Wednesday 13 August 2014

Kiama cha wafanyakazi wa mizani chaja



  •  Watendaji TANROAD, madereva wa malori wawekwa kikaangoni

MOHAMMED ISSA NA 
MWAMVUA MWINYI
SERIKALI imesema itaingia mkataba maalumu na wafanyakazi wa mizani ya Vigwaza, Kibaha mkoani Pwani kwa lengo la kuwadhibiti ili wasiuchakachue na kupitisha magari yaliyozidisha mizigo.
Pia imewaonya baadhi ya watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, kuacha mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mbali na hilo, imewatangazia kiama madereva wa malori wanaozidisha mizigo na kuharibu barabara na kwamba tayari dawa yao imepatikana.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alisema hayo jana alipofanyaziara ya kukagua ujenzi wa mzani wa Vigwaza, ambao hadi kukamilika utagharimu sh. bilioni 10.1.
Alisema kabla ya mzani huo kuanza kazi, atamuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mussa Iyombe na Mtendaji Mkuu wa TANROAD, Mhandisi Patrick Mfugale, kuingia mikataba maalumu na watumishi wa mzani huo ili kuwadhibiti na kuhakikisha hawauchakachui.
Dk. Magufuli alisema kuanzia sasa serikali itahakikisha inawabana baadhi ya watendaji wa TANROAD wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na amewataka kuacha mara moja vitendo vya aina hiyo.
Alisema mzani huo utakuwa na alama maalumu ambapo gari likiwa umbali wa mita mbili, litabainika kama limezidisha uzito au la na kwamba gari ambalo litakuwa halijazidisha, litapita moja kwa moja bila ya kupima.
“Huu mzani ndio dawa pekee ya wanaozidisha mizigo na kufanya ujanjaujanja, utaondoa mzizi wa fitina na malalamiko yaliyokuwepo kwenye vituo vya mizani kwa muda mrefu,” alisema.
Ameagiza mtu yeyote atakayezidisha mizigo, atozwe faini kwa mujibu wa sheria bila ya kuonewa huruma.
“Sasa wasafirishaji wataipatapata hapa, atakayezidisha uzito ni faini kwenda mbele, nafahamu kuwa tunadili na watu wenye fedha nyingi, lakini lazima sheria zifuatwe ili kulinda barabara zetu,” alisema.
Waziri huyo alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kujenga barabara, hivyo haitavumilia kuona watu wachache kwa manufaa yao binafsi wanaharibu barabara hizo.
Alisema njia ya kuzilinda barabara zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ni kujenga mizani ya kisasa.
Dk. Magufuli alisema barabara nyingi zinaharibika kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuzidisha mizigo kwenye magari yao.
Alisema wanatarajia kujenga mizani mingine mitatu ya kisasa kwenye maeneo mengine ili kuwadhibiti wanaozidisha mizigo na kuondoa malalamiko yaliyokuwepo kwenye vituo vya mizani.
Waziri huyo alisema utafiti unaonyesha kuwa, asilimia 25 ya magari yanaharibu barabara kutokana na kuzidisha kiwango kikubwa cha mizigo.
Dk. Magufuli alishauri mizigo inayotoka katika bandari ya Dar es Salaam, ipakiwe kwenye treni mpaka Ruvu na ndio ianze kupakiwa kwenye malori ili kupunguza foleni.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi sasa wameshajenga kilomita 11,000, za barabara na kama zingejengwa kwenye nchi za Burundi na Rwanda, hata sehemu za kulima wangekosa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Iyombe, alisema mzani huo ni wa kisasa na wa kwanza kujengwa hapa nchini.
Alisema utakapokamilika utaondoa malalamiko ya rushwa yaliyokuwepo kwenye vituo vya mizani na kwamba dereva atakayezidisha uzito atajiona mwenyewe.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mfugale, alisema ujenzi wa mzani huo ulianza Juni, mwaka jana, na unatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Alisema mzani huo una uwezo wa kulipima gari zima ndani ya sekunde 30 hata kama lina urefu wa kiasi gani .

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru