Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Thursday, 13 November 2014

Wakwepa kodi sasa kuanikwa


NA THEODOS MGOMBA NA NJUMAI NGOTA
SERIKALI imewasilisha Bungeni muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi, ambao pamoja na mambo mengine, utaweka utaratibu wa kuwatangaza kwenye vyombo vya habari wakwepa kodi wote.
Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema madhumuni ya muswada huo ni kuweka mfumo wa kisasa.
Waziri alisema nia ya kuwatangaza wakwepa kodi hao, ambao watathibitika kufanya hivyo, kutapunguza  makosa sugu na ya makusudi.
Alisema  mfumo huo wa kodi wa wazi, utahusisha kuhuisha ndani ya sheria moja vifungu mbalimbali vya sheria za kodi vinavyohusu usimamizi na utawala wa kodi.
Saada alisema mfumo uliopo sasa haujazingatia vigezo vya kimataifa, vinavyosisitiza kuwepo kwa sheria moja ya usimamizi na utawala wa kodi, ambayo inasimamia kodi zote.
Alisema kwa kupitisha sheria hiyo mpya, itasaidia kupunguza gharama za utawala, gharama za walipakodi kutimiza wajibu wao na kuepuka mianya ya rushwa.
Waziri alisema mambo mengine muhimu katika muswada huo ni pamoja na kuweka viwango vyenye uwiano sawa wa adhabu na faini kadri ya aina na ukubwa wa makosa ya kodi kwa kila aina ya kodi inayohusika.
Alisema  muswada huo utaweka vifungu vya kuzuia ukwepaji kodi ndani ya sheria moja, badala ya kuwa na vifungu hivyo katika sheria ya kodi kama ilivyo katika utaratibu wa sasa.
Saada alisema kupitia muswada huo, watafanya marekebisho ya sheria za kodi husika kwa kuondoa vifungu vinavyohusiana na utawala na usimamizi.
Mjumbe wa kamati hiyo, Kidawa Hamid Salehe (Viti MaalumuñCCM), akisoma maoni ya kamati kuhusu muswada huo, alipongeza vifungu vya 93 hadi 99, ambavyo vinaruhusu mashauri ya kodi, ambapo kamishna mkuu anapewa mamlaka ya kufanya upekuzi, kukamata, kuchukua na kuuza mali za mlipa kodi kwa lengo la kukomboa kodi na kuzuia ukwepaji kodi.
Alisema sehemu hiyo inatoa mamlaka ya kutangaza kwenye vyombo vya habari wakwepa kodi sugu.
Kidawa alisema kamati imeona umuhimu wa kuwepo kwa kifungu cha 97, kinachomwezesha kamishna mkuu kuwatangaza wakwepa kodi sugu bila kujali hadhi zao.
Alisema kufanya hivyo kutakuwa fundisho kwa walipa kodi wote, ambao vitendo vyao huinyima serikali mapato na hivyo kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi.
Kidawa alisema kamati hiyo inaona umuhimu wa kuwa na usimamizi wa kifungu hicho utaowezesha upatikanaji wa mapato stahiki kwa serikali.
Kwa mujibu wa Kidawa, kwa upande wa adhabu, muswada umeweka masharti mbalimbali yatakayotumika kupima ukubwa wa makosa ya kodi na kiwango stahiki cha adhabu.
ìKuhusu makosa mengine yatakayotendwa kutokana na kukiukwa kwa sheria hii, yataadhibiwa kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha muswada huu. Kifungu hiki pia kitahusika kutoa adhabu kwa yeyote atakayetoa siri kama zinavyoelezwa katika kifungu cha 21 cha muswada huu,îalisema.
Mjumbe huyo alisema kifungu cha 62(7), pia kimeboreshwa ili kutoweka ulazima wa mlipa kodi kuanza kudai kodi aliyolipa kwa ziada, badala yake, kamishna mkuu kuirudisha mara moja kodi hiyo iliyozidi bila kusubiri mlipa kodi kuomba kurejeshewa.
Alisema ili kutambua kwamba fedha hizo ni mali ya mlipa kodi, si sahihi kumtaka mlipa kodi kurejesha fedha hizo.
Kidawa alisema sehemu hiyo inabeba kifungu cha 70 hadi 74, ambacho kinabainisha masuala ya malipo na marejesho ya kodi yatafanywa  chini ya mamlaka ya kamishna mkuu.
ìKifungu cha 71 kinaainisha taratibu zinazopasa kufuatwa wakati wa kuwasilisha maombi kwa ajili ya marejesho ya kodi kwamba yatafanyika kwa maandishi, yakionyesha ukokotoaji sahihi wa kodi husika, yakiambatana na ushahidi wa maandishi unaounga mkono maombi hayo,î alisema.
Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi-CCM), akichangia muswada huo, alisema ukipitishwa utaboresha makusanyo ya kodi na mapato ya serikali yataongeza na hivyo changamoto zinazolikabili taifa ni pamoja na kutokutekeleza baadhi ya miradi na kutegemea wahisani.
Alisema muswada huo umeweka utaratibu wa adhabu na kwamba adhabu kubwa aliyoiona  ni ya kutangazwa katika vyombo vya habari kuwa hakulipa kodi.
ìKwa mtu mzima, kiongozi, mfanyabiashara mkubwa ambaye hataki biashara yake iingie doa, ambaye atataka benki zote zimuone ana thamani kubwa na anakopeshwa, hatataka kutangazwa katika vyombo vya habari, hili naliunga mkono,î alisema.
Mbunge huyo alisema utaratibu huo utakaowekwa, utekelezwe kwa sababu wakwepa kodi ni wafanyabiashara wakubwa, kwani wafanyabiashara wadogo hawajarasimishwa, kama wangeweka utaratibu rasmi, wangeweza kulipa kwani kodi yao ndogo.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya TIN kwa walipa kodi, alisema jambo hilo ni zuri na kutoa maoni yake kwamba taarifa zilizoambatanishwa katika TIN ni chache, ikilinganishwa na taarifa za takwimu zilizopo kwenye vitambulisho vya taifa.
Akichangia muswada huo, Jitu Soni (Babati Vijijini-CCM), alisema ni mzuri ila ufanyiwe marekebisho kadhaa, kwani kwa kufanya hivyo, serikali itakusanya kodi kwa wingi zaidi.
Pia, aliiomba serikali itoe kipaumbele katika elimu ya mlipa kodi ili watu wengi waweze kulipa kodi ili nchi iweze kuwa na maendeleo makubwa.

Mauaji ya Kiteto yalitikisa Bunge


JESHI Polisi linawashikilia watu watano kuhusiana na mauaji katika mapigano kati ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Matui wilayani Kiteto.
Katika mapigano hayo, watu wanne waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Akitoa kauli ya serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mathias Chikawe, alisema mapigano hayo yalitokea juzi katika wilaya hiyo.
Chikawe alisema Jumanne iliyopita katika kijiji hicho, mkulima Hassan Kondeja, mkazi wa Kijiji cha Bwawani, alikwenda katika Kituo cha Polisi Matui kutoa malalamiko kuwa kuna wafugaji wameingiza mifugo yao katika shamba lake la mihogo.
Waziri huyo alisema mkulima huyo aliwaambia polisi kuwa, anawafahamu wafugaji hao na atakwenda nyumbani kwao kuzungumza nao ili kumaliza tatizo hilo.
Alisema utaratibu huo wa kuzungumza uliwekwa na wanakijiji wenyewe ili kuondoa migogoro.
ìPolisi baada ya kuambiwa hivyo, walikubaliana na mlalamikaji huyo na kumruhusu kwenda kuzungumza na wafugaji hao,íí alisema.
Waziri Chikawe alisema juzi mkulima huyo alikutwa ameuawa na kuzikwa katika shamba lake huku kichwa kikiwa nje.
Alisema baada ya wanakijiji wenzake kupata taarifa hiyo na hasa wale wa kabila lake, walijikusanya na kuanza kuchoma moto maboma ya wamasai na kuswaga mifugo yao.
Kwa mujibu wa Chikawe, katika muendelezo wa kuswaga mifugo hiyo, wakulima hao walikutana na mama mmoja wa kimasai akiwa amebeba mtoto wa miaka minne mgongoni.
Waziri huyo alisema wakulima hao walimkatakata mama huyo na kumuua huku wakimuacha mtoto huyo bila kumdhuru.
Chikawe alisema mpaka sasa, mbali ya kuwakamata watuhumiwa hao watano, pia wamekamata ngíombe 309 walioibwa katika mapigano hayo.
Alisema ngíombe hao walikamatwa katika eneo la Kijiji cha Chitego, wilayani Kongwa na wengine katika eneo Chemba.
Hata hivyo, Chikawe alisema hali katika eneo hilo bado haijarudi kuwa nzuri, licha ya viongozi wa serikali wa mkoa kwenda katika eneo la tukio.

Serikali kulipa deni la watumishi wa umma


WATUMISHI wa Umma wanaidai serikali zaidi ya sh. bilioni nane, ikiwa ni malimbikizo ya madeni.
Hata hivyo, serikali imesema kiasi hicho ni kidogo ikilinganishwa na madai yaliyokuwepo awali, ambapo watumishi walikuwa wakiidai serikali fedha nyingi.
Hayo yameelezwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, ambapo alisema jitihada zinaendelea kufanywa ili kumaliza deni hilo.
Alikuwa akijibu swali la Masoud Abdalla Salim (Mtambile- CUF), ambaye alitaka kufahamu kuhusiana na malimbikizo na madeni ya askari.
Salim alisema serikali inaweza kuwaepusha askari na watumishi wa umma na vitendo vya rushwa kwa kuwalipa madeni.
ìWaziri umesema kuna wimbo wa maadili wa askari ambao wanatakiwa kuimba kila siku, wimbo huo utaimbwa na utaendelea kuimbwa kila siku, suala hapo ni madeni na mishahara ambayo askari wanaidai serikali,î alisema.
Celina alisema asilimia kubwa ya madeni tayari yamelipwa, ambapo alisema kwa sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inadaiwa sh. milioni 800.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu, deni hilo litakuwa limelipwa.
Awali, Mwanahamisi Kassim (Viti Maalumu-CCM), alihoji sababu zinazochukuliwa na serikali baada ya kuwafukuza kazi askari waliotiwa hatiani kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alikiri kuwa baadhi ya askari kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Kwa kipindi cha Januari mwaka jana na Septemba, mwaka huu, askari 54 walituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kati yao 19 walifikishwa mahakamani na 34 hatua mbalimbali za kinidhamu, ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi.

DC aagiza ofisa mtendaji, mwalimu mkuu waadhibiwe


Na Clarence Chilumba, Mtwara
MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo, kutoa adhabu kali kwa Ofisa  Mtendaji wa Kata ya Madimba na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari  ya Mayanga, kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa maabara.
Pia ameagiza watendaji hao kushushwa vyeo kutoka Ofisa Mtendaji wa Kata hadi Mtendaji wa Kijiji, ambapo kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Mayanga, kwa sasa anatakiwa kuwa mwalimu wa kawaida.
Aidha, ametoa angalizo  kwa watendaji wote wa halmashauri hiyo watakaoshindwa kuendana na kasi ya utekelezaji wa agizo la ujenzi wa maabara, kuwa ni bora watafute kazi zingine mapema.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya ujenzi wa maabara ndani ya wilaya yake.
Alisema kutotimiza majukumu kwa baadhi ya watendaji,ndio chanzo cha kudorora kwa ujenzi huo.
Alisema amelazimika kuchukua maamuzi hayo magumu kwa wakati huu wa utekelezaji wa maagizo ya  kiongozi wa nchi, ili kutoa fundisho kwa watendaji wengine, ambao ni wazembe na wasioendana na kasi ya ujenzi wa maabara.
“Unajua unaweza kuwa mwalimu mzuri, lakini usiwe kiongozi bora mwenye uwezo wa kuongoza wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye eneo lako. Hivyo kwa mwalimu kama huyu pamoja na mtendaji wa kata, hawastahili kuachiwa waendelee kuzorotesha kasi ya ujenzi wa  hizi  maabara,” alisema. 
Akizungumza  kwa njia ya simu, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Madimba,  Mahamudu Mtota, alisema  hajapokea taarifa za kupunguzwa madaraka na kwamba anachojua ni maagizo aliyoyatoa mkuu huyo wa wilaya alipokuwa Msimbati kuwa kesho (leo) asubuhi aende ofisini kwake.
Alisema ni kweli kuwa ujenzi wa maabara katika shule mbili za sekondari zilizoko kwenye kata hiyo unaenda kwa kusuasua, kutokana na kukosekana kwa vifaa vya ujenzi, ikiwemo mawe,mchanga pamoja na maji na kwamba hadi sasa maabara zote mbili ziko kwenye hatua ya msingi.

Halmashauri Magu yapigwa jeki


NA SARAH ONESMO, MWANZA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, imepokea vifaa vipya vya afya na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Msaada huo umetolewa na Taasisi ya Grena Youth Production School (GYPS) ya Denmark na utaihusu Kata ya Nyanguge, ambako tayari vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa uongozi.
Vifaa hivyo ni robota moja ya mashuka ya wagonjwa, nguo za madaktari na wauguzi, mashine ya utrasound, mashine moja ya EKG ya kupimia wagonjwa wa moyo na kompyuta 95.
Akizungumza na  wananchi, Diwani wa Kata ya Nyanguge,  Hilali  Elisha, alisema lengo la kutafuta wadau na wafadhili mbalimbali ni kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.
 “Mashine hizi zilizotolewa, zitasaidia  wanawake wajawazito kufanyiwa uchunguzi, ambao utakuwa wa uhakika na kupewa majibu, lakini wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo pia watapimwa na kupata dawa,”alisema.
Aliongeza kuwa kompyuta 95 zilizotolewa na taasisi hiyo, zitapelekwa katika shule za msingi na sekondari, makanisa, Chuo cha Maendeleo cha Nyanguge , Ofisi ya Ofisa Tarafa ya Kahangara pamoja na kituo cha Polisi Nyagunge.
“Pamoja na wapinzani kupiga kelele, lakini CCM inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kuhakikisha kero na matatizo ya wananchi yanatafutiwa ufumbuzi wa haraka ili huduma za jamii ziweze kupatikana katika maeneo mbalimbali hapa nchini,”alisema. 
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jackiline Liana, alimpongeza diwani huyo kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi wa kata yake maendeleo na kuwataka wanasiasa kuiga mfano huo na si kupiga kelele jukwaani bila kuonyesha vitendo.
“Vifaa hivyo  vitasaidia upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi na pia wanafunzi watapata maarifa kwa kutumia teknolojia ya kompyuta kwa vitendo na kuongeza weledi wawapo shuleni,” alisema.
Alisema diwani huyo anatekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo na amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha kero na matatizo ya kijamii yanatafutiwa ufumbuzi wa haraka,  pia huduma kwa wananchi zinapatikana.
 Mganga   wa Kituo cha Afya cha Nyanguge, Innocent Charles, alisema  pamoja na kituo hicho kupata mashine hizo,  hakuna wataalamu wa kuzitumia, hivyo alimuomba diwani huyo  kupeleka ombi la kupata wataalamu wa kuzitumia.

Wananchi wagoma kuchangia maabara


NA EVA-SWEET MUSIBA,TARIME
WANANCHI wa Kata ya Matongo-Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wamekataa kuchangia fedha za ujenzi wa maabara  kwa madai kuwa, fedha zao za maendeleo ya kata hazijalipwa kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.
Akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Madiwani, Mtendaji wa Kata ya Matongo, Chacha Muniko, alisema wananchi wamekataa kuchangia fedha hizo kutokana na kuudai mgodi huo asilimia tano, ambayo ni sawa na sh. milioni 700.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilikataliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime, Nyanja Maiga, na kumtaka mtendaji huyo kutoka nje ya ukumbi.
Kauli hiyo ilizua  tafrani kubwa katika kikao hicho, ambapo madiwani wote walimtetea mtendaji huyo na kumtaka mkurugenzi  awajibike na si mtendaji wa kata hiyo.
Tafrani hiyo iliwekwa sawa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, ambaye alisema ofisi yake ilishugulikia madai hayo na kwamba, taarifa itatolewa kwa madiwani baada ya kukamilisha mazungumzo kati ya serikali na mgodi huo ili waweze kulipa deni hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa kata hiyo, Machage  Bathromew, alisema wapo baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wanachangia kuwafanya wananchi kugomea michango hiyo kwa madai kuwa serikali imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sekondari.

Mgimwa awapa darasa waongoza watalii


NA JAMES LANKA, MOSHI
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utaliii, Mahmoud Mgimwa, amewataka waongoza watalii kuhakikisha wanapewa  mikataba halali ya kazi na wamiliki wa kampuni wanayofanyakazi ili kuepuka kunyonywa haki zao. 
Mgimwa alitoa rai katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Waongoza Watalii Mlima Kilimanjaro (KGA), kilichofanyika juzi mjini hapa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Respicius Baitwa, alimueleza naibu waziri kuwa,  pamoja na ugumu wa kazi yao, baadhi ya wamiliki wa kampuni za utalii wamekuwa wakiwanyonya haki zao waongozaji hao.
 “Nimesikiliza risala yenu kwa makini, changamoto kubwa mliyoeleza ni maslahi duni kutokana na kulipwa ujira mdogo na waajiri wenu, hivyo nawasihi muwe makini, hasa katika suala la mikataba yenu ya kazi ili serikali iweze kutetea haki zenu, maana ninyi ni mabalozi wa utalii,” alisema.
Waziri huyo aliwaahidi waongoza watalii hao kuwa atakutana na Chama cha Wamiliki wa Kampuni ya Utalii nchini (TATO), pamoja na Chama  cha Wamiliki wa Kampuni ya Utalii Kilimanjaro (KIATO), ili kuona namna ya kulinda maslahi ya waongoza watalii hao.
Mgimwa alisema Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ambayo inaiingizia serikali mapato makubwa, inapaswa kuwa na wafanyakazi makini na wanaofanya kazi zao kwa uadilifu. 

Escrow kaa la motoNA THEODOS MGOMBA, DODOMA
KASHFA ya madai ya kuchotwa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya ESCROW, imezidi kuwa moto kutokana na kuibua mjadala mkali bungeni kila kukicha.
Tayari serikali iliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo malipo hayo kwa Kampuni ya PAP, iliyonunua IPTL, yalifanyika kihalali, ambapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imepewa jukumu hilo.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema kuwa, mbali na watendaji wa serikali, baadhi ya wanasiasa wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani na wabunge, ni miongoni mwa wanaodaiwa kunufaika na mabilioni hayo kila mmoja kwa namna yake.
Kwa upande wa wanasiasa, taarifa zinasema yumo mbunge wa upinzani, aliyechota kiasi cha sh. bilioni 20 kama mgawo, ambapo kwa sasa amekuwa na wakati mgumu kutokana na ukimya wake kutiliwa shaka na wanasiasa wenzake.
Hivi karibuni, ilielezwa kuwa taarifa ya uchunguzi huo itakabidhiwa kwa mamlaka husika muda wowote na kwamba, iko kwenye hatua za mwisho huku taarifa zingine zikidai kuwa imeshakamilika.
Tangu kuanza kwa Bunge, hoja kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi wa akaunti ya ESCROW, imekuwa ikizuka kwa wabunge kuhoji ni lini itawasilishwa, ambapo serikali hutoa majibu, lakini jana ikaibuka tena.
Baadhi ya wabunge walitaka Bunge kuiagiza serikali kuwasilisha taarifa hiyo ili ijadiliwe kwa kina, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisimama na kuwaeleza kuwa TAKUKURU haiwajibiki kupeleka taarifa yake ya uchunguzi Bungeni.
Alisema hakuna kitu ambacho kitafichwa kuhusiana na sakata hilo na kwamba, taarifa zote za uchunguzi zitakazobainika, zitawekwa hadharani kwa maslahi ya taifa.
Ndugai alisema taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sakata la akunti ya Escrow, itakayowasilishwa bungeni ni ile itakayowasilishwa na CAG wakati ya TAKUKURU itawasilishwa kwa mamlaka zingine, ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.
‘’Kwa kawaida taarifa hizo zikija bungeni, haziwasilishwi moja kwa moja ndani ya Bunge bali zinapitia katika kamati husika na kamwe TAKUKURU haiwajibiki kuleta taarifa yake kwetu,” alisema Ndugai.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Wizara Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, alisema serikali itaangalia namna itakavyofaa ili taarifa ya TAKUKURU iwasilishwe bungeni bila kuathiri uchunguzi wake. 
Awali, baadhi ya wabunge walilitaka Bunge kuiagiza TAKUKURU kutoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusiana na akaunti Escrow kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuomba mwongozo wa Naibu Spika, wabunge hao walisema pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kukabidhi taarifa yake kwenye kamati hiyo, pia TAKUKURU hawana ujanja wa kutokabidhi taarifa yake.
Akiomba mwongozo wa Spika, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema pamoja na kamati yake kupatiwa taarifa ya CAG, bado inahitaji taarifa zaidi kutoka TAKUKURU.
‘’Tuna changamoto kuwa pamoja na taarifa ya CAG, ili kamati yangu iweze kufanya kazi yake vizuri, taarifa ya TAKUKURU iwepo,” alisema.
Alisema kumekuwa na minong’ono mingi kati ya wabunge juu ya watu wanaohusishwa na fedha kwenye akaunti ya Escrow, hivyo ili kuondoa giza hilo ni muhimu jambo hilo likawekwa wazi.
‘’Tunakuomba uiagize serikali kuileta taarifa ya TAKUKURU ili tuwe na taarifa zote mbili kwa pamoja na mchakato mzima uwe wazi.
‘’Wabunge wenzangu mimi najua mnapitiwapitiwa huko, hivyo mchakato mzima uwe wa wazi na kila mtu ahukumiwe kwa kile alichofanya,’’ alisema Zitto.
Mbunge achota bil.20/-
Wakati wabunge wakipambana kuhakikisha taarifa ya uchunguzi wa akaunti ya Escrow inawekwa wazi, taarifa zinadai kuwa mbunge mmoja (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwa miongoni mwa waliochota fedha hizo.
Habari kutoka kwenye chanzo chetu zinadai kuwa, mbunge huyo, ambaye ni mahiri wa kupiga kelele bungeni, amevuta mabilioni hayo kwa malengo ambayo hayajafahamika mpaka sasa.
Imedaiwa kuwa mbunge huyo kutoka kwenye chama cha upinzani, kwa sasa amekuwa kimya tangu kuanza kurindima kwa sakata hilo, jambo ambalo limewafanya baadhi ya wanasiasa wenzake kutilia shaka ukimya wake.
Hata hivyo, kumekuwepo na orodha ndefu inayotolewa kwenye mitandao, ikihusisha baadhi ya watendaji na wanasiasa, wakiwemo wa vyama vya upinzani, kudaiwa kuhusika kwenye kupata mgawo wa mamilioni ya shilingi ya fedha za Escrow.

JK azungumza na viongoziNA MWANDISHI WETU
Rais Dk. Jakaya Kikwete akiwa hospitalini nchini Marekani
Taarifa ya Ikulu ilisema jana kuwa Rais Kikwete ameanza kuwasiliana na mamia kwa mamia ya wananchi nchini na kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wa kumpa pole na kumtakia heri.
Tangu alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume wiki iliyopita, Rais Kikwete amepokea mamia kwa mamia ya SMS zikimpa pole na kumtakia nafuu ya haraka.

“Rais Kikwete bado anaendelea kujibu SMS hizo na wananchi ambao wamemtumia, waendelee kusubiri majibu yake kwa sababu anakusudia kujibu SMS zote ambazo ametumiwa,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, Rais Kikwete jana alizungumza kwa simu na uongozi wa juu kwa mara ya kwanza tangu afanyiwe upasuaji. Rais alizungumza na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Mabomu hatari yanaswaNA CLARENCE CHILUMBA, MASASI
JESHI la Polisi mkoani Mtwara, linawashilkilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na mabomu 18 ya kutengenezwa kwa kutumia vifaa hatari vya kupasulia miamba.
Habari za kuaminika zinasema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kutokana na kuishi maeneo tofauti. Pia walinaswa na nyaya na unga maalumu ambao ni malighafi zinazotumika katika kutengeneza mabomu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustino Ullomi, alisema watuhumiwa hao walitiwa mbaroni mapema wiki hii, ambapo kila mmoja alikutwa akiwa nyumbani kwake.
Alisema watuhumiwa wote walikutwa na mabomu hayo wakiwa wameyahifadhi na kuwa kukamatwa kwao kumefanikishwa na raia wema.
Kamanda Ullomi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Abdallah Hamisi (25) na Kibode Dua (37).
Alisema mtuhumiwa wa kwanza kutiwa mbaroni alikuwa Abdallah, ambaye baada ya kubanwa alieleza yalipo mabomu hayo na kuwa aliyapata kutoka Nanyumbu kwa Dua.
Kamanda Ullomi alisema askari walikwenda na mtuhumiwa huyo nyumbani kwa Dua na kufanikiwa kunasa mabomu mengine 17, barua, unga na nyaya zinazotumika katika utengenezaji wa mabomu hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda Ullomi, watuhumiwa hao walipohojiwa zaidi, walidai waliyapata Tunduru mkoani Ruvuma na mengine Nachingwea mkoani Lindi.
Aliongeza kuwa baada ya uchunguzi kwa kushirikiana na wataalamu wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu, walibaini mabomu hayo ni hatari na yana uwezo wa kuuawa watu wengi kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Kamanda Ullomi, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.

Ajinyonga kisa? Wivu wa mapenzi


NA CHIBURA MAKORONGO,KAHAMA 
MFANYAKAZI wa kampuni ya uchambuaji pamba ya Kahama Oil Mills Ltd, Yusuph Abdallah (55) amekutwa amekufa bafuni baada ya kujinyonga kutokana na wivu wa mapenzi. 
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhongolo, Elias Chuma,  alisema tukio hilo lilitokea juzi  saa tano asubuhi, baada ya mfanyakazi wa usafi wa nyumba ya kampuni aliyokuwa anakaa Abdallah, Pili Makoye, kumkuta Abdallah akiwa amejinyonga.  
Kiongozi huyo alisema baada ya kuona hivyo, Pili alipiga owe ambapo watu walifurika na kushuhudia tukio hilo. 
Mwenyekiti huyo alisema kuna taarifa kwamba Abdallah alikuwa mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia hali iliyomfanya atoweke  nyumbani kwa muda mrefu huku akimtamkia mkewe kwa maneno makali. 
Chuma aliwaeleza waandishi wa habari kwamba  kabla ya kujinyonga, Abdallah alimuwekea mtoto wake sh. 38,500 mfukoni ili zimsaidie.Alisema walikuwa na mgogoro wa kifamilia wa muda mrefu ambapo ulianza  Ijumaa iliyopita, hivyo kuamua kuondoka nyumbani kwa siku kadhaa. 
Aliporejea nyumbani, mkewe naye aliamua kuondoka na ndipo
mwanamume huyo alipochukua jukumu la kujinyonga. 
Kwa mujibu wa Chuma, siku ya tukio Abdallah alirudi nyumbani kwake na mkewe, na kuaga kuwa anakwenda kwa dada yake kuishi huku akimtelekeza mtoto wa miaka mitano ambaye wakati anakwenda kujinyonga alimwachia fedha hizo na kuaga anakwenda kujisaidia.  
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus  Kamugisha,  alithibitisha tukio hilo na kueleza kwamba lilitokea juzi.