Thursday, 5 March 2015

Mvua ya maafa KAHAMA  • Nyumba zaharibiwa, JK atuma rambirambi
     
  • Watu 40 wapoteza maisha, 85 wajeruhiwa

    • Hali ya hewa yasema zitanyesha zaidi


Na waandishi wetu, Dar na Kahama
WAKATI Watanzania wakiomboleza kifo cha mwanasiasa mahiri, Kapteni mstaafu John Komba, taifa limeingia tena kwenye huzuni na simanzi kutokana na watu 40 kupoteza maisha.
Pia, watu wengine 82 wamejeruhiwa vibaya na wengine hali zao ni mbaya huku nyumba, mifugo na mazao, vikiharibiwa kutokana na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kutikisa kwa dakika 45 juzi usiku.
Mkazi wa kijiji cha Mwakata akionesha sehemu ya mawe ya barafu yaliyoangushwa na mvua kubwa iliyonyesha katika kijiji cha Mwakata kata ya Mwakata wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga. 
Maafa hayo yametokea katika kata ya Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga, ambapo vijiji vitatu ndivyo vilivyoathiriwa zaidi na watu wake kupoteza maisha.
Mvua hiyo, ambayo bado imewaacha wananchi katika sintofahamu, iliambatana na upepo mkali na vipande vya mawe vyenye ukubwa wa ndoo ya lita 10, ilinyesha mfululizo kwa dakika 45 wakati watu wakiwa wamelala.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mvua hiyo imeathiri zaidi vijiji vya Mwakata, Nhumbi na Magung’humwa, ambapo awali ilikuwa ya kawaida kabla ya kufuatiwa na upepo mkali ulioambatana na mawe.
Tayari watu 38 waliopoteza maisha kwenye tukio hilo, walizikwa jana jioni kwenye makaburi pembezoni mwa maeneo ya tukio lilipotokea.
Hata hivyo, watu hao wamezikwa kwenye makaburi tofauti badala ya utaratibu wa kuzika pamoja kutokana na kutambuliwa na ndugu na jamaa.
Wamesema vifo vingi vimetokana na watu kupigwa na mawe, kuangukiwa na nyumba na kuzidiwa na maji yaliyokuwa yakienda kwa kasi huku mvua hiyo ikiendelea kunyesha.
Mchungaji ambaye hakufahamika jina lake mara moja akiuombea mwili wa mtoto aliyekufa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana huko katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Hatujawahi kuona mvua kubwa kama hii, bado tunaitafakari kwani ni kitu cha ajabu katika historia ya eneo letu, nadhani hata nchini. Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuangukiwa na nyumba na kupondwa kwa mawe,” alisema Masanja Juma, ambaye ni mmoja wa mashuhuda.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwakata, Mahega Mwelemi, alisema katika tukio hilo watu 35 walipoteza maisha papo hapo na wengine wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama.


“Mvua hii imeleta maafa, mpaka sasa kuna maiti 35 na majeruhi zaidi ya 60, bado tunaendelea kufanya uchunguzi ili kuona kama bado kuna watu wamefukiwa ama kusombwa na maji. Mpaka sasa hatujapata idadi halisi ya mifugo iliyokufa, lakini ng’ombe na mbuzi wengi wamekufa,” alisema.


Moja ya nyumba iliyobomolewa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamika jana huko kijiji cha Mwakata wilayani Kahama.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, akizungumza eneo la tukio, alisema hali si shwari na taifa limepatwa na msiba mzito kutokana na kupoteza idadi kubwa ya wananchi wake.

Alisema uchunguzi unaendelea katika kila kaya ili kubaini watu waliokufa na kujeruhiwa pamoja na mifugo iliyokufa kutokana na mvua hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, Elisa Mugisha, alisema kikosi maalumu cha uokoaji kilifika eneo la tukio na kuanza kazi ya kuwaokoa watu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema idadi ya waliokufa na majeruhi, inaweza kuongezeka kutokana na hali halisi ya tukio hilo.

Alisema kazi ya kuokoa na kusaidia waliojeruhiwa inaendelea, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini, ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa watoto wengi wamepoteza maisha kwenye tukio hilo.

Aidha, mchakato kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tukio hilo unaendelea. Tayari vyakula, mablanketi na nguo vimeanza kupelekwa kwenye eneo la tukio na wafanyabiashara mjini hapa jana walikutana kuangalia namna ya kushiriki.
 JK atuma salamu za pole
Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, kuomboleza vifo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, katika tukio hilo, watu 3,500 waliathirika na maafa hayo yaliyotokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali.
Katika salamu zake, Rais Kikwete alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya wananchi hao na waliojeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama.

“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu baada ya nyumba zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha,” alisema.

Alisema msiba huo sio wa wana-Shinyanga pekee bali ni wa Taifa zima ambalo, limepoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.

“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 38 kwa mara moja katika mkoa wako. Kupitia kwako naomba rambirambi ziwafikie wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa.

“Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema azipokee na kuzilaza roho za marehemu wote mahali pema peponi,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.

“Namuomba Mola awawezeshe majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama kawaida,” alisema.


TMA: Mvua za mawe zaidi zinakuja
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema mvua iliyonyesha juzi wilayani Kahama ni miongoni mwa mvua walizotabiri kwenye utabiri wao wa msimu wa masika.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alizungumza na Uhuru Dar es Salaam jana, kuwa utabiri huo ulionyesha uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria.
Alisema kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, maeneo mengi ya Tanzania tofauti na miaka ya nyuma, yanaweza kupata mvua hizo za mawe, ambazo mara nyingi hunyesha kwa muda mfupi, lakini husababisha madhara makubwa kutokana na ukubwa wa barafu zinazodondoka.
Dk. Agnes alisema hali hiyo husababishwa na mawingu mazito, ambayo humeguka kutokana na uzito huo, kisha kutegemewa kuyeyushwa na joto angani, ambalo kama halitoshi kuyeyusha vipande hivyo vya barafu, hufika kwenye uso wa dunia katika hali hiyo.
Alisema tahadhari ya uwepo wa mawingu mazito kwenye maeneo mbalimbali ya nchi itaendelea kutolewa na TMA kupitia vyombo vya habari, hivyo Watanzania wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru