Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Tuesday, 18 February 2014

TAMWA kuzindua ripoti utafiti wa kijinsia

Na Mwandishi wetu

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), leo wanatarajia kuzindua ripoti ya utafiti wa kijinsia uliofanyika Desemba, mwaka jana katika wilaya 20 za Tanzania.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuzinduliwa katika ofisi za TAMWA zilizoko Sinza Mori, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka, alisema jana kuwa uzinduzi huo unatokana na utafiti uliofanyika baada ya mafunzo kutolewa kwa waandishi wa habari  juu  ya habari za uchunguzi kuhusu a ukatili wa kijinsia, chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu UNFPA.
Alisema ripoti hiyo ya utafiti inaonyesha hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii pamoja na mambo yanayokwamisha juhudi za vyombo vinavyotetea haki za wanawake na watoto hapa nchini.
Kwa mujibu wa Valerie, utafiti huo ulifanywa kwa kushirikiana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema waandishi wa habari waliweza kuwahoji wanajamii mbalimbali kuanzia ngazi za familia na kupata ukweli wa hali halisi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo, ukeketaji, ubakaji, mauaji ya vikongwe, mimba katika umri mdogo na watoto wa kike kulazimishwa kuolewa.
Wilaya ziliyofanyiwa utafiti ni Kahama (Shinyanga), Tarime (Mara), Sengerema (Mwanza), Newala (Mtwara), Mbulu (Manyara), Singida Vijijini (Singida), Bariadi (Simiyu), Busega (Simiyu), Nkasi (Rukwa), Dodoma (Dodoma), Babati (Manyara), Chunya (Mbeya) na Bunda (Mara).
Kwa upande wa Zanzibar utafiti ulifanywa katika wilaya sita za mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Unguja Kusini na Kaskazini Unguja.

UWT yampongeza JK


Na Mwandishi Wetu

UMOJA wa Wanawake wa Tanzania (UWT) umempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uteuzi wake wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba lililoanza jana mjini Dodoma.
UWT imewataka wajumbe waliochaguliwa kuwepo katika bunge hilo kutambua dhamana waliopewa na Rais kwa kuhakikisha wanahakikisha wanawatetea wananchi ndani ya bunge hilo katika kupata Katiba Mpya.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa UWT, Eva Kihwele, ilisema wajumbe wanapaswa kuzingatia ueledi na uadilifu katika kutengeneza katiba ya Tanzania yenye kulinda kutetea na kusimamia maslahi ya taifa.
"Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, anampongeza Rais Kikwete kwa uteuzi huo, kwa kuwa umezingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii na hasa kutimiza 50/50 ya uwakilishi wa wajumbe,''alisema.
Hivyo, UWT ilisema inawatakia kazi njema katika kuhakikisha wanalijenga taifa moja na imara katika upatikanaji wa Katiba mpya.

Mkutano biashara Manyara kuanza leo

Na Mwandishi wetu, Manyara

MKUTANO wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Manyara ambao ulikuwa unasubiriwa kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa Kongamano kubwa la Uwekezaji mwaka jana, unafanyika leo chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa huo, Elaston Mbwilo.
Mbwilo aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba maandalizi yote ya mkutano huo muhimu yamekamilika na moja ya agenda kuu itakuwa matokeo ya kongamano la uwekezaji na utekelezaji wake.
“Wajumbe wote kutoka sekta za umma na ile binafsi wamethibitisha ushiriki wao hapo kesho (leo) na kila kuhusiana na mkutano wetu kipo safi,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Mbwilo alisema mkutano huo una maana kubwa sana ikizingatiwa kuwa mwaka jana uliandaa kongamano kubwa la uwekezaji ambalo lilivuta wawekezaji wengi wa ndani na wale wan je hivyo utatoa nafasi kubwa kwa wajumbe kujadili matokeo yake kwa kina.
“Wajumbe wa baraza watapata fursa ya kupitia utekelezaji wa mambo yote yaliyokubaliwa wakati wa kongamano ambalo lilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,” alisema.
Akifafanua zaidi umuhimu wa mkutano huo, Mbwilo alisema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo la biashara mkoa, sekta za umma na binafsi zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu mkubwa na hivyo kuibua fursa mbalimbali za kibiashara.
“Mkoa huu Manyara una utajiri mkubwa sana na sisi kama baraza la mkoa tunatumia mikutano kama huu kujadiliana kwa kina ni namna gani tunaweza kutumia fursa hizi kubadilisha maisha ya watu na kujenga kujenga uchumi imara.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mhandisi Raymond Mbilinyi, ambaye anahudhuria mkutano huo, amelisifu baraza la Mkoa wa Manyara kwa kuandaa mkutano na kuiomba mikoa mingine kufanya hivyo.

TANESCO yapokea mitambo ya Umeme

SERIKALI imepokea mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa megawati 75 kwa ajili ya mradi wa Kinyerezi I ambao unatarajiwa kukamilika  Oktoba, mwaka huu.
Mitambo hiyo kutoka Marekani, ilipokewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ambaye alikuwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, katika bandari ya Dar es Salaam.
Maswi alisema mradi wa Kinyerezi I utazalisha megawati 150 na kwamba mitambo hiyo ni ya awamu ya kwanza ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 75.
"Serikali tunatekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi katika kupunguza ghrama za uzalishaji umeme. Meli hii kubwa ina shehena ya mitambo ya kuzalisha megawati 75 ambayo tutaisimika Februari 28, mwaka huu," alisema.
Alisema mitambo hiyo haitakuwa na athari kwa kuwa ni ya kisasa na awamu ya pili itawasili nchini mwezi ujao. Mitambo hiyo imetengenezwa na kampuni ya General Electric.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Mramba, alisema kuwasili kwa mitambo hiyo ni hatua za msingi za kutatua tatizo la umeme nchini, ambapo tangu uhuru uwekezaji wake ulikuwa duni.
"Katika historia ya nchi tangu Uhuru hatujawahi kuwa na uwekezaji mkubwa kama huu. Mitambo  ya kuzalisha umeme itatatua suala la uzalishaji umeme hivyo bado usafirishaji na usambazaji. Watanzania tuna mipango mingi inayotekelezeka jitihada za leo (jana) ni sehemu ya mipango hiyo," alisema.
Mhandisi Mramba alisema katika eneo la Kinyerezi kuna miradi minne ambayo ni Kinyerezi I, II, III, IV ambayo itapunguza matatizo ya uzalishaji umeme.
Aliwaomba Watanzania kuwa na subira kwa kuwa matatizo ya umeme yatafika mwisho kutokana na miradi mikubwa iliyopo ambayo utekelezaji wake ni wa makini na madhubuti.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi ya Uzalishaji Umeme TANESCO, Mhandisi Simon Jirima, alisema mitambo hiyo itahifadhiwa katika eneo la mradi na baada ya uzalishaji, umeme utaingizwa kwenye gridi ya taifa.
Mhandisi Jirima alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 183 (zaidi ya sh. bilioni 250).

Sunday, 16 February 2014

Wabunge kulamba 300,000 kwa siku

Na Mwandishi wetu

KITENDAWILI cha posho za wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba sasa kimeteguliwa, ambapo imeelezwa itakuwa sh. 300,000 kwa siku.
Tayari wabunge wameanza kuwasili tangu Jumamosi na leo watapewa mafunzo maalumu ya namna ya kutumia ukumbi na miundombiu mingine ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema jana kuwa malipo hayo yatahusisha posho ya kikao sh. 80,000 huku posho zingine ikiwemo usafiri, madereva zitakuwa sh. 220,000 kwa siku.
Pia, alisema ukarabati wa jingo pamoja na miundombinu miengine ya ukumbi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wabunge zaidi ya 650, yamegharimu kiasi cha sh. Bilioni 8.2.
Dk. Kashillilah alisema mkutano wa Bunge hilo maalum utazinduliwa rasmi Februari 26, mwaka huu, kesho utafanyika mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Alisema wabunge wameanza kusajili jana na kazi hiyo itaendelea tena leo na kwamba, kesho asubuhi mkutano wa maelekezo utaanza hadi mchana utafanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda, kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge.
“Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Katibu wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi. Mwenyekiti wa muda atasimamia kuchaguliwa kwa Mwenyekiti na Makamu wake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Dk Kashillilah.
Alisema Mwenyekiti wa muda pia atasimamia kuandaliwa kwa kanuni na baada ya kupatikana kwa viongozi hao, ndipo Katibu wa Bunge na Naibu wake watateuliwa kwa Sheria.
Pia, alisema kabla ya viongozi hao kuanza kutekeleza majukumu hayo mazito kwa taifa, watendaji hao wataapishwa na Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete atazindua rasmi Bunge hilo Jumatatu saa 10 jioni na kwamba, wabunge wote wataapishwa siku hiyo saa 4 asubuhi na baadaye kuunda Kamati za Bunge Maalumu.
Uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu hilo utafanyika Februari 26 na kwamba, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba na utahitimishwa Aprili 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya
Katiba inayopendekezwa na kutunga masharti ya Mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalumu litakavyoona inafaa.
Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu la Katiba, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi
ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar.
Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na wabunge 629 ikiwa ni wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi pamoja na wale wa kuteuliwa.

JK azionya jumuia CCM

Na Mwandishi wetu

KWA mara nyingine tena, Rais Jakaya Kikwete amezionya jumuia za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kujikita katika kuimarisha chama na kujenga mshikamano badala ya kuwa wapigadebe wa makada wanaosaka uongozi.
Amesema jumuia za Chama ni taasisi muhimu na kazi yake kubwa ni kuimarisha na kujenga umoja hivyo, zinapoanza kutumiwa kwa malengo tofauti zinaweza kuleta madhara makubwa na kuzusha mpasuko.
Rais kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliyasema hayo juzi wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma, ambapo aliwaonya viongozi wote wa jumuia hizo kuacha tabia hizo haraka.
Jumuia ambazo ziko chini ya CCM ina Umoja wa Wazazi, Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Kauli ya Rais Kikwete inakuja wakati Chama kikianza kuchukua hatua dhidi ya makada wake wanaotuhumiwa kuvuruga na kukiuka taratibu kwa kuanza kufanya kampeni za kusaka urais katika uchaguzi wa 2015 kabla ya muda mwafaka kufika.
Kutokana na hatua hiyo, Rais Kikwete kwa nyakati tofauti aliagiza kamati zinazohusika na nidhamu kuchukua hatua dhidi ya wanaotaka kukivuraga Chama.
Alisema iwapo jumuia hizo iwe wanachama wake ama viongozi wakianza kujiweka kwenye makundi ya wasaka uongozi, Chama kinaweza kujikuta kwenye mpasuko mkubwa hasa pale wanaowapigia debe wasipopewa ridhaa ya kuwania uongozi.
‘’Kazi kubwa ya jumuia ni kuimarisha Chama na kujenga mshikamano, lakini kuna watu wameanza kuwa wapigadebe wa watu wanaosaka uongozi. Haya mambo hayatakiwi na hatupaswi kuyapa nafasi.

"Mambo yanaweza kuwa magumu pale wagombea mnawaopigia debe watakapokosa nafasi ya kuteuliwa kuwania uongozi. Rudini kwenye kazi mliyopewa na mtambue kuwa hizi jumuia ni taasisi nyeti,’’ alisema Rais Kikwete huku akionyesha kuchukizwa na namna mambo yanavyoendelea.
Juzi, wakati akifungua kikao hicho, Rais Kikwete aliwataka wanachama wa CCM kuacha kuwa wanyonge dhidi ya hila za wapinzania.
Alisema kwa muda mrefu wana-CCM wamekuwa wanyonge na sasa wanapaswa kuwa ngangari pindi wanapofanyiwa vitendo visivyo vya kistaarabu ikiwemo kuumizwa na wafuasi wa CHADEMA.
Mbali na kuimarisha Chama, jumuia hizo ikiwemo UVCCM ndizo zimekuwa na jukumu la kuhakikisha shughuli za Chama zinafanyika kwa amani na utulivu.

Polisi Dom yajipanga kwa Bunge la Katiba

NA MWANDISHI WETU

WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likitarajiwa kuanza kesho, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, amekutana na viongozi wa serikali za mitaa ili kujadili namna na kuimarisha ulinzi na usalama.
Kamanda Misime, alikutana na viongozi hao juzi ambapa aliwataka viongozi wa mitaa na kata kushirikiana kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ili kuhakikisha tukio hilo la kihistoria linafanyika kwa usalama.
Viongozi hao wakiwemo viongozi wa dini, madiwani, maofisa tarafa walikutaka katika ukumbi wa Polisi Dodoma, ambapo walijadiliana na kusisitiza masuala ya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha tukio la kihistoria cha kupata Katiba mpya.
Kamanda Misime, aliwapongeza wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kuvifufua vikundi vya ulinzi shirikishi hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa kupata katiba mpya ili kuweza kuzuia uhalifu hasa wa uvunjaji amani.
Aliwaomba viongozi hao kushirikiana katika kupunguza ajali za usalama barabarani pamoja na kujenga utamaduni wa kusema familia yangu haina uhalifu.
Aliwataka wamiliki wote wenye baa na kumbi za starehe kuzingatia sheria za kufungua na kufunga baa na kumbi hizo kwani zimekuwa ni sehemu ya maficho ya wahalifu.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, ambapo wajumbe wameanza kuwasili mjini hapa kwa ajili ya kuanza vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kufanyika kwa siku 70.

Ndungulile awafunda vijana

Na Emmanuel Shilatu

MBUNGE wa Jimbo la Kigamboni (CCM), Faustin Ndugulile, amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya.
Ndugulile, alitoa wito huo jana alipokuwa akifungua baraza la vijana la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Temeke, Dar es Salaam.
Alisema matumizi ya dawa za kulevya yana madhara kwa jamii na taifa na kwamba yanachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Ndugulile, alisema pamoja na juhudi za serikali za kupunguza matumizi ya dawa za kulevya, lakini idadi ya vijana wanaotumia dawa hizo inazidi kuongezeka na kusababisha madhara mbalimbali.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia dawa za kulevya, wawili kati yao wameathirika na virusi vya ukimwi na wanaume wawili wanaotumia dawa za kulevya, mmoja ana maambukizi ya ukimwi.
Alisema wakati umefika sasa, vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Ndungulile, ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Temeke, aliwataka vijana kuchagua viongozi wenye sifa watakaowahudumia wananchi.
Katika baraza hilo, Arnord Sangawe, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jimbo la Temeke na Juma Ndwangila, alichaguliwa kuwa katibu wa jimbo hilo.
Pia, wajumbe wa baraza la UVCCM, walimchagua Yasin Kanyama kuwa mwenyekiti wa jimbo la Kigamboni na Mustafa Pilla, alichaguliwa kuwa katibu wa jimbo hilo.

Miradi mikubwa ya barabara kuanza

Na mwandishi wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, leo atashuhudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara katika mikoa ya Ruvuma na Mtwara. Miradi hiyo itahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Namtumbo na Tunduru, ambayo imegawanywa katika sehemu tatu ambazo ni Namtumbo – Kilimasera (km 68.20), Kilimasera – Matemanga (km 58.70) na Matemanga-Tunduru (km 60.70).
Tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambayo inafadhili ujenzi huo kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), imetoa kibali kwa ujenzi wa sehemu mbili za kuanzia Namtumbo hadi Kilimasera na Matemanga hadi Tunduru. 
Sehemu kati ya Matemanga na Kilimasera itasubiri kibali kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambacho pia kinatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Hii ni mara ya pili kwa sehemu hiyo ya barabara kupata makandarasi. Awali kampuni ya Progressive-Higleig Joint Venture kutoka India ndiyo iliyokuwa imeshinda zabuni hiyo mwaka 2010, lakini baadaye ikasimamishwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya kimkataba na kuonyesha udhaifu katika utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, pia kutasainiwa mkataba wa ujenzi wa sehemu ya barabara inayoanzia Mangaka mkoani Mtwara hadi Nakapanya (km 70.50) katika mkoa wa Ruvuma.
Vile vile utasainiwa mradi mwingine wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Nakapanya hadi Tunduru (km 66.50) utakaotekelezwa mkoani Ruvuma.
Kusainiwa kwa miradi hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma pamoja na mikoa yote ya kusini kwani, barabara hiyo ni kichocheo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kesi ya Wachina wa meno ya tembo leo

NA FURAHA OMARY

KESI ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya sh. bilioni 5.4, inayowakabili raia watatu wa China, inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), ambao watapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Isaya Arufani.
Mbele ya Hakimu Arufani, mashahidi wa upande wa mashitaka wataanza kutoa ushahidi kuhusu mashitaka yanayowakabili Gin na wenzake ambao wanasota rumande.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa baada ya upande wa jamhuri kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kukutwa na vipande 706 vya meno ya tembo, vyenye uzito wa kilogramu 1,889, vikiwa na thamani ya sh. 5,435,865,000 wakivimiliki bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shitaka la kwanza, wanadaiwa siku na tarehe hiyo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na ganda la risasi lililotumika bila ya kuwa na kibali.
Pia, wanadaiwa siku hiyo walitaka kutoa hongo  ya sh. 30,250,000 kwa maofisa wa polisi, Mrakibu msaidizi wa polisi, Heri Lugaye, Gerwin na ofisa wa wanyamapori Simon Saye na watu wengine waliokuwepo eneo la tukio ili wasiwakamate.

Mwinyi: Tujikite kilimo cha kisasa

Na Mohammed Issa

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Alli Hassan Mwinyi, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa nchi inayozalisha chakula kwa wingi duniani, iwapo wananchi watajikita kwenye kilimo cha kisasa.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, lakini wananchi hawajakipa umuhimu.
Mzee Mwinyi alisema hayo jana nyumbani kwake Mikocheni, Dae es Salaam, alipozindua mpango wa kumsaidia mkulima yoyote wa Tanzania, ulioratibiwa na Diwani wa Kata ya Kwadelo, Omari Kariati.
Alisema pamoja na sekta ya kilimo kuwa sekta inayoweza kumtajirisha mtu haraka lakini Watanzania wengi hawajakipa umuhimu licha ya kuwa na ardhi ya kutosha.
Mzee Mwinyi alisema iwapo kilimo kitapewa umuhimu wa kutosha, taifa linaweza kuwa miongoni mwa mataifa yanayozalisha kilimo kwa wingi duniani.
"Kasi ya kulisha nchi ni ya wananchi wenyewe, ninawashauru vijana hususan wanaomaliza vyuo vikuu kujiajiri kupitia kilimo kwani ni ajira inayomtajirisha mtu haraka haraka," alisema.
Alisema wakati umefika sasa, vijana wanaomaliza vyuo vikuu, sekondari ni vyema wakajiariji kupitia kilimo na kwamba wasisubiri kuajiriwa na sekta zingine.
Rais huyo mstaafu, alisema kinachofanywa na Kariati cha kuhamasisha kilimo kinapaswa kuungwa mkono na watu wote kwani anaunga mkono juhudi za Rais Jakaya Kikwete kupitia Mpango wa Kilimo Kwanza.
Kwa upande wake, Kariati alisema mpango huo utamuwezesha Mtanzania yoyote kupata zana za kilimo ikiwemo matrekta popote alipo.
Alisema katika wilaya za Kondoa, kila kijiji kitapatiwa trekta tano na kwamba, mpango huo umeanza kwenye wilaya za Kongwa, Kondoa, Chemba na Kiteto.

RC Kandoro acharuka

Na Shomi Mtaki, Tunduma

SERIKALI mkoani Mbeya imewaagiza viongozi kuwakamata na kuwachukulia hatua wavamizi wanaochimba kokoto katika barabara ya Sumbawanga-Tunduma.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, mjini Tunduma baada ya kuwanasa baadhi ya watu wakichimbua kokoto katika eneo la Mwaka akiwa safarini kwenda Kapele kukagua miradi ya maendeleo.
Alisema watu hao hawatakiwi kufumbiwa macho kwa kuwa wameanza kufanya uharibifu mkubwa, ambao umesababisha athari kubwa wakati wa kuitumia.
Awali, Mhandisi wa Kampuni ya CCC, Eliazary Rweikiza, alisema wavamizi hao wamekuwa wakichimba na kozoa mchanga usiku na mchana.
Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamedai kuwa wavamizi hao wamekuwa wakikusanya malighafi hiyo na kwenda kuziuza kwa bei ya sh 5000 kwa kiroba cha kilo tano.

Thursday, 13 February 2014

Wamiliki shule binafsi walia kodi kubwa.

NA TUMAINI MSOWOYA, IRINGA

SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Kiserikali (TAMONGSO) limeiomba serikali kupunguza kodi zisizo za lazima ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya elimu.
Kwa kufanya hivyo, TAMONGSO imesema wananchi wa kawaida pia wataweza kumudu gharama za masomo.
Shirikisho hilo limetoa kilio hicho wakati wazazi wengi wakilalamika kuhusu kupanda holela kwa ada za shule binafsi, hivyo kuongeza ugumu wa maisha na kushindwa kuwasomesha watoto.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa shirikisho hilo kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu, mjini Iringa, Mwenyekiti wa shirikisho hilo,  Celestino Mafuga, alisema wingi wa kodi unasababisha wamiliki kupandisha ada ili kufidia gharama za uendeshaji.
Mafuga alisema kuendelea kupandisha gharama kutawaumiza wananchi wengi, hususan wa kipato cha chini.

“Kodi kubwa kwenye shule zetu inatufanya kupandisha bei ya ada, tutaendelea hivi mpaka lini? Kama nchi inaona elimu ni jambo la muhimu, isaidie kupunguza kodi,” alisema.

Katika hotuba iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Gerald Guninita, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, aliwataka wamiliki wa shule binafsi kupanga viwango vya ada kwa mujibu wa sera ili wasiwaumize wananchi.

Dk. Christine alisema kuwatoza wazazi ada kubwa ni kuwaumiza na ni ukiukwaji wa haki za mtoto katika kupatiwa elimu.
Akitoa mada kuhusu mpango wa uendeshaji shughuli za serikali kwa uwazi (OGP), Ofisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Hadija Maggid, amewataka wamiliki wa shule hizo kuwajibika na kudai mishahara kulingana na utendaji kazi.

Ujenzi wa madarasa 67 kukamilishwa.

NA WILLIAM SHECHAMBO

SERIKALI inaendelea na ujenzi wa madarasa 67 katika Manispaa ya Ilala, ili kupunguza idadi ya wanafunzi waliokosa nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza.
Madarasa hayo yanajengwa kwenye shule 10 za manispaa hiyo na yako katika hatua za mwisho kukamilishwa.
Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Ilala, Violet Mlowosa, alisema jana kuwa, hatua hiyo imechukuliwa ili kuwasaidia wanafunzi kupata haki ya msingi ya elimu kwenye shule walizochaguliwa.
Alizitaja shule hizo kuwa, Mchanganyiko, Binti Mussa, Juhudi, Pugu Stesheni, Majani ya Chai, Ulongoni, Magoza, Ugombolwa, Zawadi na Msimbazi.
Violet alisema ujenzi umezingatia uwepo wa eneo kwenye shule husika na mahitaji kutokana na idadi ya wanafunzi wasio na madarasa.
Ofisa huyo alisema utaratibu huo ni endelevu kwa mujibu wa serikali kuu, hadi itakapohakikishwa tatizo la uhaba wa madarasa limemalizwa.
Alisema changamoto inayoikabili manispaa katika taaluma ni walimu wa sayansi, hususan masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu.
Violet alisema vitabu si tatizo katika manispaa hiyo kwa kuwa serikali imejitahidi kukabiliana na tatizo hilo kwa kutoa fedha za ununuzi wa vitabu.
Aliwataka wazazi kutoa kipaumbele katika elimu ya watoto wao kwa kuwa elimu si jukumu la serikali pekee.
Ofisa huyo aliwaomba wazazi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya elimu kwa kuchangia michango michache shuleni, ikiwemo ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Dk. Bilal ahimiza usimamizi wa amani

NA JANE MIHANJI

VIONGOZI wa dini wametakiwa kuhubiri amani na kuwakemea bila woga wenye nia ya kuivuruga.
Wito huo ulitolewa juzi, jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alipotembelea maonyesho ya picha za kazi zinazofanywa na Mtukufu Aga Khan.
Alisema nchi haiwezi kuendelea bila kuwepo amani. 
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal
"Hatuwezi kukaa, kusali makanisani, misikitini na katika nyumba zingine za ibada kama majumbani mwetu kumechafuka."
Dk. Bilal aliwasihi viongozi wa dini kuendelea kutoa mafunzo ya kazi za kijamii ili wananchi wajikite katika maendeleo na kujiinua kiuchumi.
Alisema wajibu wa viongozi wa dini hauishii katika elimu ya kiroho pekee, kwa kuwa waumini wanahitaji huduma zingine za kimwili na kiakili.
Makamu wa rais alipongeza juhudi zinafanywa na Jumuia ya Ismailia katika kuenzi na kuendeleza kazi ya kiongozi wao, Mtukufu Aga Khan,  kwa kuwasaidia wasiojiweza.
Alisema wana-jumuia ya Ismalia wamekuwa wakitoa huduma kadhaa, zikiwemo za elimu na kushiriki katika masuala ya uchumi na afya nchini.
"Huu ni mfano wa kuigwa katika biashara, faida wanayoipata ndiyo huwasaidia watu wengine, tunatakiwa kujifunza katika hili," alisema.

Viongozi mbalimbali, wakiwemo mawaziri wamekuwa wakitembelea maonyesho hayo, ambayo Rais mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa kuyatembelea leo.

Jopo lakwama kusikiliza rufani.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohammed O. Chande
NA FURAHA OMARY

JOPO la majaji watano wa Mahakama ya Rufani, likiongozwa na Jaji Mkuu Mohammed Chande Othman, limeshindwa kusikiliza rufani ya mfanyabiashara Kibute Otienyeri, anayepinga adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa ubakaji.
Rufani hiyo haikusikilizwa jana kutokana na mkata rufani kutofikishwa mahakamani.

Kutokana na hilo, majaji hao wamemuelekeza msajili wa mahakama kuwasiliana na magereza ili kuhakikisha anafikishwa mahakamani Februari 19, mwaka huu.

Majaji wengine katika jopo hilo ni   Ibrahim Juma, Bethuel Mmila, Kipenka Mussa na Engela Kileo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, ulidai rufani hiyo ilipangwa kusikilizwa jana na wako tayari lakini mshitakiwa hajapelekwa mahakamani.
Wakili Majura Magafu, anayemwakilisha mkata rufani, alidai hajui gereza ambalo Otienyeri yuko, hivyo ikiwezekana mahakama  iwasiliane na magereza ili kujua aliko mshitakiwa.
Jaji Mkuu Chande alisema kwa mujibu wa kumbukumbu, mara ya mwisho alikuwa gerezani mkoani Arusha. 
Magafu aliomba shauri liahirishwe kwa sababu hajui iwapo mkata rufani anataka iendelee kusikilizwa ikiwa hayupo au la.
Jaji mkuu alisema baada ya kushauriana na majaji wenzake na kulingana na shauri lilivyo, wameamua kuahirisha kwa muda hadi Februari 19, mwaka huu, na msajili awasiliane na magereza ili afikishwe mahakamani.
Rufani hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la majaji watano kutokana na mapendekezo ya jopo la awali la majaji watatu.
Uamuzi ulitolewa na Jaji Mkuu Chande, Jaji Benard Luanda na Jaji Bethuel Mmila, ulipendekeza rufani hiyo isikilizwe mbele ya jopo la majaji watano ili kupata tafsiri sahihi ya vifungu vya sheria vinavyotumika wakati watoto wadogo wanapotoa ushahidi mahakamani.
Katika kutafsiri vifungu hivyo, majaji hao walielekeza rufani za kutiliwa maanani, ikiwemo namba 56/2005 ya Nguza Viking au Babu Seya na mwanawe Johnson ‘Papii Kocha’ wanaotumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto na za Herman Hanjewele na Hamis Shaban.
Katika rufani ya Otienyeri, inadaiwa Agosti 23 mwaka 2008 saa nne asubuhi, katika kijiji cha Manyiri, Arumeru, mkoani Arusha, alimbaka mtoto wa miaka 11.
Kesi hiyo ilikuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambayo ilimtia hatiani mshitakiwa na kumhukumu kifungo cha maisha jela kutokana na kuridhika na ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa Jamhuri.
Mshitakiwa hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ambapo Jaji Kakusulo Sambo, alikubaliana na hukumu hiyo na kusema anaamini ushahidi uliotolewa na mtoto ni wa kweli.
Otienyeri alikata rufani Mahakama ya Rufani mbele ya jopo la majaji watatu ambao walipendekeza isikilizwe mbele ya jopo la majaji watano.

Wednesday, 12 February 2014

JK: Marufuku kuuza meno ya tembo nje

NA RABIA BAKARI

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Tanzania haitauza nje shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa katika matukio mbalimbali nchini, ambayo yamehifadhiwa.
RAIS Jakaya Kikwete
Amesema yuko tayari kuamuru meno hayo yachomwe moto iwapo hayatakuwa na kazi mbadala lakini siki kuuzwa nje ya nchi.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi, amesema hatatoa kibali cha kuuzwa meno hayo ili kusaidia harakati za kukabiliana na ujangili nchini.
Alisema hayo juzi usiku, alipozindua mabango ya kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika vita dhidi ya ujangili, akiwa njiani kwenda London, Uingereza, ambako leo atahutubia kwenye mkutano maalumu kuhusu kupambana na ujangili wa tembo.
Mkutano huo umeitishwa na mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles, ambapo viongozi wa mataifa zaidi ya 50 duniani watahudhuria, Rais Kikwete akiwa kiongozi wa kwanza kuhutubia.
Alisema miaka kadhaa iliyopita Tanzania ilifanikiwa kupambana na wimbi la ujangili lakini mambo yameharibika kutokana na kurejea kwa biashara ya meno ya tembo, ambayo vinara wa ununuzi ni mataifa makubwa.
“Tumewahi kukumbwa na majanga makubwa ya ujangili mara mbili, awamu ya kwanza ilikuwa miaka ya 70 hadi 1980. Wakati wa Uhuru tulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini walipungua hadi kufikia 50,000,” alisema.
Kutokana na hilo, alisema mwaka 1989 serikali iliingiza jeshi katika Operesheni Uhai na mikakati mbalimbali ya kupambana na ujangili, ambapo mafanikio makubwa yalipatikana.
Alisema hadi mwaka 2009 idadi ya tembo iliongezeka maradufu na kufikia zaidi ya 150,000 lakini sasa imeanza kuwa mbaya kutokana na kushamiri kwa ujangili.
Kuhusu faru, ambao wanakabiliwa na tishio la kutoweka kwa kasi, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambapo wote walikuwa majike kabla ya kuingia dume kutoka Hifadhi ya Ruaha na kuanza kuzaliana.
“Sasa tuna faru 32 na tumeingia kwenye rekodi ya faru wanaozaliana kwa haraka duniani,” alisema.
Alisema kuendelea kwa ujangili kunatokana na kuwepo soko la meno ya tembo na nyara zingine.
Rais Kikwete alisema jitihada za ndani pekee haziwezi kuwa na mafanikio makubwa, hivyo ni lazima mataifa mengine yahusishwe.
“Nakwenda London kwa mazungumzo ambayo yalianza mwaka jana, yakilenga kufunga masoko ya meno ya tembo na faru. Nitakwenda kuwaambia wazungumze na wenzao kukomesha biashara ya meno ya tembo,” alisema.
Alitaja masoko makubwa ya meno ya tembo kuwa, Thailand, Vietnam na China na kwamba, yakifungwa ujangili utakuwa historia.
Rais Kikwete alisema pia kumeanza kushamiri biashara ya ngozi za simba,  chui na wanyamapori wengine, ambayo inatishia ustawi wa wanyama hao nchini.
Awali, akizungumza kabla ya kuzinduliwa mabango hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo ni kuchochea ushiriki wa Watanzania katika kupambana na ujangili.
MSIGWA AITWA MSALITI
Katika hatua nyingine, mwandishi wetu anaripoti kuwa, Umoja wa Wabunge wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira (TPGSNRCU), umemshukia mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), ukidai ni msaliti na mnafiki.
Umoja huo umesema kauli zilizotolewa na Msigwa alipozungumza na mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kuwa serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali hazina ukweli.
Pia umemtaka Msigwa kuwa mzalendo na kuacha kutoa kauli zinazolidhalilisha taifa kwa lengo la kujipatia umaarufu kisiasa kwa mambo yasiyo na chembe ya ukweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika Ofisi Ndogo za Bunge mjini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TPGSNRCU, Athumani Mfutakamba, alisema serikali imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ujangili.
Mwandishi wa gazeti la Daily Mail, Martin Fletcher, katika chapisho la Februari 8 na 9 mwaka huu, alimshutumu Rais Kikwete, akidai   ameshindwa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda tembo na faru.
Gazeti hilo lilimnukuu Msigwa, ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa, serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali, taarifa ambazo hazina ukweli.
Kwa mujibu wa Mfutakamba, Rais Kikwete yuko mstari wa mbele kupambana na ujangili na aliidhinisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kupinga biashara hii haramu kwa nguvu zote, kusema haonyeshi juhudi ni kumdhalilisha,” alisema.
Alisema mwandishi wa gazeti hilo, alipaswa kumuuliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli, ili kupata ukweli na si Msigwa, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
Mfutakamba alisema umoja huo unafikiria kuiomba serikali imtake mwandishi huyo aombe radhi kwa kuandika taarifa za uongo na udhalilishaji kwa taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa umoja huo, Sylvester Mabumba, alisema wataitaka serikali imuamuru mwandishi huyo kuomba radhi kutokana na taarifa hizo.
Alisema kabla mwandishi huyo hajachapisha habari, alitakiwa kumuuliza Lembeli na serikali ili apate ukweli wa mambo.

Vigogo CCM kitanzini leo

NA MWANDISHI WETU

KAMATI Ndogo ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo inaanza kuwahoji wanachama sita, wakiwemo viongozi waandamizi kwa tuhuma za kuanza harakati za urais mwakani  kinyume cha utaratibu.
Nape Nnauye

Wanachama hao wanatuhumiwa kufanya kampeni kabla ya wakati, jambo linalodaiwa limekuwa likiwavuruga wanachama.
Ni kutokana na vitendo hivyo, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM (Bara), John Malecela, aliibuka na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Malecela pia alikitaka Chama kutoa msimamo kuhusu wanachama hao, akisema wafuasi wengine wa CCM wamekuwa wakishindwa kufahamu msimamo wa Chama.
Kamati hiyo inakutana mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti Philip Mangula, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara). Wahusika wote wameshakabidhiwa barua za kuitwa kuhojiwa.
Wanachama watakaohojiwa ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Akizungumza na Uhuru jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema baada ya kuwahoji makada hao, kamati itatoa uamuzi kwa mujibu wa utaratibu wa Chama na kamati hiyo.
“Uamuzi utategemea ukubwa wa kosa, kama wataona kuna mtu ana kosa wanaweza kumuonya yakaisha katika kamati kwa namna watakavyoona inafaa.
“Lakini kama kutakuwa na kosa kubwa zaidi, kamati itapeleka kwenye Kamati ya Usalama na Maadili kwa ajili ya kutoa uamuzi,” alisema.
Hatua ya kuwaita na kuwahoji makada hao ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na uongozi wa juu wa CCM kwa nyakati tofauti kutokana na kukiukwa utaratibu wa Chama na kuleta mgawanyiko.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa CCM, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Jakaya Kikwete, alisema viongozi wa aina hiyo hawafai kupewa uongozi na kwamba, kamwe hawatafumbiwa macho.
Aliziagiza kamati za Chama zinazohusika na maadili kutimiza wajibu wake kwa kuwahoji watu wanaolalamikiwa kukiuka utaratibu.
Rais Kikwete alisema baadhi ya makada wamekuwa wakigawa fedha kwenye maeneo mbalimbali na kuwataka wananchi kuhoji wema wa aina hiyo ulioanza kushika kasi hivi karibuni.

Wabunge waonywa kutokuwa wabinafsi.

Na Hamis Shimye

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba kuijadili rasimu ya katiba kwa misingi ya Utanzania na si matakwa binafsi.
Amesema mchakato huo ni mgumu, hususan kutokana na kushirikisha binadamu ambao wana mtazamo tofauti lakini kinachotakiwa ni maridhiano na ikishindikana sanduku la kura liachwe liamue.
Dk. Bilal amesema wanasiasa wanapaswa kuweka kipaumbele katika kukubaliana kwa hoja na kwamba, viongozi wa vyama vya siasa wana wajibu mkubwa katika kusimamia hilo.
Makamu wa rais alisema hayo jana katika kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa, wakiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, mawaziri na viongozi wa vyama vya siasa nchini.
“Tukikubaliana na kupata maridhiano tutaweza kupata katiba ya Watanzania, itakayoendeleza misingi ya kuvumiliana na amani, kwa kuwa katiba ni suala muhimu,’’ alisema.
Alisema kumekuwapo kauli mbalimbali, hususan katika suala la Muungano, ambapo ofisi yake inayojishughulisha na mambo ya Muungano inaona kuna umuhimu mkubwa wa kubaki kama ulivyo.
“Muungano bado una umuhimu mkubwa na ningependekeza kuna mambo kama mawili ambayo yangewekwa katika Muungano, ikiwemo afya na elimu, kwa kuwa masuala haya ni muhimu,’’ alisema.
Dk. Bilal alisema lazima wajumbe wahakikishe zinatolewa hoja za kuuboresha Muungano na si kuuvunja.
“Hakuna binadamu anayejua zaidi ya mwingine, serikali tunakwazwa na kauli za vitisho. Vyama vya siasa vinapaswa kuonyesha mfano kwa wengine,’’ alisema.
Makamu wa rais alisema anatambua vyama vimeanza kuingia katika joto la uchaguzi lakini visikubali likaharibu mchakato mzima wa katiba mpya.
Alisema katiba ni ya Watanzania na si ya vyama vya siasa, hivyo hakuna haja ya kuzungumza kwa jazba au kutoana ngeu, bali wasimame pamoja katika kupata katiba.
Awali, Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, alisema katiba ni suala muhimu na lazima maridhiano yawepo katika upatikanaji wake, ili kizazi kijacho kiweze kufaidi matunda.
“Tumekutana ili kuonyesha umoja wa taifa letu na tunapongeza juhudi za serikali katika suala hili. Katiba tunayoitaka iwe ya maridhiano, iliyowashirikisha Watanzania wote,’’ alisema.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema kongamano limepewa kaulimbiu ya tafakuri na maridhiano kuelekea katiba mpya na wanasiasa wanapaswa kuwa wamoja katika kujadili suala hilo.
Alisema anaamini zipo changamoto katika suala hilo lakini watakaa pamoja na watavuka salama kwa kuwa kinachohitajika ni busara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema katiba ni suala muhimu na katika mchakato wa maoni wananchi walitoa maoni mbalimbali ili yawemo katika katiba.
Alisema suala la Muungano lilijadiliwa kwa kina na lina umuhimu mkubwa kwa kuwa likiachwa litaibua mgogoro wa kikatiba kwa wananchi kuhusiana na mambo mbalimbali.
“Hata ndani ya tume kulikuwepo mawazo na kuna mgawanyiko hasa kutokana na wapo wanaoamini katika Muungano wa serikali moja, mbili na tatu huku wengine mkataba. Tumeanza na serikali tatu,’’ alisema Warioba.
Mbunge wa kuteuliwa katika Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Ibrahimu Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, alisema uvumilivu unahitajika na kinachotafutwa ni katiba ya Watanzania.
“Tuheshimiane katika maoni kwa kuwa kinachotafutwa ni katiba ya Watanzania na si ya chama fulani, hivyo tuvumiliane katika utoaji maoni,’’ alisema.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema katiba ni suala muhimu hivyo vyama visiingize maoni binafsi katika mambo mbalimbali kwa kuwa wananchi wameshaamua.
Mkutano huo unaendelea leo, ambapo maazimio yatafikiwa, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni.

Serikali yafunga mjadala juu ya mashine za EFD

NA MOHAMMED ISSA

SERIKALI imeonya kuwa, mashine za kielektroniki (EFD) zisiwe chanzo cha kuvuruga amani ya nchi, na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa sheria.
Imesema msimamo wake uko pale pale na kamwe hautabadilika.
Kwa mujibu wa serikali, hakuna sababu ya kuendelezwa mjadala huo, kikubwa ni wafanyabiashara kufuata sheria za nchi.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, akizungumza kwa simu jana, alisema msimamo wa serikali ni kwamba mashine zitaendelea kutumika.
Alisema wataendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi ya mashine hizo na kwamba, elimu imeshatolewa kwa wafanyabiashara wengi.
“Mashine hizi zipo kisheria, zitaendelea kutumika na tunaomba zisiwe sababu ya kuleta mtafaruku, kuvuruga nchi na kuhatarisha amani,” alisema.
Saada alisema kabla ya kuanza matumizi ya mashine hizo, elimu ilitolewa kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wake na inaendelea kutolewa, hivyo wanaozipinga ni kwa utashi wao.
Waziri alisema madai mengi ya wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizo yameshafanyiwa kazi, hivyo kuwataka kuendelea kuzitumia kama sheria ilivyoelekeza.
Kwa mujibu wa Saada, baadhi ya watu waache wamekuwa wakiwashawishi wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizo.
Kwa takriban siku tatu baadhi ya wafanyabiashara wameingia kwenye mgomo wa kutokufanya biashara wakigomea matumizi ya EFD.
Wafanyabiashara hao, wakiwemo wa maduka eneo la Kariakoo, Dar es Salaam na baadhi ya mikoa, wanapinga matumizi ya mashine hizo, wakiitaka serikali kubadilisha mfumo huo wa ukusanyaji mapato.

CCM yapuliza kipenga Kalenga

NA SELINA WILSON

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imemteua Godfrey Mgimwa (32), kuwa mgombea ubunge jimbo la Kalenga katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Machi 16, mwaka huu.
Pia imemteua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula,  kuratibu kampeni za uchaguzi jimboni humo, zitakazoanza wiki ijayo.
Godfrey Mgimwa

Uchaguzi unafanyika kuziba pengo lililoachwa wazi na Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari mosi, mwaka huu, nchini Afrika Kusini.
Dk. Mgimwa pia alikuwa Waziri wa Fedha, ambaye mwanawe Godfrey anawania kuvaa viatu vyake.
Uteuzi ulifanywa jana na Kamati Kuu iliyokutana jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Alisema kampeni zitaendeshwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iringa Vijijini na kusaidiwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa, ambapo  Mangula ataratibu.
Nape alisema kamati za siasa za kata ndizo zitakazofanya kampeni, tofauti na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo hutoa watu kutoka makao makuu kwenda kufanya kampeni kwenye jimbo husika.
Alisema CCM imejipanga vyema na ina uhakika wa kupata ushindi wa kishindo.
Katibu huyo aliwaomba wapiga kura walioiamini CCM mwaka 2010 na kuipatia ushindi wa asilimia 85 kwenye jimbo hilo, waendelee kujenga imani katika uchaguzi huo.
VURUGU KATIKA KAMPENI
Nape alisema CCM haitavumilia unyanyasaji na vurugu kama zilizofanywa katika uchaguzi wa udiwani uliofanyika Jumapili iliyopita katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema CCM itaendelea kufanya kampeni za kistaarabu lakini haiko tayari kunyanyaswa na vyama vya upinzani, badala yake mwenye mawazo ya kufanya vurugu afute dhamira hiyo.
“Tunawatahadharisha wenzetu waliozoea siasa za vurugu, hatuko tayari kwa hilo na tunawaomba wananchi wa Kalenga wawaadhibu kama vile walivyoadhibiwa kwenye uchaguzi wa udiwani. Wametumia helikopta tatu, wamepata kata tatu kutokana na vurugu zao,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hoja ya kufanya jimbo la Kalenga kuwa la familia, alisema Godfrey hakuchagua kuzaliwa na Dk. Mgimwa, hivyo hawezi kuhukumiwa kwa hilo.
Nape alisema Godfrey amepitia utaratibu wa mchakato ndani ya Chama na ameshinda katika mchuano uliohusisha wanachama wanane.
Alisema wenye mawazo ya kufananisha Kalenga na Arumeru Mashariki, wasubiri matokeo ya uchaguzi, ambayo CCM itashinda kwa kishindo.
Katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, CCM ilimpitisha Sioi Sumari, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Jeremiah Sumari na kupoteza jimbo.
Alisema CCM haina shaka na ushindi na kwamba, CHADEMA isijidanganye kuwa itapata kitu na kwa uzoefu iliyoupata kwenye uchaguzi wa udiwani, iongeze helikopta zifike 13 ili zitoshe kata zote za jimbo la Kalenga.
KAULI YA GODFREY
Akizungumza na waandishi wa habari, Godfrey aliishukuru Kamati Kuu kwa kumteua kuwa mgombea wa CCM na anaamini ushindi utapatikana.
“CCM tuko tayari, tunajiamini na tuna uwezo wa kushinda uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa ni mwanachama wa CCM kwa miaka 10 sasa.
Alisema anafanya kazi Benki ya Stanbic katika masuala ya biashara na uchumi, aliyoyasomea katika vyuo tofauti nchini Uingereza.
Godfrey alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa kura ya maoni ndani ya CCM, baada ya kuibuka na kura 342  kati ya 697 zilizopigwa na kuwabwaga wanachama wengine wanane.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kifo cha Dk. Mgimwa.
Wagombea wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga aliyepata kura 170, Gabriel Kalinga (90), Hafsa Mtasiwa (42), William Pamagila (8), Bryson Kibasa (7), Sevelin Mtisi (3), Edward Mtagimwa (2) na Thomas Mwikuka (2).
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julius Malaba, ametangaza uteuzi wa wagombea utafanyika Jumatatu ijayo, siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi.

Waliokodiwa na CHADEMA kufanya fujo watekelezwa

NA PETER KATULANDA, MWANZA

ZAIDI ya vijana 50 waliokodiwa na kupelekwa na CHADEMA katika Kata ya Nyasula wilayani Bunda, kwa lengo la kufanya vurugu na kuzuia wananchi kupiga kura kwa madai ya kulinda kura, wametelekezwa.
Joyce Masunga, Katibu wa CCM (M) Mwanza
Hata hivyo, vijana 10 wamefanikiwa kurejea jijini Mwanza na kuwashushia tuhuma nzito viongozi wa M4C Kanda ya Ziwa kwa kushindwa kutimiza makubaliano na badala yake kuwatekeleza.
Tayari baadhi wamejisalimisha kwa uongozi wa CCM Mkoa wa Mwanza kufichua siri hizo na kuomba kujiunga na Chama.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga, alisema kilichowapata CHADEMA ni fundisho kwa vyama vinavyoeneza vurugu na uchochezi badala ya kueleza sera za kuwakomboa watanzania.
Habari za kuaminika na kuthibitishwa na baadhi ya vijana waliokuwa kwenye msafara huo, zimesema wenzao zaidi ya 30 wamekwama mjini Bunda kutokana na kukosa nauli ya kurejea Mwanza.
“Wenzetu wamekwama Bunda kutokana na kuishiwa fedha, tunafanya utaratibu wa kuchangishana tuwatumie hata kwa M-Pesa warudi, hali ya Bunda ni mbaya na tulitaitiwa…” alisema kijana mmoja bila kufafanua jinsi walivyobanwa.
Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA, wakionekana kushangazwa na kusononeshwa na matokeo hayo, juzi na jana asubuhi kwenye kijiwe maarufu cha Kemondo katika Kata ya Nyamagana, walisema viongozi wao waliwatelekeza bila kuwaaga baada ya matokeo kutangazwa.
Katibu wa M4C Kanda ya Ziwa, Tungaraza Njugu, na viongozi wenzake hawakuweza kupatikana kutokana simu zao kuzimwa.
“Niliwambia CHADEMA inatapatapa na inajua ‘itanyolewa’ na CCM ndiyo maana ilipeleka vijana wakafanye fujo na kuzuia wana CCM wasipige kura, cha moto wamekiona, wamevuna uasi waliokuwa wakipanda kwa kucharanga watu mapanga,” alieleza Masunga na kuwapongeza wananchi wote na wana CCM kwa ushindi walioupata.

Mzimu wa Zitto watikisa

NA PETER KATULANDA, MWANZA

WAKATI mzimu wa Zitto Kabwe ukizidi kukimomonyoa
Zitto Kabwe Mb. (CHADEMA)
CHADEMA katika maeneo mbalimbali nchini, hususan mkoani Mwanza, Chama  Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo kinazidi kujiimarisha kwa kuzoa wanachama wapya.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Mwanza, Simon Mangelepa, aliiambia Uhuru jana kuwa, kwa kipindi cha wiki moja Chama
kimepata wanachama wapya 1,596 wakiwemo 1,206 kutoka CHADEMA.
Alisema, wamepata wanachama hao wakati wa wiki ya
maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM, katika wilaya mbalimbali  za mkoa huo na kutamba kwamba, CHADEMA wajiandae kung’oka katika majimbo yote waliyoshinda katika uchaguzi Mkuu uliopita mkoani humo.
“Nawapongeza wanachama wapya waliojiunga na Chama Bora wakati wa maadhimisho ya miaka 37, watambue wajibu wa kiapo walichokula wakati wakikabidhiwa kadi za CCM na kudumisha amani na mshikamano na watanzania wote, CCM hatuna sera ya ‘kukunja ngumi’,” alisema Mangelepa.
Katibu huyo alifafanua wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Januari 26 hadi Februari 5, mwaka huu, katika kila wilaya, CCM ilivuna wanachama 1,596 wakiwemo 180 waliojiunga na jumuia zake.
Alizitaja jumuia hizo na wanachama wake wapya kwenye mabano kuwa ni UVCCM (80), UWT (50) na Wazazi (50) katika wilaya zote za mkoa huo.
Alisema wananchi 1,416 walijiunga na Chama katika wilaya tano za Sengerema (39), Kwimba (67), Misungwi (561), Nyamagana (520) na Ukerewe wanachama 229 na hivyo jumla kuwa 1,596.

Monday, 10 February 2014

Madabida kizimbani.

NA FURAHA OMARY

MMILIKI na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) Ltd, Ramadhani Madabida, amepandishwa kizimbani akidaiwa kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi (ARV).
Ramadhan Madabida, Ofisa mtendaji TPI
Madabida na wenzake watano, wakiwemo watumishi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mmiliki huyo wa TPI, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na wenzake wanadaiwa kuisababishia MSD hasara ya sh. milioni 148.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka huu, ni wafanyakazi wa TPI, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Seif Shamte; Meneja Masoko, Simon Msoffe na Mhasibu Msaidizi Fatma Shango.
Watumishi wa MSD ni Meneja Udhibiti Ubora, Sadiki Materu na Ofisa Udhibiti Ubora, Evans Mwemezi.

Vigogo wa TBA wachungulia jela.

NA FURAHA OMARY

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na mwenzake, wamehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela au kulipa faini ya sh. milioni 15, kila mmoja.
Washitakiwa hao wametiwa hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kutoa kibali cha ujenzi wa ghorofa 18 mtaa wa Chimara, Dar es Salaam, jirani na Ikulu.
Kimweri (60) na aliyekuwa Msanifu Mkuu wa TBA, Richard Maliyaga (55), waliohukumiwa adhabu hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, walinusurika kwenda jela baada ya kulipa faini.
Hukumu ilisomwa na aliyekuwa Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Sundi Fimbo, aliyesikiliza shauri hilo. Kwa sasa amehamishwa katika mahakama hiyo.

CHADEMA mzigo kwa taifa - Nape

NA SELINA WILSON

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukuru Watanzania kwa kukiamini na kukipatia ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika katika kata 27, ambapo CCM imeshinda kata 23. 
Katibu wa kamati kuu NEC (CCM) itikadi na uenezi, Nape Nnauye akiteta jambo.


Kimesema siri ya kuimwaga CHADEMA ni uadilifu katika kuwatumikia wananchi na kwamba, kushindwa kwa chama hicho ni ushahidi kwamba hakikubaliki na Watanzania wamewathibitishia kwamba hawajazoea vurugu.

Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo na kuongeza kuwa matokeo hayo ni ushahidi kwamba CCM inakubalika zaidi na Watanzania walio wengi.
Nape alisema CCM inaahidi kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa amani na utulivu kwa kuwa ina uzoefu wa kufanya siasa kistaarabu na ndio siri ya kukubalika kwa wananchi.
Akizungumzia kushindwa kwa CHADEMA alisema wamehukumiwa kutokana na vurugu na kupiga watu kwenye kampeni za uchaguzi na ndio maana wametumia gharama kubwa na helkopta tatu na kuambulia kata tatu.
"CHADEMA wamevuna walichopanda Watanzania hawapenda vurugu, wamezoea amani na utulivu sasa wamewaadhibu kwa kuwanyima kura na huo ni ushahidi kwamba Watanzania hawakiamini," alisema.

Katika uchaguzi huo CCM ilishinda katika kata CCM ilishinda katika kata 23 za Kibindu na Magomeni (Pwani), Kiwalala na Namikage (Lindi), Ubwage (Shinyanga), Ibumu na  Nduli (Iringa), Kiomoni na Mtae (Tanga), Nyasura(Mara), Malindo na Santillya (Mbeya).

Zingine ni Partimbo(Arusha, Mkwiti (Mtwara), Tungi na Ludewa (Morogoro), Mrijo (Dodoma).

Bandari Dar kufanya kazi saa 24

NA MOHAMMED ISSA

SERIKALI imesema tatizo la msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, utakuwa historia baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuanza kufanyakazi saa 24.
Imesema utaratibu huo utaanza kutumika muda wowote kuanzia sasa na utaongeza tija na ufanisi kwa watumiaji wa bandari.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dk. Shaaban Mwinjaka
Hatua ya kuanzisha utaratibu wa kufanyakazi kwa saa 24, imefikiwa na wadau wanaotumia bandari hiyo kwa ajili ya kuongeza huduma bora zinazotolewa na TPA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, aliseama hayo jana mjini Dar es Salaam, kwenye hafla ya utiaji saini wa kufanyakazi kwa saa 24 kwa siku saba katika kipindi cha mwaka mmoja baina ya TPA na wadau wengine wa bandari.
Alisema utaratibu huo utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa mizigo bandarini na kuongeza ufanisi wa utendajikazi.
“Tunataka kuwahakikishia wananchi kuwa utaratibu huu, utaboresha huduma zinazotolewa na TPA na utaondoa msongamano wa mizigo bandarini,” alisema.
Alisema serikali imeridhishwa na utaratibu huo na itahakikisha unafanikiwa ili kuondoa changamoto zilizokuepo bandarini hapo na kuleta ufanisi kwa watumiaji. 
Dk. Mwinjaka katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, tayari wametenga maeneo kwa ajili ya huduma za kibenki na kwamba nchi zingine wanazofanyanazokazi zitapatiwa maeneo ya ofisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Madeni Kipande alisema utaratibu huo utaiwezesha bandari kufanyakazi kwa uhakika na ubora wa hali ya juu.

Hakuna Mtanzania aliyenyongwa China.

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imekanusha taarifa zilizosamba kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna Watanzania 160 wamenyongwa nchini China kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.
Imesema hakuna Mtanzania yeyote aliyenyongwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao na vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na wizara hiyo ilisema taarifa hizo ni za uvumi na hazina ukweli wowote.
Taarifa hiyo ilisema mtuhumiwa anmayedaiwa kunyongwa aliyefahamika kwa jina la Mapusa yupo hai, gerezani anatumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kuingiza dawa za kulevya nchini humo.
Ilisema hivi karibuni mfungwa huyo alishiriki kuandaa maonyesho ya utamaduni wa Kiafrika wakati wa kuadhimisha sherehe za mwaka mpya wa China.

EFD ni lazima zitumiwe na Wafanyabiashara nchini - KAYOMBO

NA mwandishi wetu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema wafanyabiashara wanapaswa kufuata sheria na matumizi ya mashine za kielectronics (EFD) hayatasitishwa.

Richard Kayombo Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi TRA
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa msimamo huo jana alipozungumza na Uhuru kuhusu mgomo wa wafanyabiashara.
Baadhi ya wafanyabiashara jijiji Dar es Salaam na mikoa ya Iringa na Mara jana waligoma kufungua maduka kupinga matumizi ya mashine hizo.

"Msimamo wa serikali upo pale pale hakuna mabadiliko, wafanyabiashara wanatakiwa kutumia mashine hizo na kama elimu ilishatolewa na kwa ambaye bado aje tupo tutamuelekeza," alisema.
Aliongeza kuwa mfanyabiashara ambaye hataki kutumia mashine hizo aendelee kutofungua duka na asijaribu kushawishi wengine kwa kuwa ni kinyume cha sheria na atachukuliwa hatua.
Alisema wafanyabiashara walipewa muda wa kutosha kujiandaa na matumizi ya mashine hizo hivyo, kinachotakiwa kwa sasa ni utekelezaji tu.

Mgomo huo unatokea kwa mara ya tatu kwa wafanyabiashara wa maeneo ya Kariakoo kufunga maduka yao wakigomea kutumia mashine hizo.

Watatu wafa kwenye ajali za Barabarani jijini Dar

NA JUMANNE GUDE

WATU watatu wamekufa jijini Dar es Salaam, katika matukio ya ajali za barabarani likiwemo la Antony Severine na mwenzake ambao walikufa katika ajali ya gari, huko katika barabara ya Mandela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala Marietha Minangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa nne usiku eneo la Buguruni, kiribu na benki ya KCB.
Alisema gari lenye namba za usajili T 858 CDZ aina ya Toyota Opa iliyokuwa inaendeshwa na Domonick Maliki ilipofika eneo hilo ilimshinda na kuacha njia hatimaye kuwagonga watu wawili waliokuwa wanatembea kwa miguu akiwemo Severine (24) ambaye alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Marietha alisema mtu mwingine aliyegongwa ambaye hakufahamika jina lake alifariki wakati akipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.


Kamanda wa Polisi (Ilala) Marietha Minangi
Aidha, Marietha alisema maiti ya Severine imehifadhiwa katika hospitali ya Amana na ambaye jina lake halijafahamika maiti yake imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika tukio lingine, mkazi wa Magomeni, Khadija Salum (82) amekufa baada ya kugongwa na basi linalotoa huduma ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), huko katika barabara ya Morogoro eneo la Magomeni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wKinondoni Camillus Wambura alisema jana, ajali hiyo ilitokea juzi saa 5.49 usiku katika eneo hilo.
Alisema gari hilo lenye namba za usajili T 685 CPA aina ya Eicher, iliyokuwa ikiendeshwa na Boniface Paul ilimgonga Khadija ambaye alikuwa akivuka kutoka upandea kushoto wa barabara kuelekea upande wa kulia.
Wambura alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala, ambapo dereva wa gari hiyo amekamatwa, huku upelelezi ukiwa unaendelea kuhusiana na ajali hiyo.