Wednesday 23 July 2014

Kigogo kortini kwa uhujumu uchumi


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Mbeya, imempandisha kizimbani, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya Mbeya, Gerishon Bwire.
Bwire anakabiliwa na makosa matatu tofauti, ambayo ni kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake, ubadhirifu na kuisababishia hasara mamlaka.
Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Nimrod Mafwele, alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa Mbeya, James Mhanusi, kuwa Bwire alifanya makosa hayo  Mei mwaka jana, akiwa ni mtumishi wa umma.
Mafwele alidai katika shitaka la kwanza, Bwire alitumia nyaraka za serikali kumdanganya mwajiri wake ambaye ni halmashauri ya wilaya ya Mbeya na kujipataia fedha kinyume cha kifungu 22 cha sheria ya TAKUKURU namba 11 ya mwaka 2007.
“Mshitakiwa akiwa ni mhasibu wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, alitumia risiti yenye namba 0009, iliyoandikwa jina la Rich & Mrs Mufat Decoration na kuidhinisha malipo ya mapambo yenye thamani ya sh. 1,350,000 wakati si kweli,” alidai Mafwele.
Alilitaja kosa lingine kuwa ni ubadhirifu , kinyume cha kifungu cha 28(1) namba 11 cha mwaka 2007, ambapo mshitakiwa  alijipatia kiasi cha sh. 1,350,000 alichokabidhiwa na halmashauri ya wilaya ya Mbeya.
Katika shitaka la tatu, mshitakiwa huyo anadaiwa kuisababishia hasara mamlaka kinyume cha vifungu namba 10(1),(i),57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi namba 200,  iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo halmashauri ilipata hasara ya sh. 1,350,000.
Mshtakiwa alikana mashitaka yote huku huku upande wa mashitaka ukidai kukamilisha upelelezi na  kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.
Kesi iliahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu kwa ajili kusikiliza maelezo ya awali.
Hivi karibuni TAKUKURU mkoani hapa, iliwafikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Upendo Sanga  na watumishi wengine wanne kwa kosa la kuhujumu uchumi, ambapo kesi hiyo bado inaendelea.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru