Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Saturday 28 December 2013

KAIMU Kamanda wa Kikosi cha Polisi TAZARA, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Innocent Mgaya akionyesha vipande vya meno ya tembo na jino la kiboko yaliyokamatwa wilayani Morogoro Vijijini yalipokuwa yakisafirishwa kwa treni ya abiria kupelekwa Dar es Salaam,juzi.Kulia ni Mrakibu wa Polisi, Shaban Ng'wamkay.(Picha na Jumanne Gude).

Wiki ngumu kwa Kikwete


NA MWANDISHI WETU
Wiki inayoanza kesho, ni ya kufanya uamuzi mgumu kwa Rais Jakaya Kikwete  kutokana na mtikisiko ulioikumba serikali yake wakati uliopita wa Bunge.
Hivi ndivyo inavyoonekana kutokana na mazingira ambayo yalisababisha mawaziri wane,  kujiuzulu na yeye kuridhia kutengua uteuzi wao.
Mawaziri waliojiuzulu na nafasi zao kwenye mabano ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la KujengaTaifa), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Mawaziri hao waling’atuka katika nafasi hizo baada ya ripoti ya Kamati ya Kudumu  ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kubaini matatizo yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kutokana na dosari hizo, wabunge waliwataka mawaziri hao kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia watendaji wao wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Mbali na mawaziri hao, wabunge pia walitaka Rais Kikwete amwajibishe Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa madai ya kushindwa kusimamia serikali katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa tuhuma za ubadhirifu uliokithiri ndani Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMESEMI) ambayo iko chini yake.
Wabunge hao walikwenda mbali zaidi kwa kutaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, pia ang’oke  na mwenzake wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika.
Waziri Hawa alidaiwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya maofisa wa TAMISEMI waliotafuna mabilioni ya fedha wakati Mkuchuka awajibishwe kutokana na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, iliyo chini yake, kuhusika na vitendo viovu wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Licha ya mawaziri hao,  Rais ana jukumu la kutafakari na kuchukua hatua dhidi ya mawaziri waliodaiwa kuwa mizigo katika utendaji wao, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya kusini.
Mabadiliko hayo makubwa ya baraza la mawaziri yanatarajiwa kuwa ya tatu tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005. Mabadiliko ya kwanza yalifanyika mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kujiuzulu na mawaziri wengine wawili.
Wengine walikuwa Dk. Ibrahm Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Nazir Karamagi (Nishati na Madini) kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ilitoundwa kuchunguza mkataba wa ufuaji umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond Development LLC. Kuwagusa.
Mara ya pili ilikuwa mwaka jana baada ya mawaziri kadhaa kutuhumiwa katika ripoti mbalimbali za kamati za bunge juu ya vitendo vya ubadhirifu na ufisadi.
Mbali na Rais kuwa katika wakati mgumu wa kulisuka upya baraza lake la mawaziri,  pia ana kazi ngumu ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambalo linatarajiwa kufanyika Februari, mwakani.
Rais katika kutafakuri huko, haishii hapo, kwani pia atakuwa na kazi ngumu ya kufikiria juu ya Ripoti ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na wabunge, kushauri na kutaka watendaji wa serikali, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika kutokana na madudu yaliyojitokeza wakati wa Opereshini Tokomeza Ujangili.
Kutokana na mambo hayo, Rais ataumaliza mwaka na pengine hata kuuanza mwaka kwa kuwa na majukumu mazito ya kufanya.
Wakati Rais akiwa katika wakati huo, pia wapo mawaziri ambao huenda wakamaliza mwaka na wengine kuanza mwaka wakiwa na huzuni ya kutemwa na wengine furaha ya kuteuliwa.

Sumaye awazodoa wasaka madaraka


NA MWANDISHI WERU
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amewazodoa wanaotafuta madaraka kuwa uongozi hautafutwi kwa udi na uvumba wala kwa rushwa bali anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii.
“Anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii husika kutokana na ubora wake na siyo vishawishi vyake. Ni ukweli uliowazi kuwa uchaguzi wetu sasa umegubikwa na rushwa na vishawishi vingi na siyo ubora, uhodari wala tabia ya anayetaka nafasi hiyo ya uongozi,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa: “Hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za kuwanunua wapiga kura vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi ngazi ya urais. Huu ni utaratibu wa hatari na lazima tuupige vita kwa pamoja.”
Sumaye aliyasema hayo jana wakati wa kuchangia ujenzi wa ukumbi wa Parokia ya Mawella ya Kanisa Katoliki jimbo la Moshi.
Alisema wakati Watanzania wanasubiri kuingia mwaka mpya wa 2014, wanapaswa kutambua kuwa huo ni mwaka muhimu kwa kwa mustakabali wa taifa kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi katika ngazi za serikali za mitaa na ni mwaka wa maandalizi kwa uchaguzi mkuu.
“Nataka niliweke wazi tangu mwanzo kuwa mimi siisemi serikali yangu wala sitamsema mtu yeyote bali nitakayoyasema na siyo mara yangu ya kwanza kuyasemea ni kupiga vita tabia mbaya. Katika kukemea mabaya hayo inawezekana mtu akajihisi anasemwa kama hayo mabaya anayafanya. Dawa siyo kumchukia anayekemea tabia hiyo mbaya, bali ni kuachana nayo,” alisema.
Aliendelea kufafanua kuwa katika utaratibu wa demokrasia sahihi na halisi wapiga kura hutakiwa kuwachagua viongozi au kiongozi kufuatana na sifa nzuri za uongozi alizonazo mgombea kama vile ushupavu, uaminifu, uadilifu na nyingine muhimu.
Sumaye alisema kama ilivyokuwa zamani, mtu anayetakiwa kuwa kiongozi anatafutwa na jamii na siyo yeye kusaka uongozi.
“Mbaya zaidi ni pale msaka uongozi atakapotafuta nafasi hiyo kwa njia zisizofaa kama vile rushwa na kuwanunua wapiga kura....utaratibu wa kuwekwa au kuchaguliwa katika nafasi bila vishawishi vya rushwa uliotumika tangu enzi za kale ndiyo unaotakiwa kutumika hadi sasa, labda kwa kuboreshwa kutegemeana na mazingira,” alisema.
Huku akinukuu baadhi ya vifungu katika Biblia, alisema wananchi wanapaswa kuigopa rushwa kwa kuwa hata vitabu vya dini vimeikemea.
Alisema kiongozi mtoa rushwa hafai kuchaguliwa kwa kuwa hawezi kuwafikisha mahali popote wananchi na badala yake atatumia nafasi atakayopewa kutengeneza maslahi yake binafsi na marafiki zake.
Sumaye alisisitiza kuwa: “Huo ndiyo mwisho wa upeo wa macho yake kuona. Ataona ndani ya duara lake na marafiki zake na wengine akitutazama anaona giza tu kwa sababu kwetu, yeye amepofuka na tuko nje ya duara la upeo wa macho yake.”
Kutokana na hali hiyo aliwaomba viongozi wa dini kushiriki kikamilifu kupiga vita vitendo viovu vya rushwa, ufisadi, kuuza dawa za kulevya au kuua.

Alisema wakati wa kuingia kwenye kipindi cha uchaguzi, hivi sasa kuna mambo yameanza kujitokeza ikiwemo fadhila kuwa nyingi kwa baadhi ya wanaowania nafasi hasa zile za juu.
“Fadhila zimeanza kuwa nyingi katika baadhi ya sehemu na kwa baadhi ya nafasi hasa nafasi za juu na wapiga kura tayari wameanza kupigwa mnada na kupangiwa bei kulingana na uhodari au umuhimu wa nafasi aliyonayo mhusika. Haya ni mambo machafu ambayo hatutakiwi tuyafumbie macho bali tupambana nayo kwa nguvu zote,” alionya Sumaye.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi anazofanya kupambana na uoza wa rushwa katika jamii, hasa rushwa nyakati za uchaguzi.
Pia, Sumaye alibainisha kuwa hatakoma kupiga vita rushwa na kuwa anafanya hivyo sio kwa malengo ya kuwania urais mwaka 2015, bali anatimiza wajibu kwa nchi yake.

TAZARA wakamata meno ya tembo


NA MWANDISHI WETU
KIKOSI cha Polisi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) kinamshikilia Ally Juma baada ya kumkuta akisafirisha vipande 14 vya meno ya tembo na jino moja la kiboko.
Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho, Innocent Mgaya, alisema mjini Dar es Salaam, jana, kuwa vipande hivyo vilikamatwa saa 12.15, jioni, Desemba 26, katika Stesheni ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro.
Alisema vipande hivyo vilikuwa ndani ya treni ya abiria yenye namba M2 iliyokuwa ikitokea Zambia kwenda Dar es Salaam.
Mgaya alisema kwa mujibu wa maofisa wa wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasi na Utalii, vipande hivyo vina thamani ya sh. milioni 25.5 wakati jino la kiboko ni sawa sh. milioni 2.4.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati askari wao wa intelijensia wakiwa kazini katika eneo hilo walipopata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwepo kwa mtu mwenye meno hayo.
Alisema vipande vya meno ya tembo vina uzito wa kilo 29, huku jino la moja kiboko lina uzito wa gram 900, ambapo vyote vilikutwa kwenye mabegi mawili na begi moja lilikuwa na vipande vinane huku lingine likiwa navyo saba.

Kinondoni yaibua kidedea Dar


NA JUMANNE GUDE
MANISPAA ya Kinondoni imeongoza kutoa wanafunzi wengi waliofaulu na kujiunga na kidato cha kwanza mwakani katika mkoa wa Dar es Salaam.
Wanafunzi waliofaulu mtihani katika manispaa tatu za mkoa wa Dar es Salaam wako 46,648 ambapo kwa Kinondoni watakaojiunga kidato cha kwanza mwakani ni asilimia 80, ikifuatiwa na manispaa Ilala yenye asilimia 75 huku Temeke ikitoa asilimia 70.
Akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani mkoani humo, Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Raymond Mapunda, alisema wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu walikuwa 63,378 ambapo kati yao 46,468 wamefaulu.
Mapunda alisema wanafunzi waliochaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na kidato cha kwanza wako 34,852, huku wanafunzi 11,796 wakikosa nafasi ambapo watasubiri chaguo la pili.
Alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za ufaulu mzuri wako 70 ambapo wasichana ni 36 na wavulana wako 34, wakati wanafunzi waliochaguliwa kujiunga katika shule za ufundi wako 76.
Pia, Mapunda alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni ambazo kwa vijijini ni 41, huku shule zinazomilikiwa na Mkoa wa Dar es Salaam wamepelekwa wanafunzi 1,892.
Alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za serikali za wananchi wako 32,773 ambapo Manispaa ya Kinondoni ina wanafunzi 12,218 huku Temeke wanafunzi wakiwa 11,179 na Ilala wako 9,376.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo, Theresia Mmbando, alisema mkoa humo umebaini wanafunzi wanafaulu kutoka katika shule za msingi za mijini.
Alisema ifikapo Februari 15, mwakani, manispaa hizo zinapaswa kuwasilisha taarifa ya hali halisi ya wanafunzi wote walioripoti ili waandae chaguo la pili mapema kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

January awawezesha wapanda pikipiki Mza


NA MWANDISHI WETU, MWANZA
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amewamwagia neema vijana wa bodaboda mkoani  Mwanza kwa kuwapatia mikopo ya pikipiki 1,745.
Pia amewakatia bima ya maisha waendesha bodaboda 100 ili kuhakikisha wanafanya kazi yao katika mazingira salama
wanaposafirisha abiria katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika semina ya masuala ya bima kwa wanachama wa Umoja wa Waendesha Pikipiki mkoa wa Mwanza, January alisema lengo ni kuwawezesha vijana wa kujiajiri na kuwa waajiri.
Semina hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Nyamagana ambapo vijana wa bodaboda zaidi ya 1,000 walikusanyika wakiwa wamevaa fulani zenye ujumbe usemao ‘boda boda ni ajira, lakini usalama kwanza’.
Alisema mchakato wa kuwawezesha waendesha pikipiki wa Mwanza ulianza miaka mitatu iliyopita baada ya kuombwa na
Mwenyekiti wa umoja wao, Makoye Kayanda.
January alisema lengo ni kuhakikisha vijana hao wanakuwa na ajira ya uhakika na usalama wa maisha yao kwani kwa sasa  pikipiki zao zina bima lakini wenyewe hawana bima.
Alichezesha bahati nasibu kwa kwa kuwasshindanisha waendesha pikipiki waliojiandikisha majina na namba za bodaboda zao, ambapo washindi 100 , walikatiwa bima ya sh. 5,000 kila mmoja kwa ajili ya kujilinda na safari.
January ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alisema ajali za pikipiki zinaua ambapo mwaka 2011 watu 695 walikufa kwa ajali hizo na mwaka jana idadi ya vifo ilifikia 930.
Alisema kupitia bima hiyo vijana watakaoumia watalipwa fedha za matibabu na akipata ulemavu wa kudumu atalipwa sh. milioni 10.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alimpongeza January kwa jitihada za kuwawezesha vijana hao na kuwataka kufanya kazi kwa kujiwekea malengo ya kufanya kazi zingine, kwa kuwa pikipiki ni kazi ambayo
inafanywa na vijana na sio wazee.
Mapema Mwenyekiti wa vijana hao, Kayanda, alisema January ametimiza ndoto za vijana hao kwa kuwa wengi wao wameajiriwa na watu na wamekuwa wakifukuzwa kazi bila taarifa na kusababisha maisha yao kuyumba.
Katika semina hiyo iliyoshirikisha kampuni za bima za NIC na Ndege, January alikubali ombi la kuwa mlezi wa umoja wa waendesha bodaboda ambao una wanachama zaidi ya 400 mkoani huo.

Wahimizwa kupeleka majina wajumbe bunge la katiba


Na Hamis Shimye
SERIKALI imewataka wananchi wanaoongoza makundi mbalimbali katika jamii kupeleka majina ya watu ambao wanaona yanafaa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kabla haujafika.
Uamuzi huo, unatokana na taarifa ya Rais Jakaya Kikwete iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi ikitoa mwaliko kulingana na mamlaka aliopewa Rais katika kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) ambapo mwaliko huo ulitangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 443 la Desemba 13, mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema umeshatolewa muongozo wa namna ya kupatikana kwa wajumbe hao ambao watawakilisha wananchi, ambapo mwisho wa kupokea majina hayo ni Januari 2, mwakani.
Alisema bunge hilo linatarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 200 kutoka makundi mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kutuma majina yao kabla muda haujafika.
“Majina ya makundi yanayotakiwa kutumwa ni yale yaliyosajiliwa kisheria, ambapo watume majina yao. Kutakuwepo na wajumbe 20 kutoka katika taasisi mbalimbali zisizokuwa za kiserikali kati yao nusu wanatakiwa watoke Zanzibar wakiwemo wanawake na wanaume pamoja na wajumbe wengine 20 katika taasisi za kidini, wajumbe 40 kutoka vyama vya siasa vilivyoandikishwa na kusajiliwa,”alisema.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitoa taarifa ya mwaliko huo ambao pia ulitangazwa katika magazeti ya kawaida.
Makundi ambayo yametajwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za dini, yyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu, makundi ya watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wafugaji, vyama vinavyowakilisha wavuvi, vyama vya wakulima na makundi mengine yenye malengo yanayofanana.

Tuesday 24 December 2013

Ongezeko bei ya umeme sawa, lakini...


NA WAANDISHI WETU
WASOMI na wanasiasa wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa kupandishwa gharama za umeme, zitakazoanza kutumika Januari mosi, mwakani.
Wamesema kupanda bei nishati hiyo  kunapaswa kwenda sambamba na utoaji huduma bora ya umeme, na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA), juzi ilitangaza kupandisha viwango vya bei ya umeme, ambavyo vimepanda kwa kati ya sh. 100 na sh. 306 kwa uniti, kulingana na aina ya watumiaji kuanzia wateja wadogo wa nyumbani, wa kati na wenye viwanda vikubwa. Bei hizo zitadumu hadi mwaka 2016.
Wizara ya Nishati na Madini, imesema imeridhia ongezeko hilo ili kuifanya nishati ya umeme kuwa endelevu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, alisema jana kuwa, Sera ya Nishati ya mwaka 2003 inaeleza kuwa, gharama za huduma ya umeme ziendane na gharama halisi za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji kwa watumiaji.
Alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo ya dharura ya kufua umeme, ili kuiwezesha TANESCO kuendelea kutoa huduma.
Mhandisi Mwihava alisema takwimu zinaonyesha gharama za kuzalisha umeme kwa mitambo ya maji ni rahisi, lakini kwa sasa uzalishaji umeshuka kutokana na uhaba wa maji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwihava, mitambo hiyo kwa sasa inazalisha megawati 111 wakati uwezo wake ni megawati 561, hivyo kiasi kikubwa cha umeme kinazalishwa kwa mitambo inayoendeshwa kwa mafuta na gesi asilia. Mitambo ya gesi inazalisha megawati 320 na mafuta megawati 210.
Alisema kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu, chenye uwezo wa kuzalisha megawati 204 kwa sasa hakizalishi kabisa kutokana na uhaba wa maji, huku kituo cha Mtera kikizalisha megawati 30, badala ya 80, na Pangani kinazalisha megawati 20 badala ya 68.
Mhandisi Mwihava alisema inapowashwa mitambo ya IPTL na kuendeshwa kwa mwezi mmoja, huigharimu serikali sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura ili kuiwezesha TANESCO kuendelea kutoa huduma.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa EWURA, Felix Ngamlagosi, alisema juzi kuwa, bei mpya imetolewa baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa maombi ya TANESCO.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wasomi na wanasiasa walisema kuna umuhimu wa ongezeko hilo la bei kuangaliwa kwa makini ili liwe na manufaa kwa shirika na wananchi.
Profesa Hosea Kayumbo, alisema si mchumi, lakini kuna umuhimu wa kupandisha bei kwa kuwa itasaidia kuboresha huduma ya umeme na mtumiaji (mwananchi) anapaswa kutekeleza.
“Bei hazirudi nyuma, na suala hili halikwepeki. Wananchi wanapaswa kulipa ingawa kweli ni mzigo mkubwa kwa mwananchi,’’ alisema.
Dk. Benson Bana alisema kupanda kwa bei ni suala nzuri lakini kwa wakati huu si muafaka, kwani ni kuwaumiza wananchi na inaonyesha udhaifu na ukinzani wa sera kati ya serikali na taasisi zake.
“Serikali ipo katika mpango wa kuhakikisha inawaunganishia watu wengi zaidi umeme lakini hapo hapo  mnakuja na tangazo la kupandisha bei. Hii ni kuwaumiza wananchi, hivyo tunapaswa kulitazama kwa makini,’’ alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema uzalishaji wa umeme uko juu na TANESCO lazima ifidie gharama za uzalishaji. Alisema mwenye jukumu la kuchangia ni mwananchi.
“Tumekuwa tukisikia TANESCO ikizalisha umeme kwa bei kubwa na mauzo yake ni madogo, hivyo lazima itafilisika. Kuongezwa bei kutasaidia kupungua gharama za uzalishaji wa umeme,’’ alisema.
Mwenyekiti wa TLP, Dk. Augustino Mrema, alisema bei hiyo inawaumiza wananchi na kwamba, TANESCO ilipaswa kutatua matatizo yaliyopo na si kupandisha bei ya umeme.
Alisema taifa linakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ya nishati ya umeme, ambao umekuwa wa shida na hakuna uhakika wa upatikanaji wake.
Katika mchanganuo wa viwango vipya vya bei, EWURA imesema wateja wamegawanywa katika makundi matano, la kwanza likiwa D1, ambalo ni la wateja wadogo wa nyumbani wanaotumia uniti 0 hadi 75, ambalo bei imepanda kutoka sh. 60 hadi sh. 100 kwa uniti.
Kundi la pili ni T1, lenye watumiaji wakubwa wa umeme wa nyumbani, wafanyabiashara ndogo ndogo, mashine za kusaga nafaka, taa za barabarani na mabango wanaotumia uniti 76 na kuendelea, ambao watanunua uniti moja kwa sh. 306 badala ya sh. 221 za awali.
Katika eneo hilo, TANESCO walitaka ongezeko la sh. 131 kwa uniti lakini EWURA ilipitisha ongezeko la sh. 85.
EWURA imesema kundi la tatu ni T2 la watumiaji wa umeme wa kawaida, unaopimwa katika msongo wa voti 400, ambao wastani wa matumizi yao kwa mwezi ni zaidi ya sh. 7,500.
Kundi hilo linahusisha  wafanyabiashara wakubwa na viwanda vya kati, ambao watanunua uniti kwa sh. 205 badala ya sh. 132 za awali, sawa na ongezeko la sh. 73. TANESCO iliomba kuongeza sh. 148.
La nne ni kundi la T3- MV, lenye wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa kati, ambalo EWURA imeridhia  kiwango cha sh. 166 kwa uniti badala ya sh. 121 za awali (ongezeko la sh. 45). Shirika hilo liliomba kuongeza sh. 148 kwa uniti.
Kundi la tano ni la T3-HV la wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu wa voti 66,000 na zaidi, ambao watalipa sh. 159 kwa uniti badala ya sh. 106 za bei ya sasa (ongezeko la sh. 53). TANESCO iliomba kuongeza sh. 80.
Hata hivyo, EWURA imesema bei hizo zitakuwa zikifanyiwa marekebisho kila baada ya miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango cha bei za mafuta, mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha na upatikanaji wa ruzuku kutoka serikalini.

Kova: Watoto, walevi marufuku kuogelea


NA JUMANNE GUDE
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku watoto na walevi kwenda kuogelea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alitoa onyo hilo jana alipozungumza kuhusu kuimarishwa ulinzi wakati wa sikukuu ya Krismasi leo.
Alisema ulinzi umeimarishwa maeneo yote ya jiji na kwenye ufukwe wa bahari kutakuwa na vituo vya polisi vya muda.
“Watoto wenye umri chini ya miaka 15 hawataruhusiwa kuogelea. Pia kuna baadhi ya watu wakishalewa wanataka kuogelea, hawa nao watadhibitiwa na askari,” alisema.
Aliwataka wananchi watakaokwenda ufukweni kuwa waangalifu au wawe na utaalamu wa kuogelea ili kuepusha vifo vinavyotokana na watu kushindwa kuogelea.
Kwa mujibu wa Kova, wamejiandaa vyema na watashirikiana na askari wa Zimamoto na Uokoaji, Wanamaji na Kikosi cha Usalama Barabarani kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani.
Alisema wakati wa sikukuu nyumba zote za ibada, hususan makanisa yatalindwa kwa kushirikiana na kamati za ulinzi za makanisa.
Kova aliwataka wananchi watoe taarifa mapema kwa askari endapo watabaini kuna uvunjifu wa amani katika maeneo yao, ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka.
Alitoa rai kwa madereva kuzingatia na kuzifuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea.
“Kuna baadhi ya madereva wamekuwa wakiendesha magari wakiwa walevi au kwa mwendo kasi, kikosi cha usalama barabarani kitawashughulikia,” alisema.

Pinda akabidhiwa msaada pikipiki 44


Na mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amepokea pikipiki 44 za msaada kutoka Ubalozi wa China na Kampuni ya Fu-Tang ya nchini humo.
Alikabidhiwa msaada huo jana, mbele ya viongozi wa Wilaya ya Mlele, katika hafla iliyofanyika kijiji kwao Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing, akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo na wakazi wa kijiji cha Kibaoni, kabla ya kukabidhi msaada huo, alisema anaamini pikipiki hizo zitasaidia kuleta maendeleo.
“Tunatarajia matumizi ya pikipiki hizi yatasaidia kuleta maendeleo ya haraka na hatimaye kuongeza kipato cha wakazi wa wilaya hii,” alisema. Ofisi ya balozi huyo imekabidhi msaada wa pikipiki 20.
Alisema China ina wakazi takriban bilioni 1.3 na anatamani kuona walau kila raia wa nchi hiyo ananunua kilo moja ya chakula kutoka Tanzania.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza pikipiki cha FEKON, ambacho ni kampuni tanzu ya Fu-Tang, Zheng Bing, alisema utaratibu utakapokamilika, watajenga kiwanda cha kutengeneza pikipiki na kompyuta nchini ili kuongeza ajira kwa Watanzania. Kampuni hiyo ilikabidhi pikipiki 24.
Waziri Mkuu Pinda kwa upande wake, alimshukuru Balozi Lu na kampuni ya Fu-Tang kwa msaada huo, na kuahidi kuzigawa ili ziwasaidie watendaji kusimamia kazi, hivyo kuharakisha maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo.
“Tuna kata 24, kwa hiyo kila kata itapewa moja. Hiyo pikipiki si ya katibu kata binafsi, bali ya kata, kwa hiyo katibu kata atakuwa ndiye msimamizi,” alisema.
Waziri mkuu ambaye yuko Kibaoni kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka, alisema pikipiki saba zitapelekwa kwenye vituo vitano vya afya vya Mamba, Usevya, Inyonga, Katumba na Kanoge, na zahanati za Nsimbo na Kasansa.
Alisema pikipiki zingine nane zitapelekwa katika shule za sekondari za Sitalike, Machimboni, Magamba, Nsimbo, Mtapenda, Utende, Inyonga na Kasokola.
Pinda alisema wengine watakaofaidika na mgawo huo ni watendaji wa CCM wa wilaya ya Mlele, ambao watapatiwa moja, jumuia za Chama katika wilaya hiyo zitapatiwa tatu na moja itagawiwa kwa CCM mkoa wa Katavi.
Kuhusu uzalishaji wa chakula cha kutosha wakazi bilioni 1.3 wa China, alisema itabidi Tanzania izalishe magunia milioni 13 ya nafaka ili kufikisha lengo hilo.
Waziri Mkuu Pinda alikwishapokea msaada wa pikipiki 23 kutoka kwa wafadhili wengine na kuzigawa sita kwa Jeshi la Polisi, 13 kwa vikundi vya vijana na nne kwa shule za sekondari.

Afariki kwa kujirusha kutoka kwenye bodaboda


NA WATANDA BURERWA, DACICO
MKAZI wa Dar es Salaam, ambaye hajafahamika jina, amekufa baada ya kuruka kutoka kwenye pikipiki na kugongwa na kichwa cha treni.
Pikipiki hiyo ilikaribia kugonga kichwa cha treni, eneo la Buza, Tandika, wilayani Temeke.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni.
Alisema mtu huyo alikuwa amepanda pikipiki yenye namba ya usajili T 179 CDB, aina ya Boxer, iliyokuwa ikiendeshwa na Kelvin Alinda (27), mkazi wa Yombo Makangarawe.
Kamanda Kiondo alisema abiria huyo aliona dereva anakwenda kugonga treni, hivyo aliamua kujirusha.
Alisema baada ya kuruka alianguka kwenye reli, hivyo kukatwa mguu wa kulia na treni na alikufa papo hapo.
Kamanda alisema dereva wa pikipiki hiyo alinusurika na kukimbia. Alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.

Heroin yawatupa selo vijana wanne


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
VIJANA wanne wanashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa eneo la Elikyurei, wilayani Arumeru, wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi, saa 12.30 jioni, wakiwa na gramu 100 za dawa hizo, ambazo zingeuzwa sh. milioni 10 zingepatikana.
Kamanda Sabas aliwataja vijana hao kuwa, Seif Bakari (28), Hamid Makame (29), Evance Gidion (29), mkazi wa Ngarenaro na Abraham Hamis (23) wa Kaloleni.
Alisema kukamatwa kwao kunatokana na taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Sabas alisema watuhumiwa walikamatwa wakiwa ndani ya chumba cha mmoja wao, wakiwa wametengeneza kete 25 za dawa hiyo.
Alisema polisi wanaendelea kuwahoji watuhumiwa na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, watu wanne wamekamatwa eneo la daraja la Engotooleshokopeyi, wilayani Ngorongoro, wakiwa na bunduki iliyofutwa namba aina ya SMG, ikiwa na risasi tano.
Aliwataja waliokamatwa kuwa, Papai Tooko (40), Leshnga Mawoi (45), Silanga Olesitoi (42) na Sombe Ngaina (30).

Saturday 21 December 2013

Mawaziri kufumuliwa


WAANDISHI WETU, DAR NA DODOMA
BAADA ya mawaziri wane kuachia ngazi kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza Ujangili, hofu ya kutemwa imetanda miongoni mwa mawaziri, imefahamika. Mawaziri waliojiuzulu baada ya shinikizo la wabunge kutaka wawajibike ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi.
Kujenga Taifa) na Dk. David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi). Habari ambazo Mzalendo imezipata, zinaeleza kuwa
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kufumua baraza la mawaziri, huku baadhi ya waliomo wakidaiwa kuachwa kutokana na utendaji na kuhusishwa na kashfa ya ujangili.
Kwa mujibu wa habari hizo, mabadiliko hayo huenda yakatangazwa wakati wowote kuanzia sasa na huenda yakawafanya baadhi ya mawaziri kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya kwa huzuni.
Chanzo cha habari kimebainisha kuwa baadhi ya mawaziri ambao wako katika hatari ya kuachwa wamekuwa katika
wakati mgumu baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kuwatuhumu kuwa wana uhusiano katika
ujangili ama kupitia ndugu zao au wanasiasa.
“Kwa jumla hali ni tete baada ya ripoti ya (James) Lembeli
(mwenyekiti wa kamati hiyo) kuwasilishwa na baadhi ya wabunge
na mawaziri kudaiwa kuhusika kwenye mtandao wa ujangili. Wengi wamejawa hofu huku baadhi wakisema wazi kwamba hawana hakika na hatima yao,” kilisema chanzo chetu.
Mbali na mawaziri waliojiuzulu kisha na Rais Kikwete kuridhia na kutengua uteuzi wao, pia wamo baadhi ya mawaziri ambao
wabunge wamekuwa wakitaka watimuliwe.
Licha ya ripoti ya Lembeli, wakati wa mjadala wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyowasilishwa wiki
iliyopita, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora, alitamka
bayana kwamba Rais anapaswa kumtimua Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Ofi si ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),
Hawa Ghasia, kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji
wanaofanya ubadhirifu wa malimioni ya shilingi. Mbunge huyo pia pamoja na wengine, juzi walisisitiza kuwa Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kuwa kasoro zilizojitokeza kwenye operesheni tokomeza pamoja na ubadhirifu unaofanywa
na maofi sa wa serikali katika wizara mbalimbali.
Hilo pia liliwekewa msisitizo baada ya Moses Machali (Kasulu Mjini- NCCR Mageuzi) ambapo alisema wabunge wanatafuta saini kwa ajili ya kuwasilisha hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani
na Pinda.
Mbali na mawaziri hao, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, alisema Waziri wa Nchi Ofi si ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, pia anapaswa kuwajibika kwa kuwa maofi sa wa Usalama wa Taifa, walishiriki katika operesheni hiyo ambayo imelitia doa taifa.
Hofu ya kupanguliwa kwa baraza la mawaziri pia inakuja baada ya hivi karibuni kuwepo kwa orodha ya mawaziri ambao wamekuwa wakidaiwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu
yao. `
Mawaziri hao ni Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika) na naibu wake Adam Malima, Dk. William Mgimwa (Fedha), Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk. Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara).
Dalili za kuwepo kwa mabadiliko ya baraza hilo zilianza kuonekana kabla ya kuanza kwa mkutano wa bunge uliomalizika
jana, baada ya Rais Kikwete kumteua Dk. Asha Rose Migiro kuwa mbunge.
Wakati huo huo, serikali imewapongeza mawaziri wane waliojiuzuru jana kwa hiari yao ili kulinda heshima na imani ya
wananchi kwa serikali yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akihitimisha bunge mjini hapa. Pinda alisema serikali
imesikia uamuzi huo wa mawaziri mawaziri wa kuona ni vyema
wakajiudhuru.
Alisema serikali inawapongeza mawaziri hao kwa kuonyesha ujasiri
wao kwa kutambua dhamana yao na Rais Jakaya Kikwete ameridhia.
Pinda alisema serikali itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya
kamati ya Bunge kuhusiana na Operesheni tokomeza iliyotolewa juzi iliyosababisha mawaziri hao kujiudhuru.
Alisema katika taarifa hiyo ya kamati matatizo mbalimbali yalijitokeza ikiwemo mateso dhidi ya watuhumiwa, matumizi mabaya ya silaha, uchomaji wa nyumba za wananchi na kuua mifugo.

Nape apumua kuwajibishwa mawaziri


NA BASHIR NKOROMO
KATIBU wa NEC ya CCM (Itikadi na Uenezi), Nape Nnauye amesema amepokea kwa faraja hatua ya mawaziri wanne kuenguliwa nyadhifa zao kwa ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete.
"Najisikia vizuri, maana kwa kitendo cha mawaziri hao wanne kuchuliwa hatua naamini kitasaidia wale wengine waliolala nao waamke. Bila shaka sasa hakuna atakayelala na akilala anajua itakula kwake," alisema Nape akijibu swali la mtangazaji wa Kituo cha luninga cha ITV, mjini Dar es Salaam, jana.
Awali, mtangazaji wa luninga hiyo, Emmanuel Buhohela alitaka kupata mawazo ya Nape akiwa kiongozi wa ngazi ya juu wa Chama kuhusu hatua ya Bunge kushinikiza na hatimaye Rais kuwawajibisha mawaziri hao kwa kuridhia kutengua uteuzi zao, juzi.
Mawaziri waliofutiwa uteuzi wao na Rais na nafasi walizotoka zikiwa kwenye mabano ni, Dk. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai (Waziri wa Ulinzi), Mathayo David Mathayo ( Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Khams Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye ndiye pekee pamoja na uteuzi wake kutenguliwa na Rais, lakini alitangaza kujiuzulu akiwa bungeni.
Nape alisema pamoja na mawaziri hao kuwajibika, ipo haja ya kwenda mbali zaidi kwa kutazama mifumo na sheria zilizopo sasa kwa kuwa inaonekana ni miongoni mwa vyanzo vya vikwazo katika utekelezaji wa utawala bora.
"Kwa mfano leo hii, mawaziri wameng'oka, sawa ni jambo jema. Sitetei, lakini inawezekana kabisa kuna mifumo na sheria ambazo zilimkwaza waziri huyu kutimiza wajibu wake. Mfano, alihitaji kumfukuza mtu kazi kwa kuzembea jambo fulani, lakini mamlaka ya kufukuza kazi mtumishi yapo kwa Katibu Mkuu wa Wizara, hapa atafanyaje?" alihoji Nape na kuongeza;
"La msingi hapa ni lazima sasa hatua hizi ziende mpaka chini huko kwa watendaji ili isiwe mawaziri wanawajibishwa tu kwa sababu ya dhamana zao za kusimamia kisiasa, huku watendaji wanazidi kuvuta shuka bila hofu wakati baadhi yao ni sehemu ya matatizo".
Akijibu swali kuhusu ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Sekretarieti ya Chama mikoani, alisema ndiyo kwanza zimeanza na moto zaidi unakuja hasa utakapokaribia uchaguzi mkuu wa 2015.
Nape alisema ziara hizo zimeonyesha matunda makubwa kwa kuwa zimesaidia kupunguza kero nyingi katika maeneo zilikofanyika.
Alitoa mfano wa ziara hiyo ilivyoweza kuondoa msongamano wa malori wilayani Tunduma mkoani Mbeya, akisema wakati Kinana na msafara wake unaingia sehemu hiyo ulikuta msongamano mkubwa kutokana na wafanyakazi wanaohudumia malori  kufanya kazi kwa muda mfupi.
"Baada ya kuiagiza serikali isimamie wafanyakazi wa eneo hilo wafanye kazi kwa saa 24, kwa zamu, siku ya pili yake ya agizo hilo msongamano ulionekana kupungua sana na kuleta nafuu kwa madereva na wafanyabiashara kwa ujumla," alisema Nape.
Akizungumzia wabunge wanaodaiwa kulipwa posho bila kuzifanyia kazi, Nape alisema kurudisha fedha pekee hakutatosha, kwa upande wa CCM ambayo ndiyo yenye wabunge wengi itabidi ichukue hatua zaidi dhidi ya waliohusika bila kumuonea mtu.
Alisema katika uchaguzi ujao CCM itakomba viti vyote vya ubunge na udiwani vililivyoko chini ya vyama vya wapinzani, baada ya wapinzani kujaribiwa na kushindwa kuonyesha matunda yoyote ya kusaidia wananchi na hivyo kutokuwa mbadala wa CCM.

Wahamiaji haramu warejea, wajiita M23

Na Angela Sebastian, Kyerwa
SERIKALI imewataka wahamiaji haramu waliorudi nchini huku wakijiita M23 na ‘kuteka’ Kijiji cha Kibingo, wilayani Kyerwa, huku wakiendelea kutoa vitisho kwa wananchi, kuondoka mara moja.
Wahamiaji hao ambao wamerejea baada ya kutoa hongo kwa baadhi ya viongozi wa vijiji wasiokuwa waadilifu, wamekuwa wakiwasumbua wananchi katika eneo hilo.
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fabiani Massawe, amewataka watu hao kuondoka haraka alipofanya ziara wilayani humo na kumtaka Mkuu wa Wilaya, Benedict Kitenga, kutoa taarifa juu ya maendeleo ya oparesheni kimbunga awamu ya nne katika eneo lake.
ìNimepata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa wahamiaji haramu wamerudi kwa nguvu na wanawatisha kwa kuwaeleza kuwa watawaua, serikali haitavumilia watu hao waendelee kuwatisha wananchi.
“Naagiza Kamati za Ulinzi na Usalama hususan Usalama wa Taifa kufanya uchunguzi na kuweka mtandao ambao utatoa taarifa zitakazowezesha kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahamiaji haramu hao kwa kosa la ujambazi. Kwa kweli hatuwezi kuwaita wahamiaji haramu, bali hawa ni majambazi,îalisema Massawe kwa ukali.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alitoa sh. bilioni 3.6 na kutuma vikosi vya ulinzi na usalama mkoani Kagera ili waondoe wahamiaji haramu, majangili na majambazi wa kutumia silaha.
“Leo akisikia wamerudi tena hii ni aibu. Nawataarifu wahamiaji hao kuwa oparesheni hii ni endelevu kwa hiyo hakuna wa kubaki wala kurudi kama kauli mbiu yetu inavyosema,îalisema mkuu huyo wa mkoa.
Alisema kiongozi yeyote kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa atakayeonekana kuwakingia kifua wahamiaji hao kwa kuchukua fedha na mifugo, atashitakiwa kwa kosa la usaliti wa taifa.
Aliwataka wananchi kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa pindi wanapowaona watu hao katika vyombo husika na pia kupitia simu yake ya mkononi ili waweze kushughulikiwa.
Kwa upande wake, Kitenga alisema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama walipata taarifa wahamiaji haramu wamerudi kwa kasi katika kijiji hicho na kuteka eneo la kijiji hicho huku wakijiita M23 wakiwa na silaha za jadi.
Alizitaja silaha hizo kuwa mikuki, mapanga, visu na marungu ambavyo walivitumia kuwatisha wananchi na watendaji wa maeneo hayo kuwa wakiwasema watawajeruhi.
ìTulienda mpaka kijijini hapo na tulipofika katika eneo walilokuwa wamejimilikisha tulifanikiwa kukuta wahamiaji haramu zaidi 20 kutoka nchi za Uganda na Rwanda waliokuwa katika harakati za kutafuta chakula wakiwa na silaha hizo ila tulifanikiwa kuwakamata wote na kuwarudisha kwao na kuwanyangíanya silaha hizo, “ alisema mkuu huyo wa wilaya.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, George Mikindo, alisema viongozi wa maeneo hayo ndio wanaowalea wahamiaji haramu hao.
“Kwa hiyo inakuwa shida sana kuwajua kwani hawatoi ushirikiano kwa sababu viongozi hao hao wamekuwa wakiwafuata  wahamiaji hao haramu Rwanda na kuwarudisha nchini  ili wawachungie mifugo,” alisema.

Bunge la Katiba laiva .


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameyaalika na kuyakaribisha makundi mbalimbali katika jamii kupendekeza majina ya watu ambao wanaona yanafaa kuteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Rais Kikwete ametoa mwaliko huo kulingana na mamlaka anayopewa katika kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) na aliutangaza rasmi mwaliko huo katika Gazeti la Serikali Na. 443 la Desemba 13, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa juzi mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, mwaliko huo ambao pia utatangazwa katika magazeti ya kawaida, makundi yaliyokaribishwa kutoa mapendekezo yametakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa kila kundi.
Makundi hayo ambayo yametajwa katika sheria ya mabadiliko ya katiba ni taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za dini, vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wafugaji, vyama vinavyowakilisha wavuvi, vyama vya wakulima na makundi mengine yenye malengo yanayofanana.
Taarifa ya Balozi Sefue ilisema katika kuwasilisha mapendekezo ya majina yao, makundi yaliyoalikwa yanalazimika kuonyesha umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu anayependekezwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia.
Katika mwaliko wake, Rais Kikwete ameelekeza kuwa orodha ya majina ya wanaopendekezwa iwasilishwe kwa maandishi ama kwa kupelekwa na mtu kwa mkono ama kwa kutumia huduma ya Posta.
Ilisema orodha hizo ziwasilishwe kupitia anuani zifuatazo Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais, Ikulu, Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, ambapo mwisho wa kupokea orodha ya majina yanayopendekezwa ni Januari 2, mwakani.

Watu 10 washikiliwa mauaji ya Mabina


NA PETER KATULANDA, MWANZA
WATUHUMIWA wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza na Diwani wa Kata ya Kisesa wilayani Magu, Clement Mabina, wameongezeka na kufika 10.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Valentine Mulowola, alisema jana kwamba, watuhumiwa wengine watatu tofauti na saba waliokamatwa awali walikamatwa kwa nyakati tofauti kufuatia upelelezi unaoendelea kufanywa na makachero.
“Hadi sasa tunawashikilia watu 10 kuhusiana na mauaji hayo ya kujichukulia sheria mkononi na ya kikatili. Bado tunaendelea na uchunguzi wa kina, tutawapeni taarifa. Nawaomba wananchi waendelee kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji,” alisema.
Bila kuwataja watuhumiwa hao, alisema watu hao watatu walikamatwa katika maeneo mbalimbali tofauti ambayo hakuyataja.
Mabina aliuawa kikatili na kundi la baadhi ya wakazi wa Kisesa na Kanyama, Desemba 15, mwaka huu, mchana, kufuatia mgogoro wa kugombea eneo la mlima wa Kanyama ambalo alikuwa akilimiliki kwa hati.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu, aliagua kilio msibani huku akisisitiza kuwa hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Dk. Limbu alilia juzi wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya misa ya mazishi ya Mabina, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Chama Cha Msalaba Mwekundu Kisesa na kuongozwa na Paroko wa Parokia ya Bujora, Padre Fabian Mhoja.
“Kuna maneno maneno yanazunguka kwamba Limbu sasa amesema hagombei ubunge, nasema mwaka 2015 sigombei naomba mnielewe hivyo na msiniulize maswali kwa nini,”alisema mbunge huyo.

Bunge lafuta kodi ya simu


Na Theodos Mgomba, Dodoma
BUNGE jana lilipitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa wa mwaka 2013 kwa kufuta kodi na ushuru wa sh. 1,000 kwa kadi za simu kwa kila mwezi.
Pamoja na kufuta kodi hiyo, serikali imepandisha kiwango cha ushuru wa huduma ya mawasiliano kutoka asilimia 14.5 hadi 17 ili kufidia pengo litakalotokana na kufutwa kwa kodi hiyo.
Akiwasilisha muswada huo kwa hati ya dharura, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema muswada huo umelenga kuanza kutoza ushuru kwa huduma zote za mawasiliano ya kielekroniki.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni usambazaji wa mitandao, huduma za kusafirisha taarifa (data), huduma za nukushi na huduma za kusafirisha mawasiliano kwa njia ya waya na zisizotumia za waya.
Alisema kwa upande wa kadi za simu sasa mtumiaji atatozwa kodi kufuatana na matumizi yake.
Muswada huo uliwasilishwa kwa hati ya dharura baada ya Rais Jakaya Kikwete kuweka sahihi urudishwe bungeni kwa ajili ya kufuta kodi ya kadi za simu.
Alisema awali serikali ilitarajia kukusanya sh. bilioni 178 fedha ambazo zilipangwa kutekeleza miradi ya maji na umeme vijijini.
Saada alisema kupandisha kwa ushuru huo wa mawasiliano na kupanua wigo wa kutoza ushuru katika mawasiliano kunatarajia kuipatia serikali mapato ya sh. bilioni 148.
Alisema kampuni za simu zitachangia sh. bilioni 30 ili kukamilisha mapato ya sh. bilioni 178 yaliyolengwa kupatikana wakati wa kukadiria kodi za kadi za simu.
Akizungumzia muswada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, alisema imeridhia marekebisho ya muswada huo na kuishauri serikali katika mwaka ujao wa fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza asilimia 17 iliyoongezwa katika kodi ya mawasiliano hadi  asilimia 12 ili kuendana na viwango vya nchi za Afrika Mashariki.
Akichangia muswada huo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Mwigulu Nchemba, alisema serikali ilikuwa na nia nzuri ya kuweka kodi hiyo kwa kuamini kutakuwepo na mtambo utakaowezesha watumiaji wa simu kutozwa ushuru kwa kadri wanavyotumia.
Aliiomba serikali kuhakikisha inabana matumizi yake ili Watanzania waridhike kwamba kodi zao zinafanya kazi nzuri ikiwemo kuiona miradi inayotekelezwa.

CCM imepata pigo- Mwigulu


NA TUMAINI MSOWOYA, MBARALI
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, ameongoza mamia ya wakazi wa mikoa ya Iringa na Mbeya katika mazishi ya aliyekuwa Katibu wa CCM mkoani Iringa, Emmanuel Mteming’ombe yaliyofanyika kwenye makaburi ya Rujewa Mkoa wa Mbeya.
Akitoa salamu za mwisho katika mazishi hayo, Mwigulu ambaye muda mwingi alikuwa akibubujikwa na machozi, alisema kitu pekee kitakachowaunganisha wanachama wa CCM ni upendo wa kweli, hasa wakati wa furaha, huzuni na misiba.
Nchemba alisema Chama kimepata pigo kwa kuondokewa na kiongozi ambaye alitegemewa katika kuendelea kukijenga.
Alisema upendo wa kweli haubagui, bali unajali utu na kwamba, baada ya msiba huo lazima uonekane kwa familia ya kiongozi huyo akiwemo mkewe na watoto.
“Lazima kuwe na upendo wa dhati miongoni mwetu ili tuendelee kuwa na umoja na mshikamano wa dhati, Mteming’ombe ameondoka wakati CCM inamhitaji na mchango wake katika kuijenga CCM yetu tuuenzi kwa kuipenda familia yake,”alisema Mwigulu ambaye muda mwingi alibubujikwa na machozi.
Aliwataka viongozi wa serikali na Chama hicho kujenga tabia ya kufanya kazi karibu na watu na sio kujibagua kwa kujiona bora kuliko jamii waliyoamua kuitumikia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema mkoa huo umesikitishwa kuondokewa na kada waliyemuamini ambaye aliweza kufanya kazi kwa uadilifu katika mikoa mingine na kwamba, aliendelea kuwa mshauri wa karibu kwa CCM katika mkoa.
“Alikuwa Iringa lakini alikuwa mshauri wetu wa karibu. Tumeumia sana kumpoteza kada wetu ambaye tulimhitaji,”alisema Kandoro.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, alisema mkoa wa Iringa umepata pengo ambalo halitaweza kuzibika kwa madai kuwa kifo cha Mteming’ombe kimetokea wakati ambao hakuna aliyetarajia.
“Niliwahi kufanya kazi na Mteming’ombe nikiwa mkoani Ruvuma na baadaye Iringa, imeniumiza sana lakini sina ujanja kwani namuachia Mungu ambaye ndiye aliyeruhusu haya yatokee,”alisema Dk. Christine.
Mkuu huyo alisema, alibahatika kumjulia hali wakati alipougua, lakini haikuonyesha kama hali yake ingeweza kusababisha mauti kama ilivyotokea.
Akisoma wasifu wa marehemu huyo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema kiongozi huyo alifariki siku moja baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa akisumbuliwa na homa ya matumbo pamoja na athma.
Hata hivyo alisema, wiki mbili kabla ya kufariki alianza kuumwa na kwamba alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani hadi siku alipozidiwa.
Kabla ya kuwa Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Mteming’ombe alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Mbeya, Diwani wa Kata ya Rujewa Wilayani Mbarali, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Rujewa na Katibu wa CCM wa wilaya za Kyela, Ileje na Mbozi.
Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Katibu wa CCM mkoani Mbeya, Ruvuma na hatimaye Iringa ambako mauti yamemkuta. Mteming’ombe ameacha watoto watatu na mjane.

Walipa kodi 200,000 kutumia EFD


NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imelenga kuingiza walipa kodi 200,000 kati ya 1,500,000 waliopo ili waweze kutumia mashine za kieletroniki za kutoa risiti (EFD).
Wafanyabiashara wadogo na wanaoendesha bishara zisizo rasmi kama vile wamachinga na wanaotembeza bidhaa barabarani na mama lishe hawatahusika na utaratibu huo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa akiahirisha mkutano wa Bunge, mjini hapa.
Pinda alisema walengwa wa utaratibu huo ni wafanyabishara wakubwa wenye biashara zenye mtaji wa kati ya sh. milioni 14 na sh milioni 40.
Alisema ingawa kumekuwa na malalamiko juu ya bei kubwa ya mashine hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kujadiliana na wasambazaji wa mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei.
Waziri Mkuu alisema kwa kutumia mashine hizo mfanyabishara anaweza kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda ofisi ya TRA na mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo.
Alisema mamlaka nyingine ni pamoja na EWURA, SUMATRA na Taasisi ya Taifa ya Takwimu na Benki Kuu (BoT).
Pinda alisema mashine hizo zinatumia lugha za Kiswahili na Kiingereza ambazo zinatumiwa na Watanzania wengi.
Alisema ili kuhakikisha ubora wa mashine hizo, watengezaji wametoa muda wa miaka mitatu wa kutengeneza bure mashine itakayoharibika katika kipindi hicho bila kukusudia.
Kwa mujibu wa mkataba ulioingiwa kati ya wasambazaji na TRA, wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengezaji wao wenyewe.
“Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizo katika kuongeza mapato ya ndani, serikali inaendelea kushughulikia malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara juu ya matumizi ya mashine hizo, “ alisema.
Bunge limeahirishwa hadi Mei 6, mwakani litakapokutana kwa ajili ya mkutano wa bajeti. Hata hivyo wabunge ambao ni wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba watakutana litakapoitishwa bunge hilo.

Thursday 19 December 2013

Dawa matatizo ya walimu yachemka



Na Theodos Mgomba, Dodoma
SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuanzisha chombo maalumu kitakachoshughulika na matatizo ya walimu, badala ya kuwa chini ya wizara zaidi ya moja.
Pia imesema malimbikizo ya madai ya walimu yamepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba, itaendelea kulipa ambayo yanadaiwa kwa sasa ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hayo bungeni jana, alipojibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa  wabunge, ambapo alisema walimu ni kada muhimu katika utumishi wa umma.
Awali, Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki -CCM), alitaka kufahamu ni kwa nini serikali isiondoe malalamiko mengi ya walimu kwa kuanzisha chombo kimoja cha kushughulikia matatizo yao, badala ya sasa kuwa na vyombo zaidi ya viwili.
Waziri Mkuu Pinda alisema walimu ni kundi kubwa la watumishi nchini, na limekuwa na matatizo mbalimbali.
Alisema licha ya wazo la kuanzisha chombo maalumu cha kushughulikia walimu, ni lazima serikali iangalie changamoto mbalimbali kabla ya kuanzisha chombo hicho.
Waziri mkuu alisema kwa sasa walimu ni zaidi ya asilimia 50 ya watumishi wote wa serikali, hivyo kundi hilo ni kubwa na lazima litakuwa na matatizo ya hapa na pale.
“Jambo hilo la kuwa na chombo kimoja kwa ajili ya walimu tumelifanyia kazi lakini nalo lina changamoto zake na tuangalie kwa nini walimu? ila tutaendelea kulifanyia kazi na endapo tutaona kuna haja ya kufanya hivyo tutafanya,’’ alisema.
Kuhusu malimbikizo ya madeni ya walimu, alisema yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa, lakini kuna baadhi hawajalipwa jambo linalotokana na serikali kutaka kujiridhisha kabla ya kulipa madeni hayo.
Alisema sehemu kubwa ya madeni hayo yameshathibitishwa na yapo njiani kulipwa.
Akizungumzia upungufu wa wahadhiri katika vyuo vikuu, Waziri Mkuu Pinda alisema unatokana na baadhi yao kustaafu.
Pinda alisema umri wa kustaafu kwa wahadhiri umebaki miaka 60 lakini wanaweza kuajiriwa kwa mkataba wa miaka mitano zaidi.
Kwa mujibu wa waziri mkuu, kada ambayo imeongezwa umri wa kustaafu ni ya mahakama, ambayo majaji wa Mahakama ya Rufani umri wao wa kustaafu ni miaka 65.
Hata hivyo, alisema Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kinajitahidi kusomesha na kutoa wahadhiri.
Alikuwa akijibu swali la Murtaza Magungu (Kilwa Kaskazini -CCM), aliyetaka kujua serikali ina mpango gani katika kuondoa upungufu wa wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu.

JK kuchunguzwa afya


Na mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameondoka nchini juzi jioni kwenda Marekani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ikulu ilisema uchunguzi huo ni utaratibu wa kawaida.
Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za uchunguzi wa afya na umbali wa safari hadi Marekani na kurudi nchini, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea Alhamisi ijayo.

Katibu wa CCM Iringa afariki dunia



NA MOI DODO, UoI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata pigo baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Emmanuel Mteming’ombe, kufariki dunia usiku wa kumkia jana.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema Mteming’ombe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa pumu uliosababisha kifo chake.
“Ni ugonjwa aliokuwa nao kwa muda mrefu tangu utotoni, lakini haukuwahi kumsumbua kwa muda mrefu,” alisema Jesca.
Alisema wanachama wa CCM wameupokea msiba huo kwa mshituko mkubwa kutokana na kumpoteza kiongozi mahiri na makini na kwamba, alikitumikia Chama hadi dakika ya mwisho ya uhai wake.
“Ni pigo kwa Chama mkoa na taifa, tumempoteza mpiganaji wa kweli na aliyekuwa akijituma kipindi chote kukiimarisha Chama. Ila yote ni mipango ya Mungu kwahiyo hatuna budi kukubali,” alisema.
Alisema mwili wa marehemu utasafirishwa leo kwenda kijijini kwao Rujewa wilayani Mbarali, ambapo mazishi yake yatafanyika kesho.
“Kila kitu kimekamilika na baada ya Misa ya kumuombea itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Kihesa tutausafirisha mwili mpaka Rujewa tayari kwa maziko kesho,” alisema Jesca.
Baba mzazi wa marehemu, Mzee Yustin Mteming’ombe, alisema kifo cha mwanae kimeacha pengo kubwa kwake na kwa familia.
“Kifo hiki kimenipa wakati mgumu mno. Alikuwa tegemeo langu, licha ya kuwa mtoto, lakini alikuwa rafiki yangu,” alisema Mteming’ombe.
Marehemu ameacha mjane, watoto wanne na wajukuu watatu.
Kutokana na msiba huo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Tumaini Msowoya, ameahirisha ziara yake iliyokuwa imepangwa kuanza jana.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuboresha na kuimarisha uhai wa Chama na Jumuia ya Vijana.


Wednesday 18 December 2013

Abiria 213 wanusurika kifo


NA LILIAN JOEL, Arusha
NDEGE kubwa ya Shirika la Ethiopia Air Line, aina ya Boing 767 imetua kwa dharura katika uwanja mdogo wa Arusha.
Hatua hiyo inatokana na kushindwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kutokana na ndege nyingine ya Shirika la TFC kupata pancha kwenye njia ya kuruka na kutua ndege katika uwanja huo.
Ndege hiyo Boing 767 yenye namba ET- AQW iliyokuwa ikitoka Ethiopia ilitakiwa kutua KIA, lakini kutokana na kuwapo iliyopata hitilafu, rubani alitakiwa kwenda kutua Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, nchini Kenya.
Hata hivyo, imeelezwa kutokana na ndege hiyo kutokuwa na mafuta ya kutosha, rubani alilazimika kutua uwanja mdogo wa Arusha.
Ndege hiyo ilitua saa 6.52 mchana lakini kutokana na udogo wa uwanja huo, ililazimika kutua kwenye tope.
Wakati ndege hiyo ikitua, kulizuka taharuki miongoni mwa wafanyakazi wa uwanja huo na abiria waliokuwa wakisubiri kusafiri kwa ndege za kampuni nyingine.
Baada ya kutua salama, abiria zaidi ya 213 waliokuwa ndani ya ndege hiyo na wafanyakazi 23 walitakiwa kushuka kwa kutumia ngazi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zilizofungwa kwenye gari la zimamoto lakini walikataa.
Kutokana na hilo, walilazimika kukaa ndani kwa zaidi ya saa tano wakisubiri ngazi kubwa kutoka KIA. Milango ya dharura ililazimika kufunguliwa ili abiria wapate hewa.
Abiria aliyeamua kushuka kwa kutumia mlango wa dharura akiwa nje aliwasha sigara lakini aliombwa na mhudumu wa ndege hiyo kuizima na kurudi ndani.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliyefika eneo la tukio saa moja baada ya ndege kutua, alisema hilo ni changamoto kubwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuangilia jinsi ya kuboresha uwanja huo.
Alisema rubani aliuona uwanja huo alipokuwa akiendelea kuwasiliana na waongoza ndege wa Jomo Kenyatta.
UWANJA WAFUNGWA
Kutokana na ukubwa wa ndege hiyo,  sehemu ya nyuma ilikuwa kwenye njia ya kuruka na kutua ndege, hivyo uwanja ulifungwa kwa saa kadha, huku abiria waliokuwa uwanjani wakishindwa kuendelea na safari.
Raia wa Uingereza Joachim Leon, alisema kwa zaidi ya saa tano walikwama kwenda Serengeti kutokana na njia kuzibwa.
MASHUHUDA WALONGA
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo jijini Arusha na viunga vyake walisema haijawahi kutokea kwa ndege kubwa kama hiyo kuruka chini chini, huku kukiwa na mngurumo mkubwa uliozua taharuki.
“Nilikuwa dukani nikaona ndege kubwa ikipita chini sana tofauti na tulivyozoea kuona ndege nyingine. Pia ilikuwa inayumbayumba hali iliyotufanya tupige kelele kwa kuhofia kuangukiwa na ndege hiyo,” alisema mwanamke aliyejitambulisha kuwa Mama Best.
Umati ulijitokeza nje ya uzio wa uwanja kuiangalia ndege hiyo.
Mkazi wa Arusha, Annet Josia, alisema amekuwa nje ya uwanja huo kwa zaidi ya saa tano akisubiri kumpokea kaka yake ambaye ni abiria wa ndege hiyo.
Maofisa wa Idara ya Uhamiaji walifika uwanjani hapo saa tisa alasiri kwa ajili ya utaratibu wa kikazi.
ABIRIA WAKUBALI KUSHUKA
Baada ya kusubiri kwa takriban saa tatu bila ngazi waliyokuwa wanahitaji kuletwa kutoka KIA, abiria hao waliwalazimisha wahudumu wa ndege hiyo kuwaruhusu washuke,  ambapo walitumia mlango wa dharura.
Baadhi walishuka wakiserereke kupitia kwenye mabawa ya ndege hiyo na kupokewa na wahudumu wa uwanja wa Arusha.
Akizungumza baada ya kushuka katika ndege hiyo Glory Maeda, alisema anamshukuru Mungu kwa kushuka salama, licha ya taharuki kubwa baada ndege kushindwa kutua KIA na kutokuwa na mafuta ya kufika Jomo Kenyatta.

Sakata la posho Kombora la Mwigulu lamchakaza Mbowe


“Rejea mazungumzo bwana Kabunju kuhusu Joyce Mukya, ambaye yupo safarini nitashukuru kama utambadilishia booking aweze kurudi, aondoke New York Desemba Mosi na aje Dubai, by Mbowe Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni
Na Theodos Mgomba, Dodoma
MBUNGE wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM), amemlipua Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwa kuhusika kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwigulu alieleza bungeni jana kuwa, Mbowe (CHADEMA) alimrudisha mbunge wake, Joyce Mukya, aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi na kumtaka kukutana naye Dubai.
Kombora hilo la Mwigulu limetolewa wakati wabunge wakituhumiwa kuchukua posho za safari bila kwenda kwenye maeneo wanayotakiwa, badala yake kuzitumia kwa matanuzi binafsi.
Bunge limewataka wabunge wote waliochukua posho za safari bila kusafiri kurejesha mara moja fedha hizo, ambazo ni mali ya walalahoi.
Hali ilianza kuwa tete baada ya Mwigulu kusimama na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti kuhusu baadhi ya wabunge, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kutuhumiwa kuchukua posho na kutokwenda safari.
Mwigulu alisema Mbowe alimrejesha Joyce kutoka nchini Marekani na kwenda kwa muda Dubai.
“Mheshimiwa Mwenyekiti baadhi ya magazeti leo (jana) yameandika kuwepo baadhi ya wabunge waliolipwa fedha za safari, lakini hawakwenda. Jambo hili linachafua taswira ya Bunge zima.
“Wengine tuna maadili ya uongozi, magazeti mengine yameandika kuna kigogo mmoja amemzuia hawara yake kusafiri na alikuwa amelipwa kila kitu na hakusafiri, hili ni jambo binafsi.
“Na nina ujumbe nimeupata Kiongozi wa Kambi ya Upinzani humu bungeni akimwandikia mtumishi wa Bunge kuwa:
‘Rejea mazungumzo bwana Kabunju kuhusu Joyce Mukya ambaye yupo safarini nitashukuru kama utambadilishia booking yake aweze kurudi, aondoke New York Desemba Mosi na aje Dubai, lakini baadaye ataunganisha na kurejea  Dar es Salaam by Mbowe Kiongozi wa kambi ya Upinzani bungeni nakala kwa Joyce Mushi’.
“Haya ni mambo binafsi, naomba kujua ofisi yako inasema nini kwa mbunge aliyetumwa kuwakilisha taifa halafu mtu binafsi kwa kutumia nafasi yake anamrudisha, mtu ambaye ametumia fedha za serikali anamuita Dubai kwa kazi yake binafsi, taifa langu lina bahati mbaya kiasi gani,” alisema.
Aliongeza: “Naomba mwongozo wako juu ya hatua stahili ya kupambanua wabunge wa namna hii na hatua stahili kwa mbunge kuingilia kazi za kiti na hatua stahili kwa watumishi wa bunge wanapoingiliwa.’’
Kauli ya Mwigulu iliamsha miongozo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge, ambapo David Silinde (Mbozi Magharibi -CHADEMA), alisimama na kueleza kuwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, aliwahi kuchukua fedha, lakini hakwenda safari na Kamati yake ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo wako, suala la kuchukua fedha na kutokwenda safari lisiangaliwe kwa upande wa upinzani tu, hata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya naye aliwahi kuchukua fedha na hakwenda safari na kamati yake.
“Cha kufanya Mwenyekiti ni kwa namna gani Bunge lako litachukua hatua na iwapo wabunge wengi tu ambao ni wajumbe hapa wanawajua wanaochukua fedha, lakini hawaendi,” alisema.
Katika harakati za wabunge wa CHADEMA kumuokoa Mbowe, Mariam Msabaha (Viti Maalumu), alisimama kuomba mwongozo na kusema kuna baadhi ya watu wameandikwa katika magazeti kuwa wameiba vidani.
“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi ni mtu mwenye nidhamu na huwa sisimami mara kwa mara, lakini leo naomba niseme kuna watu humu wameandikwa kuwa wameiba vidani mbona hawasemwi, mambo ya mapenzi kila mtu na mpenzi wake, kuna mambo mengi yanafanyika humu bungeni mbona hayasemwi,’’ alisema.
Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini -CHADEMA), alisimama kuomba mwongozo akisema ni jambo la aibu kwa Bunge kuingia katika matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Alisema tayari Kamati ya Hesabu za Serikali imeshamuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua safari zote za wabunge na kutoa taarifa kwa Spika, na kama itaonekana inafaa taarifa hiyo iwasilishwe bungeni kujadiliwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ni jambo la aibu kwa Bunge kuingia katika mgogoro namna hii wa matumizi mabaya ya fedha na hii inaonyesha taswira mbaya kwa wananchi.
“Tayari kamati imemuomba CAG kufanya uchunguzi wa safari zote na kutoa taarifa. Kamati itapeleka kwa Spika na kama ataona inafaa italetwa bungeni ili mambo hayo tuweze kuyamaliza, ni aibu,’’ alisema.
Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alisema wabunge wote waliochukua fedha za safari na hawakwenda ni lazima wazirejeshe.
Zungu alisema tayari malalamiko hayo yamefikishwa mezani kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na yanaendelea kushughulikiwa.

Vitalu vya gesi vyatikisa Bunge


Na waandishi wetu
UTOAJI vitalu vya mafuta na gesi nchini umelitikisa Bunge, serikali ikitakiwa kuvitoa kwa kampuni zenye uwezo, ambazo zitakuwa na tija kwa uchumi wa taifa.
Wabunge wameonya vitalu hivyo visitolewe kwa kampuni zisizo na uwezo kwa kigezo cha uzawa, kwani kampuni nyingi za madini zinamilikiwa na Watanzania, lakini hazina mchango au tija kwa maendeleo ya taifa.
Pia wameitaka serikali kuhakikisha inawadhibiti watu wanaopewa vitalu, kwani wapo ambao hugeuka kuwa madalali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, akiwasilisha taarifa bungeni jana, alisema ni lazima mchango wa kampuni zitakazopewa vitalu uonekane na ulete tija kwa Watanzania.
Alisema kampuni za ndani zikiwemo zinazomilikiwa na wazawa kwa asilimia 50 kwa mujibu wa sheria na zilizoingia ubia na kampuni za nje, zipewe upendeleo.
Mwambalaswa alionya kuwa, Bunge lisingependa serikali irudie makosa iliyoyafanya kwenye sekta ya madini kwa kumilikisha vitalu kwa kampuni za watu binafsi, ambao hawataviendeleza.
“Kitendo cha kuwamilikisha watu au kampuni eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 3.886 ambazo ni sawa na asilimia 0.4 ya eneo lote la nchini bila kulifanyia kazi si jambo la busara.
“Mtu anamiliki eneo ambalo ukubwa wake ni mara nne ya mkoa wa Dar es Salaam bila kulifanyia kazi, hili halikubaliki kabisa. Tunataka tuone tija katika hili la vitalu na si ubabaishaji,’’ alisema.
Alisema utaratibu wa wazawa kupata vitalu vya gesi upo wazi chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wazawa hawajazuiwa na hawabaguliwi ilimradi utaratibu wa TPDC ufuatwe.
Mwenyekiti huyo alisema ni vyema wazawa wakaelewa kuwa, uwekezaji katika sekta ya gesi unahitaji fedha nyingi, na wazawa wenye uwezo wanaombwa kujitokeza katika kuwekeza.
“Kamati inawaomba wazawa wenye uwezo kujitokeza na kuacha kulalamika, lakini ikumbukwe kuwa TPDC ni shirika la serikali na umiliki wake ni asilimia 65,’’ alisema.
Alisema ni vyema serikali ikalichukulia suala la kuwa na kampuni ya mafuta ya taifa kuwa la kufa au kupona.
Kuhusu mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, lenye urefu wa kilomita 542, alisema
lina uwezo wa kusafirisha gesi futi za ujazo milioni 784 kwa siku na hadi sasa vipande vya mabomba vyenye urefu wa kilomita 161 vimeunganishwa.
Mwambalaswa alisema ni vyema serikali ikaharakisha utaratibu wa utoaji vibali vya ajira za vijana wa Kitanzania ili waweze kupata uzoefu wakati bomba likikamilika.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa Nkasi Kaskazini Ally Keissy (CCM), alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa kutumia gesi asili.
“TPDC ishughulikie masuala yote ya gesi. Gesi inayopatikana popote nchini ni ya nchi nzima na hakuna gesi ya mtu binafsi.
“Nani akubali tukupe kisima wewe na familia yako, gesi ya mtu binafsi anayo tumboni mwake, hatuwezi kumpa mtu na familia yake akamiliki gesi,” alisema.

MUHAS inafadhiliwa na serikali -Waziri


CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ni miongoni mwa vyuo vikuu vitano vya umma vinavyofadhiliwa na serikali.
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema hayo jana alipojibu swali la Deogratius Ntukamazina (Ngara -CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itakipa chuo hicho kipaumbele.
Saada alisema serikali imekuwa ikikifadhili chuo hicho kwa kugharamia wataalamu wake.
Alisema mwaka 2013/2014  wataalamu 295 walipata mafunzo, kati yao 195 waliendelezwa kwa kiwango cha Shahada za Uzamili.
Kwa mujibu wa Saada, wengine 100 waliendelezwa katika ngazi za Shahada ya Uzamivu.
Naibu waziri alisema MUHAS pia ni miongoni mwa vyuo vikuu sita vilivyofaidika na ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknolojia katika kugharamia mafunzo ya wataalamu 184.
Wataalamu hao walipata mafunzo katika ngazi za Shahada ya Uzamili na 84 katika ngazi za Shahada ya Uzamivu.
Alisema serikali pia imekuwa ikitoa udhamini kwa wanafunzi wa kozi za udaktari walioko katika vyuo binafsi.
Licha ya juhudi hizo, alisema serikali ilikwisharidhia mpango wa ujenzi wa Kampasi ya Mlonganzila, Dar es Salaam kwa ajili ya MUHAS.

Ulaji usiofaa hatari kwa afya


ULAJI usiofaa, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi husababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Magonjwa hayo ni ya moyo na mishipa ya damu, saratani, kisukari, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kuoza meno na magonjwa ya fizi.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema hayo bungeni jana alipojibu swali la Dk. Maua Daftari, aliyetaka kujua athari za ulaji pipi na ushari wa kitaalamu kwa Bunge ili kutafuta kitu kingine mbadala wa pipi wanazotoa kwa wabunge.
Dk. Seif alisema ulaji pipi na vyakula au vinywaji vyenye sukari ni kiashiria hatarishi cha ulaji usiofaa na husababisha madhara mwilini.
Alisema mgonjwa wa kisukari anapokula pipi anaongeza sukari zaidi mwilini, ambapo tayari mwili unashindwa kutumia sukari iliyopo.
Naibu waziri alisema mtu wa aina hiyo anaongeza uwezekano wa kupata matatizo yatokanayo na sukari kama vile figo kushindwa kufanya kazi, magonjwa ya moyo na mishipa ya fahamu na macho.
Dk. Seif alisema kwa kuwa ulaji pipi unaleta athari kwa meno, ni vyema watumiaji wakapiga mswaki kwa kutumia dawa za meno zenye ‘floraidi’ baada ya kutumia vyakula vyenye sukari.

Sheria ya mitandao kuanza rasmi Machi


NA MOHAMMED ISSA
SERIKALI imesema sheria ya kudhibiti uhalifu wa mitandao inatarajia kuanza kutumika Machi, mwakani.
Imesema sheria hiyo itadhibiti uhalifu wa mitandao ambao umekithiri nchini.
Pia, imesema inakamilisha ujenzi wa mtambo wa kudhibiti mawasiliano ya nje na ndani ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu, alisema tatizo la uhalifu wa mitandao ni kubwa.
Alisema bila kudhibitiwa, linaweza kusababisha athari kwa taifa na jamii.
Alisema sheria hiyo itapunguza na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao mbalimbali.
Profesa Mangu, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipokuwa akifungua kikao cha wadau cha kujadili Rasimu ya Sheria ya Matumizi Salama ya Mtandao.
Alisema kutokana na kuwepo tishio la uhalifu kwenye mitandao, serikali imeamua kutunga sheria ya kudhibiti uhalifu huo na kwamba, itamtaka aliyekumbwa na tatizo hilo kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria.
“Hii sheria itatoa adhabu kwa yeyote atakayebainika kuhusika na uhalifu wa kwenye mitandao, ambao hivi sasa umekithiri,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa wizara hiyo, Dk. Ally Simba, alisema sheria hiyo itahusu pia uhalifu wa kumbukumbu, usalama wa mtandao na biashara ya mtandao.
Alisema sheria itamtaka aliyekumbwa na tatizo kutoa taarifa na asipotoa atawajibika.
Dk. Simba, alisema mkutano huo utasaidia ukamilishwaji wa sheria ya usalama wa mitandao.

Walinzi wa mgodi wadaiwa kuua raia


NA MARCO KANANI, GEITA
WALINZI wa mgodi wa dhahabu wa GGM mkoani Geita, wanadaiwa kumpiga hadi kufa Emmanuel Mwita, ambaye aliingia kwenye eneo la mgodi kuokota mawe ya dhahabu.
Habari za kuamini zilisema Mwita (32), aliingia kwenye eneo hilo kuokota mawe yaliyokuwa yamemwagwa katika vifusi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi saa 7:00 usiku, ambapo walinzi hao walimkamata na kuanza kumshambulia hadi kumsababishia kifo.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa vijana waliokwenda kuokota mawe na Mwita, alisema wakiwa eneo la tukio, walikurupushwa na walinzi.
Alisema baadhi walifanikiwa kutoroka, lakini Mwita alikamatwa na kuanza kupigwa sehemu mbalimbali za mwili.
“Tulisikia mwenzetu akilia na kuomba msaada na kuwataka walinzi hao wasiendelee kumshambulia, lakini hawakufanya hivyo na badala yake walizidi kumshambulia,’’ alisema.
Alisema siku iliyoafuata walienda Kituo cha Polisi Geita ili kufahamu kama mwenzao alifikishwa kituoni hapo, lakini walielezwa kuwa hakufikishwa.
“Tulikwenda hospitali zote ili kupata taarifa, lakini hakuwepo ndipo baadaye tukaelezwa kuwa kuna mgonjwa ameletwa na kutelekezwa na askari wa GGM ana hali mbaya. Baadaye tukaelezwa kuwa amefariki dunia,’’ alisema.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema mwili wa Mwita ulikuwa na jeraha kubwa kichwani na alikuwa ametokwa na damu nyingi.
Pia, alisema baadhi ya viungo vyake ikiwemo mikono ilikuwwa imevunjika.
Hili ni tukio la pili kutokea ndani ya miezi miwili, ambapo Oktoba 17, mwaka huu, walinzi hao wa mgodi walidaiwa kumuua Zakaria Thobias (35) kisha kumwekea jiwe kubwa kifuani kwa lengo la kuficha ushahidi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita Amina Baturumili, alisema hajapata taarifa za tukio hilo na kuahidi kulifuatilia kwa karibu.