Monday 15 June 2015

Wanafunzi wakoma
kutumia vibatari
 
 TATIZO lililokuwa likiwakabili wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Tulya, wilayani Iramba, mkoani Singida la kutumia mishumaa na vibatari wakati wa kujisomea usiku, hatimaye limepatiwa ufumbuzi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Asasi ya The Bourke Family Foundation(BFF) ya nchini Marekani, kuipatia shule hiyo msaada wa taa za umeme wa jua katika maktaba ya shule hiyo.
 BFF pia imewapatia taa za umeme wa jua wanafunzi wote wa shule ya sekondari Tulya, zitakazowawezesha kujisomea nyakati za usiku ili wafanye vizuri katika masomo yao.
 Akizungumza  baada ya kupokea msaada huo, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo,John Eliudi John alisema kabla ya kupatiwa msaada huo wa umeme wa jua,  walikuwa wakitumia mishumaa na vibatari, ambavyo viliwasababishia kuumwa na vifua kutokana na moshi waliokuwa wakiuvuta..
“Lakini kwa sasa tumepata sola, najua tutaongeza juhudi katika kusoma na tutasoma kwa muda mrefu zaidi ya pale mwanzoni tulivyokuwa tunafanya, kwa hiyo nawashukuru waliotusaidia kwa hilo,”alisisitiza.
 Mwanafunzi mwingine,  Mwanaidi Athumani, alisema kabla ya kupatiwa umeme wa jua ,walikuwa wakipata madhara mbalimbali wakati walipokuwa wakijisomea.
 Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo madhara hayo ni pamoja na makaratasi ya mitihani waliyokuwa wakijisomea  kuungua na wengine nyumba walizokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Mwenyekiti wa Taasisi PEN TRUST,Mungwe Athuman, alibainisha kwamba taasisi ya kujitolea ya BFF kutoka nchini Marekani, imeamua kutoa msaada wa umeme wa jua kwenye maktaba zote 160, zilizopo mkoani Singida.
 Akizindua mradi huo wa umeme wa jua, Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk. Parseko Kone, alifafanua kwamba asasi hiyo ya BFF iliamua kusaidia taa hizo kwa kila mwanafunzi wa shule zilizopo pembezoni, ili wajisomee kwa urahisi.

Mkuu wa Shule hiyo,Daud Mavyombo, aliwashukuru wafadhili kwa msaada huo na kueleza changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni upungufu wa walimu wa sayansi,kukosekana mabweni ya wasichana, ukosefu wa maabara na vifaa vyake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru