Thursday 17 July 2014

Mbowe ashindwa kufika mahakamani


Na William Paul, Hai
MAHAKAMA ya Wilaya ya Hai, jana ilishindwa kuendelea na kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, anayetuhumiwa kumshambulia mwangalizi  wa ndani wa uchaguzi mkuu.
Ilielezwa kuwa sababu ya kutoendelea kwa kesi hiyo ni mshitakiwa kutofika mahakamani.
Ilidaiwa kuwa, Mbowe alishindwa kufika mahakamani kutokana na kuharibika kwa gari alilokuwa akisafiria.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi, Denis Mpelembwa, wakili wa utetezi, Issa Rajabu,  alidai mahakamani  kuwa mshitakiwa alishindwa kufika kutokana na gari lake kupata hitilafu alipokuwa akienda uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Mteja wangu amechelewa kufika mahakamani kutokana na gari alilokuwa akisafiria kuelekea uwanja wa ndege kuja mkoani hapa, kuharibika na kusababisha kuchelewa ndege aliyokuwa aje nayo,” alidai Rajabu.
Wakili Rajabu alidai katika kesi hiyo, upande wa utetezi unategemea kupeleka mahakamani  mashahidi wawili, akiwemo mshtakiwa na Clement Kwayu.
Pia  hatakuwa na vielelezo vyovyote vya msingi ambapo watatumia ushahidi wa kiapo.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Agosti 18, mwaka huu.
 Mwenyekiti huyo, anakabiliwa na kesi ya Kumshambulia mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi kwa kupata kura  28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, 
Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru