia lilianza Julai 23, mwaka huu, hadi sasa limemalizika. Tuache  dawati hilo lipitie kuona malalamiko hayo kama ni sahihi ili haki iweze kutendeka,’’ alisema Amanzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Yona Maki. alisema ulipaji fidia kwa wananchi hao umekamilika kwa asilimia 90  na kwamba bado watu wachache ambao bado hawajakamilishiwa malipo yao kutokana na sababu maalumu, zikiwemo za taratibu za mirathi.
Alisema wananchi 1,218 kati ya 1,239 katika eneo la mradi wamelipwa na kwamba waliobakia ni wananchi 21, huku katika eneo la barabara inayopita katika mradi huo 1,318 wamelipwa bado 46 tu.
Hata hivyo, alisema ili kuwawezesha wananchi hao kuondoka katika eneo hilo la bwawa na kupisha mradi huo baada ya kulipwa fidia zao, halmashauri imetenga viwanja 1,000 kwa ajili ya wananchi hao.
Alisema tayari viwanja 300 vimeshapimwa  katika eneo la Bwira Juu kwa ajili ya wananchi hao na kwamba taratibu za upimaji viwanja vilivyobakia unaendelea.
Pia alisema wanatarajia kuchimba visima vitatu vya maji thamani y ash milioni 350 kuwawezesha wananchi hao kupata huduma ya maji safi.

Afa kwa kuangukiwa na ukuta wa kanisa


NA RACHEL KYALA
M Grace Zephaniah (9), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwenge, wilayani Kinondoni, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa Kanisa la Calvary, lililoko Mlalakuwa, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema kifo hicho kilitokea juzi saa 1.30 usiku. Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi huku upelelezi ukiendelea.
Wakati huo huo, mtu mmoja ambaye hakufahamika jina, alifariki dunia jana saa 6.30 usiku, baada ya kutumbukia katika Bahari ya Hindi, maeneo ya Ferry, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu anakadiriwa kuwa  na umri wa kati ya miaka 40 hadi 45.
Kamanda Kihenya alisema mwili wa mahehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Vijibweni.

NHC yakarabati majengo ya shule


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limetumia sh. milioni 31.5 kukarabati majengo ya utawala na madarasa katika Shule ya Msingi Hassanga, iliyopo Uyole jijini Mbeya.
Hatua hiyo inatokana na ombi la Kamati ya Uongozi wa shule hiyo iliyowasilishwa na Ofisa Elimu wa wilaya kwa uongozi wa NHC mkoa wa Mbeya, mapema mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro,  akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi majengo hayo ambayo ni madarasa manne na jengo moja la utawala, alipongeza hatua ya NHC na kusema ni ya kipekee inayopaswa  kuwa mfano wa kuigwa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na  Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu,  Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, Kaimu Mkurugenzi wa jiji, Dk. Samuel Razalo na viongozi wengine.
“NHC hawalazimiki wala kulazimishwa kusaidia shule hii, lakini waliamua kutoa mamilioni ya shilingi kusaidia kuboresha miundombinu ili watoto wetu wasome kwa raha na amani.Hii ni ishara kuwa NHC inawajali Watanzania na lipo kwa ajili ya kuhudumia taifa,” alisema Kandoro.
Kwa upande wake, Mchechu alisema NHC imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia huduma mbalimbali za kijamii.
Alisema katika jengo la utawala, ukarabati uliofanywa ulihusu ujenzi wa paa na  ujengaji upya wa ukuta.
Alisema majengo hayo sasa yana hadhi ya kisasa na NHC ina imani walimu na wanafunzi wataongeza ufanisi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Neema Sanga, alisema shule ilianzishwa mwaka 1975 na ina wanafunzi 856 kati yao wasichana ni 438 na walimu waliopo kwa sasa ni 26.
“Shule imekuwa na mafanikio mazuri katika taaluma kwani, mwaka 2011 wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa ni 79 na waliofaulu walikuwa ni 64, wakati kwa mwaka 2012, waliofanya mtihani walikuwa ni 123 na waliofaulu walikuwa ni 115,” alisema Neema.

JK: Sera mbaya za ubaguzi chanzo cha ugaidi


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amesema moja ya vyanzo vikubwa vya kuzalisha, kulea na kukuza ugaidi duniani ni sera mbaya za ubaguzi zinazowanyima haki za msingi baadhi ya jamii.
Alisema ni muhimu kwa mataifa mbali mbali duniani kubuni na kutunga sera ambazo zinalenga kutoa nafasi na haki za msingi kwa kila mwanajamii na mwananchi kufurahia sehemu ya keki ya taifa.
Rais Kikwete  alisisitiza kuwa  sera za kichumi na kijamii zina mchango mkubwa katika kukabiliana na kupambana dhidi ya ugaidi na vitendo vya msimamo mkali wenye kutumia nguvu na fujo katika nchi yoyote.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi, wakati alipozungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta mjini Nairobi, Kenya chini ya uenyekiti wa Rais Idrisa Debby wa Chad.
Katika mchango wake kwenye mkutano huo, Rais Kikwete alisema  ni dhahiri kuwa ugaidi ni tishio la kweli  barani Afrika kama ambavyo ripoto ilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambayo ilielezea kwa uwazi  tishio la ugaidi.
“Kwa kuongozwa na ripoti hii, tunatambua sasa kuwa ugaidi ni tatizo gumu sana kwa sababu hakuna nchi duniani isiyoguswa nao na hakuna nchi hata moja duniani yenye uwezo wa kukabiliana nao peke yake. Hivyo ni muhimu kuunganisha juhudi zetu kwenye ngazi zote kitaifa, kikanda, kibara na duniani ili kuweza kukabiliana nao,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kuna maswali mawili muhimu ambayo tunastahili kujiuliza na kuweza kupata majibu mwafaka juu ya kwa nini kuna balaa la ugaidi na jinsi gani tunavyoweza kukabiliana nalo. Katika jitihada zaidi za kukabiliana na tatizo hili ni lazima tutafute kiini hasa cha kujaribu kumaliza ugaidi na vitendo vya msimamo mkali wa kutumia nguvu na fujo. Katika hali hii, sera za kiuchumi na kijamii katika kila nchi zina mchango mkubwa katika mapambano haya.”
Alisema mataifa lazima yabuni na kutunga sera zenye maslahi kwa watu,  ambazo zinalenga kuleta maendeleo na ustawi kwa  wote, sera ambazo hazimbagui yeyote kwa sababu ya kabila lake, dini yake,  ama wilaya ama mkoa atokako.
 “Ni lazima tuwe na sera ambazo kila mwananchi ana haki ya kupata huduma za msingi za kijamii na kichumi na kupata mgawo wao wa haki katika keki ya taifa,” alisisitiza.
Rais Kikwete alisema kuna umuhipi pia kubuni na kutunga sera zinazotoa uhuru na haki za msingi kwa watu wote bila kujali mwelekeo na misimamo yao ya kisiasa.
Hata hivyo alisema wakati mwingine ugaidi unaweza usiwe na mazingira ya kuzaliwa ndani ya nchi kama ilivyotokea kwa ofisi za ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam na Nairobi zilipolipuliwa kwa mabomu.
“Kikundi cha Al-Qaeda kilikuwa na matatizo na Marekani na kikaamua kuzifanya Tanzania na Kenya uwanja wa mapambano,” alisema.

Makame amtolea uvivu Prof. Lipumba


Na Mwandishi Wetu, Pemba
CHAMA cha Allience for Democratic Change (ADC), kimemtaka Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, asiishie kudai kuvunjwa mkono na polisi,  badala yake akiri kuwa alijiunga na chama hicho kwa lengo kutafuta madaraka na njia ya kuingia Ikulu.
Kimesema kuwa Profesa Lipumba ni mfano wa wanasiasa wenye uchu wa madaraka na kwamba, hakuwa na dhamira ya kujiunga na upinzani, bali ilikuwa kuwania urais.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Uenezi na Habari wa ADC, Ali Makame, wakati akizungumza na Uhuru mjini Wete, Mkoa wa Kaskzaini Pemba jana.
Alisema wakati wana mageuzi wakishiriki na kupigania harakati za mabadiliko ya kisiasa na kidemokrasia, kupata harufu na misikosuko, Profesa Lipumba alikuwa nyuma akiwa ni shabiki na mtumishi wa watawala, lakini kwa sasa anasimama na kupotosha umma kuwa yeye ni mwanamapinduzi.
“Matamshi yake kuwa amevunjwa mkono na polisi ni mbinu za kujikweza kisiasa, anasaka umaarufu  na hakuwa miongoni mwa wanasiasa waliotoa jasho la kupigania mfumo wa  vyama vingi mwaka 1992,” alisema Makame.
Alisema ADC kimeshituka kumsikia kiongozi huyo akilalama mbele ya umma kuwa alipata misukosuko ikiwa ni pamoja na kuvunjwa mkono na polisi jambo ambalo alisema ni uzushi mtupu.
“Profesa Lipumba akisema hivyo, Mapalala, Kasela Bantu, Kasanga Tumbo, Shaaban Mloo na Ali Haji Pandu waseme nini? alihoji na kuongeza kuwa kiongozi huyo wa CUF amedandia treni ya mageuzi kwa mbele kwa lengo la kupata umaarufu,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati kundi la wanamageuzi wakipambana na utawala, Profesa Lipumba alikuwa Mshauri wa Uchumi wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Ikulu.
Makame alimtaja Mbunge wa Wawi Hamad Rashid Mohamd ndiye aliyemshawishi kiongozi huyo ili ajiunge na CUF, wakati akifundisha Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam na hakuonekana kuwa na ndoto ya kushiriki siasa nchini.
 “Maalim Seif anapata mshahara wa SMZ, marupupu na uhakika wa mafao yake milele, Lipumba ana uhakika wa kupata mgawo wa ruzuku kila mwezi, kuwazuia wajumbe wa CUF waisiingie kwenye bunge maalum la katiba na kufinya haki zao si sahihi,” alisema Makame aliyejitoa CUF na kuanzisha ADC.

Mkandarasi Muleba akalia kuti kavu


Na Julieth John, Muleba
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, kumsimamisha mkandarasi anayejenga miradi ya maji ya Kyota na Katoke kwa kushindwa kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa.
Mradi huo wa maji ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, wakati alipokuwa akikagua miradi hiyo ambayo ilitakiwa kukamilika  Oktoba, mwaka jana na Mei mwaka huu.
Pia mkandarasi wa miradi hiyo Kampuni ya M/S Sajac Investment ya Dar es Salaam na Dynotech Engineering ya Morogoro, ameshalipwa kiasi cha sh. milioni 837.7 kwa miradi yote miwili kati ya zaidi ya bilioni 1.2.
Awali, Mbunge wa Muleba, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema kukwama kwa miradi hiyo kunatokana na halmashauri kutoa tenda bila kutangaza wala kushindanisha wakandarasi.
Alisema baadhi ya miradi imekuwa ikitolewa kwa kujuana na hiyo ndio sababu ya kutokamilika kwa wakati.
“Mwenyekiti,  mradi huu wa Kyota ulianza kutekelezwa Aprili 25, mwaka 2013 na ulitarajiwa kukamilika Oktoba 27, mwaka huu, lakini mkandarasi ana visingizo kila kukicha na alishaongezewa miezi minane. Ukiwauliza halmashauri hawajui mkandarasi alipo,” alisema.
Alisema madiwani na viongozi wamekuwa wakiwalea wakandarasi wabadhirifu kwa madai kuwa wakiwasimamisha wataishitaki serikali na kuwataka kuwatumia wanasheria wa halmashauri kusimamia jukumu hilo.
“Huyu mkandarasi ndiye aliyepewa mradi wa Katoke wakati mradi wa Kyota haijakamilika hii ni kutuhujumu,” alisema Profesa Anna.
Kaimu Mhandisi wa Maji wa Halmshauri ya Muleba, Injinia Gilbert Isaac, alikiri mkandarasi wa miradi hizo kuchelewa pamoja na kwamba kampuni hiyo ni ya mtu mmoja licha ya majina kuwa tofauti.

MBIO ZA URAIS 2015 Sitta awararua wapinzani wake

  • Awafananisha na wachekeshaji wa mfalme
  • Wasifu wake ukiaminiwa, atajitosa kuwania
  • Atuma salamu yuko imara, hatishiwi nyau
Na Happiness Mtweve, Dodoma 
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ameibuka na kujibu mapigo dhidi ya watu wanaomkejeli na kumtolea lugha za matusi kuwa ni sawa na wachekeshaji wa mfalme.
Amesema yuko imara na kamwe hawezi kutishwa na kauli za watu wasio na maono na kwamba, ataongoza bunge hilo kwa kasi na viwango vile vile.
Akifungua kikao cha Bunge hilo baada ya wajumbe kurejea kutoka kwenye Kamati zilizogawanyika tangu Agosti 8, mwaka huu, Sitta alisema mambo mengi yalikuwa yakiendelea na alikuwa kimya.
Alisema kumekuwepo na matusi, kejeli nyingi na sasa kuna kesi iliyofunguliwa mahakamani dhidi yake na kwamba, kwa mtazamo wake haina uzito wowote.
Sitta, ambaye amekuwa akirushiwa makombora na baadhi ya wanasiasa wenye malengo binafsi, alisema pingamizi za kisheria zilizofunguliwa dhidi ya Bunge hilo hazina nia thabiti na kwamba nyuma yake kuna maslahi binafsi ya kusaka riziki.
“Nawasihi waheshimiwa wajumbe, msifadhaike na maneno ya kejeli tunayotupiwa hapa. Watu wanazungumzia posho na mambo mengine. Niko imara na kwa hulka yangu hizi kejeli na matusi ni kama vile maji katika mgongo wa bata kwani hawezi kulowana. 
“Kwa hiyo waendelee tu, pengine tunaanza kuwabaini na ni fursa nzuri na kuna rafiki yangu mmoja anaitwa Kubenea (Saed-Mhariri wa Kampuni ya Hali Halisi),” alisema Sitta na kuongeza: 
“Matukio yanayojitokeza dhidi yangu ni sawa na simulizi ya kuwepo wachekeshaji wa wafalme huko Ulaya kati ya karne ya 15 na 17.”
“Sasa wafalme wa Ulaya, waliajiri wachekeshaji kwa malengo mawili. Moja ni kumsikia mfalme kwa kila kitu, nyingine ni kuwasema wote ambao mfalme ni wabaya wake. Kwa hiyo kuna watu wa namna hii tunaanza kuwaona,” alisema.
Kuhusu dhana ya wasifu na nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, Sitta alisema mpaka sasa hajatangaza nia, lakini kama watu wataonyesha kuvutiwa na wasifu wake, anaweza kujitosa kuwania nafasi hiyo.
Katika kile kinachoonekana kujibu shutuma za kisiasa kwa kiongozi wa CUF, Juma Haji Duni, kuhusiana na wasifu wake wa kugombea urais, Sitta alisema kiongozi huyo hana uwezo wa kumpima bali wenye uwezo wa kufanya hivyo ni wananchi.
“Nasema wanaochagua ni wananchi. Inawezekana mwakani Watanzania wakatamani mtu mzima aliyetulia na asiyeogopa wapuuzi, wakatamani hilo, mtu makini na mwadilifu. Basi kama itakuwa hivyo, wajue tupo na sisi wengine wa kuweza kufikiriwa katika nafasi hiyo nyeti,” alitamka Sitta na kuamsha shangwe.
Kuhusu utaratibu ulioanza kutumika bungeni jana, alisema wenyeviti wa kamati 12 waliwasilisha mapendekezo yaliyojadiliwa wakati wa kupitia Rasimu ya Katiba huku Kamati ya Uongozi ikipanga kila siku katika siku tano za kupokea taarifa za kamati.
Alifafanua kuwa, watapitia sura zilizoteuliwa ambazo ni Sura namba 2, 3, 4, 5, na kumaliza saa 12 jioni na kwamba, waliona ni vizuri kuwa na ulinganifu wa sura chache badala ya kamati moja kumaliza kusoma sura zote.
Aidha, wenyeviti hao walipewa muda wa dakika 20 kwa kusoma maoni ya walio wengi na dakika 10 kwa maoni ya walio wachache.
Sitta alisema wananchi wengi wameonyesha shauku ya kupeleka maoni yao katika Kamati ya Uongozi kinyume na ilivyokuwa ikitangazwa.
“Makundi mbalimbali ya wananchi waliosoma Rasimu, yamebaini ina mapungufu kama sisi kwenye kamati tulivyoona rasimu ina mapungufu na hili sio jambo la ajabu wala kupuuza kazi iliyofanywa na Tume hapana. Imefanya vizuri na tukumbuke ilipokea maoni kutoka kwa wananchi zaidi ya 334,000 na mabaraza zaidi ya 700, lakini walichokileta ni tafsiri yao kuhusu maoni hayo,”alisema Sitta.
Aliongeza kuwa chombo cha juu cha tume ni bunge hilo, ambalo ndilo lenye wajibu shahiri, kwa sababu baada ya kazi yake, halitarajiwi kutoa rasimu bali litatoa Katiba inayopendekezwa.
Alisema katika kipindi hiki, wameendelea na makundi na kujigamba kuwa yamekuwa msaada mkubwa kwa vile wametoa maoni na mengine yamekubalika katika kuboresha Katiba.

Viongozi CHADEMA watifuana kikaoni

Na Chibura Makorongo, Maswa
MBUNGE wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, ambaye ametoa notisi ya kuachana na chama hicho, amevurumishiana maneno na mbunge mwenzake, Sylvester Kasulumbayi.
Shibuda na Kasulumbayi, ambaye ni mbunge wa Maswa Mashariki kupitia CHADEMA, waliingia katika mzozo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Mvutano huo nusura uvunje kikao hicho, ambapo Mwenyekiti wa Baraza hilo alilazimika kuingilia kati ili kutuliza munkari.
Hali hiyo ilijitokeza juzi wakati Shibuda aliposimama kuchangia hoja mbalimbali, ambapo aligusa kinachoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba na hatua ya kundi la UKAWA kususia bunge.
Pia alisisitiza kauli zake za mara kwa mara kuwa haungi mkono siasa chafu zinazofanywa na UKAWA, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu.
Wakati Shibuda akiendelea kuchangia hoja, Kasulumbayi  alinyoosha mkono na kumtaka Mwenyekiti kumzuia mbunge huyo kuzungumzia masuala ya UKAWA kwa kuwa si mahali pale.
“Mwenyekiti nakuomba umzuie Shibuda aache kuzungumzia masuala ya UKAWA, hapa si mahali pake, ipo sehemu ya kuzungumzia,” alisema mbunge huyo kwa sauti ya ukali.
Hata hivyo, mwenyekiti alimpa nafasi Shibuda kumalizia hoja huku akieleza kuwa, hicho ni kikao cha baraza la madiwani na mbunge ni mjumbe halali, hivyo ana haki kueleza msimamo wake wa kisiasa kwa wananchi waliompigia kura ambao wako Maswa.
Kutokana na kauli hiyo ya mwenyekiti, Kasulumbayi kwa kushirikiana na baadhi ya madiwani wa CHADEMA, walianza kupiga kelele huku wakimtaka Shibuda kutoka wakati madiwani wa CCM wakimshangilia na kupiga kelele huku wakisisitiza kuwa Shibuda amalize muda wake.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ndila Mayeka, Mkuu wa wilaya hiyo, Luteni Mstaafu, Abdalah Kihato na Mkurugenzi Mtendaji, Trasias Kagenzi, walipigwa butwaa.
Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, wabunge hao kila mmoja alimtupia lawama mwenzake kwa kutokuwa na subira.
Shibuda alimtuhumu Kasulumbayi kuwa hana uvumilivu wa kisiasa na ni mwanasiasa aliyekosa maono.
Kwa upande wake, Kasulumbayi alidai kuwa iwapo Shibuda amechoshwa na CHADEMA, anaweza kwenda anakotaka.

Wafanyabiashara wasitisha mgomo


NA WAANDISHI WETU
BIASHARA katika Jiji la Dar es Salaam, zimeanza kurejea kwenye hali yake ya kawaida baada ya juzi baadhi ya wafanyabiashara wa maduka kugoma na kuyafunga, wakipinga matumizi ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD).
Mgomo huo uliodumu kwa saa kadhaa, ulileta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali, hususan maeneo ya Kariakoo.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao walisitisha mgomo huo baada ya kufikiwa kwa maazimio katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa, ambacho kiliamuru maduka hayo kufunguliwa.
Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said  Mecky Sadiki, kiliazimia kufunguliwa kwa maduka hayo na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukutana na wafanyabishara hao ili kumaliza mgogoro huo.
Gazeti hili jana, lilishuhudia idadi kubwa ya maduka yakiwa yamefunguliwa, huku baadhi ya wanunuzi wa bidhaa mbalimbali katika maduka hayo wakiitaka TRA kufanya uhakiki katika maduka  kutokana na kuendelea kupatiwa risiti zisizokuwa za kielektroniki bila ya kupewa maelezo ya msingi.
Mmoja kati ya wanunuzi waliofika katika maduka hayo, Ngole Ramadhani, alisema inashangaza kuona bado utoaji wa risiti zisizokuwa za kielektroniki unaendelea wakati TRA ikiwasisitiza kutopokea risiti hizo kwa kuwa kufanya hivyo ni ukwepaji wa kodi.
Alisema ni vyema kwa wafanyabishara hao kukutana na TRA ili kuondoa tofauti zao na kuiwezesha serikali kukusanya kodi kwa maendeleo ya taifa na kulinda maslahi ya pande zote husika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mgomo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alisema kimsingi wanakubaliana na matumizi ya mashine hizo huku akitoa angalizo kwa TRA kurekebisha baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye mashine hizo.
Aliongeza kuwa mfumo wa EFD kutambua manunuzi pekee bila kuhifadhi kumbukumbu ya matumizi na gharama nyingine za uendeshaji wa biashara ni vyema ukaangaliwa upya, kutokana na kuwasababishia hasara.
Minja alisema kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, wanatarajia kukutana na Kamishna Mkuu wa TRA ili kujadili kuhusiana na malalamiko yao.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema msimamo wa mamlaka hiyo ni kuwataka wafanyabiashara hao kuzingatia taratibu za kisheria na kutumia mashine hizo.
Alisema operesheni ya kukagua na kuhakiki matumizi ya mashine hizo, itaendelea kama kawaida.

Tuesday, 2 September 2014

TUHUMA ZA KIFO CHA MAHABUSU


NA WAANDISHI WETU
JESHI la Polisi limeunda timu kwa ajili ya kuchunguza tukio la askari wake kudaiwa kumshambulia na kusababisha kifo cha mtuhumiwa aliyekuwa mahabusu.
Jopo hilo ambalo majina na viongozi wake hawajawekwa hadharani, limeundwa wakati ndugu wa marehemu wakiweka ngumu kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi, wakitaka uchunguzi wa tume huru.
Mtuhumiwa huyo, Liberatus Damian, anadaiwa kushambuliwa wakati akiwa kwenye mahabusu ya Kituo cha Polisi Stakishari, Dar es Salaam, kabla ya hali yake kuwa mbaya na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Damian, alitiwa mbaroni Agosti 22, mwaka huu, kwa tuhuma za kumjeruhi Juma Magoma, ambaye walikuwa na mgogoro naye baada ya kutofautiana walipokuwa kwenye baa ya Meku Pub.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mke wa marehemu, Naomi Liberatus, alisema taarifa ya madaktari inaonyesha mumewe alishambuliwa na kitu kizito kichwani.
Hata hivyo, Naomi alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, Materu alifikishwa katika Hospitali ya Amana akiwa hajitambui huku akiwa uchi, ambapo askari waliomfikisha walidai ni kibaka na wamemuokota hivyo kuomba apatiwe matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Damian kabla ya kupelekwa Muhimbili, alikuwa na majeraha yaliyosababishwa na kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira baada ya kumshambulia Magoma kwa mapanga.
Kamanda Kova alisema aliona ni vema ukafanyika uchunguzi wa kina kwa lengo la kuondoa utata wa tukio hilo ili kupata taarifa kamili kuhusiana na ugomvi uliosababisha Damian na Magoma kushambuliana mara kwa mara kila wanapokutana.
Alisema lengo linguine la kuundwa kamati hiyo ni kuchunguza jinsi Damian alivyokamatwa, alivyokaa mahabusu na hadi alivyopelekwa MNH, ambapo watahusisha madaktari bingwa wanaohusika na uchunguzi wa watu waliokufa katika mazingira yenye utata.
“Endapo itagundulika kwamba kuna mkono wa mtu katika kifo cha Damian, polisi haitasita kuchukua hatua ili sheria ichukue mkondo wake.
Kama kuna mtu yeyote anazo taarifa za ziada kuhusiana na shauri hili, aziwasilishe kwa mkuu wa upelelezi ambaye ndiye kiongozi wa jopo hilo,” alisema.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari, Naomi alisema baada ya Damian kukamatwa, siku iliyofuata walianza harakati za kufuatilia dhamana ambapo, waliambiwa wasubiri kuangalia hali ya afya ya Magoma.
Alisema Agosti 29, mwaka huu, akiwa katika harakati za kufuatilia barua za dhamana, alipigiwa simu ya kumtaka asiende tena kituoni bali awahi Amana kwa sababu mumewe alipelekwa kwa ajili ya matibabu.
“Nikiwa katika hali ya mshangao baada ya kuambiwa kuwa mume wangu anaumwa na ana hali mbaya wakati jana yake nilikwenda kituoni na nikaongea naye na hakuwa na jeraha au hali yoyote ya kuonyesha kuwa ni mgonjwa.
“Nilimpigia simu shemeji yake ambaye anamiliki gereje iliyoko Amana, ambapo alifika kabla ya gari la polisi lililompakia halijafika, lakini hakuweza kumuona.
“Baada ya muda aliona gari la polisi likiwa limempakia marehemu mume wangu, ambaye alikuwa amevimba uso na macho yakiwa yamevilia damu na majeraha mikononi huku akiwa uchi ndipo, akanieleza kinachoendelea,” alisema Naomi.
Mke huyo wa marehemu aliongeza kuwa baada ya askari kumfikisha hospitalini hapo, walidai ni kibaka na alikuwa amepigwa na wananchi wenye hasira, ndipo baadhi ya ndugu walipokuja juu na kuwaeleza ukweli madaktari kuwa ndugu yao si kibaka bali ni mahabusu.
Alisema baada ya hapo madaktari walishauri akimbizwe Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, ambapo baada ya kufika huko alifanyiwa kipimo cha CT Scan ya kifua na kugundulika kuwa alikuwa amepigwa na kitu kizito upande wa kushoto na damu nyingi zilikuwa zinavuja na kuchanganyika na ubongo.
Mke huyo wa marehemu alisema baada ya taarifa hiyo, waliambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa haraka, ndipo walipoanza kuchangishana na Ijumaa usiku alifanyiwa upasuaji huku akiwa chini ya ulinzi.
Alisema siku iliyofuata walipeleka taarifa kituo cha Sitakishari kuhusu hali ya ndugu yao na kuwaomba wafike hospitali kwa ajili ya kufuatilia matibabu yake.
Kutokana na mazingira ya kifo hicho, msemaji wa familia hiyo, Jimy Sanga, alisema leo mwili wa Damian unatarajia kufanyiwa uchunguzi ili kubaini sababu za kifo chake na hawatauzika hadi watakapoelezwa sababu za ndugu yao kushambuliwa hadi kufa huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi.