Wednesday 9 July 2014

Dovutwa: Slaa, mkewe wote ni makapi ya CCM



  • Msomi ainanga CHADEMA

NA MOHAMMED ISSA
MWENYEKITI wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa amemvaa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbord Slaa na kumtaka ajitokeze hadharani kufafanua tatizo la msingi la Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia, ameshangazwa na kauli iliyotolewa na Dk. Slaa kuwa, CHADEMA haitasubiri wanachama watakaoachwa na CCM, kwenye uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu ujao, wakati yeye na mkewe ni makapi ya CCM.
Dovutwa amesema Dk. Slaa alitokea CCM na kwamba, anatakiwa kuueleza umma ubaya wa Chama unatokea wapi wakati alilelewa ndani ya CCM na hatimaye kupata umaarufu kabla ya kudondoshwa kwenye kura za maoni.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Dovutwa alisema anashangazwa na kauli hiyo ya Dk. Slaa wakati alijifunza siasa ndani ya CCM.
“Huyu Dk. Slaa katokea CCM, mama watoto wake alitokea CCM, kwa hiyo wote hawa ni makapi ya CCM. Au anataka kutuambia kuwa ubaya wa CCM, umeanza leo wakati yeye kaanzia huko huko,” alisema Dovutwa, ambaye aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2010 na kushindwa na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema ni vyema Katibu Mkuu huyo wa Chadema ajitokeze hadharani na kueleza tatizo la msingi la CCM hadi kusukumwa kutoa kauli hizo ambazo hazina mashiko zaidi ya kuuhadaa umma.
Dovutwa alisema inawezekana Dk. Slaa alitoa kauli hiyo kwa sababu ameshapata alichokuwa akikihitaji na anataka wenzake wasipate.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema CHADEMA haijaimarika kama Dk. Slaa anavyofikiria.
Alisema hata viongozi wengi wanaochagulika wanatoka ndani ya CCM na sio chama kingine cha siasa.
Dk. Bana alisema vyama vya upinzani vinahitaji kuimarisha uongozi wao kabla ya kuzungumzia chama kilichopo madarakani.
Alisema Dk. Slaa ametoa kauli hiyo akidhani chama chake kimeimarika, jambo ambalo ni tofauti na anavyofikiria.
Juzi, Dk. Slaa aliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema mara hii chama chake hakitakuwa tayari kuwapokea wanachama wanaotoka CCM.
Alisema kutokana na tamaa ya kuingiza watu wengi kwenye Bunge, vyama vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwapokea wanachama wa CCM wanaoshindwa kwenye kura za maoni na baadaye kuwapa nafasi ya kugombea ubunge na kwamba safari hii hawatakuwa tayari kufanya hivyo.
“Tulishasema kwamba ngazi zozote hata ngazi za udiwani au ubunge, hatutasubiri makapi yanayotokea CCM ndiyo yaje kwetu,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru