Thursday, 13 February 2014

Ujenzi wa madarasa 67 kukamilishwa.

NA WILLIAM SHECHAMBO

SERIKALI inaendelea na ujenzi wa madarasa 67 katika Manispaa ya Ilala, ili kupunguza idadi ya wanafunzi waliokosa nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza.
Madarasa hayo yanajengwa kwenye shule 10 za manispaa hiyo na yako katika hatua za mwisho kukamilishwa.
Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Ilala, Violet Mlowosa, alisema jana kuwa, hatua hiyo imechukuliwa ili kuwasaidia wanafunzi kupata haki ya msingi ya elimu kwenye shule walizochaguliwa.
Alizitaja shule hizo kuwa, Mchanganyiko, Binti Mussa, Juhudi, Pugu Stesheni, Majani ya Chai, Ulongoni, Magoza, Ugombolwa, Zawadi na Msimbazi.
Violet alisema ujenzi umezingatia uwepo wa eneo kwenye shule husika na mahitaji kutokana na idadi ya wanafunzi wasio na madarasa.
Ofisa huyo alisema utaratibu huo ni endelevu kwa mujibu wa serikali kuu, hadi itakapohakikishwa tatizo la uhaba wa madarasa limemalizwa.
Alisema changamoto inayoikabili manispaa katika taaluma ni walimu wa sayansi, hususan masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu.
Violet alisema vitabu si tatizo katika manispaa hiyo kwa kuwa serikali imejitahidi kukabiliana na tatizo hilo kwa kutoa fedha za ununuzi wa vitabu.
Aliwataka wazazi kutoa kipaumbele katika elimu ya watoto wao kwa kuwa elimu si jukumu la serikali pekee.
Ofisa huyo aliwaomba wazazi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya elimu kwa kuchangia michango michache shuleni, ikiwemo ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru