Thursday 5 March 2015

Bunge laitaka serikali kulipa fidia Kipunguni



NA EMMANUEL MOHAMED
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuharakisha malipo ya fidia kwa wananchi wa eneo la Kipunguni, Dar es Saalam kabla ya kuanza kwa vikao vya Bajeti vya Bunge.
Imesema kuendelea kucheweleshwa kwa juhudi za kulipa fidia hiyo inahatarisha kusitishwa kwa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Awali, wananchi wa eneo hilo walitakiwa kulipwa kiasi cha sh. bilioni 11, lakini kutokana kuchewelewa huko na mabadiliko ya taratibu ya sheria ya mpya ya fidia ya ardhi mwaka 1997 imeongezeka na kufikia sh. bilioni 18.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Juma Kapuya alisema deni hilo ni kubwa na kwamba kuchewelewa kulipwa pesa hiyo kutachangia kuanza kuteteleka kwa utekelezaji wa mradi huo.
Kapuya alisema kamati hiyo itajitahidi kufanya mawasiliano ya karibu na Serikali ili kutafuta pesa hizo na kuanza kuwalipa kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleman Suleiman, alisema deni hilo ni miongoni mwa changamoto zinazoikumba utekelezaji wa mradi huo.
Mbali na hilo, pia utafiti unaonesha kuwa ifikapo 2020, miaka mitano kuanzia sasa abiria watakao kuwa wanatumia kiwanja hicho watakuwa zaidi ya milioni tano hivyo changamoto kubwa ni kuunganishwa kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza na ya pili kwa pamoja.

“Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha deni hilo linalipwa kwa wakati asilimia 15 ya gharama za mradi inalipwa na TAA kupitia tozo la abiria ambayo hupitia hazina na kurejeshwa huku lakini bado pesa hizi zinachelewa na kuletwa kidogo kuliko makusanyo mpaka sasa tumeshawalipa bilioni moja tu,” alisema.

Naye Zerina Madabida, aliwataka TAA kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo TRA,Hazina na mashirika mengine ya Serikali ili kuharakisha fidia hiyo na kuondokana na usumbufu huo.
Zalina alisema  kuendelea kwa tabia za kuchelewesha fidia inachangia kuharibika kwa miradi kama hiyo yenyec faida kubwa kwa taifa ikiwemo barabara, viwanja vya ndege  na majengo.
Aidha, kamati hiyo imeisifia hatua inayoendelea kwa ujenzi huo ambao unagharimu sh. bilioni 518, huku awamu ya kwanza unagaharimu bilioni 293 na awamu ya pili itagharimu sh. bilioni 225.
Pesa hizo ni mkopo kutoka benki ya HSBC ya uingereza kwa asilimia 85 kwa dhamana ya serikali ya Uholazni kupitia Export Credit Agency na Benki ya CRDB kwa asilimia 15.
Asilimia 30 ya ujenzi huo itajikita katika majengo ya kibiashara ikiwemo maduka na hoteli ili kuasaidia kukua kwa uchumi wa taifa na kukua kwa uchumi kwenye sekta ya anga pia itawanufaisha watanzania katika fursa ya ajira.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru