Monday, 15 June 2015

Hispania yaridhishwa
na kazi ya  TASAF

SERIKALI ya Hispania imeridhishwa na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya mbalimbali nchini ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania  (TASAF).
Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya vijiji vya Wilaya ya  Bagamoyo kwa wanufaika wa mpango huo, Balozi wa Hispania nchini, Luis Cuesta Civis,  alisema mpango huo unaonyesha unatekelezwa kikamilifu na kwa mafanikio makubwa.
Alisema lengo la serikali ya Hispania na nchi nyingine wafadhili ni kuona umasikini unapungua kwa kasi nchini Tanzania na ikiwezekana kuutokomeza, ifikapo mwaka 2025.
“Tumeridhishwa na utekelezaji wa mpango, kwani tumepata  fursa ya kuzungumza na walengwa kutoka kaya masikini na kutudhihirishia manufaa yake,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa TASAF,Ladislaus Mwamanga, alisema mpango wa kunusuru kaya masikini na uhawilishaji fedha ni moja ya mipango ya serikali  katika kuhakikisha inapunguza wimbi la umasikini
Mwamanga alisema utekelezaji wa mpango huo umekuwa ukitekelezwa katika njia kuu mbili, ikiwemo mpango wa kunusuru kaya masikin na mpango wa utoaji wa ajira za muda.
Naye Mratibu Mkazi wa Shirika  Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo(UNDP),Alvaro  Rodriguez, aliipongeza jamii katika
maeneo waliyoyatembelea na kueleza kwamba kila penye mafanikio panahitaji mipango ya uhakika .

Alisema jambo kubwa ni kuweka dhamira  ya kweli  katika ushiriki na utekelezaji wa mpango huo, hivyo wanapaswa kuupiga vita umasikini kwa vitendo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru