Sunday, 16 February 2014

Mwinyi: Tujikite kilimo cha kisasa

Na Mohammed Issa

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Alli Hassan Mwinyi, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa nchi inayozalisha chakula kwa wingi duniani, iwapo wananchi watajikita kwenye kilimo cha kisasa.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, lakini wananchi hawajakipa umuhimu.
Mzee Mwinyi alisema hayo jana nyumbani kwake Mikocheni, Dae es Salaam, alipozindua mpango wa kumsaidia mkulima yoyote wa Tanzania, ulioratibiwa na Diwani wa Kata ya Kwadelo, Omari Kariati.
Alisema pamoja na sekta ya kilimo kuwa sekta inayoweza kumtajirisha mtu haraka lakini Watanzania wengi hawajakipa umuhimu licha ya kuwa na ardhi ya kutosha.
Mzee Mwinyi alisema iwapo kilimo kitapewa umuhimu wa kutosha, taifa linaweza kuwa miongoni mwa mataifa yanayozalisha kilimo kwa wingi duniani.

"Kasi ya kulisha nchi ni ya wananchi wenyewe, ninawashauru vijana hususan wanaomaliza vyuo vikuu kujiajiri kupitia kilimo kwani ni ajira inayomtajirisha mtu haraka haraka," alisema.
Alisema wakati umefika sasa, vijana wanaomaliza vyuo vikuu, sekondari ni vyema wakajiariji kupitia kilimo na kwamba wasisubiri kuajiriwa na sekta zingine.
Rais huyo mstaafu, alisema kinachofanywa na Kariati cha kuhamasisha kilimo kinapaswa kuungwa mkono na watu wote kwani anaunga mkono juhudi za Rais Jakaya Kikwete kupitia Mpango wa Kilimo Kwanza.
Kwa upande wake, Kariati alisema mpango huo utamuwezesha Mtanzania yoyote kupata zana za kilimo ikiwemo matrekta popote alipo.
Alisema katika wilaya za Kondoa, kila kijiji kitapatiwa trekta tano na kwamba, mpango huo umeanza kwenye wilaya za Kongwa, Kondoa, Chemba na Kiteto.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru