Thursday 28 August 2014

Washirikiana na wateja kuhujumu TANESCO


Clarence Chilumba, Masasi
UKOSEFU wa maadili, uaminifu na kuwapo kwa ubinafsi wa baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani  Masasi, vimesababisha kushindwa kudai zaidi ya sh. bilioni moja kutoka kwa wateja. 
Hayo yalibainishwa na Meneja wa TANESCO Masasi, Basilius Kayombo, alipozungumza na Uhuru jana ofisini kwake, kuhusu oparesheni kata umeme kwa wateja sugu inayoendelea wilayani humo. 
Alisema ndani ya shirika kuna baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi kwa kukiuka maadili, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu hivyo kusababisha kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Meneja huyo alisema shirika kwa sasa linadai zaidi ya sh. bilioni mojaambazo ni malimbikizo ya madeni kutoka kwa wateja, zikiwemo  taasisi binafsi, za umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali na watu binafsi.
Alisema baadhi ya wateja wamekuwa wakilipa ankara zao za umeme kwa kutumia njia ambazo si sahihi kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi waminifu na wanaofanya kazi ambazo haziko kwenye mamlaka yao.
Kwa mujibu wa Kayombo, hatua hiyo imesababisha hasara kubwa kwa shirika pamoja na migogoro na malalamikko kutoka kwa wateja bila ya sababu ya msingi.
Kayombo alisema kupitia oparesheni inayofanywa kwa ushirikiano na kikosi cha kanda ya kusini cha shirika hilo, wamebaini kuwapo kwa madeni mengi yaliyosababishwa na uzembe na urasimu wa baadhi ya wafanyakazi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wateja kuacha mara moja kushirikiana na wafanyakazi hao wanaolihujumu shirika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru