Wednesday 30 July 2014

Wanunua mashine za kupakilia miwa


Na Igamba Libonge, Kilombero
CHAMA cha Wakulima wa Miwa cha Msolwa Ujamaa (MUCGA), wilayani Kilombero kimenunua mashine mbili za kupakilia miwa zenye thamani ya sh. milioni 264.8.
Chama hicho pia  kwa mwaka huu kinatarajia kununua magari sita yenye thamani ya sh. milioni 400 kwa ajili ya kusombea miwa ya wanachama na kujenga ofisi mpya itakayowagharimu sh. milioni 250.
Hayo yamesemwa juzi na Mwenyekiti wa MUCGA, Sebastian Sangilindege, alipokuwa akisoma taarifa ya chama katika mkutano mkuu. Alisema hayo ni mafanikio makubwa ya chama licha ya kuanzishwa kwake mwaka 2009. 
Sangilindege alisema ununuzi wa mashine hizo hizo umerahisisha kupakiwa kwa wingi miwa ya wanachama kwa kuwa awali miwa mingi ilibaki mashambani. Pia alisema ununuzi wa magari utafanikisha kumalizwa kusombwa kwa miwa yote iliyokatwa katika mashamba.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na chama kurekebisha miundombinu ya barabara hasa sehemu korofi  ambazo zilikuwa hazipitiki kwa urahisi, kuokoa miwa mingi iliyoungua kwa ajali na kuzuia milipuko ya moto na kuwapatia pembejeo za kilimo wanachama wasiokuwa na fedha taslimu na baadaye kukatwa asilimia 10.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru