Wednesday 13 August 2014

ACT-Tanzania kuiburuza CHADEMA mahakamani


NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.
 CHAMA Cha ACT-Tanzania mkoa wa Mbeya, kimesema kitaiburuza mahakamani CHADEMA kwa tuhuma za wizi wa kadi 50 na bendera za chama hicho, vilivyoibwa kwenye ofisi yake iliyoko Uyole jijini Mbeya.
Imeelezwa kuwa tayari ACT-Tanzania imeshakamilisha taratibu za kufungua kesi hiyo na mwanasheria wa chama hicho kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, anatarajiwa kuwasili leo (jana).
Mratibu wa ACT-Tanzania mkoa wa Mbeya, Bahati Rongopa, aliyasema hayo jana wakati akielezea kuhusu habari iliyotoka kwenye gazeti moja la kila siku (siyo UHURU), likiwa na kichwa cha habari ‹ACT Wakwama Mbeya›.
Rongopa alisema habari zilizoandikwa na gazeti hilo hazina ukweli wowote, kwani kadi 50 na bendera vilivyokabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, viliibwa katika mazingira tata kwenye ofisi ya chama hicho.
Akifafanua zaidi, Rongopa alisema Agosti 8, mwaka huu, walifanya sherehe za ufunguzi wa ofisi yao, inayohudumia mkoa wa Mbeya, iliyoko eneo la Uyole jijini Mbeya na kuhudhuriwa na wanachama mbalimbali.
Aliongeza pia kuwa wenyeviti wa CHADEMA wa kata, Silipa Tenga (Isanga) na Zuber Kilale (Iwambi), pamoja na mwanachama mwingine, Thobias Sebastin, walihudhuria sherehe hizo, licha ya kuwa hawakuwa na mwaliko.
«Katika ufunguzi huo, tulikabidhi kadi kwa wanachama wapya, akiwemo mwana-CHADEMA, Geofrey Sanga.Wenyeviti wa CHADEMA wa kata nilizokueleza wao muda wote walikuwa wanarandaranda, kwenye ofisi zetu na sisi hatukuwatilia maanani kwani tunawatambua,» alisema Rongopa.
Aliongeza kuwa siku ya pili walipofungua ofisi, ndipo walipopigwa na butwaa baada ya kubaini kadi 50 zilizokuwepo juu ya meza, zilikuwa zimetoweka na baadaye walipata taarifa kuwa hata bendera yao iliyokuwa imewekwa eneo la njia panda-Uyole, imeondolewa.
Mratibu huyo wa ACT-Tanzania mkoa wa Mbeya, alisema baadaye walibaini kuwa kadi hizo zilikuwa zimechukuliwa na Sebastian, kwani aliingia ofisini humo jana yake na alipotoka hakuonekana tena hadi sherehe zinamalizika.
Rongopa alisema walikwenda kuripoti tukio hilo la kuibwa kadi 50 pamoja na bendera ya chama katika kituo kidogo cha polisi Uyole na kupewa  UY/RB.1815.
Aliongeza kuwa wiki moja kabla ya ufunguzi wa ofisi hizo, Sebastian alikwenda kuomba kujiunga na ACT-Tanzania, lakini walimkatalia baada ya kubaini mwenendo wake si mzuri na hilo lilifanyika chini ya kamati ya muda.
Rongopa alisema wamesikitishwa na kitendo cha CHADEMA Mbeya Mjini, kupitia gazeti hilo, kudai kadi hizo zilikuwa zimetupwa na wana-CHADEMA waliokuwa wameshawishiwa kujiunga na ACT-Tanzania.
“Kama kweli viongozi wa CHADEMA wana uhakika na hiki walichokiandika gazetini, tunawataka wazilete kadi hizo zaidi ya 100 wanazodai zilitupwa nje ya ofisi yao kwani tunao uhakika kadi zilizoibwa ni 50 tu na zilikuwa hazina majina,” alisema Rongopa.
Alisema wamesikitishwa na kitendo hicho kwani huo ni uchochezi wa vurugu kushusha bendera ya chama kingine cha siasa,kuiba kadi  na kisha kutaka kuudanganya umma kuwa zilitupwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru