Tuesday 17 March 2015

‘Vidhibiti kesi za mihadarati vipo’


SERIKALI imesema ipo sheria na utaratibu maalumu wa kusimamia vidhibiti vya kesi zinazohusu dawa za kulevya na mauaji.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni mjini Dodoma hapa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu, wakati akijibu swali la nyongeza la Rukia Kassim Ahmed (Vita Maalumu-CUF).
Mbunge huyo alitaka kujua zinakopelekwa dawa za kulevya alizokamatwa nazo mshitakiwa mara kesi husika inapomalizika.
“Nataka kujua dawa wanazokamatwa nazo watuhumiwa hupelekwa wapi au huwa zinatumika tena, tunataka tuzione zikiharibiwa,” alisema.
Naibu Waziri Ummy alisema mambo yote kuhusu kesi hizo hufanyika kwa kuongozwa na sheria na kufuata taratibu mahususi za kisheria.
Aidha, alisema adhabu kuhusu kosa hilo zinazotolewa kwa wale wanaothibitika kutenda kosa na si vinginevyo.
Ummy alisema kifungu cha 327 cha sheria ya mwenendo wa makosa  ya jinai, Sura ya 20 kinatamka kwamba mtuhumiwa ataanza kutumikia kifungo chake siku hukumu ilipotolewa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru