Thursday 28 August 2014

Jk Rais wa kwanza kufika Kibati


NA LATIFA GANZEL
RAIS Jakaya Kikwete ameweka historia ya kuwa rais wa kwanza kufika katika kata ya Kibati iliyoko Mvomero mkoani hapa.
Pia amekuwa kiongozi wa pili wa juu wa taifa kufika Kibati baada ya awali Mwalimu Julius Nyerere kufanya hivyo mwaka 1961 wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mara baada ya kuwasili Rais Kikwete, Mbunge wa Mvomero (CCM), Amos Makalla, alisema ujio wa Kikwete umekonga nyoyo za wakazi wa kata hiyo.
Makalla alisema kilio kikubwa cha wananchi wa kata hiyo kilikuwa kutaka  kumwona Rais na kwamba ziara yake hiyo imetoa jibu la hitaji hilo.
“Ndugu zangu wa Kibati kazi mliyonituma kuhakikisha Rais Kikwete anakuja katika kata yetu nimeitekeleza. Leo Rais Kikwete amefika na ameona kero zinazotukabili, bila shaka sasa zitatatuliwa,’’ alisema.
Makalla ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, alisema kero kubwa iliyokuwa ikiikabili kata hiyo ni kukosekana kwa barabara ambayo imepatiwa utatuzi baada ya serikali kujenga barabara inayopitika kipindi chote cha mwaka.
Hata hivyo, alisema barabara hiyo itaendelea kuboresha kwa kujengwa kwa kiwango cha lami na kukomesha kabisa kero ya usafiri wa barabara kwa vijiji vya kata hiyo.
“Zamani tulikuwa tunatembea muda wa saa tano hadi sita kufika Kibati lakini sasa huchukua saa 1.30 tu kufika hapa,’’ alisema.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema, kero nyingi tayari zimeshughulikiwa  zikiwemo za barabara, elimu afya na mawasiliano.
Alisema aliona umuhimu wa kufika katika kata hiyo kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi na kuahidi kurudi tena Juni mwakani kwa ajili ya kuzindua mradi wa umeme wa kata hiyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru