Wednesday 23 July 2014

Sita mahakamani kwa matukio ya ugaidi



  •  Ulinzi waimarishwa, wake wapigwa ‘stop’

NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
ALIYEKUWA Imamu wa Msikiti wa Quba, Arusha, Jafari Lema na wenzake watano, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha, wakikabiliwa na mashitaka manne ya ugaidi.
Katika mashitaka hayo, watuhumiwa wanadaiwa kuhusika na tukio la kulipua bomu katika mgahawa wa Vama na kuwajeruhi watu saba.
Mbali na Lema, washitakiwa wengine ni Shaaban Mmasa, Athumani Mmasa, Mohamed Nuru, Abdul Mohamed na Said Temba.
Wakili wa Serikali Augustino Kombe,  akishirikiana na Felix Rwetukia, waliwasomea washitakiwa hao mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Rose Ngoka.
Shitaka la kwanza la kula njama linawahusu Mmasa na Lema, ambao wanadaiwa kuwa kati ya Februari na Julai, mwaka huu, walikula njama ya kutenda kosa la ugaidi.
Katika shitaka la pili, washitakiwa  wanadaiwa Julai 7, mwaka huu, usiku, katika mgahawa wa Vama, walilipua bomu  la kutupwa kwa mkono, katika mgahawa wa Vawa  na kusababisha madhara kwa watu saba.
Mmasa na Lema wanadaiwa pia kugawa mabomu kwa ajili ya kutekeleza tukio la ugaidi.
Katika shitaka la nne la kufadhili fedha kwa ajili ya ulipuaji wa bomu kwenye mgahawa huo, linawakabili Lema, Mohamed na Temba,  ambao wanadaiwa walifadhili fedha kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Washitakiwa hao hawautakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka  kusikiliza shauri hilo.
Wakili Kombe alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 6, mwaka huu na washitakiwa walirudishwa rumande.
Wakati watuhumiwa hao wanafikishwa mahakamani jana, ulinzi uliimarisha  katika eneo la mahakama.
Washitakiwa  walipelekwa mahakamani wakiwa katika magari mawili tofauti  ambayo yalitembea barabarani kwa kupiga ving’ora na kuomba njia.
Kutokana na kesi hiyo, mahakama ililazimika kuendesha kesi nyingine asubuhi sana  kwa kuhofia mkusanyiko mkubwa wa watu mahakamani hapo.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani saa  7.26 mchana, ambapo kulikuwa kimya huku kukiwa na watu wachache.
Katika hatua nyingine, wanawake watatu walitimuliwa mahakamani hapo baada ya kujitambulisha kuwa ni wake wa washitakiwa.
Wanawake hao walidai walifika mahakamani kwa ajili ya kuwapa waume zao nguo za kubadilisha wawapo lupango.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru