Wednesday 13 August 2014

Vijana 10 kusomea mafuta na gesi China


NA SELINA WILSON
VIJANA 10 wa Kitanzania waliopata ufadhili wa kusomea shahada ya uzamili na uzamivu katika masuala ya gesi na mafuta, wamekabidhiwa nyaraka muhimu ikiwemo viza.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa serikali kuhakikisha inazalisha wataalamu wazawa wa kutosha katika sekta ya mafuta na gesi, ambao watashiriki kikamilifu.
Nafasi hizo zilitolewa na serikali ya China baada ya kuombwa na Tanzania, ikiwa ni mkakati wa kutimiza lengo hilo la kuwa na wataalamu wazawa wa kutosha.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitabu hivyo pamoja na fomu za viza, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema nafasi hizo zimepatikana kwa ushindani baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari.
Alisema vijana tisa kati ya 46 wamechaguliwa katika masomo ya shahada ya uzamili na mmoja  kati ya wanne walioomba nafasi hizo, anakwenda kusomea shahada ya uzamivu.
Profesa Muhongo aliwataja waliopata nafasi hizo na vyuo kwenye mabano kuwa ni Erasma Rutechura (Ocean University of China) ngazi ya shahada ya uzamivu.
Wengine wanaokwenda kusomea shahada ya uzamili katika fani mbalimbali za mafuta na gesi ni Abel Masanja (Chuo Kikuu cha Sayansi ya Jiolojia (Huadong), Beatrice Tubuke na Kunugula Lwitakubi (Chuo Kikuu cha Petroli China).
Pia wamo Faustine Matiku (Chuo Kikuu cha Uhai) fani ya uhandisi wa mito na bahari, Alvin Mulashani, Nigel Kimaro na Herbert Msangi (Chuo Kikuu cha Xi`an Shiyou).
Wengine ni Ansila Kiusa (Chuo Kikuu cha Sayansi ya Jiolojia Wuhan) na Victor Mgalula (Chuo Kikuu cha Petroli Beijing).
Profesa Muhongo aliwataka vijana hao kukamilisha taratibu zingine kwa wakati ili waweze kuondoka mapema na kuanza masomo mwezi ujao nchini China.
Katika kuhakikisha serikali inajiimarisha katika gesi na mafuta, alisema wanatarajia kuwa na wataalamu wasiopungua 300 wa fani za mafuta na gesi ifikapo mwaka 2020.
“Tanzania inakwenda kwenye uchumi wa gesi. Gesi iliyogunduliwa ni futi trilioni 50.5 za ujazo, ni sawa na mapipa bilioni 10 na kwa utafiti unaoendelea kusini mwa Mtwara, huenda tukavuka trilioni 150 za ujazo, hivyo ni lazima tuwekeze kwenye utaalamu,” alisema.
Alisema hapa nchini wanatarajia kuwa na wataalamu zaidi ya 60 ifikiapo mwaka 2016, ambao baadhi yao wapo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwakani watapelekwa wengine  Canada na Marekani.
Awali, akizungumzia ufadhili wa wanafunzi hao 10, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisema walishindanishwa kwa sifa na kati ya 46, walipatikana 20 wenye sifa ambapo 10 walipata nafasi hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru