Wednesday 25 March 2015

‘Vyama vingi vya ushirika vimejaa walaji’



CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM), kimesema vyama vingi vya ushirika hapa nchini vimejaa walaji na hivyo wananchi walio wengi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao na vyama hivyo kufa hovyo.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mabogini, katika Wilaya ya Moshi Vijijini.
Kinana alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la vyama vya ushirika kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ya watu hapa nchini.
Alisema pamoja na ongezeko hilo, bado baadhi ya vyama hivyo vinaongozwa na wajanja na walaji.

"Nataka niwaambie ndugu zangu ninyi ambao mna ushirika wenu wa wakulima wa mpunga ni lazima kuwa makini katika kuchagua viongozi, msichague kiongozi ambaye hana shamba katika umoja wenu huu," alisema Kinana.


Kinana alisema endapo mtu ambaye si mkulima wa mpunga, akichaguliwa  kuongoza ushirika huo, atakuwa hana uchungu na mali za ushirika.
Aidha katibu mkuu aliujia juu uongozi wa Halmamshauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini kwa kushindwa kufikia malengo ya mradi wa kilimo cha mpunga  Mabogini.
Alisema mradi huo wa kilimo cha mpunga ulifadhiliwa na serikali ya Japan miaka 30 iliyopita kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mpunga, lakini mpaka sasa haujafikia lengo.

"Mradi huu ulikuwa na lengo maalum la kuongeza uzalishaji wa zao hili la mpunga, lakini leo ni miaka 30 toka uanzishwe,  kuna hekta 600, lakini wakulima waliopo katika mradi huu ni 3000, sasa tija iko wapi hapa?" alihoji Kinana.

Aliushangaa uongozi huo kuomba fedha zaidi ya sh. milioni 800, wakati hakuna tija yoyote katika mradi huo.

 “Hapana, lazima tuwe na maswali magumu ya kujiuliza,” alisema Kinana.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru