Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Monday 29 July 2013

Serikali yadhibiti ‘mchwa’ Utumishi


NA KHADIJA MUSSA
MFUMO mpya wa taarifa na ulipaji mishahara kwa watumishi wa umma, umewezesha kukatwa mirija ya ulaji kwa baadhi ya watendaji waliokuwa wakitafuna mabilioni ya shilingi kila mwezi.
Kuanzishwa kwa mfumo huo kumeifanya serikali kudhibiti tatizo la mishahara hewa kwa watumishi.
Awali, watumishi waliofariki dunia waliendelea kulipwa mishahara na kuchukua mikopo, jambo lililokuwa likifanywa na watendaji wasio waadilifu.
Mfumo huo pia umezima safari za maofisa waliokuwa wakisafi kutoka mikoani kwenda Dar es Salaam kuwasilisha taarifa za watumishi, ambao walikuwa wakilipwa posho, hivyo kuiongezea mzigo serikali.
Tangu kuanza kutumika kwa mfumo shirikishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara katika utumishi wa umma (HCMIS),
serikali inaokoa sh. bilioni 1.5 kila mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Florence Temba, alisema mfumo huo pia umepunguza tatizo la malimbikizo ya mishahara kwa watumishi.
Temba alisema umesaidia kurahisisha kuingizwa kwa taarifa za watumishi wapya kwa ajili ya utaratibu wa malipo katika kipindi cha muda mfupi, tofauti na ilivyokuwa awali.
Alisema mfumo huo umesaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu na mishahara katika utumishi wa umma.
“Kabla ya mfumo huu kuwepo, taarifa nyingi za watumishi zilipotea na kuleta usumbufu kwa wengi kufuatilia, ilichukua miezi sita hadi 12 kuchelewesha kuingiza watumishi wapya katika orodha ya malipo. Kwa kutumia HCMIS kazi hufanyika kwa dakika 30,” alisema.
Temba alisema mfumo huo pia umepunguza tatizo la malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma linalosababishwa na kuchelewesha mishahara ya watumishi wapya au wanaopandishwa vyeo.
Alisema ukokotoaji wa malimbikizo ya mishahara ulianza Mei hadi Novemba, mwaka jana,  ambapo malimbikizo ya sh. bilioni 7.9 ya watumishi 15,677 yalifanyiwa kazi.
Kupitia mfumo huo, alisema umerahisisha malipo ya mishahara na stahili kwa watumishi wa umma na kwa wakati, na umewezesha kuondoa watumishi takriban 34,645 kwenye orodha ya malipo ya mishahara kutokana na sababu mbalimbali tangu mwaka 2010 hadi Juni 30, mwaka huu.
Temba alisema wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za serikali zinazopata ruzuku kwa asilimia 100 kutoka HAZINA zinapaswa kutumia mfumo huo katika kusimamia rasilimali watu na mishahara.

Waliotaka kuiibia serikali waumbuka


NA SAMSON CHACHA, TARIME
MAJINA 281 kati ya 1,102 ya wakazi wanaotakiwa kulipwa fidia baada ya nguzo za umeme kupita katika maeneo yao, yamebainika kuwa hewa.
Wakazi hao ni wa kutoka vijiji vya Mogabiri na Itiryo, vilivyoko wilayani Tarime, mkoani Mara.
Imeelezwa pia kati ya majina hayo, 132 ya watu kutoka maeneo mengine yaliingizwa katika orodha ya walipwa fidia kwa lengo la kuihujumu serikali.
Kati ya hayo majina 132 yalikuwa na fomu hewa ambayo yaliingizwa na baadhi ya watu waliokuwa wakitaka kuiibia serikali hivyo hajalipwa fedha kutokana na udanganyifu huo.
Ufisadi huo uliibuliwa na wakazi 200 kutoka katika vijiji 11 ambavyo mradi huo wa umeme unapita.
Walifanya kikao cha dharura na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amos Sagara na Mkurugenzi Mtendaji, Athuman Akalama juzi.
Awali, Halmashauri iliunda Tume ya kuchunguza tatizo hilo, ambapo ilikuja na majibu kama yanayodaiwa na wakazi wa vijiji hivyo, baada ya kufanya uhakiki wa majina na kubaini mengi ni hewa.
“Serikali Kuu ilituletea sh.bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wale waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha nguzo za umeme kwenda katika vijiji vyenu 11, vikiwemo vya Mogabiri, Nyamwigura, Rosana, Kemakorere, Nyarero, Nyamwaga, Kisangura, Muriba A na Mriba B, Bungurere na Itiryo,” alisema Mkurugenzi mtendaji Akalama.
Hata hivyo, alidai kuwa baada majina yaliyoorodheshwa awali yalikuwa 1,102.
Alisema kabla kazi ya kuanza kulipa fidia, walipeleka majina katika ofisi za vijiji hivyo 11, ambapo yalubandikwa kwenye mbao za matangazo.
Akarama, alisema hatua hiyo iliibua malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali kuwa majina yao hayapo.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya kupokea malalamiko, walikaa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kuunda tume iliyofanya kazi ya  kuhakiki majina kabla ya kuanza kulipa fidia hiyo.
Alisema tume hiyo iliwashirikisha maofisa usalama wa taifa wilaya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na  wa idara ya ardhi.
“Ndipo ilibainika kuwepo kwa majina 281 hewa, majina 132 yalikuwa yana fomu za majina hewa na majina  halali yalikuwa 430,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Sagara, alisema serikali hailipi fedha bila kuhakiki na kujiridhisha kwa wanaodai ili haki itendeke kwa pande zote mbili.
Alisema baada ya uhakiki huo, wataanza kulipa Agosti 22, mwaka huu. Hivyo, alitoa wito kwa wote ambao wanastahili kufika bila kukosa.

Ulinzi kuimarishwa sikukuu ya Eid Elftri


PETER NKANDUZO, DACICO
POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imewahakikishia ulinzi wakazi wote wakati wa kipindi cha sikukuu ya Eid Elftri, ambapo askari zaidi ya 120 wameongezwa.
Kamanda wa Kanda hiyo Suleiman Kova, jana alisema kuwa watu wasiwe na wasiwasi katika kipindi cha  kuelekea sikukuu kwani wameshanza kuimarisha ulinzi.
“Waambieni waende wakanunue bidhaa zao bila kubughudhiwa na mtu yeyote kwakuwa tumejipanga vyema,” alisema Kova.
Kova alisema wataendelea kufanya misako na doria kwa muda wote ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahalifu sugu.
Aidha, aliwataka wenye maduka kuhakikisha wanafunga taa za kutosha, kamera za CCTV na kuweka walinzi waaminifu ili kuhakikisha usalama wa maeneo yao ya kufanyia biashara.
Hata hivyo, Kamnada huyo, alisema wataendelea kushirikiana na jamii ili kuzuia wahalifu wakati wa sikukuu inayotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.
Alitoa wito kwa wakazi wa jijini humo kujiepusha na vitendo vya uvunjaji wa amani na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha kuwa na hasira kali.

Mchungaji awashukia wavaa vimini kanisani


Na Frank Kibiki, Iringa
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Usharika wa Iringa mjini, Huruma Bimbiga, amepiga marufuku mavazi ya aibu ambayo yanaonyesha sehemu za miili yakiwemo mabega kwa maharusi, wasimamizi na wapambe wao kanisani hapo.
Akizungumza na Uhuru, Mchungaji Bimbiga alisema kufuatia baadhi ya maharusi kuvaa mavazi yasiyo ya kimaadili, wameamua kuanzisha somo la kuwaelimisha maharusi juu ya mavazi yafaayo kuvaliwa kanisani.
Mchungaji Bimbiga alisema elimu hiyo huitoa katika mafundisho ya ndoa.
Alisema lengo ni kuwataka watambue kuwa siku ya harusi wakivaa vibaya, wakikataliwa kuingia kanisani, wasione kama wananyanyaswa na watumishi wa Kanisa.
Alisema kufuatia hali hiyo, wamejiwekea utaratibu wa kuwavalisha kanga au kuwakatalia kuingia kanisani wale wanaovaa hovyo.
“Ni aibu na ni kinyume na maadili ya kanisa kwa mabinti zetu kuvaa nguo zinazoonyesha miili yao.
“Japo wao wanadhani ni fasheni, lakini kwetu hatupo tayari kuongoza Ibada ya ndoa wakati mavazi yanayovaliwa hayatubariki,” alisema Bimbiga.
Alisema, wakati wa ibada za kawaida wasichana wengi huvaa mavazi ya heshima, tatizo kubwa huwa wakati wa ibada za ndoa. Wengi wao huvaa magauni yanayoonyesha miili yao.
Alitoa wito kwa wazazi kuwaelimisha mabinti namna ya kuvaa mavazi ya heshima.
Alisema hiyo pia ni moja ya kazi ya kuwajengea maadili ndani ya jamii.
Mmoja wa wazee wa kanisa hilo, Peter Sanga, alisema miongozi mwa kazi zinazopaswa kufanywa na viongozi wa Kanisa, ni kuangalia nidhamu ya mavazi kwa waumini wake.
“Binafsi, mtu akija na nguo ya ajabu, awe mwanamke au mwanaume, siwezi kumruhusu aingie kanisani, ni bora nimvishe kanga au nimwambie ukweli akabadilishe ili Neno la Mungu litimie,” alisema Sanga.

Ufadhili, rushwa unaharibu uchaguzi Afrika Mashariki


Na Anne Kiruku, EANA
KUKOSEKANA kwa utashi wa kisiasa katika vita dhidi ya rushwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kunatokana na jinsi kampeni za uchaguzi wa kisiasa zinavyofadhiliwa.
Mkutano wa kanda uliofanyika mjini Kigali, Rwanda hivi karibuni, ulifafanua kuwa ufadhili huo umechochea upendeleo katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za umma, utoaji wa tenda na mikataba mingine ya huduma za jamii.
Washirika wa mkutano huo, waliwataka viongozi wa EAC waongeze vita dhidi ya rushwa kwa kusimamia utawala bora na kuzingatia uwajibikaji, uwazi na utawala wa sheria na siyo maneno bila vitendo.
Mkutano huo pia ulipendekeza kuoanisha sheria zinazohusu vita dhidi ya rushwa katika kanda hiyo na kujumuisha kipengele cha uwajibikaji wa kisiasa.
Wakizungumzia athari hasi za rushwa, wajumbe hao waliambiwa kuwa ni kubwa zaidi kwa makundi yaliyo katika hali ya unyonge wakiwemo wanawake, watoto na masikini katika jamii.
“Ili kufikia lengo la kuwa na Afrika Mashariki yenye mafanikio na umoja wa kisiasa, wadau wote hawanabudi kuzingatia utaratibu wa uwazi na uwajibikaji,” walisema wajumbe wa mkutano huo.
Mkutano wa Nne wa Mwaka wa EAC juu ya utawala bora, umewaleta pamoja wajumbe kutoka serikali za nchi wanachama na wadau binafsi wanaojihusisha na masuala ya kukuza utawala bora.
Mkutano huo ulioandaliwa na EAC, uliunda jukwaa la majadiliano ya mambo muhimu yanayohusu utawala bora yanayogusa mwenendo mzima wa mtangamano wa Jumuiya.
Akifungua mutano huo, Spika wa Bunge la Rwanda, Rose Mukantabana, alikiri kuwa rushwa ni ‘kansa kwa maendeleo ya kiuchumi.’
Alisema inakandamiza demokrasia na kubeza utawala wa sheria, hivyo, aliwataka viongozi wa EAC, kutafuta njia mbadala ya kupambana nayo.

Mbunge atoa angalizo kwa wana-Mtwara


Na mwandishi wetu
WAKAZI mkoani Mtwara, wameonya kutokubali kuuza ardhi kwa wawekezaji wanaoendelea kuingia kwa kasi mkoani humo.
Alisema hiyo itawasaidia kuepuka kuja kugeuzwa ‘watumwa’ ndani ya mkoa wao, badala yake, waiendeleze wenyewe.
Wito huo ulitolewa juzi jioni na Mbunge wa Tandahimba Juma Njwayo, alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara jimboni humo.
Njwayo, yupo jimboni humo kukagua shughuli za maendeleo.
Alisema wimbi la wawekezaji kununua mashamba makubwa na madogo mkoani humo, linaweza kuwa na madhara makubwa baadaye.
Mbunge huyo, alisema Mtwara una fursa nyingi za kiuchumi ambazo zimeanza kuwavutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Katika ziara hiyo, Njwayo alitembelea kata zote 14 zinazounda jimbo hilo na kufanya mikutano ya hadhara, iliyohusisha pia kupokea kero za wakazi hao pia kusaidia harakati za wapigakura wake kujiletea maendelo.
“Kataeni kuuza ardhi, ndio mkombozi Wenu wa baadaye. Wawekezaji wengi wanakimbilia mikoa ya Kusini kwa sasa kutokana na fursa za kiuchumi zinazoendelea kujitokeza,” alisema Njwayo.
Lakini pia aliwatahadharisha kuwa makini na madalali wanaotumiwa na wawekezaji hao kuska ardhi.
Wakati huo huo; aliwaeleza waazi hao kuwa serikali imeanza kuweka umeme kwa awamu ya pili ya 2013-2014, katika vijiji vilivyosalia.
Aliwataka wakazi wa Tandahimba, kujipanga kwa ajili ya kutumia fursa hiyo ya kuwekewa nishati hiyo muhimu kwa maendeleo.
Njwayo alisema vijiji vitakavyokuwa kwenye mpango wa kupata umeme ni Namikupa, Maundo, Nawahonga, Mtikila, Mnyawa, Mahena, Binembo, Mikunda, Lubangala na Mahuta.
Alisema njia nyingine ya umeme itafungwa Tandahimba hadi Mbarala, Lyenje hadi Mkoanjoano, Luagala hadi Itehu na Madaba mpaka Kitama.
Katika ziara hiyo, Njwayo alichangia zaidi ya sh. milioni 14 kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za jamii.

Sunday 28 July 2013

Siasa chafu zatikisa Tarime


na mwandishi wetu
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tarime, Mara, wameuomba uongozi wa juu wa chama hicho kuwachukulia hatua kali baadhi ya makada wanaofanya kampeni chafu.
Wamesema makada hao wamekuwa wakifanya kampeni chafu zenye lengo la kuwagawa wanachama makundi katika kata mbalimbali kwa lengo la kusaka ubunge mwaka 2015.
Pia, wameonya kuwa hawako tayari kugeuzwa bidhaa ya kisiasa kwani mchezo huo ni hatari kwa mustakabali wa Chama wilayani humo na wameapa kulifikisha suala hilo kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, ili alidhibiti mapema.
Kauli za wanachama hao zimetokana na baadhi ya makada kudaiwa kuanza kampeni za kusaka ubunge katika Jimbo la Tarime, ambapo wengine wamekuwa wakikusanya wajumbe na viongozi kadhaa kufanya vikao vya siri na kupanga mikakati nyakati za usiku.
Jimbo la Tarime kwa linaongozwa na Nyambari Nyangwine, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutatua kero za wananchi wake ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizotoa wakati wa kampeni.
Wakizungumza juzi wanachama hao wamesema wamekuwa wakikerwa na kuchukizwa na siasa chafu
zinazoendeshwa na wenzao na kwamba, zisipokomeshwa mapema zinaweza kuleta mpasuko. Wamesema wanatambua kila mwana-CCM ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, lakini hilo ni lazima lifanyike kwa mujibu wa taratibu za Chama na kinyume cha hapo ni usaliti ambao haustahili kufumbiwa macho.
Wamesema mbunge wa sasa (Nyambari), amefanya kazi kubwa katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa na suala la msingi ni kupewa ushirikiano na fursa ya kutimiza yale aliyoahidi.
“Mwenyekiti wetu taifa, Rais Jakaya Kikwete anasema kila siku tuache siasa chafu na tuwasaidie waliopo madarakani kutekeleza Ilani. Tumechoshwa na hawa wanaotaka kutulaghai kila kukicha wakitaka tuwaunge mkono wakati muda wa kampeni na uchaguzi bado,” alisema Marwa  Nyamhanga.
Alisema kwa muda mrefu CCM ilikuwa na wakati mgumu katika Jimbo la Tarime kutokana na kutawaliwa na upinzani, walijenga umoja na kufanikiwa kulirejesha mikononi ila kuna wachache wanataka kuleta mpasuko.
Naye Masero Mroni alisema, aliwatuhumu baadhi ya makada wa CCM walioshindwa kwenye mchakato wa kura za maoni na Nyangwine, ambao sasa ndio wameanza kuleta chokochoko na kuwagawa wanachama.
Hata hivyo, alisema kuwa kamwe hawatakubali kuingizwa kwenye siasa chafu kwa maslahi ya watu wachache na kwamba, watasimama imara kwa maslahi ya CCM na si vinginevyo.
Pia, alimtuhumuwa mkuu wa wilaya (jina linahifadhiwa) kuwa ni miongoni mwa chanzo cha kuleta mpasuko na makundi kwa wana-CCM.
Alisema kiongozi huyo amekuwa akiwarubuni wanachama kujiunga na kambi yake kwa madai kuwa ana uhakika mwaka 2015 ubunge ni wake, jambo ambalo kwa sasa halikubaliki kwa kuwa Chama bado kina viongozi wanaoendelea na kazi.
Kwa upande wake, Bhoke Mwita, alisema kwa wanachama kukubali kuanzisha makundi ni usaliti kwani, utaratibu wa Chama ni kumsaidia aliyepo madarakani kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Bhoke alitumia fursa hiyo kumuomba Katibu Mkuu wa CCM, Kinana kuingilia kati na kuwaonya wale wote wanaojaribu kuvuruga utaratibu wa Chama.
“CCM ina wenyewe na ndio sisi, kitendo cha watu wachache kutaka kutuvuruga na kutugawa ni kuandaa mazingira ya kurejesha jimbo kwa upinzani na hilo hatutalikubali. Namuomba Mheshimiwa Kinana awaadhibu hawa wenzetu ili tuendeleza umoja na mshikamano wetu,” alisema Bhoke.

Wednesday 24 July 2013

Masele: Wakamateni watoroshaji madini


Na Mohammed Issa
WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), wametakiwa kuwadhibiti na kuwakamata wale wote wanaotorosha madini nje kwa njia za panya.
Hatua hiyo imetajwa kuwa itasaidia kuokoa rasilimaliza za taifa, ambazo zipo kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Stephen Masele, alipozungumza na Baraza la Wafanyakazi la wakala huo.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara wanadaiwa kutorosha madini nje na kwamba, TMAA inapaswa kuendelea kuwabana zaidi ili kuokoa rasilimali hiyo.
Naibu Waziri huyo, alisema TMAA inafanya kazi kubwa na nzuri, hivyo, haina budi kuongeza kasi ili kuleta tija kwa Watanzania kwa kuokoa rasilimali zinazotaka kutoroshwa.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka kuendelea kuwabana wachimbaji wadogo kwa kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za serikali.
“Nawapongezeni kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya, lakini ongezeni juhudi zaidi, wale wote wanaojaribu kutorosha rasilimali za taifa wadhibitiwe. “Wakamateni wote watakaobainika kutorosha madini,” alisema Masele na kuongeza: Madini ni miongoni mwa rasilimali muhimu za taifa, lazima zipate usimamizi na ulinzi wa kutosha.
Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini kubanwa, Masele alisema baadhi hufanya ujanja kwa kukwepa kulipa kodi hivyo kupoteza mapato ya serikali.
Kwa mujibu wa Masele, kiasi kikubwa cha fedha za serikali hupotea kutokana na wachimbaji wadogo kukwepa kodi.
Naye Mtendaji Mkuu wa TMAA Mhandisi Paulo Masanja, alisema wakala huo umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Alisema hivi sasa wanazidi kusonga mbele katika kutekeleza wajibu waliopewa na serikali.
Mhandisi Masanja, alisema baadhi ya wamiliki wa migodi mikubwa na midogo, wameanza kulipa kodi stahiki za serikali na kiasi cha sh. bilioni 473.9 kimekusanywa toka 2009 mpaka sasa.
Alisema kutokana na kuimarisha kwa ukaguzi wa kimkakati unaofanywa na TMAA, zaidi ya sh. bilioni 1.8 zimekusanywa kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, zikiwa ni mrahaba.

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Paulo Masanja akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala huo, lililoketi jijini Dar es Salaam, jana. Anayefuata ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele.
WAJUMBE wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Madini Tanzania (TMAA) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri Masele baada ya kufungua kikao cha Baraza hilo kilichofanyika jana katika Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam.
MJUMBE wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), akitoa mada kwenye mkutano wa baraza hilo uliofanyika jana mjini Dar es Salaam.
WAJUMBE wa Baraza la wafanyakazi la WAkala wa Madini Tanzania (TMAA) wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika jana Dr es Salaam.

PRINCE Williams na mkewe Cate Middleton kwa raha zao.



HUYU ndiye mtoto wa Prince Williams.

PRINCE Williams na mkewe Cate Middleton wakiwasili kwenye kasri lao.

HAIJAPATA KUTOKEA UINGEREZA

PRINCE Williams na mkewe Cate Middleton, wakitoka ndani ya Hospitali ya St Marry.

Friday 19 July 2013

RAIS Jakaya Kikwete akizungumza na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba. Mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, Ikulu, mjini Dar es Salaam,  yalihusu masuala mbalimbali ya kiasa na kiuchumi nchini. (Picha na Freddy Maro).

Madudu ya watumishi hadharani


NA MWANDISHI WETU
TUME ya Utumishi wa Umma imebaini madudu katika utendaji wa watumishi wa umma, ikiwemo kuzembea katika kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanaoboronga kazi.
Kuchelewa kuchukua hatua kumesababisha baadhi ya watumishi kufanya makosa na kuendelea na kazi.
Tume imebaini tukio la mtumishi kutoroka kwa siku 200 huku akiendelea kulipwa mshahara.
Madudu hayo yamebainika baada ya viongozi wa tume kufanya ziara katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, ambako walizungumza na waajiri na watumishi wa umma wa kada mbalimbali.
Mwenyekiti wa tume, Jovin Kitambi, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, kuhusu ziara hiyo, iliyohusisha pia wakala 37 za serikali.
Alisema tume ilifanya ukaguzi kwa taasisi 42 kuangalia uzingatiaji sheria, kanuni na utaratibu katika maeneo ya ajira, upandishwaji vyeo, nidhamu, likizo za watumishi na upimaji wa wazi wa utendaji wa kazi kwa watumishi (OPRAS).
Kitambi alisema wamebaini  changamoto nyingi, ikiwemo baadhi ya waajiri na mamlaka za ajira na nidhamu kutozingatia sheria katika kushughulikia usimamizi wa rasilimali watu.
Changamoto nyingine ni watumishi kuchelewa kupandishwa vyeo na kuthibitishwa kazini na mashauri ya nidhamu kuendeshwa bila kufuata utaratibu.
“Kwa mfano mamlaka ya nidhamu kutochukua hatua pale mtumishi anapothibitika kufanya makosa, mtu anatoroka kwa siku 200 na anaendelea kulipwa mshahara,” alisema.
Akifafanua kuhusu watumishi kusimamishwa na kupumzishwa kazi, Naibu Katibu wa Tume, Idara ya Utumishi wa Serikali za Mitaa, Richard Odongo, alisema kanuni ya 38, kanuni ndogo ya nne ya utumishi wa umma imeweka wazi suala hilo.
Odongo alisema mtumishi akisimamishwa kazi anapaswa kulipwa nusu mshahara, lakini akipumzishwa anapaswa kulipwa mshahara na haki zake zote.

Tanzania kuuza gesi nje ya nchi


NA SELINA WILSON
SERIKALI inakusudia kujenga kiwanda cha gesi kwa ajili ya mauzo ya nje, ambapo kitaliwezesha taifa kuvuna mapato ya dola za Marekani milioni 200 (sh. bilioni 320) kwa mwaka.
Imesema kiwanda hicho kitajengwa eneo la Rushungi, ambalo liko katikati ya mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba, mchakato wa ujenzi wake unaendelea na kampuni mbili zimeonyesha nia ya kuwekeza.
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli wa Wizara ya Nishati na Madini Injinia Hoseah Mbise, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam.
Injinia Mbise, alikuwa akizungumza kuhusu faida zitokanazo na gesi asilia na manufaa yake kwa Watanzania, ikiwa ni utaratibu wa wizara mbalimbali kukutana na vyombo vya habari kueleza utekelezaji wa kazi za serikali.
Alisema mradi huo ni mkubwa na utekelezaji wake utachukua miaka mitano hadi sita na unatarajiwa kukamilika ifikiapo 2020.
Alisema kiwanda hicho kitakuwa kinachakata gesi asilia (LNG) na kuisafirisha kwa bomba kwa mauzo ya nje ya nchi.
Alizitaja kampuni zilizoonyesha nia ya kutekeleza mradi huo ambazo zinafanya mazungumzo na serikali kuwa ni BG ya Uingereza na State Oil ya nchini Norway.
Akizungumzia faida za gesi asilia, Injinia Mbise, alisema tangu 2004 hadi mwaka huu, sh. trilioni saba zimeokolewa kutokana na kutumia gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Alisema hadi Desemba 2012 sh. milioni 885 zimelipwa kwa Halmashauri ya Kilwa kama kodi ya huduma na kwa sasa, zaidi ya asilimia 50 ya umeme nchini unazalishwa kwa gesi asilia.
Tangu 2004 hadi sasa, megawati 418.5 za umeme zinazalishwa kutokana na gesi asilia.
Utafiti wa mafuta na gesi nchini ulianza 1952 hadi 1974, ambapo kampuni ya Agip ya Italia ilifanikiwa kupata gesi katika eneo la Songosongo na 1982 eneo la Mnazi Bay.
Hata hivyo, wataalamu wa kampuni hiyo waliondoka bila kuivuna gesi hiyo baada ya kuhisi kuwa kuna kiasi kidogo, baadae kampuni zingine zilifanya utafiti na kuanza kuvuna nishati hiyo.
Kwa sasa, kuna kampuni 19 na mikataba 27 ya utafutaji mafuta na gesi katika maeneo ya nchi kavu, mwamba na katika kina kirefu cha bahari.

Jecha Mwenyekiti mpya SUZA


Na mwandishi wetu
RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Sheni, amemteua Said Bakari Jecha, kuwa Mwenyeki wa Baraza la Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Dk. Sheni alifanya uteuzi huo kwa mujibu wa madaraka aliyopewa chini ya kifungu Namba 9(1) cha Sheria ya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Namba 8 ya 1999.
Pia, Dk. Sheni amemteua Abdulrahman Rashid kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Dk. Sheni alifanya uteuzi huo kwa mujibu  wa uwezo aliopewa chini ya kifungu Namba  8 (a) (1) cha sheria ya Bodi ya Mapato Zaznzibar (ZRB) Namba 7 ya 1996 kama ilivyorekebishwa na Sheria Namba 8 ya 2009.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi  Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi wa Jecha unaanza leo na uteuzi wa Abdulrahman ulianza juzi.

Chenge awajia juu askari Polisi


Chibura Makorongo, Simiyu
MBUNGE wa Bariadi Mashariki mkoani hapa Andrew Chenge, amekemea tabia za baadhi ya askari Polisi kuwanyanyasa madereva wa bodaboda.
Alisema madereva hao wanapaswa kuheshimiwa na inapotokea wanavunja sheria, wanapaswa kuelekezwa na kupewa adhabu stahili badala ya kunyanyaswa ikiwemo kuchapwa viboko.
Kauli hiyo ya Chenge imekuja baada ya kupokea malalamiko ya madereva wa bodaboda waliyoyatoa kwenye mkutano wa hadhara aliokuwa akiuhutubia.
Walidai kuwa huchapwa viboko na Polisi pale wanapowabaini kufanya makosa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo vijana na viongozi wa CCM, madereva hao waliwanyooshea vidole Polisi.
“Naona malalamiko mengi yanaelekezwa  kwa Polisi na bodaboda, sasa suala hili nitalifanyia kazi haraka ili vijana waachwe wafanye kazi, ili wasaidie maendeleo. “Wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na ikitoa wamekosea waelezwe si kuwakimbiza huku ni kuwakosesha riziki,” alisema Chenge.
Katika madai yao, madereva hao walisema mara nyingine husababisha ajali kufuatia kukimbizwa na Polisi.
Baadhi yao walidai kuwa huchapwa viboko na askari hao.
Pia, wamedai huombwa kutoa rushwa na kwamba, wamekuwa wakibambikiwa makosa ili wahalalishe rushwa.

Katibu Mkuu Ardhi apanda kizimbani


NA FURAHA OMARY
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, ameieleza mahakama kuwa, sh. milioni 100 zilihamishwa kutoka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi, kwenda wizarani kinyume cha utaratibu.
Rutabanzibwa alidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alipotoa ushahidi katika kesi inayowakabili waliokuwa Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Simon Lazaro, Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Gerald Mango na Kaimu Mhasibu Mkuu, Charles Kijumbe.
Mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, alidai hajui kama fedha hizo zimeibwa, kwani hazijulikani zilivyotumika.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, kutoa ushahidi Rutabanzibwa alidai mwishoni mwa mwaka wa fedha 2010/2011, Mango aliomba sh. milioni 200 kwa ajili ya mipango bora ya matumizi ya ardhi, kwa msingi wa dharura.
Rutabanzibwa alidai mkurugenzi huyo aliandika barua kwa katibu mkuu wa wizara, ambapo alimwelekeza kaimu mkurugenzi wa sera na mipango ashughulikie hilo kwa kuomba fedha HAZINA, ambazo zilikuwa nje ya bajeti.
Alidai fedha zilizoombwa zilikuwa kwa ajili ya mipango ya dharura katika matumizi ya ardhi katika wilaya tano.
Shahidi huyo alidai hana uhakika wa jinsi zilivyotumika, lakini aliambiwa sh. milioni 100 zilirejeshwa wizarani na kukabidhiwa kwa Lazaro, ambaye ni mshitakiwa katika kesi hiyo.
“Baada ya mwaka mmoja tulielezwa na TAKUKURU kuwa kuna tatizo la matumizi mabaya ya fedha. Lazaro na Mango walinieleza fedha hizo zimerejeshwa wizarani na kwamba, Lazaro alitia saini stakabadhi tatu kueleza amepokea sh. milioni 100 na kumkabidhi mhasibu.
“Stakabadhi zilikuwa zinasema Lazaro anakiri kupokea sh. milioni 100 kwa tarehe tofauti ambazo zilikuwa kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi ya wizara,” alidai.
Katibu mkuu alidai alichogundua katika fedha hizo ni kwamba, hazikuombwa kwa maandishi kutoka tume kwenda wizarani na zilipelekwa kinyume cha utaratibu wa kuhamisha fedha za serikali.
Alidai tume ilitakiwa kuandika hundi kwenda wizarani, ambako zingeingizwa kwenye akaunti ndipo zitumike kama ilivyokusudiwa.
“Kazi iliyokuwa ifanyike kwa mujibu wa stakabadhi ni tofauti na kazi iliyoombwa ya sh. milioni 200. Stakabadhi za sh. milioni 100 ni za kienyeji za Lazaro, ambazo alizifanyia marejesho ya masurufu zilizokuwa za kazi iliyokuwa na bajeti yake katika wizara,” alidai.
Sehemu ya ushahidi wa Rutabanzibwa akihojiwa na mawakili wa utetezi Henry Massaba na Msemwa ni kama ifuatavyo:
Massaba: Kosa la Mango ni nini, alichukua fedha na kumkabidhi Lazaro?
Shahidi: Hawezi kutueleza hizo fedha zilipelekwa kwa Lazaro kwa kitu gani kama kanuni zinavyosema.
Massaba: Anatakiwa na nani kueleza hilo?
Shahidi: Sheria na vifungu mbalimbali na kwamba, nyaraka za serikali hazikutumika katika kuhamisha fedha hizo.
Massaba: Katika ushahidi wako, Mango ana kosa gani?
Shahidi: Ametoa sh. milioni 100 kwa matumizi ambayo hayaeleweki na kinyume cha matumizi ya fedha za serikali.
Msemwa: Fedha ziliibiwa au?
Shahidi: Usiniingize huko. Sijui kama zimeibwa, kwani hazijulikani zilivyotumika na zimekwenda kinyume cha sheria.
Kesi hiyo itatajwa Agosti 15 na  itaendelea kusikilizwa Septemba 2 na 3, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Lazaro anadaiwa kuwa Mei 18, 2012, katika ofisi za tume hiyo, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa na wadhifa huo kwa nia ovu aliwasilisha nyaraka za marejesho kwa Mkurugenzi wa tume, kuonyesha alipokea sh. milioni 100 kutoka tume, kwa ajili ya mipango ya ardhi wilaya za Babati, Kilolo na Bariadi, huku akijua si kweli.
Lazaro, Mango na Kijumbe wanadaiwa kati ya Julai 4, na Agosti 5, 2011, Ilala, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa nia ovu walitumia madaraka yao vibaya.
Katika shitaka lingine, Lazaro anadaiwa tarehe tofauti kati ya Julai 4 na Agosti 5, 2011, Dar es Salaam, kwa kujua alibadilisha  matumizi ya sh. milioni 100 alizopewa na tume kwa ajili ya mipango ya ardhi katika wilaya za Arusha, Muleba, Ngorongoro, Songea, Kilosa na Mpanda.
Katika shitaka la nne, akiwa mtumishi wa umma, Lazaro anadaiwa katika tarehe hizo, wilayani Ilala, aliiba sh. milioni 100 alizoaminiwa na tume kwa ajili ya matumizi ya mipango ya ardhi katika wilaya hizo.

Miili ya askari JWTZ kuletwa leo


Na Mwandishi Wetu
MIILI ya askari saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur, nchini Sudan, inawasili leo alasiri.
Askari hao waliuawa wiki iliyopita, baada ya kushambuliwa na waasi katika jimbo hilo. Wengine 14 walijeruhiwa.
Miili ya askari hao itawasili kwa ndege maalumu ya Umoja wa Mataifa, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa tisa alasiri.
Taarifa iliyotolewa jana, mjini  Dar es Salaam, kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi ilisema baada ya kuwasili miili hiyo itapelekwa Hospitali ya Rufani ya Jeshi ya Lugalo.
Imeelezwa miili hiyo itaagwa keshokutwa, saa tatu asubuhi, katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga, Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ilisema miili ya askari hao itaagwa kwa heshima za kijeshi na baadaye itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
Hadi sasa waasi waliohusika na shambulio hilo hawajakamatwa, ambapo Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na Rais Omar al Bashir wa Sudan, alimtaka kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na mauaji ya askari hao.
Rais al Bashir aliyezungumza na Rais Kikwete kwa njia ya simu, alisema anaamini waliohusika ni wahalifu, hivyo watasakwa na kuchukuliwa hatua.
Umoja wa Mataifa umeahidi kuzilipa fidia familia za askari hao kiasi cha sh. milioni 100 kila moja.

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akizindua jarida maalum la Vivutio vya Uwekezaji mkoani Tabora, jana wakati wa mkutano wa pamoja kati ya taasisi za serikali na sekta binafsi. Mkutano huo uliojadili fursa za uwekezaji zilizoko mkoani humo ulifanyika jana, Hoteli ya Serena, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo,  Fatma Mwasa. Kulia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

Ahukumiwa bakora 70 kwa kusema uongo


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
KIJANA wa jamii ya Kimasai, Lomayani Mitewasi, amenusurika adhabu ya viboko 70 akituhumiwa kusambaza taarifa ya uongo kwenye mitandao ya kijamii.
Mitewasi alipewe adhabu hiyo juzi na viongozi wa jamii hiyo, pia aliamriwa kulipa ng’ombe dume kwa kosa la kukiuka mila za Kimasai.
Kijana huyo mkazi wa kata ya Elerai, alilazimika kusimama mbele ya wazee wa kimila (Malaigwanani) na kukiri kuwa taarifa hizo ni za uongo, na amekiuka mila za jamii hiyo kwa kuandika taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii.
“Wazee wangu naomba mnisamehe nilighafilika ninakiri  kuandika habari za uongo katika mitandao hiyo. Sikijui Kimasai, huwa ninasikia neno mojamoja tu, ingawa nilikuwepo kwenye mkutano uliopita sikujua hata mlizungumza nini, kwa kuwa mlikuwa mnazungumza kilugha,” alisema.
Kwa mujibu wa kijana huyo, aliandika Malaigwanani wamegawanyika katika makundi mawili, moja linatetea CCM na lingine CHADEMA jambo ambalo ni uongo.
Pia aliandika Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye, amewatumia Malaigwanani kuvuruga uchaguzi mdogo wa madiwani jijini Arusha.
Mitewasi aliandika kikao hicho kililenga kubagua wakazi wa Arusha kwa tofauti za makabila, ambapo alilazimika kufuta kauli na kuomba radhi mbele ya Malaigwanani hao kwa kile alichodai alighafilika.
Awali, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Katibu wa Baraza la MAA, Amani Lukumay, alisema wazee hao wamesikitishwa na taarifa hizo za uongo, ambazo zilisambazwa katika mitandao ya kijamii.
Lukumay alisema lengo la taarifa hiyo ni kuvuruga amani ya Jiji la Arusha na kuwagawa wazee hao. Alisema kikao cha wiki iliyopita kililenga kuzungumzia amani na hakuna kingine kilichozungumzwa.
Katibu huyo alitoa ufafanuzi baada ya kikao chao cha wiki iliyopita kuelezwa kuwa kilikuwa kina mwelekeo wa kisiasa, uliolenga kuinufaisha CCM dhidi ya CHADEMA.

JK mgeni rasmi Siku ya Mashujaa


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa.
Taarifa iliyotolewa jana, mjini Dar es Salaam na Ofisi ya Waziri Mkuu, Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa, ilisema maadhimisho hayo yatafanyika Julai 25, mwaka huu.
Maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika mkoani Kagera katika makaburi ya Kaboya.
Taarifa hiyo ilisema shughuli zitakazofanyika ni gwaride na uwekaji silaha katika mnara wa mashujaa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutakuwa na dua kutoka kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini.

Tanzania kufikia malengo ya chanjo


Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limesema Tanzania ni nchi inayotarajiwa kufikia malengo matano ya chanjo ifikapo 2020.
WHO imesema vigezo ambavyo Tanzania inaweza kujivunia ni kutokomeza polio, kufikia malengo ya chanjo na kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Mwakilishi wa WHO nchini, Dk. Rufaro Chatora, alisema hayo jana, katika hafla ya kukabidhi magari 24 kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha malengo ya mpango kazi wa chanjo yanafanikiwa.
Dk. Chatora alisema magari hayo yana thamani ya sh. bilioni moja na kwamba, 22 yatapelekwa wilayani kwa ajili ya kusambaza chanjo.
Magari mawili alisema yatapelekwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema taifa linaendelea kufanya vizuri katika huduma za chanjo.
Alisema asilimia 90 ya watoto wamepatiwa chanjo na kwamba, serikali itaendelea kuboresha huduma za afya.
Dk. Mwinyi aliishukuru WHO kwa msaada huo na kuahidi kuyatumia magari hayo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mama Salma akemea ubaguzi


Na Anna Nkinda, Maelezo
MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete, amewataka wanawake kutobaguana kutokana na itikadi za kisiasa au dini, badala yake wawe mstari wa mbele kuhubiri amani na upendo.
Alisema hayo jana wakati wa futari aliyowaandalia wanawake Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Mama Salma alisema ukosefu wa amani ukitokea katika nchi wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa, hivyo wasikubali kudanganywa.
Amewataka kuwa na msimamo ili kuilinda amani, ambayo ni silaha ya ukombozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Shamim Khan, alimshukuru Mama Salma kwa upendo wake.
Shamim alisema kukutana kwao kumewafanya wajifunze kuwa, wakitaka amani ni lazima washirikiane bila kujali rangi, dini au kabila, kwani wanawake wote wana matatizo yanayofanana, ambayo wanaweza kuyatatua kwa pamoja.
Naye Olive Lwema, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake Wakristo Tanzania, alisema wamefurahishwa na mwaliko wa Mama Salma.
Alisema wanapokutana wanawake, ambao ni wazazi wa watoto wa taifa na wake wa wanaume wanaoongoza nchi, hakuna jambo litakaloharibika.
Olive aliwaomba wanawake wanaofunga katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wajitoe kwa ajili ya kuomba amani.

Wednesday 17 July 2013

Maghorofa yaburuza vigogo kortini Dar


NA FURAHA OMARY
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), imewaburuza kizimbani vigogo wanne wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Wizara ya Fedha, wakituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu.
Vigogo hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kusomewa mashitaka mbele ya mahakimu tofauti.
Waliofikishwa mahakamani kutoka TBA ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Makumba Kimweri na Msanifu Mkuu wa wakala huo, Richard Maliyaga.
Kutoka iliyokuwa Wizara ya Fedha na Uchumi, waliopandishwa kizimbani ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Ernest Mwakitalu na Ofisa Ugavi, Liipu Nelingwa.
Kimweri na Maliyaga walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, wakikabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya madaraka.
Wanadaiwa kukiuka madaraka katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kwenye viwanja namba 45 na 46, vilivyoko mtaa wa Chimara, wilayani Ilala.
Akiwasomea mashitaka, mwendesha mashitaka kutoka TAKUKURU, Leonard Swai, alidai Kimweri, Agosti 6, 2007, katika ofisi za wakala huo wilayani Ilala, akiwa Mkurugenzi Mtendaji kwa nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini hati ya makubaliano namba TBA/JVA/DSM/ROI/001 kati ya TBA na Royalle Orchard Inn Ltd.
Swai alidai hati hiyo ilianzisha uhusiano kati ya serikali na sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi na umiliki wa jengo hilo bila kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo, hivyo kuipatia manufaa Royalle.
Kimweri anadaiwa siku hiyo, katika ofisi za TBA, alitumia madaraka vibaya kwa kutia saini hati ya makubaliano yenye namba TBA/JVA/DSM/ROI/002, kati ya wakala huo na Royalle ili kuanzisha uhusiano kati ya serikali na sekta binafsi kwa ujenzi na umiliki wa ghorofa katika kiwanja namba 46.
Maliyaga anadaiwa Julai 21, 2008, katika ofisi za TBA, akiwa Msanifu Mkuu, kwa nia ovu alitumia vibaya madaraka yake na kutoa kibali cha ujenzi namba TBA/BP/155 kuruhusu Royalle kujenga jengo la biashara la ghorofa 15 katika viwanja namba 45 na 46, bila kupata kibali kutoka kwa Idara ya Mipango Miji ya Manispaa ya Ilala.
Pia anadaiwa Aprili 9, 2009, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa kibali cha ujenzi namba TBA/BP/155(a) kwa Royalle kuongeza jengo la biashara kutoka ghorofa 15 hadi 18, bila kupata kibali kutoka mamlaka husika.
Kimweri na Maliyaga wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 6, 2007 na Aprili 9, 2009, kwenye ofisi za TBA, wakitekeleza majukumu yao, walitumia madaraka vibaya kwa kutoa kibali kwa Royalle kujenga jengo la biashara bila kibali na kubadilisha matumizi ya ardhi.
Washitakiwa walikana mashitaka, ambapo Swai alidai upelelezi umekamilika na hana pingamizi kuhusu dhamana.
Hakimu Sundi alitoa masharti ya dhamana akiwataka kila mmoja awe na wadhamini watatu, ambao ni wafanyakazi wa serikali, watakaoitia saini dhamana ya sh. milioni 50. Kesi itatajwa Agosti mosi, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.
Katika hatua nyingine, Mwakitalu na Liipu, walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba, wakishitakiwa kwa makosa 10.
Wanadaiwa kula njama, kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri, matumizi mabaya ya madaraka, kughushi, ufujaji na ubadhirifu wa sh. milioni 19.8 na kuisababishia mamlaka husika hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Swai akiwasomea mashitaka, alidai kesi hiyo inawakabili washitakiwa wanne lakini mahakamani wapo Mwakitalu na Liipu, kwa kuwa wengine hawajapatikana.
Alidai Mwakitalu, Liipu na wenzao ambao hawapo mahakamani, kati ya Juni na Julai, 2009, Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri.
Mwakitalu na mwenzake, ambaye hajafikishwa mahakamani, wanadaiwa Juni, 2009, katika Wizara ya Fedha na Uchumi, walitia saini na kutumia nyaraka ya ununuzi ya Juni 29, 2009, ikiwa na maelezo ya uongo kuonyesha kampuni ya AND-LINE (2000) International Co imepewa idhini ya kutoa huduma ya habari.
Maelezo hayo yalionyesha  walitakiwa kutoa habari nne kwenye vituo vya televisheni, nane kwenye vituo vya redio, tano kwenye magazeti, picha 10 na kipindi cha dakika tano kuhusu wizara hiyo kurushwa kwenye vituo vinne vya televisheni.
Kazi hizo zingefanyika wakati wa Maonyesho ya 33 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), katika Viwanja vya Mwalimu J.K Nyerere, kuanzia Juni 28 hadi Julai 10, 2009.
Washitakiwa wanadaiwa kughushi, kufuja na kufanya ubadhirifu wa sh. milioni 19.8, walizopewa na wizara kwa ajili ya vyombo vya habari wakati wa maonyesho hayo. Pia wanadaiwa kuisababishia hasara mamlaka husika ya kiasi hicho cha fedha.
Washitakiwa walikana mashitaka, ambapo Swai alidai upelelezi umekamilika.
Hata hivyo, aliomba shauri hilo litajwe ili wapate muda wa kuwatafuta washitakiwa ambao hawapo mahakamani.
Hakimu Nyigulila alitoa masharti ya dhamana, akimtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, watakaotia saini bondi ya sh. milioni tano. Kesi itatajwa Agosti 15, mwaka huu.

CCM yakataa tozo ya simu


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepinga tozo ya sh. 1,000 kwa mwezi kwa kila kadi ya simu.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, imesema CCM inapinga tozo hiyo kwa sababu itaongeza mzigo kwa wananchi wa kawaida.
Nape amesema tozo hiyo pia itasababisha usumbufu usiokuwa na sababu kwa wananchi.
Tozo hiyo ilipitishwa na Bunge mwezi uliopita, ikielezwa ni utaratibu wa kawaida wa kuibua vyanzo vipya vya kodi, pale vinapoondoshwa vilivyopo kwa sababu mbalimbali.
Nape alisema licha ya umuhimu wa tozo hiyo, vigezo vilivyotumika kupanga viwango sawia kwa kila mtu mwenye kadi ya simu havijazingatia hali tofauti za kipato kwa Watanzania.
Alisema Watanzania wengi matumizi yao ya simu ni ya kiwango cha chini mno.
“Chama tawala tunaona hatuwezi kukaa kimya kwenye jambo ambalo tunaliona linawabebesha mzigo wananchi, na huenda likarudisha nyuma maendeleo na
kuchelewesha jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania kwa jumla,” alisema.
Kutokana na hilo, CCM inaitaka serikali kuangalia njia mbadala ya kukusanya kodi ili kuziba pengo litakalosababishwa na kuondoshwa tozo ya kadi za simu bila kusababisha usumbufu kwa umma.
Utekelezaji wa malipo ya tozo hiyo umeanza Julai mosi, mwaka huu, ambao ndiyo mwezi wa kwanza wa mwaka wa fedha wa  2013/2014.
Katika hatua nyingine,
mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, alisema anakusanya maoni ya mtu mmoja mmoja kabla ya kufanya mkutano wa hadhara ili kujua wananchi wanataka nini kuhusu tozo hiyo.
Naye mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, alisema kwa kuwa suala hilo limeshapitishwa na Bunge, hakuna la kufanya.
“Kodi hii itaongeza uwezo wa nchi kuboresha miundombinu na mahitaji ya wananchi vijijini,” alisema.
Selemani Bungara, mbunge wa Kilwa Kusini, kwa upande wake alisema ana wakati mgumu jimboni kutokana na wananchi kutoa maneno ya kashfa kwamba, waliopitisha tozo hiyo wamewaangusha wananchi.
Alisema wananchi hawajaelewa kwa nini wabunge wamepitisha tozo hiyo.
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, akifafanua kuhusu tozo hiyo wiki iliyopita alisema kila mteja anayemiliki kadi ya simu atakatwa sh. 33.35 kwa siku.
Dk. Mgimwa alisema mapato yote yatakayokusanywa takriban sh. bilioni 160, yatasaidia kuboresha sekta ya nishati na maji.
Kwa mujibu wa serikali, mapato yatakayotokana na tozo hiyo yataharakisha maendeleo katika sekta ya maji, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Mfuko wa Barabara, kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijiji.
Dk. Mgimwa alisema uamuzi wa kuwalipisha wananchi tozo hiyo ni sahihi, kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji na uharakishaji maendeleo yao.
Alisema kiasi hicho cha fedha ni kidogo, kwa kuwa awali tume ya wataalamu iliyoundwa kutathmini suala hilo ilipendekeza tozo ya sh. 1,450, lakini serikali ikabadili kwa kuwa haipendi kuwaumiza wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alisema mchakato wa tozo hiyo haukuja juu juu, bali ulifanyiwa utafiti, hivyo kuwataka wanasiasa kuacha kuchanganya siasa na uchumi.
Naibu waziri alisema anashangazwa na maneno ya propaganda yanayoenezwa kutoka kwa wanasiasa na kampuni za simu, kwa kuwa hayana mashiko, kwani wanachanganya siasa na utaalamu

JK ampa kazi Rais wa Sudan


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amemtaka Rais Omar al Bashir wa Sudan, kuchukua hatua haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na mauaji ya askari saba wa Tanzania.
Askari hao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliuawa wakilinda amani katika jimbo la Darfur, nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Kikwete alisema hayo kupitia mazungumzo kwa simu na Rais Bashir.
Rais Kikwete ametaka wote waliohusika wafikishwe mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.
Katika mazungumzo yao, Rais Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kuahidi kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.
Rais Bashir alisema anaamini waliohusika ni wahalifu, hivyo ni lazima watasakwa na kuchukuliwa hatua.
Kiongozi huyo amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha, kwa kuwa wanajeshi wa Tanzania wako Sudan kulinda amani na usalama wa wananchi wa nchi hiyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alimpigia simu Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo uliotokea wakati askari hao wakitekeleza jukumu la kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi kilichokiri kuhusika na shambulio hilo, ingawa kumekuwa na kutupiana lawama kati ya vikundi vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano kati ya vikundi vya kikabila na koo yamesababisha uvunjifu wa amani na usalama katika jimbo hilo kwa miaka 10 sasa. Mapigano hayo yamesababisha vifo kwa wananchi wa Sudan na wageni.
Mwishoni mwa mwaka jana wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa jirani na El Geneina, Magharibi mwa Darfur.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi takriban 50 wameuawa tangu kikosi cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa pamoja chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze operesheni mwishoni mwa mwaka 2007.
Taarifa za UN zinaeleza kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania Jumamosi iliyopita, wanajeshi sita wanaolinda amani Darfur waliuawa tangu Oktoba mwaka jana, huku watu 300,000 wakiripotiwa kuyakimbia makazi yao.
Kiini cha mgogoro huo kinasadikiwa kuwa ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo.
Miili ya askari wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya maziko.

Tuesday 16 July 2013

Mapya yaibuka tozo ya simu


NA RABIA BAKARI
MALIPO ya tozo ya sh. 1,000 kwa kila kadi ya simu, yameibua mapya, ambapo maelfu ya wananchi wamepinga kulipa fedha hizo.
Wananchi hao wameorodhesha majina na kutia saini fomu, ambayo itapelekwa bungeni kupitia wawakilishi wao.
Tayari wananchi 23,569 katika jimbo la Ubungo, kupitia mbunge wao John Mnyika, wametia saini fomu hiyo.
Serikali imesema kila mwenye kadi ya simu ya mkononi atakatwa sh. 1,000 kwa mwezi, ambapo kwa siku atakatwa sh. 33.35.
Akizungumzia suala hilo jana kwa waandishi wa habari, mjini Dar es Salaam, Mnyika alisema wananchi wanataka taarifa zitolewe kwa umma kuhusu tozo hiyo.
Mnyika alisema wananchi wengi wanataka muswada wa sheria upelekwe bungeni katika mkutano ujao ili kufuta tozo hiyo.
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, akitoa ufafanuzi kuhusu tozo hiyo wiki iliyopita, alisema kila mteja anayemiliki kadi ya simu atakatwa sh. 33.35 kwa siku.
Alisema mapato yote yatakayokusanywa takriban sh. bilioni 160, yatasaidia kuboresha sekta ya nishati na maji.
Kwa mujibu wa serikali, mapato yatakayotokana na tozo hiyo yataharakisha maendeleo katika sekta ya maji, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Mfuko wa Barabara, kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijiji.
Dk. Mgimwa alisema uamuzi wa kuwalipisha wananchi tozo hiyo ni sahihi, kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji na uharakishaji maendeleo yao.
Alisema kiasi hicho cha fedha ni kidogo, kwa kuwa awali tume ya wataalamu iliyoundwa kutathmini suala hilo ilipendekeza tozo ya sh. 1,450, lakini serikali ikabadili kwa kuwa haipendi kuwaumiza wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alisema mchakato wa tozo hiyo haukuja juu juu, bali ulifanyiwa utafiti, hivyo kuwataka wanasiasa kuacha kuchanganya siasa na uchumi.
Naibu waziri alisema anashangazwa na maneno ya propaganda yanayoenezwa kutoka kwa wanasiasa na kampuni za simu, kwa kuwa hayana mashiko, kwani wanachanganya siasa na utaalamu.

Tanzania kuuza umeme nje


NA SELINA WILSON
TANZANIA itajitosheleza kwa nishati ya umeme ifikapo mwakani, na kuuza ziada ya megawati 500 nje ya nchi.
Imeelezwa ifikapo mwaka 2015 megawati 1,500 zitauzwa nje na mwaka 2016 zitauzwa megawati 1,800, hivyo kuliingizia taifa mapato makubwa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema hayo baada ya kutiwa saini mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya China Power Investment Co Ltd (CPI).
Profesa Muhongo alisema malengo hayo yatafikiwa baada ya kukamilika ujenzi wa bomba kubwa la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.
Alisema wameanza kupokea mabomba kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo, na mikakati ni kuhakikisha ujenzi unakamilika katika muda uliopangwa kwa kuwa mahitaji ya gesi ni makubwa.
Waziri alisema sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo sita ya kipaumbele cha serikali, hivyo katika mpango wa kutekeleza miradi yenye matokeo makubwa (BRN), inakusudiwa kufikia uzalishaji wa megawati 3,000 ifikiapo mwaka 2015.
Profesa Muhongo alisema mauzo ya umeme nje yataiwezesha nchi kubadilisha bajeti na kuondokana na kutegemea mapato kutokana na viberiti na bidhaa zingine.
Aliwataka Watanzania waepuke kuweka vikwazo katika matumizi ya rasilimali zilizopatikana nchini, kwani kwa kufanya hivyo wanakwamisha ukuaji uchumi.
“Gesi ni rasilimali ya Watanzania, lazima itumike kuleta maendeleo ya wote. Wanaotaka isitumike wanachelewesha jitihada za kupeleka nchi katika uchumi wa kati.
“Itafika wakati itabidi tugawanyike makundi mawili, wanaotaka maendeleo wakae peke yao na wale wasiotaka wabaki kwenye kundi lao, ili tusikwamishane,” alisema.
Alisema kuna tatizo kubwa la ajira, hadi wengine wanaliita bomu linalosubiri kulipuka, ambalo utatuzi wake ni kuongeza viwanda na kufungua fursa za kibiashara, mambo yanayowezekana kama kutakuwa na umeme wa uhakika.
Profesa Muhongo alisema umeme ukizalishwa kwa wingi, viwanda vingi vitajengwa na kuwezesha vijana kupata ajira, huku uzalishaji bidhaa ukiongezeka maradufu na kuuzwa nje.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alisema Tanzania inateswa na mfumuko wa bei kila wakati kutokana na kutegemea bidhaa nyingi kutoka nje.
Alisema utegemezi huo unatokana na kushindwa kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa kwa sababu ya ukosefu wa nishati ya uhakika na ya kutosha.
Balozi huyo alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete, za kuzalisha umeme wa kutosha, anaamini Tanzania itaondokana na tatizo hilo.

Ni msimu wa neema


JUMANNE GUDE NA
RACHEL KYALA
SERIKALI imesema hali ya chakula kwa mwaka huu ni nzuri, kutokana na mavuno ya kuridhisha katika mikoa 19 nchini.
Msemaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Richard Kasuba, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Kasuba alisema upatikanaji wa vyakula sokoni unaridhisha na bei zinaendelea kushuka kadri msimu wa mavuno unavyoendelea.
Hata hivyo, serikali imewaasa wakulima kutouza chakula chote na kuhakikisha wanaweka akiba ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia.
Alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), umeanza kununua nafaka kwa ajili ya kuongeza hifadhi ya chakula, ambapo unatarajia kununua tani 200,000 kutoka kwenye maeneo yenye ziada, hususan vijijini.
Serikali imewataka wakulima kuuza nafaka zinazokidhi vigezo vya ubora, kama vile kukaushwa vizuri, kutokuwa na takataka, zisiwe na punje zilizovunjika au kuliwa na wadudu, zenye rangi tofauti na ambazo hazijaathiriwa na ugonjwa wa mahindi.
Kasuba alisema NFRA itanunua chakula kwa kuzingatia gharama za uzalishaji na bei ya soko katika eneo la ununuzi, ili kurudisha gharama za uzalishaji kwa mkulima.
Alisema majukumu makuu ya wizara ni kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha, na kilimo kinachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kuondokana na umasikini.
Naye Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo, alisema ili kutunza mazao yasiharibiwe, wizara imeweka ramani ya aina ya udongo wa kila eneo na aina ya mbolea inayofaa kutumika.
Pia kushauri wakulima kujikita katika kilimo mseto ili kutunza rutuba.
Mtambo alisema ili kukabiliana na ugonjwa unaoathiri mahindi, wizara imeamua kutokuingiza mbegu za nafaka kutoka nchi jirani.

Dk. Magufuli amshitukia mkandarasi


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli, amemshukia mkandarasi wa kivuko kinachotengenezwa mjini Dar es Salaam, na kuagiza Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), kumchunguza kama ana uwezo kutekeleza mradi huo.
Mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya Scheepsbouw Noord Nederland b.v ya Uholanzi, alipewa kazi kwa mkataba wa sh. bilioni 2,840, na kilitakiwa kukamilika tangu Februari, mwaka jana.
Dk. Magufuli alitoa agizo hilo jana alipotembelea kukagua maendeleo ya kivuko hicho eneo la bandari Dockyard, Kurasini mjini Dar es Salaam, na kuagiza kazi hiyo ikamilishwe kabla ya Agosti 30, mwaka huu.
Alisema utekelezaji wa kazi hiyo hauridhishi na kwamba, kivuko hicho kinatakiwa kutumika katika eneo la Msanga Mkuu kwa ajili ya kuhudumia wananchi kati ya eneo la Msanga Mkuu na Msemo, mkoani Mtwara.
“Mkandarasi huyo achunguzwe endapo kweli anao uwezo wa kutekeleza mradi huu na kama ana usajili halali wa kufanyakazi zake hapa nchini,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema mkandarasi huyo alipewa kazi ya ununuzi wa kivuko kipya tangu Juni 17, 2010, kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Msangamkuu mkoani Mtwara.
Dk. Magufuli, alisema kivuko hicho ni cha tani 50, ambacho kitabeba magari sita na abiria 100 kwa wakati mmoja.
Mkandarasi huyo alianza kazi rasmi Desemba, 2011, na alitakiwa kuikamilisha miezi 10 na kukabidhi rasmi Februari, 2012.
Hata hivyo, alisema muda ulipofika alishindwa kukabidhi kazi na kutakiwa aikamilishe Mei, mwaka jana.
Baadaye aliomba aongezewe muda hadi Desemba, mwaka jana, hata hivyo, alishindwa kuikamilisha kazi hiyo mpaka sasa.
“Mkandarasi huyo amekaa hapa karibu miaka mitatu na ameshalipwa asilimia 78 ya fedha za kazi, sioni sababu ya kuchelewa hivi, hata mafundi gereji wangekuwa wameshaikamilisha,” alisema Magufuli.
Waziri Dk. Magufuli, aliwatahadharisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuwa makini wakati wanapoingia mikataba ya aina hiyo.
Fedha hizo alizolipwa ni kwa ajili ya kuagiza kivuko na kinachoendelea sasa ni kukiunganisha ili kipelekwe Mtwara.

Dawa za mabilioni kuteketezwa moto


Na Theodos Mgomba, Dodoma
WILAYA ya Kondoa inatarajia kuteketeza dawa za aina mbalimbali zilizoisha muda wake zenye thamani ya sh. bilioni 80.
Hayo yalisemwa jana na Mfamasia Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mayanja, katika mkutano wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Alisema tayari halmashauri imeshaoomba kibali cha kuteketeza dawa hizo toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Mfamasia huyo, alisema kati ya dawa zilizoisha muda wake ni pamoja za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi (ARVs) na malaria.
Kwa mujibu wa Mayanja, wilaya hiyo ina dawa nyingi zilizoimeisha muda wake, lakini wanasubiri utaratibu wa kuteketeza.
Alisema baadhi ni za mwaka 2000, lakini kutokana na utaratibu wa kuteketeza kuwa mrefu, dawa hizo bado zinahifadhiwa.
“Tumeshaandika barua Wizara ya Fedha kuomba fedha kwa ajili ya kazi hiyo na tayari mkurugenzi wa halmashauri ameshasaini,”alisema.
Mayanja alisema moja ya sababu ya kuwepo kwa shehena kubwa ya dawa hizo, ni kutokana na Bohari ya Dawa (MSD), kuleta dawa ambazo hazilingani na mahitaji husika.
Alisema ili kuondokana na tatizo hilo,  tayari wameanzisha mfumo wa kuunganisha wahudumu wa vituo vyote vya afya na ofisi yake, ambapo sasa wanapata taarifa za uwepo wa dawa za kila mwezi.
Mfamasia huyo, alisema mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwasilisha maombi ya dawa kwa wakati kwenye ofisi za MSD.

Bulembo awashika pabaya watendaji shule za Jumuia


NA RODRICK MAKUNDI, MOSHI
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, ameagiza watendaji wote waliosababisha madeni katika shule zinazomilikiwa na Jumuia hiyo, wakamatwe.
Bulembo, alitoa agizo hilo juzi, katika ziara yake mkoani ya kukagua uhai wa Chama na Jumuia zake sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alisema wote waliohusika kufanya hujuma hiyo, wasionewe haya, bali waamatwe na kuchukulia hatua kali za kisheria.
Bulembo, alisema hayo baada ya kusomewa taarifa ya Jumuia hiyo mkoani Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo mengine, ilielezwa kuwa shule nane kati ya 11 zinakabiliwa na madeni yanayofikia sh.milioni 800.
Kufuatia taarifa hiyo, Bulembo alisema hatakuwa tayari kupokea madeni hayo mpaka wahusika watakapokamatwa ili watoe maelezo kwa uzembe walioibebesha Jumuia hiyo mzigo huo.
Taarifa hiyo ilisema deni hilo linatokana na makato ya watumishi katika shule hizo ikiwemo ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutowasilishwa kwenye mamlaka hizo.
“Haiwezekani madeni haya yajionyeshe kwenye taarifa wakati tayari yalikatwa na ilipaswa yawe yamewasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika, na mnaposema wahusika wameacha kazi, lazima waje wajieleze, naagiza wakamatwe na wafikishwe mahakamani,” alisema.
Alisema atahakikisha wote waliosababisha madeni hayo wanakamatwa.
Naye Menyekiti wa Jumuia Mkoa wa Kilimanjaro  Festo Kilawe, alisema deni hilo  linahusisha malimbikizo ya mishahara, makato ya NSSF na TRA.

Babu amuua mjukuu kwa kumchapa bakora


NA ANITA BOMA , NJOMBE
MTOTO mwenye umri wa miaka miwili, Gift Fute, amekufa baada ya kupigwa fimbo na babu yake kwa madai ya kukutwa akichezea maji na wenzake.
Gift ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ikwega, Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani hapa, alikutwa na mkasa huo, Julai 13, mwaka huu, saa moja jioni.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa Fulgence Ngonyani, jana alisema mtoto huyo alikuwa akichezea maji na wenzake ndipo babu yake Nicolaus Fute (78), aliamua kumchapa na fimbo kwa lengo la kumwadhibu.
Alisema marehemu baada ya kuchapwa, inadaiwa aliumia na alipelekwa katika zahanati ya Usuka kwa matibabu, lakini alikufa akiwa anaendelea kutibiwa.
Kamanda Ngonyani, alisema chanzo cha tukio hilo ni kipigo kilichotoka kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Wakati huohuo;  mkazi wa Kijiji cha Lyamluki mkoani hapa, Hilda Mtega (86), amekutwa amekufa ndani ya nyumba yake.
Kamanda Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea Julai 14, mwaka huu, saa tano asubuhi.
Alidai kuwa marehemu alikuwa na tabia ya kwenda kanisani kushiriki Ibada na mambo mengine ya kidini, baada ya kutoonekana kwa siku kadhaa, ndipo waumini wenzake waliamua kwenda nyumbani kwake kujua kulikoni na ndipo walipobaini kuwa amekufa.
Aidha, Kamanda huyo alisema chanzo cha tukio hilo hakijajulikana ingawa inadaiwa huenda marehemu amekufa kutokana na shinikizo la damu, alikuwa akiishi peke yake.

Monday 15 July 2013

Mbowe ajisalimisha polisi


Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amejisalimisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kutokana na tuhuma zinazomkabili, zikiwemo kauli za uchochezi dhidi ya jeshi hilo, vyombo vingine vya dola na serikali kwa jumla.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, mwenyekiti huyo alijisalimisha jana mchana.
Advera alisema polisi inaendelea kumhoji Mbowe kuhusu kauli hizo za uchochezi na kuijengea jamii taswira mbaya kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama na kuwafanya wananchi kuwa na hofu.
Kwa mujibu wa Advera, uchunguzi wa kina unaendelea na itakapothibitika kuhusika kwake au mtu mwingine yeyote kutoka ndani au nje ya CHADEMA hatua za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Wakati Mbowe akijisalimisha, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeionya CHADEMA na vyama vingine vinavyofikiria au kutaka kuanzisha vikundi vya ulinzi.
Imeitaka CHADEMA kuacha mara moja mpango huo na kwamba, atakayekaidi atachukuliwa hatua kali za kisheria, ambazo hazitaweza kukatiwa rufani katika mahakama yoyote.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo, Uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ni wa mwisho.
Tamko hilo lilitolewa jana kupitia taarifa kwa vyombo vya habari baada ya CHADEMA kutangaza kuanzisha kambi ya mafunzo kwa kikundi chake cha vijana cha ‘Red Brigede’.
Mafunzo hayo yalitangazwa mbele ya waandishi wa habari na Mbowe, ikiwa ni moja ya maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
Mbowe alisema uamuzi huo umefikiwa ili kuwapa mbinu vijana hao za kukilinda chama hicho na viongozi wake, kwa madai kuwa wanaonewa na polisi.
Kauli ya Mbowe iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa chama hicho, Singo Kigaila, aliyesema mafunzo hayo yataanza wiki hii, na hakuna mtu yeyote atakayewazuia kufanya hilo.
Jeshi la Polisi kwa mara kadhaa lilitoa tamko kuionya CHADEMA kuacha mpango huo, likisema yeyote atakayehusika kufadhili, kuwahifadhi na kuwakusanya vijana atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Rajab Juma, kwa niaba ya Tendwa, ofisi ya msajili imeelezea kusikitishwa na kauli ya Mbowe kuhusu uanzishwaji wa kikundi hicho bila kuwasiliana na ofisi hiyo.
“Ofisi ya msajili inashangazwa na uamuzi huu, awali CHADEMA ilishawahi kutaka kuanzisha kikundi kama hiki na kuelezwa ni kukiuka sheria ikaacha kufanya hivyo,’’ ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema wakati huo, CHADEMA iliandikiwa barua kwa msajili yenye kumbukumbu namba RPP/CHADEMA/72/29 ya Desemba 31, mwaka 2004.
Imeelezwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa barua yenye kumbukumbu namba CAB/208/208/353/03/2 ya Desemba 29, mwaka 2004, ilielezwa kufanya mafunzo ya kujilinda ni kukiuka sheria za nchi.
Ofisi hiyo ilisema mwaka 2004 CUF iliandika barua kwa msajili ikitaka maelezo juu ya kuanzishwa kwa kikundi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CUF iliandika barua kwa msajili yenye kumbukumbu namba CUF/Ak/DSM/RPP/0034/7G/2004/14 Aprili 3, mwaka 2004
iliyoandikwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wilfred Lwakatare, kumtaarifu na kuomba ufafanuzi kutoka kwa msajili kuhusu kikundi hicho.
Katika majibu ya msajili kwa CUF, kupitia barua yenye kumbukumbu namba RPP/CUF/77/42 ya Mei 15, mwaka 2004, ilielezwa kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pia aliwaelewesha CUF kuhusu suala hilo na kupiga marufuku mpango huo kwa barua yenye kumbukumbu namba AB 286/386/353/01/73.
Kutokana na hilo, ofisi hiyo  imesisitiza kwamba, sheria zinazokataza suala hilo hazijabadilika na viongozi wa CHADEMA ni wale wale walioonekana kuelewa na waliositisha kutekeleza mpango huo mwaka 2004.
“Nia ya CHADEMA haieleweki. Kama ni kupima matokeo iwapo watatekeleza mpango huu, basi uamuzi wao hautakuwa wa busara kwa uhai wa chama chao.
“Kuendelea kufanya mafunzo kwa chama ni kukiuka sheria za nchi, ikiwamo ya vyama vya siasa ya 1992 kifungu 9(2)(c), ambacho kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu na vurugu ili kufikia malengo yake ya kisiasa,” alisema.
Ofisi hiyo imesema msajili atachukua hatua kali za kisheria kwa chama kitakachoshindwa kutii agizo hilo, kwa kuwa kifungu cha 19 kinatoa mamlaka ya kukifuta chama kinachokiuka masharti ya usajili na kifungu cha 20 kinaeleza uamuzi wa msajili ni wa mwisho.
UFAFANUZI KATIBA ZA VYAMA
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, ofisi ya msajili ilishatoa ufafanuzi mwaka 2004, wakati vyama vya siasa vilipoandika barua kutaka kuanzisha vikundi hivyo kwa kuwa katiba za vyama vyao zinaruhusu.
“Ufafanuzi tuliotoa ni kwamba, vikundi hivi ni wanachama wanaopewa jukumu na chama kuangalia usalama wa mali na viongozi wa chama.
“Hili ni kama ambavyo majumbani tunaangalia au tunaweka watu wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au ukakamavu kuangalia usalama wa nyumba zetu mchana hata usiku,’’ ilisema taarifa hiyo.
Katiba ya nchi imempa jukumu kila mwananchi kulinda amani na usalama, pia kujilinda yeye na mali zake, kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale anaposikia au kuona mtu anataka au anafanya uhalifu au anataka kumdhuru.
Taarifa hiyo ilisema katiba ya nchi au katiba za vyama hazina maana ya kila mwananchi au kikundi fulani kifanye mafunzo ya kijeshi au ukakamavu ili kufanikisha jukumu  hilo.
Alisema vinapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola na si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kwa kuwa, wenye jukumu la ulinzi ni vyombo vya ulinzi na usalama.
USHAHIDI JUU YA CCM
Taarifa hiyo ilisema madai kuwa CCM ina kambi za mafunzo ya vijana kupambana ni kisingizio cha kuvunja sheria na hayana msingi.
Imeviasa vyama vya siasa kutumia muda wake kufanya siasa ili kuchangia maendeleo, badala ya kubuni mambo yanayoleta mtafaruku.
Ofisi hiyo ilisema amani ikitoweka vyama vya siasa vitakuwa katika makaratasi, hakutakuwa na mikutano ya vyama, kamati kuu, mkutano wa waandishi wa habari au operesheni kwa kuwa demokrasia hutekelezwa na kukua mahali penye amani na utulivu.

Ujambazi wa kutisha


NA ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA
MAJAMBAZI 10 yakiwa na silaha za kivita, yameteka mabasi mawili, kumpora askari polisi bunduki na kuiba mali za abiria.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.30 asubuhi katika eneo la Kasindaga, ndani ya Pori la Akiba la Biharamulo, mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Philip Kalangi, alisema majambazi hayo yakiwa na bunduki sita aina ya SMG na mbili aina ya LMG yaliteka mabasi hayo.
Alisema mabasi yaliyotekwa ni la Kampuni ya RS, lenye namba ya usajili T 495 AGT, lililokuwa likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam na NBS, lenye namba  T 644 BUR, lililokiwa likitoka Bukoba kwenda Arusha.
Kamanda Kalangi alisema  majambazi hayo yaliteka mabasi hayo baada ya kuwaweka chini ya ulinzi abiria na polisi wanne waliokuwa wakiyasindikiza.
Alisema majambazi hayo yaliwaamuru abiria kushuka ndani ya basi na kutoa kila walichokuwa nacho, zikiwemo  simu na fedha taslimu.
Baada ya kutoa mali hizo, majambazi hayo yaliwaamuru abiria kulala kifudifudi.
Alisema abiria na polisi walitii amri hiyo, ambapo baadaye basi la Kampuni ya Mohamed Trans lililokuwa likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam, lilipita likiwa na askari, ndipo walipobaini wenzao wametekwa.
Kalangi alisema askari huyo alishuka ndani ya basi na kuanza kupambana na majambazi hayo, hivyo basi hilo kupata nafasi ya kuondoka.
Alisema askari huyo alizidiwa nguvu na majambazi hayo, ambayo yalimnyang’anya bunduki aina ya SMG, yenye namba ya usajili 14302551.
Kamanda alisema katika tukio hilo, Fredrick Rugaihura (47), mkazi wa Bukoba, aliyekuwa anakwenda Dar es Salaam, alibishana na majambazi hayo, hivyo yalimjeruhi kwa risasi shingoni.
Alisema Rugaihura amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo kwa matibabu na kwamba, abiria wengine waliendelea na safari.
Kamanda alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako ili kuyanasa majambazi hayo.
Alisema abiria walipohojiwa walisema majambazi hayo yalikuwa yakitumia lugha ya nchi za jirani. Thamani ya mali iliyoporwa bado haijajulikana.

Mbeki: Mandela atarejea nyumbani


JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema anaamini Rais wa kwanza Mzalendo wa nchi hiyo, Nelson Mandela, ataruhusiwa kutoka hospitalini.
Mbeki, aliyekuwa Makamu wa Rais katika serikali ya Mandela, alisema hayo mwishoni mwa wiki alipoalikwa kwenye hafla maalumu iliyoandaliwa na chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC.
Kwa mujibu wa Mbeki, amemtembelea Mandela mara kadhaa hospitalini alikolazwa na kwamba, hali yake imeimarika kiasi cha kuweza kuruhusiwa kutoka katika hospitali ya Pretoria alikolazwa tangu Juni 8, mwaka huu.
Kwa upande wake, Graca Machel, ambaye ni mke wa Mandela, hivi karibu alikaririwa akisema hana hofu na hali ya kiongozi huyo kama ilivyokuwa wiki kadhaa zilizopita.
Graca alisema Mandela anaendelea vizuri kutokana na juhudi zinazofanywa na madaktari wanaomhudumia na kwamba, anaamini anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali.
Baadhi ya marafiki na watu walio karibu na Mandela waliomtembelea hospitalini walisema bado anapumua kwa msaada wa mashine.
Wiki iliyopita Denis Goldberg, rafiki wa karibu wa Mandela  alipinga taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuwa hali ya kiongozi huyo ilikuwa mbaya na kwamba, familia yake ilikuwa ikiangalia  uwezekano wa kuondoa mashine inayomsaidia kupumua.
“Mpiganaji Mandela anaendelea vizuri. Taarifa zinazotolewa kuhusu afya yake kuwa mbaya sana si za kweli,” alisema.
Goldberg aliyewahi kufungwa miaka 22 jela katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo, alisema alipomtembea Mandela hospitalini licha ya kumkuta mgonjwa, alikuwa akijitambua na kujaribu kuzungumza.
Mbeki ndiye mrithi wa Mandela baada ya kustaafu mwaka 1999, na kuwa rais wa pili mweusi wa nchi hiyo.
Mandela alilazwa hospitalini hapo baada ya kuugua magonjwa mbalimbali, ikiwemo wa mapafu. Afya yake imekuwa ikibadilika mara kwa mara.

Aliyemjeruhi sheikh kwa tindikali mbaroni


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
POLISI inamshikilia Mustafa Kiduka (50), kwa tuhuma za kummwagia maji yanayodaiwa tindikali Kaimu Sheikh wa wilaya ya Arumeru, Said Makamba, na kumsababisha maumivu makali usoni na kifuani.
Sheikh Makamba alimwagiwa maji hayo Ijumaa iliyopita, saa tano usiku, alipokuwa akitoka katika Msikiti wa Jabal Hald.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa, mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Sekei na anaendelea kushikiliwa.
“Mtuhumiwa tunamshikilia hadi upelelezi utakapokamilika. Tunasubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini kama kweli kimiminika hicho kilikuwa tindikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Sabas, sheikh huyo pia ni Imamu wa Msikiti wa Jabal Hald, ulioko eneo la Kwa Mrombo.
Alisema mkasa huo ulimpata wakati akitoka kusalisha sala ya Tarawehe, ambapo alipofika nyumbani kwake alitoka nje kwenda kujisaidia, ndipo ghafla aliposikia kishindo cha mtu aliyekuwa amebeba kikombe chenye maji na kumwagia usoni.
Mganga Mkuu wa mkoa, Frida Mokiti, alithibitisha kulazwa kwa sheikh huyo katika Hospitali ya mkoa ya Mount Meru na hali yake inaendelea vizuri.
Wakati huo huo, mkazi wa  Olmatejo, Zainabu Maulid (25), anashikiliwa akituhumiwa kughushi shahada ya kupigia kura yenye namba 32468790, aliyojaribu kuitumia juzi, kupiga kura katika kata ya Elerai.
Katika tukio lingine, bweni la Shule ya Sekondari ya Diozon, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha liliteketea moto.
Sabas alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 1.30 usiku. Alisema bweni hilo lilikuwa na wanafunzi 142, ambao mali za zimeteketea.
Chanzo cha moto huo alisema ni hitilafu ya umeme.

Twiga Bancorp yatua Bunda


Na Ahmed Makongo
WAFANYABIASHARA na Kandarasi wanaofanya kazi na halmashauri ya wilaya ya Bunda, wametakiwa kufungua akaunti katika benki zilizopo wilayani humo, ili kusaidia kuinua uchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Tuppa, alitoa wito huo juzi, alipokuwa akifungua kituo cha kutolea huduma za kibenki cha Twiga Bancorp.
Mirumbe, alisema wilaya hiyo ni ya uwekezaji wa kibiashara. Vyema wale wote wanaopatiwa zabuni katika halmashauri hiyo, wakafungua akaunti katika benki hizo.
Alisema kuanzia sasa kandarasi yeyote anayeomba kazi katika halmashauri hiyo, lazima awe ana akaunti kwenye benki iliyoko wilayani humo, kinyume na hapo, hawatapatiwa zabuni.
Mkuu huyo wa Wilaya, alizitaja benki hizo kuwa ni Twiga Bancorp, inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na NMB.
“Tutafanya utaratibu ili mkandarasi anayefunga mkataba na halmashauri yetu lazima awe na akaunti ya Benki yoyote iliyoko wilayani kwetu…Unajua hali hiyo itafanya mzunguko wa pesa kuwa mkubwa na uchumi wa wilaya yetu utakuwa” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Twiga Bancorp Limited, Profesa Ammon Mbelle, alisema benki hiyo ndiyo pekee  nchini inayomilikiwa na serikali kwa aslimia 100.
Alisema ni vyema kwa kila Mtanzania popote  alipo, aitumie ipasavyo.
Profesa Mbelle, alisema dhana ya benki hiyo ni kuungana na umma wa Watanzania waliodhamiria kuboresha hali ya maisha yao pamoja na kulijenga taifa kiuchumi.
 Naye Mkuu wa Shughuli za Utendaji wa Kibenki wa benki hiyo, Richard Kambole, alisema kituo hicho cha Bunda ni cha kwanza kufunguliwa nchini na wilaya hiyo imepewa kipaumbele.

Red Brigade’ ni magenge ya kigaidi, utekaji nyara, utesaji, uuzaji wa dawa za kulevya na umwagaji damu


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza rasmi kuanzisha kambi za kijeshi nchini kote ili kuwapa mbinu za kivita vijana wake wanaoitwa “Red Brigade”, kazi ambayo hata hivyo ilishaanza siku nyingi.
Katika kufanya hivyo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa chama chake kimechukua hatua hiyo baada ya serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kushindwa kuyafanyia kazi malalamiko yao kuhusu mauaji, vitisho na matukio na kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wao.
Siku moja baadaye, chama hicho kililisusia Kongamano la Amani lilloiandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam na mgeni wake rasmi kuwa Rais Jakaya Kikwete, yule ambaye katika hotuba yake ya ufunguzi alishangaa kitendo hicho cha Chadema na kuhoji:
“Hawa kweli wanapenda amani yetu wakati hawapendi tuzungumze? (Ina maana wao) wanataka watu wauane au wapigane?”
Alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita, Mkurugenzi wa Mafunzo na Organaizesheni wa Taifa wa Chadema, Benson Kigaila alisisitiza kuwa mafunzo hayo hayatasitishwa ila yataendelea ingawa tayari yameshapigwa marufuku na polisi nchini.
Akizungumzia suala hilo Alhamisi iliyopita, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Senso alisema hatua yoyote ile chama chochote cha siasa kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume cha sheria, hivyo kama Chadema haitasitisha nia yake hiyo itachukuliwa hatua mara moja.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki ya raia yeyote kujilinda. Chadema ni taasisi (na hivyo) ni haki yetu kuilinda na ndiyo maana tumesajili kikundi chetu cha ulinzi.
“Sasa nani anatutisha? Tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao katika mafunzo yao wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha”, alisema Kigaila ambaye kwa wanaoifahamu hulka yake wanajua jinsi anavyopenda shari muda wote.
Ndiyo maana alishiriki kutaka kumpindua Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha United Democratic (UDP), John Momose Cheyo mwaka 2003 na kujikuta akifukuzwa uanachama na uongozi aliokuwa nao huko na kukimbilia Chadema.
Alidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliweka makambi yenye jumla ya vijana 800 katika mikoa ya Shinyanga, Singida na Tabora ambao baadaye walipelekwa Igunga wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo mwaka 2011 na kusababisha kifo cha kada mmoja wa Chadema, Msafiri Mbwambo.
Alidai hata mwaka jana, CCM iliandaa mafunzo ya kitaifa kwa vijana wake wanaoitwa Green Guard huko Mwanza, yale ambayo yalihitimishwa kwa gwaride lililokaguliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Jakaya Kikwete; Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Sipendi kuamini uongo na hata uzushi kwa vile sipendi kabisa kuwadanganya wananchi na hata vinginevyo.
Vijana wa Green Guard ambao wanatoka katika Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) siyo wanajeshi, mgambo na wala hawana kabisa mbinu za kijeshi kama alivyodai Kigaila na kamwe kazi zao siyo za kivita.
Mafunzo makubwa wanayopewa wanapokwenda kambini ni ujasiriamali kikiwemo kilimo cha mashamba makubwa, kilimo cha umwagiliaji kama vile bustani, ufugaji wa nyuki, kazi za mikono na kujitolea, uvuvi, uvumilivu, mapokezi ya viongozi wa chama chao na maisha ya kijamaa.
Wanapata mafunzo hayo kwa kutumia mapanga, shoka na majembe kwa kilimo na kufyeka misitu kwa ajili ya kilimo na maandalizi ya mashamba, nyavu za kuvulia samaki, mbao zilizotengenezwa kama bunduki kwa ajili ya kufanyia mazoezi ya gwaride la kuwapokelea viongozi wa chama chao, zile ambazo hata hivyo wanapokuwa wakiwapokea hawazitumii popote wala silaha yoyote.
Hawapigi saluti yoyote ile ya kijeshi kama alivyodai Kigaila isipokuwa za mfumo wa aina yake na salaam tu maalum kwa ajili ya viongozi waandamizi wa chama chao, jambo ambalo halina ubaya wowote isipokuwa linapotoshwa ili kutaka kuhalalisha malengo ya kigaidi ya Red Brigade!
Hata kambi hizo zenyewe hazifanyiki mijini isipokuwa vijijini kwenye mashamba, mifugo, mabwawa ya ufugaji au yenye samaki, mizinga ya kufugia nyuki, bustani za kuku na kazi nyingine za kijasiriamali.
Anayetaka kujua ukweli huu aende katika Chuo cha Itikadi cha Ihemi kilichopo wilayani Iringa ili akayaone mashamba makubwa kabisa ambayo yapo mahali hapo. Atajionea namna vijana hao wa CCM wanavyofundishwa kazi za mikono, kilimo cha bustani na mashamba makubwa, uvumilivu pamoja na upendo kwa kila mtu.
Kana kwamba haitoshi, CCM kamwe haina kabisa mfumo wa gwaride moja la chipukizi wake au vijana wa Green Guard kukaguliwa wakati mmoja na zaidi ya kiongozi wake mmoja isipokuwa vinginevyo.
Haina utaratibu wa ovyo wa Kichadema wa viongozi wake wakuu kama Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu kufuatana pamoja katika tukio moja.
Hata tarehe 5 Februari ya kila mwaka hawafuatani pamoja kwenye sherehe  zake isipokuwa hukutania uwanjani na hatimaye hutawanyika kila mmoja kwa muda wake, halafu hawafanyi kabisa kazi zinazofanana ila kila kiongozi anakuwa na jukumu lake na kuzingatia itifaki.
Mafunzo yanayotolewa kwa vijana wa Chadema ambayo kwanza yalishaanza siku nyingi katika baadhi ya mikoa kama Shinyanga ni mbinu za kijeshi, mapigano ya kivita zikiwemo kung-fu, utumiaji wa silaha hususan mapanga, visu vya kurusha, fimbo na kadhalika.
Ndivyo ilivyokuwa kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mazinge iliyopo kata ya Ndembezi na baadhi ya maeneo ya Ibinzamata, Kizumbi na Ngokolo mjini Shinyanga.
Wamekuwa wakifundishwa hasa nyakati za jioni hadi usiku kwa kubadili mafunzo kadri muda unavyokwenda ambapo mchana huanza kama watu wanaofanya mazoezi ya kawaida ya viungo, halafu usiku ndipo wanafundishwa mbinu za kijeshi wakianza na nadharia na hatimaye vitendo.
Mbowe na Kigaila wanapodai eti chama chao ndiyo kwanza kinataka kiwafundishe vijana wake mafunzo ya kuwalinda viongozi na wanachama wao wanadanganya waziwazi na bila aibu japokuwa kidogo!
Wanajua kuwa vijana kutoka nje ya mkoa wa Shinyanga ndio waliokuja kuwafundisha Red Brigade wao mbinu za kigaidi, na kwamba wanapodai hayo eti ni mafunzo ya kujilinda ama kuwalinda viongozi na wanachama wao wanasema uongo.
Hivi viongozi wa Chadema kama Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa au Wajumbe wa Kamati Kuu akina Zitto Kabwe, Godbless Lema, Peter Msigwa, John Mnyika, John Heche, Tundu Lissu na kadhalika wawe wanalindwa na vijana wa Red Brigade dhidi ya nani au kwa kitu gani walichonacho?
Kama hata viongozi waandamizi wa serikali kama vile Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya au Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji au Wilaya ambao kuna wakati hutoa maamuzi mazito yanayohusu mpaka maisha ya watu wengine hawana ulinzi; hawa wa Chadema wana nini?
Mbali na hayo, kudai eti kazi kubwa ya kikosi cha Red Brigade ni kuwalinda viongozi na wanachama wa Chadema kutokana na tishio lolote lile ni uongo na uzushi.
Nafahamu kwamba kinachofanywa na chama hicho ni kuibua visingizio vya kutaka shari kila kunapokucha ili kutafuta mbinu au mikakati ya kuendeleza vurugu zao, kusimamisha majukumu ya serikali zikiwemo kazi za kushughulikia maendeleo ya wananchi na badala yake ibaki ikihangaikia malumbano yasiyokuwa na tija yoyote kwa taifa letu.
Nawashangaa Mbowe na Kigaila wanapodai kuwa Chadema imeamua kutoa mafunzo hayo kwa Red Brigade wake baada ya serikali na vyombo vyake ya ulinzi na usalama kushindwa kuyashughulikia madai yao ya mauaji, vitisho na matukio mengine ya kutisha yanayofanywa dhidi ya wanachama na viongozi wao.
Rekodi ya mauaji yatokanayo na harakati mbalimbali za vyama vya siasa nchini yamekuwa yakisababishwa kwa kiwango kikubwa zaidi na Chadema yenyewe, hivyo haiwezekani kuja kuisingizia serikali au vyombo vya ulinzi na usalama kwamba haviwasikilizi wanapokwenda kulalamikia suala hilo.
Mathalani, vurugu zilizoacha mauaji ya wananchi watatu yaliyotokea Januari 5, 2011 mjini Arusha zilisababishwa na viongozi wa Chadema ambao ni pamoja na Mbowe binafsi, Dk. Slaa, Kigaila pamoja na wabunge takribani wote wanaotoka chama hicho na kadhalika.
Wote walishirikiana kwa jeuri, kejeli, kebehi na dharau kwa kukaidi ushauri wote waliopewa kwa kuelimishwa, kuonywa na hata kubembelezwa kwamba wasifanye maandamano wakati wa kwenda kwenye mkutano wao uliokuwa ufanyike mjini humo.
Kilichotisha zaidi ni kuandamana kwa ghasia, vurugu au fujo kwa kupita barabarani, mitaani na maeneo mbalimbali ya jiji hilo huku wakipiga watu, kuchoma nyumba, magari, ofisi ama maduka na vibanda vya wafanyabiashara waliokuwa wakiwashutumu kwamba hawawaungi mkono na kuwa upande wa serikali, CCM au Jeshi la Polisi.
Walikuwa wakiandamana huku wakimwaga kila aina ya matusi yakiwemo yale ya nguoni, kuwatisha au kuwashambulia watu bila hatia yoyote au kuwakejeli kwa maneno machafu mpaka viongozi waandamizi wa serikali ya nchi yetu!
Kibaya kinachotisha zaidi ni pale walipobadili mwelekeo wa kwenda mkutanoni na kutaka kwenda kukiteka kituo Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa huo ili wakaibe silaha zilizokuwa ndani zikiwemo za kivita, wawatoroshe mahabusu wa makosa mbalimbali waliokuwemo, wawakamate askari wake na hatimaye wakichome moto ili kisiwepo kabisa!
Licha ya kuonywa kwa zaidi ya mara tatu wakitangaziwa kwa kipaza sauti kwamba watawanyike mara moja, wafuasi hao wa Chadema waliotiwa jeuri na viongozi wao waliendelea kukisogelea kituo hicho muhimu kwa usalama wa maisha ya wananchi na mali zao huku wakirusha mawe na kubeba hadi mapanga, sime pamoja na silaha nyingine.
Ni kutokana na hali hiyo ndipo Jeshi la Polisi lilipolazimika kufyatua risasi za moto zilizoua watatu kati yao huku wengine wakijeruhiwa kwa viwango tofauti, hatua iliyopelekea kituo hicho kinusurike kuteketezwa kwa mikakati ya kigaidi.
Mbali na tukio la Arusha, vurugu za Chadema pia zilisababisha kada mmoja wa CCM katika kata ya Ndago huko Iramba, Singida naye apoteze maisha yake na hatimaye mauaji mengine huko Msamvu mjini Morogoro na kijiji cha Nyororo wilayani Mufindi, Iringa.
Wafuasi hao wa Chadema wanatuhumiwa kwenda kumshambulia kada huyo wa CCM kwa silaha za jadi akiwa ndani ya nyumba alimokimbilia ili kunusuru maisha yake, halafu mauaji ya Msamvu na Nyororo yalitokana na ukaidi wa viongozi wa chama hicho kwa vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi nchini.
Wanataka wanapofanya mikutano yao ya hadhara ni lazima waende kwa maandamano hata kama hali na mazingira ya usalama hayaruhusu.
Wakiwa bado Morogoro, serikali ilisitisha kwa muda wa siku saba mikusanyiko yoyote ya kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara ili kupisha zoezi muhimu la sensa na makazi ya watu, lakini viongozi hao wa Chadema walikaidi huku Dk. Slaa akimwandikia ujumbe mfupi wa maneno ya kejeli Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Tanzania, Saidi Mwema akimwambia kuwa apeleke askari wa kwenda kupambana naye Iringa!
Aidha, kurushwa kwa bomu lililoua watu watatu wengine siku ya mwisho ya kampeni za Chadema katika Viwanja vya Soweto jijini Arusha hivi karibuni, kuna kila viashiria kwa chama hicho chenyewe kuwa pia kilihusika nalo kwa namna moja ama nyingine.
Haiwezekani kuwa hata baada ya bomu hilo kurushwa na kuibua taharuki nzito mkutanoni, mpigapicha za video iliyodaiwa na Mbowe na Lema kwamba wanayo nakala yake aendelee kuifanya kazi hiyo na bila wasiwasi.
Haiwezekani kabisa Mbowe na Lema eti wasikimbie au kutoroshwa kwa kuyahofia maisha yao, badala yake wakabaki wamesimama kwa utulivu hatua chache tu kutoka lilipolipukia bomu lile huku wananchi wengine wakikimbia ovyo kwa taharuki na baadhi yao wakiangua kilio cha kujeruhiwa kwa viwango tofauti.
Huo ndio ukweli wa vurugu zote za Chadema zinazotokea nchini ambazo hatimaye hivi leo wanataka kuzitumia kwa kutengeneza kikosi cha kigaidi.
Tofauti na jinsi alivyodanganya Kigaila aliposema kuwa “kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki kwa raia yeyote kujilinda”, hakuna kifungu hicho popote katika ibara zote za Katiba ya nchi hii.
Tofauti na upotoshaji wake huo, Ibara ya 14 ya Katiba hiyo inasema: “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria”.
Mbali na hiyo, Ibara ya 16(2) ya Katiba ileile inasema: “Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kwa mujibu wa ibara hii, Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu ya faragha na ya usalama wa nafsi yake, mali yake na maskani yake yaweza kuingiliwa bila ya kuathiri ibara hii”.
Wapi panaposema “ni haki ya raia yeyote kujilinda” kama inavyopotoshwa na Kigaila? Ni ibara gani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoruhusu taasisi au kikundi chochote cha watu vikiwemo vyama vya siasa kama Chadema kuanzisha jeshi ama kikosi cha ulinzi?
Ni sehemu gani katika mamlaka halali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako Red Brigade ya Chadema imesajiliwa kama kikosi au hata kikundi cha ulinzi kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa?
Kinyume kabisa cha uongo aliousema Kigaila ambaye namjua kwa miaka mingi kuwa ni mmoja kati ya wazushi mahiri kabisa hapa nchini, Ibara ya 147(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano nayo inasema ifuatavyo:
“Ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote”, halafu Kifungu Kidogo cha (2) kinaongeza:
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania” (mwisho wa kunukuu).
Huo ndio ukweli ambao viongozi wa Chadema wanautengenezea uongo ili kuhalalisha uovu wao kwa nchi yetu. Huo ndio ukweli ambao wanajitahidi sana kuuficha kwa kuwadanyanga Watanzania ili kukidhi matakwa yao ya kigaidi kwa nchi hii.
Mbali na ukweli huo wote, hakuna jeshi lolote duniani lenye Red Brigade (au Brigedi Nyekundu) liwe la mgambo na hata la ulinzi. Kila jeshi la serikali yoyote lina brigedi zake zenye majina yasiyokuwa ya vitisho ama ya shari kama kikosi cha kigaidi cha Chadema.
Mfano katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo mimi nimewahi kuwa afisa wake lina brigedi zenye majina ya Tembo, Chui, Twiga, Faru, Mbuni, Nyuki na kadhalika kama ishara ya kuonyesha utajiri wa asili tulionao nchini. Red Brigade au Brigedi Nyekundu inaashiria shari na vitendo vya kikatili.
Hilo ndilo jina la genge lililotikisa Italia miaka iliyopita likiongoza kwa matukio ya kigaidi ambayo ni pamoja na kuwateka nyara viongozi wa dini na serikali ya nchi hiyo, utesaji wa aina zote, uchinjaji na umwagaji mwingine wa damu ili kuilinda na kuihami biashara yake ya madawa ya kulevya huku pia likiitwa Red Brigade kama ya Chadema!
Huo ndio ukweli ambao mtu yeyote anayetaka ni hivyo na hata asiyetaka pia ni hivyohivyo.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Friday 12 July 2013

Tenga: Aluta kontinua


NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametaka wachezaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kushinda mchezo wa leo dhidi ya Uganda.
Tenga, amewataka wachezaji kujiamini na wasikaribishe makosa ambayo yatatoa fursa kwa Waganda kupata bao.
Kingozi huyo alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wachezaji wa Taifa Stars kwenye kambini kwenye Hoteli ya TANSOMA, Dar es Salaam.
Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars, alizitaka safu za ulinzi, kiungo na ushambuliaji kufanya kazi kwa umakini ili ushindi upatikane.
“Sioni sababu ya kupoteza mechi hii, lazima tushinde ili kuwapa matumaini Watanzania mara ya mwisho ukweli mlicheza vizuri sana na Ivory Coast na kila mtu alifahamu hivyo ingawa tulifungwa,” alisema Tenga.
Tenga amewataka wachezaji kutokurudia makosa yaliyotokea katika mechi mbili za kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast.