Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Tuesday, 23 September 2014

Chenge kuwasilisha Katiba Pendekezi Bungeni leo

Na mwandishi wetu, Dodoma
Andrew Chenge
WAKATI wajumbe wa kundi la Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakiendelea kususa, Bunge Maalumu la Katiba leo linaingia kwenye hatua muhimu pale Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge, atakapowasilisha Katiba Pendekezi.
Chenge, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, anatarajiwa kuwasilisha Katiba Pendekezi kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, baada ya kukamilisha kazi hiyo.
Mara baada ya kuwasilishwa, wajumbe wa Kamati zote 12, watapata fursa ya kuijadili Katiba Pendekezi ili kuwezesha kufanyiwa marekebisho kwenye maeneo, ambayo yataonekana kuwa na upungufu kabla ya  kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.

“Ikirudi kwenye kamati ya uandishi, itaandikwa upya, ikijumuisha hoja mbalimbali, ambazo awali zilikuwa zimeachwa au kufanyiwa marekebisho.
“Kazi hiyo itafanywa kwa siku mbili, kuanzia Septemba 27 hadi 28, mwaka huu,” alisema Sitta alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana.
Alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu, wajumbe wataanza kupiga kura, wakiwemo wale walioko nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
Juzi, Bunge liliridhia na kupitisha Azimio la kufanya marekebisho ya kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, ili kuwaruhusu wajumbe walioko nje ya Bunge, ikiwemo wale walioko nje ya nchi kupiga kura.
JUKWAA LA KATIBA
Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), limesema lina wasiwasi na utaratibu wa kupiga kura kwa wajumbe wa bunge maalumu la katiba watakaokuwa nje ya bunge na nje ya nchi, uliowekwa baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kanuni.
Kanuni zilizofanyiwa marekebisho na bunge hilo linalotarajiwa kuhitimisha kazi yake, ni tatu ambazo lengo kuu lilikuwa ni kurahisisha zoezi la upigaji kura ndani ya bunge hilo, litakaloanza Septemba 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba, hatua hiyo inatakiwa kuangaliwa kwa makini ili kuondoa dhana ya baadhi ya watu kuwa ni moja ya njia za kuchakachua mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Ilisema baadhi ya mambo ya kuyaangalia kwa undani ni pamoja na gharama za kuendesha mfumo huo, unaotegemewa kufuatwa kutokana na marekebisho ya kanuni namba 30, 36 na 38 za bunge hilo maalumu la katiba.
Aidha, taarifa hiyo ilishauri kutafutwe njia mbadala ya kutafuta theluthi mbili ya wajumbe wa bunge hilo maalumu la katiba, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wajumbe wanaoruhusiwa kupiga kura watakuwa wale tu walioko ndani ya bunge hilo katika tarehe husika ya zoezi hilo.

CCM yahofu uchaguzi mkuu 2015 kuvurugika

Na Suleiman Jongo, Chalinze
Nape Nnauye
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuna uwekezano wa Uchaguzi Mkuu wa mwakani kuvurugika kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kulazimisha matumizi ya mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR).
Kimesema mfumo huo utaigharimu serikali mabilioni ya shilingi na kwamba, unaweza usitoe mafanikio yenye tija kama inavyotarajiwa kwa kuwa tayari umetoa matokeo mabaya kwenye baadhi ya nchi zilizoanza kuutumia.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana kuwa mfumo huo unaweza kuleta matatizo makubwa katika uchaguzi, lakini NEC imekuwa ikishinikiza kutumika kwa lengo la kutengeneza ulaji.
Kiasi cha sh. bilioni 290 kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kufungwa kwa miundombinu ya kuwezesha mfumo huo kutumika na kwamba, umegubikwa na usiri mkubwa nyuma yake.

“Huu mfumo una siri kubwa nyuma yake.Mbali na hofu ya kuvuruga uchaguzi, lakini ni matumizi mabaya ya fedha za umma zinazotaka kutafunwa na wajanja wachache kwa maslahi yao binafsi,” alisema Nape.
NEC imetangaza kuanza kutumika kwa mfumo huo wa BVR katika uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kuandikisha upya daftari la wapigakura.
Nape alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Chalinze mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Alisema mfumo huo unazua maswali mengi yasiyo na majibu huku baya zaidi ikiwa ni historia ya BVR katika nchi mbalimbali, zikiwemo za Malawi na Kenya ambazo zililazimika kuacha kuutumia licha ya kutumia fedha nyingi.

“Nchi zote zilizotumia mfumo huo ziliingia kwenye matatizo. Mfano mzuri ni Kenya, ambao walilazimika kuuacha hatua za mwisho huku mabilioni ya fedha yakiwa yameingia mifukoni mwa wajanja.
“BVR itazusha maswali mengi katika uchaguzi mkuu mwakani. Uchaguzi ukivurugika, lawama zitakuja kwa CCM kwamba tulikuwa tunataka kuchakachua matokeo. Hatukubaliani na hilo na hatuko tayari kuona likitokea,” alisema Nape.
Mbali na kuvuruga uchaguzi, Nape alisema mfumo huo pia utaigharimu nchi mabilioni ya fedha za umma zinazoweza kutumika kuhudumia sekta zingine za kijamii ili kuwaletea Watanzania maendeleo.

“Inaonekana wajanja wachache wanataka kuitumia NEC kutengeneza mazingira ya ulaji wa fedha za umma. Sidhani kama nia yao ni kuboresha mfumo wa kupiga kura bali kuvuruga kama ilivyotokea kwenye nchi zingine,” aliongeza.
Nape alisema badala ya NEC kutumia mabilioni hayo, ilipaswa kukaa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kutumia taarifa zake kuboresha daftari la kupigia kura.
Kwa mujibu wa Nape, NEC ikishirikiana na NIDA watapunguza gharama hizo kwa kuwa katika zama hizi za sayansi na teknolojia, NEC itapata kila wanachokitaka kupitia NIDA, zikiwemo taarifa za wapiga kura.
Aliitaka NEC kujifunza kwenye nchi zingine zilizotumia mfumo huo na kushindwa kusaidia uchaguzi, badala yake kuibua vurugu.

“NEC iwe na huruma na fedha za Watanzania kwani kwa teknolojia ya sasa, nchi nyingi zinatumia kadi moja kupata taarifa mbalimbali, ikiwemo upigaji kura,” alisema.

Arusha kupandisha kiwango cha ufaulu

NA LILIAN JOEL ARUSHA
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha kupitia mpango wa matokeo makubwa (BRN), inatarajia kupandisha kiwango cha ufaulu kwa mwaka 2014, hadi kufikia asilimia 92  kwa elimu ya msingi.
Takwimu zinaonyesha katika matokeo ya mwaka jana, ufaulu ulikuwa asilimia 85.
Hayo yalisemwa juzi na Ofisa ElimuTaaluma wa Shule za Msingi katika halmashauri ya Jiji hilo, Mbwana Juma, alipokuwa akizungumza wakati wa mafunzo ya  mbinu za kufundisha masomo ya hisabati na sayansi.
Alisema  kupitia BRN wanatarajia ufaulu mwaka huu kupanda
hadi kufikia asilimia 92,

“Elimu hii tunatoa kwa walimu wa shule za serikali ambapo kwakushirikiana na Chama cha Walimu Tanzania(CWT), tunawapa walimu mbinuza kufundisha, ili tuongeze ufaulu zaidi kwani tunatoa elimu ya mazingira pia, ” alisema.
Awali Katibu wa CWT  Jiji la Arusha, Magreth Hovokela, alisema
mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa walimu 92 kutoka katika shule zote
46 za Msingi zilizopo jijini hapa, yalianza kutolewa tangu mwaka 2000.
Hivi sasa mpango huo umeendelea katika mikoa ya Kilimanjaro na Manyara. Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Shirika la Helvetos, la Uswis.
Aliiomba serikali  isaidie ili mradi huo ufike katika mikoa yote nchini katika kuhakikisha watoto wanaokuwa na nafasi sawa.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Zulina
Rajabu, alisema  mafunzo hayo yamewasaidia kujifunza namna ya
kushirikisha wanafunzi wakati wa ufundishaji.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Mwalimu Roselyn Mosha, kutoka Shule ya Msingi Sinoni, alisema kuwa mafunzo hayo yanawasaidia kuboresha namna ya ufundishaji na kuiomba serikali kuboresha zaidi sekta ya  elimu.

‘Serikali isambaze teknolojia ya usindikaji mazao’

Na Nathaniel Limu, Manyoni
SERIKALI imetakiwa  kushirikiana na wadau katika kusambaza teknolojia ya usindikaji wa mazao ya kilimo kwa wananchi na kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa na zana za kisasa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,  Andreas Whero, aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano  kwa wajasiriamali juu ya  teknolojia ya usindikaji mazao ya matunda, vinywaji na vyakula.
 Whero alisema  wakati huu ambapo kuna changamoto kubwa ya uzalishaji wa bidhaa zinazohimili ushindani kitaifa na kimataifa,  kuna haja kubwa ya wakulima  na wajasiriamali kufikiwa na teknoloji ya usindikaji wa vyakula.
 Alisema lengo ni kuhakikisha  bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima mashambani, zinaongezwa thamani kwa kusindikwa na kufungashwa vizuri, ili zisiharibike.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema kuna changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi na serikali.
Changamoto hizo walizitaja kuwa ni ukosefu wa zana na vifaa kwa ajili ya usindikaji vijiji, ukosefu wa nishati ya umeme na dawa ya kuzuia mazao kuoza.
Walisema bidhaa za vyakula, vinywaji na matunda, zinazosindikwa kwa teknolojia   ya kisasa, zinaweza kudumu kwa zaidi ya miezi sita bila kuharibika wala kupoteza ubora wake.
Mafunzo hayo  yaliandaliwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na VETA kanda ya kati.

MUCCoBS chapandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu

 Na Rodrick Makundi, Moshi
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imekipandisha hadhi Chuo Kikuu kishiriki cha Ushirika Moshi (MUCCoBS) cha mkoani Kilimanjaro, kuwa Chuo Kikuu rasmi.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Philemon Luhanjo, alitangaza hatua hiyo juzi mjini hapa, mbele ya viongozi wa serikali mkoa wa Kilimanjaro, uongozi na watumishi wa MUCCoBS.
Baada ya kupandishwa hadhi chuo hicho, sasa kitaitwa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, kikiwa chini ya baraza la mpito linaloongozwa na Mwenyekiti, Profesa Gerald Monela, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa SUA.
Akitangaza mabadiliko hayo, Luhanjo,ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, alisema chuo hicho kimepandishwa hadhi kuanzia Julai 3, mwaka huu, baada ya  kufanyiwa tathmini  na vyombo vya usimamizi wa taasisi za elimu ya juu nchini, ikiwemo tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kwa mujibu wa Luhanjo, mabadiliko hayo pia yameambatana na uteuzi uliofanywa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa wa viongozi wa muda na vyombo vya uamuzi kwa kipindi cha mpito.
Mbali ya Profesa Monela kuwa mwenyekiti wa baraza, pia iliyokuwa bodi ya uongozi ya MUCCoBS na kamati zake, zimekuwa baraza la mpito mpaka litakapoundwa baraza kamili.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa mkuu wa chuo cha MUCCoBS, Profesa Faustine Bee, ameteuliwa kuwa kaimu makamu mkuu wa chuo, akisaidiwa na Basil Liheta, anayekuwa Kaimu Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) na Ndayizera Manta, anayekuwa Kaimu Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo (Utawala).

Serikali yapania kutokomeza utapiamlo

NA SOPHIA ASHERY
SERIKALI imesema itaweka mikakati kuhakikisha inatokomeza utapiamlo nchini na kutoa elimu ya lishe kuanzia ngazi za awali katika jamii.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, wakati akifungua warsha ya siku tatu kujadili mikakati ya kutoa elimu juu ya lishe bora.
Pallangyo alisema Tanzania inayo idadi kubwa ya watoto na wanawake wajawazito, ambao wana utampiamlo unaosababishwa na kukosekana kwa lishe bora, hali ambayo inasababisha watoto kuzaliwa na uzito mdogo, kudumaa, kuwa na upungufu wa damu, madini na vitamini.

Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania imeamua kulivalia njuga suala la lishe na kuhakikisha  inaweka mikakati mizito, ambayo itaboresha hali ya lishe kwa watoto na kutokomeza utapiamlo.
 

“Wananchi wengi hawana elimu juu ya umuhimu wa lishe bora na kama elimu itatolewa, basi kuna uwezekano mkubwa wa idadi ya watoto na wajawazito wenye utapiamlo ikapungua,” alisema Pallangyo.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano, wamedumaa wakati asilimia 16 walipoteza maisha na asilimia 21 ya watoto walizaliwa wakiwa na uzito wa chini.
Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania imejiwekea mikakati ya kutomomeza utapiamlo kwa kushirikiana na wadau wengine na imekuwa nchi ya kwanza kutia saini mpango wa uanachama wa lishe bora uliotiwa saini na  Rais Jakaya Kikwete mwaka 2011.
Alisema pia Mei 2013, serikali  ilizindua kampeni ya kitaifa kwa ajili ya utekelezaji wa lishe ya kisasa, kampeni ambayo inalenga kuhakikisha jamii inazingatia ulaji wa vyakula vyenye lishe bora.
Naye mshauri wa masuala ya lishe kutoka Ujerumani, Maria Pizzini, alisema warsha hiyo itawawezesha kubadilishana mawazo na kupanga mikakati ya kutokomeza utapiamlo.
Maria alisema huu ni wakati wa kila nchi kuhakikisha inasimamia suala la lishe bora, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu.
Warsha hiyo inashirikisha washiriki kutoka nchi tisa za Afrika, ambazo ni Kenya, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Uganda, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania, pamoja na nchi mwanachama wa mpango wa lishe, ambazo ni Marekani, Uingereza, Uswisi na Bangladesh.

TAWOMA waomba kupatiwa mafunzo

NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Eunice Negele, amesema wanakabiliwa na changamoto  ya elimu ya uchimbaji, biashara na madini.
Hayo aliyasema jana mjini Dar es Salaam, wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho, unaofanyika kwa siku mbili kuanzia jana, uliofunguliwa na Kamishna Msaidizi wa Madini, Hamisi Komba, kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

“Lengo la chama chetu ni kuwaunganisha wanawake wachimbaji pamoja na kusaidiana kutoka mahali walipo na kuwaweka sehemu itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Lakini tunakabiliwa na changamoto ya elimu ya uchimbaji, biashara, madini na ufahamu wa thamani na ubora wake ili tufanye biashara kwa ufanisi na kuongeza kipato,” alisema Eunice.
Eunice aliishukuru serikali kwa jitihada wanazozifanya kuwapatia ruzuku ya Dola za Marekani 50,000 na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kuwapatia mikopo kwa mtu aliyetimiza masharti.
Hata hivyo, alisema wanahitaji mafunzo ya usanifu wa madini, ambayo yatawawezesha kuyatengeneza na kuyaboresha.
Awali, akifungua mkutano huo, Kamishna Msaidizi, Komba alisema serikali imekuwa ikiwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa na uongezaji thamani.
Alisema imeendelea kuwasiliana na wachimbaji hao na kutoa bei elekezi za madini mbalimbali .
Mkutano huo unatarajiwa kufungwa leo na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi.

Saturday, 20 September 2014

ZIARA YA KINANA MKOANI PWANI

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akikaribishwa wilayani Kisarawe, kuendelea na ziara yake mkoani Pwani ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza kero za wananchi na kushauriana nao jinsi ya kuzitatua.

WANANCHI wakishangilia baada ya Kinana kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Palaka, Kisarawe.

KINANA akiwa amembeba kijana Chipukizi, Suma Iddi. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao na kushoto ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akihutubia wananchi katika Kijiji cha Maneromango,Kisarawe.

KINANA akipanda mti wa kumbukumbu katika eneo la ofisi za CCM Wilaya ya Kibaha

Thursday, 18 September 2014

Mbowe aufyata



  • Ajisalimisha Polisi kuhojiwa, Tundu Lissu amzuia
  • Wanavyuo wamvaa , Bunge kama kawaida 
  • Changoja acharuka, maandamano ni marufuku
  • LHRC yachoshwa, yakemea kauli za uchochezi

Na waandishi wetu
JESHI la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini, ikiwa ni pamoja na kuonya kuwa hakuna mtu atakayeingia barabarani kuandamana atayevumiliwa.

Habari za kuaminika zinasema kuwa, wafuasi na viongozi wa CHADEMA katika mikoa mbalimbali, wamejipanga kufanya maandamano leo, ikiwa ni maagizo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe ametii amri ya Jeshi la Polisi baada kutakiwa kufika Makao Makuu kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na kauli zake za uchochezi zinazolenga kuvuruga amani ya nchi.
Hata hivyo, Mbowe anajisalimisha polisi leo baada ya kutakiwa na Kamati Kuu ya CHADEMA kuitikia wito huo, baada ya awali Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, kumzuia kwa kuhofia nguvu ya dola kutokana na kauli alizotoa.
Jana, Lissu alikiri mbele ya waandishi wa habari kuwa, alimzuia Mbowe kujisalimisha polisi, wakati ambao tayari kiongozi huyo na chama chake wameshapokea barua ya wito kutoka jeshi hilo.
Mbowe atasindikizwa na baadhi ya viongozi na wanasheria wa CHADEMA, akiwemo, Lissu, Halima Mdee, Mabere Marando, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari.

Polisi yacharuka
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, alisema wana taarifa za uhakika kuwa CHADEMA wamepanga kufanya maandamano leo.
Alionya polisi hawatasita kuchukua hatua kali na kwa mujibu wa sheria kwa yeyote ambaye atajaribu kuvunja sheria.
Kamishna Chagonja, alitoa msimamo huo ikiwa ni mara ya pili jana, alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo alionya kuwa kauli za Mbowe haziwezi kuachwa zikapita kama upepo.
“Tumeanza kupokea maombi ya CHADEMA kikitaka kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kifupi ni kinyume cha sheria na hayaruhusiwi,” alisema Chagonja.
Alisema maandamano hayo ni batili kwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, lipo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hakuna sheria iliyokiukwa.
“Kitendo cha kufanya maandamano kushinikiza kuvunjwa kwa bunge hilo ni kinyume cha sheria, jambo ambalo hatutalivumilia hata kidogo,” alisema na kuongeza: “Jeshi la Polisi lina jukumu la kulinda watu wote.”
Pia alisema kuna kesi inayoendelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, inayohoji uhalali wa bunge hilo, ambayo haijafika mwisho na kutolewa uamuzi, hivyo maandamano hayo ya CHADEMA ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Haki za Binadamu wachoshwa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimewaonya wanasiasa kuacha mara moja kutoa kauli za kupotosha jamii na zenye kebehi kwa kuwa hazijengi.
Kimewataka kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi katika Bunge Maalumu la Katiba na kwamba, mchakato huo unavurugwa na wachache wasio na mapenzi mema kwa taifa.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio, aliyasema hayo mjini Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.  Hellen Kijo Bisimba.
“Tunawataka wanasiasa kuacha kutoa kauli za kupotosha jamii, kwa kuwa hazitajenga bali ni kuwavuruga wananchi,” alisema.
Pamoja na tamko hilo, Urio alisema bunge hilo linahitaji kura 16 kutoka Zanzibar ili kutimiza namba ya theluthi mbili ya wajumbe ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa.
Alisema kwa sasa akidi haiwezi kutimia kutokana na masharti ya kifungu namba 26 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambacho kinataja akidi kuwa ni theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema Rais Jakaya Kikwete kwa nafasi yake kikatiba, ana nguvu ya kuteua wajumbe wengine wa bunge hilo, hivyo ni vyema akatumia nafasi hiyo ili kutafuta mwelekeo mpya.

Wanachuo wamvaa Mbowe
WANAFUNZI wa Vyuo vya Elimu ya Juu, wamepinga na kulaani vikali kauli ya Mbowe kuhamasisha vurugu na migomo isiyo na tija nchini.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Dar es Salaam, Musa Omar, alisema jana kuwa, kauli ya Mbowe haina nia njema kwa Watanzania na ni lazima hatua zichukuliwe, vinginevyo taifa litaangamia.
Alisema wamechukizwa na kauli hiyo ya kibabe kwa kuwa inaweza kusababisha machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Tunalaani vikali kauli ya Mbowe kutaka nchi kuingia kwenye machafuko kwa kuitisha maandamano na migomo nchi nzima…ni kauli ya kihuni na haipaswi kuachwa ipite hivi hivi,” alisema.

CHADEMA DOM WAZIMWA
Polisi mkoani Dodoma imepiga marufuku maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika leo kuanzia viwanja vya Nyerere Square na kuishia Ofisi za Bunge.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula, alisema maandamano hayo ni batili na kuonya atayethubutu kuingia barabarani atakutana na sheria.
 “Chama hicho kimejipanga kufanya maandamano hayo katika wilaya zote za mkoa wetu, hii ni kinyume cha sheria na tunaonya wasijaribu na tumekataa,” alisema.
Alisema walipokea barua kutoka Ofisi ya CHADEMA kuomba kibali cha maandamano, ambayo yatadumu kwa saa mbili, lakini Polisi imeyapiga marufuku na kutangaza kuwa ulinzi zaidi utaimarishwa kukabiliana na yeyote.
Imeandikwa na Mariam Mziwanda, Furaha Omary, Mariam Zahoro na Happiness Mtweve, Dodoma.

Wanafunzi wadungwa sindano kuzuia mimba


NA MWANDISHI WETU
WAKATI taifa likihaha kusaka tiba ya mimba za utotoni ili kuwezesha watoto wa kike kupata elimu, baadhi ya wauguzi wilayani Newala, Mtwara, wameibuka na mbinu mpya.
Wauguzi hao wanadaiwa kuwachoma sindano za uzazi wa mpango wanafunzi wa shule za msingi, kinyume cha utaratibu kwa lengo la kuwakinga na mimba zisizotarajiwa.
Hayo yamebainika kupitia taarifa ya Matokeo ya Ripoti ya Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA). 
TAMWA iliendesha utafiti maalumu kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia katika wilaya 10 nchini, kuanzia mwezi Mei, mwaka huu. 
Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa baadhi wasichana walishindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya ujauzito, jambo ambalo kwa sasa wenyeji wa Newala wamesema limekuwa historia.
Hatua hiyo inatokana na matumizi ya sindano za uzazi wa mpango,  mkakati ambao umekuwa ukiendeshwa kwenye baadhi ya shule wilayani humo.
“Baada ya kuona wasichana wengi wanaishia darasa la tano kwa kupata ujauzito, sasa wanachomwa sindano za uzazi wa mpango na huo ni ushauri wa wazazi ama wanaume wenye mahusiano nao,” alisema mkazi mmoja wa kijiji cha Luchungu wilayani Newala.
Ofisa mmoja wa afya (jina linahifadhiwa) wa Zahanati ya Makote, wilayani humo, alithibitisha jambo hilo na kusema kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto kupatiwa huduma kuwezesha kuhitimu elimu ya msingi.
Akizindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa TAMWA, Rose Reuben, alisema ripoti imebainisha kupungua kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia nchini, ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na  mwamko wa wanawake.
Alisema wanawake wengi wamekuwa wakipatiwa elimu ya masuala kupitia vyombo vya habari nchini, hivyo kupungua kwa matukio hayo.
“Kabla ya kuanza utafiti huu mwaka 2011, takwimu za idadi ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyoripotiwa, hazikuwa sahihi kama ambavyo matokeo ya utafiti yanavyoonyesha,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi wa TAMWA, Gladness Munuo, alisema takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi nchini, isipokuwa wilayani Ilala, Dar es Salaam, ambapo mwaka jana yalikuwa 124 na mwaka huu yameongezeka hadi 310.
“Katika wilaya ya Ilala, matukio ya kubakwa ndio yameonyesha kushika kasi zaidi kuliko aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa watoto watano hulawitiwa kila siku,” alisema.
Akizungumzia madhara ya dawa za uzazi wa mpango, Dk. Magreth Mathew wa Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, alisema watu wengi wanapotumia, hujiona wapo huru na salama, hivyo kuruhusu wengine kufanya ngono zembe.
Alisema dawa hizo zinapoingia kwenye mwili wa binadamu, mpangilio wa homoni huvurugika hadi muda wake unapokwisha, ndipo mwili hurejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Dawa hizo zina madhara yake, kwani wengine hawawezi kupata ujauzito katika hali ya kawaida hadi wapatiwe matibabu. Hii inatokana na miili kutofautiana homoni, ingawa kwa wengine hurejea baada ya dawa kwisha nguvu,” alisema.
Madhara mengine ni mtumiaji kuumwa kichwa, tumbo, kupata hedhi kwa wingi bila mpangilio maalum ama wakati mwingine kutopata hedhi kabisa.

Askari polisi watupiwa bomu Songea


NA MWANDISHI WETU
ASKARI watatu  wa polisi mkoani Ruvuma wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa huo mjini Songea, baada ya kushambuliwa  na kitu kinachosadikiwa kuwa bomu la kurushwa kwa mkono.
Tukio hilo lilitokea juzi, jioni katika kata ya Msufini, karibu na daraja la Matarawe, wilayani Songea, mkoani Ruvuma,  ambapo watu watatu wasiofahamika walitupa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kurushwa kwa mkono.
Askari hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakiwa kwenye doria katika eneo hilo ni WP. 10399 PC Felista aliyejeruhiwa mguu wa kulia  kwenye unyayo na pajani na G.7351 PC Ramadhani aliyejeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni .
Mwingine ni  G. 5515 PC John aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma,  Dk. Daniel Malekela, alithibitisha kuwapokea askari hao na kueleza walitoa  vipande vya bati na misumari katika majeraha yao.
Kutokana na tukio hilo, polisi mkoani Ruvuma wameanza uchunguzi  wa kina ili kuwakamata wahusika.
Akizungumzia tukio hilo,  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu,  alisema amesikitishwa na kitendo hicho cha wahalifu kujeruhi askari, tena kwa makusudi.
Alisema serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama, itahakikisha wanawasaka na kuwakamata wahusika na hatua zitachukuliwa. Aliowamba wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi.

Silima: Ajali ni janga la taifa


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema kwa sasa inawekeza zaidi katika mapambano dhidi ya ajali za barabrani kutokana na idadi kubwa ya Watanzania kupoteza maisha.
Imesema kwa sasa ajali zimekuwa janga la taifa kuliko hata ugonjwa wa Ukimwi, hivyo jitihada za haraka zinahitajika katika kudhibiti.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima, aliyasema hayo  jana  alipokuwa akipokea hundi ya  sh. milioni 40 kutoka kwa Kampuni ya Puma, kwa ajili ya Maadhimisho ya Wiki ya Nenda  Usalama Barabarani.
Hata hivyo, alisema kuwa wimbi la ajali hizo haimaanishi kwamba, serikali na Jeshi la Polisi zimelala, bali mikakati madhubuti inaendelea kuchukuliwa ili kukomesha kabisa.
Pia alisema kuanzia sasa utoaji wa leseni kwa madereva wa mabasi yote ya mikoani utazingatia mafunzo ya kutosha kwa wahusika wote.
Alitumia fursa hiyo kuwataka madereva kuwa makini na kuwa uzembe na uamuzi usio makini barabarani, ikiwemo ulevi, mwisho wake ni mbaya na kuwa sheria itachukua mkondo wake.

Mawakili waomba kesi ya ugaidi ifutwe


NA MWANDISHI WETU
MAWAKILI wanaowatetea viongozi wa Jumuia ya Uamsho Zanzibar wameiomba mahakama kuiondoa hati ya mashitaka ya ugaidi dhidi  ya wateja wao.
Sheikh FArid Hadi Ahmed na wenzake,  wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama, kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi,  kukubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili washiriki vitendo.
Ombi hilo liliwasilishwa jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako ulinzi uliimarishwa kwa kuwepo askari wengi wakiwemo askari kanzu na mbwa wanne.
Wakili wa utetezi, Rajabu Abdallah kwa niaba ya jopo hilo, aliwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka kudai upelelezi haujakamilika.
Abdallah aliomba kuondolewa kwa hati hiyo, kutokana na kuwa na shaka kwamba mahakama hiyo si mahali sahihi pa kufunguliwa kesi hiyo.
“Nimeipitia hati ya mashitaka na nimeona shaka kuhusu kutuhumiwa kufanya makosa katika sehemu mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Kwa mujibu wa kifungu cha 244 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinatamka hatua za awali zitafanyika katika mahakama ya chini yenye mamlaka. Hati ya mashitaka haijaeleza eneo husika ambalo watuhumiwa wanadaiwa kufanya makosa,” alidai wakili huyo.
Alidai wanapata shaka iwapo mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa ilikuwa vyema iwapo hati hiyo ingekuwa imetaja eneo husika.
Aliomba hati hiyo iondelewe mahakamani hapo kwa sababu hati ya mashitaka imeshindwa kueleza sehemu husika.
Wakili Kweka alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani husikilizwa na Mahakama Kuu na kwamba hati imeletwa hapo kwa ajili ya washitakiwa kusomewa mashitaka, kuamriwa kwenda mahabusu, kuelezwa hatua ya upelelezi na kusomewa maelezo ya mashahidi upelelezi ukikamilika.
Alidai hati hiyo ipo sahihi mahakamani hapo na suala la kudai haipo sahihi linahitaji ushahidi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Hellen alisema atatoa uamuzi kuhusu maombi hayo Oktoba Mosi, mwaka huu. 
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sheikh Mselem Ali Mselem, Abdallah Said Ali au Madawa, Nassoro Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassani au Jibaba, Hussein Ally, Juma Sadala na Said Ally.
Pia wamo Hamis Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange au Mapala, Amir Juma, Kassim Nassoro, Salehe Juma na Jamal Noordin Swalehe.
hivyo. Wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Juni, 2013 na Julai, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Farid na Mselem wanadaiwa katika kipindi hicho huku akijua waliwaajiri Sadick na Farah ili kushiriki katika vitendo vya kigaidi.
Shitaka la nne linamkabili Sheikh Farid ambaye anadaiwa katika kipindi hicho aliwahifadhi watu hao, huku akijua kabisa kuwa walitenda vitendo hivyo. Mawakili wengine wanaowatetea washitakiwa hao ni Abubakar Salim, Ubaid Ahmed na Abdulfatar.

Wednesday, 17 September 2014

ZIARA YA KINANA MKOANI PWANI

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakiwa kwenye mtumbi, wakielekea Pwani ya Mafia baada ya kushuka kwenye boti wakati msafara wao ulipowasili wilayani humo. Katikati anayepunga mkono ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Mwishehe Mlao.

KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akihutubia wakazi wa Mafia kwenye uwanja wa Mkunguni uliopo stendi ya mabasi mjini Mafia.

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akifurahia jambo pamoja na wabunge, Abdulhimid Shah (kulia) na Abdull Marombwa (nyuma ya Kinana) wakati Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipokuwa akiwaaga wananchi katika mji wa Nyamisati.

KINANA, Nape na Shah wakiwa pwani ya Mafia baada ya kushuka kwenye boti wakitokea Nyamisati.


NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga, akiwahutubia wananchi wa Mafia na kuwaelezea mipango ya serikali kuhusu huduma ya umeme katika kisiwa hicho.

UMATI wa wananchi wa Mafia uliojitokeza kumsikiliza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mkutano wa hadhara.

Dk. Bilal avipasha vyombo vya ulinzi na usalama, waandishi wa habari


NA WILLIAM SHECHAMBO
MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama  na waandishi wa habari nchini kushirikiana  katika majukumu yao ya kazi ili kulinda amani ya nchi.
Pia amezitaka taasisi hizo kuzingatia mipaka yao na  katika utendaji ili kuepuka migongano au chuki zinazoweza kutokea wakati wa kutimiza wajibu wao kazini.
Alitoa wito hiyo katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam,  jana, alipokuwa akifungua  mkutano  wa mashauriano  kati ya vyombo vya habari, ulinzi, usalama na sheria ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Vyombo vya ulinzi mnapaswa kujua kwamba waandishi wa habari si maadui zenu…mnaweza kukaa nao vizuri,” alisema.
Washiriki wa mkutano huo walitakiwa kutambua kazi zao na  kuhakikisha wanatekeleza majukumu , kuepusha migogoro hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.
Makamu wa Rais alisema mkutano huo wa kwanza wa kihistoria kuwakutanisha watendaji hao, umekuja wakati mwafaka kutokana na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la vyombo vya habari,  huku jamii nayo ikiwa na shauku ya kusambaza habari kadri  iwezavyo.
Alisema waandishi wanapaswa kudhibiti usambaaji wa habari zisizotakiwa kusambaa kwa maslahi ya ulinzi na usalama wa nchi kwa sababu sheria zilizoko hazina nguvu tena ya kufanya hivyo.
“Habari nyingine zinaweza kusababisha chuki na kuchochea vurugu, hivyo pande hizo zinapaswa kushirikiana katika kutetea maslahi ya taifa na amani kwa wananchi,” alisema.
Alivishauri vyombo vya habari kujenga taswira chanya kwa vyombo vya ulinzi na usalama  huku akivitaka vyombo hivyo navyo, kutoa ushirikiano wa dhati kwa wanahabari.
“Kila upande una mipaka yake ya kiutednaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku… kinachotakiwa ni kuelewana kwani nia na jukumu lenu nyote ni kulinda amani,” alisema.
Kupitia mkutano huo, alisema ni vema vyombo hivyo vikafungua ukurasa mpya wa mawasiliano.
Pia Dk. Bilal alivitaka vyombo vya habari kuanza mfumo wa kuwa na waandishi wataalam wa maeneo mbalimbali ikiwemo uandishi wa habari za mafuta na gesi.
“Wananchi wanapaswa kujua mambo haya vizuri, pia masuala ya afya, ukimwi, lazima kuwe na waandishi wataalam,” alisema.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Habari Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, alisema mkutano huo ni zao la mpango mkakati ulioandaliwa na MCT kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Naye Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga, Mtendaji wa MCT, sababu kubwa ya kuandaa mkutano huo ilichangiwa na tukio lililoleta hofu ya usalama nchini, pale ambapo mwandishi wa habari  Daudi Mwangosi alipouawa na vyombo vya usalama wakati akitekeleza majukumu yake mkoani  Iringa.
Alisema baada ya tukio hilo, uaminifu kati ya wanahabari na wanausalama  ulipungua, hali ambayo haina tija kwa maendeleo ya taifa.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo, Joseph Kulangwa, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, alieleza kufurahishwa na kauli ya Dk. Bilal na kusema imetoa mwongozo wa kufikia malengo ya mkutano.
Alisema wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu baadaye mwakani, suala la amani na mshikamano ni muhimu.
Hoja zilizojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuhusiana na usalama wa mwanahabari, utawala na sheria, uandishi wa habari za uchunguzi, mazingira na uzoefu pamoja na uwezekano wa vyombo vya usalama kuchangia uhuru wa kujielewa.
Hata hivyo jeshi la polisi halikutuma mwakilishi yeyote katika mkutano huo, licha ya kwamba, ratiba ilionyesha ofisa mmoja wa jeshi hilo kuwasilisha mada.

JK awapandisha saba JWTZ


NA MWANDISHI WETU
AMIRI Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete amewapandisha vyeo Maofisa saba  wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kutoka cheo cha Brigedia hadi kuwa Meja Jenerali.
Hatua hiyo aliitekeleza kwa mujibu wa kanuni za majeshi ya ulinzi ya Tanzania ambazo zinatambulika kisheria.
Maofisa waliopandishwa vyeo ni Brigedia Jenerali Gaudence Milanzi, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa, Brigedia Jenerali Ndetaulwa Zakayo na Brigedia Jenerali Venance Mabeyo.
Wengine ni Brigedia Jenerali Simon Mumwi, Brigedia Jenerali Issa Nassor na Brigedia Jenerali Rogastian Laswai, ambao wamekuwa na vyeo vya Meja Jenerali kuanzia Septemba 12, mwaka huu.
Katika tafrija ya kuwavisha vyeo vipya maofisa hao, iliyofanyika makao makuu ya jeshi eneo la Upanga, Dar es Salaam, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alimwakilisha Rais Kikwete.
Uteuzi huo pia umempandisha Meja Jenerali Gaudence Milanzi kuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC).
Meja Jenerali Milanzi amechukua nafasi hiyo baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho,  Luteni Jenerali Charles Makakala.

Watendaji legelege TAKUKURU kukiona


NA EVA-SWEET MUSIBA, SIRARI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imezitaka idara za udhibiti za katika mpaka wa Sirari, kufanya kazi uadilifu ili kudhibiti bidhaa zisizofaa kuingizwa nchini.
Imeonya kuwa kinyume cha agizo hilo, watendaji watakaobanika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Joseph Holle, alisema kuwa idara hizo zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha bidhaa zisizofaa kutoka nchi jirani haziingizwi nchini.
Alisema kuwa uingizwaji wa bidhaa mbovu ndiyo chanzo cha magonjwa hatari,  ikiwemo kansa na kwamba, hata ajali za barabarani nyingi zinasababishwa na vipuri bandia.
Mpaka wa Sirari unatajwa  kuwa ni miongoni mwa inayotumika kuingiza bidhaa zisizo na ubora, hivyo TAKUKURU imejikita kusaidia udhibiti wake.
Naye Ofisa kutoka TRA, Paulo Mkondokwa, aliomba vibali vyote kupelekwa mpakani ili taasisi husika zifanye ukaguzi.

Meli ya matibabu kuzinduliwa Mwanza


NA MWANDISHI  WETU, MWANZA
MRADI wa meli ya huduma za matibabu, ulio chini ya  Dayosisi ya Africa Inland Church Tanzania (AICT), mkoani hapa, unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
 Askofu Mkuu Dayosisi ya Geita, Musa Magwesela, alisema meli hiyo inatarajia kutoa huduma za matibabu katika visiwa mbalimbali vilivyopo ndani ya ziwa Victoria na mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza.
Alisema Ziwa Victoria lina takribani visiwa 90 huku, vikikisiwa kuwa na wakazi wapatao 450,000.
 “Kupitia meli hiyo, huduma ya matibabu zitawafikia wakazi hao kwa urahisi na kutolewabila malipo yoyote, alisema.”
Magwesela alieleza kuwa meli hiyo iligharimu kiasi cha sh. bilioni 2.5 za kitanzania na madaktari watakuwa wakitibu magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na meno, huduma za uzazi kwa wanawake na wanaume, chanjo, afya ya mtoto, kinga na kutoa elimu ya afya.
Alisema meli hiyo ina vyumba viwili vya madaktari, vitanda 18 kwa ajili ya wafanyakazi na sehemu ya kupumzikia wagonjwa zaidi ya 40.

Wawili wapoteza maisha Ubena Senge


NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
WATU wawili wamekufa na wengine 25 wamenusurika baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika eneo la Ubena Senge, Bagamoyo, barabara kuu ya Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea jana, saa 12.15 asubuhi, baada ya gari aina ya Toyota Coaster no.T 663 BKP, kugongana na gari la mafuta, aina ya Leyland lenye namba T858 CLK na tela T 421 CKY, mali ya kampuni ya Ramader . Gari hilo lilikuwa likitokea  jijini Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Athumani Mwambalasa, alisema gari la mafuta lilikuwa likiendeshwa na dereva Rashid ambaye alitoroka mara baada ya ajali hiyo.
Kamanda huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Neema Mile (39) na Jane Mtani (38), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema  majeruhi walipelekwa katika hospitali ya Tumbi mkoani Pwani.
Mwambala alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa coaster baada ya kuhama upande wake.
Dereva huyo anashikiliwa na  polisi.

Kagera yazindua kampeni ya kuimarisha Chama


NA  ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA.
CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kimezindua rasmi kampeni ya kuimarisha Chama ili kujiweka sawa na kujihakikishia ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.
Uzinduzi wa kampeni hizo uliofanyika jana, katika kata za Ruhunga na Kyaitoke wilayani Bukoba vijijini, ulikwenda sambamba na ugawaji wa vifaa kama bendera, milingoti na kamba ikiwa ni hatua mojawapo ya kufufua kazi za mabalozi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya  CCM (NEC), Nazir Karamagi, alisema vifaa hivyo vitakabidhiwa kwa mabalozi wote 5,520, na kwa wenyeviti wa matawi na kata.
Karamagi alisema kuwa mabalozi ni jeshi muhimu katika mapambano na kuwa haiwezekani  kuwaacha bila kuwapa nyenzo wakati wanategemewa katika Chama.
Naye katibu wa CCM Bukoba vijijini, Acheni Maulid, alisema mabalozi wamekuwa wakilalamika kuwa wanakumbukwa wakati wa uchaguzi na ndiyo maana CCM imeamua kuitisha mikutano ya mabalozi katika wilaya.
“Hii maana yake tunawatambua na kuwathamini,” alisema Maulid.
Karamagi anafanya ziara ya wiki mbili katika wilaya hiyo kwa lengo la kuzungumza na mabalozi na viongozi wengine wa Chama.

Thursday, 11 September 2014

Yona azidi kujitetea kortini


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, amekiri kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, aliagiza mchakato wa kumpata mkaguzi wa dhahabu usitishwe.
Akiendelea kutoa utetezi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana, Yona alidai kuwa hakutekeleza ushauri huo kwa kuwa Ikulu ilishatoa kibali cha kuendelea na mchakato.
Akiongozwa na wakili wake, Elisa Msuya, mbele ya jopo la majaji linaloongozwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Msajili Saul Kinemela, alidai Mei 2, 2003 aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, aliwaruhusu kuendelea na mchakato wa kumpata mkaguzi wa dhahabu, lakini alishauri serikali ichague mkandarasi atakayekuwa kama mtumishi wa serikali.
Barua hiyo ya Chenge, alidai, ilishauri mkandarasi huyo aajiriwe na kulipwa kwa mujibu wa kazi atakayokuwa akifanya na kuwa malipo yalipwe na serikali badala ya kampuni za madini.
Yona alidai aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, aliagiza Mei 15, 2003 kwamba mchakato wa kumpata mkaguzi huyo usitishwe.
“Nilimjibu Naibu Waziri kwa kumkumbusha kuwa alipokea maagizio ya Ikulu ya Mei 20, 2003. Sikutekeleza  agizo lake kwa sababu lilipitwa na maagizo ya Ikulu.
“Sikuwa na chaguo, nilifuata maagizo ya Ikulu ili mchakato uendelee na wote tuliopata dokezo la Ikulu tulifanya hivyo,” alidai.
Alidai kuwa alipokea mapendekezo kutoka kwa Mtaalamu wa Madini, Godwin Nyelo, yakitaka pia mchakato huo usitishwe wakati kamati ilikuwa ikiendelea.
“Tulitegemea Nyelo aende katika kamati kama mshauri na kuzikingia kifua hoja zake na wala si kurudisha majibu ya mapendekezo ya kusitisha mchakato.
“Nyelo alipendekeza kusitishwa kwa mchakato akidai malipo ya asilimia 1.9 ya mapatio ya dhahabu hayawezi kuiingizia kipato serikali,” aliongeza.
.
Mshtakiwa huyo alidai hakukaidi ushauri wa Nyelo isipokuwa aliuangalia akaona hautasaidia, akashauri arudi katika kamati.
Yona kutokana na muda aliishia hapo kujitetea. Jopo liliahirisha kesi hiyo hadi leo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali harasa ya sh bilioni 11.7.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja, walitenda makosa hayo Agosti, 2002 kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart Asseyers ya Uingereza kinyume cha sheria.

Waumini wa Sunni Jamaat wamvaa Turki


Na Mwandishi Wetu
WAUMINI wa Jumuia ya Sunni Muslim Jamaat, Dar es Salaam, wamemtaka mbunge wa Mpendae-CCM, Salim Turki, kufuata utaratibu na kuacha kuwanyanyasa waumini wenzake.
Imedaiwa kuwa Turki amekuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyume na huwatisha waumini wenzake kuwa hakuna wa kumfanya lolote kwa kuwa ni mbunge.
Wakiunguza na waandishi wa habari jana, waumini hao walidai kuwa Turki amekiuka maagizo ya Mahakama Kuu iliyozuia uchaguzi wa jumuia hiyo hadi pande mbili zinazovutana zitakapokutana na Ofisi ya Mrajisi ili kuhakiki wajumbe.
Hata hivyo, Turki alilazimisha kufanyika kwa uchaguzi huo huku akiwatumia polisi kuwadhibiti waumini, jambo ambalo limezusha malalamiko.
Uchaguzi huo ulifanyika Agosti 8, mwaka huu, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ambapo ulifanyika chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU).
Mmoja wa waumini hao, Ahmadia Mohammed, alisema mbunge huyo amekuwa tatizo kwenye jumuia hiyo huku akitumia wadhifa wake huo kisiasa kama ngao.
Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Turki hakuwa tayari kupokea simu yake ya kiganjani na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu, alijibu kuwa yuko kikaoni.

Raisi Kikwete akutana na Yoweri Museveni


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete, amefanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikulu, Dar es salaam.
Rais Museveni ambaye alikuwa kwenye ziara ya siku moja ya kikazi katika Tanzania, aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 4:10 asubuhi na kupokelewa na Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, yalianza saa 5:30 asubuhi na kuchukua kiasi cha saa 1.15.
Rais Museveni aliondoka Ikulu baada ya chakula cha mchana na aliagana na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwenye uwanja wa JNIA, kabla ya kupanda ndege yake kurejea nyumbani.

‘Kifaru’ cha JWTZ chavamia nyumba


  • Watatu wafariki papo hapo, wamo wanajeshi
  • Wengine taabani hospitali, JWTZ yachunguza

Na Rashid Mussa, Mtwara
WATU watatu wakiwemo askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia baada ya gari maalumu la kubebea askari la jeshi hilo kugonga nyumba katika Kijiji cha Mnollela mkoani Lindi.
Katika ajali hiyo iliyotokea jana alfajiri wakati gari hilo likitokea Mtwara kwenda Masasi, askari wengine sita walijeruhiwa huku wawili kati yao wakiwa na hali mbaya.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi, Renata Mzinga, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kutaja namba za gari hilo kuwa ni 018APC la kikosi cha Reget, lililokuwa likisendeshwa na askari wa JWTZ, Shadhil Nandonde (28).
Alisema gari hilo liliacha njia na kugonga nyumba mbili katika kijiji hicho na kusababisha kifo cha raia mmoja na askari hao wawili.
Renata aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni mkazi wa kijiji hicho, aliyekuwa katika nyumba moja kati ya mbili zilizogongwa, Someye Kamteule (75) na askari namba MT 10728 Pascal Komba (23) aliyekuwa katika gari hilo.
Alisema askari mwingine alikufa wakati akipata matibabu katika hospitali ya mkoa wa Mtwara ya  Ligulla, na kufanya idadi ya waliyokufa katika ajali hiyo ya aina yake  kufikia watatu.
Mwingine ni askari namba MT. 106842 Feruzi Haji (22), ambaye alifariki baada ya kufikishwa hospitali ya Ligula kupatiwa matibabu.
Kamanda Renata aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  askari namba MT 99018 Mbaruku Duchi (28), ambaye hali yake ilikuwa mbaya, MT. 10744 Simon Edward (23), MT. 1077263 Omari Makao, MT, 107442, Simon Maselle (23) na MT107218 Ndekenya (22) na dereva Nandonde.
=Akizungumzia ajali hiyo, Mganga Mfawadhi wa Hospitali ya Ligula, Lobi Kissambu, alisema kati ya majeruhi wawili walipokelewa wakiwa katika hali mbaya, mmoja wao Feruzi alikufa wwakati  akipatiwa matibabu.
Alisema Duchi alihamishiwa katika Hospitali ya Misheni Nyangao iliyoko mkoani Lindi kwa matibabu zaidi na wengine waliolazwa wodi namba nane hali zao zilikuwa zinaendelea vizuri.
Kutokana na ajali hiyo, JWTZ imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali  hiyo iliyosababisha vifo vya askari waliokuwa katika msafara wa kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Makao Makuu ya JWTZ, askari hao walikuwa wakitumia magari maalumu ya kubeba askari.
Taarifa hiyo ilisema JWTZ imeungana na familia za marehemu katika kuomboleza vifo vya askari hao pamoja na raia.
Pia JWTZ inafanya uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo kwa kushirikiana na  polisi.

Jaji Mutungi atangaza vita


  • Wanachama vyama vyote nchini kuhakikiwa
  •  Teknolojia mpya kutumika kubaini ubabaishaji
NA RABIA BAKARI
UBABAISHAJI na uendeshaji wa ujanja ujanja wa baadhi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumua nchini, umeanza kuitisha Ofisi ya Msajili na sasa inajiandaa kuvifanyia uhakiki ili kubaini udanganyifu.
Hatua hiyo inalenga kufichuliwa kwa vyama vyote vinavyoendeshwa kwa ujanja ujanja ama kutokuwa na vigezo vya kuendelea kuwa na usajili wa kudumu kutokana na mabadiliko mbalimbali.
Habari za kuaminika zimebainisha kuwa, kuna baadhi ya vyama vina usajili wa kudumu, lakini kwa sasa havina vigezo kutokana na kuzorota kwa uendeshaji wake na vingine kukimbiwa na wanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alisema baada ya uhakiki huo, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Alikuwa akipokea msaada wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP).
Alisema mwanzo ilikuwa ngumu kufanya uhakiki ama kuwa na majibu ya haraka, hivyo baadhi ya vyama kupata mwanya wa kufanya udanganyifu.
“Tumepokea vitendea kazi vyote kuanzia kompyuta za mezani, skana, simu za mkononi na kompyuta mpakato. Kusema kweli hatuna cha kusingizia isipokuwa kuwahakikishia Watanzania matokeo mazuri katika utendaji kazi wetu.
“Sasa hakuna chama kitakachodanganya, kikisema Mtwara kina wanachama kiasi kadhaa au kuna hili na lile, tunaingia mtandaoni na kuthibitisha,” aliongeza.
Alisema kadri wanavyoboresha ofisi hiyo, ndivyo atakavyojitahidi kuboresha vyama ili mawasiliano yaende sambamba na kuhakikisha hakuna atakayeachwa nyuma.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Phillipe Poinsot, alisema vifaa hivyo vina thamani ya sh. milioni 400, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha demokrasia nchini (DEP), ulioanza kutekelezwa na Ofisi ya Msajili mwaka huu.
Alisema mradi huo upo kwa takriban vipindi viwili vya uchaguzi, lakini ukiwa unatekelezwa na ofisi tofauti, ikiwemo Tume ya Uchaguzi Bara (NEC) na Zanzibar (ZEC), kabla ya kuhamishiwa katika ofisi hiyo.
Meneja Mtekelezaji wa DEP, Beatrice Stephano, alisema tayari wamepokea sh. milioni 500 za kuanza utekelezaji wa mradi, ambapo ukomo wake utategemea ufanisi wa utendaji katika mradi huo.

Mwigulu awavaa waajiri



  • Aagiza wakamatwe na kushitakiwa haraka

NA MOHAMMED ISSA NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SERIKALI imeagiza kushitakiwa kwa waajiri wote nchini, ambao hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Pia imewaonya waajiri kuacha mara moja tabia ya kutopeleka ama kuchelewesha michango ya wafanyakazi kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Mbali na hilo, imesema inaridhishwa na utendaji unaofanywa na uongozi wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, kwa kuongeza thamani ya mfuko huo.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa 24 wa wanachama na wadau wa mfuko wa PPF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Alisema waajiri ambao hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, wasifumbiwe macho na kwamba washitakiwe kwa mujibu wa sheria.
Mwigulu alisema katika miaka ya hivi karibuni, kumetokea tabia ya baadhi ya waajiri kuchelewesha ama kutopeleka michango ya wafanyakazi kwenye mifuko hiyo kinyume cha sheria.
Alisema ni kosa kisheria kwa mwajiri kuchelewesha ama kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wanaofanya hivyo, wachukuliwe hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kushitakiwa.
”Waajiri ambao hawawasilishi michango ya watumishi wao, wasionewe huruma, washitakiwe kwa mujibu ya sheria,” alisema.
Aliwataka baadhi ya waajiri kuacha tabia ya kusubiri wafanyakazi mpaka wanapostaafu ndio wawapelekee michango yao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali imeunda kamati kwa ajili ya kuhakiki madeni inayodaiwa na PPF ili iweze kulipa.
Alisema madeni hayo yakianza kulipwa, mfuko mfuko unaweza kuliendeleza taifa kwenye miundombinu mbalimbali.
Mwigulu alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina mchango mkubwa kwa jamii na kwamba asilimia 12 ya uchumi wa taifa, unatokana na mifuko hiyo.
Alisema wakati umefika sasa, PPF kutoa mikopo kwa ‘saccos’ ambazo si za mfuko huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, alisema kauli mbiu ya mkutano huo ni Hifadhi ya Jamii Chachu ya Maendeleo ya Kijamii.

Yona ajitetea, amtaja Mkapa


Na mwandishi wetu
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ameileza mahakama kuwa mchakato wa kumpata mkaguzi wa madini ya dhahabu ulifuata utaratibu zote na kusimamiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Yona ambaye jana alipanda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuanza kujitetea, alidai mwaka 2002 kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu mapato ya dhahabu iliyokuwa ikichimbwa na kampuni tano za kigeni.
Akiongozwa na wakili wake Elisa Msuya mbele ya Jopo linaloongozwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Msajili Saul Kinemela, alidai wizara iliamua kuhakiki gharama za madini hayo kwa kuwa BoT ndiyo iliyokuwa ikisimamia akaunti za kampuni hizo.
Alidai kuwa ilikubaliwa kutafutwa kwa mkaguzi wa dhahabu, ambapo mchakato huo ulisimamiwa na BoT na Wizara ya Nishati na Madini.
Aliendelea kudai baada ya majadiliano aliamua kumuandikia Rais aliyekuwepo wakati huo, Benjamin Mkapa dokezo kuhusu ukaguzi wa dhahabu Mei 11, 2003.
Alidai alimfahamisha Rais Mkapa majadiliano waliyofanya kati ya Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, BoT na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanaendelea vizuri.
Yona alidai Machi 3, mwaka 2003 alimuandikia Rais dokezo kwa mara ya kwanza kumfahamisha kwa maandishi, akiomba aruhusu kutekeleza ukaguzi wa dhahabu kwa kufuata taratibu na sheria.
Alidai Machi 20, 2003 Rais aliandika majibu kwamba anakubali waendelee na mchakato haraka.
“Tulimuahidi Rais kwamba mchakato utazingatia mapato ya nchi na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kweli katika hilo tulizingatia ushauri wa AG,” alidai.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo hakuweza kuendelea na ushahidi baada ya Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya kupinga kupokelewa kwa kielelezo kutoka ofisi ya AG.
Jopo hilo kwa pamoja lilikubaliana kuahirisha hadi leo kwa ajili ya kumpa nafasi Wakili Oswald kujiridhisha na kielelezo hicho.
 Washtakiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali harasa ya sh. bilioni 11.7.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo Agosti, 2002 kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart ya nchini Uingereza kinyume cha sheria.

Watano kortini kwa tuhuma za ubakaji


NA PETER KATULANDA, MAGU
MWENYEKITI wa CCM Kata ya Mwamanyili wilayani Busega, Simiyu, Ramadhani Msoka na wenzake watano, wamepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji.
Washitakiwa hao akiwemo Mshauri wa Mahakama ya Mwanzo ya Nyashimo wilayani humo, Libent Rwegarulila, ambaye ni mshitakiwa namba moja, walisomewa mashitaka hayo juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Magu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Robert Masige.
Awali, Msoka na wenzake watatu walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo, Agost 29, mwaka huu na kusomewa mashitaka hayo bila ya watuhumiwa wenzao wawili, Yela Magubu na Lupoja Mbeyo (ambao sasa ni washitakiwa namba tatu na nne, kukamatwa na kuunganishwa.
Washitakiwa wengine wa awali katika kesi hiyo namba 126/2014 ni Meshack Samson (ambaye ni mshitakiwa namba mbili) na Kubin Nkondo ambaye (mshitakiwa wa sita), ambapo Msoka sasa ni mshitakiwa wa tano.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Edward Mokiwa, alidai washitakiwa walitenda makosa hayo Agosti 23, mwaka huu, saa 7 usiku katika eneo la Nassa Ginnery wilayani Busega.
Alidai siku ya tukio washitakiwa wakiwa na silaha za jadi walimvamia Mwalimu Samuel Mkumbo na kuporac sh. milioni 18 kisha kundi hilo kumbaka kwa zamu mpangaji wa mwalimu huyo (jina linahifadhiwa) ambaye pia ni Mwalimu.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo. Hata hivyo, walidai kuwa kesi hiyo ni ya kisiasa na wamesingiziwa. Madai hayo yalipingwa na Mokiwa, ambaye aliieleza mahakama kuwa mashitaka ya unyang’anyi na ubakaji si ya kisiasa.
Upepelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na washitakiwa wote wako rumande kutokana na Hakimu Masige kusema mashitaka hayo hayana dhamana chini ya kifungu namba 148, kifungu kidogo cha 5 a (1). Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 24, mwaka huu.


NAPE akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe katika ofisi za Ubalozi huo, juzi.

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akikaribishwa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, tawi la Uingereza, Maino Owino kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Mafunzo cha Barking.

MWENYEKITI wa CCM, tawi la Uingereza, Kapinga Kangoma akimkaribisha Nape (Katikati) kutoa mada kuhusu wajibu wa matawi ya CCM yaliyoko nje ya nchi, alipozungumza na WanaCCM walioko nchini Uingereza.



VIONGOZI wa mashina ya CCM nchini Uingereza wakimsikiliza Nape.


NAPE akizungumza na wajumbe wa mashina waishio Uingereza.



VIONGOZI wakiandika taarifa zilizojiri wakati wa mkutano huo. (Picha zote na Adam Mzee).

Wednesday, 10 September 2014

Serikali ya kijiji Ruvu yadaiwa kuuza shamba kinyemela


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WANANCHI wa kitongoji cha Ruvu darajani, wilayani Bagamoyo, wameilalamikia serikali ya muda ya kitongoji cha Ruvu, kata ya Vigwaza,  kwa kuuza shamba la ekari 10 mali ya kijiji.
Imeelezwa kuwa shamba hilo limeuzwa kwa maslahi binafsi na bila kuwashirikisha wana kijiji.
Mwana kijiji, Athumani Mkali, alisema  uongozi wa muda wa kijiji cha Ruvu kuuza eneo hilo ni batili. “ Ukizingatia pia baadhi ya wananchi wengi hawana maeneo ya makazi na mashamba, leo eneo linauzwa kwa mtu mwingine, si haki,” alisema.
Alisema eneo hilo la ekari 10, limetolewa kwa mwekezaji huyo kinyemela na inasemekana limeuzwa kwa sh. milioni 50, ambapo mwekezaji huyo ametoa ahadi ya kuwajengea vyumba vya zahanati yenye thamani ya sh.milioni 25, jambo ambalo wananchi hawakubaliani nalo.
Naye Hemed Idd, alisema kuuzwa kwa  eneo la kijiji kwa faida binafs ni ukiukwaji wa sheria za serikali za mitaa.
Alisema jambo hilo likifumbiwa macho linaweza kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi kunakofanywa na uongozi huo .
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, alipoulizwa suala hilo alisema  hajui uwepo wa mgogoro huo, ila atawasiliana na katibu tarafa wa eneo hilo kujua kinachoendelea.

DC Iringa awaasa wanaoishi na VVU


NA TUMAINI MSOWOYA, IRINGA
MKUU wa wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba, amewataka wananchi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi  (VVU), kutokata tamaa, badala yake wafuate masharti ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Alitoa wito huo wakati Shirika la  Utafiti wa Tiba na Afya Barani Afrika, (AMREF),  lilipokuwa likitoa msaada wa baiskeli 50 kwa vikundi 17 kati ya 36 vya watoto salama, vinavyoundwa na wanawake wenye  VVU,  Iringa Vijijini.
Alisema kuishi na VVU sio mwisho wa maisha, kinachotakiwa ni kutokata tamaa na kufuata ushauri wa madaktari.
Aidha aliwapongeza wanawake hao kwa kujishughulisha na ujasiriamali na kutunza familia zao. Alisema jambo hilo ni mfano wa kuigwa.
Aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kupima afya zao ili kujua kama wameambukizwa au la.
Mmoja wa  mama mwenye maambukizi, Kalista  Haule, kutoka kijiji cha Migori, alisema wameamua kuvunja ukimya ili kuwasaidia wanaoogopa kupima, wajitokeze kujua afya zao.
Alilishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada wa baiskeli, jambo ambalo litawasaidia kwenye shughuli za kiuchumi.
 Aliwashangaa baadhi ya Watanzania wanaoendelea kuwacheka au kuwasimanga wenye maambukizi ya VVU.
Kwa upande wake, Thadei Madege wa kijiji cha Kihanga,  alisema baiskeli walizopewa zitawasaidia katika safari zao za kufuata dawa katika vituo vya afya, pamoja na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Pudenciana Kisaka, alisema vikundi hivyo vinasaidia kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na  wanawake wenye maambukizi hayo kuzingatia ushauri ili wanapopata mimba wajifungue watoto wasio na maambukizi.

‘Msiwabebe wanaojipitisha majimboni’


NA MWANDISHI WETU, MUFINDI
HALMASHAURI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mufindi, imewataka viongozi wa matawi na kata kutokubali kuwabeba baadhi ya wanachama walioanza kujipitisha kwenye majimbo, kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi mkuu  mwakani.
Katibu wa CCM wilayani Mufindi, Miraji Mtaturu, alisema hayo wakati akisoma maazimio ya halmashauri hiyo, iliyokuwa na lengo la kupokea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.
Alisema  ni kosa kikanuni kuanza kujipitisha wakati ambao chama kinatakiwa kufanya kazi za maendeleo kwa kushirikiana na viongozi waliopo madarakani.
Aliwataka viongozi wa kata na matawi kutokubali kuwabeba, wala kuwaruhusu watu wa aina hiyo, kwa madai kuwa wanadhoofisha utendaji wa kazi wa viongozi waliopo madarakani.
Mtaturu aliahidi hatua kali za kikanuni zitachukuliwa dhidi ya wanaojipitisha na wanachama wanaowapokea.
Alisema moja ya adhabu inayoweza kutolewa kwa viongozi hao ni pamoja na kuenguliwa uongozi.
Wabunge wa majimbo ya wilaya ya Mufindi ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa wa Mufindi Kaskazini  na Mendrad Kigola wa wa  Mufindi Kusini.
Awali, Mkuu wa wilaya hiyo, Evarista Kalalu, alisema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unaendelea vizuri kiasi cha kuondoa malalamiko ya wananchi katika sekta mbali mbali, ikiwemo maji na elimu.
Alisema upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo bado sio mzuri, kwani umeongezeka kwa kiasi kidogo, kutoka  asilimia 61.5 hadi 63 mjini  na asilimia 61.6 hadi 62 vijijini.

Vijana Kibaha watakiwa kugombea uongozi

NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kibaha Mjini, kimewataka vijana kuthubutu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ucaguzi ujao wa Chama na serikali.
Mwenyekiti wa UVCCM Kibaha Mjini, Idd Kanyalu, aliyasema hayo juzi,  katika eneo la Mzizizma  Zegereni, kata ya Visiga, alipokuwa akizungumza na wananchi, wakati wa ziara ya kamati ya maboresho inayolenga kukagua uhai wa jumuia hiyo.
Kanyalu aliwaasa vijana hao kujipanga kwenye mchakato wa uchaguzi kuanzia serikali  za mitaa, ili kuhakikisha wagombea wote wanaosimamishwa na chama hicho wanashinda kwa kishindo.
Aidha Kanyalu aliwataka vijana, hususan wajasiriamali, kuacha tabia ya ubinafsi,  badala yake wajiunge na vikundi ili waweze kupata fursa za kimaendeleo na kupatiwa mikopo kwa urahisi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho, Hamza Duluge, aliwataka vijana na wananchi kutokubali kurubuniwa  na wanasiasa kutoka nje ya CCM .
Alisema wanasiasa hao hawaonekani katika kipindi chote, lakini uchaguzi unapokaribia, wanajitokeza na kuanza kuwarubuni wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo Nicolaus Maliga, alisema ni wakati mwafaka kwa vijana kujitambua na kutokubali kutoa mwanya kwa watu wachache nje ya chama hicho, wenye lengo la kutaka madaraka wakitumia fursa ya kuwagonganisha ili watimize malengo yao.

Tuesday, 9 September 2014

JK, TCD watoa mwelekeo mpya



  • Bunge la Katiba kuendelea, UKAWA waridhia
  • Katiba iliyopo kuboreshwa kwa uchaguzi ujao

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
KIKAO baina ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimetoa mwelekeo mpya katika mchakato wa Katiba Mpya.
Mwelekeo huo ni matunda ya vikao viwili, ambavyo Rais Kikwete alivifanya na vyama wanachama wa TCD, kwa ajili ya kujadili changamoto za Bunge Maalumu la Katiba, baada ya baadhi ya vyama kususia vikao vya bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma.
Katika kikao hicho, TCD imebariki kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na kwamba, haliwezi kusitishwa kama ilivyokuwa ikipendekezwa na wachache.
Pia imependekezwa kufanyika kwa mabadiliko madogo kwenye Katiba ya sasa ili kuiwezesha kuendelea kutumika katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Kituo hicho kinaundwa na vyama vya siasa vyenye wabunge bungeni, ambavyo ni CCM, CUF, NCCR-MAGEUZI, TLP, CHADEMA, UDP, UPDP, ambapo wenyeviti wake na makatibu wakuu walihudhuria.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, Bunge litaendelea na vikao vyake hadi litakapokamilisha kazi yake Oktoba 4, mwaka huu.
‘’Wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuwa hatua hii ya mchakato wa Katiba iendelee hadi Oktoba 4, mwaka huu, ambapo Katiba inayopendekezwa inategemewa kupatikana,’’ alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na bunge hilo, Katiba inayotafutwa haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu mwakani kutokana na muda kutokidhi kukamilisha kazi hiyo.
Cheyo alisema kwa mujibu wa mchakato huo, kura ya maoni itakayopigwa na Watanzania inatarajiwa kufanyika mwezi Aprili, mwakani.
Alisema iwapo kura hiyo italazimika kurudiwa, kazi hiyo inaweza kufanyika Juni au Julai, mwakani, muda ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa kuvunjwa kwa ajili ya Uchaguzi  Mkuu.
“Kama tutalazimisha Katiba Mpya itumike kwenye uchaguzi mkuu mwakani, itatulazimu kuongeza uhai wa Bunge na serikali kwa zaidi ya mwaka, jambo ambalo haliwezekani,” alisema Cheyo.
Aliongeza kuwa wamekubaliana kurekebishwa kwa baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye katiba ya sasa, ikiwemo kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itasimamia uchaguzi na mshindi wa Urais ni lazima ashinde kwa zaidi ya asilimia 50.
Mapendekezo mengine ni kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika uchaguzi.
Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyama vingine vya siasa,  ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine katika Katiba, kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliopangwa ni mdogo.
‘’TCD kwa kupitia vikao vyake, itaratibu, itajadili mapendekezo hayo na kuyapeleka serikalini kwa hatua zaidi kwa kuwa muda tulionao ni mdogo na mabadiliko hayo yatajadiliwa kwenye Bunge la Novemba, mwaka huu na ikitokea tukichelewa basi hadi Februari mwakani,’’ alisema na kutumia fursa hiyo kumpongeza Rais Kikwete kwa usikivu wake na kukubali ombi la kukutana na TCD.
 ‘’Tunataka nchi iende kwenye uchaguzi ikiwa ni nchi ya kujivunia, yenye amani, mshikamano na itakayokuwa na uchaguzi huru na wa haki,’’ alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema tangazo la rais linalitaka Bunge hilo kukamilisha kazi zake ifikapo Oktoba 4, mwaka huu.
Hata hivyo, Hamad alisema Bunge hilo limesha andika barua kwenda serikalini ili kuomba siku za mapumziko zitolewe na kuongezwa katika siku za kazi.
Alisema ni mategemeo yake kuwa Bunge hilo litafanya kazi yake iliyotumwa ya kutoa katiba pendekezi.
‘’Suala la kutumika au kutotumika kwa Katiba katika uchaguzi mkuu ujao si kazi ya Bunge hili, tumepewa kazi ya kutunga Katiba pendekezi na hapo itakuwa mwisho wa kazi yetu ya Bunge Maalumu,” alisema.