Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Saturday, 30 November 2013


KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akishirki ujenzi wa nyumba ya daktari wa Hospitali ya Isansa, Kata ya Mtunduru, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, jana, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. (Picha zote na Bashir Nkoromo).Kinana akitoka katika nyumba ya mjumbe namba nane, katika Kijiji cha Mtunduru, wilayani Mbozi, Hongera Myola. Kushoto ni Dk. Migiro na mbele (mwenye koti) ni Kandoro.

Walimu wamshtakia Kinana


NA SULEIMAN JONGO, Mbozi
WALIMU wilayani Mbozi katika mkoa wa Mbeya, wameeleza kukerwa na tabia ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia ya kuwa mbabe na kukataa kusikiliza kilio chao.
Wamesema waziri huyo hataki kusikiliza matatizo yao na kukaa nao meza moja kwa ajili ya kujadili mambo yanayohusu maslahi yao.
Pia, wamelalamikia kukopwa kwa fedha zao sh. milioni 200 za Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) wilayani humo zinazodaiwa kutumika kwenye maandalizi ya sherehe za Mei Mosi, mwaka huu, iliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya.
Akizungumza katika kikao, Mwakilishi wa walimu wa wilaya ya Mbozi na Momba, Leonard Nyang’uye, alisema wanashangazwa na hatua ya waziri kukataa kuwasikiliza walimu badala ya kuwa msaada katika kutatua kero zao.
Nyang’uye alisema Novemba 13, mwaka huu, waliomba kukutana na waziri  ili kuwasilisha malalamiko yao, lakini alikataa kusikiliza kwa madai kuwa serikali imeshamaliza matatizo ya walimu.
“Waziri alimkataza Katibu wa Chama Cha Walimu, Emilia Mwakyoma kusoma taarifa badala yake alimwamuru kukaa chini mara moja kwa madai kwamba matatizo yetu yamekwisha baada ya kushughulikiwa na serikali. Jambo hili lilituumiza kichwa na kutukera walimu. Katibu Mkuu wa CCM tunaomba ufahamu kuwa waziri huyu amekuwa kiburi kwa walimu na siku hiyo alionyesha ukali usio na sababu mbele yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa kauli ya Waziri Hawa kwa walimu aliokutana nao siku hiyo iliwafanya washindwe kuwasilisha malalamiko yao na kwamba wamefarijika na ujio wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana,  kwa kuchukua hatua ya kuwaita ili kujadili mambo yatakayoweka sawa mustakabali wa maslahi yao.
“Tunaamini utatusaidia kwa kuwa waziri mwenye dhamana ameshindwa kutusikiliza,” alisema mwakilishi wa walimu hao.
Kuhusu madai ya fedha za SACCOS kuliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, walimu walimwambia Kinana kuwa wamekuwa wakifuatilia fedha hizo, lakini wamekuwa wakipewa majibu yasiyoridhisha.
Mwakilishi huyo alisema kila wanapofuatilia wamekuwa wakielezwa kuwa fedha zao zilitumika kwenye sherehe za Mei Mosi.
Alisema fedha zilizoliwa ni zile walizokuwa wakidunduliza na kujiwekea ili kusaidiana angalau kuinua hali zao kimaisha.
Nyang’uye, alisema fedha hizo zilitumiwa na halmashauri yao pasipo kushirikishwa na sasa wamekuwa wakisumbuliwa kila wanapozihitaji.
“Tulipohoji kuhusu fedha zetu tulielezwa kuwa zilitumiwa na uongozi wa Wilaya za Mbozi na Momba kuandaa sherehe za Mei Mosi,” alisema.
Baada ya kusikiliza kilio cha walimu hao, Kinana aliahidi kukifanyia kazi ambapo alisema suala la waziri majibu yake yatatolewa na Rais kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kufanya hivyo.
“Hili la waziri nimelisikia, ninawaahidi nitakwenda kuonana na wahusika, siwezi kusema hapa tutachukua hatua gani, tutalifikisha kwa utataribu unaoeleweka,” alisema Kinana.
Kuhusu fedha za walimu kuliwa na halmashauri ya wilaya, Kinana alitaka walimu kurudishiwa fedha zao haraka na kwamba katika hilo hataki kusikia linachukua zaidi ya mwezi mmoja.
Kinana alimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Charles Mkombachepa,   kuhusu matumizi ya fedha za walimu.
ìMkurugenzi  tueleze fedha za walimu hawa zimetumika vipi, ukizingatia kwamba mishahara yao ni midogo na hata hicho kidogo wanachokipata mmekikopa, eti kwa kuandaa Mei Mosi, kwani siku hizi Mei Mosi inaandaliwa na walimu?î alihoji.
Mkurugenzi huyo alikubali kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa na taasisi mbalimbali wilayani humo.
Alisema fedha hizo hazikutumika kwa ajili ya Mei Mosi, bali zilitumiwa kuandaa usafiri, kurekebisha magari na
shughuli nyingine zisizohusiana na walimu moja kwa moja.
Mkombachepa aliomba kulipa fedha hizo katika kipindi cha miezi miwili ijayo. Hata hivyo, Kinana alimtaka Mkurugenzi huyo kulipa fedha hizo mara moja.

Pangua pangua ndani ya polisi


NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi limefanya mabadiliko makubwa ambapo limemhamisha aliyekuwa  Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Philip Kalangi,  kwenda Makao Makuu, Dar es Salaam.
Pia, mabadiliko hayo yamewagusa baadhi ya wakuu wa upelelezi wa mikoa na wakuu wa polisi wa wilaya.
Katika mabadiliko hayo, Kalangi atakuwa Mkuu wa Kikosi cha Kusimamia Usalama wa Mazingira na nafasi yake itachukuliwa na Kamishana Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Mayunga ambaye alikuwa mkuu wa kikosi hicho, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, baadhi ya Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa (RCO) na Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) waliobadilishwa ni RCO Tabora, (ACP) Edward Bukombe ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam.
RCO wa Geita, (ACP) Francis Kibona amehamishiwa Mkoa wa Njombe kuwa RCO na nafasi yake itachukuliwa na SSP, Simon Pasua,  kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dar es salaam.
Wengine ni aliyekuwa OCD wa Wangingíombe,  SSP, Francis Maro amehamishiwa Mkoa wa Katavi kuwa RCO na aliyekuwa RCO Katavi, ACP, Emmanuel Nley,  amehamishiwa Kikosi cha Polisi  Wanamaji Dar es Salaam.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Rukwa, SSP,  Peter Ngussa amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es salaam, nafasi yake inachukuliwa na SSP Alan Bukumbi.
Aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Kati, Mrakibu wa Polisi (SP) Salum Ndalama, anakwenda kuwa Kaimu Mkuu  wa Upelelezi Mkoa wa Tabora na aliyekuwa OCD wa Tunduru, SP, Amadeus Tesha anakwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Kikosi cha Polisi Reli.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limezindua bodi ya udhamini wa mfuko wa usalama wa raia utakaosaidia polisi kutekeleza mpango wake wa maboresho katika jeshi hilo.
Mkuu wa Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, alisema maboresho yana gharama kubwa, ambapo kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza zinakadiriwa kufikia sh. bilioni 294.
IGP Mwema alisema polisi imefanikiwa kuanzisha bodi yenye wajumbe tisa, ambapo Mwenyekiti ni Ali Mufuruki, huku wajumbe wengine wakiwa Yogesh Manek, Deo Mwanyika, Salum Bisarara, Paolo Chiaro, Nassor Salum, Mussa Ally Mussa, Suleiman Kova na Said Salim Bakhresa.

Sumaye: Wasomi msikae kimya


NA MWANDISHI WETU, Morogoro
WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema umefika wakati kwa wasomo kushirikikikamilifu katika masuala yanayohusu nchi badala ya kuwaachi wanasiasa tu.
Sumaye alitoa changamoto hiyo jana katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa albam katika Kanisa la Calvarian mjini Morogoro.
Alisema kuwa msomi ni sifa muhimu hasa kama mtu atafanya yale yanayotegemewa na usomi wake na kuwa msomi maana yake ni mwelewa na ana taaluma fulani aliyosomea na bila shaka umebobea katika fani hiyo.
“Kwa kuwa msomi una uwezo wa kuona mbele ya huko tunakoelekea kama tunaenda sawa au la hasa kama jambo lenyewe liko katika fani yako. Ukiwa msomi una nafasi kubwa ya kushauri kwa kutumia utaalamu wako na elimu yako bila uwoga kwa sababu una uhakika na unayoyasema,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa mtu akiwa msomi ana nguvu kubwa zaidi ya kushawishi kwa sababu atatumia nguvu ya hoja, hivyo sio vizuri msomi akawa mtazamaji na mlalamikaji tu kama wale ambao upeo wao wa kuona na kuchambua mambo ni mdogo.
“Usomi unaheshimika hasa pale mtakapotoa uchambuzi na ushauri wa kitaalamu ambao unasimamia misingi ya taaluma na siyo ya chuki, uhasama, upendeleo au urafiki. Kama rafiki yako akikosea, taaluma haisemi umpongeze bali inataka umshauri kwa kumrekebisha, na vivyo hivyo, kama adui yako au ambaye humpendi akisema kilicho sahihi taaluma inataka uungane naye mikono na kama kwa waziwazi huwezi basi hata kimoyo moyo,” alifafanua Sumaye.
Kwa maoni yake, alisema wasomi wa hapa nchini hawajachukua nafasi yao katika nchi na labda hata katika jamii kwa kuwa kuna mambo mengi makubwa yanayotokea, lakini wasomi wamekaa kimya halafu yakiharibika wanatafuta wa kuwanyooshea vidole wakati madhara yake yanawaumiwa wananchi wote.
Sumaye alisema vyuo vikuu hapa nchini vina maprofesa waliobobea wa fani mbalimbali, madaktari wahadhiri na wanachuo wanaoweza kufanya uchambuzi na utafiti ili kuwa na mchango chanya katika jambo lolote lililoko mbele ya nchi au jamii,nafasi ambayo haijatumika ipasavyo na wakati mwingine kuhisi imetumika vibaya.
“Najua hili lina changamoto zake na mara nyingine mnaweza mkagongana au kukwaruzana na wanasiasa. Hayo tusiyaogope kwa sababu kukwaruzana kwa lengo la kujenga ndiyo afya ya jambo lenyewe. Kunyamaza wakati unajua tunavyokwenda sivyo ni kutokutenda wajibu na hilo ni dhambi,” alisema.
Alisisitiza kuwa: “Wasomi lazima mchukue nafasi yenu katika mambo ya nchi na katika jamii. Msiwaachia tu wanasiasa kila kitu na ninyi mkabaki watazamaji na baadaye walalamikaji. Timiza wajibu wako sasa. Wanasiasa pamoja na kwamba si wajinga, lakini usisahau wana tabia ya kuangalia zaidi kipindi cha uchaguzi.”
Pia, Sumaye alisema upungufu wa maadili mema ni tatizo kubwa katika jamii kwa kuwa unaleta matatizo mengine ikiwemo rushwa, ufisadi, ujambazi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Thursday, 28 November 2013

Pinda kuzindua tovuti ya serikali


Na mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tovuti Kuu ya Serikali katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa Tovuti hiyo inayopatikana kwa anuani ya www.tanzania.go.tz, utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi, wafanyabiashara, washirika wa maendeleo, taasisi zisizo za serikali na wawakilishi kutoka vyuo vikuu.
Imeelezwa kuwa hizo ni juhudi za serikali  katika kuhakikisha kuwa taarifa na huduma inazozitoa zinapatikana na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Taarifa na huduma katika Tovuti Kuu hiyozimegawanywa katika maeneo makuu sita ya serikali, wananchi, taifa, biashara, sekta na mambo ya nje.
Inalenga kutoa huduma mbalimbali kama upatikanaji wa nyaraka zote za Serikali, huduma zinazotolewa na serikali kwa njia ya simu na mtandao, viwango vya fedha, hali ya hewa, na soko la hisa.
Huduma nyingine katika Tovuti Kuu hiyo imetengwa katika ukarasa wa Nifanyeje? ambao  unamjengea uwezo mwananchi wa kufahamu utaratibu wa upatikanaji wa huduma zinazotolewa na taasisi mbali mbali za Serikali.
Inalenga pia kuziunganisha tovuti na mifumo ya taasisi mbali mbali inayotoa taarifa na huduma kwa wananchi na wafanyabiashara katika dirisha moja.
Tovuti Kuu hiyo ilianza kutengenezwa mwaka 2009 na kupatikana kwa anuani ya www.egov.go.tz chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Iliboreshwa na kuunganishwa na iliyokuwa Tovuti ya Taifa kwa anuani ya www.tanzania.go.tz mwaka 2012 chini ya Wakala wa Serikali Mtandao.

Maelfu wamzika Mhariri wa Uhuru


Na Mwandishi Wetu
WAANDISHI wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini na watu mbalimbali, jana waliungana katika maziko ya aliyekuwa Mhariri Mwandamizi wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora.
Mzobora (49), alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa shinikizo la damu, alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
Mbali na waandishi wa habari, maziko hayo pia yalihudhuriwa na mamia ya wananchi, wanasiasa wakiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam.
Naye Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi  Nape Nnauye, wamemtumia salama za pole, kwa uongozi, familia na wafanyakazi wa kampuni ya Uhuru Publications Ltd (UPL) kufuatia kifo hicho.
Viongozi hao, walisema wameshtushwa, na na kuhuzunishwa kufuatia kifo.
“Tutaendelea kuuenzi mchango wa marehemu Mzobora ambao aliutoa katika kampuni hii enzi ya uhai wake,” walisema.
Marehemu Mzobora, alianza kujisikia vibaya juzi usiku akiwa nyumbani kwake, Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili, ambapo alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakifanya jitihada za kuokoa maisha yake.
Hadi anafariki dunia, alikuwa Naibu Msanifu Kurasa Mkuu wa Uhuru. Alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.
Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.
Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.
Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari. Marehemu ameacha mke na watoto.

‘Kampuni za simu ziache ukiritimba’


NA RABIA BAKARI
KAMPUNI za simu nchini, zimetakiwa kuungana katika matumizi ya minara ya mawasiliano na kuacha ukiritimba wa kila kampuni kutumia minara yake.
Agizo hilo lilitolewa jana mjini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, alipokuwa akizindua sherehe za maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Alisema kushirikiana katika matumizi ya minara kutapunguza fedha za kigeni zinazotumika kuagiza minara hiyo, badala yake zitasaidia kusambaza huduma za mawasiliano sehemu mbalimbali ambazo bado hazijafikiwa.
Pia, alizitaka kampuni hizo zitoe fursa ya mafunzo na elimu ya kisasa ya mifumo mipya ya mawasiliano kwa wafanyakazi wake, ili waendane na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
Dk. Bilal aliipongeza TCRA kwa juhudi kubwa ya kuhakikisha sekta ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano inapiga hatua kwa kasi kubwa na kuisisitiza kutunga sheria na kuweka mikakati ya usalama wa TEHAMA ikamilishwe mapema na wananchi wapewe elimu.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Makame Mbarawa, alisema juhudi za CCM, kupitia ilani zake za mwaka 2005 na 2010, zimesaidia ukuaji wa kasi wa sekta ya mawasiliano na kuchangia pato la taifa.
“Tanzania imeweza kupokea mawaziri, viongozi na wataalam kutoka nchi marafiki kama Kenya, Uganda, Burundi, Malawi, Botswana, Namibia, Msumbiji na Lesotho kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kusimamia sekta ya mawasiliano nchini mwao,” alisema.

Mzee adaiwa kubaka kibinti, ajitosa majini


Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi Zanzibar
MKAZI wa Kijiji cha Kidutani Gando mkoa wa Kaskazini Pemba, Muslih Mserembe, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 kisha kujitosa bahari kukwepa mkono wa dola.
Mserembe (55), alikamatwa na watu waliokuwa wamekizingira kibanda chake kilichojengwa kwa miti wakati akimbaka binti huyo bila huruma.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12.00 asubuhi wakati binti huyo akiwafuatilia wenzake kwenda shambani kuokota maembe, ndipo mzee huyo alipomuona na kumuita.
Alisema baada ya binti huyo kumsogelea, alimwambia waingie ndani ya nyumba yake akidai kuwa angempatia maembe badala ya kuwafuata wenzake, ndipo alipombaka na binti huyo alipiga kelele za kuomba msaada.
Kamishna Mussa, alisema baada ya kelele hizo majirani walifika nyumbani kwa Msarembe na wakati wakiizingira nyumba yake, alitoka na kutimua mbio na kwenda kujitosa baharini.
Watu hao walimkimbiza nao walijitosa baharini na kumvua kama samaki.
Alisema baada ya kumkamata walimpeleka katika kambi moja ya KMKM ambapo Polisi walifika na kumchukua kwa hatua zaidi.
Kamishna huyo alisema binti aliyebakwa alipelekwa katika Hospitali ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kwa matibabu zaidi na hali yake imeelezewa kuendelea vizuri.

CCM yakomalia madai ya walimu

Na Solomon Mwansele, Mbeya
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kuibana serikali kuhusu madai ya malimbikizo ya walimu, ambayo sasa yanafikia sh. bilioni 6.
Kimeitaka serikali kuhakikisha inalipa haraka madai hayo ili kuwawezesha walimu kuongeza ari katika utendaji kazi.
Walimu ni taaluma muhimu kwa ustawi wa taifa na kwamba, kimeitaka serikali kuwachukulia hatua kali watendaji wanaokwamisha ulipaji huo na kuisababishia madeni.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, ambaye yupo katika ziara mkoani hapa kuwa, madai hayo ya walimu yanamkosesha usingizi.
Zambi, ambaye pia ni Mbunge wa Mbozi Mashariki, alisema deni hilo linatakiwa kulipa haraka na serikali ili kuondoa hisia za uhusiano ulioyumba baina ya walimu na CCM.
Kwa upande wake, Kinana, alisema CCM kamwe haiwezi kukaa kimya bila kuwatetea wakati walimu wanaidai serikali kiasi kikubwa cha fedha zao, lazima zilipwe haraka.
Alisema tayari CCM imeiagiza serikali kuhakikisha kero zote za walimu zinapatiwa ufumbuzi tena kwa wakati.
“Walimu ni kundi kubwa katika utumishi wa umma, wenyewe ni zaidi ya asilimia 60 ya watumishi wote wa serikali, ni vyema mlitambue kabisa.
“Kero zao zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa haraka ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuleta tija kwa taifa,” alisema Kinana.
Pia, alionyesha kushangazwa na madeni ya walimu kuachwa kuwa makubwa, ambapo alisema madeni yao hupatiwa ufumbuzi na baadaye hurundikana tena na kufikia mabilioni ya shilingi.
“Unaweza kukuta madeni yanafikia hadi sh. bilioni 50 na serikali inayahakiki na kulipa, lakini katika kipindi kifupi huanza kurundikana tena na kuzua migogoro,’’ alisema.
Hata hivyo, alisema hilo linapaswa kuepukwa na tayari Rais Jakaya Kikwete, alitoa agizo la walimu kutohamishwa bila kulipwa stahili zao, kama hakuna fedha za kumlipa asihamishwe.
Kurejea kwa malimbizo ya walimu inaashiria kuwa agizo hilo halifanyiwi kazi na baadhi ya watendaji hususan kwenye halmashauri, ambako matatizo mengi huanzia.NSSF yawafanyia tathimini watoa hudumaNa Theodos Mgomba, Dodoma
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF),  limeanza utaratibu wa kufanya tathimini  kwa watoa huduma ya fao la matibabu kwa wanachama wake.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dk. Ramadhan Dau, aliyasema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa za awali katika Mkutano wa Sita wa watoa huduma ya matibabu wa Shirika hilo.
Dau, alisema kazi hiyo ya kufanya tathimini ya watoa huduma inafanywa kwa ushirikiano na Taasisi ya Pharm Acces International.
Alisema nia ya utafiti huo ni kuona uwezo wa vituo hivyo na utoaji wake wa huduma kwa wanachama hao ili kupunguza malalamiko, ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba katika baadhi ya vituo husika.
“Baadhi ya Hospitali ambazo tumewapa kazi ya kutoa huduma kwa wanachama wetu, wamekuwa wakitoa huduma chini ya viwango tulivyotegemea, hivyo kusababisha malalamiko kwa wanachama wanapotaka huduma,” alisema Dk. Dau.
Mkurugenzi huyo, alisema imekuwa ikiwapa wasiwasi wanachama na kuwafanya baadhi yao kutojiunga na fao hilo.
Alisema mpaka sasa, kuna watoa huduma 375 wa vituo na hospitali mbalimbali  na wanachama waliojiunga na fao hilo kwa sasa wanafikia 102,089, toka kuanzishwa kwa fao hilo miaka saba iliyopita.
Hata hivyo, aliwatoa wasiwasi wanachama wa NSSF, kuwa kujiunga na fao hilo hakusababishi kukatwa pensheni yao siku ya mwisho, kwani katika makato ya sasa fao hilo nalo lipo.
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, aliitaka NSSF kutoa elimu kwa wanachama wake juu ya kujiunga na fao hilo bila kuwachanganya au kuwalipisha mara mbili.
Alisema kwa sasa changamoto kubwa ni kwa wataalamu wa afya wanaotoa huduma kwa wanachama hao kuzingatia miiko ya taaluma ya fani ya utabibu wakati wote wakiwa kazini.

Luhanjo awaasa viongozi


NA FRANK KIBIKI, NJOMBE
VIONGOZI wa serikali na vyama vya siasa nchini, wametakiwa kutumia nafasi zao kuhakikisha wanashirikiana na wananchi, kujiletea maendeleo kwenye kila ngazi ili kuondokana na umaskini.
Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo, wakati wa Ibada ya shukrani na kumbukumbu ya kifo cha Waziri wa zamani wa Elimu, na aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini, Jackson Makweta, iliyofanyika nyumbani kwake, Kijiji cha Hagafilo, mkoani Njombe.
Alisema kama ilivyokuwa kwa Makweta, kila kiongozi atumie nafasi yake kuhakikisha anasaidiana na wananchi katika kujiletea maendeleo.
Luhanjo, alisema ni vyema kwa viongozi kujua wanaacha alama gani kwa jamii wanayoongoza kama mchango wao kwa maendeleo.
Huku akimtolea mfano wa Makweta, katika kuboresha sekta ya elimu mkoani Njombe, alianzisha shule za wazazi kwa kila tarafa ambazo zilikuwa zikiitwa Njombe District Development Trust (NDDT).
Zililenga kuwasaidia wanafunzi wanaokosa nafasi ya kujiunga na shule za sekondari za serikali.
“Makweta ameacha historia na alitumia talanta zake kama kiongozi kusukuma maendeleo na wananjombe, tutamkumbuka daima, ni vyema viongozi wa sasa waige mfano wake,” alisema Luhanjo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Kapteni Aseri Msangi, alisema kiongozi huyo aliacha pengo kubwa mkoani humo na aliahidi kuiga mfano wake.
Wakitoa maoni yao, wakazi wa Njombe, waliwashauri viongozi wasio na maadili na uwezo wa kuchapa kazi, wawapishe wenye uwezo.
Naye mjane wa marehemu, Twihuvila Makweta, alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali na watu waliokuwa pamoja wakati wote wa maombolezo na msiba wa mume wake.

Wednesday, 27 November 2013

Mhariri Uhuru afariki dunia


NA MWANDISHI WETU
MHARIRI Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora, amefariki dunia.
Mzobora (49), alifariki dunia ghafla leo saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi, akitokea Hospitali ya Aga Khan pia ya Dar es Salaam.
Mussa, mdogo wa marehemu, alisema jana kuwa Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku akiwa nyumbani kwake, Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili.
Alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.
Mzobora, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya msanifu mkuu, akiwa buheri wa afya.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia, zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mzobora, ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.
Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.
Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.
Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi daraja la pili na hadi kufariki dunia kwake, alikuwa Mhariri Daraja la Pili.
Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.
Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari.
Marehemu ameacha mke na watoto.
Mungu ailaze roho yake mahali pema paponi. Amina.
Wakati huo huo; Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kufuatia kifo hicho.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa habari shupavu na mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alimfahamu Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema kalamu yake.
Katika salam hizo, Rais Kikwete ametoa pole pia kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru na Waandishi wote wa habari nchini, kwa kumpoteza mwenzao waliyekuwa wakifanya naye kazi kila siku.
“Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza baba, kiongozi na mhimili wa familia,” alisema Rais Kikwete.
Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba  Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.
Amewataka wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa kiungo cha familia yao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.

Mauaji ya bodaboda yawatikisa Polisi Dar


Na Mohammed Issa
MATUKIO ya mauaji ya waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda na wengine kujihusisha kwenye uhalifu, yamezidi kushika kasi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Tayari watu watatu wanadaiwa kupoteza maisha wilayani Ilala, Dar es Salaam, katika kipindi cha wiki moja baada ya kushambuliwa na makundi ya waendesha bodaboda kwa tuhuma za kupora pikipiki.
Kufuatia hali hiyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imetoa onyo kwa wanaojihusisha na matukio hayo, ikiwemo kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji.
Pia, imesema imeanza kukomesha matukio ya wizi wa pikipiki pamoja na mauaji ya wanaotuhumiwa kuiba pikipiki hizo.
Walisema kama kuna dereva au mmiliki wa pikipiki anapata usumbufu kwenye masuala ya kiupelelezi waonane na wakuu wa vituo ili kupatiwa ufumbuzi wa kesi zao.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, aliwataka wamiliki na madereva wa boda boda kufuata sheria badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema kuanzia sasa, Polisi hawatavumilia vitendo vyovyote, vitakavyosababisha uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na damu za watu kumwagika.
“Matukio ya wizi wa pikipiki yasiwe sababu ya watu kuuana, na si sahihi kumuua mtu kwa sababu hiyo, tunataka kila mmoja afuate sheria.
“Kama madereva wa bodaboda wanapata shida kwenye masuala ya upelelezi, waende kwa wakuu wa vituo au makamanda, kupatiwa ufumbuzi wa kesi zao…wasidhani kama wanapopeleka kesi hazifanyiwi kazi, wanapoona uzito waende mbele zaidi kuliko kujichukulia hatua,” alisema.
Kwa mujibu wa Msangi, Polisi wanajitahidi kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki na alitoa wito kwa jamii, kutoa ushirikiano ili kuwafichua wahalifu wa aina hiyo kwenye maeneo yao.
Alisema wananchi wajiepusha na uvunjifu wa sheria na kwamba, wanapomkamata mwizi, wampeleke kwenye vyombo vya sheria.
Msangi, alitoa kauli hiyo kufuatia ongezeko la mauji ya wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa pikipiki, kushamiri jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alisema waendesha boda boda 16 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya fujo na kusababisha mauaji ya mtu waliyedhani ni mwizi wa pikipiki.
Alisema kati ya watuhumiwa hao, mmoja alikamatwa na sare za Jeshi la Polisi.
Juzi, waendesha bodaboda zaidi ya 100, walifanya msako wa kuwasaka wezi wa pikipiki katika mtaa wa Kivule, Ilala Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Marietha, waendesha bodaboda hao, walimkamata mtu waliyedhani ni mwizi ambapo walimchukua mpaka Msongola na kisha walimpiga na kumchoma moto na kabla ya kufa papo hapo.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, madereva hao, walikwenda Kivule CCM na kuvamia nyumba ya mtu waliyedhani ni mwizi wa pikipiki na kufanya uharibifu wa mali mbalimbali, ikiwemo magari mawili.
Kamanda huyo, alisema Polisi wanaendelea na msako wa kuwakamata waliohusika katika tukio hilo.
Alisema Polisi hawatakubali kuona vitendo vya mauaji ya raia vikiendelea kutokea, kuanzia sasa, wamejipanga kukabiliana na wanaotekeleza mauaji hayo.
Habari kutoka eneo la tukio, zilisema madereva wa bodaboda walijikusanya kwa ajili ya kufanya msako wa nyumba kwa nyumba baada ya kupata majina ya mtandao wa wezi wa pikipiki katika mtaa huo na maeneo ya jirani.
Yussuf Makame, ambaye ni dereva, alisema jana kuwa waliamua kufanya msako huo kufuatia vitendo vya wizi wa pikipiki kuendelea kushamiri katika maeneo hayo.
“Hapa tunalizwa sana, pikipiki nyingi zinaibiwa na kesi zikienda polisi zinachukua muda mrefu, ndio maana vijana wameamua kumalizana na wezi kwa kuwashambulia,” alisema.
Kwa mujibu wa Makame, licha ya kuibiwa bodaboda zao, baadhi yao wanauawa na majambazi hayo na kisha kutokomea sehemu zisizofahamika.
Alisema wanapowafikisha watuhumiwa hao polisi, upelelezi wa kesi huchukua muda mrefu na mara nyingine kesi zinamalizwa katika mazingira ya kutatanisha.

Mwakyembe aonya wafanyabiashara


Na Innocent Ng’oko, Mbeya
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameonya kuwa wafanyabiashara wasipotumia vyema fursa ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, wataugeuza mkoa wa Mbeya na mingine ya jirani kuwa jalala la bidhaa kutoka nje.
Aliwataka kuhakikisha wanatumia ipasavyo fursa ya uwanja huo kukuza biashara na mataifa mengine na kupanua masoko ya bidhaa kwa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Biashara mkoani hapa ‘Mbeya Expo 2013’ katika eneo la Ukumbi wa Mkapa, ambayo yameandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA).
Alisema maonyesho hayo yenye lengo la kufungua mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kama fursa ya uwekezaji, hayatakuwa na maana iwapo wafanyabiashara hawatawekeza na kuchangamkia fursa za masoko mapya na kubadilishana mbinu za kibiashara.
Alisema maonyesho hayo yanatakiwa kuwa chachu ya wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda, kujitathimini katika kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi na ambazo zitakidhi ushindani wa kibiashara na mataifa ya jirani yakiwemo ya Kenya, Uganda, Malawi, Zambia na mataifa mengine.
“Unajua maonyesha haya ni muhimu kwa kuwa yanatupa picha ya moja kwa moja na yenye ulinganifu wa bidhaa tunazozalisha na wanazozalisha wenzetu wa nje,’’alisema Dk. Mwakyembe.
Akitolea mfano, alisema Mbeya imejaaliwa kuwa na mazao adimu na yenye ubora yakiwemo maparachichi, viazi vitamu na mviringo, kokoa, kahawa, chai, mpunga na matunda mbalimbali.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alishitushwa na tabia ya baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa kampuni za kigeni kutumia bidhaa zikiwemo mbogamboga, matunda, ndizi na mchele kutoka nje ya nchi.
Awali, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mbeya, Lwitiko Mwakalukwa, alisema kusuasua kwa maonyesho hayo kunatokana na kuwepo kwa kongamano kubwa la wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali, lililofanyika Dar es Salaam.

Sheni awafunda watendaji


Na mwandishi wetu, zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuimarisha utafiti kwa kuwa majukumu ya msingi ya wizara hiyo yanategemea zaidi utafiti.
Hivyo, alisema Wizara haina budi kuzingatia hilo pindi ipangapo bajeti yake kwa kuzipa kipaumbele kazi za utafiti ili kuleta uwiano wa vipaumbele katika mipango ya wizara.
Aliitaka Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuchangamkia masuala ya utafiti hata kama ni kwa kuwashajiisha watafiti kutoka nje ya wizara.
Dk. Sheni aliyasema hayo alipokuwa akihitimisha kikao cha Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi wa wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013, jana.
Aliikumbusha kuendeleza ushirikiano wa karibu pia na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei ndogo ya zao la mwani.
Alisema limekuwa jambo jema kwa wananchi kuitikia wito wa serikali wa kuendeleza kilimo cha mwani ambacho kinaifanya Zanzibar sasa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa zao hilo.
“Ni lazima jitihada zifanywe kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei kabla ya wananchi hawajakata tama,” alisema Dk. Sheni. 
Akitoa maelezo ya awali ya Wizara katika kikao hicho, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdillah Jihad Hassan, alisema wizara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 iliweza kutekeleza malengo yake kwa ufanisi kwa asilimia 64.
Alisema Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, ilitekeleza malengo yake kwa asilimia 72, Idara ya Uendeshaji na Utumishi asilimia 81, Idara ya Huduma za Utabibu wa Mifugo asilimia 59, Idara ya Uzalishaji Mifugo asilimia 77, Idara ya Maendeleo ya Uvuvi asilimia 47 na Idara ya Mazao ya Bahari asilimia 85.
Alisema katika kipindi hicho, Wizara ilitoa huduma mbalimbali kwa walengwa ili kuimarisha maendeleo ya mifugo na uvuvi nchini.
Alisema wastani wa wafugaji 34,000, wavuvi 38,000, wazalishaji wa mwani 21,000 na vikundi 146 vya wafugaji wa mazao ya baharini, walifaidika na huduma hizo.
Waziri huyo, alikieleza kikao hicho kuwa sekta ya mifugo ilikuwa kwa asilimia 3.1 na kuchangia asilimia 4.2 ya pato la taifa mwaka jana, huku sekta ya uvuvi ilikuwa kwa asilimia 2.3 na kuongeza mchango wake kwa pato la taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 hadi asilimia 7.1 mwaka jana.
Sekta ya uvuvi imezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa uvuvi wa baharini na ufugaji wa samaki na mazao ya baharini.
Ilielezwa kuwa jumla ya tani 9.7 za samaki waliovuliwa kutoka katika mabwawa ya wananchi mwaka jana.
Tani 7.7 zilivuliwa Pemba ikilinganishwa na tani 2.0 katika kisiwa cha Unguja.    

Mtumishi CRDB afa ajalini


NA JUMANNE GUDE
WATU wawili wamekufa jijini Dar es Saalam, katika matukio tofauti, likiwemo la mfanyakazi wa CRDB, Emmanuel Masanyuti, aliyekufa katika ajali ya gari baada ya kupinduka katika barabara ya Mandela.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kipolisi wa Temeke, Anglibert Kiondo, alisema tukio hilo lilitokea jana, saa 6.30 usiku, karibu na mlango wa kuingilia katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Kiondo, alisema Masanyuti anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35, alikuwa akiendesha gari yenye namba za usajili T969 BJT, aina ya Toyota Corolla, iliyokuwa inatoka Vetenary kuelekea mataa ya TAZARA.
Alisema gari ilimshinda na kuacha njia ambapo lilipanda tuta kisha kugonga taa za barabarani na hatimaye kupinduka na kusababisha kifo cha mtu huyo.
Kamanda Kiondo, alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke na upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Katika tukio lingine, msukuma mkokoteni aliyetambulika kwa jina moja la Mashaba amekutwa amekufa katika eneo la Jangwani Minazi Mirefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alisema mwili marehemu ulikutwa juzi, saa 4.00 asubuhi katika eneo hilo ukiwa umelala bila ya kuwa na jeraha lolote.
Kwa mujibu Marietha, marehemu enzi ya uhai wake alikuwa mnywaji wa pombe haramu aina ya gongo, hata hivyo, chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.
Alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo chake.

Mgomo mpya wanukia TRL


NA MWANDISHI WETU
MGOMO mwingine unanukia katika Shirika la Reli Tanzania, safari hii ukiwahusisha askari wanaolinda usalama wa abiria pindi wawapo safarini.
Askari hao wanadai kutolipwa posho za safari kwa zaidi ya mwaka mmoja, wanadai kila wanapoubana uongozi ili uwalipe, hupigwa danadana.
Habari za kuaminika zinadai kuwa baadhi ya askari hao wanajipanga kuingia kwenye mgomo wa kutotoa huduma za ulinzi kama njia ya kushinikiza kulipwa.
Ilielezwa kuwa askari hao ambao hufanya doria ya ulinzi wakati wa safari za treni, hulipwa posho za safari kwa ajili ya kujikimu lakini tangu Novemba, mwaka jana, hawajalipwa.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa inaweza kusababisha askari hao kusafirisha abiria kinyume cha utaratibu kwa lengo la kujipatia kipato.
“Inafikia wakati mtu unakosa hata fedha ya kujikimu njiani, jambo hili ni la hatari kwa sababu mtu unalazimika kuwa omba omba na familia zetu hazituelewi kabisa,’’ kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho, kilidai kuwa askari wa nchi nzima walifikisha malalamiko yao katika ngazi husika na tangu wakati huo, walielezwa madai yao yanashughulikiwa.
Akizungumza kwa njia ya simu na Uhuru jana, Kamanda wa Kikosi cha Reli, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Saada Haji, alithibitisha kuwepo kwa madai hayo na kuwa bado yanashughulikiwa.
Pia, aliwataka askari kufuata sheria na utaratibu wa kazi yao katika masuala mbalimbali hasa wanapokuwa na madai na si kukimbilia katika vyombo vya habari.
“Masuala yao yanashughulikiwa, ni kweli wanalidai Shirika la Reli na hata kama wanamadai, wanapaswa kufuata utaratibu wa kudai kwa mujibu wa kanuni na sheria za kazi yao kwani zipo,” alisema.

Saturday, 23 November 2013

Yametimia CHADEMA


NA SULEIMAN JONGO, NYASA
HASIRA za wanachama wa CHADEMA kutokana na kuvuliwa uongozi kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, zimeanza kuibuka  baada ya vijana wa chama hichoi wilayani Nyasa, kujiengua.
Wakati hali ikiwa hivyo,  Zitto na viongozi wengine waliovuliwa uongozi, leo wanatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuweka mambo hadharani kuhusiana na CHADEMA.
Vijana hao kwa makundi makubwa, wamejiengua katika chama hicho na kukabidhi kadi zao kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ikiwa hatua ya kupinga iliyochukuliwa na Kamati Kuu ya CHADEMA dhidi ya Zitto.
Mbali na yaliyojitokeza wilayani Nyasa, wanachama wa chama hicho mkoani Kigoma wamepanga kufanya maandamano makubwa kupinga hatua ya chama hicho ya kumvua uongozi Zitto na wenzake.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya CHADEMA, kutangaza kumuondoa mbunge huyo katika nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama hicho ikiwemo za naibu katibu mkuu na naibu kiongozi wa upinzani bungeni.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake katika mkutano uliofanyika jana wilayani hapa, Timoth Ndunguru, alisema hatua ya CHADEMA kumtimua Zitto kwenye uongozi, imedhihirisha wazi vijana hawana nafasi ndani ya chama hicho.
Alisema kutokana na hatua hiyo, kundi la vijana 50 wameamua kundoka CHADEMA, kutokana na kuonyesha wazi kuwa viongozi wake  hawataki hoja vijana na changamoto zake.
“Nilijiunga CHADEMA kutokana na kuvutiwa na siasa za Zitto ambaye kwetu hapa Lituhi tumekuwa tukivutiwa sana na mwanasiasa huyo kijana, lakini kitendo cha chama kutangaza kumvua nyadhifa zake za ndani ni wazi kinachofuata ni kufukuzwa kabisa uanachama.
“Kwa hali hii tunatamka rasmi kujiondoa ndani ya chama hiki na sasa tunajiunga na CCM na tunaomba tupokewe. Tuliamini  katika demokrasia, lakini imekuwa kinyume chake,” alisema Ndunguru.
Alisema kwa sasa CHADEMA imekosa demokrasia ya kweli , hivyo kitendo cha kumfukuza Zitto ni wazi vijana sasa hawana nafasi ndani ya chama hicho.
Alisema wamefuatilia mwenendo wa CHADEMA, lakini sasa wanaona umefika wakati wa kuondoka katika chama hicho na kutangaza kujiunga CCM huku wakimuomba Kinana kuwapokea.
Kwa upande wake,  Kinana alisema vijana wanatakiwa kuwa makini kwa kupima sera za kila chama kabla ya kujiunga nacho.
“Ni wakati muafaka kwa vijana kutambua wana wajibu wa kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi lakini pia kilichotokea CHADEMA ni somo kwenu kujua umefika wakati kujiunga CCM.
“Sisi tukiahidi tunatekeleza na tukishindwa tunawaeleza ila kubwa kwenu vijana mnatakiwa kutambua taifa hili linategemea mchango wenu kuliendeleza na chama ambacho kitafanikisha hilo ni CCM ambacho kinatambua wajibu wake kwa jamii,” alisema Kinana.
Katibu Mkuu wa CCM alitumia nafasi hiyo kuhamasisha vijana wa mkoa huo kujikita zaidi kwenye shughuli za maendeleo huku akiahidi kuwa chama chake kitahakikisha kinawasimamia katika kutimiza malengo yao kwa kulitumikia taifa.
KIGOMA KUZIZIMA
Kutoka Kigoma, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa wanachama wa CHADEMA mkoani humo wamepanga kufanya maandamano makubwa na kurejesha kadi zao kupinga uamuzi wa chama hicho kumvua Zitto uongozi.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana kutoka kwa viongozi wa chama hicho, wanaomuunga Zitto, maandamano hayo tayafanyika leo mchana kuanzia Kibindo hadi Mwandiga. Katika maandamano hayo, pia watachoma vipeperushi na bendera za chama.
Walisema mbali na leo, pia wanatarajia kufanya maandamano kama hayo siku astakapowasili Zitto mjini Kigoma na kwamba watafanya hivyo kumpongeza kama shujaa anayependa haki.
Katika hatua nyingine, Zitto anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari leo kuelezea mambo yaliyojitokeza hadi kuvuliwa kwake uongozi na pia mustakabali wake kisiasa.
CHADEMA MORO LAWAMANI
Naye Mwandishi Wetu kutoka Morogoro, anaripoti kuwa viongozi wa CHADEMA katika serikali ya kitongoji cha Mgudeni kijiji cha Mkangawalo, kata ya Mngeta wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamelalamikiwa kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji wananchi wa eneo hilokuwapakia katika pikipiki na  kuwafunga pingu mikono katika machuma ya pikipiki .
Wananchi hao walisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara  wakati wa ziara ya Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Rojas Romuli, uliofanyika katika kitongoji hicho.
Wananchi hao walisema viongozi hao ambao wengi ni viongozi wa serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na afisa mtendaji aitwaye Rajabu Kipolelo   wamekuwa wakiwafanyia wananchi  vitendo hivyo pale wanaposhindwa kulipa faini mbalimbali.
Mmoja wa wananchi ambaye aliwahi kufanyiwa unyanyasaji huo, Maduka Mwela,, alisema alitakiwa kulipia sh. 300,000 kama malipo ya kodi ya ardhi na kwamba alitoa sh. 180,000 za awali lakini cha kushangaza siku iliyofuata alikuta amewekewa alama ya msalaba mwekundu katika shamba lake kisha kufuatwa na askari mgambo na kumkamata.
Alisema mgambo hao walimfunga mkono mmoja nyuma ya pikipiki  baada ya kumpakia na kisha kuondoka naye hadi kwa mtendaji wa kijiji.
‘’ Nilipofika mtendaji huyo alinipokea kwa maneno ‘’nyinyi ndio mnakaa vikao  na chama chenu cha CCM halafu mnapinga kulipa ada ya ardhi, tulibishana kwa saa kadhaa,” alisema.
Alisema wananchi wa kijiji, baada ya kuona tukio hilo,, waliandamana hadi katika ofisi ya mtendaji kushinikiza mwenzao ambaye ni balozi wa CCM aachiwe na ndipo alipomwachia.
Kwa upande wake, Richard Mwamwanga, mjumbe katika serikali ya kijiji, alisema viongozi hao wamekuwa wakijipangia bei za ada kinyume cha utaratibu, kwa lengo la kuwakomoa wananchi.
Alisema awali wakati serikali ya kijiji hicho ilipokuwa ikiongozwa na CCM, walikuwa wakilipia ardhi sh. 20,000 ambapo walipoingia walipandisha hadi kufikia sh. 40,000 kwa ekari.
Hata hivyo mjumbe huyo alisema mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, ambaye anatokana na CHADEMA, Stelatoni Njaani, amekuwa akiongoza kwa njia ya udikteta kutokana na uamuzi anaotoa hataki mtu mwingine ahoji.
Naye Deus Makaranga, katibu wa baraza la wazee kijijini hapo alisema kuwa viongozi hao kwa kushirikiana na mtendaji huyo wamekuwa wakitoa risiti feki katika kulipia mashamba pamoja na michango mbalimbali ya maendeleo.
Alisema wamekuwa wakitumia risiti moja kuandika mchango zaidi ya mmoja sambamba na kutoa risiti  kwa watu tofauti zenye namba zinazofanana.
Kwa upande wake, Gidius Alois Mwagombeka, alisema yeye alikuwa mweyekiti wa kitongoji cha Mkangawalo na kwamba viongozi wa CHADEMA walimfanyia hila kwa kumtuhumu kufanya ubadhilifu wa fedha za maendeleo katika kitongoji hicho hali iliofanya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti,  kumwondoa madarakani.
Alisema kuwa hiyo ilikuwa mwaka jana na kwamba tume iliundwa katika kitongoji hicho dhidi ya tuhuma hizo na kubaini kuwa si za kweli.

JK: Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya  Kikwete amesema wajibu wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.
Aidha, amesema kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya kwa kuiga utamaduni wa kigeni kupita kiasi.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio Poland. Alhamisi, wiki hii kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne.
“Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea, mtaihangaikia na kuleta faida nyumbani. Ni jambo ambalo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya, viongozi hawafai, mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?, alihoji.
Aliongeza kuwa:  “Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba mtasukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”
“Mbona kazi za NGO mnazifanya vizuri bila kusukumwa au kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Hata kama hamuwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?” alihoji.
Rais alisema kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa uraia pacha ambao Watanzania waishio nje wanaulilia.
Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
“Rasimu ya kwanza ya Katiba ilikataa jambo hilo kwa sababu halina ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu jipangeni vizuri kutetea hoja hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na kusahau mambo yenye maslahi kwenu.”
Akizungumzia kuiga utamaduni wa nchi zingine na kusahau wa nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea baadhi yao wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni kuwauza watoto wa kike.
Rais ambaye alionyesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”

Lema njia panda


NA SHAABAN MDOE,ARUSHA.
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Arusha, umemweka njia panda Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbles Lema, kwa kumuuliza tangu lini amemtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudance Lyimo(CCM) hadi  kushiriki kumchagua Naibu Meya kutoka chama chake, Prosper Msofe.
Swali hilo linatokana na mbunge huyo kuwa mstari wa mbele kupinga kuchaguliwa katika nafasi ya naibu meya aliyekuwa diwani wa Kimandolu (CHADEMA), Estomii Mallah aliyefukuzwa uanachama na wenzake wane.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya soko kuu la Arusha, <wenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha, Robson Meitinyiku, alisema Lema anapaswa kuwaeleza muafaka gani alioupata katika jambo hilo lililogharimu maisha ya watu hadi kukubali kufanyika kwa uchaguzi huo wa naibu meya hivi karibuni.
“Wananchi lazima tuamke sasa na tuwe na uthubutu wa kuhoji, yeye alisababisha ndugu zetu kupoteza maisha hapa katika maandamano ya kumpinga meya huyu huyu aliyehudhuria kikao kilichoongozwa naye na kumchagua naibu meya halafu tunakaa kimya tu. Mtu akikwambia jambo analojua ni la kijinga akijua ni la kijinga na wewe ukalifanya atakudharau sana,” alisema.
Meitinyiku alisema yeye alikuwa mmoja wa wananchi  waliokuwa wakisubiri kwa hamu majibu ya maswali mengi katika mkutano alioufanya hivi karibuni kuhusu ahadi zilizotolewa na mbunge huyo ikiwemo ya kumpinga meya kwa kuwa alidai uchaguzi uliomuweka madarakani haukuwa halali.
Alisema kutokana na mbunge huyo kutokuwa na majibu sahihi juu ya ushiriki wake kumpigia kura naibu meya kutoka chama chake, kunaonyesha ubaguzi wa wazi na hofu ya nafasi yake ya ubunge dhidi ya Mallah.
Mbali na swali hilo lililotarajiwa na wananchi, alisema pia Lema alitarajiwa kujibu swali na lini atajenga Machinga Comlex aliyoiahidi, hospitali ya akina mama yenye bwawa la kuogelea, kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoani, kutoa mikopo kwa wajasiriamali na wapi alipopeleka gari la wagonjwa na trekta alilopewa na wahisani.
Alisema matarajio hayo yote yaliyeyuka katika mkutano huo baada ya kuonekana akizungumzia zaidi masuala ya picha zake chafu zilizozagaa katika mitandao ya kijamii akipeleka tuhuma hizo kwa UVCCM na mgogoro wake na aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
“Alichotakiwa kukifanya ni kueleza fedha za mfuko wa jimbo alivyozitumia katika kuwakwamua kiuchumi vijana, wanawake na wakazi wa jimbo lake kwa ujumla badala ya kubaki kuzitumia fedha kwa manufaa yake au kuziacha bila kuzifanyia kazi na wananchi wakikosa msaada hata wa mikopo.
Akijibu tuhuma za kuzagaa kwa picha zake chafu, alisema Lema anapaswa kujifungia chumbani na wenzake na kutafakari kwa kina namna picha hizo zilivyopatikana na kisha kusambazwa katika mitandao hiyo, kwa kuwa jumuiya yake ina kazi nyingi za kufanya kwa vjana na wananchi na si kukimbizana naye.
Naye katibu wa WAZAZI Mkoa wa Arusha, Rehema Mohamed, alisema Lema hapaswi kutafuta mchawi katika mambo yaliyomkuta kwa kuwa hizo ni mbegu chafu alizozipanda  mwenyewe kwa madai ya kuwajengea wananchi ujasiri.
Alisema kwa kipindi kirefu Lema amekuwa akiwachochea na kuwagombanisha wananchi na viongozi wa serikali yao hadi kufikia kuwafundisha ukosefu

Wednesday, 20 November 2013

Operesheni tokomeza ujangili mazito yaibuka


NA RABIA BAKARI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki, amesema baadhi ya wabunge walitaka Operesheni Tokomeza Ujangili isitishwe kwa kuwa ilianza kuwagusa.
“Tulianza kuwagusa wenyewe (wabunge)... ndipo kelele zilipoanza, tatizo la ujangili ni kubwa mno, Tanzania kila mtu mtaalamu, kila mtu mjuaji,” alisema Kagasheki.
Alitoa kauli hiyo jana, mjini Dar es Salaam wakati akifanya majumuisho ya kikao kati ya wizara na viongozi wa dini, waliomtembelea kwa ajili ya kujadiliana na kupeana mawazo ya namna ya kupambana ili kuokoa maliasili za nchi, ikiwemo tatizo la ujangili.
Balozi Kagasheki alisema wakati Operesheni Tokomeza Ujangili inaanza, wabunge walitoa mapendekezo mazuri na kusifia kwamba ianze, lakini ilipoanza na kasi yake kuwa kubwa na kuanza kuwagusa, wakapiga kelele isitishwe.
Aliongeza kuwa hoja ya kusitisha operesheni hiyo si kubwa kama ambavyo tatizo la ujangili lilivyo.
“Tembo wanauawa kila siku, watu wanapiga kelele isitishwe kwa sababu ya jambo fulani... lakini ukweli huwezi kuacha tembo wanateketea kwa visingizio hivyo,” aliongeza.
Operesheni hiyo ilisitishwa na bunge kwa madai ya kuwepo ukiukwaji wa haki za binadamu, ambapo Balozi Kagasheki alisema ingawa  kulikuwa na mapungufu, lakini kutokana na umuhimu wa operesheni husika isingepaswa kusimamishwa.
Aliugeukia upande wa mahakama kuwa nacho ni chanzo cha kuzorotesha juhudi za kupambana na ujangili huo nchini, kwani sheria kali zilizowekwa hazifuatwi.
“Sheria inasema vingine, mahakama inafanya vingine, inawavunja moyo wadau na askari wanaopambana na ujangili, ni tatizo kwa kweli,” alisisitiza.
Alisema Tanzania ilikuwa ya kwanza duniani kwa kuwa na tembo wengi, lakini baadaye ikashika nafasi ya pili, ikitanguliwa na Botswana, ila kwa hali ilivyo sasa, huenda isiwepo tena kwenye ramani ya nchi yenye tembo.
Aliongeza kuwa mbuga ya Selous ilikuwa na tembo takriban 55,000, lakini takwimu za hivi karibuni zilionyesha kuwa kuna tembo 15,000, na idadi hiyo huenda imeshuka zaidi siku za hivi karibuni.
“Kwa hali ilivyo, sidhani kama hata ndani ya miaka mitano Tanzania itakuwa na tembo hata mmoja... hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposema tutunze maliasili, si kwa kizazi kijacho, bali kwa dunia nzima, kwani ni zawadi ya pekee tuliyopewa na Mungu, lakini itafika kipindi tutabaki na kumbukumbu za picha,” alisema.
Alitolea mfano kontena lililokamatwa na meno ya tembo siku kadhaa zilizopita Zanzibar ni kitu ambacho kimewatisha wadau walio nje ya nchi, kwamba amepokea barua pepe nyingi kuhusiana na jambo hilo na ujangili kwa jumla.
Viongozi wa dini kwa pamoja, walitoa mapendekezo matatu kwa waziri huyo, kwamba kuwe na ushirikishwaji kwenye mambo ya rasilimali za taifa, uundwaji wa chombo kitakachoshirikisha wizara na viongozi wa dini kwa ajili ya kusimamia rasilimali za nchi na muundo wa utekelezaji wa majukumu hayo.
Aidha, walimkabidhi maoni na mapendekezo juu ya kusimamia rasilimali za nchi, na kumueleza kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuandaa kongamano lililokuwa na mafanikio, lakini wizara hiyo haikuwa na mwakilishi.
Akijibu hoja hizo, Balozi Kagasheki alikiri kusahau upande wa viongozi wa dini, lakini ukweli wao ndiyo wenye wananchi ambao wanaingia misikitini na makanisani, hivyo wakipata elimu ni rahisi kuelimisha watu wengine.
Alitoa agizo kuwa ndani ya wiki moja, upatikane muafaka wa chombo hicho na muundo wa utekelezaji wake, kwa kuwa wizara na serikali kwa jumla haina tatizo na jambo hilo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakurugenzi wa idara, watendaji wa ngazi za juu na viongozi wa dini waliwakilishwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Stephen Munga, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Salum na watendaji wengine wa kamati ya viongozi wa dini

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (wa pili kushoto) na viongozi aliofuatana nao, wakishirikiana na wananchi kusomba matofali wakati wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nakahewa,  katika jimbo la Peramiho, Songea Vijijini, jana. Wengine ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (wa tatu kushoto),akifuatiwa na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro. Picha zaidi.uk.17. (Na Bashir Nkoromo).

Kitanzi chamgeukia Waziri Dk. Mgimwa


NA SULEIMAN JONGO, PERAMIHO
WAZIRI wa Fedha, Dk. William Mgimwa ni miongoni mwa mawaziri watakaoitwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na uchelewashaji wa fedha za malipo ya wakulima wa mahindi.
Akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Masangu, Kata ya Magagula wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, Waziri wa Fedha ndiye mwenye dhamana ya fedha zote za serikali.
Kinana alisema waziri huyo hawezi kuachwa, huku wakulima na wadau wa mazao ya mahindi wakiwemo waliosafirisha wakiwa hawajalipwa fedha zao.
“Ninachokisimamia ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa Nane ulioagiza Chama kusimamia serikali zake mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar. Hivyo sifanyi mimi binafsi,” alisema.
Alisema waziri huyo lazima aitwe na kuhojiwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kitakayofanyika mwezi ujao mjini Dodoma.
Kinana alimtaka Dk. Mgimwa kujiandaa na mambo manne, ikiwemo kujibu hoja kuwa kwa nini wakulima wa mahindi hawakulipwa fedha zao baada ya kuuuza kwenye ghala la taifa.
Swali la pili ni kwa nini fedha za pembejeo hazilipwi kwa wakati, huku zikiwa tayari zimeshatengwa kwenye bajeti ya serikali.
Alitaja hoja nyingine anayopaswa kujiandaa kuijibu ni kwa nini bajeti ya serikali ilichelewa kutekelezwa, licha ya kusomwa Aprili badala ya Julai kwa lengo la kuanza kutekelezwa mapema.
Kinana alitaja hoja ya mwisho kuwa kwa nini kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kila eneo, ikiwemo serikalini kuhusu ucheleweshaji fedha za kutekeleza shughuli mbalimbali.
“Haiwezekani wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wa serikali wote walalamike kutopatikana fedha wakati zilishaidhinishwa. Viongozi wote walipoteuliwa kushika nafasi mbalimbali hawakukataa, bali walifurahi na kuahidi kuwahudumia wananchi, hivyo hilo ndilo tunalolisubiri na kulitarajia,” alisema.
Wakati huo huo, Dustan Ndunguru anaripoti kuwa, CCM imesema wakati umefika kwa serikali kuangalia upya utaratibu wa kununua mazao ya wakulima, ambapo inapaswa inunue kwa fedha taslimu badala ya kuwakopa.
Kutokana na hilo, kimetaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuwalipa wakulima wa mahindi fedha zao wanazodai baada ya kuuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili wapate uwezo wa kugharimia mashamba waliyoyaandaa kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.
Kinana alitoa mapendekezo hayo alipokuwa akihutubia mkutano huo, ambapo alisema kimsingi watendaji na viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia kilimo hapa nchini hawatekelezi majukumu yao kwa umakini na kutokana na hali hiyo, wazalishaji wa mazao kama korosho, tumbaku na mahindi wamejikuta wakikosa mtetezi wa dhati, hivyo kuibua manungíuniko.
Alisema CCM ndiyo iliyopewa ridhaa na wananchi ya kuunda dola, hivyo ina wajibu wa kupambana na wavivu, wazembe ambao wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, kwani wamekuwa wakilipwa mishahara kwa kodi za Watanzania na kuwa walichotakiwa kufanya ni kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Katika hatua nyingine, Kinana alishangazwa na taarifa zilizotolewa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wilayani hapa kuwa baada ya serikali kubadili mfumo wa utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa vikundi, sasa hali hiyo imebadilishwa na kuwapa jukumu mawakala ambao kwa muda mrefu wamekuwa sio waaminifu.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, alisema wakulima wengi walihamasika kujiunga na kuanzisha vikundi kwa malengo ya kupata pembejeo hizo, lakini wamekatishwa tamaa na kitendo cha jukumu hilo kwa asilimia 20 kuwapa vikundi, huku mawakala wakipewa jukumu la kusambaza pembejeo hizo kwa asilimia 80.

Sumaye: Utatuzi wa masuala ya elimu ufanyike kwa haraka


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu  Mstaafu, Frederick Sumaye, tatizo la kushuka kwa kiwango cha ufaulu linapaswa kutatuliwa kwa haraka na kwamba kulumbana juu kubadilisha majina ya madaraja ya viwango vya ufaulu hakuna tija.
Sumaye alisema hayo jana katika mahafali ya 11 ya shule ya Sekondari ya wasichana ya Amani inamilikiwa na Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, Jimbo Katoliki la Singida.
ìLeo tunaanza kulumbana kama matokeo ya kidato cha nne yawe na daraja sifuri au daraja hilo sasa liitwe daraja la tano na kwa kufanya hivyo kiwango cha kufeli sasa kianzie alama 20 badala ya 34 ya huko nyuma.
ìUtafiti unaonyesha hata kiwango cha ufaulu wa alama 34 yenyewe iko chini sana, je tukikishusha kiwango hicho itakuwaje? Kama badiliko hili litapitishwa, basi itaingiza sura mpya kabisa katika shule zetu,î alisema.
Alisema hakuna mtihani usio na madaraja na daraja la mwisho ni la walioshindwa kufikia kiwango cha kufaulu.
Unapokuwa na daraja F au 0, si kwamba huna chochote kichwani, bali kilichoko hakifikii kiwango kinachotakiwa kwa kufaulu,î alisema Sumaye.
Alisema kama isivyo sahihi kwa mwanafunzi aliyepata alama 34 kupewa daraja 0, hata aliyepata alama 5 naye hastahili kupewa daraja 0 maana na yeye ana kitu japo kidogo kichwani.
Hata hivyo, aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii ya Bunge kwa kuona upungufu huo na kuishauri serikali kipi cha kufanya.
ìNi matumaini yangu kuwa serikali yetu sikivu itauchukua ushauri huo kwa umuhimu unaostahili,î alisema Sumaye.
Alisema dawa ya matatizo haya yanayojitokeza sasa katika sekta ya elimu ni kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu na si kucheza na mitaala au kushusha alama za ufaulu.
Sumaye  pia alionya  wanaoiangalia elimu katika sura ya kupata ajira ya ofisini  kuwa si fikra sahihi na mawazo hayo hayapaswi kuendekezwa.
Huku akinukuu vifungu vya Biblia na nukuu za Baba wa Taifa Julius Nyerere, Sumaye alisema; ìKatika kitabu kitakatifu cha Biblia, tunaambiwa ëMkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Mithali 4:13.î
Alisema katika kitabu cha Elimu ya Kujitegemea, hayati Mwalimu Nyerere, aliandika kuwa lengo la elimu ni kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maarifa na mila za taifa, kulitumikia na kuliendeleza Taifa.
Mwalimu Nyerere alifafanua kuwa lengo la elimu ya sekondari ni kuwapatia vijana elimu, ufundi na fikra ambazo zitawafaa wakati watakapoishi katika jamii inayobadilika,î alisema Sumaye.
Hivyo, alisema maana ya elimu si kuwapatia ajira pekee vijana wamalizao masomo yao, bali ilenga kuwawezesha kujiajiri ili wamudu maisha yao na kuwapatia fikra mpya zinazokwenda na wakati.
ìHivyo ni dhahiri kuwa yeyote anayepata fursa ya kusoma, anakuwa na bahati, maana amepata uhai, anapata ufunguo wa maisha bora na anakuwa na bahati ya kuutumikia umma walau kurudisha asante au fadhila kwa yote ambayo jamii imemsaidia mpaka akapata elimu,î alisema.
Alisema ajira itaendelea kuwepo na watakao ajiriwa ni wale watakao kuwa na  elimu nzuri.
Hivyo, alitoa rai kwa wazazi na walezi nchini, kuwahimiza watoto wao wasome kwa bidii ili wawe washindani wazuri katika soko finyu la ajira.
Alitolea mfano elimu ya sayansi na teknologia, kuwa itaendelea kuwa na soko kubwa kwa muda mrefu katika ulimwengu wa utandawazi kutokana na mahitaji yake.
ìNi kweli ajira katika soko rasmi haikui kwa kiwango sawa na idadi ya wanaohitaji ajira katika soko hilo, lakini hii si kwa Tanzania tu, bali ni kwa nchi zote duniani.
ìHivyo tusitarajie kuwa kuna siku itafika vijana wote wanaomaliza kidato cha nne, cha sita na vyuo vya elimu juu tutawakuta wote maofisini wamevaa tai wameajiriwa na soko rasmi, si kweli,î alisema Sumaye.
Alisema umefika wakati sasa wa kuichochea sekta isiyo rasmi ikue kwa kasi, ili kila Mtanzania apate fursa ya kujiajiri.
ìHapa ndipo elimu itawawezesha watu wamudu ushindani hata katika sekta hiyo pia,î alisisitiza.
Akizungumzia malumbano yaliyoibuka hivi karibuni kuhusiana na viwango vya madaraja ya ufaulu, alisema tangu kale elimu ilipewa nafasi ya pekee katika maisha ya binadamu, tofauti kubwa ilijionyesha kati ya watu wenye elimu na ambao hawakuwa nayo.
ìHali kadhalika hata katika ulimwengu wa leo, elimu bado imeendelea na itaendelea kutoa tofauti kati ya wenye elimu na wasio na elimu au hata kati ya wenye elimu bora na wasio na elimu bora,î alisema Sumaye.
Alisema nchi zilizozingatia utoaji wa elimu bora, zimeendelea kufanya vizuri katika medani za maendeleo, ikilinganishwa na ambazo hazikuzingatia.
ìMaendeleo ya haraka ya viwanda na teknolojia katika nchi mbali mbali duniani yametokana na nchi husika kuzingatia utoaji wa elimu katika fani za sayansi na teknolojia kwa watu wao hasa vijana,î alisema Sumaye.
Alisema ili kufikia malengo, nchi inapaswa kutoa elimu bora kwa watoto na vijana kwa lengo la kuondoa ujinga ambao ni chanzo cha matatizo mengi katika jamii, yakiwemo ya  umasikini na maradhi.
Sumaye alisema ifike wakati sasa Watanzania wajengewe imani kwa vitendo, kuwa elimu inayotolewa na taasisi na shule nchini, iwe na ubora usiotiliwa shaka na mtu yeyote. Alisema haitakuwa busara kwa taifa kusomesha watoto wote, lakini kwa viwango vya chini kuliko vinavyokubalika.
ìLazima elimu yetu iwe na ubora kitaifa kulingana na mitaala inayokubalika, na pia iwe na ubora wa kimataifa.
ìTusijitengenezee viwango vyetu wenyewe ambavyo havikubaliki au vinatiliwa shaka na watu wengine au hata sisi wenyewe,î alionya Sumaye.
Hivi karibuni  Naibu Waziri wa Elimu,  Philipo Mulugo alitofautiana na Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo, Profesa Sifuni Mchome juu ya viwango vya alama za ufaulu na ubadilishaji wa madaraja , suala ambalo limezua mjadala mkali ambapo mpaka sasa bado haujalewa masimamo.

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na viongozi wa nchi za Afrika kwenda katika ukumbi, kuendelea na mkutano wa tatu wa nchi za Kiarabu 'Afro Arab', uliofanyika Kuwait, juzi.

Mwakyembe ashtukia janja ya mwekezaji


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
SAKATA la kudaiwa kuuzwa kwa kipande cha eneo la reli kwa mwekezaji Arusha limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuonyesha wasiwasi  juu ya taarifa za kukodishiwa eneo hilo kwa miaka miwili huku mwekezaji akitumia sh. milioni 500 kujenga uzio.
Dk. Mwakyembe akizungumza katika eneo hilo alisema taarifa kuwa mwekezaji huyo, Philimon Mollel, kupitia Kampuni ya Monaban,  ambaye amepewa eneo hilo na Shirika Hodhi la Kusimami Mali za Reli (RAHACO) kwa miaka miwili  kwa ajili ya maegesho ya magari yake, alisema litakuwa na undani zaidi kwa kuwa hakuna anayeweza kutumia fedha nyingi kiasi hicho kujenga ukuta kwa ajili ya maegesho ya magari kwa miaka miwili tu.
Kabla ya Dk. Mwakyembe hajatoa maamuzi kuhusu suala hilo, alimpa nafasi Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema,  kuzungumza ambapo alisema anachokiamini ni kwamba mwekezaji huyo ana lengo la kulitwaa eneo hilo kiujanja ambapo kwa sasa ameonyesha kulihitaji tu kwa ajili ya maegesho ya magari na kuwa hiyo sio nia yake pekee.
ìMheshimiwa Waziri hapa ninachokiona ni mpira umetangulizwa mbele halafu anapima upepo, tukinyamaza sisi pamoja na nyie serikali, kesho mtakuta mambo mengine yanafanyika hapa....mimi nakueleza wazi usikubali kudanganywa,îalisema Lema.
Mbunge huyo aliongeza kuwa hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi inayongozwa na Dk. Hamis Kigwangwala ilipokuwa Arusha, ilimuita na kumuhoji mwekezaji huyo ambaye alikuwa na majibu tofauti tofauti juu ya matumizi ya baadaye ya eneo hilo.
Alisema mara ya kwanza aliieleza kamati hiyo kuwa aliliomba eneo hilo na kupewa kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kufanya shughuli za maegesho na kuoshea magari yake na magari ya wananchi wengine kama njia ya kutoa ajira kwa vijana wapato 150.
Lema alisema kutokana na maelezo yake hayo,  kamati ilimhoji iwapo kuna mwekezaji anaweza kutumia sh. milioni 500 kujenga ukuta kwa ajili ya kuegesha magari kwa mkataba wa miaka miwili kwa kuwa itakua ni sawa na kutupa fedha zake au vinginevyo ana lengo lingine tofauti ya kulitwaa kinyemela eneo hilo.
Aliongeza kuwa baada ya kuulizwa swali hilo, mwekezaji huyo alijibu kuwa siyo fedha zote sh. milioni 500 amezitoa yeye,  bali wamegawana nusu kwa nusu na wamiliki wa eneo hilo RAHACO kwa niaba ya Shirika la Reli  Tanzania (TRC) ambapo yeye alitoa sh. milioni 250.
Lema alisema mara baada ya mwekezaji huyo kuona amebanwa juu ya suala hilo, alitoa maelezo ya nyongeza kuwa mbali na uwekezaji huo wa maegesho na kuoshea magari,  ana mpango wa kujenga majengo ya kibiashara na stesheni ya treni.
Mbunge huyo alisema kutokana na maelezo hayo, pamoja na kamati nzima waliingiwa na wasiwasi juu ya uwekezaji huo wa sh. milioni 500 ukilinganisha na faida anayoipata kutokana na maegesho ya magari yake binafsi na eneo la kuoshea magari yake na ya wananchi wengine.
Kutokana na mkanganyiko huo, Lema alimshauri Waziri Dk. Mwakyembe kuwa eneo hilo iwapo lingetangaziwa zabuni ya kukodishwa na TRC wenyewe kupitia wasimamizi wake RAHCO, serikali ingeweza kupata fedha nyingi kiasi cha sh. milioni 15 kwa mwaka tofauti na fedha wanayolipwa sasa ya sh. 500,000 kwa mwezi.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Mwakyembe alimuuliza mwekezaji huyo iwapo ni kweli ana nia ya kujenga maduka hayo na stesheni ya reli na njia zake baada ya kukabidhiwa eneo hilo kwa mkataba wa miaka miwili ya uwekezaji mdogo na wa muda mfupi.
Mwekezaji huyo alimjibu kuwa ni kweli na tayari ameshafanya mawasiliano ya namna ya kupata vichwa viwili vya treni na mabehewa kutoka Afrika Kusini, jambo ambalo lilimashangaza waziri.
Hapo hapo, aliwageukia viongozi wa RAHCO na kuwahoji aliyewapa ruhusa ya kufanya makubaliano ya namna hiyo bila kuishirikisha ofisi yake ambapo walijibu kuwa hakuna makubaliano ya namna hiyo baina yao na mwekezaji huyo katika mkataba wao.
ìKumbe kuna mambo makubwa hivyo, sasa nikwambie Mollel kama kuna kitu nyuma ya pazia mbali na haya tunayoelezwa hapa katika mkataba wenu, tambua hakitafanyika, hakuna kujengwa kwa ‘shopping mall’ wala stesheni ya treni na njia zake. Hiyo ni kazi ya wizara,”alisema Dk. Mwakyembe.
Alimtaka mwekezaji huyo kuendelea na shughuli zake za uegeshaji wa magari yake pamoja na uoshaji magari katika eneo hilo kama mkataba unavyosema pasipo kuongeza ujenzi wa jengo lolote la kudumu kwa kuwa siku yoyote baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika serikali italichukua eneo hilo kwa ufufuaji wa njia za reli.
ìNdugu yangu endelea na kazi zako kwa mujibu wa mkataba wako na hawa jamaa baada ya hapo tuna mpango wa ujenzi wa reli kutoka Tanga hadi Musoma, hivyo usijidanganye kufanya ujenzi mwingine kwa kuwa hutafanikiwa. Sitaki kusikia siku tunataka eneo letu uanze kuleta habari zako za mahakamani, kwa kuwa hutashinda,îalisema Dk. Mwakyembe.
Katika habari ya mwanzo iliyoandikwa na gazeti dada na hili la MZALENDO, Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO, Mhandisi Tito, alikiri kutoa kibali kwa mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa uzio huo hadi kuingilia eneo la barabara ya treni kwa maelezo kuwa maamuzi hayo yalifikiwa na bodi nzima ya RAHCO.
Gazeti hili pia lilimnukuu Mkurugenzi wa Kampuni ya Monaban Mollel ambaye alisema eneo hilo amepewa baada ya kuandika barua ya maombi kwa RAHCO na hatambui iwapo uzio huo umejengwa kimakosa kwa kuingilia njia ya treni wala iwapo kuna eneo linalomilikiwa na TBA ambalo uzio huo umeingilia.
Pia, aliongeza kuwa hatambui iwapo eneo hilo lina mgogoro na kuwepo kwa kesi mahakamani kwa kuwa yeye ni mpangaji tu na iwapo itafikia hatua ya kutakiwa kuvunja uzio huo,  hatokubali kuingia hasara na atahitaji kurejeshewa gharama zake za ujenzi kwa asilimia 50.
Mbali na eneo hilo la reli kuchukuliwa na mwekezaji huyo,  pia liko eneo la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambalo limezua mgogoro mkubwa baina ya wakala huyo na RAHCO hadi kufikishana mahakamani kila mmoja akidai eneo hilo ni mali yake.
Akizungumza mbele ya Dk. Mwakyembe, msanifu majengo wa TBA, Pheres Tarimo, alisema eneo wanalogombania na RAHCO ni mali yao halali kutokana na mgawanyo wa mali za TRC uliofanyika miaka iliyopita na hati za umiliki na ramani zake wanazo ambazo walimkabidhi waziri huyo.
Pia, alisema mvutano huo ulisababisha RAHCO kukimbilia mahakamani kuwashitaki TBA kuwa ni wavamizi wa eneo hilo jambo ambalo liliwazuia kuendelea kuzungumzia suala hilo hadi kesi itakapomalizika.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Mwakyembe aliuagiza uongozi wa RAHCO kuiondoa kesi hiyo mahakamani mara moja kwa kuwa sio vyema kwa idara mbili za serikali kushitakiana na badala yake atawaita ofisini kwake ili kulizungumza suala hilo ambalo anaamini litamalizika.

TCAA yawakana marubani


Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema haihusiki na malalamiko ya marubani wa Kitanzania kukosa ajira katika mashirika ya ndege, licha ya kuwa na leseni zilizotolewa na mamlaka.
Pia, TCAA imesema mamlaka hiyo ipo kuangalia maslahi ya pande zote na sio mdau mmoja, hivyo ni wakati wa chama cha marubani kuthamini mchango wa mamlaka hiyo na si kuivunja nguvu.
Msimamo wa TCAA ulitolewa jana katika taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari, kuhusiana na malalamiko ya chama cha marubani kuhusiana na matatizo wanayokumbana nayo.
Taarifa hiyo ilisema mamlaka haihusiki na matatizo ya marubani hao, kwani haikushiriki katika mchakato wa wao kwenda mafunzoni na hakuna mkataba wa kuwaendeleza, kwani kazi ya mamlaka ni udhibiti wa sekta (masuala ya ki-usalama  na kiuchumi) na sio kutoa mafunzo au ajira kwa kuwa haina ndege.
Ilisema katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa za malalamiko ya baadhi ya marubani wa Kitanzania kuhusu kukosa ajira katika mashirika ya ndege yanayoendesha shughuli zake hapa nchini, licha ya kuwa na leseni zilizotolewa na TCAA zinazothibitisha kuwa wamefuzu kufanya kazi hizo za urubani.
Katika malalamiko hayo,  marubani kupitia chama chao, wameinyooshea kidole TCAA kuwa imeshindwa kutatua tatizo hilo na kwamba imeonekana kuegemea upande wa watoa huduma za usafiri wa anga nchini, ambao chama kinawatuhumu kutoa ajira kwa upendeleo.
Aidha, taarifa ilisema chama hicho kiliituhumu TCAA kuwa ilipuuza ushauri wake uliotaka kipaumbele cha udhamini wa mafunzo ya urubani kupitia Mfuko wa Mafunzo ya Marubani na Wahandisi Ndege kutolewa kwa marubani Watanzania ambao hawajapata ajira ili kuwajengea uwezo na hivyo kuwaongezea sifa za kupata ajira, na kuichukulia mamlaka kama kikwazo cha jitihada zao katika kupata ajira.
Taarifa ya TCCA ilisema matatizo mengi yanatokana na mabadiliko katika sekta, ambapo awali marubani kama ilivyokuwa katika fani nyingine, waligharimiwa mafunzo yao na serikali au wafadhili, ikiwemo mafunzo ya marubani yaligharimiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Wakala wa Ndege za Serikali.
Ilisema kuanzia miaka ya 1980, mfumo wa mafunzo ulibadilika ambapo wanafunzi kupitia wazazi au walezi wao wamekuwa wakijigharimia mafunzo yao wenyewe. Licha ya kufanikiwa kufanya mafunzo ya awali, inakuwa vigumu kwa watu binafsi kulipia gharama kubwa za mafunzo zaidi.
Hivyo, taarifa ilisema chama cha marubani kinaelewa kuwa juhudi za mamlaka kushawishi serikali na wenye ndege waweze kusaidia kupunguza tatizo la ajira, hatua hizo zimeanza kuzaa matunda, hivyo wauthamini mchango wa mamlaka na sio kuivunja nguvu.

Tuesday, 19 November 2013


KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (wa pili kulia) na msafara wake, wakinywa chai nyumbani kwa Mjumbe wa Shina Namba Sita, Saidi Hussein (kulia), katika Kijiji cha Mchomora, Namtumbo. Kushoto ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro.

Wanaotambiana CCM wazodolewa


NA SULEIMAN JONGO, SONGEA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema viongozi wanaotambiana, kupigana vikumbo na kusema hadharani kupitia vyombo vya habari hawana sifa ya kuwa viongozi bora.
Amesema wanaofanya hivyo wanasukumwa na ulafi wa mali na uroho wa madaraka. “Wameshindwa kutumia muda wao kushughulikia matatizo ya wananchi, badala yake wanapigana vikumbo kusemana na kushambuliana kwa lengo la kupata uongozi.”
Kinana aliyasema hayo jana, mjini Peramiho wilayani hapa mkoani Ruvuma, alipozungumza na wajumbe wa shina namba 26 lililoko katika Kata ya Peramiho.
Aliwataka wana-CCM kutowachagua viongozi wa aina hiyo kwenye nafasi za uongozi kwa kuwa, dhamira yao si kuwatumikia Watanzania, bali wanataka kujilimbikizia mali.
"Wote walioko juu wanaosemana kupitia vyombo vya habari hawafai. Kusemana kwao kunawaondolea heshima, hivyo wazomeeni hao kwa kuwa si viongozi bora, hawana heshima na sifa stahili,î alisema.
Kinana alisema wanaoshindana na kurushiana maneno wanalipwa fedha, posho na wengine mishahara ambayo huwapa shibe na kuwahamasisha kuwa na uroho wa madaraka.
Alifafanua kuwa, ili kuamini kauli hiyo siku zote wanaosemana ni viongozi wa juu, na kwamba katu huwezi kusikia mabalozi wa nyumba 10 na wanachama wa kawaida wakijibizana au kusuguana kupitia vyombo vya habari.
ìHivi mmewahi kusikia wapi mabalozi wa nyumba 10 wanagombana na kushambuliana kwenye magazeti. Haiwezi kuwa hivyo kwa sababu hakuna wanacholipwa, bali kazi yao ni kuwatumikia wananchi na CCM,” alisema Kinana.
Alisema wananchi wanataka kutatuliwa kero na changamoto zinazowakabili na si malumbano, kwani wanaofanya hivyo wanafanya kwa sababu ya madaraka, wanaleta aibu.
Hii ni aibu, aibu, aibu tena aibu kubwa, viongozi kusema kwenye vyombo vya habari kisa madaraka ni aibu.
Katibu Mkuu aliongeza kuwa viongozi wa aina hiyo ndio wanaokivuruga Chama badala ya kutoa ushirikiano kutatua matatizo ya wananchi.
Awali, akimkaribisha Kinana katika eneo hilo, Kiongozi wa Kimila na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Maposeni, Julius Ndiu, alimkabidhi silaha za jadi ambazo ni ngao, mgolole, mkuki na shoka dogo ni silaha anazotakiwa kuzitumia katika kukilinda Chama.
ìNakukabidhi silaha hizi kwa ajili ya kupambana na mafisadi ndani ya Chama na kuwapiga vita wanaokwamisha maendeleo ya CCM,” alisema.

Ajira za vigogo wa KIA zawekwa rehani


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
AJIRA za vigogo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), zimewekwa rehani.
Hatua hiyo inatokana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kusema atawafukuza kazi pindi atakapata taarifa ya kupita kwa wahamiaji haramu, dawa ya kulevya na nyara za serikali.
Dk. Mwakyembe alitangaza kiama hicho na kuweka rehani ajira hizo jana, alipozungumza na menejimenti na watumishi wa Kampuni ya Uwakala katika uwanja huo ya KADCO ili kujua uendeshaji na changamoto zinazowakabili.
Alisema ana taarifa za kutosha kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, hasa Kitengo cha Usalama na Uhamiaji wanaoshiriki kutoa hati feki za kusafiria, kuvusha dawa za kulevya na nyara za serikali, jambo ambalo hatalivumilia kwa kuwa linaitia doa nchi, kimataifa.
Mwakyembe alisema vitendo hivyo vimeshamiri kwa kasi katika uwanja huo kipindi kifupi baada ya kudhibiti vitendo hivyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa waziri huyo, baadhi ya watu ambao wanajihusisha na biashara hizo haramu, wameugeuza uwanja huo kuwa uchochoro.
Alisema atahakikisha kila aliyehusika katika utekelezaji wa matendo hayo maovu anatimuliwa, hata kama yuko wizara tofauti na anayoiendesha kwa kuwa wafanyakazi wote wanafanya kazi chini ya serikali moja inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Mwakyembe alisema kuanzia sasa atazungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuhusu jambo hilo na kumtahadharisha kuwa atamshangaa pindi atakapompokea mtumishi wa wizara yake ambaye atabainika kuhusika na masuala hayo.
ìHapa hakuna cha kwamba mimi niko Wizara ya Mambo ya Ndani, kwamba huhusiki... mimi na nyinyi sote tuko chini ya serikali moja, na nitampigia simu Waziri Nchimbi nimwambie kuwa nitamshangaa endapo atampokea mtumishi nitakayemfukuza kazi kwenye wizara yangu,î alisisitiza Dk. Mwakyembe.
Hata hivyo, aliutahadharisha uongozi wa KADCO kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria watumishi wanaoonekana kushiriki vitendo hivyo viovu, hususan usafirishaji wa dawa za kulevya, nyara za serikali na utoaji wa hati feki za kusafiria, vinginevyo akiligundua yeye kosa hilo na wao kuwa kimya, hawatasalimika.
Alisema mtu yeyote atakayekamatwa akiwa na hati feki ya kusafiria, nyara za serikali na dawa za kulevya na kubainika alipitia KIA, uongozi mzima na wale waliokuwa zamu watawajibika kutafuta kazi nyingine ya kufanya.
ìMuda umekwisha naomba anzeni kuwataja wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, meno ya tembo na hati feki, na msingoje nije hapa nyie mkisikia tu naulizia jambo hilo, bakini nyumbani mtafute kazi za kufanya. Barua zenu mtaletewa kwenu ili mjisafishe badala ya kuendelea kuchafua jina zuri la uwanja huu,î alisema Dk. Mwakyembe.
Akijibu hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi ya KADCO, Balozi Gumbo Kibelloh, Waziri Mwakyembe, alipongeza mafanikio yaliyofikiwa na uwanja huo ya kuongeza idadi ya ndege, tuzo mbili kubwa za kimataifa zilizopatikana kutokana na kazi nzuri iliyofanyika.
Alisema kiwango cha ongezeko la asilimia 25 kwa jumla kwa wageni wa kimataifa kutoka asilimia 12 na wale wa ndani kufikia asilimia 36 na asilimia 44 kwa wanaobadilisha ndege ni suala la kujivunia, kwani ni mafanikio makubwa kwa uwanja huo hadi kuwa uwanja wa pili kwa ubora baada ya Australia.
Nakumbuka Novemba 12 au 13, nilipokea simu ya mwekezaji akiwa na ndege ya KLM, ambapo walifika hapa na kukuta giza tupu baada ya umeme kukatika. Sasa hii ni aibu kubwa na inaweza kutupunguzia mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa, lakini niliongea na TANESCO wanalishughulikia hilo,î alisema Dk. Mwakyembe.
Katika taarifa yake, Balozi Kibelloh alisema KIA unaliingizia taifa fedha nyingi kupitia kiwango kikubwa cha kodi ya zaidi ya sh. bilioni moja inayolipwa na uwanja huo kutokana na shughuli mbalimbali.

CCM inafuatilia kwa karibu kero za walimu


NA SULEIMAN JONGO, SONGEA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinasubiri utekelezaji wa maagizo yake kwa serikali kuhusu sekta ya elimu, ikiwemo kero za walimu.
Imesema Chama hakiwezi kufumbia macho kuchezewa kwa maslahi ya walimu kwa kuwa, kufanya hivyo ni sawa na kucheizea serikali.
Kauli hiyo alitolewa jana, mjini hapa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakati akizungumza na walimu wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu.
ìWalimu ni asilimia 68 ya watumishi wote wa serikali, hivyo kucheza na walimu ni sawa na kuichezea serikali inayoundwa na CCM,î alisema Kinana.
Alisema CCM inafuatilia kwa karibu mwenendo wa serikali katika kushughulikia changamoto za walimu, ikiwemo kulipwa maslahi na kuwekwa sawa kwa utaratibu wao wa ajira.
Akiwa ziarani kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, alitoa miezi sita kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuhakikisha inatatua changamoto za walimu na sekta ya elimu kwa jumla.
“Bado tunasubiri ripoti na utekelezaji wa agizo hilo, baada ya hapo tutajua cha kufanya, lakini kwa hili hatuna mzaha tutalifuatilia kwa karibu kwa kuwa hatuko tayari kulaumiwa kutokana na kasoro za baadhi ya watu tuliowapa madaraka,” alisema.
Kinana alisema anakerwa na vitendo vya dharau vya kutowalipwa kwa walimu, licha ya umuhimu wao kwa taifa.
“Tunaweza kuendesha nchi bila ya baadhi ya watumishi, lakini si walimu, bila wao taifa litaangamia kielimu.
“Tunasubiri muda tuliotoa, endapo utamalizika bila kufanyika kile tulichoelekeza tutatumia njia sahihi za kisheria, ikiwemo kuwatumia wabunge wetu kuwango’a wote walioshindwa kutimiza Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema.
Wakati huo huo, Kinana amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kufuatilia na kukomesha vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wanavyofanyiwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph mjini hapa.
Aidha, alimwagiza, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, kushughulikia masuala ya ubadilishaji wa kozi na mitaala ya chuo bila kuzingatia mfumo wa Tume ya Vyuo Kikuu nchini (TCU) unaoathiri taaluma nchini.
Katibu mkuu alisema, nakala za malalamiko ya walimu na wanafunzi yatapelekwa TCU na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili waeleze namna chuo hicho kinaendeshwa.

Mashauri ya rufani kutolewa uamuzi


Na Mary Gwera wa Mahakama ya Tanzania
MASHAURI 188 yanatarajiwa kusikilizwa na kutolewa uamuzi katika kipindi cha Novemba na Desemba, kutokana na vikao vya Mahakama ya Rufani vilivyoanza rasmi wiki hii.
Vikao hivyo vimeanza rasmi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar, ambapo kikao chake kitaanza rasmi Desemba 2, mwaka huu.
Kaimu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma, aliyasema hayo kupitia taarifa yake kuhusu vikao hivyo vya mahakama hiyo.
Alisema miongoni mwa mashauri ambayo yatasikilizwa yanahusisha mashauri ya rufani za jinai, madai na maombi mbalimbali ya rufani hizo.
Zahra alisema katika mkoa wa Arusha, rufani  45 zitasikilizwa na kutolewa uamuzi mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande.
Majaji wengine watakaosikiliza mashauri hayo ambayo 35 ni ya jinai na 10 ya maombi ya madai ni Nathalia Kimaro, Bernard Luanda na Jaji Bethuel Mmila.
Kwa upande wa Dar es Salaam, mashauri 81 yamepangwa kufanyiwa kazi na yatasikilizwa na majaji tofauti, kulingana na idadi ya kesi akizopangiwa kila mmoja.
Zahra aliwataja majaji wataosikiliza kesi katika mkoa huo kuwa Jaji Engela Kileo, Jaji  Sauda Mjasiri, Jaji William Mandia, Jaji Mbarouk Mbarouk na Jaji Stephen Bwana.
Alisema kwa upande wa Mwanza, mashauri 44 yatasikilizwa chini ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Edward Rutakangwa, Jaji Semistocles Kaijage na Jaji Kipenka Mussa.
Kaimu msajili huyo alisema kikao kingine kinatarajia kufanyika Zanzibar Desemba 2, mwaka huu, ambapo mashauri 18 yakiwa ni rufani za jinai na madai yatasikilizwa na kutolewa uamuzi katika kikao hicho.
Alisema katika kikao hicho kitakachofanyika visiwani Zanzibar, kitakuwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mbarouk, Jaji Luanda na Jaji Ibrahim Juma.
Zahra alisema vikao  hivyo vyote vitakamilika rasmi Desemba 13, mwaka huu na hivyo alitoa wito kwa wahusika kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha kazi hiyo muhimu.
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu nchini zimejiwekea utaratibu wa kusikiliza mashauri katika mikoa mbalimbali, lengo likiwemo  kupunguza idadi ya mashauri katika mahakama hizo.  Hali hiyo, inalenga pia katika kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.

Mkapa azilipua taasisi za binafsi


NA MOHAMMED ISSA
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, amezitaka taasisi binafsi kuwajibika kikamilifu badala ya kujifungia kwenye hoteli kubwa na kuandaa maandiko ya kuomba misaada.
Alisema taasisi nyingi za kiraia hapa nchini, kazi yake ni kuandaa makongamano, semina, badala ya kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hizo.
Mkapa, alisema hayo mjini Dar es Salaam jana, katika kongamano lililoandaliwa na taasisi ya Clb de Madrid na Uongozi Institute, ambapo alisistiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa kutegemea misaada.
Lengo la kongamano hilo, ni kutoa fursa kwa viongozi wa Afrika kuchambua upungufu na vikwazo vya maendeleo Afrika na kupendekeza mifumo mbadala itakayoweza kufungua kurasa mpya za mchakato wa maendeleo.
Rais huyo mstaafu, alisema pamoja na kuwa na taasisi nyingi nchini, lakini bado hazitekelezi wajibu wao kama ilivyotarajiwa.
Alisema bado zina wajibu mkubwa wa kuleta mabadiliko katika maendeleo ya nchi, bila kutegemea misaada kutoka kwa wahisani.
Kwa mujibu wa Mkapa, kazi zinazofanywa na taasisi hizo ni kujifungia kwenye mahoteli makubwa na kuandaa maandiko ya kuomba misaada kutoka nje, na kwamba, umefika wakati kwa taasisi hizo kutekeleza wajibu wake ipasavyo badala ya kutegemea misaada ya wahisani.
Naye Rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, alisema ni vyema taasisi zote za kiraia kuhusishwa katika hatua za awali za mipango ya maendeleo, jambo ambalo zitasaidia kusukuma maendeleo ya taifa.
Obasanjo, alisema iwapo itabainika kuwa kuna tatizo la mikataba mikubwa ya nchi ni vyema ikatafutwa taasisi itakayotoa miongozo kwenye sekta ya uwekezaji.
Rais mstaafu wa Boswana, Festus Mogae, alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika nchi yake yameigwa Ulaya.
Alisema nchi hiyo ni ndogo kuliko Tanzania na Nigeria, lakini imepiga hatua kubwa kutokana na kuiga mafanikio kutoka kwenye nchi nyingine, zikiwemo za Ulaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, alisema maoni ya Rais Mkapa na Obasanjo ni mazuri na kuna umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha, kwenye sekta za uwekezaji.

Ujenzi kituo cha afya UDOM wakamilika


Na Theodos Mgomba, Dodoma.
UJENZI wa kituo cha uchunguzi wa kiafya kilichogharamiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umekalimika kwa asilimia 96.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula, alisema kituo hicho kinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Kikula, kitakuwa na uwezo wa kuchunguza magonjwa yote makubwa ambayo kwa sasa baadhi hayana uwezo wa kuchunguzwa nchini.
Alisema pamoja na kufunguliwa kwa kituo hicho, mfuko huo pia unatarajia kujenga hospitali kwa ajili ya kufundishia wanafunzi.
Alisema ujenzi huo utaanza hivi karibuni na hospitali hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya, kwa kuwawezesha kupata uelewa mkubwa katika masomo yao.
Kitatoa pia huduma kwa wananchi wa kawaida na wale wa nje ya nchi.
Wakati huo huo; Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Zhengzhough cha nchini China, kimeanzisha kituo cha kufundishia lugha ya Kichina katika chuo cha UDOM.
Makamu Mkuu wa Chuo cha UDOM, alisema kilianzishwa mapema Februari mwaka huu.

Polisi yamteua Athumani Hamis


NA JESSICA KILEO
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limemteua aliyekuwa Mpigapicha Mkuu wa gazeti la HabariLeo, Athuman Hamis, kuwa balozi wa uzinduzi wa kampeni ya usalama barabarani kuelekea mwisho wa mwaka.
Kampeni hiyo imeanzishwa kutokana na changamoto ya ajali za barabarani zinazotokea kwa wingi mwishoni mwa mwaka na kusababisha madhara maklubwa ya vifo, ulemavu wa kudumu, uharibifu wa mali na miundombinu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana mjini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, alisema, wamemteua balozi huyo katika kampeni hiyo ili kupunguza wimbi la ajali.
Silima alisema kwa kuwa Hamisi ni muhanga wa ajali za barabarani, wanaamini atatoa elimu kwa watumiaji wa aina zote wa barabara na kukubalika kwa kuwa anayo picha ya njia zinazosababisha ajali.
Hamisi ambaye amekuwa mlemavu wa viungo baada ya kupata ajali ya gari miaka mitano iliyopita, anatarajiwa kuongoza kampeni hiyo ili kuelimisha jamii juu ya madhara ya ajali hiyo.

Nchi masikini kususia mikutano ya kimataifa


NA RAMADHANI MKOMA, WARSAW, POLAND
NCHI zinazoendelea zimetishia kujitoa katika mikutano ijayo ya kimataifa ya mabadiliko ya hali ya hewa, iwapo mataifa yaliyoendelea yataendelea kusuasua kutoa fedha kusaidia nchi masikini kukabiliana na athari zake.
Hayo yalijitokeza katika mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Mazingira kutoka Afrika uliofanyika juzi, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unaofanyika mjini hapa.
Waziri wa Nchi Ofisi za Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huviza, alizasema hayo alipokuwa akizungumzia vikao vya awali vya maandaliazi ya mkutano huo, unaofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Warsaw mjini hapa.
Hata hivyo, Terezya alisema kilio cha mawaziri hao kitawasilishwa kwa marais wa Afrika kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete ili kuzungumza na viongozi wa mataifa makubwa ili kushawishi watekeleze ahadi zao kwa mataifa masikini.
Rais Kikwete atawasilisha kilio hicho akiwa ni Rais wa Kamati za Mazingira katika Umoja wa Afrika. Rais Kikwete aliwasili mjini hapa jana.
Kwa mujibu wa Dk. Terezya ambaye ni Rais wa Mawaziri wa Mazingira Afrika, mataifa yaliyoendelea yana kila sababu za kufidia mataifa masikini kutokana kuwa wazalishaji wakuu wa hewa ukaa ambayo imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko hayo.
Alisema Afrika inachangia asilimia tatu tu za hewa ukaa, licha za madhara na athari kubwa inazokumbana nayo kutokana na mabadiliko ya hali za hewa.
Waziri huyo alisema matukio za mafuriko, mmomonyoko katika maeneo za fukwe ya bahari yanachangiwa kwa kiasi kukubwa na mabadiliko hayo ya hali za hewa.
Kutokana na hilo, Terezya amewataka Watanzania kujikita katika upandaji wa miti itakayosaidia kunyonya hewa ukaa na kupooza bahari na hivyo kuepuka mawimbi makubwa yanayoweya kusababisha mafuriko.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza ya Rais, Zanzibar, Fatma Ferej, alisema athari za mabadiliko ya hali ya hewa zimeanza kujionyesha visiwani humo, ambapo baadhi ya maeneo ya fukwe yameliwa na bahari.
Pia, alisema utafiti uliofanywa umebaini kuwepo kwa maeneo zaidi ya 100 ambayo ardhi yake imemegwa na bahari na hivyo kutishia shughuli za kilimo kutokana na maeneo hayo kuwa na chumvi.
Fatma alisema katika maeneo hayo, wananchi wamekuwa wakipata ugumu wa kupata maji safi ya kunywa kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha chumvi.
Kwa mujibu wa Fatma, mabadiliko hayo ya hali ya hewa yameanza kuathiri miundombinu, ikiwemo kuharibika kwa baadhi ya madaraja kutokana na kuliwa na maji chumvi.