Thursday 28 August 2014

Zimamoto Mwanza yapigwa jeki


NA BLANDINA  ARISTIDES, MWANZA
KIKOSI cha Zimamoto mkoani Mwanza, kimepokea msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni mbili kutoka washirika wa maendeleo.
Msaada uliokabidhiwa ni buti jozi sita, majaketi 12, makoti 15, suruali 22, kofia ngumu 10, kofia za kawaida 10, fulana tano na ovaroli mbili kwa ajili ya utekeleza wa majukumu yao ya kazi.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto, Inspekta Augustine Magere, alisema kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu katika jiji la Mwanza, wanakabiliwa na changamoto nyingi za vitendea kazi.
Inspekta Magere, alisema kwa sasa jiji hilo lina magari manne ya zimamoto ambapo kati ya hayo  mawili yako uwanja wa ndege na mengine katikati ya jiji. 
Alisema magari hayo hayakidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu walioko mkoani hapa huku matukio ya moto yakitokea mara nyingi nje ya mji.
“Tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kutendea kazi, lakini tumewasiliana na marafiki zetu wa Wurzburg, Ujerumani na Tampere nchini Finland ili waweze kutusaidia. Leo hii hawa Wajerumani wametusaidia baadhi ya vifaa kiasi,” alisema Magere.
Magere alisema hayo wakati akikabidhiwa vifaa na mwakilishi wa afisa uhusiano wa jiji hilo, Idd Hussein, vilivyotolewa na jiji rafiki la  Wurzburg.
Alisema kutolewa kwa vifaa hivyo ni kutokana na urafiki wa majiji hayo mawili kwa kipindi kirefu, baada ya baadhi ya watumishi wa Zimamoto kupelekwa kujifunza mambo mbalimbali mwaka 2008.
Kwa upande wake, Hussein aliyekabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Jiji la Warzburg, alisema lengo ni kukiboresha kikosi hicho ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru