Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Thursday 28 August 2014

Sekretarieti ya Ajira yawananga wasomi

  • Yasema wengi wanawasilisha nyaraka duni
  •  Wengine wamesoma vyuo visivyotambuliwa 
Na Mwandishi Wetu
WAHITIMU wengi wanaotuma maombi ya kazi serikalini hawajui taratibu za kufuata, hivyo kushindwa kunufaika na fursa hizo kutokana na kuwasilisha nyaraka zisizokithi vigezo, imeelezwa.
Pia baadhi ya waombaji hao wamekuwa wakiwasilisha vyeti vya elimu visivyokidhi viwango na wengine kusoma katika vyuo ambavyo havitambuliki na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kutokana na sababu hizo, baadhi ya wadau wamekuwa wakiitupia lawama serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kuwa imekuwa ikifanya upendeleo katika utoaji wa ajira kwa kushindwa kuwaita kwenye usaili walioshindwa kukidhi viwango mapema.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar er Salaam, jana, Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira,
Bi.Riziki Abraham
Riziki Abraham, alisema baadhi ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha nyaraka za kupotelewa na vyeti vya shule badala ya vyeti vya taaluma.
Alisema idadi kubwa ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha barua kutoka Jeshi la Polisi kuonyesha wamepotelewa vyeti hivyo ama kuharibika, jambo ambalo si sahihi.
Pia alisema baadhi ya waombaji hususan wa vyuo vya nje, wamekuwa wakiwasilisha vyeti vya taaluma visivyo na vigezo kumwezesha mhusika kupata ajira nchini.
Kutokana na matatizo hayo, serikali imewataka waombaji wenye matatizo katika vyeti vyao vya taaluma na taarifa zingine muhimu, kuwasiliana na mamlaka husika kwa msaada zaidi.
Wahitimu waliopoteza vyeti
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imewataka wahitimu waliopoteza, kuibiwa ama kuharibikiwa na vyeti vya taaluma, kutoa taarifa polisi kisha kuwasilisha taarifa hizo katika mamlaka zinazohusika kama Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kwa vyeti vya kidato cha nne na sita.
Kwa vyeti vya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na elimu ya juu ni TCU ili waweze kuelekezwa taratibu za kufuata ikiwamo kutangaza kwenye vyombo vya habari.
Hatua hiyo inalenga kumwezesha mhusika kupata vyeti vingine huku taarifa zake za kupotelewa zikiwasilishwa Sekretarieti ya Ajira kwa wakati.
Waombaji waliosoma nje
Wahitimu waliosoma nje ya nchi iwe ngazi ya sekondari ama vyuo vikuu, wanatakiwa kuwasilisha taarifa pamoja na vyeti vyao kwa mamlaka husika ili kuhakikiwa na kupewa barua za uthibitisho kuwa vyuo walivyosoma vinatambulika ama la.
Taarifa hizo zinapaswa kuwasilishwa NECTA, VETA, NACTE na TCU, ambazo ndizo zenye mamlaka ya kuthibitisha na kuwasilisha taarifa za mhusika katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira.
Utaratibu wa mwombaji kuwasilisha taarifa za kupotelewa vyeti kuwasilisha utambulisho wa matokeo ama nyaraka pindi anapoomba ajira, haukubaliki.
Wenye majina tofauti 
Kumekuwepo na baadhi ya watu kubadilisha majina kwa kutotumia ya utotoni, kubadili dini, kutumia ubini wa mume hali, ambayo imechangia kuwa na majina tofauti na cheti za kuzaliwa.
Kutokana na hilo, wanatakiwa kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuwasilisha maombi ya kazi kwa Sekretarieti ya Ajira.
Mikataba ya ajira kwa wastaafu
Abraham alisema kuwa serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuzuia wastaafu kuongezwa mikataba ya ajira ili kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini kupata ajira.
Alisema kwa sasa wastaafu waliopewa mikataba ya ajira serikalini ni asilimia 0.1 na kwamba, hilo limetokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete.
“Rais Kikwete aliagiza kupunguzwa kwa mikataba ya watumishi wa serikali waliostaafu ili kutoa fursa kwa vijana wapya kuingia kazini. Agizo hilo limeendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa na limepungua,” alisema.
Pia, alisema sekretarieti imeanza utaratibu wa kufanya makongamano katika vyuo mbalimbali  kuhamasisha vijana kuwa na mawazo ya ujasiriamali ili kujiajiri kwani fursa ya ajira ni ndogo nchini.
“Tunawataka pia kujitahidi kufanya vizuri katika masomo yao kwani, tunatarajia kuanza utaratibu mpya wa kuangalia viwango vya ufaulu,” alisema.

Vyama vya siasa vyatakiwa kuweka utaifa mbele

  • Vyaonywa maslahi ya vyama yataiweka nchi pabaya
NA KHADIJA MUSSA
VIONGOZI wa vyama vya siasa watakaokwenda kukutana na Rais Jakaya Kikwete, wametakiwa kuweka mbele masuala yanayohusu taifa na si misimamo binafsi ya vyama vyao.
Aidha wasomi nchini wamempongeza Rais Kikwete kwa kukubali kukutana na viongozi wa vyamaa hivyo vya siasa kwa kuwa ni ishara nzuri kwa kiongozi wa nchi kutokuwa na ubaguzi hata kwa watu wasiomuunga mkono.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Rais Kikwete kukubali kukutana na viongozi wa vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Viongozi hao waliazimia kutafuta nafasi ya kukutana na Rais Kikwete kwa lengo la kushauriana naye kuhusu mambo mbalimbali, ukiwemo mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, unaoendelea mjini Dodoma. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
TCD inaundwa na vyama vyenye uwakilishi bungeni, ambavyo ni CCM, CUF, CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na UDP. Mwenyekiti wa sasa wa TCD ni
MH.John Cheyo
John Cheyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda, alisema ni vyema viongozi hao wa vyama vya siasa watakapokwenda kukutana na Rais Kikwete, wabebe maslahi ya taifa na si ya vyama.
Mwakagenda alisema viongozi hao wanapaswa kuweka kando misimamo ya vyama vyao na badala yake waungane pamoja na kwenda kujadili masuala yanayohusu taifa.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya JUKATA, George Mollel, amesema hakuna sababu ya kufanyika kwa maandamano ya kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu hayana faida, badala yake watu wengi wasiokuwa na hatia wataumia na wengine kupoteza maisha.
Mollel alisema jana kuwa, badala ya kufanyika kwa maandamano, wanaotaka kuyafanya watumie hoja katika kupinga kuendelea kwa vikao hivyo.
Hivi karibuni, viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), walitangaza kuitisha maandamano nchi nzima kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, amempongeza Raisk Kikwete kwa kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini.
Dk. Bana alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, hiyo ni ishara tosha kuwa kiongozi huyo wa nchi hana ubaguzi na ni karama aliyojaaliwa na Mola ya kumsikiliza kila mtu.
Msomi huyo alisema anaamini kikao hicho kitasaidia kufikiwa kwa muafaka iwapo viongozi hao wa kisiasa watakuwa na hoja kwa sababu Bunge walilogomea kushiriki baadhi ya vyama, lipo kwa mujibu wa sheria na Rais yupo kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, alisema amefurahishwa na hatua ya Rais ya kukubali kukutana na viongozi hao kwa sababu ameonyesha kuwa ni muungwana na ana dhamira ya dhati ya kutaka maridhiano yafikiwe na hatimaye katiba mpya ipatikane.
Hata hivyo, Mhadhili huyo alitoa ombi kwa UKAWA, ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo vizuri na hatimaye maridhiano yapatikane, lengo likiwa ni kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana na mwisho wa siku wasije wakadai kuwa Rais amevuruga mchakato huo.
Wafuasi wa UKAWA walitoka nje Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (mjumbe wa bunge hilo) kuhitimisha kuchangia. Katika mchango wake, Lipumba alidai hawawezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.
Baada ya kauli hiyo, Lipumba aliotoka ndani ya Bunge hilo, akifuatiwa na Mwenyekiti wa UKAWA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wafuasi wao.

Rushwa ya pilau, soda yawang’oa vigogo CHADEMA


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
MWENYEKITI wa CHADEMA wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Ernest Sheshe na viongozi wengine 10, wameachia ngazi kutokana na kuchukizwa na vitendo vya rushwa.
Sheshe na wenzake hao wamefikia uamuzi huo baada ya makada wengine kumwaga rushwa ya vyakula na vinywaji kwenye uchaguzi.
Makada wengi wa CHADEMA wamekuwa wakilalamika kuchezewa rafu na wapinzani wao, ambao wanatajwa kubebwa na baadhi ya viongozi wa makao makuu, ambapo vitendo vya rushwa vimetawala bila kukemewa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sheshe alisema ndani ya CHADEMA hakuna demokrasia na vitendo vya rushwa vinapewa kipaumbele.
Sheshe, ambaye alikuwa akitetea nafasi hiyo, alisema kabla ya kuanza kwa uchaguzi ngazi ya wilaya, wagombea walikuwa wakitoa rushwa na hata taarifa zilipofikishwa makao makuu, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, alituma waraka wa uchaguzi unaowataka viongozi wa mkoa na kanda kukemea vitendo vya rushwa, lakini hakuna kilichotekelezwa.
DK.SLAA
Alisema Katibu wa Kanda, Amani Golugwa, alishindwa kukemea rushwa hata za vyakula kwa kuwa wahusika ni wanaowaunga mkono.
“Wagombea wanagawa mpaka pilau na soda kwa wajumbe na viongozi wanaona ila hakuna hatua zinazochukuliwa kwa sababu ni watu wao. Unakaaje kwenye chama ambacho kimeshika hatamu kwa rushwa,” alisema Sheshe.
Pia alimrushia kombora, mgeni rasmi katika mkutano huo, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwa kushindwa kukemea wala kuchukua hatua dhidi ya rushwa hiyo.
Kwa upande wake, Lema alisema madai ya Sheshe ni kutapatapa na kuwa iwapo hakuridhika na matokeo, alipaswa kukata rufani na si kuhama.
Alisema wagombea wote waliridhika na matokeo hayo kasoro yeye na kwamba, chakula kilichotolewa kwenye mkutano huo kwa baadhi ya wajumbe ni fedha zilizochangwa na wajumbe wa mkutano huo.
“Chakula na vinywaji haikuwa rushwa ili mgombea fulani ashinde, bali kiliandaliwa kwa sababu wajumbe wasingeweza kukaa na njaa, aache umasikini,” alisema. 
Mkoani Tabora nako mambo si shwari kutokana na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa, Kansa Mbarouk, kujiengua ndani ya chama hicho.
Mbarouk alisema amechukua uamuzi huo kutokana na mambo kutokwenda vizuri huku akiwashushia lawama viongozi wa ngazi za juu kuvunja Kanuni.

Spika Makinda ataka ushirikiano Bunge la EAC


Na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amewataka wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutengeneza utaratibu wa kuongeza uhusiano kati ya bunge hilo na yale ya nchi wanachama.

Akizungumza katika ufunguzi wa bunge hilo, Spika Anne alisema tayari maspika wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), wamekubalina kuunda kamati zitakazoshughulikia mambo ya jumuia hizo.
“Lakini jambo kubwa ni kwamba ukanda huu umetengeneza bunge lenye uwezo wa kutunga sheria, mikataba na kusimamia masuala mbalimbali, hivyo kusababisha nchi za afrika kufuata utaratibu huo,” alisema Makinda.
Alisisitiza kuwa Maspika wa nchi za Afrika wamekubaliana kuunda Bunge la Afrika litakalokuwa kamili, ambalo wabunge wake watachaguliwa kama wanavyopatikana wa bunge la EALA na kutaka kuimarishwa zaidi ili kuendelea kuwa mfano.
Akizungumzia mgogoro wa kumuondoa Spika wa Bunge hilo, Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania katika bunge hilo, Adam Kimbisa, alisema mjadala huo umefungwa kisheria na kinachoendelea ni migogoro ya kisiasa tu.
Kimbisa alisema katika kikao hicho cha wiki mbali watajadili amsuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na viwnago vya elimu kwa nchi zote kumuwezesha mtu kuajilika katika nchi hizo pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.
Naye Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Abdulla Juma Saadalla alisema Tanzania kuwa wa kwanza kukubali umoja wa fedha kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kunatokana na umoja huo kuwa na faida kwa wananchi wa Tanzania.
“Sio kweli kuwa Tanzania tunachelewesha mambo isipokuwa lazima tufanye kwa uamakini kama hili la umoja wa foroza tumepeleka bungeni na kukubalika baada ya kueleza faida kwa nchi na wananchi wake,” alisema.
Aliongeza kuwa ni lazima kuwa na shirikisho lenye faida na kutoa mfano wa matumizi ya vitambulisho kuingia katika nchi hizo ambayo Tanzania ilitaka vitumike vya kielektroniki na siyo vya shule.

Alisema sasa nchi zote zimeanza mchakato wa kuwa na vitambulisho hivyo, huku Tanzania tuliokuwa wa mwisho tumeishaanza kutoa kwa 
wananchi wake hivyo kuonesha kwa jinsi nchi ilivyo makini.

Wapongeza DASIP kuwatoa kimasomaso

Na Ahmed Makongo, Bunda
WAKULIMA walioko kwenye vikundi vinavyowezeshwa na Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo Wilayani (DASIP) wilayani Bunda,  wameupongeza mpango huo kwa uwainua kiuchumi.
Baadhi ya wakulima hao waliipongeza DASIP kwa kusaidia kuinua maisha yao tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Wakiongozwa na mkulima bora wa mkoa wa Mara, Mugole Lusungura, walisema kabla ya mradi huo kuanza, walikuwa na maisha duni ikilinganishwa na sasa.
“Kabla ya DASIP, maisha yetu yalikuwa dunia lakini baada ya kupata mafunzo kupitia mashamba darasa tumepata maendeleo makubwa mno. Binafsi nimejenga nyumba, nimenunua mifugo na ninasomesha watoto kutokana na kilimo,” alisema Lusungura.
Lusungura alisema kupitia mradi huo, pamoja na elimu waliyopewa ya kilimo cha tija, kwa sasa wanazalisha mazao mengi yanayoinua kipato cha wakulima wengi wanaozingatia sheria na kanuni za kilimo bora.
Kwa  niaba ya wenzake alipongeza mafunzo hayo yaliyoendeshwa kupitia shamba darasa la Shule ya Msingi Kinyambwiga, wilayani humo na kusema yamekuwa yakiwaongezea uwezo.
Aidha, wakulima hao waliipongeza serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao umewainua kiuchumi na kwamba miradi mingine ya kuendeleza wakulima iendelee kuletwa kwa sababu kilimo ndicho kinachoweza kuwainua watu wa vijijini.
Mratibu wa DASIP Wilaya ya Bunda, Blasius Ogola, alisema mradi huo umewawezesha wakulima wengi wilayani humo kujiinua kiuchumi na kupata maendeleo.
Ogola alisema DASIP imekuwa ikiwawezesha wakulima kupitia mashamba darasa, ili kuwajengea uwezo wa kulima kilimo chenye tija ambacho kitawaletea maendeleo.

CCM yatoa mifuko 100 ujenzi sekondari Nduli


NA ANITA BOMA, IRINGA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimetoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Nduli.
Ujenzi huo ulisimama kutokana na wananchi kuhamasishwa kutochangia ujenzi wake na kusababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Akipokea msaada huo kutoka kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa,  Hassan Mtenga, Katibu wa Kata wa Nduli, Petro Mpogole, alisema utafanikisha kukamilisha ujenzi wa sekondari hiyo ambao ulianza mwaka 2010.
“Agosti 23 Katika sherehe za kumsimika Kamanda wa UVCCM Mkoa Salim Abri, Katibu wa CCM Mkoa aliahaidi kutoa mifuko 100 ya saruji ili kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari ya Nduli na leo ametimiza ahadi yake,” alisema.
Kwa mujibu wa katibu huyo, wanafunzi wamekuwa wakilazimika kwenda Kihesa, Lugalo na hata shule ya sekondari Miyomboni.
Naye Diwani wa kata hiyo, Bashiri Mtove, alisema ujenzi wa shule hiyo ulikwama kutokana na mambo ya kisiasa ambapo baadhi ya wanasiasa walikuwa wakiwahamasisha wananchi kutochangia.
Mtove alisema msaada huo ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba  utafanikisha ujenzi huo kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi, aliwashukuru Katibu na Diwani kwa jitihada walizofanya katika kukwamua ujenzi huo.

Wataka wadaiwa sugu wasakwe


Na Ahmed Makongo, Bunda
WADAU wa pamba katika wilaya ya Bunda, wamepitisha azimio la kuwasaka wakulima wanaodaiwa na kampuni zinazonunua zao hilo na kuwekeza katika kilimo cha mkataba wilayani hapa.
Azimio hilo lilipitishwa jana baada ya wadau hao kubaini kwamba wakulima wengi waliokopeshwa pembejeo na dawa za kunyunyizia pamba wilayani hapa, wanadaiwa mamilioni ya fedha.
Wadau hao wakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Demunicus Lusasi, walipitisha azimio hilo katika kikao kilichoketi katika ukumbi wa Halmashauri mjini Bunda.
Katika kikao hicho wawakilishi wa kampuni hizo walilalamikia hali hiyo na kuitaka serikali kuingilia kati ili wakulima wanaodaiwa waweze kulipa madeni hayo kabla ya kuanza msimu wa kilimo wa mwaka 2014/1015.
Walisema kampuni zao ziliwekeza kwenye kilimo cha mkataba ili wakulima watakapovuna mazao yao walipe fedha hizo lakini, baadhi yao wameingia mitini na kukataa kulipa madeni yao.
Aidha, waliwalaumu baadhi ya wakulima am,bao baada ya kuvuna waliuza pamba kwenye kampuni zingine tofauti na makubaliano.
Kwa upande wake Mkaguzi wa pamba Mwandamizi wa Wilaya ya Bunda, Igoro Maronga, alisema kutokana na madai ya wanunuzi hao, kikao hicho kiliazimia kuwasaka wakulima ambao bado hawajalipa mikopo hiyo.
Maronga alizitaja baadhi ya kampuni zinazowadai wakulima hao kuwa ni pamoja na Oram inayodai  zaidi ya sh.milioni 23, S&C sh.milioni 60 na Birchard inayodai zaidi ya sh.milioni 50.

Washirikiana na wateja kuhujumu TANESCO


Clarence Chilumba, Masasi
UKOSEFU wa maadili, uaminifu na kuwapo kwa ubinafsi wa baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani  Masasi, vimesababisha kushindwa kudai zaidi ya sh. bilioni moja kutoka kwa wateja. 
Hayo yalibainishwa na Meneja wa TANESCO Masasi, Basilius Kayombo, alipozungumza na Uhuru jana ofisini kwake, kuhusu oparesheni kata umeme kwa wateja sugu inayoendelea wilayani humo. 
Alisema ndani ya shirika kuna baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi kwa kukiuka maadili, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu hivyo kusababisha kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Meneja huyo alisema shirika kwa sasa linadai zaidi ya sh. bilioni mojaambazo ni malimbikizo ya madeni kutoka kwa wateja, zikiwemo  taasisi binafsi, za umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali na watu binafsi.
Alisema baadhi ya wateja wamekuwa wakilipa ankara zao za umeme kwa kutumia njia ambazo si sahihi kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi waminifu na wanaofanya kazi ambazo haziko kwenye mamlaka yao.
Kwa mujibu wa Kayombo, hatua hiyo imesababisha hasara kubwa kwa shirika pamoja na migogoro na malalamikko kutoka kwa wateja bila ya sababu ya msingi.
Kayombo alisema kupitia oparesheni inayofanywa kwa ushirikiano na kikosi cha kanda ya kusini cha shirika hilo, wamebaini kuwapo kwa madeni mengi yaliyosababishwa na uzembe na urasimu wa baadhi ya wafanyakazi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wateja kuacha mara moja kushirikiana na wafanyakazi hao wanaolihujumu shirika.

Zimamoto Mwanza yapigwa jeki


NA BLANDINA  ARISTIDES, MWANZA
KIKOSI cha Zimamoto mkoani Mwanza, kimepokea msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni mbili kutoka washirika wa maendeleo.
Msaada uliokabidhiwa ni buti jozi sita, majaketi 12, makoti 15, suruali 22, kofia ngumu 10, kofia za kawaida 10, fulana tano na ovaroli mbili kwa ajili ya utekeleza wa majukumu yao ya kazi.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto, Inspekta Augustine Magere, alisema kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu katika jiji la Mwanza, wanakabiliwa na changamoto nyingi za vitendea kazi.
Inspekta Magere, alisema kwa sasa jiji hilo lina magari manne ya zimamoto ambapo kati ya hayo  mawili yako uwanja wa ndege na mengine katikati ya jiji. 
Alisema magari hayo hayakidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu walioko mkoani hapa huku matukio ya moto yakitokea mara nyingi nje ya mji.
“Tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kutendea kazi, lakini tumewasiliana na marafiki zetu wa Wurzburg, Ujerumani na Tampere nchini Finland ili waweze kutusaidia. Leo hii hawa Wajerumani wametusaidia baadhi ya vifaa kiasi,” alisema Magere.
Magere alisema hayo wakati akikabidhiwa vifaa na mwakilishi wa afisa uhusiano wa jiji hilo, Idd Hussein, vilivyotolewa na jiji rafiki la  Wurzburg.
Alisema kutolewa kwa vifaa hivyo ni kutokana na urafiki wa majiji hayo mawili kwa kipindi kirefu, baada ya baadhi ya watumishi wa Zimamoto kupelekwa kujifunza mambo mbalimbali mwaka 2008.
Kwa upande wake, Hussein aliyekabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Jiji la Warzburg, alisema lengo ni kukiboresha kikosi hicho ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Jk Rais wa kwanza kufika Kibati


NA LATIFA GANZEL
RAIS Jakaya Kikwete ameweka historia ya kuwa rais wa kwanza kufika katika kata ya Kibati iliyoko Mvomero mkoani hapa.
Pia amekuwa kiongozi wa pili wa juu wa taifa kufika Kibati baada ya awali Mwalimu Julius Nyerere kufanya hivyo mwaka 1961 wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mara baada ya kuwasili Rais Kikwete, Mbunge wa Mvomero (CCM), Amos Makalla, alisema ujio wa Kikwete umekonga nyoyo za wakazi wa kata hiyo.
Makalla alisema kilio kikubwa cha wananchi wa kata hiyo kilikuwa kutaka  kumwona Rais na kwamba ziara yake hiyo imetoa jibu la hitaji hilo.
“Ndugu zangu wa Kibati kazi mliyonituma kuhakikisha Rais Kikwete anakuja katika kata yetu nimeitekeleza. Leo Rais Kikwete amefika na ameona kero zinazotukabili, bila shaka sasa zitatatuliwa,’’ alisema.
Makalla ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, alisema kero kubwa iliyokuwa ikiikabili kata hiyo ni kukosekana kwa barabara ambayo imepatiwa utatuzi baada ya serikali kujenga barabara inayopitika kipindi chote cha mwaka.
Hata hivyo, alisema barabara hiyo itaendelea kuboresha kwa kujengwa kwa kiwango cha lami na kukomesha kabisa kero ya usafiri wa barabara kwa vijiji vya kata hiyo.
“Zamani tulikuwa tunatembea muda wa saa tano hadi sita kufika Kibati lakini sasa huchukua saa 1.30 tu kufika hapa,’’ alisema.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema, kero nyingi tayari zimeshughulikiwa  zikiwemo za barabara, elimu afya na mawasiliano.
Alisema aliona umuhimu wa kufika katika kata hiyo kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi na kuahidi kurudi tena Juni mwakani kwa ajili ya kuzindua mradi wa umeme wa kata hiyo.

Waaswa kufuga nyuki kwa manufaa yao


WANANCHI mkoani Morogoro wametakiwa kufuga nyuki kwa njia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji, kuinua kipato na kujitengenezea fursa za ajira.
Hayo yalibainishwa jana na mtaalamu wa ufugaji nyuki  kutoka asasi ambazo zinafuga nyuki kwa njia ya kisasa katika Tarafa ya Turiani wilaya ya Mvomero, Baiton Mshani, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema ufugaji nyuki unaweza kutoa ajira kwa vijana wengi na kuondoa dhana potofu ya kusubiri ajira toka serikalini iliyojenga kwa Watanzania wengi hivi sasa.
Alisema iwapo mtu atakuwa na mzinga mmoja wa nyuki wanaofugwa kisasa anaweza kuingiza hadi sh.300,000 kila mwezi.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wananchi wanapaswa kutambua faida zitokanazo na ufugaji nyuki ambazo ni pamoja na kupata asali, nta gundi.
Aidha, alisema nyuki pia wanasaidia kustawisha mimea  jambo ambalo husaidian kustawisha na kuongeza mazao ya kilimo.
Hata hivyo, alisema changamoto iliyopo sasa ni ukosefu wa vifungashio ambapo aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuusaidia kila mikoa ili iwe rahisi kutekeleza kazi hiyo.
Mshani alisema kwa sasa vifungashio hivyo hulazimika kufuatwa mkoani Arusha jambo ambalo huongeza gharama za uzalishaji asali.
Alisema serikali imekuwa ikitilia mkazo ufugaji nyuki kwa ajili ya kutunza mazingira mbalimbali na kuhamashisha wananchi kutumia asali kwenye maisha ya kila siku.

Kikwete atoa agizo zito Morogoro


SERIKALI imewaagiza viongozi wa wilaya ya Mvomero na mkoa wa Morogoro kukaa pamoja kujadili tatizo la wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kushindwa kumaliza kidato cha nne kwa idadi ile ile.
Agizo hilo lilitolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati  akiwahutubia  wananchi wa kata ya Kibati, wilayani Mvomero akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.
Rais Kikwete alisema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kupata taarifa kuwa  wanafunzi 3,060 kati  ya 5,255 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2009, walishindwa kumaliza kidato cha nne mwaka jana. 
Alisema idadi  hiyo inamaanisha kuwa ni asilimia 42 tu ya wanafunzi hao ndio waliweza kumaliza kidato cha nne huku asilimia 58 wakishindwa kuhitimu elimu hiyo.
“Kaeni mtafakari juu ya tatizo hilo mjue nini cha kufanya, ni kwa nini wanafunzi hao wanashindwa kumaliza shule kama walivyoanza, wanaishia na wapi,” alisema.
Rais aliahidi kuwapatia sh.milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana la shule ya sekondari ya Nguru iliyoko kata ya Kibati wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, alipoulizwa juu ya tatizo hilo, alisema kuna sababu nyingi zinazochangia hilo, ikiwemo wafugaji kuhama na familia zao.
Sababu nyingine, kwa mujibu wa Mtaka, ni wazazi kuamua kuwapeleka watoto shule za  binafsi, hivyo kufanya idadi ya watoto waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kwenye shule za serikali kupungua.
Aidha, alisema baadhi ya wazazi hawana uwezo hivyo kushindwa kuwaendeleza watoto wao ikiwemo kuwasimamia kitaaluma.
“Idadi kamili ya watoto wanaochanguliwa na kujiunga kidato cha kwanza haiwezi kuwa sawa kutokana na sababu hizo.
“Tumekuwa tukifutilia wanafunzi ambao hawaendi shule na badala yake wanafanya kazi za ndani, tunawarejesha shuleni na kuwachukulia hatua wazazi wao,” alisema.
Hata hivyo, alisema Baraza la Madiwani katika halmashauri ya wilaya hiyo liliridhia watoto wote wanaochanguliwa kuingia kidato cha kwanza wapokelewe bila kujali ada na michango mingine.
Pia alisema mikakati mingine wanayofanya ili kukabiliana na tatizo hilo ni kuhimiza  ujenzi wa mabweni na kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa sekondari zote.

Wednesday 27 August 2014

Serikali kufuta ada sekondari



  •  Lengo kuwa na elimu bure hadi kidato cha nne
  •  JK asema ni mkakati wa kuboresha elimu nchini  

NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza rasmi kuwa serikali inaangalia uwezekano wa kufuta ada katika shule zake za sekondari.
Hatua hiyo inalenga kuboresha Sera ya Elimu na kuhakikisha kila mwanafunzi anayeanza darasa kwanza anamaliza kidato cha nne.
Rais Kikwete alikuwa akizungumza jana na wanajumuia ya Chuo Kikuu  Mzumbe, Morogoro na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho ikiwa  sehemu ya ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20, mwaka huu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alitumia muda wa kutosha kuelezea historia ya maendeleo ya elimu nchini, mabadiliko ya mwelekeo wa elimu na sera ambazo zimeongoza mageuzi makubwa katika elimu chini ya uongozi wake.
Alisema serikali yake iliibua mpango wa ujenzi wa sekondari za kata ili kupanua wigo wa wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kada hiyo ya elimu kwa kuwa nafasi za wanafunzi kuingia sekondari zilikuwa finyu.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati anaingia madarakani mwaka 2005, wanafunzi waliokuwa wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa kati ya asilimia sita na 10 ya watoto wote waliokuwa wanamaliza elimu ya msingi. 
Alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata, ikiwa pamoja na kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni,  shule hizo zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio makubwa katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
Aliwaeleza mamia ya wanazuoni hao, watumishi wengine wa chuo na wananchi kuwa serikali wakati wote imekuwa inasaka kubuni sera za kuendeleza elimu na pia kuziboresha sera hizo.
ìKwa mfano sasa hivi tunaangalia jinsi gani ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za serikali kama namna ya kuhakikisha kila mtoto anayeanza darasa la kwanza anakuwa na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada,î alisema.
Aliongeza kuwa: ìTunaangalia kuondoa ada hii ambapo wazazi wanalipa sh. 20,000 kwa shule za kutwa na sh. 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila ya wasiwasi wa kukwamishwa na ada.î
Kuhusu historia ya kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alisema wakati serikali yake inaingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya.
ìKwa miaka mingi, hatukujenga shule mpya za sekondari, na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata.î
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zilikuwepo shule za sekondari 1,745 mwaka 2005 zikiwemo shule 1,202 za serikali na sasa ziko 4,576 zikiwemo shule 3,528 za serikali.
MAFANIKIO MAKUBWA 
Kuhusu maendeleo ya shule za kata, Rais Kikwete alisema zimekuwa na mafanikio makubwa kama ambavyo sekta nzima ya elimu imekuwa na mafanikio makubwa.
Rais Kikwete alielezea baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni upanuzi mkubwa wa elimu ya msingi na uandikishaji wa watoto kuingia shule, upanuzi wa elimu ya sekondari na ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari.
Pia alisema kumekuwa na upanuzi wa elimu ya juu ambapo sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma, ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka sh. bilioni 16 mwaka 2005 hadi kufikia sh. bilioni 345 kwa sasa, na kuongezeka kwa wakopaji kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi 95,000 katika kipindi hicho.
Rais Kikwete alisema kwa sasa serikali yake inapambana na changamoto zilizojitokeza kutokana na kupanuka kwa elimu nchini. 
Alisema moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo sasa imefikia kikomo kwa sababu, sasa wapo karibu wa kutosha kwa shule za sekondari zote nchini.

Mkapa: Maslahi binafsi yanaathiri uwajibikaji


NA RABIA BAKARI
RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa, amesema mgongano wa kimaslahi baina ya viongozi na watumishi wa umma, ni janga ambalo halijapewa uzito wa kutosha katika kulipatia ufumbuzi.
Amesema tatizo hilo limekuwa likizikumba nchi mbalimbali duniani na kwamba viongozi wenye maslahi binafsi ni tatizo katika kuleta usawa na uwajibikaji.

Akizungumzia wakati akifungua warsha ya kujadili Mapendekezo ya Sheria Mgongano wa Kimaslahi miongoni mwa watumishi wa umma mjini Dar es Salaam, jana, alisema tatizo hilo limekuwepo tangu Uhuru.
Alisema tatizo hilo linajidhihirisha kwa namna  ambayo wenye mamlaka au watoa uamuzi wanapokuwa katika maslahi na jambo fulani,  kutumia madaraka yao badala ya kutoa kipaumbele kwa maslahi ya umma.
Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Rais Mkapa alisema tatizo hilo haliko nchini pekee, bali duniani kote na katika baadhi ya nchi wameweka na sheria ya kuhakikisha mtumishi wa umma haruhusiwi kuwa na biashara bila kibali maalumu.
Mbali na hilo, pia hutakiwa kujiepusha na mazingira yanayoweza kumwingiza kwenye mgongano wa maslahi wakati wote.
“Msukumo huu wa kudhibiti mgongano wa maslahi kwa kuandika sheria rasmi ni mwendelezo tu wa vita hii. Miaka ya 1960 tulikuwa na mifumo ya kudhibiti tatizo hili kwa viongozi wa umma ambayo lilifafanuliwa katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.
“Azimio la Arusha lilimzuia kiongozi wa Chama na serikali kutokuwa na hata nyumba ya kupangisha au kuwa na mshahara zaidi ya mmoja. Kwa  bahati mbaya baada ya Azimio la Arusha hakuna mwongozo wala sheria inayosimamia tatizo hili zaidi ya makatazo yanayotajwa kwenye baadhi ya sheria.
“Ni vyema sasa makatazo haya yakaainishwa katika sheria moja ili kuondoa ombwe la kisheria na kuimarisha usimamizi wa suala hili,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia viongozi kutumia vibaya rasilimali na madaraka waliyopewa na umma, hivyo kupoteza imani waliyo nayo kwa serikali.
Mkapa alisema athari kubwa anayoiona ni mtazamo hasi wa baadhi ya wanajamii kuweka kipaumbele maslahi ya umma, kwamba siku hizi imejengeka katika ubinafsi kuliko kuangalia maslahi ya yenyewe.
Alisema kinachohitajika ni kuelimisha umma ili kubadilisha kwanza mtazamo wa jamii na iwapo itafanikiwa katika hilo, kazi itakuwa rahisi  kujenga uchumi ambao ndani yake kuna ushindani wa haki na usawa.
Alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianza kutumika akiwa madarakani, na wakati huo na hata sasa hajawahi kuona tatizo la sheria hiyo. 
“Kinachosisitizwa hapa ni ukweli na uwazi kwenye kuchuma mali, kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria. Ni kweli kuwa taasisi hii (Sekretarieti ya Maadili) ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kukuza maadili, hususan mienendo ya viongozi wa umma,“ alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, alisema utungwaji wa sheria hiyo mpya ni mwendelezo wa maoni ya wengi kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika uongozi unazingatiwa.
Pia alisema itasaidia kuipa meno Sekretarieti, ambapo jambo hilo imesisitizwa hata kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inajadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba. 
Awali, Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema miongoni mwa madhara ya mgongano wa maslahi ni pamoja na uchumi wa nchi kudidimia, wananchi kukosa haki za msingi, kuathiri maamuzi na michakato ya kidemokrasia na wananchi kupoteza imani na serikali.
Kwa kifupi, yaliyomo ndani ya mapendekezo ya sheria hiyo mpya nchini ni iwapo itapitishwa viongozi wa umma watachagua ama kuwa na baishara au kubaki katika uongozi.

CCM yanena kuhusu Dk. Salim


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema taarifa zilizoripotiwa na gazeti la Dira ya Mtanzania kuhusu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama  Dk. Salim Ahmed Salim, hazina ukweli.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijinui Dar es Salaam jana, ilisema habari hiyo iliyochapishwa kwenye toleo la Jumatatu yenye kichwa cha  ‘CCM yamsulubu Dk. Salim mbele ya JK’, kuwa ni uzushi na imelenga kujenga chuki na uhasama.
Katika habari hiyo, gazeti hilo lilidai kuwa Dk. Salim amegeuzwa mbuzi wa kafara kwa kushambuliwa kwenye vikao vya Kamati Kuu ya CCM, kikiwemo kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
“CCM inasisitiza kuwa habari hiyo si ya kweli, imeandikwa kwa lengo la kugombanisha, kujenga chuki na uhasama baina ya Chama. Pia kumchafua kwa makusudi Dk. Salim,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dira ya Mtanzania ilidai kuwa Dk. Salim aliwekwa kitimoto akitakiwa atoe ufafanuzi ni kwa vipi Tume ya Marekebisho ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, ilikuja na mapendekezo ya serikali tatu huku takwimu zikionyesha waliotaka muundo huo ni wachache.
Katika taarifa yake hiyo, CCM ilisema katika vikao vyote vya Kamati Kuu, hakuna mwanachama au mjumbe yeyote ambaye amesakamwa kwa namna yoyote iwe kwa maneno au majibizano ya kawaida.
“Vikao vyote vya Kamati Kuu ya CCM, chini ya Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete, vimekuwa vikifanyika kwa amani na utulivu na hakuna mjumbe yeyote, ambaye amewahi kurushiwa maneno kwa namna yoyote ile,” ilisisitiza.

Mzumbe waunga mkono Bunge la Katiba


NA WAANDISHI WETU
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Mzumbe, wameunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, wakisema wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mwenendo mzima wa Bunge hilo.
Pia wamesema mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya.
Wanafunzi hao walieleza msimamo wao juzi jioni chuoni hapo kwenye risala ambayo waliisoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete. Rais alitembelea chuo hicho ikiwa sehemu ya ziara yake mkoani Morogoro.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Boniface Juma, wanafunzi hao walisema ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.
Akijibu risala hiyo, Rais Kikwete aliwaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni, watumishi wengine wa chuo hicho na wanavijiji vya jirani na chuo kuwa: "Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama."
Aliongeza kuwa: ìNiliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa si Katiba ya CCM ama ya CHADEMA, ya NCCR au ya CUF. Niliwaambia hii ni Katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti.î
Kuhusu madai kuwa Rais Kikwete anakataa kukutana na wajumbe wa Bunge hilo ambalo wanaendelea kususia shughuli za Bunge hilo, alisema:  "Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.î
Hata hivyo, Rais Kikwete aliongeza kuwa ana matumaini mchakato huo utawwapatia Watanzania Katiba mpya. 
ìMimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri."

JK kukutana na vyama vya siasa


Katika hatua nyingine, Rais Kikwete, anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vinayounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alisema jana kuwa Rais Kikwete atakutana na viongozi wa vyama hivyo wiki hii baada ya ombi lao kukubaliwa.
Viongozi hao waliazimia kutafuta nafasi  ya kuonana na Rais Kikwete kwa lengo la kushauriana naye na tunashukuru amekubali na tutakutana naye wiki hii, alisema Cheyo.
TCD inaundwa na vyama vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni CCM, UDP, CHADEMA, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na UPDP ambacho hakina uwakilishi bungeni. 
Hata hivyo, hakuwa tayari kutoa maudhui wala mahali patakapofanyika kikao hicho zaidi ya kupongeza Rais Kikwete kukubali ombi hilo.
Bunge la Katiba lawaka 
BUNGE Maalumu la Katiba, limewajia juu waandishi wa habari kwa kile walichoeleza kuwa wamepotosha taarifa zake.
Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge hilo, Jossey Mwakasukya, alisema jana wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya taarifa kuwa wabunge hao hawajlipwa kwa siku 10.
Alisema habari hizo ni upotoshaji mkubwa tofauti na taarifa zilizotolewa na Katibu wa Bunge hilo na kuwa wajumbe wote walishapata baadhi ya malipo na mengi yalitarajiwa kufanyika juzi.
Alisema iwapo kuna ucheweshaji wa malipo basi  hutokana na sababu maalumu za kiserikali kwani, kila malipo hufuata taratibu.

Tuesday 26 August 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA CHUO KIKUU MZUMBE

RAIS  Jakaya Kikwete, akiwa  na wajumbe wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, mkoani Morogoro, baada ya kuwahutubia chuoni hapo, juzi. (Picha zote na Ikulu).

RAIS Jakaya Kikwete, akikata utepe, kuzindua jengo la mihadhara la chuo hicho.



RAIS Jakaya Kikwete, akipokea risala toka kwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya chuo hicho, Boniface Maiga.

RAIS Jakaya Kikwete, akipokea zawadi ya picha yake ya kuchorwa, chuoni hapo.

WANAFUNZI, wahadhiri na wananchi, wakimsikiliza Rais Jakaya Kikwete,alipowahutubia chuoni hapo.



Toleo letu la leo, linapatikana kote mitaani kwa bei ile ile ya Tsh 700/=

JK aamuru wahanga wapewa viwanja 400



  • Acharuka kwa kucheleweshwa kwa ahadi yake

  • Atoa siku saba, wananchi wapagawa kwa furaha

Na mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga wa mafuriko.
Mafuriko hayo yalitokea miaka minne iliyopita mjini Kilosa, ambapo Rais Kikwete aliagiza wahanga kupewa viwanja.
Alitoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na wahanga hao kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,” alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao kuhusu ahadi hizo.

Baada ya kuambiwa kuwa vimepimwa viwanja 800 katika halmashauri hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao wa mafuriko.

“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho (jana) hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote ziwe zimekamilika na kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazungumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete. 

Mapema,  Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la Msolwa, Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini Hydropower  Project unajengwa kwenye milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na 2.3 kwa ajili ya mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Umeme Vijiji– REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro leo.

Dk. Sheni apangua mawaziri, Ma-RC



Na mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya.
Mabadiliko hayo yanalenga kuendelea kuimarisha utendaji wa shughuli za serikali na tayari jana, amewaapisha wateule wote katika Viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar.
Walioapishwa jana ni Dk. Sira Ubwa Mamboya, ambaye anakuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili. Aliyekuwa Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, amebadilishwa kwenda kuongoza Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na nafasi yake kujazwa na Rashid Seif Suleiman.
Wengine walioapishwa ni Mahmoud Thabi Kombo, ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Afya. Katika mabadiliko hayo pia wamo wakuu wa mikoa ambapo, Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Omar Khamis Othman anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mwanajuma Majid Abdulla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ayub Mohamed Mahmoud kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi pamoja na Hanuna Masoud Ibrahim, ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji na Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Sira alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, ambaye hivi sasa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Suleiman Othman Nyanga.
Meja Mstaafu Kassim Tindwa alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, ambaye kwa hivi sasa anajaza nafasi iliyowachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Pembe, Mwajuma Majid Abdulla alikuwa Mkuu wa Wilaya ya ChakeChake Pemba, ambaye kwa hivi sasa amepanda kuziba nafasi ya Meja Mstaafu Tindwa.
Omar Khamis Othman alikuwa Mkuu wa Wizaya ya Wete, ambaye hivi sasa najaza nafasi iliyowachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, Ayoub Mohamed Mahmoud alikuwa Ofisa Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi, ambaye hivi sasa anajaza nafasi iliyowachwa na aliyekuwa Mkuu wa Wizaya hiyo, Hassan Mussa Takrima.
Kwa upande wake, Hanuna Masoud Ibrahim alikuwa Ofisa Tawala Mkoa wa Kusini Pemba ambaye hivi sasa anajaza nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa wizaya hiyo, Mwanajuma Majid Abdulla.