Wednesday 6 August 2014

Kazi imeanza



  • Sitta acharuka, arusha makombora UKAWA
  • Aonya hawana uhalali mbele ya Watanzania
  • Dk.Kigwangalah naye amtolea uvivu Warioba

Na Waandishi Wetu
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amewapasha wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa, hawana uhalali wala hadhi kuliko wajumbe wengine.
Amesema jambo la kutofautiana katika kujadili Rasimu ya Katiba Mpya ni la kawaida na kwamba, kamwe vikao vya bunge hilo havitasitishwa kwa sababu ya wachache kususa.
Amesema masuala na matakwa ya kisheria yatazingatiwa katika kufikia hatma ya upatikanaji wa Katiba mpya, ambayo imekuwa ikijenga imani na matumaini mapya kwa Watanzania.
Alitoa msimamo huo jana wakati akifungua kikao cha bunge hilo, ambapo alisema hoja za uzushi na upotoshaji zinazozungumzwa nje, haziwezi kukwamisha shughuli za bunge hilo.
Alisema kutokana na tofauti ya kimtazamo na maoni, ndio sababu umewekwa utaratibu wa kupiga kura pamoja na ule wa maridhiano.
Sitta alisema utaratibu mpya ulioanza kujengwa na baadhi ya viongozi kususia mijadala halali ya Bunge na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja, hauna nafasi katika jamii inayojali amani na upendo.
‘’Kuna mengi yanazungumzwa kujadili mchakato wa Katiba Mpya nje ya bunge hili, ni muhimu wahusika wapunguze jazba, chuki na upotoshaji na Bunge Maalumu lisaidiwe kwa mawazo chanya ili limalize kazi yake,’’ alisema Sitta.
Kuhusu tuhuma zinazotolewa kuwa bunge hilo linajadili mambo nje ya Rasimu ya Katiba, Sitta alisema hazina ukweli wowote na kuwa msingi wa majadiliano hayo ni kuipitia Rasimu hiyo.
Hata hivyo, alisema kiutaratibu wajumbe wana haki ya kurekebisha baadhi ya maeneo iwapo wataona inafaa na kuwa si kosa kufanya hivyo.
Sitta alisema kwa kaida Rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu zaidi, likiwemo Bunge Maalumu la Katiba.
“Anayekabidhiwa Rasimu anayo haki na mamlaka ya kuirekebisha, vinginevyo hakuna sababu ya kuijadili,’’ alisema Sitta.
Rasimu ni mali ya Bunge
Mjumbe wa bunge hilo, Hamad Rashid Mohamed, alisema jambo lolote likishakabidhiwa kwa Bunge, ni mali ya Bunge, hivyo wanaweza kulifanyia lolote katika kuliboresha.
Hamad, ambaye ni Mbunge wa Wawi (CUF), alisema kwa mujibu wa taratibu zote duniani, jambo hilo linakuwa ni mali ya Bunge, ambalo pia ni chombo kinachowawakilisha wananchi, kwa hiyo hakuna kosa lolote kufanya baadhi ya marekebisho au maboresho ya rasimu .
Kigwangala na Jaji Warioba
Dk. Hamis Kigwangalah, akichangia bungeni jana, alimtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuacha kuingilia mchakato huo.
Alisema kazi ya Jaji Warioba na Tume yake ilishamalizika na kwamba, kilichobaki kwa sasa ni nafasi ya wajumbe wa bunge hilo kutimiza wajibu wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.
Alisema amekuwa akishangazwa na baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo kuendelea kutetea maoni yao huku wakitoa kauli zenye kuudhi dhidi ya wajumbe wa bunge hilo.
“Inashangaza, wakati wao walipokuwa wakifanya kazi sisi tulinyamaza, lakini sasa tunafanya kazi wao wanaingilia, kila siku kazi ni kuliponda Bunge, ni vyema Mwenyekiti ukae chini na wazee wenzako na kuzungumza nao ili waache bunge lifanye kazi. Kila kukicha kwenye midahalo kutetea maoni yao na kuzungumza maneno ya kejeli, hii si sawa kabisa, kaa na wazee wenzako mzungumze,’’ alisema.
Aidha, aliiomba Kamati ya Kanuni kuweka kanuni itakayomshauri Rais Jakaya Kikwete kufuta uteuzi wa wajumbe watakaosusa kuhudhuria vikao vya Bunge hilo.
Watoto wa vigogo kusoma nje
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), umesema kuna mambo mengi ya kujadiliwa katika mchakato wa Katiba Mpya kuhusiana na elimu.
Pia umependekeza kuwepo kwa sheria katika Katiba Mpya ijayo, inayokataza watoto wa vigogo kwenda kusoma nje ya nchi kama chachu ya kuboresha elimu nchini.
Mtandao huo umesema kushuka kwa elimu nchini ni matokeo ya mambo mengi, ikiwemo watoto wa wakubwa kupelekwa kusoma nje huku wale wa masikini wakiendelea kupambana na changamoto zilizopo kwenye elimu nchini.
Katibu Mkuu wa TSNP, Alphonce Lusako, alisema mjini Dar es Salaam, jana, kuwa wamependekeza kuongezwa kwa ibara ya 21, katika sura ya 3 (a), itakayohusu maadili ya viongozi .
“Tunapendekeza iwepo sheria itakayowabana viongozi kuwasomesha watoto wao katika shule na vyuo vya ndani badala ya kuwakimbiza nje ya nchi. Wakiwepo hapa, watajenga uzalendo na hata kuwa wepesi kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoukabili mfumo wa elimu nchini,” alisema.
Pia aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuweka kando itikadi na misimamo ya vyama vyao, badala yake waungane kutengeneza Katiba ya Watanzania.
“Tunawaomba CCM, UKAWA, Tanzania Kwanza na wajumbe wengine kufahamu kuwa, kushindwa kwa mchakato huu sio kushindwa kwa chama chochote cha siasa bali ni Watanzania ndio watakuwa wameshindwa,” alisema.
Mwigulu na posho
Kwa upande wake, Mwigulu Nchemba, alishauri bunge hilo kuendeshwa kwa mujibu wa bajeti na wabunge wasiowajibika wabanwe kikamilifu.
Alisema ni muhimu kwa uongozi wa Bunge kujiridhisha katika kuhakikisha wajumbe wanaolipwa posho ni wale waliohudhuria vikao na pia kuorodhesha wajumbe ili kufahamu idadi.
Pia alieleza umuhimu wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa ajili ya kuendesha shughuli za Bunge hilo ili kuokoa muda na fedha za umma.
“Tuwabane wale wote wasiohudhuria ili wasilipwe posho kwa sababu hata vitabu vya dini vimesema asiyefanya kazi na asile,” alisema Mwigulu.
Naye Goodluck Ole Medeye, alisema anaomba mjumbe ambaye hakushiriki mjadala, asishiriki kupiga kura na ikiwezekana afutwe ujumbe wake.
Naye, Fahmi Dovutwa, alisema ni kebehi na dharau kwa vyama vya upinzani kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete alipozindua bunge hilo, alilenga kuharibu mchakato.
“Jamani tukubali Rais wetu ni smart, hawa walikuwa wanamtega, walitaka wamwambie andika hiki, futa hiki ili baadaye waje kusimama kusema rais amewaingilia. Hila na mchezo mchafu waliotaka kuufanya sasa umekwama,” alisema.
Wajumbe waapishwa
Katika bunge hilo, wajumbe watatu Ridhiwani Kikwete, Godfrey Mgimwa na Haroun Ali Seleman, waliapishwa kabla ya kuanza kwa bunge hilo. Wajumbe hao waliapishwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru