Thursday 7 August 2014

Pinda atoa agizo kubadili wafugaji

Na Happiness Mtweve, Dodoma
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameagiza watendaji kuhakikisha wanabadili fikra za wafugaji ili kuwawezesha kuendesha ufugaji wa kisasa na wa kibiashara, badala ya kuendelea na ule uliozoeleka, ambao hauna tija kubwa katika kukabiliana na umasikini.


Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua mashindano ya Maonyesho ya Mifugo, ambayo kitaifa yanafanyika Dodoma katika viwanja vya Maonyesho ya Nanenane vilivyopo Nzuguni mjini hapa.
Pinda alisema ni lazima wizara ibadili fikra za wafugaji kwa maendeleo ya taifa.
Alisema iwapo agizo hilo litasimamiwa kwa umakini kwa kutoa elimu ya ufugaji bora na wa kisasa kwa wafugaji nchini, itawawezesha wafugaji kujikwamua na umasikini na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa.
Alifafanua kuwa bado hitaji la mifugo bora hapa nchini ni changamoto kubwa licha ya Tanzania kuwa na idadi nyingi ya mifugo, lakini pia mchango wake kwa pato la Taifa ni mdogo.
Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus  Kamani, alisema kwa sasa wamekamilisha ujenzi wa maabara ya uhamilishaji katika wilaya ya Mpwapwa.
Alisema lengo la kujenga maabara hiyo ni kupata mbegu bora ya mifugo na kuongeza wigo wa huduma hiyo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakuomba utusaidie kuongea na taaisis za fedha ili ziwe na sera moja ya fedha na kuwawezesha wafugaji kukopesheka,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru