KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imemteua Godfrey Mgimwa (32), kuwa mgombea ubunge jimbo la Kalenga katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Machi 16, mwaka huu.
Pia imemteua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kuratibu kampeni za uchaguzi jimboni humo, zitakazoanza wiki ijayo.
Godfrey Mgimwa |
Uchaguzi unafanyika kuziba pengo lililoachwa wazi na Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari mosi, mwaka huu, nchini Afrika Kusini.
Dk. Mgimwa pia alikuwa Waziri wa Fedha, ambaye mwanawe Godfrey anawania kuvaa viatu vyake.
Uteuzi ulifanywa jana na Kamati Kuu iliyokutana jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Alisema kampeni zitaendeshwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iringa Vijijini na kusaidiwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa, ambapo Mangula ataratibu.
Nape alisema kamati za siasa za kata ndizo zitakazofanya kampeni, tofauti na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo hutoa watu kutoka makao makuu kwenda kufanya kampeni kwenye jimbo husika.
Alisema CCM imejipanga vyema na ina uhakika wa kupata ushindi wa kishindo.
Katibu huyo aliwaomba wapiga kura walioiamini CCM mwaka 2010 na kuipatia ushindi wa asilimia 85 kwenye jimbo hilo, waendelee kujenga imani katika uchaguzi huo.
VURUGU KATIKA KAMPENI
Nape alisema CCM haitavumilia unyanyasaji na vurugu kama zilizofanywa katika uchaguzi wa udiwani uliofanyika Jumapili iliyopita katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema CCM itaendelea kufanya kampeni za kistaarabu lakini haiko tayari kunyanyaswa na vyama vya upinzani, badala yake mwenye mawazo ya kufanya vurugu afute dhamira hiyo.
“Tunawatahadharisha wenzetu waliozoea siasa za vurugu, hatuko tayari kwa hilo na tunawaomba wananchi wa Kalenga wawaadhibu kama vile walivyoadhibiwa kwenye uchaguzi wa udiwani. Wametumia helikopta tatu, wamepata kata tatu kutokana na vurugu zao,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hoja ya kufanya jimbo la Kalenga kuwa la familia, alisema Godfrey hakuchagua kuzaliwa na Dk. Mgimwa, hivyo hawezi kuhukumiwa kwa hilo.
Nape alisema Godfrey amepitia utaratibu wa mchakato ndani ya Chama na ameshinda katika mchuano uliohusisha wanachama wanane.
Alisema wenye mawazo ya kufananisha Kalenga na Arumeru Mashariki, wasubiri matokeo ya uchaguzi, ambayo CCM itashinda kwa kishindo.
Katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, CCM ilimpitisha Sioi Sumari, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Jeremiah Sumari na kupoteza jimbo.
Alisema CCM haina shaka na ushindi na kwamba, CHADEMA isijidanganye kuwa itapata kitu na kwa uzoefu iliyoupata kwenye uchaguzi wa udiwani, iongeze helikopta zifike 13 ili zitoshe kata zote za jimbo la Kalenga.
KAULI YA GODFREY
Akizungumza na waandishi wa habari, Godfrey aliishukuru Kamati Kuu kwa kumteua kuwa mgombea wa CCM na anaamini ushindi utapatikana.
“CCM tuko tayari, tunajiamini na tuna uwezo wa kushinda uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa ni mwanachama wa CCM kwa miaka 10 sasa.
Alisema anafanya kazi Benki ya Stanbic katika masuala ya biashara na uchumi, aliyoyasomea katika vyuo tofauti nchini Uingereza.
Godfrey alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa kura ya maoni ndani ya CCM, baada ya kuibuka na kura 342 kati ya 697 zilizopigwa na kuwabwaga wanachama wengine wanane.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kifo cha Dk. Mgimwa.
Wagombea wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga aliyepata kura 170, Gabriel Kalinga (90), Hafsa Mtasiwa (42), William Pamagila (8), Bryson Kibasa (7), Sevelin Mtisi (3), Edward Mtagimwa (2) na Thomas Mwikuka (2).
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julius Malaba, ametangaza uteuzi wa wagombea utafanyika Jumatatu ijayo, siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru